NITAKUPATA TU
SEHEMU YA 086
"Tulieni Hivyo hivyo, kisha wewe tupa silaha yako chini." Ilikuwa sauti kutoka nyuma yao. Sauti ambayo haikuonyesha utani ndani yake. Veronica Akatii kwa kuitupa Bastola Chini. Akatulia tuli huku akiamini kuwa inaweza kuwa amesalitiwa na huyu Dereva. Wakati akiwaza hilo akakatishwa na sauti ya mtu huyu. "Nyie ni nani? Na kwa nini mko hapa?. Veronica akabaki kimya huku akimuangalia dereva ambaye alimtia tumaini kwa kuwa hakuonyesha kujali. "Ni mimi Charles, nimemleta huyu dada ana mgonjwa ambaye hali yake sio nzuri." Alijibu dereva huku akionyoosha kidole kama ishara ya kumuonyesha. Huku akiwa amekamatia Sub Machine Gun Mtu yule aliyekuwa akionekana kama mtu mzima. Kitendo cha kuiona ile bunduki kulimpa Veronica hisia. Hisia kuhusu mtu huyu ambaye alijibadilisha ili aonekane Mganga. Mganga gani amejengeka kimazoezi kwa aina Hii? Mganga gani ameweza kuikamata SMS kwa Staili hii? Yalikuwa maswali ambayo hayakuwa na majibu. Maswali magumu. Kwa mara nyingine sauti ya mwanaume huyu ikatamalaki katika ngoma za Masikio yao. "Muingizeni Ndani mtu huyu, fanyeni haraka." Veronica na dereva wakasaidiana kumuingiza Masimba ndani akiwa bado na Hali ile. Baada ya Masimba kuingizwa ndani. Taa za kijumba kile zikawashwa. Baada ya Taa kuwashwa, dereva na Veronica wakaangaliana. Kuangaliana kulikotokea baada ya mtu yule kumuita Jina Masimba. Veronica ndiye aliyeshikwa na mshangao kuliko hata dereva. Kile alichokuwa akikiwaza mwanzo, kitu ambacho alikuwa na uhakika nacho kuhusu mtu huyu. Alihisi alikuwa usalama , alihisi alikuwa ni mtu ambaye aliwahi kuwa sehemu fulani. "Masimba, masimba, unatatizo gani? " aliita mtu yule huku akimtingisha masimba. Lakini bado masimba hakuweza kuitika. Alikuwa ametulia kama Maiti.. Veronica bado alikuwa kwenye bumbuwazi. Bado alikuwa kwenye mshangao. Hata mwanaume yule alipoingia kwenye kichumba kidogo, bado Veronica alikuwa katika mshangao. Maswali lukuki yalikuwa yakikipita kichwani kwake. Bado alitaka kumfahamu huyu mtu, akalazimisha macho yake yamuangalie mwanaume huyu ambaye mara hii alikuwa ametoka akiwa na kiboksi mkononi. Hata huyu mwanaume naye akamtizama, akamtizama kwa aina ya kutaka Veronica ajue kuwa yeye alikuwa nani. Wakaangaliana tena na Tena. Veronica alikuwa akikitizama kile alichokuwa anataka kukijua. Alikuwa anamuangalia Mtu ambaye alikuwa ni mmoja kati yao. Macho yao yakatizamana tena na tena huku yakiongea. Mwanaume yule alimruhusu Veronica kusoma kila kilichopo ndani yake. Ni muda huo ambao Veronica akimtizama mtu huyu, akakiona kingine mkononi kwa Mtu yule. Kitu ambacho kilimthibitishia kile ambacho alihitaji kukijua. Mtu yule alikuwa ameishika sindano na kichupa chenye dawa ambayo ilitumika kutolea sumu kwa mtu yoyote ambaye angehisiwa kuchomwa sindano ya Sumu. Hakubisha kuwa huyu mtu alikuwa jasusi. Licha ya kuwa Jasusi, lakini bado hakujua alikuwa nani na alimtambuaje ama kumjua Masimba.
