Riwaya: Sala ya Sarah

the_legend

JF-Expert Member
Jan 14, 2019
1,405
2,000
Kamwene wakuu. Wakati tukiwa tunaendelea na riwaya ya 'Mkono wa Chuma' iliyotungwa na Alex Kileo, kwa mara nyingine napenda kuwakaribisha tena katika riwaya nyingine ya kusisimua. Riwaya hii mpya inaitwa SALA YA SARAH, mtunzi akiwa ni yule yule wa 'mkono wa chuma', yani ALEX KILEO. Twende wote kuanzia mwanzo mpaka mwisho wa riwaya hii.

Ratiba ya episodes: Kila siku muda wowote kuanzia saa 10 jioni ntakua nkiweka episodes walau mbili(2).

N.B: It's addictive

the Legend☆
 

the_legend

JF-Expert Member
Jan 14, 2019
1,405
2,000
RIWAYA : SALA YA SARAH.

MTUNZI : ALEX KILEO.

SEHEMU YA KWANZA.

UTANGULIZI.

Katika maisha tunapitia nyakati tofauti na ngumu sana, ila katika maisha yetu ya kawaida yupo wengi ambao tunaangaika kwa ajili ya kupata ridhiki tu, tunaamini katika utafutaji ili tujiepushe na njaa na matatizo mengine ambayo utatuka kwa pesa.

Pia kuna watu ambao hawajajenga ila uishi, hawajalima wala kutafuta ila wanakula, asilimia kubwa ya watu hawa uwa wamezikuta mali zilizotafutwa na babu zao au baba zao na wao hurithishwa bila kuvuja jasho, mara nyingi vitu vya mirathi uwa na migogoro, nakuapia msomaji wangu, hakuna kitu cha mirathi kisicho na migogoro hususani kikiachwa kwa mtu zaidi ya mmoja.

Riwaya yetu itagusa sana upande huo ila ndani kutakuwa na matukio yatayokuacha na taharuki za hatari, kama kawaida yangu napenda sana kusimulia vitu vya kipelelezi na mapigano ndani yake, yote yamo humu.

Riwaya hii ni kitu tu cha kubuni na wala sio simulizi ya kweli na wala haikuwahi kuandikwa sehemu yoyote ile duniani, kama itatokea kufanana na hadithi yoyote ile, basi ujue ni mawazo ya waandishi tu yamegongana na kamwe haiwezi kufanana hadithi yote.

Nawakaribisha tena wadau tue wote mwanzo mpaka mwisho wa riwaya hii.
----------------------
MWANZO.
-----------------------

Ni nyakati za alasiri jua likiwa bado halijapoa ukali wake na baadhi ya watu wakiwa katika pilika pilika za kujitafutia riziki zao kwa ajili ya kuendesha maisha yao katikati ya jiji.

Ndani ya hoteli moja kubwa na maarufu hapa mjini kulikuwa na kikao kidogo kinaendelea kati ya watu wawili, mwanaume mmoja na mwanamke mmoja, hawa watu ni ndugu, mtu na Dada yake, yaani mtoto wa mkubwa na mtoto wa mdogo.

Mwanaume anaitwa Denis Michael Dege alimaarufu alikuwa anaitwa Taita, na mwanamke anaitwa Mage Stewart Dege, ndani ya kikao kuna kitu kilikuwa kinajadiliwa, walikuwa wanajadili mirathi ambayo iliachwa na baba zao ambao walikuwa ni ndugu wa baba na mama mmoja, baba zao walishafariki na wakaacha mali nyingi ambazo walizirithi kutoka kwa baba yao.

Bahati nzuri asilimia kubwa ya mali walikuwa wameshagawana, walichokuwa wanajadili ni nyumba mbili tu ambazo zilikuwa katikati ya mji.

