Riwaya: Mwanamke Uliyekula Pesa Zangu Nakutafuta

Abtali mwerevu

JF-Expert Member
May 5, 2013
637
432
Mwanamke Uliyekula Pesa Zangu Nakutafuta
Mwandishi: Mwalimu Makoba

Sehemu ya Kwanza

Nilipita siku ya Jumatatu huko Mwananyamala katika nyumba za ndani sana. Baada ya kuvuka mitaro mitatu, nikaona nyumba iliyokuwa na baraza kubwa. Hapo barazani alikaa binti mrembo sana ambaye kwa uzuri wake angetosha kushtua, kuchanganya na kupunguza ufanisi wa akili ya mwanamume yeyote. Binti huyu aliyekuwa na sura iliyochongeka kwa mfano wa umbo la yai, alivalia dela lililoficha umbo lake.

Nilitembea hata nikawa mkabala na mahali alipokaa, nikaporomosha salamu huku nikipunga mkono, “Habari.”

“Nzuri,” msichana alijibu akibadili mkao, nami nikaendelea na hamsini zangu.

Nilipita siku ya Jumanne huko Mwananyamala katika nyumba za ndani sana. Baada ya kuvuka mitaro mitatu, nikaona nyumba iliyokuwa na baraza kubwa. Kama jana, binti yule alikaa, nami nikaporomosha salamu, “Habari.”

“Nzuri,” msichana alijibu akibadili mkao, nami nikaendelea na hamsini zangu. Lakini wakati nikitembea, nilisikia vishindo vikija. Nilipogeuka, niligongana uso kwa uso na msichana niliyemsabahi.

“Kaka…” aliita akitazama chini kwa aibu. “Naomba nisaidie elfu moja.”

Sikufikiria mara mbili, nilitoa mfukoni noti moja ya shilingi elfu moja nikampa. Kisha nikatoa kikaratasi na kalamu, nikaandika 1,000/=.

Nilipita tena siku ya Jumatano eneo hilohilo. Baada ya salamu, binti alinifuata akaniomba elfu moja, nikampa kisha nikaandika katika kikaratasi changu.

Nilipita kwa mara nyingine eneo lile siku ya Alhamisi. Binti akaomba elfu moja. Nikampatia kisha kama kawaida nikaandika katika kikaratasi. Sasa hesabu jumla ilisomeka shilingi za Kitanzania elfu tatu.

Basi nilivutiwa na upitaji wa njia ile, Ijumaa nayo nikapita. Kama kawaida binti akaniomba elfu moja, nikampa kisha nikaandika kwenye kikaratasi changu. Wakati nataka kuendelea na hamsini zangu, alinidaka mkono akaniomba tukae kibarazani kwa muda.

“Huwa unaandika vitu gani ukinipa hela zako?” msichana aliuliza akinitazama bila aibu, huenda alikwisha nizoea.

“Huwa naandika hela ninazokupa. Sasa zimefika shilingi elfu nne,” nilijibu nikitabasamu.

Binti aliangua kicheko, kisha akasema, “Mwanaume bahiri wewe, sijawahi kuona… jina lako nani wewe?”

“Naitwa Mako.”

“Oooh… kumbe!”

“Unafanya kazi gani bwana wewe?”

“Sisi wengine kazi zetu huwa hazitajwi,” nilijibu kisha msichana akacheka tena.

“Ukipita hapa huwa unakwenda wapi?”

“Huwa nakwenda maeneo tofauti, leo nakwenda Kibo Peak kutuliza kichwa.”

“Oooh, nikipata nafasi ya kutoroka nitakuja… Usiondoke mapema,” kabla hajaendelea, vilisikika vishindo vikija kutokea ndani.

“Babuu anakuja, kimbia haraka asikuone,” alinisisitiza, nami nikakimbia kwa kasi kumshinda mwanariadha Usain Bolt. Njiani niliwaza mambo mawili: Babuu ni nani? Na huyu msichana niliyeongea naye jina lake nani? Nilipata kona nzuri nikajificha, nikatazama ili nimuone huyo Babuu, hakuwa mzee kama lilivyo jina lake, alikuwa kijana au mwanamume wa makamo makadirio miaka arobaini mwisho hamsini. Alivaa mavazi chakavu, juu kichwa kipara na chini alikuwa na kandambili. Sikutaka kuchunguza sana, nikaondoka.

Inaendelea Kesho...

Tupate Wadhamini:

Kwa Mahitaji ya kuandikiwa CV, Barua ya Maombi ya Kazi na Masomo kwa Wanafunzi wanaorudia mitihani, Gusa Hapa Tuwasiliane Whatsapp.
 
Mwanamke Uliyekula Pesa Zangu Nakutafuta

Sehemu ya Tatu

Burudani iliendelea kutoka kwa ma Dj ambao nilitambua walikuwa wawili na walifanya kubadilishana, muda huu alisimama mwingine, mwembamba, kavaa kiatu cheusi kirefu na amenyoa kiduku. Nikasikia kionjo, “Auto waharibiee.” Nikabaini bila ya mashaka yoyote kuwa, pale palikuwa na Dj Auto Run.

