Riwaya: Sala ya Sarah

Riwaya: Sala ya Sarah

RIWAYA : SALA YA SARAH

MTUNZI : ALEX KILEO.

SEHEMU YA KUMI NA SITA.

ILIPOISHIA.

Dereva wa gari ndogo akashusha kioo, alikuwa ni yule dalali wa Sarah, vijana wa Taita wakamsalimia,

"Unaweza kutufungulia milango kuna mtu tunamtafuta" Kijana wa Taita aliongea huku akimuangalia Dalali,

"Hakuna mtu zaidi yangu ndani ya gari" Dalali alijibu baada ya kufikiria kwa muda, vijana wa Taita wakamtilia shaka,

"Basi fungua milango" kijana mmoja akaongea kwa hasira,

"Hakuna mtu, si nimeshawaambia" Dalali aliongea,

"Mbona mnambeleleza sana" kijana mwingine aliongea huku akimuwekea bastola usawa wa kichwa yule dereva,

"Haya fungua milango" Kijana aliongea huku akiwa hana mzaha hata kidogo, dalali akalegeza kamba, aka unlock milango yote, kisha kwa pupa vijana wa Taita wakakimbilia kufungua milango ya nyuma ya ile gari ya dalali.........

************ENDELEA**************

Baada ya kufungua milango hawakukuta mtu ndani ya gari,

"Niliwaambia nipo peke yangu, mbona mnanichelewesha? kwanza nyie ni wakina nani, mbona hamjajitambulisha?" Dalali aliuliza kwa kulalamika lakini hakujibiwa kitu, vijana wa Taita walikuwa bize na upekuzi wa gari.

Walipekua na walipojiridhisha ndipo wakamruhusu dalali aondoke, Dalali aliondoka huku akinung'unika sana, alihisi hakutendewa haki kabisa.

Vijana wa Taita wakaendelea kusimama pale huku wakiendelea na kazi ya kukagua kila chombo cha usafiri kinachoingia na kutoka eneo lile.

**********_**

Tekso akiwa na vijana wawili walifanikiwa kufika mpaka guest ile aliyokuwa anaishi Sarah, waliweza kufika kaunta na kumkuta dada wa mapokezi akisugua kucha zake,

"Karibuni kaka zangu, vyumba vipo" Dada wa mapokezi aliongea kwa uchangamfu,

"Hapana hatuna shida na vyumba, kuna dada tunamtafuta anaishi hapa" Tekso aliongea huku akimtazama Dada wa mapokezi aliyekuwa na mwili mkubwa, uswahilini tunawaita vibonge,

"Yukoje?" Dada wa mapokezi akauliza,

"Mwembamba na ana kimo cha wastani, mweupe" Tekso alitoa jibu kulingana na maelezo ya Taita,

"Ameondoka muda sio Mrefu" Dada wa mapokezi alijibu,

"Atarudi muda gani?" Tekso aliuliza,

"Yaani ameondoka moja kwa moja, amesema anaenda kuishi kwa rafiki yake kwa kuwa kuishi hapa ni gharama. Ni ndugu yenu kwani?" Dada wa mapokezi aliuliza,

"Ameondoka muda gani?" Tekso aliuliza huku akiwa amekata tamaa,

"Sasa hivi tu, yaani hana hata dakika tano" Dada wa mapokezi alijibu na kufanya Tekso awaze kwa muda,

"Ameondoka na usafiri?" Tekso aliuliza,

"Ndio, amechukuliwa na gari ndogo nyeusi" Dada wa mapokezi alijibu na kufanya Tekso akumbuke kuwa alipishana na gari ndogo nyeusi iliyokuwa na vioo vya Giza (tinted),

"Ebu wapigie simu wenzako waulize kama wameiona hiyo gari pale njiani" Tekso aliongea huku akimgeukia kijana mmoja waliyeambatana nae, yule kijana akatoa siku mfukoni na kubonyeza vitufe kadhaa kisha akaiweka simu sikioni, baada ya sekunde akaanza kuongea na upande wa pili wa siku na kisha akakata,

"Hiyo gari wameiona ila wanadai ndani alikuwepo mtu mmoja tu, mwanaume" Kijana aliyeongea na simu alimpa taarifa Tekso,

"Dah, kwa hiyo inawezekana huyo dada bado yupo mtaa huu huu?" Tekso aliwauliza wenzake,

"Kama hawajamuona basi inawezekana yupo" Kijana mmoja alijibu,

"Dada unaweza kunipeleka chumba alichokuwa anahishi?" Tekso alimuuliza Dada wa mapokezi,

"Lakini kaka yangu hamjajitambulisha" Dada wa mapokezi aliongea,

"Utatujua baadae, nipeleke katika chumba alichokuwa anaishi" Tekso aliongea na kisha Dada wa mapokezi akatoka kaunta na kuelekea moja kwa moja katika chumba alichokuwa akikaa Saraha na kukifungua mlango kisha akaingia na nyuma yake alikuwa Tekso, baada ya kuingia ndani Tekso akaanza kukichunguza kile chumba kama ataambulia chochote, ila hakubagatika kupata kitu chochote, akatoka nje huku akifuatwa na dada wa mapokezi.

Walielekea mpaka kaunta,

"Unaweza kutusaidia jina lake?" Tekso alimuuliza yule dada, na kufanya yule dada achukue daftari lake la orodha ya wageni walichukua vyumba na kuanza kupekua kutafuta jina la Sarah ila hakuliona, akarudia tena pia hakuona,

"Jina lake halionekani" Dada wa mapokezi aliongea,

"Kwani wewe hulijui jina lake?" Tekso alimuuliza,

"Silijui" Dada wa mapokezi alijibu na kufanya Tekso amuangalie tu bila kuongea kitu, kisha akawaamuru vijana wake waondoke eneo hilo.

Tekso na vijana wake wakaenda mpaka walipokuwa wenzao na gari lao, wakaongea maneno mawili matatu kisha wakaingia kwenye gari na kuondoka zao.

******************

Kipindi hicho chote Sarah alikuwa ameshafika mbali sana, kumbe hakuingia ndani ya gari la dalali, badala yake Sarah alimuuliza dalali kama kuna njia nyingine ya kuondoka eneo lile tofauti na hiyo inayotumiwa kila siku, ndipo dalali aliposema kuwa njia ipo ila ni ya watembea kwa miguu tu, vyombo vya moto haviwezi kupita kwa maana mbele kuna mto umekatiza na hakuna daraja kubwa, kuna kadaraja kadogo tu kwa ajili ya watu.

Sarah ndipo akachagua kupita njia hiyo, alifanya hivyo baada kuhisi huenda vijana wa Taita wanaweza kusambazwa njia kubwa na ikawa kazi kwake kutoka salama eneo hilo. Sarah akaamua kupita uko huku akimwambia dalali watawasiliana baada ya muda mchache.

