SEHEMU YA KUMI NA SITA
Majira ya saa mbili usiku akiwa anaambatana na watu
wawili wababe alirejea nyumbani.
Huku akamkuta mkewe akiwa mkiwa sana, akamsalimia
na hapohapo akamuulizia Aneth.
Mama akamtazama mumewe kwa muda na kisha akatoa
jibu lililozua tafrani katika kichwa cha mzee Fidelis.
Aneth alikuwa ametoweka na hajamuaga mtu yeyote
lakini ameacha ujumbe mfupi kabisa.
“SITAKANYAGA HAPA NA MAITI YANGU ITUPWE
JALALANI ISILETWE HAPA….Na kuanzia dakika hii
naitwa ANETH RAMADHANI JOSEPH.”
Mzee Fidelis alipigwa na bumbuwazi, wale watu
alioambatana nao walipojaribu kumuuliza
aliwagombeza na kisha kuwafukuzia mbali.
Wakaondoka huku wakijiuliza iwapo huyu mzee
amechanganyikiwa ama la!
______
MJI ulikuwa tulivu tofauti na siku nyingine, familia
ilishazoea ile tabia ya baba yao kufoka kila mara, iwe
anakuita ama likitokea kosa umefanya yeye anafoka
tu!
Uzuri alikuwa anafoka tu lakini alikuwa na mkono
mzito sana hakudiriki kuadhibu watoto wake hovyo,
alikuwa ni mtu wa mikwara tu. Mkiwa mezani mnakula
lazima atafute sababu ya kumgombeza walau mtoto
mmoja!
Ukila taratibu atakwambia unakula kama upo harusini,
ukila upesiupesi atakuuliza unakula harakaharaka
unawahi wapi.
Ukinawa mikono wa kwanza anakukaripia kuwa hauna
adabu unanawa kabla ya wakubwa, ukisubiri wakubwa
wanawe ndo wewe unawe anakukebehi kuwa utaratibu
huo ni wa kizamani yeyote anaweza akaanza kunawa.
Mkewe alikuwa anaingilia kati mara moja moja huku
akimtupia kijembe mumewe kuwa vita ya Kagera
ilimwathiri akili anajiona yupo sawa kwa kila
anachofanya.
Akishaambiwa hivi na mkewe anasusia chakula anaenda
chumbani, wakikutana huko wanayamaliza.
Japokuwa hali hii ukiisoma unaweza kudhani
ilisababisha familia hii isiwe na furaha,. Lakini tabia
hii ilifanya furaha itawale nyumbani na upendo
kuimarika zaidi miongoni mwa wanafamilia.
Lakini siku hazifanani!
Siku hii ukimya ulitawala sana, vilisikika vijiko
vikigombana na mabakuli na sahani, na midundiko ya
matonge kuanzia yanavyoshambuliwa na meno
mdomoni kisha kupita katika koromeo na kudondoka
tumboni.
Ukimya huu ukasababisha mama azungumze ili
kumchokonoa baba mwenye nyumba..
“Naona leo Pilipili imetiwa ndimu nyingi! Imeishiwa
makali?” usemi huu wa mama ukasababisha familia
nzima wavunje mbavu kidogo, kasoro mlengwa wa
kijembe hiki yeye alikuwa mtulivu.
Tofauti na matarajio ya wengi kuwa ataanza kugomba
kama kawaida yake au kurudisha kijembe kikubwa zaidi
haikuwa hivyo!
Kimya kikatanda tena!
“Afande Pilipili, unaumwa?” mkewe akamuuliza
kimasihara. Badala ya kujibu, baba mwenye nyumba
ambaye nyumba yake pia ilimwita kwa jina la utani la
Sajenti Pilipili akasimama badala ya kuelekea chumbani
akaelekea dirishani na kusimama akawa anatazama
nje.
Hapa sasa hayakuwa masihara tena mkewe
akamwendea na kumkokota wakaenda chumbani.
Tayari alishagundua kuwa ubavu wake haukuwa sawa
kabisa.
Utani kando, mapenzi yakachukua nafasi.
