SEHEMU YA 8
mikumi, Tanzania
Baada ya kilio cha dakika kadhaa nilinyanyau macho
yangu na kumtazama Nasra.
“Dada Nasra, mke na mtoto wangu wakiuwawa na
damu yao iwe juu yako…. Sijawahi kuua… sijawahi
hata kufikiria juu ya hilo umeamua kunishtaki kuwa
mimi ni muuaji wa pacha wako? Ukweli wangu kwako
umenilipa haya? Kwanini lakini… eeh kwanini Nasra…
ni kweli nastahili haya…. Nitazame ngozi yangu…
nimechapwa mijeledi nimeliwa na mbu wenye dhiki kuu
ya damu… nimeishi maisha ya hofu. Lakini sikumuua
wala kumjeruhi dada yako… nilimwokoa…” hapo sasa
sikuweza kuendelea kuzungumza nikajikuta katika
kilio tena.
Ule mwonekano wa chuki ukageuka kuwa wa huruma
na hapo akanifikia akanishika mkono tukaondoka.
Huu ulikuwa mwanzo wa safari ndefu ambayo
sikuitarajia kamwe.
MSIMULIZI ANAINGIA.
MAMA JOSE aligutuka kutoka usingizini majira ya saa
nane na nusu.
Usiku wa maneno, hii ni baada ya Jose kuanza kulia.
Mama Jose akakumbuka kuwa Jose hakunyonya vizuri
siku hiyo basi pasi na shaka kile kilio kilikuwa cha
njaa.
Mama Jose akakurupuka na kumkwapua mwanaye wa
pekee huku akitokwa na maneno ya huruma topka kwa
mama kwenda kwa mwana!
Jose alipoisikia sauti ya mama lile deko la kitopto
likaongeza kilio chake.
Mama Jose hakuhangaika akampatia ziwa mwana
akaanza kunyonya kwa fujo.
Baada ya muda akasinzia, ni hapo ndipo mama Jose
akagutuka kuwa pale kitandani mumewe waliyelala
pamoja usiku hakuwepo.
Akamlaza Jose wake na kisha kwa kunyemelea
akaanza kwenda sebuleni.
Wazo lake la kwanza akafikiria kuwa Rama atakuwa
sebuleni akazungumza na simu ya siri.
Siri gani zaidi ya kuzungumza na vimada wake?
Mama Jose alijiwazia huku akizidisha umakini katika
mwendo wake wa kunyata.
Alipokaribia sebule upesi akaufungua mlango ili aweze
kumfumania mumewe.
Holaa! Hakuna mtu….
“Baba Jose….. we Rama….” Mama Jose alianza
kuita,badala ya kupata majibu aliisikia sauti yake
mwenyewe ikijenga mwangwi!
Hapo sasa ule wivu ukatimua mbio, nafasi yake
ikachukuliwa na hofu.
Mama Jose akaufikia mlango.
Akajaribu kuufungua akaukuta umefungwa kwa
funguo.
Hilo halikuwa tatizo kwa sababu alikuwa na funguo
zake za ziada.
Hapo sasa akaiendea taa na kuwasha.
Chumba kile kidogo kikaabnza kumtisha, na akili yake
ikamfikiria yule mwanamke aliyenyongwa vibaya sana
na kisha anakuja kuonekana tena katika mfumo wa
pacha.
Sasa Mama Jose alitimua mbio kali kuelekea chumbani
huku akipiga mayowe.
Mayowe yale yakamwamsha Jose akaanza kusaidiana
naye kupiga mayowe.
Mama Jose akamkumbatia mwanaye huku akifanya
sala kwa kurudiarudia.
Hakutoka kitandani hadi jogoo wa kwanza alipowika
huku akiwa bado bandani.
Kumekucha!
Mama Jose alijisemea huku nafsi yake ikiamini kuwa
mumewe amechukuliwa na jini Nasra ama kwa jina
jingine Hajrati.
Mama Jose akamweka mwanaye mgongoni, wakatoka
nje.
Hata kabla hawajazungumza na majirani mara macho
yake kwa mbali yakaona jambo lililompa tafsiri moja
tu.
Mumewe alikuwa hajachukuliwa na jini bali alikuwa
ameenda kwa kimada.
Alimuona kwa mbali akiongozana na msichana.
“Baba Jose ameniolea mke wa pili…. Uuuuwi sikubali
nasema naondoka mimi….” Alijisemea mama Jose huku
akimweka sawa mwanaye mgongoni.
