Riwaya: Pumbazo

Riwaya: Pumbazo

SEHEMU YA KUMI NA TATU

RAMA alisubiri kwa siku mbili zaidi ili aweze kusikia
kuwa anatafutwa.
Lakini haikuwa hivyo, siku zilikatika bila kuona dalili
yoyote ya matumaini.
Rama alijutia kila alichokifanya hadi kumfikisha hapo
gerezani lakini hakujutia kulibadili jina lake kutoka
lile la Ramadhani na kujiita Alexander ili kukwepa
rungu la kuadhibiwa kwa kosa la kunywa pombe ilihali
yeye ni muumini wa dini ya kiislamu nchini Oman jiji la
Muscat.
Laiti kama Rama angejitambulisha kwa jina lake halisi
angekuwa matatani zaidi na si ajabu angeweza
kupoteza uhai wake.
“Zay B atanitafuta kwa jina la Rama!” alijifikiria
akiwa ndani ya gereza na kutambua wazi kuwa hiyo
italeta utata mkubwa sana, kichwa kilimuuma na
hakuwa na yeyote wa kumpa msaada katika mazingira
yale.
Kuhusu kumtegemea Zay B hilo ama yeyote yule
anayemtambua kwa jina la Ramadhani alifuta kabisa
kichwani kwake ili asizidi kujiumiza kifikra.
Na hapo rasmi akajiandaa kisaikolojia kutumikia
kifungo cha miezi sita gerezani.
Tabasamu la karaha likamponyoka, kisha akajiita kwa
sauti ya chini jina lake jipya.
Alexander!
_____
GEREZA lilimpokea Rama katika namna ya kipekee,
alikuta makundi makuu matatu ya wafungwa katika
gereza lile huku kundi lililokuwa na nguvu sana likiwa
lile la waarabu, kundi dhaifu likiwa la wafungwa wenye
asili ya kihindi hawa walikuwa kama watumwa wa
waarabu. Na walinyenyekea haswa kila kilichosemwa
na wafungwa wa kiarabu…
Kundi la watu weusi lilikuwepo kama halipo, wafungwa
weusi walikuwa wachache sana hivyo Rama hakuweza
kutambua upesi ni maisha gani wanapitia katika
gereza hilo.
Waarabu wa Pemba hujuana kwa vilemba!
Hata weusi nao hujuana kwa rangi zao!
Rama alipoingia gerezani, wafungwa weusi wawili
pekee katika gereza lile walimpokea, mmoja alikuwa
mfungwa kutoka nchini Brazil anayengoja nchi yake
ifanye utaratibu wa kumrudisha nyumbani akatumikie
kifungo, na mfungwa mwingine alikuwa anatokea
Jamaica.
Mbrazil akiwa pale kwa kosa la kukamatwa na madawa
ya kulevya huku yule wa Jamaica akitumikia kifungo
kwa kukamatwa na misokoto ya bangi pamoja na
vitambulisho feki.
Kesi zao zilikuwa tofauti kabisa.
Lakini walau waliweza kuzungumza kiingereza na
kuelewana, japokuwa kwa shida.
Kitu kimoja cha msingi alichokigundua Rama ni kwamba
gereza lile lilikuwa linatoa huduma nzuri sana na
wafungwa walikuwa wanajaliwa sana. Kuanzia suala
la kulala hadi chakula.
Gereza lilitoa usawa lakini wafungwa kwa wafungwa
ndo walionekana kunyimana usawa.
Hali nzuri ya utulivu na ya amani aliyoitazama pale
hakutaka kuamini kuwa miezi sita yote patakuwa
hivyohivyo, aliamini kuwa wale wafungwa
wanaojifanya gereza lilijengwa kwa ajili yao ipo siku
wataanza ‘kumzingua’
Kweli baada ya juma moja kupita ndipo vitimbi
vikaanza kutoka kwa wafungwa wenye asili ya
kiarabu.
Wakati vitimbi hivi vikianza gerezani nchini Oman, huko
nchini Tanzania, kwa kauli moja wote waliofahamu
juu ya oparesheni iliyompeleka Rama nchini Oman
walitamka wazi kuwa Rama anasadikika kupoteza
maisha nchini Oman.
Waliyatamka haya katika kikao cha dharula
kilichomuhusisha pia mke wa Rama.
Bi Aneth akiwa na mwanaye Jose.
Tofauti na wengi walivyodhani kuwa mama Jose
atatoa kilio kikubwa sana hivyo wakawa wameandaa
namna ya kumfariji, lakini baada ya taarifa ile mama
Jose alitulia tuli akiwa na mwanaye mgongoni.
Kisha baada ya sekunde kadhaa akaangukia mezani
akitanguliza uso.