"Nimeshapata Mteja wa nyumba moja ile ya ghorofa" Taita aliongea kisha akagida maji yaliyokuwa katika glass,

"Anatoa shilingi ngapi?" Magreth aliuliza huku akimuangalia usoni Taita,

"Bilioni moja" Taita alijibu,

"Hapana, hiyo haitoshi, kwa sehemu ilipo ile nyumba ni bilioni mbili, nilifuatilia wizara ya ardhi na makazi na bei niliyoambiwa ni hiyo, hata wewe unajua hilo" Magreth aliongea huku akiendelea kumuangalia kaka yake huyo,

"Nilijua tu ni lazima ulete kikwazo, kwani kuna ubaya gani tukiuza hiyo nyumba bilioni moja? kwani uliijenga wewe?" Taita aliuliza kwa hasira

"Unadhani aliyeijenga angekubali kuuza kwa bei hiyo?" Magreth aliuliza huku sura yake ikiwa imejaa ujeuri,

"Kwanza unatakiwa kujua wewe ni mwanamke tu, hata tulivyogawana mali za hawali nilifanya ubinadamu tu, kihalisia wewe hutakiwi kupata kitu, mimi ndio mrithi wa mali zote" Taita aliongea na kutoa cheko la dharau,

"Mpuuzi wewe usilete mambo ya kizamani, dunia ya leo ni haki tu kwa wote" Magreth aliongea kwa hasira,

"Ebu acha ukorofi Mage, ujue Nina shida na hela?" Taita aliongea huku akitabasamu,

"Una shida gani wewe, kila kitu unacho, una majumba una hela na una vitega uchumi vya kila aina" Magreth aliongea kwa kufoka,

"Basi toa uamuzi, nyumba iuzwe au isiuzwe kwa bei hiyo?" Taita aliuliza,

"Nyumba haiuzwi kwa bei hiyo" Magreth alijibu,

"Alafu yule mume wako ndiyo anaekushauri ujinga, yaani mkikaa hamna cha maana mnachojadili zaidi ya hizi mali, tafuteni za kwenu" Taita aliongea kwa dharau, uwa hakasirikagi huyu bwana mwenye umri wa miaka thelathini na mbili, uwa anatabasamu muda wote.

"Hatujaja kuongelea familia yangu hapa, tukisema tuongelee familia basi tuanze na wewe usiye na mtoto na bado una mke na mmeoana miaka saba iliyopita" Magreth aliongea kwa hasira,

"Nadhani tumemaliza, nyumba nitaiuza kwa hiyo pesa na nitakuletea milioni mia tano, kama utazikataa nitazichukua zote" Taita aliongea na kunywa maji tena,

"Sheria zipo" Magreth aliongea kwa hasira,

"Mwisho wa majadiliano, hati zote ninazo mimi" Taita aliongea na kunyanyuka kisha akaanza kuondoka na kumuacha Dada ake akimuangalia tu mpaka alipotoka kwenye ule mlango wa hoteli ambao ulikuwa wa vioo, Taita alitoka na kuingia kwenye gari la kifahari na kuondoka zake.

Magreth aliendelea kukaa kwa muda pale hotelini huku akionekana mwenye hasira, Dada huyu ana miaka ishirini na nane tu.

Baada ya kukaa kwa muda alinyanyuka na kutoka nje ya ile hoteli na kuingia kwenye gari lake dogo la kawaida na kuondoka zake kurudi nyumbani kwake.

Magreth ni mfanyakazi wa serikali katika wizara ya madini, ana cheo cha juu kiasi, ameolewa na ana watoto wawili, wa kwanza ni wa kike anaitwa Sarah, ana miaka mitano na wa pili anaitwa Sebastian, ana miaka mitatu tu.

Magreth alirudi kwake na kuingia mpaka sebuleni, akalakiwa na mwanaye mkubwa aitwae Sarah na kumkumbatia mama yake kisha akamsalimia,

"Shuleni leo mmefundishwa nini mwanangu?" Magreth alimuuliza Sarah,

"Kusoma na kuandika" Sarah alijibu,

"Hakuna homework leo?" Magreth alimuuliza mwanae,

"Ipo" Sarah alijibu,

"Umeshakula?" Magreth aliuliza,

"Tayari mama, nimeshiba" Sarah alijibu,

"Haya, nenda mezani ukafanye homework yako" Magreth aliongea kisha akaenda moja kwa moja kwenye kochi na kumbusu mume wake aliyekuwa amekaa hapo juu ya kochi, huyu bwana anaitwa Isack Senga, ni mlemavu wa miguu, hana miguu yote miwili, ilikatwa baada ya kupata ajali ya gari.

