Riwaya: Msako wa mwehu

Riwaya: Msako wa mwehu

SEHEMU-24

Ilikuwa ni barua iliyoandikwa kwa maandishi ya lugha ya kiarabu. Akaisoma mpaka akafika mwisho, kisha akavuta pumzi kubwa Kachero Yasmine. "Ina nini hiyo barua?" alishindwa kuvumilia Kachero Manu maana alikuwa haelewi chochote kutoka kwenye ile barua, kwake ilikuwa ni makorokocho tu kama ya watoto wa chekechea.
"Usijali Bosi wangu, huyu tumuombee azinduke ana mengi ya kutuelezea tena atatufikisha mpaka kwa mama yake "Maso Maso", maana hii ni barua ya kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto. Huenda huyu ni posta wao. Wakafanya haraka kumuingiza kwenye gari kisha Kachero Yasmine akalikimbiza mpaka hospitali ya jeshi. Baada ya hapo Kachero Manu akapiga simu kwa askari wa kikosi maalumu waje kuondosha mizoga kimya kimya kabla hakujakucha na kuvuta hisia za waandishi wa habari.
Hii ilikuwa ni operesheni chinjachinja adui kimya kimya, mpaka gaidi wa mwisho atiwe mbaroni. Baada ya hapo akarejea kwenye gari lake na kumpeleka hospitali mkewe wamcheki afya yake kisha baada ya hapo ndio warejee nyumbani. Alikuwa anaonekana amesakarika kutokana na uchovu na njaa.