Na kisha akatulia zaidi.
Mama Jose alikuwa amepoteza fahamu!!
Sajenti Pilipili aliingiwa na mchecheto mkubwa haswa,
akachukua simu yake upesi na kuwasiliana na Zay B
ambaye alikuwa Oman.
Akamueleza kilichotukia nchini Tanzania baada ya
taarifa ile, kisha akamuonya juu ya habari ya Rama
kuingizwa katika oparesheni ile iishie kwao na isiende
mbali zaidi.
Hofu yao ilikuwa juu ya umoja wa mataifa, ukifahamu
juu ya jambo hili ambalo Rama amelifanya pasi na hiari
yake mwenyewe na kisha kumgharimu maisha yake.
Hali ilikuwa tete!!
Baada ya kuzungumza na Zay B, akampigia simu
inspekta jenerali wa polisi na kumweleza hali halisi.
“Pilipili nilikuonya lakini….” Alizungumza kimalalamiko
kisha akakata simu bila kusikiliza lolote kutoka kwa
Pilipili.
Hili nalo likamvuruga zaidi Inspekta Pilipili, akaanza
kuona dalili ya kuachiwa jumba hili bovu kumuangukia
yeye peke yake.
Inspekta jenerali alikuwa anajitoa kimyakimya!
Pilipili akabaki kuduwaa, akifikiria walivyoshirikiana
vyema katika maamuzi haya baada yay eye kupeleka
wazo…. Sasa anageukwa.
Pumbazo!
____
ILIKUWA ni siku tulivu kabisa baada ya wafungwa
kufanya shughuli za hapa na pale kisha kupata chakula
cha mchana, Rama akiwa na mfungwa kutoka Jamaica
wakipiga soga, mara mfungwa wa kiarabu aliwaendea
na kuwasemesha kiarabu.
Hakuna aliyeelewa!
Kwa mara nyingine tena Rama akamkumbuka ustadhi
Karimu ambaye alikuwa mwalimu wake wa madrasa,
kitendo cha kuzikimbia zile mboko za madrasa sasa
kikawa kinamgharimu asiweze hata kulinasa neno
moja la kiarabu. Ustadhi Karim licha tu ya kufundisha
maandiko tukufu,lakini pia alikuwa akiwafundisha
maneno mawili matatu ya kiaerabu nje ya maandiko.
“Unazungumza nini we jamaa?” Rama naye akamuuliza
Kiswahili, kisha akataka kuendelea kuzungumza zaidi
Kiswahili akagundua kuwa hata yule mjamaika hakuna
anachoambulia.
Kitendo cha kuzungumza kiswahuli kikamfanya yule
mwarabu amtolee macho, kisha akapaza sauti
akiendelea kuzungumza kiarabu.
Punde yakaingia mapande ya watu wawili, ni wafungwa
Rama alikuwa akiwafahamu.
“Wamesema waarabu tunanuka!!” sasa alizungumza
kiingereza yule bwana.
Rama na yule mjamaika wakagutuka, mjamaika
akaingiwa hofu zaidi. Bila shaka alikuwa anafahamu
fika usumbufu wa wale watu waliofanya gereza kama
la kwao.
Bila kuuliza swali lolote wakawaamrisha Rama na
mjamaika wapige magoti.
Mjamaika akaenda chini Rama akahoji kulikoni!
Hiki ni kitu ambacho waarabu wale hawakutaka
kusikia, wakachukizwa na ukaidi wa Rama.
Mwarabu mmoja akamtandika konde la usoni, lakini
halikumuingia vizuri Rama aliyewahi kurudi nyuma.
Hapo sasa wafungwa wengine walianza kusogea
kutazama kinachojiri!
Jela jela tu! Huwa inafikia kipindi hata maaskari jela
wanaacha gomvi kama hizi zitokee wajionee sinema za
bure!!
Kuona Rama amemkwepa akamfuata akirusha makonde
mfululizo kizembe.
“Sitaki kupigana na wewe bila sababu jamaa…” Rama
akazungumza Kiswahili maksudi!
Hawakumuelewa zaidi aliwapandisha hasira!
Rama alikuwa hajanyanyua mkono wake hata mara
moja kurusha ngumi, alitambua kuwa wao walikuwa
wachache sana wenye rangi nyeusi na tayari aliuona
ubaguzi wa waziwazi hivyo kujitia kurusha ngumi ni
kujitafutia balaa.
Rama akawa upande wa kufyata! Hakurusha ngumi….
Lakini hili halikumfanya mwarabu amuache, sasa
walikuwa wawili….. wote wakitaka kumkaribisha Rama
kwa kipigo gerezani ili awaheshimu.