Sarah alifanikiwa kutembea mpaka alipofika eneo lenye watu wengi, akachukua simu yake na kumpigia dalali ili amfuate, haikuchukua muda Mrefu sana dalali akafika eneo lile na kisha sarah akaingia ndani ya gari, tena siti za mbele,

"Kwanini ulipita ile njia?" Dalali alimuuliza Sarah,

"Kuna kitu nilienda kununua, maana nilielekezwa kinapatikana mitaa ile" Sarah alimdanganya dalali,

"Basi mwenzako mbele nilikutana na maaskari sijui wale, wakanisimamisha, inaelekea kuna mtu wanamtafuta" Dalali aliongea na kufanya Sarah ashtuke, ila hukuonesha mshtuko wake,

"Huenda kuna kibaka au jambazi wanamtafuta, huenda waliambiwa yupo mtaa ule" Sarah aliongea huku akiuficha mshtuko wake,

"Wasumbufu tu wale" Dalali aliongea,

"Waache wafanye kazi" Sarah aliongea na kisha yakafuata maongezi mengine ya kawaida mpaka walipofika kwenye hiyo nyumba ambayo Sarah ameenda kuiangalia.

Wakashuka na kisha Dalali akaenda kumchukua mwenye nyumba, hakuwa mbali na pale,

Kipindi dalali ameenda kumchukua mwenye nyumba, Sarah alitumia muda huo kuikagua ile nyumba kwa kuizunguka, baada ya dakika tano dalali alifika huku akiwa ameongozana na mwenye nyumba,

"Karibu binti" Mwenye nyumba aliongea huku akimpa mkono Sarah,

"Asante, shikamoo baba" Sarah alimsalimia huku akimpa mkono,

"Marahaba binti, nyumba umeiona?" Mwenye nyumba alimuuliza Sarah,

"Nimeiona kwa nje, nimeridhika ila bado sijajua kwa ndani ikoje?" Sarah alijibu,

"Twendeni ndani ili apaone" Mwenye nyumba alimwambia dalali kisha wakaanza kuelekea ndani ya nyumba, walifika mlangoni kisha mwenye nyumba akafungua mlango na wote wakaingia, Sarah akaanza kuikagua ile nyumba, alikagua kila chumba na kila kitu ndani ya ile nyumba, akaridhika nayo.

"Nimeridhika Mzee wangu, je naweza kuipata leo, yaani tukauziana na kumalizana leo leo?" Sarah alimuuliza mwenye nyumba,

"Mbona haraka hivyo?" Mwenye nyumba aliuliza kwa mshangao,

"Nahitaji leo Mzee, naomba tumalizane tu" Sarah aliongea kwa mkazo,

"Sawa, twende kwa mwenyekiti wa kijiji na pia unatakiwa na mashahidi wawili" Mwenye nyumba aliongea,

.

"Shahidi yupo mmoja, huyu dalali, sina ndugu Tanzania" Sarah aliongea na kufanya wenzie wamtolee macho,

"Wewe ni mgeni?" Mwenye nyumba aliuliza,

"Mgeni, sina ndugu wala sina rafiki" Sarah alijibu,

"Umetoka nchi gani?" Mwenye nyumba aliuliza,

"Uingereza" Sarah alijibu,

"Mbona unaongea kiswahili safi?" Dalali aliuliza,

"Nilijifunza na pia Nina kidogo hapa nchini kwenu" Sarah alijibu,

"Sawa mama nimekuelewa, sasa itabidi uwe na kila kitu ili tufanikishe kuuziana hii nyumba, hata ikishindikana kufikia makubaliano leo, basi kesho naamini tutamalizana" Mwenye nyumba aliongea,

"Itabidi iwezekane leo, maana sina pa kulala" Sarah aliongea na kufanya wenzake wacheke wakidhani utani wakati mwenzao alidhamiria.

Baada ya hapo wakatoka mpaka kwa mwenyekiti wa mtaa na kuanza hatua za kuuziana nyumba, ingawa kulikuwa na hatua nyingi na ngumu, ila baada ya masaa matatu kila kitu kilienda sawa, Sarah akachukua nyumba yake, kisha akaenda mjini na kununua samani za ndani na kuchukua vijana watano kwa ajili ya kumsaidia kufanya usafi.

Baada ya masaa mawili kila kitu kilikuwa safi, nyumba ilinoga, na ikawa ndio makazi rasmi ya Sarah.

Akawalipa vijana wale kisha wakaondoka zao, yeye akaelekea bafuni kuoga, alipomaliza akaingia chumbani kwake na kuvaa suruali nyeusi na fulana nyeusi, usoni alivaa miwani yenye kioo cheupe, hiyo ilikuwa yapata saa kumi na mbili jioni.

************************

Mishale ya saa moja jioni, Taita na jopo lake la watu muhimu walikuwa wanaingia vin hotel, moja kwa moja wakaelekea kwenye chumba kidogo cha mikutano kwa ajili ya kujadili shambulio la bomu lilimuua kijana wao mmoja.

Mwenyekiti wa kikao alikuwa Taita, ila kabla hawajafungua rasmi kikao, mlango wa kile chumba ulifunguliwa na mlangoni alisimama binti akiwa na nguo nyeusi, Taita na wenzake wakabaki wamemtolea macho...............

**********ITAENDELEA**********

the Legend☆
 
RIWAYA : SALA YA SARAH.

MTUNZI : ALEX KILEO.

SEHEMU YA KWANZA.

UTANGULIZI.

Katika maisha tunapitia nyakati tofauti na ngumu sana, ila katika maisha yetu ya kawaida yupo wengi ambao tunaangaika kwa ajili ya kupata ridhiki tu, tunaamini katika utafutaji ili tujiepushe na njaa na matatizo mengine ambayo utatuka kwa pesa.

Pia kuna watu ambao hawajajenga ila uishi, hawajalima wala kutafuta ila wanakula, asilimia kubwa ya watu hawa uwa wamezikuta mali zilizotafutwa na babu zao au baba zao na wao hurithishwa bila kuvuja jasho, mara nyingi vitu vya mirathi uwa na migogoro, nakuapia msomaji wangu, hakuna kitu cha mirathi kisicho na migogoro hususani kikiachwa kwa mtu zaidi ya mmoja.

Riwaya yetu itagusa sana upande huo ila ndani kutakuwa na matukio yatayokuacha na taharuki za hatari, kama kawaida yangu napenda sana kusimulia vitu vya kipelelezi na mapigano ndani yake, yote yamo humu.

Riwaya hii ni kitu tu cha kubuni na wala sio simulizi ya kweli na wala haikuwahi kuandikwa sehemu yoyote ile duniani, kama itatokea kufanana na hadithi yoyote ile, basi ujue ni mawazo ya waandishi tu yamegongana na kamwe haiwezi kufanana hadithi yote.

Nawakaribisha tena wadau tue wote mwanzo mpaka mwisho wa riwaya hii.
----------------------
MWANZO.
-----------------------

Ni nyakati za alasiri jua likiwa bado halijapoa ukali wake na baadhi ya watu wakiwa katika pilika pilika za kujitafutia riziki zao kwa ajili ya kuendesha maisha yao katikati ya jiji.