Magreth alimfikia mume wake na kumbusu kwenye paji la uso,

"Taita anasemaje?" Isack aliuliza,

"Anataka kuuza ile nyumba ya ghorofa kwa lazima" Magreth alijibu huku akikaa kwenye kochi,

"Sio habari mbaya, anataka kuuza shilingi ngapi?" Isack aliuliza,

"Bilioni moja, aisee hiyo bei ni ya nyumba za kawaida katika eneo lile, na sio za ghorofa" Magreth alijibu,

"Kwa hiyo bei inakuwa sio sawa. Muafaka gani mmefikia?" Isack aliuliza,

"Hakuna muafaka, alichoamua ni kuuza kwa nguvu, kesho nitaongea na mwanasheria wangu" Magreth aliongea,

"Fanya hivyo, maana yule ndugu yako hana nia nzuri" Isack aliongea,

"Umeshakula mume wangu?" Magreth alimuuliza mumewe,

"Hapana, nilikuwa nakusubiri" Isack alijibu,

"Ngoja nikaoge basi" Magreth aliongea na kunyanyuka akaelekea chumbani na kumuacha mume wake akimuangalia huku akitabasamu.

Ndivyo ilivyo nyumba hii, upendo umetawala kila kona, utafikiri wameoana juzi au jana.

Baada ya saa nzima Magreth alitoka chumbani huku akiwa ameshaoga na amevaa nguo za nyumbani. Akaelekea moja kwa moja jikoni na kuchukua chakula ambacho kilikuwa kimeshaandaliwa na msichana na kazi, akakipeleka mezani na kuanza kula na mume wake huku wakiongea mawili matatu ya kifamilia.

___________
USIKU
____________

Yapata kama mida ya saa nne na nusu usiku, watoto na Dada wa kazi wakiwa tayari wamekwishalala, Magreth na Isack walikuwa wapo sebuleni wakiangalia runinga, kipindi cha dini, wakiwa wamekolea kwenye imani walisikia mlango wa mbele wa nyumba yao ukigongwa, haikuwa ajabu kwao kugongewa mlango muda huo, maana hiyo hali walishaizoea kutokana na misaada wanayotoaga kwa majirani zao, kwa hiyo usiku kama huo kupokea ugeni ukiitaji msaada ni kawaida.

Magreth akasimama na kwenda moja kwa moja kufungua mlango, alipotoa kichwa nje alikutana na mdomo wa bastola iliyokuwa imeshikwa na kijana mweupe aliyekuwa amejichora tatoo karibu mwili wake wote,

"Bila kelele wala usumbufu rudi ndani" Kijana aliongea na kumfanya Magreth ageuke taratibu na kurudi ndani na yule kijana akaingia huku bastola ikiwa mkononi, Isack alipoona hivyo nae akashtuka, hakuwa na cha kufanya maana hakuwa na miguu.

"Vipi unataka kukimbia? Kimbia mi sitokupiga risasi" Kijena mwenye tatoo aliongea kwa dhihaka huku akitabasamu, kisha akaikagua ile nyumba kwa macho kuyazungusha sebule nzima, alipolizika akapiga mluzi kwa nguvu na kufanya Magreth na Isack waendelee kushangaa bila kujua lengo la yule kijana.

