SEHEMU-26
Kwa umbile lake alikuwa ni kibushuti mfupi haswa, pandikizi la mtu akiwa ni mweusi tii kama pipa la lami huku uso wake ukiwa una makovu ya kutosha kuonyesha amepitia mikiriti na mikutuo mbalimbali ya mapigano. Huku macho yake yakiwa na makengeza, macho kumberu. Alikuwa amefuga ndevu lakini zilikuwa zimemkataa hazijanawiri vilivyo, hazina rutuba zikawa kuna sehemu kidevuni zimejikusanya kama mkutano wa inzi. Kichwani alikuwa amejifunga kilemba cha rangi nyeupe kilichokuwa kinang'ara vilivyo. Alikuwa anatisha ukimuangalia mwonekano wake hakuwa na uso wa jamala wala wenye haiba ya mvuto. Uso wake haukuvaa hata chembe la tabasamu, ulimvimba kama mvua ya masika. Alikuwa akiongea anaunguruma kama radi, sauti ya punda. Akaanza hotuba yake fupi iliyojaa amri na vitisho. "Salaam Aleikum Jamiiia, ama baada ya salamu sina mengi, kwanza nimeletewa taarifa tumepata 'Mujaahidu' mmoja amesilimu na moja kwa moja amekuja kwenye viwanja vya jihadi" akavuta pumzi kidogo kabla akaendelea. Zikaanza kulipuka kelele za vishindo vya sauti za maneno ya kiarabu "Takbiiiiiir......Allahu Akbaru, Takbiiiiiir.......Allahu Akbar" wakionyesha wamefurahia kwa huyo mgeni aliyeamua kuachana na maisha ya anasa za kidunia na kuamua kujiunga nao maporini kuja kupigania vita vya jihadi. Hapo alikusudia kuwapa taarifa za ujio wa Kachero Manu pale msikitini kwao.
Kisha baada ya vishindo hivyo akaendelea, "kizuri zaidi nimepata taarifa aliwahi kupitia jeshini lakini akashindwana nao hao madhalimu akaacha kazi miaka kama mitano iliyopita, kwa hiyo msisite kumtumia kwenye baadhi ya mambo" akakoma kuzungumza huku macho ameyakazia alipo Kachero Manu.
"Asalaaam Aleikuuum ndugu zangu katika imani ya haki, mimi ndugu yenu nilikuwa naitwa 'Raphael Kitokambali' lakini baada ya kuiona taa ya Uislamu sasa naitwa Abubakari" akasimama kuendelea kujitambulisha Kachero Manu baada ya vishindo vizito tena vya takbira vilivyokuwa vinakaribia kutaka kuezua paa la msikiti huo wa matofali ya kuchoma. "Nimechagua jina la Aboubakr kwa sababu nimesikia alikuwa rafiki wa karibu sana wa Mtume Muhammad (S.A.W). Na mimi nitafanya bidii mpaka niwe karibu na kiongozi wa harakati hizi za jihadi. Hivyo mimi ni ndugu yenu katika imani, wazazi wangu wamenitenga baada ya kusikia nimeingia kwenye imani hii mpya, ahsanteni sana" akamaliza na kukaa chini, akiongea maneno aliyokaririshwa vilivyo na Kachero Yasmine.
Wakawa wanamfuata na kumkumbatia kwa kumpa pongezi juu ya tukio lake hilo adhimu. Kisha yule mgeni mhashamu akaendelea na hotuba yake."Lakini pia kuna jambo tusha, baya la usaliti limetokea hapa kambini" akapumzika kidogo. Kila mmoja akawa ameshikwa na wasiwasi wanatazamana wenyewe kwa wenyewe. Walijua tayari pepo mchafu anataka kupita wajiandae. Kila mmoja kiroho kikawa kinamdunda kama saa mbovu, maana walijua adhabu ya msaliti ni kifo.