Ndani ya hoteli moja kubwa na maarufu hapa mjini kulikuwa na kikao kidogo kinaendelea kati ya watu wawili, mwanaume mmoja na mwanamke mmoja, hawa watu ni ndugu, mtu na Dada yake, yaani mtoto wa mkubwa na mtoto wa mdogo.

Mwanaume anaitwa Denis Michael Dege alimaarufu alikuwa anaitwa Taita, na mwanamke anaitwa Mage Stewart Dege, ndani ya kikao kuna kitu kilikuwa kinajadiliwa, walikuwa wanajadili mirathi ambayo iliachwa na baba zao ambao walikuwa ni ndugu wa baba na mama mmoja, baba zao walishafariki na wakaacha mali nyingi ambazo walizirithi kutoka kwa baba yao.

Bahati nzuri asilimia kubwa ya mali walikuwa wameshagawana, walichokuwa wanajadili ni nyumba mbili tu ambazo zilikuwa katikati ya mji.

"Nimeshapata Mteja wa nyumba moja ile ya ghorofa" Taita aliongea kisha akagida maji yaliyokuwa katika glass,

"Anatoa shilingi ngapi?" Magreth aliuliza huku akimuangalia usoni Taita,

"Bilioni moja" Taita alijibu,

"Hapana, hiyo haitoshi, kwa sehemu ilipo ile nyumba ni bilioni mbili, nilifuatilia wizara ya ardhi na makazi na bei niliyoambiwa ni hiyo, hata wewe unajua hilo" Magreth aliongea huku akiendelea kumuangalia kaka yake huyo,

"Nilijua tu ni lazima ulete kikwazo, kwani kuna ubaya gani tukiuza hiyo nyumba bilioni moja? kwani uliijenga wewe?" Taita aliuliza kwa hasira

"Unadhani aliyeijenga angekubali kuuza kwa bei hiyo?" Magreth aliuliza huku sura yake ikiwa imejaa ujeuri,

"Kwanza unatakiwa kujua wewe ni mwanamke tu, hata tulivyogawana mali za hawali nilifanya ubinadamu tu, kihalisia wewe hutakiwi kupata kitu, mimi ndio mrithi wa mali zote" Taita aliongea na kutoa cheko la dharau,

"Mpuuzi wewe usilete mambo ya kizamani, dunia ya leo ni haki tu kwa wote" Magreth aliongea kwa hasira,

"Ebu acha ukorofi Mage, ujue Nina shida na hela?" Taita aliongea huku akitabasamu,

"Una shida gani wewe, kila kitu unacho, una majumba una hela na una vitega uchumi vya kila aina" Magreth aliongea kwa kufoka,

"Basi toa uamuzi, nyumba iuzwe au isiuzwe kwa bei hiyo?" Taita aliuliza,

"Nyumba haiuzwi kwa bei hiyo" Magreth alijibu,

"Alafu yule mume wako ndiyo anaekushauri ujinga, yaani mkikaa hamna cha maana mnachojadili zaidi ya hizi mali, tafuteni za kwenu" Taita aliongea kwa dharau, uwa hakasirikagi huyu bwana mwenye umri wa miaka thelathini na mbili, uwa anatabasamu muda wote.

"Hatujaja kuongelea familia yangu hapa, tukisema tuongelee familia basi tuanze na wewe usiye na mtoto na bado una mke na mmeoana miaka saba iliyopita" Magreth aliongea kwa hasira,

"Nadhani tumemaliza, nyumba nitaiuza kwa hiyo pesa na nitakuletea milioni mia tano, kama utazikataa nitazichukua zote" Taita aliongea na kunywa maji tena,

"Sheria zipo" Magreth aliongea kwa hasira,

"Mwisho wa majadiliano, hati zote ninazo mimi" Taita aliongea na kunyanyuka kisha akaanza kuondoka na kumuacha Dada ake akimuangalia tu mpaka alipotoka kwenye ule mlango wa hoteli ambao ulikuwa wa vioo, Taita alitoka na kuingia kwenye gari la kifahari na kuondoka zake.

Magreth aliendelea kukaa kwa muda pale hotelini huku akionekana mwenye hasira, Dada huyu ana miaka ishirini na nane tu.

Baada ya kukaa kwa muda alinyanyuka na kutoka nje ya ile hoteli na kuingia kwenye gari lake dogo la kawaida na kuondoka zake kurudi nyumbani kwake.

Magreth ni mfanyakazi wa serikali katika wizara ya madini, ana cheo cha juu kiasi, ameolewa na ana watoto wawili, wa kwanza ni wa kike anaitwa Sarah, ana miaka mitano na wa pili anaitwa Sebastian, ana miaka mitatu tu.

Magreth alirudi kwake na kuingia mpaka sebuleni, akalakiwa na mwanaye mkubwa aitwae Sarah na kumkumbatia mama yake kisha akamsalimia,

"Shuleni leo mmefundishwa nini mwanangu?" Magreth alimuuliza Sarah,

"Kusoma na kuandika" Sarah alijibu,

"Hakuna homework leo?" Magreth alimuuliza mwanae,

"Ipo" Sarah alijibu,

"Umeshakula?" Magreth aliuliza,

"Tayari mama, nimeshiba" Sarah alijibu,

"Haya, nenda mezani ukafanye homework yako" Magreth aliongea kisha akaenda moja kwa moja kwenye kochi na kumbusu mume wake aliyekuwa amekaa hapo juu ya kochi, huyu bwana anaitwa Isack Senga, ni mlemavu wa miguu, hana miguu yote miwili, ilikatwa baada ya kupata ajali ya gari.

Magreth alimfikia mume wake na kumbusu kwenye paji la uso,

"Taita anasemaje?" Isack aliuliza,

"Anataka kuuza ile nyumba ya ghorofa kwa lazima" Magreth alijibu huku akikaa kwenye kochi,

"Sio habari mbaya, anataka kuuza shilingi ngapi?" Isack aliuliza,

"Bilioni moja, aisee hiyo bei ni ya nyumba za kawaida katika eneo lile, na sio za ghorofa" Magreth alijibu,

"Kwa hiyo bei inakuwa sio sawa. Muafaka gani mmefikia?" Isack aliuliza,

"Hakuna muafaka, alichoamua ni kuuza kwa nguvu, kesho nitaongea na mwanasheria wangu" Magreth aliongea,

"Fanya hivyo, maana yule ndugu yako hana nia nzuri" Isack aliongea,

"Umeshakula mume wangu?" Magreth alimuuliza mumewe,

"Hapana, nilikuwa nakusubiri" Isack alijibu,

"Ngoja nikaoge basi" Magreth aliongea na kunyanyuka akaelekea chumbani na kumuacha mume wake akimuangalia huku akitabasamu.

Ndivyo ilivyo nyumba hii, upendo umetawala kila kona, utafikiri wameoana juzi au jana.