Sekunde kadhaa tu baada ya ule mluzi, walishangaa kuona sebule ikivamiwa na vijana kama kumi na nyuma yao alikuwepo Taita huku akiwa ameshika makabrasha na sigara yake kubwa mdomoni na pia aliongozana na kijana mwingine nadhifu aliyevaa suti nyeusi,

"Dada mage, ni vizuri nimewakuta wote wawili maana mtatoa jibu sahihi" Taita aliongea na kujiweka kwenye kochi,

"Wewe shetani unadiriki kuniteka ndani ya nyumba yangu?" Magreth aliongea kwa uchungu huku akimuangalia Taita,

"Sijaja kujadili utekaji, nimekuja na mwanasheria wangu huyu hapa, nahitaji upige sahihi ili kuidhinisha nyumba kuuzwa" Taita aliongea huku akimuangalia yule kijana nadhifu waliyeingia nae,

"Ndio upuuzi uliokuleta huo? usitegee nitafanya hivyo" Margret aliongea kwa hasira,

"Kama ni suala la nyumba, ngoja kesho kukuche ili dada yako nae aje na mwanasheria wake ili mfikie makubaliano" Isack aliongea na Taita akamuangalia kwa jicho Kali, kisha akampa ishara yule kijana mwenye tatoo na yule kijana akakafyatua risasi iliyomkuta Isack mkono wa kushoto begani na kufanya atoe ukelele na Magreth akamkumbatia,

"Shiiiiiii hupaswi kuingilia kesi ya mali zangu na dada yangu, unatakiwa ukae kimya, nitakuondoa na mikono yako ubaki na kiwili wili tu" Taita aliongea huku akimuangalia Isack aliyekuwa Analia kwa uchungu,

"Jamani fanyeni haya, ila sitaki wanangu ndani wajue kinachoendelea" Isack aliongea huku akilia,

"Kumbe na watoto wapo?, Trigger kawalete wajomba zangu" Taita aliongea kisha yule Jamaa mwenye tatoo akaelekea vyumbani na kuanza kuwatafuta watoto, baada ya muda alirudi na watoto wawili na dada wa kazi,

"Shikamoo anko" Sarah alimuamkia Taita, masikini hakujua hata kinachoendelea,

"Marhaba, njoo anko" Taita alijibu huku akitabasamu na kumpakata Sarah na mdogo wake,

"Magreth saini wanachotaka, cha muhimu watoto wetu wabaki Salama" Isack alimwambia mkewe ambaye hakupinga, aliomba makabrasha na kusaini panapotakiwa,

"Safi sana" Taita aliongea huku akipiga makofi,

"Kinachofuata" Trigger aliuliza huku akimuangalia Taita,

"Funga kamba hao mbwa" Taita aliongea huku akisimama na alikuwa amewabeba Sarah na mdogo wake,

"Si tayari nimefanya utakacho? Kamba nifungwe za nini sasa?" Magret aliuliza lakini hakujibiwa, vijana walimfunga kamba yeye, mume wake na msichana wa kazi, kisha wakawatia vitambaa mdomoni ili wasipige kelele.

Taita akatoka nje akiwa na watoto,

"Tunafanyaje boss?"Trigger akiuliza, trigger ni yule kijana mwenye tatoo,

"Choma moto nyumba, wanatakiwa wafe" Taita aliongea huku akielekea kwenye gari na watoto,

"Tajiri eeh, huyu mtoto wa kike ni mkubwa, ana akili na anajua kinachoendelea, nae hatakiwi kuishi" Wakili alimshauri Taita,

"Kweli kabisa, kwanza atakuja kuwa msumbufu kama mama yake" Taita aliongea kisha akafungua mlango wa gari na kumtupa chini Sarah, Sarah akaanza kulia,

"Kitanzi, huyu nae kamtupe ndani, achomwe moto" Taita aliongea na kisha kijana wake mmoja aitwae kitanzi akambeba na kwenda kumtupa Sarah ndani, kisha milango yote ikafungwa kwa nje, nyumba ikamwagiwa mafuta na kuwashwa moto, nyumba yote ikashika moto,

"Tupotee" Taita alimwambia dereva wake na kisha gari ikaanza kuondoka taratibu na magari mengine waliyokuja nayo yakafuata...............

**********ITAENDELEA***********

the Legend☆
 

the_legend

JF-Expert Member
Jan 14, 2019
1,405
2,000
RIWAYA : SALA YA SARAH.

MTUNZI : ALEX KILEO.

SEHEMU YA PILI.

ILIPOISHIA...

