RIWAYA : SALA YA SARAH.
MTUNZI : ALEX KILEO.
SEHEMU YA KUMI NA NNE.
ILIPOISHIA.
Kijana aliondoka huku akiwa anawasiliana na Tekso muda wote ili aweze kufika sehemu Salama.
Kijana alifanikiwa kufika hilo eneo alilopo Sarah, alifika mpaka nje ya Guest, akasimamisha gari na kuanza kupiga hesabu za kuingia ndani kama atakutana na pingamizi lolote,
Mwisho akaamua kutumia ubabe endapo kutakuwa na kikwazo chochote, kijana akashuka kwenye gari na kuingia moja kwa moja ndani ya Guest, ambapo alimkuta dada wa mapokezi akisinzia sinzia kaunta,
"Karibu kaka, unahitaji chumba?" Dada wa mapokezi alimuuliza,
"Hapana, kuna dada mmoja nimemfuata, nataka kumuona" Kijana alijibu na kumfanya dada wa mapokezi akumbuke kuwa Sarah ndiye aliyesema kuna mgeni wake atakuja kumuulizia,
"Aah yupo, nenda chumba namba nne" Dada wa mapokezi alijibu na kisha yule kijana akaenda mpaka chumba namba nne, akagonga hodi na baada ya muda mchache mlango ulifunguliwa, ulifunguliwa na Sarah mwenyewe, Sarah akapata mshtuko baada ya kukutana na sura ngeni mlangoni,
"Karibu" Sarah aliongea huku akiwa amesimama mlangoni,
"Naweza kupita ndani?" Kijana aliuliza,
"Hapana, kama una shida unaweza kuongea hapo hapo" Sarah alijibu,
"Nina shida, ila nitahitaji tuongee ndani" kijana aliongea,
"Siwezi kumkaribisha chumbani kwangu mtu nisiyemjua" Sarah aliongea huku akiwa amesimama mlangoni,
"Ebu pisha bwana" Kijana aliongea na kumsukuma Sarah na kufanya Sarah apepesuke huku akirudi nyuma, kijana akajitoma ndani kibabe.............
***********ENDELEA**********
"Unataka nini kutoka kwangu?" Sarah aliuliza huku akionekana ana hasira,
"Sihitaji maswali, unachotakiwa kufanya ni kusikiliza amri kutoka kwangu tu" Kijana alijibu huku macho yake yakiangaza ndani ya chumba kile cha guest,
"Ndio useme sasa unachokitaka" Sarah aliongea,
"Unatakiwa uambatane na mimi mpaka sehemu ninayotaka uende. Sitaki swali jingine" Kijana aliongea,
"Sehemu gani hiyo? kwanza wewe ni nani?" Sarah aliuliza,
"Nimekwambia sitaki maswali, fanya ninachotaka" Kijana aliongea huku akimuendea Sarah,
"Sawa, naomba utoke nibadilishe nguo" Sarah aliongea,
"Badili tu, mimi siwezi kutoka, tutatoka wote" Kijana aliongea huku amemkazia macho Sarah,
"Sawa endelea kuniangalia" Sarah aliongea huku akiliendea begi lake la nguo na kulifungua, kisha akaingiza mkono, bila hata kutegemea ule mkono ulitoka na bastola na kumuelekezea yule kijana, kijana akapigwa na butwaa, maana hakutegemea kitu kama hicho,
"Kaa hapo kwenye kiti" Sarah aliongea huku akimuangalia yule kijana, kijana akatii huku akiendelea kushangaa namna mchezo ulivyombadilikia ghafla namna ile, akakiri ni uzembe mkubwa ameufanya kwa kumdharau mwanamke yule.
Sarah akamsogelea yule kijana,
"Toa earphone hizo, tupa hapo chini" Sarah aliongea na yule kijana akatii na kuitupa chini ile earphone, Sarah akaikota na kuiangalia kwa muda, kisha akaikata kata,
"Lete simu" Sarah aliongea na yule kijana akaitoa simu na kuitupa jirani na miguu yake, Sarah akaiendea akainama ili aiokote, Kijana alirusha teke lililoipiga bastola ya Sarah, kisha akarusha ngumi nyingine kumuendea Sarah, kwa ukali wa ile ngumi ilikuwa ngumu sarah kuidaka ingawa alikuwa na uwezo huo, alichofanya Sarah ni kurudi nyuma kisha akaachia teke jepesi kulenga tumbo la yule kijana, kijana akaudaka mguu wa Sarah, na hicho ndicho Sarah alichokikusudia, baada ya mguu wake kudakwa, Sarah aliruka sarakasi na kujibinua kisha ule mguu wake mwingine ukaenda kukipiga kidevu cha yule kijana, kijana akajikuta anayumba huku akirudi nyuma, Sarah akamuendea kwa kasi na kumpiga teke Kali la shingo na yule kijana akajikuta anatua chini kama mzigo huku akipambana na macho yake yaliyokuwa yanaona maluweluwe.