Baada ya kuishika ile sindano, mtu huyu akasogea mpaka pale alipolala masimba na kupiga magoti. Akaichoma sindano kwenye mfuniko wa kichupa na Kuivuta. Baada ya dawa kujaa kwenye bomba akautafuta mshipa mmoja mwilini na kuchoma ile sindano. Baada ya Kuchoma na kuiruhusu dawa kuingia mwilini mtu yule akainuka na Kuingia chumbani. Safari hii akatoka na kitu mfano wa kalamu, lakini ndani yake kukiwa na dawa ya Majimaji. Baada ya kufika hapo tena akautanua Mdomo wa Masimba kisha kuimimina Dawa kinywani. Baada ya kufanya Hivyo.. akamfunika vizuri kisha kukaa pembeni Yake. Macho yake yalikuwa yakimtizama masimba tu kwa muda wote. Yalikuwa yakimuangalia kanakwamba hakuwa akikiamini alichokuwa akikiona. Macho yake yalionyesha kitu ambacho kilimvuta Veronica. Macho ya mtu huyu yalikuwa yakiongea na mwili wa masimba. Hakuwa akiongea kwa mdomo lakini macho yake yalikuwa yakikizungumza kitu fulani. Baada ya Dakika kumi kupita huku ukangaliana kule kukiichukua sehemu yote ya kijumba na kuuleta Ukimya. Masimba akaanza kukohoa mfululizo. Tabasamu usoni kwa veronica halikukauka. Nguvu na imani kuwa masimba alikuwa salama ikarudi kichwani mwake. Lakini aliporudisha macho kwa mtu huyu bado alikutana na hali ile ile, bado mtu yule alikuwa akimuangalia masimba huku macho yake yakizungumza. Yakizungumza kile ambacho kila Veronica alipotaka kukisoma hakufanikiwa. Masimba akaendelea kukohoa mfululizo, damu ikishuka Kutoka mdomoni, damu ikiruka kila pale alipokuwa akikohoa. Kwa mara ya pili mtu huyu aliinua uso na kumuangalia Veronica, kisha dereva aliyemleta Veronica. "Mnaweza kuondoka sasa mkamuacha mgonjwa hapa. Veronica hutakiwi kulala hapa usiku huu. Hutakiwi kwa kuwa ulichokifanya unaweza kupewa Adhabu ya kifo. Unajua adhabu za Kundi la Mafia lilivyo." Yalikuwa maneno yaliompumbaza veronica, maneno yaliomshtua na hata kumtia baridi. Hakutegemea kujulikana mapema hivi. Hakutegemea mtu huyu angeweza kumjua hivi. Huyu ni nani? Lilikuwa Swali lililohitaji majibu kutoka Kwa Mtu Huyu. Lilikuwa swali ambalo majibu angeweza kuyapata kumtoka kwa mtu huyu. Mtu ambaye alionyesha kumjua kuliko mwenyewe anavyojijua. Veronica akabaki ameduwaa akimuangalia mtu huyu. Alikuwa akimuangalia katika namna ambayo Ilimfanya mtu yule atambue kuwa kuna kitu kinahitajika. "Hii kazi ni ngumu Veronica. Nilitambua Masimba alikuwa akipambana pasipo kumjua Teddy na Pasipokukujua wewe. Lakini hayo yote tutayaongea baada ya kuupata muda. Unatakiwa kuondoka hapa usijekulifanya suala hili kuwa kubwa." Aliongea yule mtu huku safari hii akihamisha macho yake kumuangalia Dereca. "Charles naomba umpeleke huyu dada mpaka dar es salaam. Pitia barabara zile zile ambazo tulikuwa tumepita." Alitoa maagizo mtu huyu huku akisimama na kuingia tena Chumbani akiwaacha Veronica na Charles wakiendelea kuangaliana. "Tuondoke Hapa Veronica. Aliongea Dereva yule akisimama tayari kwa kuondoka. Veronica naye akafanya hivyo.