SURA YA KUMI NA MBILI
Ngome ya Al-shabaab ndani ya Wilaya ya Kilindi - Tanga
Watu 4 kwa idadi ambao ni wafuasi wa "Al-Shabaab" walifika Wilayani Kilindi tokea mwaka 2008. Walikuwa wametokea Somalia wakiwa wameiva vilivyo mafunzo ya ugaidi. Malengo ya Al-shaaab yalikuwa ni kusimamisha ngome zao imara katika maeneo mbalimbali ya Afrika Mashariki. Kuanzia Mombasa-Kenya, Tanga, Zanzibari, Rufiji-Tanzania na Pemba ya Msumbiji. Wageni hao walifikia katika Kijiji cha Lwande, kwa muda waliishi na wanakijiji wa Lwande, na wanakijiji wakawa wamewapokea kama waislamu wenzao.
Walikuwa ni watu rahimu na wenye tabia zenye kunukia mauwaridi kijiji kizima. Kila mtu alitamani awafanye kuwa ni marafiki wa familia yake au kama wakitaka kuoa au kuongeza wake basi waje kuolea kwenye mji wao. Walikuwa ni mahodari wa kazi mbalimbali kama kilimo na ujenzi majumba.
Kizuri zaidi walikuwa wanaonekana ni watu wanaomshiriki Mwenyezi Mungu kupita maelezo. Msikitini nako wakaaminiwa kuendesha baadhi ya vipindi vya swala. Walionekana wanasoma Kurani kwa kuipendezesha masikioni mwa msikilizaji.
Wakaanza kusambaza fitina za chini kwa chini kuwagombanisha waislamu wa kijijini wenyewe kwa wenyewe na viongozi wao bila wenyewe kujua kuwa wanapigwa majungu na wageni hao. Wanapita huku na kuzusha uwongo huu na wataenda kule na kuzusha zogo jipya.
Waislamu wa kijijini pale wakaanza kupoteza umoja wao, vurumai na kitimutimu mtindo mmoja kikaibuka, ikawa mwendawazimu kaingia nyumba ya shetani. Waumini wakawafurusha viongozi wao wa msikiti wakiwatuhumu kuwa hawana elimu ya dini, wanawasomea Qur'ani majaka na kuisoma kimakosa kwa kuimong'onyoa. Rungu la uongozi sasa wakakabidhiwa vijana hao wageni wa "Al-shabaab".
Ikawa ni kama kumpa paka kazi ya kulinda maziwa. Wakaanza sasa vibweka vyao baada ya kudhibiti uongozi. Baada ya muda walianza kutoa mafundisho ambayo hayaendani na utamaduni wa Kitanzania. Mfano wakaanza kufundisha elimu ya mazingira ni haramu mutlaki. Hivyo watoto wa Kiislamu wasome Madrasa pekee wasipelekwe shule za elimu dunia.
Wakaanza kupandikiza chuki dhidi ya waislamu wanaofanya kazi serikalini kuwa wamesharitadi. Wakifa wasizikwe kiislamu kwa sababu wanaitumikia serikali ya Kisekula isiyoamini dini. Kutokana na mafundisho hayo butu, yaliyojaa shonde. Baadhi ya wananchi wakang'amua wanapoelekea sipo. Wakaanza kuwahoji wapi wanatoa mafundisho hayo ya ajabu. Wakafarakana na wanakijiji wakajitenga na kununua eneo lao kisha wakajenga msikiti unaitwa "Madina".
Lengo kuupa msikiti wao jina hilo ilikuwa ni kufananiza kitendo cha Kiongozi wa dini ya Kiislamu Ulimwenguni, Mtume Muhammad (S.A.W) kufanya hijra kutoka Mji wa Makkah kuelekea Mji Madina alipofanikiwa kuisimamisha Dola ya Kiislamu.
Wafuasi wao sasa waliendelea kuongezeka na wengi wakitokea Jijini Dar es Salaam, Kigoma na Singida. Wengine walitokea nchi za jirani kama Kenya na Somalia. Kiongozi Mkuu wa msikiti huo akijulikana kwa jina la "Master" ambalo lilikuwa maarufu Kilindi nzima. Huyu alipachikwa jina la "Master" baada ya kuanza kuutumia msikiti wa Madina kama sehemu ya kufanyia mazoezi na mbinu za kigaidi.