Ulipigwa wimbo wa Amapiano, nikashangaa kuona Asi akiwa na filimbi mdomoni, alipuliza filimbi yake kufuatisha filimbi ya kwenye wimbo, mbali na kupiga filimbi, alicheza kwa maringo hata akawa kama kishada kilichokata kamba.

Hata hivyo, burudani ilielekea ukingoni pale Asi alipoomba arejee nyumbani kwani mida ile ingekuwa rahisi kwa Babuu kuamka. Niliagana naye, nami sikukaa sana, nikaondoka kuelekea makazi yangu.

Mengi hayajulikani kuhusu mimi na sitaki kuyasema. Lakini katika Jiji la Dar es Salaam kwa sababu sikwenda kukaa kwa muda mrefu, basi niliishi katika Nyumba ya Wageni iliyoitwa London Lodge. Nyumba hii ya kulala wageni ipo Kinondoni, pembezoni kabisa mwa mahakama ya Kinondoni, mahakama nzuri ya kisasa, na ungetazama mbele ya geti la London, ungeiona shule ya Sekondari Kambangwa.

Nilipewa chumba ambacho sikumbuki namba yake, ila nakumbuka kilikuwa chumba kilichokaribiana sana na mapokezi. Vyumba vingine vilivyokuwa mbele, vilipachikwa majina ya miji, japo sikumbuki vizuri, lakini nadhani kipo chumba ambacho kiliitwa Spain.

Ndani ya chumba changu palikuwa na kitanda cha chuma kilichokuwa na godoro laini, sofa la mtu mmoja jeusi na choo pamoja na bafu. Huduma zote nilizotaka nilizipata, na niliwaomba wenyeji wangu kwa kuwa nilikuwa mkazi wa siku nyingi, basi chumba changu kiheshimiwe, na asiingie mtu yeyote kusafisha bali shughuli zote ningezifanya mimi, na niliwaomba, funguo nitembee nayo muda wote ninapotoka. Walinielewa, maisha yangu yakawa mazuri mno. Hata hivyo palikuwa na kero moja ambayo niliivumilia, dari lilionekana kuoza na vumbi lake lilielekea kunisababishia mafua.

Maisha yangu katika nyumba hii ya wageni, kwa muda wa mwezi mmoja tu niliokuwa nimekaa, nilishudia vioja vingi, lakini kikubwa zaidi ya vyote, ilikuwa ni fumanizi. Jamaa mmoja alimfumania mke wake, lakini huyu bwana aliyemfumania naye ni jamaa aliyekuwa akimdai. Basi alifoka sana na mwisho alisikika akisema, “Mayombi, deni lako tumemalizana, hunidai tena!”

XX XX XX​

Mara kwa mara niliendelea kupita alikoishi Asi, kama kawaida yake, aliomba pesa ndogo, nikampa kisha nikaandika katika kikaratasi changu. Sasa jumla ilifika Shilingi elfu kumi na tisa za Kitanzania.

Katika kumbukumbu nzuri, nakumbuka kwenda Coco Beach na Asi, huko tulikula mihogo ya kuchoma, tukaogelea na kuzungumza mengi.

“Bwana Mako,” Asi aliniita.

“Naam,” niliitika.

“Uliwezaje kuwadhibiti wale wezi wa siku ile, tena wakiwa na silaha?”

“Unajua…” nilisema nikitafakari namna ya kubadili mazungumzo ili asinichimbe sana. “Katika Jiji hili la Dar es Salaam, kuna watu wanajiona wao ni wababe mno na huwaambii chochote. Achana na huo mkasa, nakumbuka siku moja nikitoka katika matembezi yangu, jamaa mmoja alisimama katikati ya njia na kuniamrisha nitoe pesa.

“Jamaa yule wala hakuwa na silaha yoyote na alikuwa peke yake. Nilimuuliza, Unajiamini nini kutaka kuniibia mimi tena ukiwa peke yako? Jamaa akawa mkali na akaanza kusogea nilipokuwa. Alipofika hatua tatu ili aweze kunifikia, nilimpiga ‘jebu’ moja iliyofuatiwa na ‘right’ akadondoka chini huku analia, Umenipiga na jiwe, umenipiga na jiwe! Nilimsogelea alipodondoka na kumuonyesha mikono yangu huku nikisema, “Siyo jiwe ni ngumi!”

Asi alicheka sana, sikutaraji kama simulizi ya mkasa wa mapigano inaweza kumchekesha mtu. Msichana alicheka, nikaona kabisa mbavu zinamuuma na almanusura adondoke na kiti kama isingekuwa kuwahi kukikamata.