Ni huko chumbani ambapo Pilipili alimweleza mkewe juu
ya jinamizi la Rama linavyomsumbua na kumkosesha
raha. Akaelezea ni kiasi gani yule kijana asiyekuwa na
hatia alivyoingia katika domo la kifo kimasihara na
hapo akailaani kauli ya mkuu wake wa kazi ya kuamua
Rama aende Oman kwa oparesheni ya kumsaka Vonso.
“Sidhani hata kama Rama alitakiwa tu kulijua hilo
jina, ni jina zito sana kuliko umri wake! Sijui tu nini
kilitokea kati yetu…” akasita akamgeukia mkewe.
“Hivi unajua ameacha mke na mtoto mdogo… katoto
kadogo kabisa.”
Mkewe akataka kusema neno sajenti akaendelea,
“Halafu mkewe naye tumemsotesha rumande kizembe
tu!”
Mkewe akaguna kisha akamuuliza swali moja. “Lakini
mume wangu mbona Oman inasdifika kwa sheria kali
inawezekana vipi mtu kuuwawa kizembe hivyo!”
“Ni kweli sheria zao ni kali haswa lakini ukali wa
sheria hauzuii mtu mmoja kumtoa roho mwenzake kwa
sababu zisizojulikana.
Mkewe alimfariji na kumpa maneno ya kumtia nguvu
upya kabisa. Walau faraja hii ilimpa nguvu za
kutabasamu kidogo, Sajini Pilipili.
Kisha mkewe akabadili mada ili kumpunguzia mumewe
mzigo wa mawazo.
Wakati wanaanza kubadili mada, mlango wa chumbani
uligongwa mama Yohana akaenda kufungua.
Akamsikiliza mgongaji ambaye alikuwa ni mtoto wake.
“Baba Yohana, kuna ugeni….” Mkewe akamueleza kwa
utulivu huku akionekana kuchukia ugeni huo wa usiku!
Sajini akasimama na kutoka nje ya chumba chake.
Alipotoka tu akakutana na mwanamke akiwa
amesimama akibembeleza mtoto wake aliyekuwa
analia.
Sajini akashtuka vibaya mno!!
“Mama Jose!” akaita.
“Samahani kwa kukutembelea usiku huu imenibidi tu,
nahitaji kuzungumza nawe.” Alijibu mama Jose.
Sajini akajivuta na kutoka nje, mama Jose akamfuata
nyuma. Huku mkewe akiwasindikiza kwa macho yenye
viulizo vingi.
Walizungumza mengi sana huko nje, mama Jose
akajieleza.
“Sina pa kwenda Sajini, sina yeyote wa kunisikiliza, si
upande wa nyumbani kwetu wala upande wa mume
wangu… tafadhali naomba ufanye kitu.” Akasita
akamgeuza Jose ambaye alikuwa bado hajasinzia.
“Sajini, baba yangu… baba aliyenizaa mimi…
amempiga Jose kibao kwa nguvu zake zote… mwone
mwanangu asiyekuwa na baba anavyoanza
kuteseka…” akataka kuendelea koo likagoma kutoa
sauti, akajaribu tena kuzungumza akajikuta
anaangua kilio cha uchungu!
Kumwona mamaye analia, Jose naye akaanza kulia!!
Sajenti alijiskia vibaya sana na kuzidi kuwa upande wa
hatia! Alijiona amepambwa na damu mikononi mwake.
Ili kukabiliana na hatia hii, akaona ni heri amsaidie
kadri awezavyo mama Jose.
Akaamini kuwa msaada wake wa dhati pamoja na
ukaribu wake kwa Mama Jose utafuta kidogo
kumbukumbu ya Rama kupoteza maisha nchini Oman.
Sajenti Pilipili akachukua maamuzi ambayo yalimwaga
maji ya ubaridi katika moyo wake wa nyama uliokuwa
umeganda kwa sababu ya fikra juu ya Rama.
Baba wa mtoto mchanga!!
Kwa siku ile Mama Jose alilala pale nyumbani, siku
iliyofuata sajini aliwaagiza vijana wake wakatafuta
chumba na kuweka vitu vya msingi, baada ya siku tatu
mama Jose akaanza kuishi katika nyumba ya kupanga.