Taita akatoka nje akiwa na watoto,

"Tunafanyaje boss?"Trigger akiuliza, trigger ni yule kijana mwenye tatoo,

"Choma moto nyumba, wanatakiwa wafe" Taita aliongea huku akielekea kwenye gari na watoto,

"Tajiri eeh, huyu mtoto wa kike ni mkubwa, ana akili na anajua kinachoendelea, nae hatakiwi kuishi" Wakili alimshauri Taita,

"Kweli kabisa, kwanza atakuja kuwa msumbufu kama mama yake" Taita aliongea kisha akafungua mlango wa gari na kumtupa chini Sarah, Sarah akaanza kulia,

"Kitanzi, huyu nae kamtupe ndani, achomwe moto" Taita aliongea na kisha kijana wake mmoja aitwae kitanzi akambeba na kwenda kumtupa Sarah ndani, kisha milango yote ikafungwa kwa nje, nyumba ikamwagiwa mafuta na kuwashwa moto, nyumba yote ikashika moto,

"Tupotee" Taita alimwambia dereva wake na kisha gari ikaanza kuondoka taratibu na magari mengine waliyokuja nayo yakafuata...............

***********ENDELEA************

Ndani ya nyumba moto ulizidi kupamba, Sarah hakuwa na uwezo wa kufanya chochote kwa maana alikuwa mdogo, hakuweza hata kusaidia kuwafungua wazazi wake kuwafungua kamba zilikuwa zimeshika miili yao. Binti wa kazi nae alikuwa ndani ila alijaribu kuwafungua zile kamba na ilishindikana, kila alipojaribu hakufanikiwa kutokana na zile kamba kufungwa kwa ustadi wa hali ya juu, hata binti wa kazi alipojaribu kwenda jikoni kuchukua kisu, ilishindikana kwa sababu huku moto ulishashika jiko lote kutokana na mtungi wa gesi kupasuka na kulipuka,

"Dada, fanya chochote uwezacho kumtoa Sarah nje, jaribu kutumia njia yoyote ili mtoke nae" Magreth aliongea huku akilia, alishakata tamaa,

"Mama ngoja nijaribu kuwafungua tena" Dada wa kazi aliongea huku nae akilia,

"Toka nje, mtoe na mtoto" Isack aliongea kwa ukali huku machozi yakimtoka, Dada wa kazi alimbeba Sarah na kuanza kuangalia njia nzuri ya kutoka, alichoamua ni kupanda juu ya ghorofa, Dada wa kazi alipanda ghorofani huku akikimbia na Sarah alikuwa mikononi mwake, alikimbia mpaka juu na kuelekea dirishani, alipofika dirishani alifungua kioo na kumshika Sarah kwa kumning'iniza huku akijishauri amtupe chini, ila alihofia huyo mtoto anaweza kupoteza maisha kama ataanguka vibaya, au anaweza kuvunjika viungo na kipindi hicho Sarah alikuwa analia sana, wakati akiendelea kuwaza hayo, tayari sehemu ya nyumba ilianza kuporomoka na tayari moto ulikuwa umeshaanza kuenea juu ya ghorofa.

Wakati binti wa kazi akiwa anajishauri dirishani, huku mtoto akiwa amemning'iniza kwa nje, tofari lilitoka juu na kumponda kichwani dada wa kazi, na yule Dada alijikuta anamuachia Sarah na kuangukia chini umbali wa ghorofa moja, yule dada aliinguka na kupoteza fahamu ungali moto ukiendelea kushika eneo lote la ghorofa la juu.

Sarah aliangukia miguu na kupepesuka na kudondokea kisogo, akanyanyuka lakini alikuwa akihisi kizungu zungu, akajitahidi kusimama akimbie, akaanza kukimbia huku akikipesuka, alijitahidi kukimbia mita hamsini tu, akajikuta ameanguka na akapoteza fahamu, hakujua tena kilichoendelea.

*************************

Asubuhi kulikucha huku vyombo vya habari vikitangaza juu ya nyumba kuungua na watu wote waliomo ndani walitangazwa wamekufa isipokuwa mtoto mmoja mdogo ambaye hali yake haikuwa nzuri na kipindi hicho alikuwa mahututi.