Baada ya saa nzima Magreth alitoka chumbani huku akiwa ameshaoga na amevaa nguo za nyumbani. Akaelekea moja kwa moja jikoni na kuchukua chakula ambacho kilikuwa kimeshaandaliwa na msichana na kazi, akakipeleka mezani na kuanza kula na mume wake huku wakiongea mawili matatu ya kifamilia.

___________
USIKU
____________

Yapata kama mida ya saa nne na nusu usiku, watoto na Dada wa kazi wakiwa tayari wamekwishalala, Magreth na Isack walikuwa wapo sebuleni wakiangalia runinga, kipindi cha dini, wakiwa wamekolea kwenye imani walisikia mlango wa mbele wa nyumba yao ukigongwa, haikuwa ajabu kwao kugongewa mlango muda huo, maana hiyo hali walishaizoea kutokana na misaada wanayotoaga kwa majirani zao, kwa hiyo usiku kama huo kupokea ugeni ukiitaji msaada ni kawaida.

Magreth akasimama na kwenda moja kwa moja kufungua mlango, alipotoa kichwa nje alikutana na mdomo wa bastola iliyokuwa imeshikwa na kijana mweupe aliyekuwa amejichora tatoo karibu mwili wake wote,

"Bila kelele wala usumbufu rudi ndani" Kijana aliongea na kumfanya Magreth ageuke taratibu na kurudi ndani na yule kijana akaingia huku bastola ikiwa mkononi, Isack alipoona hivyo nae akashtuka, hakuwa na cha kufanya maana hakuwa na miguu.

"Vipi unataka kukimbia? Kimbia mi sitokupiga risasi" Kijena mwenye tatoo aliongea kwa dhihaka huku akitabasamu, kisha akaikagua ile nyumba kwa macho kuyazungusha sebule nzima, alipolizika akapiga mluzi kwa nguvu na kufanya Magreth na Isack waendelee kushangaa bila kujua lengo la yule kijana.

Sekunde kadhaa tu baada ya ule mluzi, walishangaa kuona sebule ikivamiwa na vijana kama kumi na nyuma yao alikuwepo Taita huku akiwa ameshika makabrasha na sigara yake kubwa mdomoni na pia aliongozana na kijana mwingine nadhifu aliyevaa suti nyeusi,

"Dada mage, ni vizuri nimewakuta wote wawili maana mtatoa jibu sahihi" Taita aliongea na kujiweka kwenye kochi,

"Wewe shetani unadiriki kuniteka ndani ya nyumba yangu?" Magreth aliongea kwa uchungu huku akimuangalia Taita,

"Sijaja kujadili utekaji, nimekuja na mwanasheria wangu huyu hapa, nahitaji upige sahihi ili kuidhinisha nyumba kuuzwa" Taita aliongea huku akimuangalia yule kijana nadhifu waliyeingia nae,

"Ndio upuuzi uliokuleta huo? usitegee nitafanya hivyo" Margret aliongea kwa hasira,

"Kama ni suala la nyumba, ngoja kesho kukuche ili dada yako nae aje na mwanasheria wake ili mfikie makubaliano" Isack aliongea na Taita akamuangalia kwa jicho Kali, kisha akampa ishara yule kijana mwenye tatoo na yule kijana akakafyatua risasi iliyomkuta Isack mkono wa kushoto begani na kufanya atoe ukelele na Magreth akamkumbatia,

"Shiiiiiii hupaswi kuingilia kesi ya mali zangu na dada yangu, unatakiwa ukae kimya, nitakuondoa na mikono yako ubaki na kiwili wili tu" Taita aliongea huku akimuangalia Isack aliyekuwa Analia kwa uchungu,

"Jamani fanyeni haya, ila sitaki wanangu ndani wajue kinachoendelea" Isack aliongea huku akilia,

"Kumbe na watoto wapo?, Trigger kawalete wajomba zangu" Taita aliongea kisha yule Jamaa mwenye tatoo akaelekea vyumbani na kuanza kuwatafuta watoto, baada ya muda alirudi na watoto wawili na dada wa kazi,

"Shikamoo anko" Sarah alimuamkia Taita, masikini hakujua hata kinachoendelea,

"Marhaba, njoo anko" Taita alijibu huku akitabasamu na kumpakata Sarah na mdogo wake,

"Magreth saini wanachotaka, cha muhimu watoto wetu wabaki Salama" Isack alimwambia mkewe ambaye hakupinga, aliomba makabrasha na kusaini panapotakiwa,

"Safi sana" Taita aliongea huku akipiga makofi,

"Kinachofuata" Trigger aliuliza huku akimuangalia Taita,

"Funga kamba hao mbwa" Taita aliongea huku akisimama na alikuwa amewabeba Sarah na mdogo wake,

"Si tayari nimefanya utakacho? Kamba nifungwe za nini sasa?" Magret aliuliza lakini hakujibiwa, vijana walimfunga kamba yeye, mume wake na msichana wa kazi, kisha wakawatia vitambaa mdomoni ili wasipige kelele.

Taita akatoka nje akiwa na watoto,

"Tunafanyaje boss?"Trigger akiuliza, trigger ni yule kijana mwenye tatoo,

"Choma moto nyumba, wanatakiwa wafe" Taita aliongea huku akielekea kwenye gari na watoto,

"Tajiri eeh, huyu mtoto wa kike ni mkubwa, ana akili na anajua kinachoendelea, nae hatakiwi kuishi" Wakili alimshauri Taita,

"Kweli kabisa, kwanza atakuja kuwa msumbufu kama mama yake" Taita aliongea kisha akafungua mlango wa gari na kumtupa chini Sarah, Sarah akaanza kulia,

"Kitanzi, huyu nae kamtupe ndani, achomwe moto" Taita aliongea na kisha kijana wake mmoja aitwae kitanzi akambeba na kwenda kumtupa Sarah ndani, kisha milango yote ikafungwa kwa nje, nyumba ikamwagiwa mafuta na kuwashwa moto, nyumba yote ikashika moto,

"Tupotee" Taita alimwambia dereva wake na kisha gari ikaanza kuondoka taratibu na magari mengine waliyokuja nayo yakafuata...............

**********ITAENDELEA***********

the Legend☆
khaaa

Sent using Jamii Forums mobile app
 
RIWAYA : SALA YA SARAH

MTUNZI : ALEX KILEO.

SEHEMU YA KUMI NA SABA.

ILIPOISHIA.

Mishale ya saa moja jioni, Taita na jopo lake la watu muhimu walikuwa wanaingia vin hotel, moja kwa moja wakaelekea kwenye chumba kidogo cha mikutano kwa ajili ya kujadili shambulio la bomu lilimuua kijana wao mmoja.

Mwenyekiti wa kikao alikuwa Taita, ila kabla hawajafungua rasmi kikao, mlango wa kile chumba ulifunguliwa na mlangoni alisimama binti akiwa na nguo nyeusi, Taita na wenzake wakabaki wamemtolea macho...............