"Mke wa ikhwa mwenzetu mmoja katoroka na amana yetu ya Dola za Kimarekani $10,000 alizopewa afikishe sehemu yapata miezi miwili iliyopita. Kawauza wenzake, wakauliwa kinyama huko bonde la Mzakwe, Dodoma yeye katokomea na pesa zetu. Sasa tumechunguza tumegundua mumewe nae ni mhusika wa njama hiyo. Mleteni hapa haraka sana laanatu-llah ziwe juu yake maluuni mkubwa huyu" alizungumza kwa jazba na raghba kubwa ya kumuadabisha msaliti. Baada ya kutoka hiyo amri ikawa ni mikikimikiki ya kumuingiza ndani ya msikiti kupitia mlango wa katikati ya msikiti aliyehisiwa kuwa ni msaliti huku akiwa amefungwa kamba za miguuni na mikononi, kamba zilizokazwa ndindindi zilizomfanya asiweze kufurukuta.
Kachero Manu alikuwa anashuhudia mubashara tukio hilo, ambalo chanzo chake anakijua nje ndani, mwanzo mwisho. Yeye na Kachero Yasmine ndio waliokoa maisha ya 'Ukhti Rayhaan' ambaye anatuhumiwa kutoroka na Dola $10,000 za magaidi. Walimkuta amezimia na kujeruhiwa vibaya kwenye ajali siku magaidi walipojileta kwenye bonde la Mzakwe, na kuchakazwa vibaya na Kachero Yasmine. Baada ya ambushi hiyo, wenzake waliuawa kinyama na yeye kuponea chupuchupu huku akikutwa na kitita cha Dola za Kimarekani $10,000 kwenye nguo zake za ndani na barua zikiwa njiani kuelekea kwa mama yake "Maso Maso", Bi Mwantumu.
Alipozinduka hospitalini baada ya kukataa katakata kutoa ushirikiano mwishowe alikubali kuuza siri za magaidi waliomtuma, hii ilikuwa ni baada ya kuhakikishiwa usalama wake. Alijieleza yeye akiwa binti anayesomea fani ya Udaktari ngazi ya Chuo Kikuu alishawishiwa kuacha chuo na kwenda kujiunga kwenye kikundi cha ugaidi cha "Al-shabaab" nchini Somalia. Waliporejea Tanzania moja kwa moja wakatua Wilayani Kilindi yeye na mumewe aliyekutana nao huko huko Somalia. Kutokana na kujitolea kwao katika jihadi yeye akachaguliwa kuwa ni mmoja wa wana baraza la shura, wasiri wa ndani wa "Maso Square The Duduman" .
Mpaka akaaminika kufanywa tarishi wake wa kupeleka barua huku na kule. Hivyo mara ya mwisho alitumwa kupeleka pesa na barua kwa mama mzazi wa "Maso Maso", Bi Mwantumu lakini pia alitakiwa kupitia Dodoma kwa Bwana Kareem Abdallah achukue barua ya siri ya kuileta kwa "Maso Maso" yenye kuelezea namna serikali walivyochukua hatua baada ya shambulizi dhidi ya wabunge wake. Ndipo akakutana na sokomoko la kukuta mwenyeji wake Bwana Kareem Abdallah meneja wa Chops Carwash & Garage ametekwa.
Hivyo kwanza akasaidia kumtorosha baba yake mzazi Bwana Kareem Abdallah kumpeleka mafichoni Tanga, kisha akatia nia ya kushiriki ukombozi wa Bwana Kareem ili apewe hiyo barua kisha ndio aelekee Dar es Salaam kwa Bi. Mwantumu. Ndipo yakamkuta yaliyomkuta mpaka akanaswa mikononi mwa Makachero mahiri wanaopambana na magaidi.