“Nitawaumiza jamani achene…” akazungumza
kiingereza, sasa hakurudi nyuma bali alisimama imara.
Maneno haya ya kishujaa yakawashangaza wale
waarabu.
Wakajaribu kuyapima kwa vitendo.
Askari mkakamavu kutoka Tanzania aliyeacha kazi hiyo
kwa sababu ya kuogopa ushirikina akasimama imara
akakunja ngumi.
Kikazuka kivumbi cha hali ya juu.
Ebwana wee! Waarabu wana ushirikiano jama….
Alipoweza kuwapasua wale wawili kwa ngumi
motomoto, wale wafungwa wengine wakamfuata ili na
wao waweze kumkabili.
Alipambana katika maana halisi ya ule usemi wa
‘kupambana kiume’
Mwishowe umoja wa waarabu ukamwangusha chini,
askari wakaingilia kati Rama akiwa hoi akivuja damu.
Ushujaa wake siku ile ukazua gumzo gerezani, na hata
alipopata nafuu na kurejea tena gerezani wengi
walikuwa wanamuogopa na hakuna aliyemtikisa.
Alikumbuka kuwapa onyo huku akiwa bendeji,
akawaeleza kuwa nchini Tanzania aliua samba wawili
kwa mikono yake mwenyewe hivyo wakimgusa tena
ataua wawiliwawili.
Licha ya umoja, waarabu ni waoga pia.
Japokuwa ulikuwa ni mkwara, wakafyata!!
Mkwara ule ukapenya hadi nje ya selo kupitia wale
wafungwa waliomaliza muda na maaskari jela
walioamua kuzishirikisha familia zao na marafiki pia.
Hatimaye zikafika mbalizaidi sifa zile.
Baada ya mwezi mmoja wa kutumikia kifungo, kwa
mara ya kwanza Rama ama Alexander kwa pale
gerezani akapata mgeni.
Mgeni aliyemtambua kwa jina la Alexander.
Maajabu, jina feki kisha unapata mgeni anakutambua
kwa jina hilo??
Rama akamsikiliza kwa makini, yule bwana alikuwa na
nia ya kumsaidia Rama ili aweze kuwa huru.
Akaelezea kuwa yeye ni muislamu na ni mtanzania,
ameguswa na kitendo cha Rama kufungwa jela kwa
kuvunja sharia asizozijua!
Alikuwa ni ngozi nyeusi na aliongea lugha ya Rama!
Rama akafarijika na kukubaliana na yule bwana
aliyeahidi pia kumrejesha nchini Tanzania.
Lakini kigezo cha Rama kuukubali msaada huu ni
kwamba alihitaji hatua zifanyike za yeye kukutana
kwanza na mwenyeji wake wa nchini Oman!
Akawatajia Zay B!
Yule mgeni akamweleza kuwa hilo halina tatizo.
Baada ya siku tatu Rama akatembelewa tena….
Mbele yake alikuwa ni yule mgeni akiwa ameambatana
na Zay B, yule mwanadada askari wa kizanzibar Nchini
Oman!!
Zay B hakuzungumza kabisa bali alimpungia tu mkono
Rama kwa muda mrefu huku akionyesha majonzi ya
waziwazi.
Rama akatambua kuwa Zay B anamuonea huruma kwa
uwepo wake gerezani.
Kwa siku hii hapakuwa na mazungumzo mengi, Rama
akakubali kiroho safi kabisa ule msaada.
Msaada kutoka kwa mgeni anayezungumza Kiswahili!
Alikuwa amedumu gerezani kwa mwezi mmoja na siku
kadhaa.
Akaachiwa huru kabisa…. Asijue wale waliomsaidia
walikuwa na nia gani.
Alipoivuta hewa nje ya gereza kitu cha kwanza
kilichokuja katika akili yake ni Vonso!
Akaapa kwa kila majina aliyojua kuwa anajitoa katika
msako huo asioujua, akafikia maamuzi magumu ya
kwenda ubalozi wa Tanzania na kuelezea kwa kina
tukio lake ili aweze kusaidiwa!
Hiyo ilikuwa ni azma yake ya kwanza kabisa katika
uhuru ule.
Alibaki na hatihati iwapo amshirikishe Zay B ama
ajichukulie maamuzi ya kibinafsi!
Akaweka kituo katika wazo lile na kujipa muda zaidi
wa kufikiri!
Waliingia katika jumba la kifahari, hakujiuliza sana
juu ya jumba lile kwa sababu Muscat kuna majumba
mengi zaidi ya kifahari zaidi ya lile, geti likafunguliwa
wakapita, likafunguliwa na geti la pili, hatimaye geti
la tatu likafunguliwa, na hapo palikuwa kama ukumbi.