************ENDELEA************

Ila huyu aliyesimama mlangoni hakuvaa suruali na fulana, alivaa suti ya kike nyeusi, alikuwa ni muhudumu wa pale Vin hotel,

"Samahanini, hamuhitaji vinywaji?" Muhudumu aliwauliza huku akiwa amesimama pale pale mlangoni,

"Kwa sasa hatuhitaji, tutakuita tukihitaji" Taita aliongea na kumfanya yule dada ageuke na kuondoka.

Ndani ya chumba cha kikao walikuwepo watu sita tu, yaani Taita mwenyewe, Trigger, Harry, Dula ambaye hufahamika kama strategic na Toisa.

Niwakumbushe tu kuwa huyu Strategic ni mtaalam wa mipango na mbinu za kumuingilia adui, wakati Toisa ni mjanja mjanja wa kupenya penya na kumuadaa adui.

"Kilichopo mbele yetu mnakijua, ni kuhusu huyu adui ambaye hatujui lengo lake ni nini hasa, au kuna mtu ana uadui na mtu kati yetu?" Taita aliuliza huku akiwatazama wenzake ambao walikuwa kimya,

"Ukimya wenu una maanisha kuwa hakuna mtu mwenye adui, sasa huyu mtu atakuwa anataka nini kwetu?" Taita alitupa swali jingine,

"Labda tukuulize wewe, huna adui ambaye hatumjui?" Harry alimtupia swali Taita,

"Ujue ukiwa na maendeleo huwezi kukosa maadui, sasa inawezekana maadui wapo ila bado sijawatambua" Taita alijibu,

"Lakini huyo adui mnayemzungumzia ni tofauti sana, kama mmesema alishajionesha zaidi ya mara moja, basi huyo mtu sio wa masihara hata kidogo, anajiamini" Strategic aliongea na kutabasamu kidogo,

"Ukitoa kujiamini pia inaonekana anafanya haya matukio kwa akili na mipango ya kutosha, maana anajua kabisa kuwa baada ya kumfanyia kitu adui na matokeo ambayo yatachukuliwa na adui" Tekso aliongea,

"Sasa kilichotuleta hapa sio kumzungumzia, ila ni nini tufanye ili tumtie mikononi" Trigger aliongea baada ya kuhisi wenzake wanatoka nje ya mada,

"Ni lazima tujue tabia zake ili tupate mbinu za kumuingilia" Strategic alimjibu Trigger,

"Sasa kwa tabia zake hizo chache mlizozijua, umepata jibu gani la kumuingilia?" Trigger aliuliza huku akimtupia jicho Strategic,

"Kabla hatujapata mbinu za kumuingilia, ni lazima tumjue yeye kwanza, sio juu juu kama sasa hivi, ni lazima tumjue hata kwa kumuhisi alafu ndio tutafute mbinu za kumjua vizuri" Strategic alijibu na kumfanya Trigger acheke,

"Hiyo njia ni ngumu sana" Trigger aliongea huku akicheka,

"Kwa maelezo ya dada wa guest, anadai aliondoka na gari ndogo nyeusi, kwanini msingemuuliza huyo dada kama anaifahamu hiyo gari?" Strategic aliuliza huku akimgeukia Tekso,

"Isingesaidia" Tekso alijibu,

"Nadhani ingeweza kusaidia endapo kama huyo mfanyakazi wa guest anaifahamu hiyo gari, ni swali muhimu hilo alilouliza bwana strategic" Harry aliongea,

"Kweli, nadhani mlitakiwa mmuulize huyo dada wa guest" Taita nae aliunga mkono,

"Na kama halijui hilo gari?" Tekso aliuliza,

"Basi tutaangalia namna nyingine" Taita alijibu,

"Na pia Mzee unadai huyo binti ameshawahi kukuletea zawadi, ingekuwa vizuri kama tungepata alama za vidole vyake" Strategic aliongea huku akimtazama Taita,

"Kwenye lile box ni ngumu kupata alama zake, maana nimelishika shika sana, mtakuta alama za vidole vyangu tu" Taita alijibu,

"Basi kesho asubuhi shughuli ianzie pale guest, Tekso utaenda mapema" Trigger aliongea huku akimtazama Tekso,

"Sawa mkuu" Tekso alijibu ingawa hakuamini kama hiyo itamsaidia kwa maana katika lile gari hawakumkuta mtu mwingine zaidi ya dereva.

" kwa leo kikao kiishie hapa, kama Tekso atakosa jibu kesho, basi tutarudi tena hapa kesho, na hata akipata tutarudi tena kesho" Taita aliongea,

"Naamini majibu yatakuja mazuri" Strategic aliongea,

"Acha tuamini hivyo" Taita alijibu huku akiinuka katika kiti chake,

"Unaelekea wapi muda huu?" Harry alimuuliza Taita,

"Naenda kupata kinywaji kidogo na kuangalia wafanyakazi wa hapa wana mpya gani, alafu nitaondoka" Taita alijibu huku akielekea nje na kufanya wenzake nao waanze kuondoka mmoja mmoja.

Kila mtu alitoka na kuelekea katika gari lake na kuondoka.

Harry yeye alipotoka aliingia kwenye gari aliingia kwenye gari lake na kubonyeza simu yake kwa muda kisha akawasha gari na kuliondoa taratibu, ila nyuma yake kulikuwa na gari ndogo inamfuata, ilikuwa gari ya dalali.

Harry aliendesha kwa muda gari lake akahisi kuna gari inamfuata kwa nyuma, akapata wasiwasi na kukunja barabara iliyoingia mitaani na kuiacha barabara kuu, ile gari iliyokuwa inamfuata ikapita barabara kuu na wala haikumfuata tena.

Harry akarudi barabara kuu na kushika njia ya kwenda nyumbani kwake bila kuiona tena ile gari, harry alifika getini na kupiga honi, geti likafunguliwa na mlinzi, Harry akaingiza gari ndani na kushuka, akamuuliza mlinzi habari za pale na mlinzi akajibu ni nzuri.

Harry akaingia ndani kwake, alipofika sebuleni tu akashtuka, hakukuta hali si ya kawaida, alimkuta Sarah ndani, ya juu ya kochi akiwa amekunja nne, usoni alivaa kinyago kilichoanzia puani na kushuka chini mpaka kidevuni kama mkionacho kwenye jalada la riwaya yetu.

Hapo mke wa Harry alikuwa amelazwa sakafuni huku amefungwa kamba mikononi na mdomoni alibandikwa gundi ya karatasi iliyomzuia kupiga kelele.