Sarah akarudi nyuma na kuikota bastola yake kisha akakaa kitandani huku akimuangalia yule kijana aliyekuwa ahamini kitu kilichofanywa na huyo binti muda mchache uliopita,
"Taita amekutuma si ndio?" Sarah aliuliza huku akiwa amemkazia macho,
"Hapana" Kijana alijibu huku macho yake yakipingana na jibu lake,
"Nimesikia kila mlichoongea na kila ulichoagizwa, napenda sana mtu mkweli. Ulitumwa unichukue?" Sarah aliuliza tena,
"Ndio" Kijana alijibu,
"Twende unipeleke" Sarah aliongea huku akimtazama yule kijana aliyekuwa anashangaa kujiamini kwa binti huyo,
"Nyanyuka wewe, hakuna muda wa kushangaana, ongoza mbele na usithubutu kugeuza shingo nyuma" Sarah aliongea kwa sauti kali na kumfanya Kijana asimame na kuanza kuelekea nje huku akifuatwa na Sarah.
Walipofika jirani na kaunta, Sarah akaificha bastola,
"Unatoka Bibie?" Dada wa mapokezi alimuuliza Sarah,
"Yap, nitarudi muda si mrefu" Sarah alijibu bila kugeuka na huku akisonga mbele. Walielekea moja kwa moja mpaka nje pembeni ya gari,
"Panda gari, wewe ndio dereva" Sarah aliongea na kijana akaingia upande wa dereva kisha Sarah akaingia siti za nyuma, kijana akawasha gari na kuiondoa kwa mwendo wa taratibu kulingana na maelezo ya Sarah.
Gari ilitembea kwa dakika kadhaa mpaka ilipoanza kuingia mitaa ya osterbay,
"Simamisha gari" Sarah aliongea na kijana akatii, kisha Sarah akaendelea,
"Kwa umri ulionao unaona kipi bora kati ya uhai na kifo" Sarah aliuliza,
"Uhai" kijana alijibu,
"Kuanzia sasa una machaguo mawili, chaguo la kwanza ni kufikisha ujumbe nitaokupa ili uendelee kuishi, na chaguo la pili ni kutofukisha ujumbe nitaokupa alafu ufe" Sarah aliongea kisha akameza mate,
"Nitafikisha ujumbe" Kijana aliongea kwa uoga,
"Kamwambie Taita kuwa yeye ni mpumbavu, huo ndio ujumbe unaotakiwa kuufikisha" Sarah aliongea na kukaa kimya,
"Sawa nitamwambia" Kijana aliongea,
"Hiyo ni juu yako wewe, ila matokeo yake nimeshakwambia. Ukifika nitakupa dakika tano za kumwambia, ukishindwa kumwambia ndio kifo chako kitatimia" Sarah aliongea kisha akampiga ngumi kali ya shingo yule kijana, kijana akapoteza fahamu na hakujua kitu chochote kilichoendelea.
Kijana alifungua macho na kujikuta amekaa siti ya nyuma ya gari, na alipoangalia siti ya dereva hakuona mtu, ndipo alipokurupuka na kuchungulia nje na kujikuta yupo kama nyumba ya tatu kutoka kwa Taita, Kijana akatelemka katika gari na kwenda moja kwa moja mpaka kwenye geti la Taita, akaingia na kupitiliza moja mwa moja mpaka sebuleni na kumkuta Taita na vijana wengine wakiwa kama na kikao, walipomuona mwenzao walishtuka,
"Yaani tulikuwa tunaangalia namna ya kukupata, maana ulipotea ghafla mtandaoni" Tekso aliongea huku akimuangalia yule kijana,
"Aisee yule Dada sio wa kawaida" Kijana aliongea,
"Kwanini unasema hivyo?" Taita aliuliza,
"Amejipanga kupambana" Kijana alijibu huku akikikumbuka kichapo alichopigwa,
"Yupo wapi sasa?" Taita aliuliza,
"Sijui, tulikuja nae ila alinipiga na nikapoteza fahamu, niliposhtuka nikajikuta nipo peke yangu" Kijana alitoa maelezo,
"Kuna ujumbe wowote amekupa?" Taita aliuliza,
"Hapana, hapana hajanipa" Kijana alijibu, sio kwamba hakuwa na kumbukumbu kwa alichoagizwa na Sarah, ila alimuheshimu sana bosi wake kwa hiyo aliona ni dharau sana kumuita bosi wake mpumbavu na ndio maana hakutaka kumwambia.