Rama akashtuka ghafla anasukumwa kwa nguvu sana,
kwa sababu hyakutarajia kitendo kile akajikuta
anapiga mweleka chini, kabla hajafukurukuta
alifungwa kamba kwa nyuma. Kisha kamba ile ikaanza
kuvutwa na kitu kisichojulikana ili kumnyanyua Rama,
kamba ile haikuishia kumnyanyua ikazidi kumvuta juu
katika namna ya kumnin’iniza.
Hapo sasa Rama alianza kupiga mayowe. Lakini wale
watu waliomfunga kamba hawakujali.
Sasa alikuwa hewani na kamba ikizidi kumvuta kwenda
juu.
Alivutwa hadi akatokea upande mwingine wa juu
kabisa.
Mara alipofika juu akasikia watu wakipiga makofi kwa
juhudi sana.
Rama akageuka kutazama makofi yanapotokea.
Hakuamini macho yake asilani, akafumbua na kufumba
kisha akafumbua tena…. Hali ilikuwa kama akili yake
ilivyokuwa imetafsiri!
BALAA!x
 
SEHEMU YA KUMI NA NNE

MACHO yake hayakukutana moja kwa moja na watu
waliokuwa wanapiga makofi, badala yake yalitua
katika miili iliyokuwa mahututi kama sio kutokwa na
uhai kabisa.
Damu ilikuwa imetapaa huku na kule. Rama akataka
kusema neno, lakini koo lilikuwa limekauka sabna
kutokana na kilio kikuu alichotoa wakati akipandishwa
na zile kamba ngumu kuelekea juu.
Laiti kama usingekuwa ukakamavu wake alioupata
akiwa katika mafunzo ya jeshi la kujenta taifa
(J.K.T) basi hali yake ingekuwa mbaya sana.
Bila kufunguliwa zile kamba alishtukizwa na pigo moja
kali katika kisogo chake!
Fahamu zikamtoka!!
_____
RAMA ANASIMULIA.

NILIKUJA kushtuka baada ya kumwagiwa maji ya
baridi, niliposimama miguu yangu ilikuwa inatetemeka
sana, na tumbo lilikuwa wazi kabisa.
Njaa ilikuwa imenishika kwa kiwango cha juu!
Mbele yangu alikuwa amesimama kijana wa kiafrika
mwenye ngozi kama yangu.
“Ako unatokea wapi wewe?” alinisemesha kwa
Kiswahili nilichobaini kuwa ni cha nchi jirani kabisa na
taifa langu.
Kenya!
Na kama si Kenya basi alikuwa ni mjaruo!!
Nikataka kumjibu kuwa natoka Tanzania lakini badala
yake nikajikuta namweleza kuwa nina njaa kali sana.
Akanitazama kwa jicho ola dharau na akionyesha wazi
kuwa hajafurahishwa na uwepo wangu pale.
Akatoka nje, baada ya muda akarejea na birika la uji
wa moto akanipatia. Nikauvamia kwa pupa, tumbo
likaupokea kwa shangwe.
Wakati naendelea kunywa uji, yeye akatoka nje na
kurejea nasahani lililokuwa na chakula aina ya tambi.
Nikaimaliza sahani ile, na hapa nikajisikia kuwa na
nguvu na imara.
Akaniuliza iwapo nimetosha, nikamkubalia.
Akasimama na kuanza kutembea kuelekea huku na kule
kisha akaanza kuzungumza.
“Naitwa Abdulkarim bin Swaleh…nimesema nani??”
akaniuliza.
“Abdulkarim bin Swalehe!” nikarejea kulitaja jina lake
kwa umakini. Akacheka kidogo nikaona kuwa hakuwa
na meno mawili ya mbele.
“Mimi ni bosi yako, kuanzia dakika hii hautaniita
Abdulkarim ila utaita mimi Masta…. Na uite jia hii
wakati Masta kubwa haiku around, akiwa around
utaniita Abdulkarim… akiwa mbali utaita mimi Masta.
Baadaye ntapeana na wewe kazi za kufanya….”
Alizungumza kwa msisitizo huku akinitazama machoni,
na kila mara akiipandisha nguo yake juu kimajigambo.
Nilibaki nimeduwaa nisijue anachomaanisha,
nikamuuliza kulikoni.
Naye akashangaa kusikia namuuliza swali.
“Kwani haukupewa instructions wakati unakuja hapa?
Hili ni eneo la kazi… na mimi ni masta wako…” majibu
ya yule bwana yalianza kunichanganya.
Nikamuuliza pale ni wapi.
“Oman…. Muscat Oman….” Alijibu kwa msisitizo.