Ni katika siku hiyo niligundua kuwa Asi alikuwa mgeni katika Jiji la Dar es Salaam, binti huyu alitoka Tanga na alikuwa na jambo fulani na Babuu. Hata hivyo, hakunieleza Babuu ni nani na alifuata nini hapa mjini.

Tulikaa mpaka saa 12 jioni, tukaanza kurudi nyumbani kwa mwendo wa kutembea polepole. Mimi kushoto, Asi kulia.

Inaendelea...

Tupate Wadhamini:

Kwa Mahitaji ya kuandikiwa CV, Barua ya Maombi ya Kazi na Masomo kwa Wanafunzi wanaorudia mitihani, Gusa Hapa Tuwasiliane Whatsapp.
 
Mwanamke Uliyekula Pesa Zangu Nakutafuta

Sehemu ya Nne

Tulichukua njia za ndanindani tukaibukia katika kanisa la Mtakatifu Petro. Ni katika kanisa hili, Marehemu Rais John Pombe Magufuli, alizungumza kwa mara ya mwisho kabla hajafikwa na mauti. Nakumbuka katika hotuba yake alisema hajakataza watu kuvaa barakoa ili kujikinga na Ugonjwa wa UVIKO-19, wengine wakiuita Korona. Ila alisisitiza kwamba, barakoa zingine ni mbaya na tuwe makini.

Hakuishia hapo, alimpongeza paroko kwa kitendo chake cha kutovaa barakoa, na alishangazwa na Masista wawili waliokuwa wamevaa barakoa. Nakumbuka alisema, “Anayeilinda nafsi yake, ataipoteza.”

Yeye hakuvaa barakoa, na hakukataza watu kuvaa barakoa, ila hakuziamini barakoa kutoka mataifa ya nje. Kuna mahali aliwapongeza sana watu waliokuwa wamevaa barakoa za kushona wao wenyewe. Alisikika akisema, “Vita ya uchumi ni mbaya.”

Alikuwa mzalendo kwelikweli aliyetamani taifa lake lipende vyake. Ndiyo maana hata katika kupambana na gonjwa la Korona, alihamasisha watu wajifukize.

Niliendelea kuuchapa mwendo na Asi, sasa tulivuka barabara ya Ali Hassan Mwinyi, kushoto tukauona ubalozi wa Ufaransa.

“Unaona jengo lile?” nilimuuliza Asi aliyekuwa kanishika mkono.

“Naliona,” msichana alijibu.

“Pale ndiyo gaidi Hamza aliwasumbua sana askari. Kile kijengo kidogo cha pembeni kile cha kukaa mlinzi, alijificha humo na kuanza kuwachachafya askari na ‘SMG’ mbili alizopora kwa askari haohao.”

“Walikufa askari wengi eeeh?”

“Sina uhakika, ila nakadiria walikufa watano.”

“Kwa nini Hamza aliamua kufanya hivyo?”

“Baada ya tukio, baadhi ya watu walisema alidhurumiwa madini yake na askari hivyo alikuwa katika harakati za kulipa kisasi. Hata hivyo, uchunguzi ulipotoka, vyombo vya sheria vilisema Hamza alikuwa kijana wa hovyo tu na hakudhurumiwa chochote ila alikuwa mtu wa hovyo, gaidi. Vyombo vya sheria vikasema tena na kuwaomba sana wazazi wasizae watoto wa hovyo kama Hamza.”

“Utajuaje kama umezaa mtoto wa hovyo?” aliuliza Asi akinitazama, mbele akapita muuza karanga, nikamsimamisha na kununua za shilingi mia tano zikiwa zimewekwa katika kikaratasi, chache nikamimina katika kiganja cha Asi, nyingi nikabaki nazo. Usinione mchoyo, baadae nilimuongeza.

“Mtoto wa hovyo…” nilikumbusha nikitafuna karanga. “Ni ngumu kufahamu, lakini simlaumu aliyesema hivyo pengine zilikuwa ni hasira za kupoteza askari wake. Laiti kama ningekuwepo siku hiyo, ningehesabu risasi anazorusha Hamza, zingefika risasi sitini, basi ningebaini bunduki zake mbili zimekwisha risasi, na hapo ndipo ningejitokeza mbele yake na kumkamata kama kuku.”

Asi alinitazama, akatabasamu, halafu akajisogeza karibu yangu zaidi, tukaendelea kutembea, tukitafuna na kuzungumza.

Mwisho tulivuka Barabara ya Kawawa. Tukakiona kituo cha Mwendokasi cha Morocco. Mradi wa mwendo kasi ulilenga kupunguza kero ya usafiri, lakini mimi sikuona upunguzaji wa kero hiyo. Niliishia kusikitika tu kuona jinsi abiria wa Mbezi walivyojazana kwenye huo mwendokasi, wengine walikosa pa kukanyaga wakiwa humohumo kwenye mwendokasi. Mtu pekee aliyekuwa amekaa kwa huru mwendokasini humo, alikuwa ni dereva. Akina siye waliibiana, wakauzidisha umasikini wao maradufu. Halafu kauli chafu za madereva, ati “We mzee geuka kule shika bomba!” Kauli gani hizi? Kauli za kishwaini ushenzi.