Walifahamika kuwa ni magaidi walipoanza kunyanyasa wenyeji kwa kupora mashamba ya wenyeji bila fidia. Maelezo yao kwa wenyeji ilikuwa ni kwamba ardhi ni mali ya Allah, na wao wametumwa na Allah kusimamisha utawala wake duniani hivyo ni haki kwao kuichukua bila fidia. Idadi ya wageni katika kambi hii ikaanza kuongezeka zaidi kadri miezi inavyozidi kusonga. Baadae wakajitanua hadi katika msitu wa Dibungo, katikati ya Kilindi na Bagamoyo.
Katika msitu huo walihodhi ardhi yenye ukubwa wa ekari 500 iliyonunuliwa na Bwana Kareem Abdallah, Meneja wa "Chops Carwash & Garage". Katikati ya eneo hili wakajenga uwanja wa mazoezi. Kwa nje walijenga vibanda kuzunguka eneo hili, na hakuna mtu aliyeruhusiwa kuingia katikati ya msitu huu. Pia walijenga msikiti katika msitu huu, na walikuwa wanafanya mazoezi mara mbili kwa siku. Walikuwa wanafanya mazoezi saa 11 alfajiri baada ya kumaliza swala ya asubuhi na saa 11 jioni baada ya kumaliza shughuli zao za kilimo na ufugaji.
Uhusiano kati ya wafuasi hawa wa "Al-Shabaab" na wanakijiji wa maeneo yaliyozunguka kambi yao hii ulizidi kuzorota siku hadi siku. Wenyeji wengi ni wafugaji, lakini wafuasi hawa wa "Al-Shabaab" walianzisha utaratibu wa kutoza kodi ya mifugo au faini ya mifugo kwa ngombe wanaoingia kwenye msitu huu. Hatari iliyo kubwa zaidi, kambi hii ikawa inatumika kutoa mafunzo kwa vijana ambao wakionekana wameiva tayari wanasafirishwa kutoka Kilindi, kupitia Mombasa na kwenda Somalia kujiunga na kundi la al-Shabaab, wao na wake zao waliotafutiwa kupitia mtandao 'Facebook' kupitia akaunti ya 'NUSRA COMMITEE'.
Usiku walikuwa wanajiliwaza kwa kuangalia video, mikanda ya vita vya Jihadi sehemu mbalimbali duniani. Kulikuwa na mikanda yenye mafundisho ya "Al-Shabaab", yenye kusisitiza kuwa Afrika Mashariki imekamatwa na makafiri, hivyo wanafundishwa namna ya kuikomboa kijeshi. Mpaka kufikia mwaka 2013 ikawa ni kambi ya siri iliyojiimarisha vilivyo yenye zana za kivita toshelevu.
Hivyo "Maso Square The Duduman" baada ya kukamilisha kazi aliyotumwa Tanzania ya kulipua jengo la Wizara ya Mambo ya Ndani na kuua vigogo kadhaa na kuifanikisha vizuri aliteuliwa kwenda kuiongoza kambi hiyo kubwa ya Kilindi akitoa amri zote kutoka mafichoni. "Maso Maso" alikuwa anaishi katika mapango ya Amboni, yeye na wateule wake wachache na wanamgambo wao wachache.
Huku ndiko alikuwa akiletewa ripoti zote za kinachoendelea kwa njia ya maandishi tu. Alikuwa hatumii simu wala kompyuta wala chombo chochote cha elektroniki. Ilikuwa ni kama kujaribu kumpitisha ngamia kwenye tundu la sindano kama utataka kumkamata "Maso Square The Duduman". Mpaka kumfikia yeye ilitakiwa upambane na "Makomandoo" zaidi ya 25 ndio uwafikie kundi la "Wasagaliwa" 10 mgambo waaminifu. Wasagaliwa hao toka nchini Somalia walikuwa ni wanaume mahanithi ambao hawatamani mwanamke kimaumbile kwa namna walivyozaliwa, hivyo huwezi kuwashawishi wamsaliti "Maso Square The Duduman" kwa pesa kwa sababu wanalipwa vizuri wala kwa wanawake kwa sababu hawana matamanio.
 