Mara kwa mara Sajini Pilipili alikuwa akienda kumjulia
hali.
Baadaye akamfungulia duka la vipodozi jirani na
nyumba aliyokuwa amempangishia!
Sajini Pilipili akabaki kuwa ndugu pekee wa Mama Jose.
Jose akaanza kumtambua sajini kama baba yake.
Rama akasahaulika!!
Wakati Rama anasahaulika Sajini kwa amri ya mkuu
wake wa kazi akatakiwa kufanya mawasiliano na Zay
B ili mara moja rejee nchini Tanzania akatulie
nyumbani kwao Zanzibar!
Na akatakiwa rasmi kulifunga jalada la kumsaka
Vonso na kampuni yake lililokaa wazi kwa miaka zaidi
ya kumi bila muafaka.
Ni simu hii ya kutoka Tanzania kwenda Oman iliyozuka
balaa jipya.
Majibu yakaelezea kuwa kuna wawakilishi rasmi
kutoka Tanzania walifika Oman katika makazi
aliyokuwa akiishi Zay B na kuelezea kuwa anatakiwa
mara moja nyumbani Tanzania, watu hao walikuja na
nyaraka zote za kiofisi kuthibitisha kuwa wapo pale
kihalali.
Watu wale wakatokomea pamoja na Zay B na mizigo
yake michache.
Walikuwa na tiketi ya ndege kabisa maalumu kwa ajili
ya Zay B.
Sajini Pilipili alichoka, lakini Inspekta generali wa
polisi alichoka zaidi.
Ilikuwa ni vita mpya!!
Vita dhidi ya watu wanaojulikana lakini wasiojulikana
kwao!!
IGP akaingia katika Pumbazo na kwa ghadhabu kubwa
sana ya kuona kuwa adui yao anawafanya kama
watoto wadogo. Akachukua simu yake akatafuta
namba aliyokuwa anaihitaji.
Akapiga na kusikiliza kwa muda, ikapokelewa na mtu
aliyekuwa kilabuni analewa, alizungumza kilevilevi.
IGP akakata simu huku akitokwa na tusi zito haswa
kwa lugha ya kifaransa.
Akaitazama simu ile kisha akalisoma lile jina katika
simu.
GEZA ULOLE!!
Akamalizia kwa kulitafsiri.
IGA UFE!
Na mwisho akaponyokwa na kicheko kisichokuwa
kichekesho!
_____
RAMA aliendelea kufanya kazi ngumu huku akipata
chakula kidogo tofauti na kazi ile iliyojaa suluba, siku
mkurugenzi akiwepo wanapewa chakula kizuri sana na
hawafanyishwi kazi nyingi sana.
Rama akaanza kujifunza kitu, kuna jambo lilikuwa
haliendi sawa hata kidogo katika chimbo lile. Akahisi
kuna manyanyaso ambayo wanafanyiwa lakini ni
nyuma kabisa ya upeo wea mkurugenzi.
Akafikiria kushtaki lakini mkurugenzi yule alikuwa
hazungumzi kiingereza wala Kiswahili.
Hapa sasa Rama akalazimika kubadili mfumo wake wa
kuishi maisha ya kimyakimya, akaamua kubadilika na
kuunda urafiki na wenzake katika geti nambari nne
ambao wote kwa pamoja walifahamu fika kuwa hatma
yao ni kufanya kazi kila siku na ili utoke mle ndani
lazima uwe umekufa!
OMANI haikujua kuhusu hili, Tanzania haikujua
kuhusu hili, Afrika ilikuwa gizani na dunia haikuwa na
huu ufahamu.
Walifahamu wachache walionufaika na mradi huu.
Katika kuunda urafiki na kuanza kuzungumza na
wenzake hasahasa wakati wa chakula… hatimaye
walianza kutambuana kwa majina na nchi
wanazotoka.
Rama akakutana na Latipha!
Binti kutoka Kenya ambaye mara yake ya mwisho
kuishi Afrika alitokea nchini Tanzania. Ni huyu ndiye
aliyemsimulia Rama na kuanza kumfungua akili yake
walau kidogo.