Tuliukanyaga mdogomdogo nikiwa na kiumbe mdogo wa kike. Tena, nilimsindikiza mpaka mitaa ya kwao na tuliagana, mimi nikarudi katika makazi yangu ya muda. London Lodge.

Baada ya siku tatu bila kupita mitaa yake Asi huko Mwananyamala ndanindani, nilipita tena ili niweze kumuona msichana huyu. Hali ilikua tofauti kuliko siku zote, msichana hakuwepo. Nilitazama kama kweli ni nyumba ileile ambayo tangu nianze kupita sijawahi kumkosa akiwa kakaa kibarazani, ilikuwa nyumba ileile na msichana hakuwepo. Hata hivyo sikuwa na wasiwasi, nilihisi huenda alikuwa na kazi humo ndani.

Nilipita tena siku iliyofuata, msichana hakuwepo. Nikapita siku nyingine, hakuwepo, nikapita tena na tena mpaka chovya chovya ikamaliza buyu la asali, lakini msichana hakuwepo. Hapo nikapatwa na hofu, hofu ya kupotea kwa mwanamke aliyekula pesa zangu. Shilingi halali za Kitanzania elfu kumi na tisa. Pengine hazikuwa zile pesa, kwani ni pesa kidogo sana zisizotosha hata kununua simu ndogo ya Kichina, pengine nilianza kumpenda Asi, binti mdogo aliyekuwa na tabasamu pana, mwepesi kuzoea watu tena aliyechangamka vyema. Basi baada ya pitapita ya siku nyingi bila kumuona, nikaahidi kumtafuta mpaka nimpate.

Inaendelea...

Tupate Wadhamini:

Kwa Mahitaji ya kuandikiwa CV, Barua ya Maombi ya Kazi na Masomo kwa Wanafunzi wanaorudia mitihani, Gusa Hapa Tuwasiliane Whatsapp.
 
Mwanamke Uliyekula Pesa Zangu Nakutafuta

Sehemu ya Tano

Siku zote nilikuwa naishia nje nimtafutapo Asi pembezoni mwa nyumba aliyokuwa akiishi. Sasa niliamua, niingie mpaka ndani, huenda Babuu alimkataza kutoka.

Nilifika katika nyumba ile, nikagonga mlango kwa dakika nyingi bila kufunguliwa. Mlango ule ulikuwa mkubwa tena wenye pande mbili zilizokutana katikati ambako palikuwa na kitasa. Baada ya gongagonga bila majibu, nilijaribu kuzungusha kitasa, hapo nikagundua palifungwa. Sikuelewa kama mwenye nyumba alikuwa ndani au alitoka, hayo ndiyo matatizo ya vitasa!

Hata hivyo nilihisi wenye nyumba hawakuwepo. Niliamua kupeleleza kidogo kuhusu nyumba ile na wakazi wake, kwa kuwa sikutaka kujulikana kama nilikuwa ninapeleleza, niliamua kutafuta watoto wadogo, hawa wasingeweza kunitilia shaka lolote.

Niliingia katika chumba kimoja cha biashara kilichokuwa kimeandikwa ‘play station’. Ndani yake mlikuwa na watoto waliokuwa wanacheza michezo mbalimbali ya kompyuta. Nami nilikwenda moja kwa moja mpaka katika sehemu moja iliyokuwa wazi, nikaomba niwekewe GTA, haraka nikawekewa na nikaanza kucheza.

Haikuchukua hata dakika moja, watoto watano walikuwa nyuma ya mgongo wangu wakitazama jinsi nilivyokimbizana na maaskari katika mchezo ule wa GTA.

“Nani anaweza kunisaidia kuwakimbia hawa askari?” niliuliza.

“Mimiiiiii!” watoto wote walijibu. “Wewe unaonekana unajua sana, kaa hapa uendelee, halafu nyinyi wengine, mtakuwa mkipeana naye zamu, nitalipia hela ya siku nzima leo mcheze tu mpaka mfike mwisho. Halafu wewe rafiki yangu, hebu njoo hapa nje mara moja nataka nikutume kitu,” nilisema nikimshika mkono mtoto mmoja, makadirio miaka tisa, ambaye alionekana mjanja zaidi ya wengine.

Nilikaa katika kiti nje ya chumba kile cha michezo. Niliyekaa naye tayari nilishamfahamu jina lake, aliitwa Iki.

“Iki, ile nyumba nani anakaa?” niliuliza nikinyooshea kidole nyumba ambayo nilimuona Asi akiishi.

“Anayeishi hapo ni mgeni,” alijibu Iki akichungulia wenzake walivyokuwa wakiifaidi GTA.