Hatari sana nilisema kwenye bonde la mzakwe hawatoki salama maana sehemu hiyo imekaa vizuri ktk umbush asante sana poti
 
Muendelezo inakuwaje kiongozi, tujiliwaze tu maana biashara hata hazifanyiki sijui ni hela hamna au corona
 
SEHEMU-25

Bi Mwantumu sasa anakula pweza gizani, matunda ya mwanawe
Bi. Mwantumu ilipita kama miezi 8 tu tokea mwanawe apatwe na umajinuni ndipo alikuja kung'amua mtoto wake kumbe ni mwehu feki. Kwanza alianza kuona viroba vya mchele, sukari, ngano na maharage havikauki nyumbani kwake kutoka kwa wanaojiita wasamaria wema, waliovalia mavazi ya kiustaadhi. Waliokuwa wanajifanya wanamuonea huruma kutokana na sakata la mwanawe pekee wa kiume kuugua uchizi. Akawa anajiuliza hapati majibu "hivi wenye watoto vichaa wote wanapata huduma kama hizo au yeye tu!".
Baada ya siri kubumburuka baada ya picha za mtoto wake kuhusishwa na ugaidi kuanza kusambazwa na serikali, wale wasamaria wema wakakata mguu. Walikuwa wanahofia vyombo vya dola watalala nao yombo. Aliyempasha kuhusu ugaidi wa mwanawe alikuwa ni shosti wake yule yule wa kufa na kuzikana Bi.Mwazani.
Siku hiyo isiyo na jina Bi.Mwazani alipata nakala ya gazeti pendwa kwa habari za kiuchunguzi Jijini Dar es Salaam la "Motomoto" likiwa limechambua makala inayomhusu "Maso Maso" namna anavyohusika na ugaidi wa matukio kedekede nchini Tanzania. Halahala bila ajizi kiguu na njia, Bibi asiyetulia maskamoni kwake kama amekula miguu ya kuku, Bi.Mwazani mpaka kwa shoga yake akiwa na nakala yake mkononi.
"Hodi hodii baada ya salamu mwanetu katuvua nguo tupo uchiii huko mitaani, hatuna pa kufichia nyuso zetu" alikuwa ni Bi.Mwazani huku tayari kurupukurupu huyo ameshaingia mpaka sebuleni na kujipweteka kwenye sofa pweteee. Huyo ndio Bi Mwazani alikuwa hawezi kulala na umbea, muda wote akipata umbea moyo wake unakuwa unapaparika, koo lake linamuwasha, anatafuta wa kumsimulia ndio roho yake itulie. Kuiweka habari anayoisikia kiporo alikuwa hawezi. Shoga yake alipopewa mchapo wote na Bi Mwazani ikabidi aitafute miwani yake na kujisomea mwenyewe uzuri alipitia madarasa ya ngumbaru hivyo kusoma haikuwa shida. Bi Mwantumu alibaki hoi bin taabani amechoka na vituko vya mtoto wake.
"Mie nimezunguka kwa waganga na waganguzi na mpaka nilisurika kubakwa na mganga, Shekhe Mbonde kule Rufiji. Nikaponea chupuchupu ili yeye apone uchizi kumbe alikuwa anatuzuga tu eeeh...ameuza jina lake kwa kina cha povu mwanangu..!" aliropoka Bi Mwantumu huku ameshika tama shavuni. Sasa mambo yakawa kweupe hadhiri kuwa mwanawe ni gaidi namba moja nchini anayesakwa kwa udi na uvumba na vyombo vya dola. Bi Mwazani alivyoaga kurudi kwake baada ya kuutua umbea kama kawaida yake na kibomu juu.
"Shoga kama mchele wetu ule wa msaada wa wale Maustaadhi umebaki nijulie hali na mimi, jiko nyumbani limenuna, na mwanetu Maso kashalitifua huko tifuu sijui kama hatukurudi kwenye kula chakula cha jela ugali au wali wa mtama kama njiwa vile". Ikabidi rafiki yake Bi Mwantumu abaki anatabasamu tu, huku anakwenda kumchotea kilo za mchele zilizokuwa zinamalizikia tena, mbwa ukimjua jina hakusumbui, Bi Mwantumu anamjua shoga tokea utotoni alishamzoea vibweka vyake.