Hii habari ilimkuta Taita akiwa mbele ya runinga yake huku akiwa amevaa pajama ya kulalia na mezani kulikuwa na chupa ya mvinyo na kiti cha pembeni yake alikuwa amekaa yule Jamaa mweupe mwenye tatoo mwili mzima pamoja na yule jamaa aliyetambulishwa kama mwanasheria.

Huyu Jamaa mweupe mwenye kipara na tatoo mwili mzima ndiye mlinzi wa Taita, ni mtu mmoja anaemuamini sana katika masuala ya kutumia silaha za moto, ni kijana aliyeacha kazi ya jeshi baada kwenda kinyume na sheria za jeshi, jina lake ni Malick Tasi, ila hapa anatumia jina la Trigger, jina la kifyatulio risasi, ni jina alilopewa tangu akiwa jeshini, jina hili alipewa kutokana na utumiaji wake wa silaha za moto, ni mtu mbaya sana ambaye akikunyooshea bastola kwa nia ya kukudhuru, uwa harudishi chini mpaka akupate, na lazima akupate hata kama ukiwa umbali mrefe, ili mradi tu bastola iwe na uwezo wa kurusha risasi kwa kiwango kinachotakiwa, ulevi wake ni wanawake tu.

Wa pili ni huyu mwanasheria, anaitwa Harry Denui, ni mhitimu wa chuo kikuu cha maarufu uko nchini uingereza, ana shahada mbili za sheria, na walijuana na Taita baada ya mwanasheria huyu kusimamia kesi yenye utata mkubwa na upande wa huyu bwana ulishinda, ni mtu maarufu sana hapa nchini na umaarufu wake umetokana na kushinda kwa asilimia kubwa katika kesi anazozisimamia.

Leo walikutana asubuhi kwa ajili ya kupanga namna Taita atavyoweza kukusanya haki zote za dada yake ambaye ndiye Magreth na muda huu alikuwa hayupo tena duniani.

"Tatizo lililopo ni ambalo ndio kikwazo ni yule binti kama ataendelea kuwa hai" Harry aliongea na kumtupia jicho Taita,

"Lakini Trigger ulikosea, ulivyomtupia ndani yule malaya mtoto, ungemfunga na kamba kabisa" Taita alijaribu kumtupia lawama kijana wake,

"Hapana, kwa kuwa moto ulishaanza kupamba ndani ya nyumba, kama angesema amfunge kamba yule mtoto, ni lazima amgeshindwa kutokana na ule moto kuwa mkali" Harry alimtetea Trigger,

"Basi yamepita, tusilaumiane. Je si inawezekana kummaliza yule mtoto pale pale hospitali?" Taita aliuliza huku akimuangalia Trigger,

"Inawezekana boss, ni kazi ndogo tu" Trigger alijibu,

"Basi mimi nitaenda hospitali kumuangalia kama mjomba wake, nikishatoka tu unatakiwa ufanye kazi hiyo" Taita aliongea,

"Je na yule mdogo wake uliyemchukua jana, una mpango gani nae?" Harry alimuuliza Taita,

"Yule mtoto nitamfanya awe mtoto wangu, si unajua sina mtoto na vizuri katoto chenyewe ni kadogo, hakana akili, kwa hiyo nitamlea kama mwanangu na hata akiwa mkubwa hatojua lolote" Taita aliongea kwa kujiamini,

"Unakosea, hawa watoto kuna kumbukumbu ndogo uwa wanakuwa nazo, kwa hiyo atakapokuwa mkubwa anaweza akajua ukweli" Harry alimshauri Taita,

"Kwa hiyo nimuue?" Taita aliuliza,

"Hapana, unatakiwa uende hospitali umpeleke akachomwe sindano ya kufuta kumbukumbu zake zote kichwani, yaani ubongo wake uanze upya, hapo itakuwa rahisi kumfanya utakavyo" Harry alimshauri Taita,

"Hilo ni wazo zuri, wazo safi kabisa" Trigger alimuunga mkono Harry,

"Basi sawa, inabidi hili litekelezwe mapema sana" Taita aliongea,

"Haraka iwezekanavyo" Harry alijibu,

"Sasa ngoja nijitayarishe ili niende hospitali nikamuangalie huyo Malaya mtoto" Taita aliongea huku akinyanyuka na kuingia chumbani kwake.

*******************

Ndani ya jengo liliteketea kwa moto, alikuwepo askari mmoja akikagua kagua ili kuangalia anaweza kupata kitu kitakachompa mwanga wa kujua hili tukio ni mipango au ni bahati mbaya, lakini kwenye pekua yake hakuweza kupata chochote zaidi ya picha ya familia iliyoungua upande wa chini na kufanya miguu ya wahusika isionekane, akatoa miwani mieusi machoni na kuiangalia kwa muda na kuiona namna ilivyokuwa imejaa vumbi, akaipulizia pumzi ya mdomo na kuifuta kwa kutumia kitambaa cheupe kilichokuwa mfukoni kwake.

Akapiga hatua za kutoka kwenye lile jengo na kuelekea kwenye gari yake ndogo na kuingia, akawasha gari na kufungulia mziki laini na kuliondoa gari kwa mwendo wa haraka.

Hii kesi alishahisi ni kuna mtu kuteketea kwa hii nyumba, maana majirani walisema muda mchache kabla nyumba haijaungua walisikia magari yakiondoka eneo hilo, na pia katika maiti zilizokutwa hakukuwa na maiti ya mtoto mdogo wa kiume hakionekana, kwa maana hiyo huyo mtoto huenda amechukuliwa au huenda hakuwepo? na kama hakuwepo atakuwa ameenda wapi na nani?. Hayo ni baadhi ya maswali aliyojiuliza mpelelezi huyo.

Safari yake iliishia nje ya hospitali ya kifahari ya binafsi, akaegesha gari lake na kwenda moja kwa moja kwenye mlango wa wodi moja na kusimama mlangoni, aliamua kusimama mlangoni baada ya kuona madaktari wakimpatia huduma mgonjwa aliyemuhitaji, ambaye ni mtoto Sarah.

Baada ya muda madaktari waliondoka na ndani akabaki daktari mmoja, mpelelezi akaingia,

"Karibu, mtoto huyu hapa amezinduka" Daktari aliongea, inaelekea wanajuana,

"Hakuna mtu aliyekuja kumuangalia?" Mpelelezi aliuliza,

"walikuja wafanyakazi wa wizara anayofanyia kazi mama yake" Daktari alijibu,

"Wamesemaje" Mpelelezi aliuliza,

"Hakuna, kwanza kipindi wanakuja bado mtoto alikuwa hajazinduka" Daktari alijibu,

"Ameongea tokea amezinduka?" Mpelelezi aliuliza,

"Hapana" Daktari alijibu na kipindi hiki ndipo Taita alikuwa anaingia wodini, alikuwa peke yake.

Alipoingia kwanza alishtuka kumuona Sarah akiwa amezinduka, akapata wasiwasi,

"Sarah unakumbuka jana nini kilitokea" Mpelelezi aliuliza na kumfanya Sarah amuangalie Taita, hapo sasa mapigo ya moyo ya Taita yakawa yanapishana bila mpangilio, yule mpelelezi akavua miwani na kumuangalia Taita kwa jicho kali.......

********ITAENDELEA*********

*Je mpelelezi atagundua nini?

*Taita yupo matatizoni, je Sarah ataeleza kila kitu?

*na mdogo wake Sarah yupo wapi muda huu?
*Hayo yote utayafahamu kesho.

the Legend☆
 

Toa taarifa ya maudhui yasiyofaa!

Kuna taarifa umeiona humu JamiiForums na haifai kubaki mtandaoni?
Fanya hivi...

Umesahau Password au akaunti yako?

Unapata ugumu kuikumbuka akaunti yako? Unakwama kuanzisha akaunti?
Contact us

Similar Discussions

Top Bottom