“Iki tukimaliza mazungumzo, nitakulipia sehemu ya peke yako ucheze bila kupeana zamu na mtu. Haya endelea, anayeishi hapo ni mgeni, eheee…”

“Kahamia juzi juzi tu.”

“Aliyekuwa anaishi hapo mwanzo ni nani?”

“Bibi Martina, sasa watu walisema yeye ni mchawi kwa hiyo akaamua kuhamia Mbeya kwa mtoto wake Boni.”

“Sasa Iki hiyo nyumba anaishi mtu mmoja tu?”

“Hapana, Dada Asi anaishi naye, huwa anakaa pale nje na anapenda sana kuongea na watu, kuna siku alikuja humu akaomba tumfundishe kucheza gemu. Alisema yeye hela siyo tatizo, kuna kaka yake huwa anapita na humpatia shilingi elfu moja kila siku.”

Nilitabasamu niliposikia jibu hili. Nilitambua wazi kuwa, zile elfu moja ni zile ambazo nimekuwa nikimpa kila nilipopita. Kumbe alizitumia kujifunza kucheza gemu kama alivyosema Iki. Iki hakunyamaza, raha ya watoto wadogo hawana hofu na wakifunguka hufunguka kwa kusema yote wayajuayo. “Ila kuna siku…” alidokeza halafu akanitazama usoni, akaona kunitazama haifai, akainamisha kichwa chake chini. “Kuna siku mama alisema mle ndani kuna wasichana wengi tu!”

“Kuna kingine alisema baada ya hapo?” niliuliza nikitazama pembeni ili Iki asiniogope.

“Hapana, hata yeye hajui sana.”

Niliridhishwa na majibu ya Iki. Nikamuita kijana aliyeshughulika na ofisi ile, nikampatia kiasi cha fedha nikimsisitiza Iki aachwe acheze ‘game’ peke yake bila bughudha, wale wengine niliowaacha wakipeana zamu, niliongeza malipo yao pia.

Taarifa za Iki kuwa mle ndani kulikuwa na wasichana wengi zaidi zilinishtua. Nilipanga usiku wa siku hiyo, lazima ningeingia ndani ya ile nyumba ili nifanye uchunguzi wa mambo mawili matatu.

Inaendelea...

Tupate Wadhamini:

Kwa Mahitaji ya kuandikiwa CV, Barua ya Maombi ya Kazi na Masomo kwa Wanafunzi wanaorudia mitihani, Gusa Hapa Tuwasiliane Whatsapp.
 
Sehemu ya Sita

Saa nane usiku nilikuwa nje ya mlango wa nyumba. Nilivalia sweta jeusi, suruali nyeusi na viatu vyeusi hata nikawa sehemu ya giza. Nilifungua kitasa kwa funguo yangu bandia isiyoshindwa kufungua milango mingi. Mlango ukatii kwa kufunguka taratibu.

Niliiingia na kuufunga mlango taratibu, kisha nikaanza kutembea kwa tahadhari kubwa. Sikutaka kuwasha taa, kwanza sikufahamu vilipokaa viwashio, nikatumia tochi yangu. Ilikuwa nyumba ya vyumba sita. Katikati korido, pembeni kushoto vyumba vitatu na pembeni kulia vyumba vitatu.

Nikiwa nasogea, nilikwaruzwa na kitu mguuni, nikazima tochi haraka halafu nikaganda kama sanamu, mkono ukiwa kiunoni nilipoipachika Beretta. Baada ya sekunde tatu, nikawasha tochi, nikaishia kumuona paka mkubwa, silaha ikarudi kiunoni, sikuwa pale kupambana na nyau!

Vyumba vitano havikufungwa, nilivichunguza vyote, nikaona dalili za watu kulala humo kwa kurundikana. Niliona magodoro chakavu yaliyopangwa kivivu, ndoo nne za kuogea kwa kila chumba na vipande vya sabuni.

Baada ya kumalizana na vile vyumba vitano, sasa nikakiendea kile chumba cha sita kilichokuwa kimefungwa. Nilitumia funguo yangu, mlango ukafunguka. Tofauti na vile vyumba vingine vilivyokuwa na magodoro machafu na mrundikano wa taka, hiki kilikuwa kizuri, tena kuna kitanda kikubwa na chini pamesakafiwa kwa vigae vya kuteleza. Hata wewe tayari umegundua kwamba, hiki ni chumba alichoishi Babuu.

Nilikichunguza lakini sikupata chochote cha maana. Zaidi niliiishia kuona misokoto miwili ya bangi iliyokuwa imefichwa ndani ya mto wa kulalia. Nilipangilia kila kitu vyema kisha nikaondoka kurejea katika makazi yangu.

Silaha niliyokuwa nayo, Beretta, iligunduliwa na mtaalamu Bartolomeo Beretta mwaka 1526 huko Gardone Val Trompia nchini Italia. Ni silaha nzuri ya kawaida ambayo imekuwa ikitumiwa na watu binafsi kwa kujilinda.