Sasa Bibi wa watu ikawa kila akipita mitaani watu wanamsoza vidole. Wengine kutaka kumrusha roho kabisa wale wenye roho za ikidi na inda, watovu wa adabu wakawa wanaenda kudurufu picha nyingi zenye tangazo la kutafutwa kwa mwehu "Maso Maso" halafu wanakuja kumbandikia picha mpaka mlangoni pake bibi wa watu, asubuhi akiamka anakutana nalo mlangoni kumkera tu bibi wa watu. Binadamu wabaya wewe acha tu unaocheka nao mchana hao hao usiku ndio wanaokung'ong'a.
Bado mapolisi, wale akina afande kunyoa mabwenzi kama ndege shore wanaokuja kupiga kambi kutaka kumtoa upepo bibi wa watu kwa kumtisha kumrundika ndani. Bado vijana wa mtaani waliposikia dau la milioni 100 kwa atakayeripoti alipo "Maso Maso" zikawa zinawatia wazimu. Wapo waliokuwa wanakesha mtaani kusubiria nazi mdondo huenda atajitokeza nyumbani kwao walau siku moja wakatoe ripoti kwenye vyombo vya dola.
Mashababi wengine wakawekeana zamu kula chabo kwa doria mpaka usiku wa maneno wakiwa na ndoto huenda siku moja akateleza kuja kumsalimia mama yake. Bado mabanati wazuri, wenye uzuri wa zuhura, vidosho vya nguvu wenye maumbile ya kusababisha kadi za Benki na pochi za Mapredeshee zipate ugonjwa wa degedege la kutaka kuwahonga. Eti nao walijileta kwa Bi Mwantumu kujifanya kuomba kazi ya uhadimu wa kazi za ndani.
Ama kweli ukistaajabu ya Musa utayaona ya Firauni, kweli walimbwende wanataka kuja kujipaka masizi kwenye kusugua sufuria za Bi Mwanatumu!. La hasha si kweli hata kidogo, nia na madhumuni kumpekunyua tu Bi Mwantumu huenda anaweza kuropoka siku moja akaelezea mahali alipojificha mwehu "Maso Maso" au kumuona akija nyumbani kwa mama kwa kificho, wakajichukulie kiangaza macho kwenye vyombo vya dola. Ili mradi Bi Mwantumu alikuwa kwenye shida tamaamu haswa.
"Maso Maso" nae akili yake ilikuwa inachemka barabara hakuwa zumbukuku ulimwengu uko huku, ikabidi abuni mbinu mpya ya kupeleka msaada na kufanya mawasiliano na mama yake mzazi. Mbinu ikawa kila usiku wa Alhamisi ya mwisho wa mwezi kuna dua maalumu ilikuwa inafanyika nyumbani kwa mama yake. Alikuja siku moja "Maso Maso" nyumbani kwao Sinza kuhudhuria dua majira ya magharibi akiwa amejibadilisha kama mwanamke wa kiislamu aliyevalia juba zuri kuja kuweka mambo sawa na kuomba msamaha kwa mama yake.
Hakuna hata mmoja aliyemtambua baki wakware tu wale wasioogopa hata wanawake waliovaa mavazi ya heshima wakabaki wanataka kumchombeza watoke nae kimapenzi. Akabaki anawachora tu kwenye kizoro chake kilichoziba uso wake na kuacha macho tu anawasanifu mngenijua mimi ni nani ningewadonyoa risasi za tumbo. Huku mkononi ameshika tasbihi kujifanya hataki mchezo kwenye utajo wa Allah hata kidogo.
Sheikh Jamsheed, Shekhe maarufu Sinza yote na vitongoji vyake ndio alikuwa anaongoza hiyo dua alikuwa ndio amepewa jukumu la kumpa pesa na barua Bi Mwantumu Kila itakapobidi na akatambulishwa kwa mama "Maso Maso". Alikuwa ni Shekhe mwenye heshima na sharafu kubwa Sinza nzima. Shekhe ambaye hakuna mtu angemuhisi kuwa ni jasusi la "Al-shabaab".
Watu wakaanza kushangazwa mambo yake Bi Mwantumu yanamuendea vyema hayateteleki lakini hawamuoni jembe lake "Maso Maso" kuleta mafao yoyote. Mpaka majirani wakaanza kupata wivu mama ambaye mwanawe chizi anaishi maisha mazuri, wao wenye watoto timamu wa akili wanaishi maisha ya kubangaiza, akhera hawapo na duniani hawapo kwa tashididi ya maisha magumu wanayoishi.