******
"Nahitaji kumjua yule mtu." Aliongea Veronica akimwambia Charles walipokuwa Njiani kurudi Jiji dar es salaam. "Unadhani mimi namjua?" Akauliza Charles Huku akiwa kwenye usukani. "Nafikiri unamjua ama kama Humjui, basi utakuwa na ufahamu kidogo juu ya mtu yule." Akajibu Veronica. Charles hakuongea chochote akanyamaza kwanza akionyesha kufikiria kitu. "Simfahamu Zaidi ya hapo. Ila kuna wakati niliwahi kuhisi kuwa labda mtu yule alikuwa Usalama Wa Taifa ama mtu ambaye aliwahi kuwa katika Shughuli inayofanana na kitu kama hicho." Akajibu Charles. "Kitu gani kilichokifanya uhisi kuwa labda alikuwa mtu Wa Idara nyeti? Akaendelea kuuliza Veronica. "Kuna wakati nilikuwa nikikutana na watu fulani ambao ukiwaangalia unaweza kudhani ni Makamandoo wale tunaowaona kwenye TV. Kuna wakati nilikuwa nikikuta mpaka Raia Wa Kigeni." Akajibu Charles, majibu ambayo yalianza kumfanya Veronica Aanze kuhisi kuwa alikuwa sahihi kuwaza. " wewe ulijuana naye vipi? Akauliza Tena Veronica.
"Tulikutana kwenye bar moja maeneo ya bagamoyo mjini. Yeye alikuwa pembeni akiwa amekaa sambamba na Binti mmoja mwembamba hivi. Nilikuwa hapo nikipata moja moto moja baridi. Sasa wakati tuko hapo wakatokea wababe fulani wakataka kumchukua mwanamke yule ki nguvu. Ndipo hapo nilipomuona akifanya kile ambacho hufanywa na watu tunaowaona kwenye Video. Jamaa alikuwa akipiga Ngumi na Mateke kama Jean Claud Van Damme. Alikuwa akiruka hewani na samasoti kama Jet Li. Hapo ndipo kila mtu pale akashangaa. Kwanza muonekano wake ulionyesha kuwa alikuwa Mtu mzima. Lakini kile alichokuwa akikifanya pale utadhani alikuwa kijana. Basi baada ya Valangati ile kuisha wale watu wakatupotea katika mazingira fulani ambayo hakuna mmoja kati yetu kwenye ile Bar Alitegemea. Waliondoka mfano wa kuyeyuka. Ni katika kuondoka hapo ndipo nilipookota pochi yake ambayo alionyesha kuidondosha wakati wa purukushani. Pochi Hiyo ndiyo iliouleta ukaribu na mtu Huyu. Ukaribu ambao ulinikutanisha na watu wengi wa Ajabu. Pia kuna siku niliiokota Hii picha katika eneo lile." Aliongea Charles Akimkabidhi Veronica picha ndogo. Vero akaichukua kisha kwa kutumia Mwanga Wa Simu Akaiangalia. "The Bastard.....??? Ilikuwa sauti kutoka kwa Veronica Huku mshangao ukigubika uso wake. Macho yake yalikuwa yakiitizama Sura ya Mwanaharamu, macho yake yalikuwa yakiitizama Picha ya Nemisis. Macho yake yalikuwa yakimtizama mpelelezi Mashuhuli Afrika. "Kuna kitu ndani yake na kuna namna kwa mtu yule kuwepo pale msituni. Nataka kumfahamu kwa nini yuko pale na Kwa nini picha ya mtu huyu imekutwa pale." Aliongea Veronica Akionyesha kushangaa.
"Una mfahamu huyo mtu?" Lilikuwa swali kutoka kwa Charles. "Yeah namfahamu zaidi. Sasa nimepata picha na kujua ni kwanini mtu huyu ananijua kiasi hiki na kwa nini anamjua Masimba. Nitamjua tu Ni Nani." Akajibu Veronica huku akiiendelea kuitizama picha ile.