Kama alivyo mtaalamu Bartolomeo Beretta, nami mtaalamu Mako, niligundua silaha kubwa ya maangamizi niliyoipachika jina Mako 29.

Mako 29, ina uwezo wa kupiga risasi 3,000 kwa dakika na inaweza kumdhuru adui akiwa umbali wa hata kilomita mbili. Ukichunguza kwa makini utagundua Mako 29, imeishinda AK 47 ya Warusi na M16 ya Wamarekani karibu mara tatu au tano, pengine hata kumi hesabu zikifanywa vyema. Silaha hiyo tayari ilikuwa mikononi mwa jeshi letu, na walikuwa wanaifanyia mazoezi ili ianze kutumika. Hata hivyo, kwa sababu mimi ndiyo mbunifu wake, nilikuwa nayo moja niliyoificha kwa siri. Na hata ningetaka, ningetengeneza nyingine. Mpishi hafi kwa njaa!

Ni kama utani, lakini zilikatika wiki tatu bila kumuona Asi wala kupata fununu zozote zenye msaada zaidi ya zile taarifa za Iki. Sikukata tamaa, niliendelea kutembeatembea nikiwa na matumaini ya kuona chochote chenye msaada wa kumpata.

Kwanza utajiuliza Asi siyo ndugu yangu, lakini namtafuta sana kwa nini? Hata nikijibu namtafuta kwa sababu ya zile pesa, shilingi elfu kumi na tisa za Kitanzania bado italeta mashaka. Vipi nikisema nilianza kumpenda msichana huyo halafu nikaongeza hoja kwa kusema, kulinda watu wasipotee wala kunyanyaswa ni jukumu langu, nisiongee sana. Wengine sisi, kazi zetu huwa hazisemwisemwi.

Mtembea bure si sawa na mkaa bure. Siku moja saa nne usiku niliamua kutoka niende matembezini. Nilipita katika geti nikakata kulia kama askari. Nikafuata njia nikikunja kona hii na ile mpaka nilipokuwa katika njia fulani ambayo pembeni kushoto kuna zahanati ya Kambangwa na kulia kuna hospitali ya Rufaa ya Mwananyamala. Nilitembea nikavuka barabara, kisha nikanyoosha na kuingia katika danguro.

Katika danguro hilo, wanawake walijiuza kila mmoja akiwa kakaa katika mlango wa chumba chake, na kama ungevutiwa naye, ungeingia ndani naye angekufuata. Malipo hayakuwa makubwa, shilingi elfu tatu zingetosha kukupatia huduma.

Kwa hivyo, lilikuwa jengo lenye vyumba vingi, lililowekwa njia upande huu na ule ili watu wapite kujionea biashara hiyo ya nyama. Mimi sikupita hapo kununua, tutunze afya zetu tafadhali. Nilipita hapo kusafisha macho, na pengine labda ningemuona mtu niliyemtafuta.

Wakati nikiendelea kutembea katika danguro lile, niliona wateja wakiingia na kutoka, bila shaka wameridhishwa na huduma. Wanawake ambao hawakuwa na wateja, walinitazama kwa uchu tena kwa kunitamanisha haswaa.

Lakini sikuwa na bahati, nikikaribia kulitoka danguro hilo, askari walivamia na kutuamrisha wote tukae chini. Sasa nikawaza kosa langu nini, ukahaba au kupita njia ile?

Inaendelea...

Tupate Wadhamini:

Kwa Mahitaji ya kuandikiwa CV, Barua ya Maombi ya Kazi na Masomo kwa Wanafunzi wanaorudia mitihani, Gusa Hapa Tuwasiliane Whatsapp.
 
Sehemu ya Saba

Askari walituchukua wanaume wakitufunga mashati wawiliwawili mpaka kwenye gari lao kubwa. Nakadiria tulikuwa wanaume ishirini, wenzangu wote walikamatwa wakiwa kwenye vyumba vya makahaba au wakiwa wametoka kupata huduma au wakivizia huduma. Ni mimi pekee niliyekamatwa kwa sababu ya kupita pale, sikuwa na mpango wowote na watu wale zaidi ya kusafisha macho na kumtafuta Asi.

Jambo moja lilinishangaza, japo tulikamatwa katika danguro, ni wanaume tu ndiyo tuliwekwa kwenye gari. Wanawake wale waliokuwa wakiifanya biashara ya ukahaba, hakukamatwa hata mmoja, na kuna baadhi ya askari niliwaona wanafunga zipu zao baada ya kutoka kwenye danguro. Nikashangaa tu!

“Aloo polisi kanitoa nimeshalipia, kaingia yeye kula zigo,” alilalamika mtuhumiwa mwenzetu mmoja aliyekuwa upande wa mlango wa gari kubwa la polisi. Mimi nikashangaa tu!

Wakati tupo kwenye lile gari, askari wawili walikuwa wanatulinda, baadae wakarudi wenzao wawili, wakabadilishana, waliotulinda mwanzo wakakimbia kuelekea kwenye danguro, walipotoka, walikuwa wanafunga zipu zao. Nikashangaa tena!