Kisha akatoa maelekezo yaliyonifanya niingiwe na
ubaridi mkali sana.
Akanieleza kuwa nimetia saini mkataba wa kufanya
kazi katika kasri lile kwa kipindi cha miaka mitano.
Wakati anazungumza haya akanipatia karatasi ambayo
niliona kweli kabisa nilikuwa nimetia sahihi yangu
katika mkataba ambao umeandikwa kiarabu nisijue
hata ni kitui gani kilikuwa kimeandikwa.
Nilijikaza nisionekane kuwa nimeingiwa na hofu lakini
kiukweli nilikuwa nimepagawa tayari.
Niliwaza kuhusu mtoto wangu Jose ambaye bado
alikuwa mdogo sana, nikamfikiria pia mke wangu.
Chozi la uchungu likanitoka!!
Na haikuwa ndoto bali kweli tupu.
Yule bwana anayetaka nimuite masta alinichukua hadi
katika chumba kingine akafungua mfuniko uliokuwa
sakafuni. Tukaingia chini……
Macho yangu yakaanza kukutana na sura nyonge
kabisa zikiwa katika kazi, hakuna hata mmoja
aliyeonyesha kuwa na furaha.
Joto lilikuwa kali na kila nilivyozidi kwenda mbele
lilikuwa linaongezeka.
Hofu ikazidi kuchukua nafasi yake. Masta akanikabidhi
kwa bwana mwingine ambaye alionekana kuwa kiongozi
kule chini ya ardhi kwenye mitambo ambayo sikujua
inahusu nini.
“Una ujuzi gani?” aliniuliza kiingereza.
Swali lile lilikuwa la kushtukiza sana, nikabaki
kujiumauma.
“Unajua kuongoza mashine? Unajua kuchanganya
kemikali? Unaweza kuendesha gari kubwa? Unaweza
kupanga pampu za mafuta?” aliuliza maswali mengine
mfululizo….. nikakosa jibu.
“Send him to Utaah! (Mpeleke kwa Utah)” akampa
maelekezo masta.
Masta akanichukua na hapohapo akawa
ananinong’oneza.
“We ako mpumbavu kiasi gani,. Ungesema profesheni
yoyote ile kwa huyu bwana, sasa Utah atakuua na
venye ulivyo legelege… atakuua mjinga yule.”
Kusikia juu ya kifo nikaingiwa ganzi, nikatamani
kukimbia lakini hadi wakati huo Masta Abdulkarim
alikuwa amenionya nisije kujaribu kufanya ujinga
kama ule kwa sababu nitakuwa nimejiingiza matatani,
akanieleza kuwa yeye alioingizwa pale akiwa na miaka
kumi na nane tu na sasa ana miaka thelathini na mbili.
Hajawahi kuipata walau njia ya kuthubutu kutoroka.
Nilipokumbuka mawaidha ya masta nikawa mtulivu.
Hadi tukamfikia Utah!
Mwarabu mwenye ngozi nyeusi, mwili mpana na uso wa
kikatili.
Nilipofikishwa mbele yake akanikamata na kunitikisa
kwa takribani sekunde thelathini.
Yule mwarabu alikuwa na nguvu ya ajabu!!
Alinitikisa hadi nikakumbwa na kizunguzungu!
“Peleka geti namba nne huyu!” alimweleza masta kwa
Kiswahili.
Masta akanichukua tena tukapita milango kadhaa,
huko nikawa nawaona watoto wa kike dhaifu kabisa
wakiwa wanashughulika, miili yao ilikuwa imelegea
haswa.
Tukalifikia geti namba nne, nikapokelewa pale masta
akazungumza na wale watu kisha akaniita kando
akaninong’oneza.
“Tajia mimi namba za simu za ndugu zako, ikiwa
utakufia huku niwape taarifa…wajue tu ati ulifia
huku.” Alizungumza kwa kusihi, hakuwa katika utani
bwana yule.
Nikamtazama kwa mshangao.
“Usinitazame machoni watauliza chenye ninaongea na
wewe… sema nambari ya simu.”
Ni kweli nilikuwa nimekariri namba za watu kadhaa
katika kichwa changu, lakini kwa kauli ile tatanishi
nikajikuta hata namba ya mke wangu naisahau
palepale.
Kifo! Nani asiyeogopa kifo, sasa masta anakitamka
kana kwamba ni kitu cha kawaida.
“Kumbuka jina langu vizuri linaweza kukusaidia….
ABDULKARIM BIN SWALEHE” alisema haya kisha
akanikumbatia na kuondoka, nilimuona waziwazi kuwa
alikuwa na wasiwasi mkubwa sana.