Akatazama kwa makini zaidi, kweli alikuwa baba Jose
na mwanamke ambaye alikuwa hajamtambua bado.
“Heeh! Tena ameenda kuoa wa dini yake…. Eeh! Baba
Jose si ungesubiri mwanao walau akue kidogo
jamani….” Alizidi kuzungumza huku akisononeka.
Alimwona kwa mbali jinsia ya kike akiwa amejitanda
kichwani huku akiwa amemshika mkono mumewe.
Mapigo ya moyo yakamwenda mbio sana, akaanza
kuugulia uke wenza hata kabla hajatambulishwa rasmi
katika uhalali wa ndoa ile.
Mara ghafla, akaanza kupiga hatua nyuma mama huyu
mwenye shahada ya wivu wa kimapenzi!
Hatua moja ikazaa nyingine, mwishowe akajikuta
amegusa ukuta.. akatokwa nay owe la hofu.
Yowe hili likamfikia mumewe, Rama akaachana na yule
mwanamama aliyejitanda…. Akatimua mbio
kumwelekea mkewe.
Alimkuta Mama Jose akiwa katika uoga mkubwa sana,
macho akiwa ameyakodoa, si kumuelekea Rama bali
binti aliyejitanda ambaye alikuwa anakuja hatua moja
baada ya nyingine.
Rama akaufuata uelekeo wa macho ya Mama Jose
akatambua alichokuwa akikihofia. Lakini wakati
huohuo naye alikuwa katika namna ya pumbazo,
aliyakumbuka maneno ya Sajenti Pilipili kuwa mkewe
amekamatwa, lakini sasa anamuona tena!
“Si kitu mama Jose… kuwa mtulivu. Tena mtulivu
haswa…. Kuna jambo la…” kabla hajasema neno
lolote la ziada mara gari ya polisi ikafunga breki kwa
fujo nyumbani kwake. Wakashuka maaskari
wasiopungua sita…. Hawakusema neno bali
waliwavamia mama na baba Jose, wakamsukuma kando
Rama, akapepesuka na kutua chini kama gunia.
Wakamtwaa mama Jose na Jose akiwa analia katika
mgongo wa mama yake.
Wakamwingiza katika karandinga kisha kama
walivyoingia kwa fujo, wakaondoka hivyohivyo!
Huu ikawa ushuhuda wa kwanza kabisa katika safari
ya Ramadhani!
Mkewe na mtoto walikuwa wametoweka!
Hakujua kilichokuwa kinaendelea…..
Akabaki mkiwa huku akitakiwa kufanya awezavyo
kuhakikisha anamtambua Vonso ilimradi tu aweze tena
kuungana na familia yake.
Kwa sababu Rama aliwahi kuwa polisi kabla, alitambua
wazi kile kilichotokea pale kuwa ni kitisho cha awali ili
atambue wazi kuwa mkewe na mwanaye wapo
matatani na ili kurejesha amani hana budi kupambana.
Hapo akamgeukia Nasra!
“Vonso ni nani kwani?” alimuuliza kiutulivu kabisa
huku akijaribu kuidhibiti ile hali yake ya kutetemeka
kutokana na hofu.
“Ni mimi natakiwa kukuuliza wewe kaka… na sio wewe
kuniuliza mimi?” alijibu kwa ukali kiasi fulani.
Rama hakusema neno badala yake akamkaribisha
ndani.
Alizungumza naye mengi sana akilielezea upya tukio la
kukutana na Hajrati na kisha kuzipata taarifa za kifo
chake kwa kushtukiza.
Na hapa ndipo Nasra alipoinamisha kichwa chake kisha
akakinyanyua na kumtazama Rama machoni moja kwa
moja na kumwelezea jambo ambalo lilizidi kuisogeza
safari yao mbele.
ILIKUWA MNAMO MWAKA 1997, ikiwa ni miaka kadhaa
tangu uchaguzi wa kwanzqa kabisa nchini Tanzania
unaohusisha vyama vingi ulipofanyika.
Pia ile ruksa iliyoasisiwa na mzee Mwinyi ikizidi
kuchukua nafasui yake.
Mwanamama Hadija, mama wa watoto wane alikuwa
amenuia kufanya jambo kwa ajili ya familia yake.