"Lakini umejua anapokaa?" Tekso akamuuliza yule kijana,
"Ndio, anaishi guest" Kijana alijibu,
"Guest? Tukienda tutamkuta kweli?" Taita aliuliza,
"Twendeni haraka, tukimkosa tunaweza kupata mwanga wowote wa kumjua" Tekso aliongea,
"Gari ipo wapi?" Taita alimuuliza yule kijana,
"Gari ipo, ipo nyumba ya tatu kutoka hapa" Kijana alijibu
"Nyumba ya tatu kutoka hapa? Kwanini umeiegesha uko?" Taita aliuliza,
"Sio mimi, ni huyo Dada, alinipiga nikazimia ndio nikajikuta ameegesha gari hapo" Kijana alijibu,
"Kaisogeze hapa basi hiyo gari" Taita aliongea na kisha kijana akatoka kwenda kuifuata hiyo gari, alipoifikia alifungua mlango na kuingia ndani ya gari, alilikagua hilo gari kama limetegwa bomu ila hakukuta kitu, akajiridhisha kupo Salama, akawasha gari na kuisogeza mpaka nje ya geti la Taita. Akafungua mlango ili ashuke, ila akaiona simu yake iliyokuwa kwenye siti ya pembeni ikiita, akaichukua na kuangalia jina la mpigaji ila hakukuta jina isipokuwa namba tu, akabofya kitufe cha kupokelea,
"Halow" Kijana aliongea,
"Ulichagua kufikisha ujumbe niliokupa, ila umeshindwa kufikisha" Ilikuwa ni sauti ya Sarah iliyofanya kijana ajiulize kuwa huyo binti amejuaje kuwa ujumbe haujafika,
"Wewe Malaya usiniendeshe, huo ujumbe ungeupeleka mwenyewe" Kijana alijibu kibabe,.
"Umefeli, angalia chini ya kiti ulichokalia" Sarah aliongea kisha akakata simu, yule kijana akainuka na kufunua kiti, papo hapo ukatokea mlipuko mkubwa wa bomu, yaani ile gari ililipuka na yule kijana akiwa ndani ya gari, huo ndio ukawa mwisho wa yule kijana.
Kule mlipuko wa bomu uliwastua mpaka Taita na vijana wake, wakatoka sebuleni ili kuelekea getini, wakakuta geti na ukuta wake vyote vipo chini na gari aliyokuwemo yule kijana ilikuwa ikiwaka moto.
Taita akaonekana dhahiri amechanganyikiwa kutokana na lile tukio,
"Mlinzi wa geti yupo wapi?" Taita aliuliza ila hakuna mtu aliyemjibu kwa maana kutokana na watu kutojua ni wapi mlinzi alipo kwa muda huo.
Na kipindi hicho watu wengine walikuwa wakianza kujisogeza eneo la tukio, na polisi pia walifika kwa ajili ya kuja kuangalia tukio hilo.
Baada ya muda, vijana wa Taita wakaanza kutoa matofali yaliyokuwa yamezagaa hapo, ni matofali ya ukuta wa geti ulioangushwa na Bomu.
Baada ya kumaliza walinyanyua geti, chini ya geti ndipo walipomkuta mlinzi akiwa amelaliwa na geti na hakuwa na fahamu,
"Bosi mlinzi huyu hapa" kijana mmoja alimwambia Taita, Taita akasogea na kumkuta mlinzi akiwa amelala na mwili umejaa damu, bahati nzuri na gari ya hospitali ilikuwa hapo, ikambeba mlinzi na kuondoka nae.
Polisi wakachukua maelezo kidogo kwa Taita kisha nao wakaondoka zao.
Baada ya muda kidogo watu wakiwa wameshasambaa na muda huo vijana wa Taita wakiwa bize na shughuli za hapo, ndipo simu ya Taita ikaanza kuita, alipoangalia kioo cha simu akakutana na namba ngeni,
"Hallow" Taita aliongea baada ya kupokea,
"Pole kwa tukio, ila huo ni mwanzo tu, watakufa watu wengi kwa ajili yako ila mwisho ni kwamba mimi naitaka roho yako" ilikuwa ni sauti ya Sarah, iliongea maneno machache ila yalikuwa makali,
"We ni nani?" Taita aliuliza,
"Unanijua vizuri tu" Sarah alijibu na kuzidi kumchanganya Taita,
"Ningekuwa nakujua nisingekuuliza" Taita aliongea,
"Kwa hiyo unataka kuniona kwa Mara nyingine tena?" Sarah aliuliza,
"Ndio" Taita alijibu kwa shahuku,
"Geuka, nipo nyuma yako" Sarah aliongea na Taita akageuka, ndipo alipomuona msichana akiwa amesimama huku akitabasamu na sikioni alikuwa na simu aliyoishika kwa kiganja chake, alikuwa ni Sarah,
"Nahisi umeniona sasa" Sarah aliongea huku akitabasamu na kufanya Taita atoe macho.......................
*********ITAENDELEA********
the Legend☆