Alikuwa anamsimulia Rama huku wakiendelea kufanya
kazi, haikuwa rahisi binti yule kuanza kumsimulia
Rama kwa sababu hakuamini kuna msaada wowote
anaweza kuupata, aliiona hatma ya wote katika ficho
lile ni kifo cha kifedhuli.
Lakini ule ukarimu wa Rama kumsaidia yule binti kazi
walizokuwa wanapewa hatimaye Latipha aliamua
kumsimulia rama. Na alimsimulia haya huku akimpa
angalizo kubwa.
LATIPHA
Naitwa Latipha… Latipha Kasim Sadiki, nina miaka
ishirini na moja sasa. Nitakufa kabla sijafikisha miaka
ishirini na mbili, nitakufa kwa mateso makali sana,
nitakufa na kutupwa kama mzoga.
Mama yangu hatajua, wala ndugu yangu yeyote.
Mchwa na wadudu watakaonitafuna pekee ndio
watatambua kuwa mimi ni mfu.
Nilifanya kazi mbalimbali jijini Mwanza nchini
Tanzania, kwa asili mimi ni mkikuyu kutoka Kenya.
Nilienda Tanzania kutafuta maisha nikipitia njia ya
Mombasa kisha Tanga.
Nimefanya kazi katika mgahawa mdogo Mwanza,
kipato kilikuwa chini na dharau kubwa kutoka kwa
wateja nilizizoea.
Maisha yangu yalipata Nuru tena baada ya kukutana
na kijana mstaarabu sana anayeitwa Eric Mlewa….
Awali nilidhani kuwa ananitaka kimapenzi lakini siku
moja aliniita kando na kupeleleza juu ya mshahara
wangu, nikamjibu akastaajabu sana na kisha
akanieleza iwapo nipo tayari kufanya kazi hiyohiyo ya
mgahawa lakini nje ya Tanzania, nikamjibu nipo tayari
lakini sio nchini Kenya.
Akanieleza ni Oman, akasema mshahara ni mara kumi
ya ule niliokuwa napokea. Nilipokea taarifa ile kwa
furaha lakini sikuamini kama itatekelezeka, ajabu
kijana yule alikeleza.
Mara nikapigwa picha za paspoti, mara pasipoti
ikakamilika.
Hatimaye ikawa safari, nakumbuka jina moja lilikuwa
linasemwa mara kwa mara lakini sikutilia maanani kwa
sababu ya ushamba wqa kupanda ndege lakini nilisikia
juu ya kampuni inaitwa VONSO kama sikosei… na hata
tulipofika Dubai nilisikia tenma kuhusu hiyo kampuni,
na Oman vilevile nilisikia.
Lakini baada ya kufika Oman tukapokonywa pasi zetu
za kusafiria, tulikuwa wane… tukapokonywa simu
zetu. Mimi na mwenzangu, wenzetu wawili hawakuwa
na simu.
Tulipofika Oman haikuwa kazi ya mgahawa wala hoteli,
ilikuwa ni kazi ya ndani ya ntyumba za watu.
Makabidhiano yao yalifanyika katika lugha ya kiarabu
na hakuna nilichoambulia asilani.
Kaka yangu, kazi ni kazi aidha iwe ya mgahawa ama
la! Lakini kilichosababisha mimi kuwa hapa sio ugumu
wa kazi bali ni changamoto katika ile kazi… ni
changamoto hizo zitakazopelekea mimi kupoteza
maisha… na nitakufa kabla sijatimiza miaka ishirini na
mbili……”
Latipha alisita kusimulia, akatazama mlangoni,
alikuwa anaitwa na yule msimamizi.
“Anaenda kunibaka…” alisema Latipha kwa sauti ya
chini. Rama akasikia kauli ile…….
Lakini angefanya nini angali yule bwana alikuwa na
bunduki katika kiuno chake??
Akasubiri sana Latipha aweze kurejea na kuendelea
kumsimulia ilikuwaje hadi akaingia katika chimbo hilo
la mauti…..
Lakini kamwe Latipha hakuwahi kurejea katika macho
ya Rama!
Alikufa binti yule!
Hakika alikufa akiwa hajatimiza miaka ishirini na mbili