Tukiwa kwenye gari tulishtushwa na sauti ya afande, “Nyie wachinga… Kila mmoja atoe elfu thelathini aachiwe au twende kituoni.”

Watuhumiwa wenzangu wapatao kumi na tano walitoa kiasi hicho cha fedha. Watano walipiga simu kwa jamaa zao wakatumiwa, wakasindikizwa na askari Tumbotumbo kwenda kwa wakala kutoa fedha hizo na huko wakaachiwa. Sasa tulibaki wawili, mimi na jamaa mmoja ambaye baadae niligundua anaitwa Chafu Tatu.

Chafu Tatu alipenda sana kwenda katika danguro lile na alikuwa maarufu sana kwa mtindo wake. Huenda katika danguro akiwa na shilingi elfu kumi. Elfu moja ananunua sigara. Anabakiwa na elfu tisa. Elfu tatu anapata huduma kwa dada wa kwanza. Anamaliza nakutoka nje, anavuta sigara. Anatoa elfu tatu tena kwa dada wa pili, anatoka na kuvuta sigara, halafu anatoa elfu tatu kwa dada wa tatu, akimaliza hapo, anaenda nyumbani kulala. Chafu Tatu!

“Chafu Tatu,” aliita askari.

“Naam afande,” aliitika Chafu Tatu kwa adabu.

“Hela unatoa au hutoi?”

“Afande naomba unielewe, tayari nilikuwa nimeshaingia kwa dada wa pili, sasa nina elfu tatu tu,” alijibu Chafu Tatu, askari wakaangua kicheko, wakachukua ile elfu tatu na kumuachia kwa masharti kwamba, asirudie tena tabia hiyo kwani ni mara ya saba sasa anakamatwa.

Chafu Tatu alishuka katika gari lile la polisi. Nikabaki mimi na wao.

“Kijana acha kutuchelewesha, leta hera haraka,” alisisitiza askari ambaye kwa sababu ya tumbo lake kuwa kubwa sana, nilimbatiza jina, Tumbotumbo.

“Pesa zangu hazipo hapa afande,” nilijibu.

“Zipo wapi?”

“Zipo kwenye simu.”

“Twende kwa wakala ukatoe basi, mbona tunacheleweshana au unataka kurara ndani?”

“Twende tukatoe afande hakuna tatizo,” nilikubali nikaongozana na Tumbotumbo kuelekea kwa wakala.

“Jina lako nani?” aliuliza Tumbotumbo.

“Mako,” nilijibu nikitembea kawaida.

“Una jina moja kama mbwa?”

“Ndiyo,” nilijibu nikimtazama usoni, huku naongeza mwendo. Tumbotumbo akacheka akiyafinya macho yake madogo. Hapo nikakimbia haraka na kuvuka barabara inayopita magari yaendayo kwa Mama Zakaria. Tumbotumbo akanikimbiza, lakini nilishavuka barabara na sasa alishindwa kuvuka kwa sababu magari yaliyopita ni mengi. Sikumjali tena, nikaingia ndanindani huko, nikakunja kona nyingi, nilipojiridhisha, nikavuka barabara katika kituo cha Komakoma, huyoo nikaelekea katika makazi yangu.

Inaendelea...

Tupate Wadhamini:

Kwa Mahitaji ya kuandikiwa CV, Barua ya Maombi ya Kazi na Masomo kwa Wanafunzi wanaorudia mitihani, Gusa Hapa Tuwasiliane Whatsapp.
 
Sehemu ya Nane

Sasa ilikatika miezi miwili na wiki moja tangu kumpoteza Asi. Nimefanya juhudi hii na ile kumtafuta lakini sijampata. Likizo yangu pia, ilikuwa imebakiwa na wiki tatu tu. Katika hali ya kukata tamaa, niliamua kwenda kusalimia wagonjwa katika hospitali ya Mwananyamala.

Majira ya saa kumi jioni, mwanamume aliyevalia suti ya kijivu na viatu vyeusi alionekana akipita katika geti la hospitali na kwenda moja kwa moja mpaka katika wodi ya watoto. Hakupata shida kupita getini kwa sababu ya ile suti lakini pia, ule ulikuwa muda wa kuona wagonjwa. Mwanamume huyo, alikuwa mimi Mako. Mtu mwenye jina moja kama mbwa!

Niliingia mpaka ndani ya wodi iliyohudumu watoto wadogo, vitandani walilala watoto na pembeni walikaa wazazi wao. Nilianza kwa kumsalimia mama mmoja aliyekuwa vitanda vya mwanzo karibu na mlango.

“Mama mwanao amepatiwa matibabu,” niliuliza baada ya salamu.

“Hajapatiwa baba, wamesema mpaka helaa!” alijibu Mama wa mtoto, machozi yakimlenga.