'Ukhti Rayhaan' ndio aliyetoa maelekezo kuwa mzigo wa pesa na barua alikuwa anaupeleka kwa 'Shekhe Jamsheed' wa Sinza ambaye yeye ndio angeufikisha siku ya dua Alhamisi ya mwishoni mwa mwezi. Ndio ukachezwa mchezo wa pata potea wa Kachero Manu akajifanye amesilimu katika msikiti unaoongozwa na Shekhe Jamsheed.
Kisha baada ya hapo ajenge nae Shekhe Jamsheed mazoea mpaka amuingize kwenye harakati za "Al-shabaab" huko Kilindi, Tanga. Pata potea ikajibu vizuri, Shekhe Jamsheed ndani ya mwezi mmoja tu akamshiba Kachero Manu na kumfanya mwandani wake mpaka kuanza kumtapikia sumu za "Al-shabaab" kuwa ni kundi lililo katika haki, ila vyombo vya habari vya nchi za kimagharibi ndio vinawachafua kwa kusambaza propaganda chafu dhidi yao. Kachero Manu akaanza kuigiza anapendezwa sana na zile shemere za hadithi za Al-shabaab. Ndipo Shekhe Jamsheed akampa mchongo wa Kilindi Kachero Manu bila kujua anampeleka adui mwenye nia ya kuisambaratisha "Al-shabaab" itoweke Afrika Mashariki, watu waanze kuishi kwa amani na usalama kama zamani.
Mikono yake Kachero Manu ilikuwa inamsisimuka akawa anatamani anyanyuke aende akalianzishe tifu, awadunde kumuokoa mumewe 'Ukhty Rayhaan' lakini nafsi yake ikamuambia vuta subira, daima mwisho mwema ulio mzuri huwafikia wenye subira.
Kwa mkululu huu wa watu zaidi ya 200 ndani ya msikiti tena wakiwa na silaha za kivita hata uwe Komandoo wa dunia ukianzisha ugomvi utegemee tu kunyakuliwa kama mwewe anavyomnyakua kifaranga cha kuku.
Yule anayetuhumiwa kuwa msaliti akatupwa miguuni mwa 'Mullah', akawa anamuangalia 'Mullah' kwa macho ya huruma huku machozi ya huzuni yanamtiririka akitaraji shufaa yake huku jasho jekejeke limetotesha kanzu yake.
Ilikuwa ni siku yake ya mashaka fundo katika siku yake ya mwisho maishani. 'Mullah' akawa anamsinzilia kwa macho yake makali yule msaliti. 'Mullah' alikuwa akipitisha maamuzi ndio yamepita hivyo, alikuwa na tabia ya kisonoko mtamba na ukoko, haambiliki kamwe. Akaletewa jambia kubwa lile la kuchinjia ngamia aliyefutwa kodi huko Arabuni.
Akaanza kulizungushazungusha hewani kwa madaha na mbwembwe, halafu anatishia kama ndio anaanza kuchinjia, umati wote macho yanawatoka juu juu kwa hofu. Alivyolizungusha mara ya tatu na kulitua chini jambia halikurudi bure likatua kwa kasi shingoni na kutenganisha kichwa na kiwiliwili vipande viwili kwa kuikata mishipa ya damu na neva ya shingoni. Damu zilikuwa zinachuruzika kwa kasi mithili ya bomba chakavu la "DAWASA" lililopasuka mtaani.
Wakajitokeza watu wamevaa makoti meupe kama madaktari wakiwa na machela yao wakaibeba maiti na kuondoka nayo kwenda kuizika kusikojulikana. Biashara siku hiyo ikawa imeishia hapo mmoja, kila akatawanyikia upande wake kichwa chini, huku wengine wanashtakia njia kama kuku mwenye mdondo huku Kachero Manu akipewa rafiki atakayekuwa anaishi nae chumba kimoja hapo kambini.
[emoji3586][emoji3586][emoji3586][emoji3586][emoji3586][emoji3586][emoji3586][emoji3586][emoji3586][emoji3586][emoji3586][emoji737]