******
Mji wa bagamoyo na vitongoji vyake ulikuwa katika hekaheka kubwa kutoka katika vyombo vya dora. Askari wenye makwanda na waliovaa kiraia walikuwa wakizunguka katika Mji wote wa bagamoyo wakiwa na picha ya Masimba mikononi mwao. Idara ya usalama wa Taifa ilikuwa imesambaza wapelelezi wengi katika kila kona kunusa huku na huko. Taarifa ya kutoroshwa kwa Masimba iliitingisha Serikali sambamba na Idara zake. Mikutano mitatu ya Siri ilikuwa imekwishafanyika katika sehemu tatu tofauti. Kikao cha kwanza kilifanyika Katika Ubalozi wa Marekani, Cha pili kilifanyika Kwenye nyumba za Siri za Serikali. Wakati cha tatu kilifanyika Ikulu. Vikao vyote hivyo havikufikia muafaka baada ya washirika kuhisi kuwa kuna usaliti umefanyika mpaka kufanikisha kutoroka kwa Masimba. Kila sehemu ilikuwa ikipekuliwa na kila nyumba ilikuwa ikiangaliwa kwa namna ya pekee. Askari walikuwa wakihaha huku kila wakati wakipokea maelezo kutoka kwa wakubwa zao. Mpaka inafikia saa kumi za Jioni hapakuwa na fununu ya wapi pale alipo masimba. Camera za usalama ndani ya kambi ya Siri ya Usalama wa Taifa zilionekana kutokuchukua picha ya aina yoyote. Kingine ambacho kiliongeza ugumu walinzi ambao walikuwa zamu usiku huo kila mmoja alikutwa akiwa amekufa kwenye Chumba chake. Kila mmoja alikuwa amechinjwa shingo. Hilo likavifanya vikao kuendelea kuitishwa ikulu. Kwa mujibu wa taarifa ambazo ikulu na Idara ya Usalama ilikuwa nayo ni kwamba. Masimba Hakuwa na Uwezo wa kutembea wala kusimama. Pia walikuwa na Taarifa kuwa sindano aliyochomwa asingeweza kuchukua wiki atakuwa Ameshapoteza Maisha. Sasa kama Taarifa Imekuja kwamba Masimba Ametoroshwa, Kwa nini Walinzi Waliokuwa zamu wameuawa sehemu zao walipokuwa wanaishi? Ina maana hawakuuawa usiku, bali waliuawa asubuhi. Kama ni Asubuhi ni nani ambaye ameua? Inaonyesha huyu muuaji alirudi kuja kuufuta Ushahidi baada ya usiku kumtorosha masimba. Kama hivyo ndivyo ilivyokuwa, aliyefanya mauaji haya ni mtu anayefahamika. Ni mtu ambaye analifahamu suala hili. Yalikuwa mawazo ya wajumbe wote waliokuwepo katika kikao kile. Kikao ambacho kiliirudisha Taharuki miongoni mwao. Taharuki ambayo haikutakiwa kupewa nafasi kwa wakati huo. Simu zikapigwa sehemu mbalumbali za Nchi. Majasusi Wa Idara ya usalama wa Taifa walikuwa wakihaha kila kona. Wakati Ndani Ya Nchi ya Tanzania Msako ukiendelea. Teddy alikuwa ndani ya Jiji la Nairobi Akiwa na majasusi wa CIA sambamba na Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani. Walikuwa katika kikao kizito kilichokuwa kikijadili kuhusu uwezekano wa kuendeleza Biashara na Nchi ya Tanzania. Pia alikuwa hapo kupokea Zawadi ambayo ilitolewa na Rais Wa Marekani kama Pongezi ya Kufanikisha kwake kuipata betri. Ni wakati wakijadili hilo, Teddy akapokea Taarifa kutoka kwa Marafiki zake. Ni taarifa hiyo ambayo ilimfanya asimame haraka. Usimamaji wake Ulimshangaza kila mmoja pale ndani. Hata macho ya wajumbe wale yalipomtizama Teddy, wakayaona Mabadiliko makubwa. Alikuwa amebadilika kama sio kuchanganyikiwa. Midomo yake ilikuwa ikicheza akitaka kuongea kitu. Lakini hakuweza kufanya hilo. Hakuweza kuongea Tena. Punde akautwaa mkoba wake na Kutoka Nje ya kikao pasipo kuongea chochote. Ilikuwa ni lazima Arudi Dar es Salaam kwa wakati huo. Alitaka kwenda kuhakikisha kile alichoambiwa. "Ni nani aliyemtorosha masimba na kuwaua Walinzi? Lilikuwa Swali lililomkuta Teddy Akiwa Ndani ya Tax akielekea uwanja wa Ndege wa Jomo kenyatta TAYARI KWA KURUDI TANZANIA.