“Matibabu ni lazima, pesa italipwa baadae,” nilisema kwa sauti iliyosikika pote mle. Mama mmoja aliyekuwa kitanda cha tatu akadakia, “Mheshimiwa hata mwanangu hajapatiwa matibabu,” kabla sijakaa sawa, bibi mmoja akapaaza sauti, “Mkuu wa mkoa nisaidie mjukuu wangu hajapewa dawa siku ya tatu baba.”

Ama hakika bibi yule sijui aliwaza nini kuniita mkuu wa mkoa! Ni kweli siku tatu zilizopita, mkuu wa mkoa alibadilishwa ama wengine wanasema alitumbuliwa na wananchi hawakumfahamu vyema mkuu wao mpya ambaye hakuwa ameanza kuonekana katika Luninga.

Sasa kitendo cha yeye kuniita mimi mkuu wa mkoa, kiliamsha watu wote wodini mle, macho yao yakawa kwangu hata manesi na madaktari wakanyanyuka katika siti zao wakija mahali niliposimama.

“Nkuu wa Nkoa kaja kwa ku shtukiza… patachimbika humu ndani nakwambia, atatumbuliwa ntu baada ya ntu,” alisema bibi mwingine aliyekuwa anamuuguza mjukuu wake.

“Unapiga simu wapi?” nilimfokea nesi ambaye alionekana kupiga simu kuwaita wakubwa wake. “Usipige simu, usimuite yeyote, hapa nimekuja kwa kushtukiza na nitaingia kila wodi kwa kushtukiza.”

“Sawa mkuu,” walijibu watumishi wale wa afya. Wagonjwa wakatabasamu.

“Sasa sikiliza,” niliendelea. “Wagonjwa watibiwe, pesa italipwa baada ya matibabu, tuhakikishe tunaokoa uhai kwa gharama yoyote. Pesa zipo tu na haziwezi kamwe kufanana na thamani ya uhai wa mwanadamu.”

“Ndiyo mkuu,” walijibu.

“Natoka humu katika ziara yangu hii ya kushtukiza, msipige makelele wala msinifuate, pia msipigiane simu, nakwenda kwenye jengo lile wodi ya wazazi, nawatakia utekelezaji mwema.”

Nilitoka katika wodi ile na kuanza kuelekea wodi ya wazazi. Nilikuwa na hofu kwamba, watu wangeongezeka zaidi, lazima ningegundulika kuwa mimi siyo mkuu wa mkoa. Hii ingekuwa kesi kubwa tena ya aibu. Vilevile sikuwa nimepanga kuwa nitambulike hivyo, ni watu niliowakuta wodini ndiyo walinipachika cheo hicho.

Nilitembea haraka nikazipandisha ngazi za jengo la wodi ya wazazi. Nilikuwa napiga jicho nyuma kwa kuibia, kumbe maelekezo yangu hayakufuatwa, kuna manesi walishapiga simu na nyuma kiasi cha hatua mia mbili, niliona watu wengi wakija nilipo, niliweza kuwatambua watu hao, mmoja wao alikuwa Daktari mkuu wa hospitali hiyo. Alikuwa anakuja nilipo akiongozana na madaktari wengine watano na askari watatu.

Sasa niliiona hatari iliyokuwa inaninyemelea. Daktari mkuu na wenzake wote wasingeshindwa kutambua kuwa mimi sikuwa mkuu wa mkoa hata kama mkuu mpya wa mkoa hakuwa ameanza kuonekana katika Luninga. Wazee hawa wanawafahamu viongozi wote kwani ni jamaa zao.

Nilitembea haraka nikalifikia jengo la wazazi na sasa nilikuwa ndani ya jengo hilo lililo juu kimo cha ghorofa moja. Niliwaacha mbali watu wale lakini nao walikuwa wakija kwa kasi zaidi. Niliingia wodini kama ninayesalimia watu. Jengo hili lina upande wa kushoto na kulia, mimi nilielekea kulia, nikatembea mpaka mwisho na bahati njema, mapokezi hapakuwa na daktari wala nesi na wodi nzima ilikuwa na mgojwa mmoja tu aliyekuwa anaongezwa damu na alilala usingizi.

Nilifungua dirisha kubwa la vioo kisha nikatoka kwa kushuka taratibu, nilipoona kimo cha chini ni kidogo, nilijitupa kikomandoo, kisha kwa kuinama, nikakimbia mpaka ulipo ukuta, nikauparamia kama mjusi na kuukwea mpaka kilele chake, halafu ‘puuu’, nilikuwa nje ya hospitali. Huko nyuma sikujali kama kuna mtu aliniona au hakuniona.

Mwisho wa Sehemu ya Bure ya Riwaya Hii, Endapo unahitaji kununua riwaya yote Gusa Hapa.
 
hichi kipande kimenikosha,mkuu tafadhali ongeza hata kimoja tu cha mwisho
 
Similar Discussions

Back
Top Bottom