Nilibaki nimesimama pale kwa sekunde kadhaa kabla
sijasukumwa ndani, nikaingia katika chumba
kilichosheheni maji yaliyofanana na kutu ama matope
ya moramu!
Niligeuza macho huku na kule mara nikamuona binti
mmoja akiwa amelalakatika maji yale akiwa ametulia
tuli.
Nikashtuka na jicho langu likaganda pale nikijiuliza
nini kimemsibu binti yule.
“Do you want to help her? (Unataka kumsaidia?)”
mwarabu mmoja liyekuwa msimamizi wa chumba kile
aliniuliza, kabla sijamjibu kauli ile ikageuka kuwa
amri, akaniamrisha niende kumchukua yule binti pale.
Nikaanza kujishauri mara akanifyatua kibao kikali
usoni. Kikaniingia sawasawa!!
Nikataka kumkabili lakini nikaona kifuko cha
kuhifadhia mtutu katika kiuno chake na hakikuwa
kitupu.
“Mchukue umlete hapa!” aliniamrisha. Nikapig hatua
moja moja hadi nikaufikia ule mwili ambao sikujua
kama una uhai ama la.
Nikamnyanyua yule dada!!
Mungu wangu! Shingo yake ikaangukia upande,
nikashtuka sana kwa jinsi alivyokuwa wa baridi.
Bila shaka hakuwa hai!
Jambo hili kwa wengine lilionekana la kawaida sana,
waliendelea na shughuli zao.
Niliunyanyua ule mwili na kuupakata katika mikono
yangu na kisha nikamwendea yule mwarabu.
“Nenda ukamzike!!” aliniambia huku akitupa mikono
yake juu, kama mtu ambaye anakueleza neno ambalo
anajua huliwezi lakini anakukomesha kwa sababu
ulijifanya kulijua sana.
Nilibaki kumtazama yule bwana huku nikitamani
yatokee mauzauza yoyote yale ili tujikute tupo wawili
mahali niweze kumfunza adabu.
“Nifuate! Mjinga wewe..” alibwatuka huku akiondoka,
nami nikimfuata nyuma…mkononi nikita na maiti.
Mwili ule ulikuwa mwepesi ajabu, uliokonda kwa kiasi
kikubwa sana.
Moyo uliniuma!
Niliendelea kluwa nyuma yake, baadaye alisimama na
kunielekeza mahali pa kuupeleka mwili ule.
Nilifuata maelekezo yake!
La! Haula… niliingia mahli ambapo nilikuta miili
mingine si chini ya kumi ikiwa imetupwa hovyo, wengi
wakiwa wanawake wasiokuwa na nguo katika miili yao.
Niliutua ule mwili na sikutaka kugeuka nyuma,
niliondoka nikiwa natetemeka sana.
“Nguo zake wapi?” nilikutana na amri nyingine. Na
hakurudia yule bwana.
Nikalazimika kurejea kuziondoa nguo katika mwili wa
yule binti asiyekuwa na uhai tena.
Niliitoa nguo yake na hapo nilisahau kuhusu harufu
kali ya pale ndani, badala yake nilishuhudia alama za
mijeledi ilivyouchana mwili wa yule dada.
Pasi na shaka alisulubiwa kabla ya kupoteza uhai.
Kwanini? Na ni mpango wa nani huu?
Nilijiuliza huku nikitoka nje, nikaelekezwa pa kuitupa
ile nguo.
Kisha nikaingia kazini rasmi, kazi ya kusafisha vyuma
chakavu vyenye kutu kali ambavyo sikujua hata
vinatumika kufanya nini.
Ama! Pale gerezani palikuwa ni sawa na paradiso
kabisa, lakini hapa nilipokuwa palikuwa ni jehanamu
penye maisha ya mashaka na hofu ya kila dakika.
Hofu ya kutokwa na uhai kisha mwili wako kutupwa
kama mzoga wa mbwa koko.
Hapa sasa nikaanza kuhisi kuwa huenda ni zile laana
ambazo baba aliwahi kunambia pindi ninamgomea
katukatu juu ya kumuoa Mama Jose.
Lakini sikutaka kuziruhusu hata kidogo fikra za
kumdhania vibaya mama Jose.
 
SEHEMU YA KUMI NA TANO

Ama! Pale gerezani palikuwa ni sawa na paradiso
kabisa, hapa nilipokuwa palikuwa ni jehanamu penye
maisha ya mashaka na hofu ya kila dakika.
Hapa sasa nikaanza kuhisi kuwa huenda ni zile laana
ambazo baba aliwahi kunambia pindi ninamgomea
katukatu juu ya kumuoa Mama Jose.