Sarah alikuwa amekunja nne, mkono wa kulia alishika bastola ndogo ya rangi ya dhahabu na mkono wa kushoto alishika bilauri ya kioo iliyokuwa na maji,

"Karibu mwenyeji wangu, ila leo wewe utakuwa mgeni kwa muda" Sarah aliongea kisha akatabasamu, bahati mbaya Harry hakuweza kuliona hilo tabasamu kutokana na kinyago alichovaa Sarah, Harry alipigwa na mshangao tu huku hakiwa hajui afanye nini,

"Sema unataka nini, iache familia yangu nitakupa utakacho" Harry alijikaza na kuongea,

"Utanipa utakacho? una uhakika?" Sarah aliuliza huku akimkazia macho,

"Ndio, sema unataka nini?" Harry aliuliza kwa kujiamini ila akiwa na wasiwasi,

"Nataka roho yako" Sarah aliongea huku akiwa bado anamuangalia na kumfanya Harry akune kichwa, hakutegemea kusikia kitu kama hicho,

"Nipe sasa ili niiache familia yako" Sarah aliongea baada ya kumuona Harry amekosa cha kuongea,

"Taja kitu chochote cha thamani tofauti na roho yangu na familia yangu" Harry alipata cha kuongea,

"Ni kipi rahisi kwako, kuchukua roho ya mtu au kutafuta pesa?" Sarah alimtupia swali Harry,

"Kutafuta pesa" Harry alijibu huku akitetemeka,

"Umejibu vizuri, ila kuna kipindi hukuwahi kufikiria kitu kama hicho" Sarah aliongea huku akisimama,

"Unamaanisha nini kusema hivyo?" Harry aliuliza,

"Maana yangu utaijua, utaijua siku nitayoamua kuja rasmi kwa ajili yako, leo sikuja kwa ajili yako" Sarah aliongea huku akiwa anazunguka zunguka ndani ya sebule ya Harry,

"Naomba uiache familia yangu" Harry aliongea,

"Kaa kwenye kochi kwanza" Sarah alimwambia Harry aliyekuwa amesimama, Harry akaenda kukaa kwenye kochi,

"Una elimu gani?" Sarah alimuuliza Harry,

"Mimi ni mwanasheria" Harry alijibu na kufanya Sarah atoe kicheko kwa sauti ya wastani,

"Sijakuuliza wewe ni nani? haya tuachane na hayo, nataka kuondoka sasa" Sarah aliongea huku akimuangalia,

"Sawa Dada, naomba utuache Salama" Harry aliongea huku akipiga magoti,

"Nakuacha Salama, ila una vitu viwili vya kuchagua, upo tayari?" Sarah alimuuliza Harry,

"Nipo tayari ili mradi visiwe na athari kwenye familia yangu" Harry alijibu,

"Cha kwanza, nikupe nafasi ya kutoka dakika mbili uende nje, ila usimwambie mlinzi wako kama kuna mtu hatari ndani, au nikufunge kamba na kukuwekea makaratasi mdomoni Ili niondoke kwa amani?" Sarah aliuliza huku akimuangalia,

"Nitoke nje" Harry alijibu huku akiamini kufanya hivyo kutamsaidia kupata msaada kutoka kwa mlinzi na pia atafunga mlango kwa nje ili kumzuia Sarah asitoke,

"Nenda, ila kumbuka kutomwambia mtu yoyote kama kuna mtekaji ndani, ukijaribu utajuta" Sarah aliongea na kumruhusu Harry aende nje, Harry akatoka nje mbio, alipotoka tu, akaufunga mlango kwa nje, kisha akakimbilia kwa mlinzi,

"Tumevamiwa, unakaa getini kizembe hujui hata kama ndani kuna uvamizi" Harry aliongea kwa hasira na kumfanya mlinzi ashtuke, maana hakuamini maneno ya bosi wake,

"Ndani? mbona hakuna mtu aliyeingia?" Mlinzi aliuliza huku akishangaa,

"Beba silaha twende ndani tukamdhibiti" Harry aliongea kisha mlinzi akabeba bunduki yake, ingawa mlinzi alihisi bosi wake huenda amelewa au amechanganyikiwa tu.

Wakasogea mpaka mlangoni, mlinzi akaanza kufungua mlango haraka haraka,

"Fungua taratibu" Harry aliongea kwa kunong'ona na kisha mlinzi akafuata maelekezo ya Harry, baada ya sekunde mlinzi akafanikiwa kufungua mlango na kisha akaingia sebuleni kwa fujo, hakumkuta mtu zaidi ya mke wa bosi wake akiwa amefungwa kamba,

"Yupo wapi?" Mlinzi aliuliza huku akimtazama Harry, Harry mwenyewe hakujua ni wapi mvamizi alipo,

"Ngoja" Mlinzi aliongea huku akielekea sehemu za vyoo, alipofika uko pia hakukuta mtu, akarudi sebuleni na kumkuta Harry akimfungua kamba mke wake,

"Ameelekea chumbani kwa watoto" Mke wa Harry aliongea baada ya kufunguliwa, alitoa kauli iliyofanya utumbo wa Harry ujikunje kwa maana alihisi hakutakuwa na usalama tena chumbani uko,

"Nenda sasa wewe kafungue, unazubaa zubaa nini wewe?" Harry alimwambia mlinzi wake kwa ukali na kufanya mlinzi aanze kuusogelea mlango wa chumba cha watoto,

"Hapana, huyo mlinzi hatomuweza huyo msichana, ni bora tumfungie mlango kwa nje alafu tuite polisi" Mke wa Harry aliongea na kufanya mlinzi asimame na ahache kuusogelea mlango,

"Ufunge huo mlango kwa nje" Harry aliongea kwa ukali huku jasho likimtiririka na kufanya mlinzi ausogelee mlango na kuufunga kwa nje, wakamsikia Sarah akicheka kwa ndani na kisha kikafuatia kilio cha mtoto wa Harry alafu kukawa kimya ghafla, ukaanza kusikika mziki tu kutoka katika chumba kile cha watoto. Hapo akazidi kuchanganyikiwa zaidi hata simu hakuweza kupiga, ilimbidi mlinzi ndio awataharifu polisi juu ya uvamizi ule.

Iliwachukua dakika tano tu polisi kufika pale, wakaelezwa juu ya kile kinachoendelea pale, polisi wakauzunguka ule mlango, kisha mmoja akaufungua na mwingine akaingia kwa fujo, alivyoingia tu ikasikika sauti kama amegongwa na chuma kichwani, akatoa ukelele, ingawa haukuwa ukelele mkubwa ila watu wote waliokuwepo pale ndani waliusikia vizuri na kufanya wasiwasi uongozeke katika familia ya Harry.........

**********ITAENDELEA*********

the Legend☆
 
RIWAYA : SALA YA SARAH

MTUNZI : ALEX KILEO.

SEHEMU YA KUMI NA NANE.

ILIPOISHIA.

Iliwachukua dakika tano polisi kufika nyumbani kwa Harry, wakaelezwa juu ya kile kinachoendelea pale, polisi wakauzunguka ule mlango, kisha mmoja akaufungua na mwingine akaingia kwa fujo, alivyoingia tu ikasikika sauti kama amegongwa na chuma kichwani, akatoa ukelele, ingawa haukuwa ukelele mkubwa ila watu wote waliokuwepo pale ndani waliusikia vizuri na kufanya wasiwasi uongozeke katika familia ya Harry.........