Uzito kimajukumu ulikuwa umemzidi… akawaweka
chini watoto wake japokuwa walikuwa wadogo
akawakabidhi kwa dada yake yaani mama yao mkubwa
na kuaga kuwa anakwenda kufabnya kazi mahali na
atakuwa akiwatumia pesa za matumizi…….
Akawaaga wanawe kwa kuwakumbatia huku akimsihi
dada yake awatunze wanawe kama ambavyo angeweza
kuwatunza watoto wake wa kuwazaa japokuwa
hakuwahi kubarikiwa kupata watoto.
Hadija akawakumbatia kwa mara ya pili watoto wake
wadogo ambao walikuwa pacha, akawaasa wapendane
kwa dhati.
Watoto hawa hawakuelewa lolote lakini huu ulikuwa
mwisho wa kumuona mama yao ambaye katika ukubwa
wao wanaambiwa kuwa alienda nchi za ugenini kufanya
kazi za ndani.
Historia hii ikawa haina uhakika sana ikaenda kushoto
ikarudi kulia kisha kushoto tena ikapinduka na kupotea
katika kumbukumbu zao.
Walichoamini ni kwamba waliwahi kuwa na mama kwa
kutazama picha chache za mama yao alizowahi kupiga
enzi za uhai wake.
Ikawa mwaka na hatimaye miaka mapacha wale hata
kabla ya kufikia makamo ya kuitwa wasichana
wakaanza majukumu ya kufanya kazi kama wasichana,
kazi gani nyingine wangefanya zaidi ya kazi za ndani?
Hawakuiwa na elimu walau ya darasa moja!
Wakatumbukia katika ajira hii kwa ajili ya kumsaidia
mama yao mkubwa ambaye alikuwa anasumbuliwa na
kansa ya matiti akiwa kitandani hajiwezi.
Kansa ambayo ilisababisha mgawanyo, wale watoto
wane kila mmoja akichukuliwa na ndugu ambaye
angeweza kumsaidia.
Mama mkubwa akabaki na pacha mmoja aliyeitwa
Hajrati.
Na alikuwa ni Hajrati aliyemletea mama yake mkubwa
jambo ambalo alihitaji ushauri wa kina.
Hajrati alikuwa amekutana na kijana nadhifu ambaye
alimweleza kuwa kuna kazi amempatia inalipa kwa
kiasi kikubwa sana.
Mama mkubwa akashindwa kukubali kirahisi hadi
alipomwomba Hajrati akutanishwe na huyo kijana.
Kweli kijana akafika akiwa nadhifu vilevile na maneno
yaliyonyooka vyema katika kinywa chake, maneno
matamu ya kuvutia haswa.
Ushawishi ukachukua nafasi hatimaye mipango ikaanza
kufanyika, kijana yule mwema alisema kuwa yeye ni
mwakilishi kutoka kampuni inayohusika na mambo ya
ajira inaenda kwa jina la VONSO ALMEIDA & CO.
Limited. Jina ambalo Hajrat alilikariri kwa sababu ya
kulisema kila siku akiwa anamshawishi mama yake
mkubwa.
Ikapatikana hati ya kusafiria na mambo yote stahiki,
Hajrati akiwaza kupanda ndege na kwenda kufanya
kazi yenye kuingiza kipato kikubwa.
Siku moja kabla hajaondoka alienda kumwaga pacha
wake…… alimkumbatia na kumpa ahadi kedekede.
“Nakupenda Nasra! Nitakutumia nauli na wewe uje
nitakapokuwa…” Hajrati alimwambia pacha wake wa
kufanana.
“Usijali Nasra nawe nitakutafutia kazi sawa…Vonso
anahitaji wafanyakazi wengi ila kwa hatua ya awali
ngoja aende mwenzako” ilisikika sauti ya kijana yule
nadhifu.
Na ule ukawa mwisho wa Nasra kuonana na Hajrati
hadi siku ile alipokuja kufananishwa katika daladala na
hatimaye kufikia hatua ya kushuhudia maiti ya pacha
wake katika namna ya kutisha sana.
Kesi ikamuangukia Rama na sasa Nasra anatakiwa
kushirikiana naye ili waweze kutatua jawabu.
Jawabu juu ya Hajrati aliyetoweka miaka saba
iliyopita na kisha kurejea kimyakimya na kushuhudiwa
akiwa maiti!
Zaidi ya yote jawabu juu ya Vonso na kampuni yake.