Lakini sikutaka kuziruhusu hata kidogo fikra za
kumdhania vibaya mama Jose.
Ila kwa kiasi fulani nilijiona kama niliyekosea sana
kutomsikiliza mzee wangu.
____ ______

Wakati Rama nchini Oman akiwa katika mkanganyiko
wa kumuwaza Aneth na kuhisi anaweza kuwa chanzo
cha yote haya yanayomtokea.
Nchini Tanzania Aneth alikuwa hana amani hata
chembe na alikuwa ni mjane rasmi!!
_____ _____
NCHINI TANZANIA

ANETH akiwa hana nywele kichwani alikuwa amerejea
nyumbani kwa baba yake, mzee Fidelis.
Alikuwa yu mjane rasmi, lakini hakuna mwanafamilia
aliyeguswa sana na jambo hili.
Wote walihesabia kuwa ni laana kutoka kwa wazazi
wake baada ya kulazimisha kufunga ndoa na
mwanaume asiyekuwa wa dini yake.
Aneth alijua karaha ambayo angekutana nayo
akirejea nyumbani baada ya kifo cha maajabu cha
mumewe, lakini hakuwa na namna baada ya ile nyumba
ambayo alikuwa akiishi na Ramadhani kuvamiwa na
nduguze Rama wakamsimanga kuwa amemroga kijana
wao na sasa amemuua.
Jopo hili la wasimangaji liliongozwa na mzee Saidi
Matelu, baba mzazi wa Ramadhani.
Huyu alifikia hatua ya kumwapia Aneth kuwa
atamsomea albadiri ili ageuke kuwa kichaa.
Mzee huyu hakusikia lolote jambo zaidi ya kumtambua
Aneth kama chanzo cha mabaya yote yaliyomkumba
kijana wake.
Sasa Aneth akageuka kuwa mpira wa kona, huku
unapigwa na huku unapigwa… kila mtu akiusaka ili
aupige.
Nyumbani kwao kila akigusa hiki anatukanwa, akisema
hili anaonekana asiyekuwa na maana.
Afya yake ikazorota, maziwa yakagoma kutoka katika
himaya yake, Jose naye akaanza kudhoofika kwa
kukosa lishe hiyo muhimu kabisa.
Jose akajikuta akiachishwa kunyonya angali
anayahitaji sana maziwa ya mama.
Licha ya kupitia magumu haya hata siku moja mama
Jose hakuwahi kujilaumu kwa uamuzi wake wa kuolewa
na Rama ndoa ya bomani.
Kila pambazuko kilizuka kisa na kabla ya jua
halijaondoka zake kilikuwa ni kisa kingine. Vyote hivi
kwa Aneth na mwanaye ambaye alikuwa amemfanana
haswa baba yake mzazi.
Jambo hili lilimkera sana baba yake Aneth ambaye
alikuwa akiona waziwazi ile damu asiyoitaka ikiwa bado
inazunguka pale ndani.
Kuna siku Aneth alikuwa anaosha vyombo alivyokuwa
amevitumia kupika chakula…. Jose alikuwa anatambaa
akaenda hadi sebuleni, huko akamkuta babu yake,
mzee Fidelis.
Aneth akiwa hana hili wala lile mara anashtuliwa na
sauti ya Jose akitokwa na kilio kikubwa haswa,
akaviacha vile vyombo na kukimbilia sauti ilipokuwa
inatokea.
Sebuleni! Masikio yake yakamuelekeza…
Akaivamia sebule na kumkuta Jose akiwa ameketi chini
akilia kwa uchungu mkubwa sana, baba yake Aneth
akiwa ameshika gazeti akiendelea kusoma.
Aneth akamnyanyua Jose, na jicho lake likaenda moja
kwa moja mahali ambapo Jose alikuwa anajikuna.
Ebwana eeh!! Alama za vidole vya mtu mzima katika
shavu la mtoto mdogo kiasi kile.
Kilio kile kilipenyeza pia katika ngoma za masikio ya
mama yake Aneth! Naye akafika pale sebuleni na
kuuliza kulikoni.
Alimkuta Jose akiwa bado analia, huku mama yake
naye akiwa anabubujikwa machozi. Akalazimika
kuhoji.
Jamani kulikoni hapa!
“Nimemchapa makofi huyu mjinga alikuwa anataka
kuvunja chupa ya chai”….. alijibu bila kumtazama
yeyote.
“Analeta akili mbovu kama za baba yake!!” aliendelea
kuzungumza.
Wakati huo mama Jose analia kwa kwikwi tu, macho
yake yakaitazama ile chupa ya chai yenye thamani ya
kawaida akamtazama tena Jose. Kisha akamtazama
mama yake bila kusema neno lolote, alimwona mama
yake jinsi alivyoguswa na tukio lile.