***********ENDELEA***********

Askari wengine wakawa wanajipanga namna ya kuingia ndani baada ya kuhisi mwenzao ameshambuliwa ndani ya chumba kile,

"Ingieni nyie" Askari wa ndani alizungumza na kufanya wenzake wapate mshtuko, hawakuingia kwa maana walihisi adui anawafanyia mtego, wakaendelea kusimama pale mlangoni.

Baada ya sekunde mlango wa chumba kile ukafunguliwa na akatoka mwenzao akiwa amembeba mtoto wa kiume, Harry na mke wake wakamkimbilia yule askari,

"Vipi mzima?" Harry aliuliza kwa pupa huku akimtazama mwanae aliyekuwa amezama ndani ya usingizi mzito,

"Sijui" Askari alijibu huku akimlaza juu ya kochi kisha akarudi chumbani kule ambapo alikuta wenzake wameshaingia tayari na walikuwa wanafanya ukaguzi wa macho ndani ya kile chumba,

"Mbona ulivyoingia uliguna alafu tukasikia kama umegongwa na chuma?" Askari alimuuliza mwenzake,

"Kulikuwa na Giza, sasa nilivyoingia nikagonga chuma hiyo chini, nimeumia sana, maana bado nahisi maumivu" Askari yule alijibu,

"Huyo mvamizi hukumkuta?" Askari akauliza tena,

"Hapana, nahisi atakuwa ametokea dirishani, maana si mnaona chuma cha dirisha kimekatwa na pia kioo kimesukumwa upande mmoja" Mwenzake alijibu na wote wakakubaliana kuwa mvamizi ametokea dirishani.

"Mtoto ndio mmemkuta huyu tu?" Harry aliuliza huku akiingia ndani ya chumba kile walichopo askari,

"Tumemkuta huyo tu, kwani wanalalaga wangapi huku?" Askari alijibu kisha akauliza,

"Mwingine hamkumkuta?" Harry aliuliza huku akiwa ameonekana kuchanganyikiwa,

"Wanalalaga wangapi chumba hiki?"Askari aliuliza tena,

"Wanakuwaga wawili" Harry alijibu,

"Kwanza fanyeni mpango huyo mtoto aliyepo apate Huduma, piga simu hospitali" Askari alimwambia Harry baada ya kuona amechanganyikiwa. Harry akatoka mpaka sebuleni na kuichukua simu yake iliyopo juu ya meza na kupiga simu hospitali akihitaji gari ya wagonjwa, alipokata tu simu yake na kuirudisha mezani, simu yake ilianza kuita tena, alipoangalia katika kioo akakuta namba ngeni, akapuuza kuipokea na kuendelea kushughulika na mwanae ambae alionekana amepoteza fahamu.

Simu ya Harry ikaanza kuita tena na namba iliyoonekana kwenye kioo ni ile ile aliyoipuuza hawali,

"Pokea simu" Mke wake alimwambia,

"Namba ngeni" Harry alijibu,

"Pokea huenda inatoka hospital ulipoagiza gari la wagonjwa" Mke wake aliongea na hapo Harry akapokea simu,

"Hallow" Harry aliongea kwa sauti iliyopoa,

"Umevunja makubaliano, nilikupa chaguzi mbili, ukaichagua moja ya kutoka nje na kutotoa taharifa ya uvamizi, lakini ulipotoka ulitoa taharifa, sasa mwanao ninae, jiandae kwa habari mbaya" Sauti ya kike iliongea, ilikuwa sauti ya Sarah iliyozidi kumchosha kabisa Harry,

"Upo wapi na unataka nini?" Harry aliuliza kwa pupa,

"Nipo kwangu, ninachokitaka nimekipata, ni hii damu yako niliyonayo" Sarah alijibu kisha akacheka na kukata simu,

"Hallow, hallow" Harry aliongea lakini simu ilikuwa imeshakatwa muda mrefu tu, Harry akaangalia kioo cha simu yake na hakukuta kitu kipya,

"Ni nani?" Mke wake alimuuliza,

"Ni yule Dada aliyetuvamia" Harry alijibu kinyonge,

"Anasemaje?" Askari aliuliza,

"Anasema mtoto amemchukua, na anadai nijiandae kupokea habari mbaya" Harry alijibu na kumfanya mkewe aangue kilio, maana alijua mwanae atakufa muda sio mrefu,

"Tupe hiyo namba yake" Askari aliongea na kumfanya Harry achukue simu yake na kwenda eneo la simu zilizompigia, akashtuka,

"Namba haionekani" Harry alijibu na kufanya askari wamshangae,

"Si dakika hii hii amekupigia, au umefuta?" Askari aliuliza,

"Sijafuta, hata mimi nashangaa" Harry aliongea kwa mshangao huku akirudia tena kuangalia,

"Ebu simu" Askari aliongea huku akiichukua simu ya Harry, nae akaangalia lakini hakukuta namba,

"Huyo sio mtu wa kawaida, kwanza njia aliyotumia kuingia na kutoka sio mtu yoyote hapa anaweza kufikiria" Harry aliongea na kipindi hicho gari ya wagonjwa ilikuwa ikisimama nje ya geti, wahudumu wakashuka na kitanda cha matairi na kuingia ndani, kisha wakambeba mtoto wa Harry na wakatoka nae nje na kumpakia ndani ya gari upande wa nyuma na kumlaza kitandani, pembeni alikuwepo mama yake, gari lile la wagonjwa likaondoka kwa kasi kumuwahisha mtoto hospitali.

Ndani ya nyumba alibaki Harry na Askari na mlinzi,

"Ngojeni na mimi niwahi hospitali" Harry aliwaambia askari,

"Kwa hiyo suala la mtoto wako kutekwa unalifikiriaje?" Askari mmoja alimuuliza Harry,

"Mimi nitafanyaje sasa, nimewaachia nyie askari" Harry alijibu,

"Dah, mtihani huo, basi wewe nenda hospitali, alafu kesho uje mapema polisi" Askari aliongea na kisha wakakubaliana hivyo na Harry, askari wakaondoka zao na Harry akaelekea hospitali.

*******************

Sarah alipoingia chumba cha watoto, alitoa kichupa kidogo cha spry na kupuliza katika kile chumba, kisha alitumia Bomu dogo sana kulipua dirisha, na alipofanikisha alimbeba mtoto mmoja wa Harry wa kike na kuruka nae ukuta na kutokea upande wa pili kisha akaliendea gari dogo la dalali alilokuja nalo na kumuingiza mtoto, kisha nae akaingia na kuliondoa gari.