Kachero Manu atinga ndani ya msikiti katika msitu wa Dibungo
Msikiti wa Dibungo maarufu wenyewe wakiuita kwa jina la "Masjidi Dibungo El-Jihaad" ulikuwa umejengwa katikati ya msitu kwa matofali ya kuchoma. Na kuezekwa na bati kuukuu. Ulikuwa una ukubwa wa wastani ukiwa na uwezo wa kuingiza waumini si chini ya 250 kwa pamoja. Ukiwa unatumia taa za mwangaza wa jua "Solar Power", zilizozunguka msikiti mzima.
Ndani ya msikiti kulitandikwa majamvi ya kufumwa na mkono yaliyoenea msikiti wote. Mbele ya msikiti kulikuwa kuna kikopesa ambacho ndio mihirabu anayoitumia Imamu kukaa kipindi anapotaka kuendesha ibada ya swala. Siku hiyo majira ya saa mbili na nusu usiku baada ya swala ya Isha, waumini zaidi ya 200 walikuwa wametulizana tuli wanamsikiliza mmoja wa viongozi wao aliyekuja kuzungumza nao. Haikuwa kawaida yao mida hiyo kuongea, ilikuwa swala ya Isha inapoisha tu, kila mmoja anaupasua msitu kurejea kwenye majumba yao yaliyopo umbali wa kilometa 2 mpaka 3 yaliyojengwa kuzunguka msitu huo. Ilikuwa ni ngumu kwa mtu mgeni kugundua kama kuna msikiti huo katikati ya msitu.
Kachero Manu alikuwa ndio kwanza amewasili msituni majira ya Magharibi na moja kwa moja akiwa na begi kubwa na mgongoni alifikia msikitini hapo akiwa na mwenyeji wake. Kilichomtisha Kachero Manu ambaye alikuwa amevalia mufti, vazi la kanzu nyeupe na kofia ya kufuma kwa mkono ni kitendo cha kuona waumini wote msikitini wamebeba silaha zao zipo pembeni yao, kasoro yeye. Huku wakiwa wanasikiliza viongozi wao kwa utiifu mkubwa bila kutikisika wala kuchezacheza. Kama ndege angeweza kujaribu kutua kwenye kichwa cha mmoja wapo wa hao wanamgambo waliomo msikitini muda huo angeweza kutulizana bila shida yoyote. Kwa muonekano wa juu juu namna alivyowachunguza wote hawakuwa Watanzania pekee, na hili lilijulikana baada ya mzungumzaji kufafanua baadhi ya mambo tata kwa kutumia lugha ya Kiingereza, na kuna wakati kuchomekea maneno ya Kisomali. Pia walionekana ni wanamgambo wenye afya zao wenye miili iliyoshiba na kukubali mazoezi magumu. Pia walionekana wana 'umoja wa huba na hawa' miongoni mwao. Na sio ule umoja wa mashaka wa paka na panya.
Ikaanza kusomwa ripoti ya wiki kupitia kwa mmoja ya wakufunzi wa mgambo hao kwa kutumia kipaza sauti. Ripoti ambayo pia ilimtisha Kachero Manu kiasi fulani kutokana na matukio yaliyokuwa yanatajwa. Ripoti ilieleza wiki iliyopita wamekufa wanamgambo wawili, mmoja kutokana na kudonyolewa na panga tumboni wakati wa mazoezi na mwingine kutokana na kulipukiwa na bomu wakati anajifunza kulitega.
"Kama kwenye mazoezi tu wanauana kikweli je kwenye mechi si kuna hatari hawa watu..!" alikuwa anawaza Kachero Manu huku akiwa amekunja miguu yake kwenye jamvi alilokalia huku ameinika kichwa chake chini kama kobe anayetunga sheria. Mara baada ya kumalizika kusomwa kwa ripoti fupi kuliambatana na tukio la kuja hadharani kwa mmoja wa viongozi wao wakubwa wa kikundi hicho cha "Al-shabaab" kutoka mapango ya Amboni, Tanga. Ambaye muda wote wa kusomwa kwa ripoti alikuwa ametungamana kwenye mihirabu mbele ya msikiti anapokaa Imamu akiwa amejifunika na kilemba. Akakaribishwa na kujitokeza mbele ya wale wanamgambo ambao walianza kuzidi kubanana pamoja na kupandwa na tashiwishi ya kumsikiliza kwa makini.
Hali hii ilithibitisha kuwa kiongozi huyo ni mtu adimu sana haonekani ovyo hadharani. Viongozi wao wakuu kuonekana kwao ni kwa nadra na wakijitokeza hadharani basi kuna tangazo muhimu ameleta, au kuna kiongozi amekuja kuvuliwa mbeleko au kuna adhabu amekuja kuleta kwa watu wakosefu. Kachero Manu alikuwa yupo kwenye safu za katikati akawa anasikia minong'ono toka kwa wale wana mgambo alioketi nao jirani. "Mullah Chambuso leo katutembelea, Allah ni mkarimu sana kutupa bahati ya kutukutanisha na kipenzi chake na mfia dini madhubuti asiyeteteleka inshallahu taala atakuwa amekuja na habari njema" alisema mmoja wapo katika wale wanaonong'ona kwa hisia kubwa za kuonyesha utiifu kwa kiongozi wake.
"Huyu ni wa peponi kabisa anachosubiria ni kifo akastarehe zake na wasichana wa peponi amekwishapigana vita vya jihadi ngumu sana zaidi ya 10 duniani, nchini Somalia, Yemeni, na Afghanistani na kote ameacha alama zake" alinogesha mazungumzo mwenzake kuonyesha nae anamkubali sana 'Mullah Chambuso'. Kisha yakapigwa makofi kuonyesha sasa wakae kimya bwana mkubwa "Mullah" anataka kuanza mazungumzo.
Akawa amesimama akiwa amezungukwa na Makomandoo watatu kwa nyuma yake waliobeba mitutu ya bunduki. Alikuwa amevalia suruali rangi nyeusi ya mtindo wa pajama, huku juu amevalia nusu kanzu na kizibao kizito cha rangi ya kijani, huku chini amevaa buti za jeshi rangi ya maziwa. Uvaaji wa viatu ndani ya msikiti huo nalo ni jambo lililomtatiza Kachero Manu. Tokea utoto wake kule Mahiwa, Lindi alikuwa anaona waislamu wakiingia msikitini wamevua viatu lakini hawa jamaa tena wafia dini wanaingia na viatu mpaka msikitini.
Kwa umbile lake alikuwa ni kibushuti mfupi haswa, pandikizi la mtu akiwa ni mweusi tii kama pipa la lami huku uso wake ukiwa una makovu ya kutosha kuonyesha amepitia mikiriti na mikutuo mbalimbali ya mapigano. Huku macho yake yakiwa na makengeza, macho kumberu. Alikuwa amefuga ndevu lakini zilikuwa zimemkataa hazijanawiri vilivyo, hazina rutuba zikawa kuna sehemu kidevuni zimejikusanya kama mkutano wa inzi. Kichwani alikuwa amejifunga kilemba cha rangi nyeupe kilichokuwa kinang'ara vilivyo. Alikuwa anatisha ukimuangalia mwonekano wake hakuwa na uso wa jamala wala wenye haiba ya mvuto. Uso wake haukuvaa hata chembe la tabasamu, ulimvimba kama mvua ya masika. Alikuwa akiongea anaunguruma kama radi, sauti ya punda. Akaanza hotuba yake fupi iliyojaa amri na vitisho.
 
Sijui itafika mwisho...?
 
Back
Top Bottom