Akapiga hatua kuelekea chumbani kwake bila kusema
neno lolote.
“TEna ufanye umpeleke huko kwao, mi sitaki kufuga
makaidi hapa kwangu!” mzee Fidelis akapaza sauti juu.
Aneth hakujibu! Akaenda hadi chumbani,
akambembeleza Jose hadi aksasinzia.
Baada ya hapo akamnon’oneza vitu kadhaa Jose aliye
katika usingizi.
Kisha akatoka.
Safari hii alitembea upesiupesi hadi akafika sebuleni.
“Mzee Fidelis, kwanini umenipigia mwanangu kiasi kile
hadi misuli imemtutumka?” alihoji Aneth, mzee Fidelis
akashtuka. Kwa mara ya kwanza katika maisha yake
mtoto wake wa kumzaa anamuita kwa ubini wake.
“Mtoto mdogo kama yule baba umemjaza kofi lenye
uzito mkubwa kiasi kile, amekuwa mwekunduu… Jose
hajawahi kulia kwa kiasi kikubwa hivyo… baba
kwanini….” Aneth akazidi kuhoji.
“Umeniitaje we mwanahizaya uliyefungia adabu zako
stoo kisha ukapoteza funguo .” Sasa alisimama mzee
Fidelis.
Kisha kama alivyokuwa akifanya utotoni, kufungua
mkanda na kuwacharaza wanawe wakifanya makosa,
akafanya tena asijue kuwa yule si Aneth tena bali ni
mama Jose.
Hata hakumaliza kuutoa ule mkanda Aneth akamvaa
mzee Fidelis mzimamzima akatua nay echini.
Akaliona shavu dodo la baba yake akauvuta mkono kwa
nguvu zote na kuutuliza katika shavu la baba yake.
“Sijawahi kukudharau baba, sijawahi hata siku moja…
ila umenipigia mwanangu kiasi kile cha kunitangazia
kuwa hunitaki mimi wala mwanangu katika macho
yako…. “ alizungumza huku akiendelea kumshambulia
baba yake, sasa alikuwa anamkwaruza na makucha
yake, mzee Fidelis akaanza kupiga mayowe.
“Wankuruuuuu…” mama mtu alishafika na kumuita
Aneth jina lake la ukoo huku akipiga mayowe.
Akamvaa Aneth ana kumchomoa pale.
“Mama… mama… nilipokuwa mdogo siwezi kusimama,
siwezi kusema mtu akinikosea sina akili… ukamkuta
baba yako mzazi amenifanya kitendo ambacho mzee
Fidelis amekifanya kwa Jose ungechukua hatua gani.
Usikwepeshe macho mama uliyenilea kwa miaka yote.”
Akavuta kwikwi kadhaa zilizoambatana na kilio kikuu
kisha akaendelea, “Mama mzee Fidelis na huu mkono
wake mzito amenipigia mtoto wangu mama… amempiga
Jose hadi misuli imemtutumka mama… eeh mama”
akasita akameza mate.
“Kama laana ipo naomba mnipe maana mlinilaani
zamani tu nilipochukua maamuzi yangu sahihi, sasa
naomba mnilaani… ila na yeyoye asije kuthubutu
kunitesea mtoto wangu ambaye hadi sasa hajui dini ya
mama wala baba yake….. yaani kweli mzee Fidelis
ametaka kuniulia mtoto mama….” Hakuweza kuongea
akamkumbatia mama yake kwa nguvu sana.
Hapa sasa hata mama yake hakuweza kujizuia alianza
kulia. Wakakokotana kuelekea chumbani kwa Aneth
wakimuacha mzee Fidelis akibwatuka maneno ya
kishujaa hasahasa akijitapa kuwa ile nyumba ni yake
na atamtimua Aneth.
Shavu lake lilikuwa limeumuka haswa.
Alitoweka bila kumuaga mtu, akiongozwa na hasira
huku akiwa amepanga lolote lile baya aweze kulifanya
kwa Aneth ikiwa ni namna moja ya kulipa kisasi.
Majira ya saa mbili usiku akiwa anaambatana na watu
wawili alirejea nyumbani.
Huku akamkuta mkewe akiwa mkiwa sana, akamsalimia
na hapohapo akamuulizia Aneth.
Mama akamtazama mumewe kwa muda na kisha akatoa
jibu lililozua tafrani katika kichwa cha mzee Fidelis
 
Utam unakuja utam unakata.. Nzuri... Inajenga interest...
 
niruhusu tu niendelee kukuita mdogo wake Ben R Mtobwa. Nafuatilia aisee
 
Back
Top Bottom