Alifika kwake na kuliingiza gari ndani ya geti kisha akamshusha mtoto na kumuingiza chumbani kwake na kumlaza kitandani, Sarah akaenda sebuleni na kutoa maji kisha akanywa,

"Muda wa kuwapa jamba jamba huu, mpaka wakonde" Sarah aliongea kisha akatabasamu, akavua nguo pale sebuleni na kuingia bafuni kuoga, alipotoka alielekea chumbani kwake kisha akazima taa na kupanda kitandani, akalala jirani na mtoto wa Harry,

"Unisamehe malaika, sina nia mbaya na wewe" Sarah aliongea kisha akambusu yule mtoto kwenye paji la uso, mtoto alikuwa hana fahamu.

Baada ya hapo Sarah akavuta shuka na kujifunika, kisha akalala.

******************

Asubuhi ilipambazuka kwa kikundi chote cha Taita kuwa na habari za kuvamiwa kwa harry na kutekwa kwa mtoto wake mmoja. Ilikuwa ni hali mbaya sana ndani ya kikundi hicho, isitoshe aliyekuwa anawasumbua ni binti mdogo tu.

Taita alichoamua ni kuwatuma vijana wake waende kwenye ile guest aliyokuwa akiishi Sarah ili wakafanye kile walijadili kwenye kikao cha siku iloyopita, na uzuri ni kwamba Harry alidai alikuwa anafuatiliwa na gari ile ile iliyoonekana ikiondoka na Sarah guest.

Kazi hiyo ya kwenda guest walipewa vijana wawili, Tekso na Toiso.

Waliondoka na gari mpaka kwenye ile guest na kumkuta Dada yule yule wa mapokezi aliyekuwepo siku iloyopita,

"Dada tumerudi tena" Tekso aliongea baada ya kumsalimia yule dada,

"Karibuni tena" Dada aliwakaribisha baada ya kumkumbuka Tekso,

"Leo tunaomba utusaidie kitu kimoja kidogo tu" Tekso aliongea huku akijikuna kidevu,

"Kipi hicho?" Dada wa mapokezi aliuliza kwa shahuku,

"Ile gari iloyombeba yule binti jana, unamjua yule dereva?" Tekso aliuliza,

"Ndio, yule kaka ni dalali" Dada wa mapokezi alitoa jibu lililowafanya vijana wale watabasamu,

"Tunaweza kumpata wapi?" Tekso aliuliza,

"Kijiwe chao kipo hapo mbele, njia mliyotokea mwisho kule kuna kijiwe cha kahawa" Dada wa mapokezi aliwaelekeza,

"Anaitwa nani?" Toiso aliuliza,

"Jina kwa kweli simjui, ila anapatikana pale" Dada wa mapokezi alijibu,

"Asante, shika hii utakunywa soda" Tekso aliongea huku akiweka noti ya shillingi elfu tano mezani kisha wakaondoka kuelekea hapo katika kijiwe cha madalali.

Walipofika walikuta watu wengi wa rika tofauti wakiwa kijiweni hapo, wakaenda moja kwa moja kwa muuza kahawa, wakamsalimia,

"Samahani, yule dalali mwenye gari ndogo nyeusi, umemuona maeneo haya?" Tekso alimuuliza muuza kahawa,

"Yule ametoka, mnataka chumba au nyumba?" Muuza kahawa aliuliza,

"Tunashida na yeye" Toisa alijibu kifupi,

" msubirini" Muuza kahawa nae akawapa ushauri kisha vijana wale wawili wakaelekea kwenye gari waliyokuja nayo,

"Wewe baki umsubiri hapa, ngoja nikaongeze mafuta" Tekso alimwambia Toisa,

"Sawa, akija kabla hujatokea mimi nitakupigia simu" Toisa alijibu kisha akatelemka kwenye gari na kujichanganya na watu wengine wanaokunywa kahawa, kwa kuwa huyu Jamaa sifa yake ni ujanja ujanja, haikumchukua muda mrefu kukizoea kijiwe.

Baada ya dakika mbili tu za Tekso kuondoka, Toisa alilishuhudia lile gari dogo likija maeneo yale, Toisa akatoa simu mfukoni na kumpigia Tekso, lakini hakufanikiwa, simu yake ilimuishia chaji, akaamua amsubiri tu.

Wakati akiendelea kusubiri ndipo alipoiona ile gari ndogo ya dalali ikianza kuondoka, Toisa akahisi akizubaa anaweza kupoteza nafasi, akanyanyuka na kuikimbilia ile gari,

"Vipi bro? Kwema?" Toisa alimsalimia dalali,

"kwema, nambie?" Dalali aliongea,

"Bro samahani, jana wakati unatoka pale guest, uliondoka na dada mmoja hivi, yule dada tulipakana vyumba ndani ya guest uliyomchukua jana, kuna kitu cha thamani alikiangusha, sasa naomba unipeleke alipo kama unapajua" Toisa aliongea huku akijifanya ana busara,

"Kitu gani?" Dalali aliuliza,

"Elewa ni kitu cha thamani, kama unanipeleka nipeleke, utakijua uko tukifika" Toisa aliongea na kumfanya dalali afikirie kwa muda, akaona bora ampeleke kwa kuwa kitu chenyewe kaambiwa ni cha thamani na isitoshe kwa sasa yeye dalali anamchukulia Sarah kama ndugu yake kwa namna walivyozoeana kwa muda mfupi tu.

Dalali akageuza gari na kumwambia Toisa aingie ndani, Toisa akaingia huku akijitahidi kuangaza kama atamuona Tekso lakini hakumuona, ubaya hata simu yake yeye Toisa iliisha chaji kwa hiyo ikawa ngumu hata kumtaharifu ni wapi anaelekea kwa sasa.

Dalali akaliondoa gari taratibu huku akijaribu kumshawishi Toisa amtajie ni kitu gani cha thamani alichokiokota, lakini Toisa alitia ngumu kutaja, kitu ambacho dalali hakujua ni kuwa Toisa alitumia ujanja tu ili kupelekwa alipokuwepo Sarah.

Gari ya dalali ilisimama nje ya geti la nyumba ya Sarah,

"Anakaa hapa, wewe shuka mimi naondoka kuna mtu namuwahi'" Dalali aliongea kisha Toisa akatelemka, dalali akaondoa gari na kumuacha Toisa akiwa amesimama getini.

Gari ilivyopotea machoni pa Toisa, Toisa hakutaka kuingia ndani ya geti, alichofanya alijifanya anatembea mpaka akafika upande wa nyuma wa nyumba, akaruka ukuta na kuingia ndani ya uzio, akawa anachungulia kila dirisha la chumba, hakuona mtu, ila alipofika kwenye dirisha la sebuleni, aliweza kumuona Sarah akiwa amelala kwenye sofa huku akitazama runinga, Toisa akaelekea kwenye mlango wa kuingilia na kuminya kitasa kwa taratibu, mlango ukafunguka na Toisa akatokea sebuleni,

"Leo umepatikana kirahisi" Toisa aliongea na kufanya Sarah ashtuke na kugeuka nyuma, hapo ndipo Sarah alipokutana na mdomo wa bastola ukimuangalia............

*********ITAENDELEA***********

the Legend☆
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom