Riwaya: Msako wa mwehu

Shupavu

JF-Expert Member
Apr 23, 2015
371
525
RIWAYA: MSAKO WA MWEHU
MTUNZI: Badi .M. Bao
MWASILIANO. 0625920847, ( whatsap )
E- mail: badi.bao11@gmail.com
Dar es Salaam

SEHEMU YA KWANZA

SURA YA KWANZA

Idara ya magonjwa ya akili, Hospitali ya Taifa Muhimbili
Gangaganga ya mganga humwacha mgonjwa na matumaini, jitihada ya kutatua tatizo humpa mwenye tatizo tumaini. Bi Mwantumu Haji alikuwa amepatwa na maswahibu ya ulimwengu. Tatizo lililompata alijiona kama kaibeba dunia nzima mgongoni mwake. Ilikuwa ni majira ya saa tatu za asubuhi tulivu, iliyopambwa na mwangaza usioumiza wa jua ambalo lilikuwa tayari limeshachomoza upande wake wa mashariki, Bibi huyo alikuwa amekaa kwenye kiti na baadhi ya watu wengine akisubiria kuingia kwenye chumba cha daktari kilichopo kwenye bloku la hospitali ya Muhimbili, idara ya magonjwa ya akili.

Uso wake tu ukimuangalia ulionyesha ana jambo limemsibu, kwani daima dumu barua ya moyo husomwa juu ya panda la uso la mtu. Mtu akiwa na hali ya furaha au huzuni yote husomeka kwenye uso wake. Alikuwa amewasili katika hospitali ya taifa ya Muhimbili tokea muda wa jogoo la kwanza kuwika akimleta mtoto wake wa kiume anayeitwa "Masoud Masoud" maarufu kwa jina la Maso Maso” aliyerukwa na akili usiku huo wa manane uliopita.

Naam "Maso Maso" sasa kawa kichaa, mwehu, mwendawazimu, majinuni, akili zake zimetadathali, vyovyote utakavyopenda kutamka, lakini "Maso Maso" sasa akili zake ni maji kupwa na maji kujaa. Mgonjwa huyo alilazwa katika wodi ya wagonjwa wa afya ya akili katika Hospitali Taifa ya Muhimbili.

Mara ikasikika sauti toka kwenye kipaza sauti cha mhudumu wa zamu, mgonjwa mwenye kadi namba 10 aelekee kwa daktari chumba namba 02. Lilikuwa ni tangazo lililoleta faraja kwenye moyo wa Bi Mwantumu hasa ukichukulia yupo hapo hospitalini kwa zaidi ya saa sita tokea saa tisa za usiku na sasa saa tatu na dakika saba za asubuhi ndio anapata nafasi ya dhahabu aliyokuwa anaisubiria kwa hamu ya kuonana na daktari.

Bila simile, Bi. Mwantumu na uzee wake wa miaka 65 akajinyanyua kwa tabu pale kitini pake alipokuwa amejipweteka na kuingia kwenye chumba cha daktari bingwa wa Afya na Magonjwa ya Akili wa Hospitali ya Taifa Muhimbili. Alipokelewa kwa uso wa bashasha na tabasamu toka kwa Dokta "Alshad Mpenumbe". Alikuwa ni daktari wa hospitali hiyo mwenye uzoefu wa zaidi ya miaka 20 sasa, na umri wake alikuwa ndio anaingia kwenye rika la uzee wa makamo, wa miaka 55.

Karibu sana mama yangu, na pole na matatizo yalikuwa ni makaribisho ya Dokta Mpenumbe kwa Bi Mwantumu. Ahsante mwanangu nimeshapoa, matatizo tumeumbiwa wanadamu hatuna budi kuyapokea na kuyakabili kwa subira na stahamala kubwa alijibu kwa unyenyekevu Bi Mwantumu huku akijiweka vizuri kitini. Samahani naomba hiyo kadi yako alisema Dokta Mpenumbe. Bi Mwantumu akajibu kwa vitendo kwa kunyoosha mkono wake wa kulia kuikabidhi kadi kwa daktari apate kuisoma.

Ukapita muda kama wa rakaateni, muda ambao Dokta Mpenumbe alikuwa ametingwa na kuandika andika kwenye kompyuta yake ya mezani kisha, akamaliza akavua miwani yake akaiweka pembezoni mwa kompyuta yake, akaitoa hanchifu yake nyeupe kutoka kwenye koti lake jeupe alilovaa, akajifuta kwenye macho akajikohoza kidogo kulisafisha koo lake na kuanza mazungumzo na Bi Mwantumu.

Daktari: “Eheemwanao Masoud hili tatizo lake la akili limemuanza lini"?. Lilikuwa ni swali lililovunja ukimya uliopita baina yao kwa dakika kadhaa.

Bi Mwantumu: "Jana kuanzia saa mbili usiku alikuwa anazungumza mambo mchafukoge mara anasema kuna watu wapo nje ya nyumba wamekuja kumchukua. Wakati mwingine anasema amepigiwa simu na Rais kuwa ameteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa. Ila ilipofika saa sita usiku, ndio akaanza kufanya fujo na kuvunja vitu vya ndani anataka tumruhusu atoke nje ya nyumba."

Daktari: "Kwenye ukoo wenu au familia yenu ameshawahi kutokea mgonjwa wa afya ya akili"? Bi Mwantumu: "Billahi wa Rasuli hakuna mtu huyo kwenye ukoo wetu, sio upande wangu wala upande wa marehemu mume wangu." alitoa kiapo kwa kutumia kidole chake cha shahada kukwangua juu ya koo lake kuweka msisitizo wa maneno yake.

Daktari: "Mwanao, ni Mwanachuo au Muajiriwa?"
Bi Mwantumu: "Mwanangu amemaliza Chuo mwaka juzi, Shahada ya Uhandisi huko nchini Uingereza, na mwaka huo huo akapata kismati cha kazi nchini Saudi-Arabia, lakini akaacha ghafla kazi, sasa ana miezi kama 6 yupo tu nyumbani, na wala hajatuambia kilichomsibu huko alipokuwa mpaka akaacha kazi."

Daktari: "Je mwanao, ni mtu wa kujichanganya na marafiki na je ameoa au kuwa na rafiki wa kike?"
Bi Mwantumu: "Zamani kabla hajasafiri kwenda masomoni Uingereza alikuwa mtu wa watu, mpenda marafiki. Nyumbani kwangu walikuwa hawakauki marafiki zake kama maji ya kisima, lakini tokea arejee masomoni akawa ni mtu wa kujitenga tu, hana marafiki na hata sijawahi kusikia wala kumuona yupo na rafiki wa kike tokea amebaleghe. Na nimemzaa akiwa ni mzima wa afya jogoo linapanda mtungi"

Daktari: (Akatabasamu kwa jibu la Bi Mwantumu akifurahishwa na msisitizo aliouonyesha kuthibitisha mtoto wake sio hanithi). "Sasa mama yangu, vipimo vya maabara vimerudi, mtoto wako hana malaria wala ugonjwa wowote ule. Maana mwanzoni nilihisi huenda malaria yamepanda kichwani, lakini hana malaria. Kutokana na maelezo yako, mtoto wako ana ugonjwa wa akili kitaalamu tunauita Schizophrenia. Huu ni miongoni mwa magonjwa makubwa ya akili. Jina hilo limetoholewa kutoka katika lugha ya Kilatini ambayo ni maneno mawili "Schizo" na "Phrenia". Mgonjwa anayeugua ugonjwa huo anakosa muunganiko kati yake na akili yake", akaweka kituo kidogo cha maelezo yake Dokta Mpenumbe kwa kumeza mate kisha akaendelea kuelezea.

"Kwa kawaida binadamu huwa na hisia tano muhimu, ambazo ni za kuona, kugusa, kuonja, kusikia na kunusa. Mtu aliyechanganyikiwa kutokana na ugonjwa huu anaweza kuona, kuhisi, kunusa, kugusa au kusikia vitu ambavyo wengine hawaoni, kuhisi wala kusikia. Mgonjwa anaweza kusema anaona simba anapita eneo ambalo mmekaa naye, lakini nyie msimuone au anasikia sauti na watu wanazungumza habari zake, wanamshurutisha au wanamtisha lakini nyie hamuoni wala hamsikii chochote". Machozi yalikuwa yanamchuruzika churururu bila kikomo Bi Mwantumu pindi alipokuwa anasikiliza maelezo ya daktari kwa umakini mkubwa.

Bi Mwantumu: "Sasa kitinda mimba wangu kweli atapona daktari"? Nieleze ukweli usinifiche kitu kabisa" alikatisha mazungumzo ya daktari kwa kuuliza swali kisha akaanza kutoa kilio cha sauti ya uchungu.
Daktari: "Mama, huwa tunatumia njia tatu kuwatibu wagonjwa wa akili ambazo ni za kibaiolojia, kisaikolojia na kijamii. Hivyo shaka ondoa mama yangu"

Bi Mwantumu: "Nashukuru sana Daktari, Mwenyezi Mungu akubariki na kukupa afya uendelee kutupa huduma wahitaji".
Daktari: "Sawa, mama yangu, tutajuzana kinachoendelea. Tutamlaza kwa siku kadhaa ili tuzidi kuangalia maendeleo yake".

Bi Mwatumu akanyanyuka na kutoka nje ya ofisi ya Daktari. Akaelekea kwa keshia kwenda kufuatilia bili yake ya matibabu ya mwana wake ili apate kufanya malipo.


"Mimi ndio "Maso Maso" msela toka Sinza kwa wajanja. Nyie Watanzania maboya tu, unakuta Mbunge anakuhonga buku tano umpigie kura, halafu unamchagua kwa miaka mitano, maana yake kila mwaka mmoja amekununua kwa buku". Ha..... Ha.....Ha.....Ha.......mazwazwa sana nyie watu tembeeni duniani mfunguke akili. Kutwa mnashindia "chips-dume" na maji, maziwa kwa watoto wenu hawanywi mpaka wanywe sumu, tokea wakiwa shule ya vidudu akili za kugundua ndege na magari kama wazungu mtapata wapi sasa, wakati watoto wa wenzenu Ulaya wanashiba baga kwa maziwa. Viongozi wenu nao ni janga la kitaifa, watoto wao wanawasomesha shule za kuzungumza "Yes... Yes.. Mzungu kala mafenesi" mpaka anamaliza chuo kikuu huko Ulaya mtoto kagharimu milioni mia tatu.

Afu anarudi 'Bongoland' kugombania ajira na watoto wa akina yahe waliosoma shule za kata. Ambao gharama zao mpaka chuo kikuu haifiki hata milioni moja. Hizo akili au matope!. Ukiwekeza kwa mtoto wako milioni mia tatu, basi muandalie mazingira ya kuja kuendeleza kampuni zako za mabilioni na sio kuja kuajiriwa kwa kamshahara cha laki nne na watoto wa walalahoi". Ha.... ha.... ha... ha.... sogeeni hapa mpate elimu kitaa bure, mupate rai tumbitumbi zenye mafundisho.

Wakulima wenu nao majanga tupu, shamba lake, mbegu za kwake, kupanda, palizi zote kwa gharama zake lakini akivuna mazao yake, serikali inaanza kumpangia sijui Ooh...usiuze nje ya nchi, huo ni unyonyaji mbona Wafanyabiashara hamuwazuii kuuza bidhaa zao nje ya nchi, mbona watumishi wa umma hamuwapangii matumizi ya ndururu zao za mwezi!.

Ningekuwa Rais wa nchi wagonjwa nyie mngekula bata tu, sio viporo mnavyoletewa na ndugu zenu. Dripu zingekuwa za juisi na sio za maji kwani nyie mmekuwa samaki... Ha...Ha..Ha....Ha....! "

Wakati Masoud anaendelea kubwabwaja mbovu, akasikika nesi mmoja anamuongelesha mwenzake, "Huyo ndio Masoud bana akianza kumwaga sera hapo ni usiku kucha mtakesha nae na kuna wakati anaongea vitu vya msingi hata sisi wenye akili timamu hatuwezi kuviwaza".

"Afu nasikia kasomea Uingereza ana Shahada ya Uhandisi, labda karogwa maana familia zetu za kiswahili nazo ni shida, wana roho ya tukose wote. Wanapenda wote tufanane hali zetu za maisha, wote tuwe wali deni mchuzi karadha. Babu dobi, Baba muuza kahawa, Mjomba fundi seremala, Shangazi kazi yake mchambaji kwenye "kitchen party", Mama mchoma vitumbua, hivyo ndivyo wanavyotaka. Akitokea mmoja tu anataka kujifanya msomi msomi wataanza kumpiga tunguri mpaka atakoma", nesi mwenzake nae alichangia kusherehesha mazungumzo yao.

"Madame Neesi eeh....Madame Neeesi....!, Nataka kwenda chooni kujisaidia, au nijisaidie hapa hapa wodini, mie sioni noma fumbeni macho tu nimtoe nyoka pangoni hadharani" ilikuwa ni sauti ya Masoud, alikatiza mazungumzo yao waliyokuwa wanateta wale manesi mawili.

"Aaaah.... hapana rafiki yangu Masoud usifanye hivyo, nenda chooni bana, tena leo simuiti mlinzi akusindikize nenda mwenyewe na urudi haraka rafiki" alisema nesi yule akimrai Masoud asijisaidie ndani ya wodi hiyo ya wagonjwa akili. Masoud alikuwa tayari ameanza kufungua mkanda wa suruali yake akitishia kujisaidia tayari.

Masoud akaondoka zake wodini kuelekea chooni kwa mwendo wa chapuchapu. Muda ulikuwa ni saa nne za usiku. Hiyo ndio ikawa ni kwaheri ya kuonana, kama vile kawapa mkono wa buriani, hawakumuona tena. Kwa ufupi Masoud alikuwa ametorokea mtaani kusikojulikana, alichoka maisha ya kufungiwa wodini kama ndege tunduni.



ITAENDELEA
 
RIWAYA: MSAKO WA MWEHU
MTUNZI: Badi .M. Bao
MWASILIANO. 0625920847, ( whatsap )
E- mail: badi.bao11@gmail.com
Dar es Salaam

SEHEMU YA PILI


Masoud Masoud au "Maso Maso Mwehu" kama alivyojipachika mwenyewe, aliacha mambo wodini hamkani si shwari kwa kutoroka kwake. Alipoingia chooni alijifungia mlango kwa ndani na kupapachua dirisha dogo la kioo lililopo chooni kisha akavunja nondo zake.
Nesi wa zamu alisubiria arudi, akawa anaona amechelewa. "Huyu amezidiwa ugonjwa huko chooni au amejiua?" ni swali alilokuwa anajiuliza nesi huyo aliyetoa ruksa kwa hofu.
Ndipo alipotoa taarifa kwa walinzi wakaja kuvunja mlango wa chooni ndipo walipokuta kidirisha kimechomolewa. Kila mtu alishangaa na kustaajabishwa na namna alivyopenya dirishani baada ya kufanikiwa kukata vyuma vya dirishani.
"Huyu atakuwa na nguvu za ajabu sana mithili ya Samson wa kwenye Biblia, haiwezekani kwa kutumia mikono na vidole uweze kupindisha vyuma vya dirisha na kufanikiwa kutoroka" aliropoka mlinzi mmoja wapo akiwa ameshikwa na butwaa haamini kama binadamu wa kawaida anaweza kupachua dirisha lile madhubuti kwa kutumia mikono tu bila kifaa chochote.
Daktari wake anayemtibu alivyopita kuzungukia wagonjwa wake asubuhi na mapema ndio akakuta kaachiwa manyoya tu kitandani kwa Masoud. "Utaratibu upo wazi kabisa kuwa lazima asindikizwe popote anapokwenda, sasa ulishindwa nini kumpa taarifa mlinzi amsindikize chooni?" Dokta Mpenumbe alikuwa anaongea kwa hamaki huku anafoka.
Yule nesi wa watu masikini ya Mungu akawa hana cha kujitetea wala pakushikilia, amejiinamia kama zoba ulikuwa ni uzembe wake kazini.
"Sasa naomba uniandikie barua ya maelezo ya utetezi kwanini nisikufikishe kwenye vikao vya nidhamu uchukuliwe hatua haraka sana, kukomesha tabia hii mbaya iliyomea ya uzembe kazini" Daktari alitoa maagizo kwa nesi yule wa zamu, ambaye alionekana amegwaya na anajuta kwa uzembe wake lakini majuto daima ni mjukuu na maji yakishamwagika hayazoleki tena. Nesi yule alitamani muda urudi nyuma aweze kurekebisha kosa lake alilolifanya lakini alikuwa ameshachelewa, "Maso Maso" mwehu kashatimka zake mtaani.
Bi Mwantumu alijihimu alfajiri na mapema jogoo la pili akiwa ameambatana bega kwa bega na shoga yake Bi Mwazani wakiwa na kapu lao kubwa ndani yake kuna chupa yao kubwa ya chai ya maziwa na mapochopocho, michapalo kedekede kwa ajili ya mgonjwa. Wakiwa hawajui yaliyompata mtoto wao hospitalini usiku wa kuamkia leo yao. Walipofika nao wakakutana na taarifa za kutoweka kwa mtoto wao Masoud.
Bi Mwantumu alikuwa hashikiki kwa kilio cha kwikwi, "mwanangu eeeeeh.......Masooo mwanangu unateseka babaaaa...upo wapi babaaa eeeeeeh...unakula nini huko ulipo.... umelala wapi sasa mwanangu,..... nguo za kuvaa utapata wapi woooohi woooooohi.... uchungu mama tumbo la uzazi uchungu mamaaaaaa... Wooooh" kilio mtindo mmoja kama vile yupo msibani.
"Shoga nilikuambia hukunisikiza ukayataka matibabu ya kizungu, huyu katupiwa jini tu, tungewahi kwa mtaalamu sasa angekuwa mzima wa afya. Jisaidie Mungu akusaidie, mambo yenu ya kudharau mila zilizotulea ndio matokeo yake haya. Kiatu cha mtoto hakimponyi mama mbigili. Njia unazotumia kumponya mtoto wako haziendani na uhalisia shoga yangu, ulikuwa ni ushauri wa Bi Mwazani kwa shoga yake, huku akiongea kwa hisia kali na uchungu mkubwa.
"Shoga nimekuelewa sasa ama zao au ama zangu, wabaya wangu wamenibipu sasa mimi nina wapigia simu wakae mkao wa mapambano", tusiombane poo tu" Bi Mwantumu alijibu, majibu ya kukubaliana na ushauri wa shoga yake wa kufa na kuzikana, tokea utotoni na unyago wamechezwa na kungwi mmoja, huko kijijini kwao Utete, Rufiji.
Bi Mwantumu na rafiki yake waliondoka zao kurejea nyumbani kwao, baada ya kupewa taarifa na daktari kuwa juhudi zote za kumsaka mwehu "Maso Maso" kila kona zimegonga mwamba. "Mama tunasikitika kukutaarifu kuwa tumeshindwa kumpata, unaweza kwenda polisi upate msaada wa kumsaka mwanao Masoud" yalikuwa ni maneno yake kuaga ya Dokta Mpenumbe kwa Bi. Mwantumu.

Shekhe Abeid Mbonde alikuwa maarufu Rufiji nzima na vitongoji vyake kutokana na kazi ya upigaji ramli. Alikuwa anaishi kijiji cha Mkongo kilichopo kama makadirio ya umbali wa kilometa 4 kutoka mto Rufiji. Zamani kijiji hicho ndio ulikuwa Mji mkubwa wa Wilaya ya Rufiji. Kijiji hiki umaarufu wake unatokana na kuwa ndipo yalipo Makao Makuu ya Mamlaka ya Maendeleo ya Bonde la Mto Rufiji "Rufiji Basin Development Authority" (RUBADA).
Shekhe Mbonde kazi yake ya kupiga ramli au kusaga mkungu hiyo ndio kazi ambayo ilimpatia umaarufu mkubwa mpaka watu walifunga safari toka pande mbalimbali za dunia kuja kupata huduma yake. Umri wake sasa alikuwa ni shaibu wa miaka 80 na ushee. Alikuwa anaogopwa haswa ikisemekana anafuga Majini anaowatumia kwenye kazi zake za uganga.
Bi Mwantumu na shoga yake Bi Mwazani asubuhi ya saa nne iliwakuta wamekaa kwenye jamvi wakisubiria huduma ya Shekhe Mbonde. Walirauka alfajiri na mapema na basi linaloelekea Rufiji wakipandia Mbagala kuu. Bi Mwazani alijifunga kibwebwe kuhakikisha mtoto wa rafiki yake anayesakwa kwa hali na mali anarudi katika uzima wa afya yake ya akili.
Hawakupata tabu sana kufika nyumbani kwa Shekhe kwa sababu nao pia kwa asili ni Wandengereko walikuwa wanasikia sifa za Shekhe Mbonde tokea wakiwa wanawali wabichi kabisa. Walipofika walikuta kadamnasi ya watu wamejazana kwenye msambweni wa nyumba ya mtaalamu huyo.
"Shosti hapa kwa Shekhe Mbonde ndio Kigoma mwisho wa reli, kuwa na matumaini mwanetu Masoud amepatikana na amepona tayari ondoa mashaka atafanyiwa ruzuna atakuwa mzima wa afya" Bi Mwazani alivunja ukimya kwa kuanzisha mazungumzo kwa shoga yake. "Nashukuru sana shoga ama kweli akufaaye kwa dhiki ndio rafiki wa kweli, wengi wa marafiki ni mafarisayo ila wanajifanya wema machoni pa watu" alitoa shukrani za dhati Bi Mwantumu kwa shoga yake huku akiwapiga kijembe marafiki zake wengine
"Kikulacho kinguoni mwako, wapo majirani zetu hata kukujulia hali kwa matatizo haya uliyopata hawajaja, pengine ni wahusika wanaona haya kukuangalia usoni" Bi Mwazani alizidi kuchochea kuni za fitina kwa majirani wenzake ili yeye aonekane peke yake ndio mwema.
"Leo ndio fainali, hapa mganga akipiga bao akanionyesha fulani ndio mbaya wangu, sitosikia la mwadhini wala la mteka maji msikitini, tutagawana majengo ya serikali nakwambia mimi naenda Segerea yeye anaenda mochwari Muhimbili." alipandisha mzuka wa hasira Bi Mwantumu.
"Haya haya aliyebakia bado kutanguliza kishauzu cha Shekhe afanye haraka kabla hajafungua kazi" ilisikika sauti ya msaidizi wa mganga. Msaidizi huyo alikuwa anapigia debe advansi anayolipwa mganga kama sadaka, unatoa yoyote ile unayoguswa nayo.
Bi Mwantumu akatumbukiza elfu hamsini taslimu kwenye kapu la mganga lilipopitishwa usoni pake. Akabaki anasubiria kwa hamu zamu yake ifike aingie kwenye kilinge cha mganga akatapike yanayomsibu.

"Woooooh...wooooooh........woooooh....paachiiithhhh... chi...chi.... chi..... paraka parakata paaaah... pepo mchafu mama mwanao ametupiwa, amepatwa na shonga, amekuwa kichaa kweli si kweli? " aliulizwa Bi Mwantumu akiwa amekaa juu ya kinu cha Shekhe Mbonde aliyekuwa amekaa kwenye jamvi akizungumza maneno ya kurogonya baada ya kupandisha ruhani wake kichwani.
"Tawile mganga tawile" alijibu Bi Mwantumu huku anahema juu juu kwa huku fundo la hasira limejikusanya kooni kwake kwa wabaya wake. "Kapotelea mtaani hajulikani alipo sawa sawa mama?" aliendelea kuuliza ramli yake Shekhe Mbonde. "Tawile Shekhe tawile nimewakosea nini hawa walimwengu mimi jamani, unalala nao, unakula nao lakini kumbe ni wabaya wako" akawa analalamika Bi Mwantumu kwa sauti ya juu huku anamwaga mchozi wa nguvu.
"Usilie mama, hapa ndio mwisho wa matatizo umefika, wabaya wako mwisho wao umefika, ukisikia mwana wa Mbonde fimbo ya chuma kwa wachawi ndio mimi, viongozi wengi wa serikali mimi ndio kamati yao ya ufundi, ndio nawapangia nini cha kuvaa na siku gani, ndio nawapangia hotuba za kuzungumza mbele ya kadamnasi ya watu ha.... ha... ha... ha...." aliongea kwa sauti ya kujigamba huku anachezea tasbihi mkononi mwake. Shekhe Abeid Mbonde alikuwa tayari ameshamuingiza kwenye kumi na nane zake Bi Mwantumu hachomoki tena.
"Sasa chukua kipande cha kanga hiki, na hii sarafu ya Mjerumani uishike mkononi. Uende msalani kuoga, ukishaoga tu usijifute maji uivae mara moja hiyo kanga kisha uikumbate hiyo sarafu uanze kunuiza unayotaka kwa wabaya wako na kwa mema unayotaka kwa mtoto wako". Bi Mwantumu akawa ananyanyuka kwenye kinu na kuelekea bafuni, huku Shekhe Mbonde jicho limemsimama dede kukodolea mirindimo ya makalio ya Bi Mwantumu yanavyotikisika alikuwa amevalia vazi teketeke la dela.
Waswahili wanasema huba mwanzowe jicho, Shekhe moyo ulikuwa unamwenda mbio kama ametumia Mkuyati wa kuongeza nguvu za kiume au amekunywa kikombe cha Alkasusu.
"Afanalek! Mwenyezi Mungu ni fundi wa kuumba mashallah.....fatabaaraka llahu ahsanul-khaaliqiina" alijikuta Shekhe Mbonde anaropoka bila kujijua kusifia uumbaji kwa kutumia maneno ya kiarabu. Tayari alishachanganywa na umbo sotojo sotojo, laini laini la Bi Mwantumu ambaye licha ya umri wake kumtupa mkono wa miaka 65 lakini bado alikuwa ana mvuto.
Kwanini asiwe na mvuto wakati hajawahi kufanya kazi ngumu maishani mwake zaidi ya kuwa ndani kukatakata vitunguu na nyanya za kumpikia biriani na pilau marehemu mumewe ambaye alikuwa ni Mfanyabiashara mwenye pesa sufufu Jijini Dar es Salaam. Baada ya dakika kama 10 kupita, Bi Mwantumu akawa anarejea kutoka msalani huku akiwa amejifunga upande wa kanga kuu kuu iliyo nyepesi.
Ilikuwa imemgandia mwilini kanga hiyo vilivyo ikilichora umbo lake nene, akitembea huku nyonga zake zikijionyesha namna zilivyoumuka kama mikate iliyosusiwa hamira na mpishi.
Mganga Shekhe Mbonde udhaifu wake mkubwa ulikuwa wanawake vibonge, tipwatipwa, wenye miili laini. Wakeze wote kwenye ndoa yake ya mitara aliowafanyia nikaha ukiwaangalia nyuma wamejazia msondo wa nguvu. Hajawahi kuoa tokea ujanani mwake mpaka uzeeni, mwanamke kimbaumbau mwiko wa pilau.
Na wote aliwapata kupitia kazi yake ya uaguzi, "kuku hula sawa na mdomo wake", hivyo wateja wake wanawake ndio walikuwa mboga yake rahisi kuwinda. Tayari Bi Mwantumu alishajiingiza kwenye rada za Shekhe Mbonde ilikuwa ngumu kwake kuchomoka.
ITAENDELEA
 
RIWAYA: MSAKO WA MWEHU
MTUNZI: Badi .M. Bao
MWASILIANO. 0625920847, ( whatsap )
E- mail: badi.bao11@gmail.com
Dar es Salaam

SEHEMU YA TATU

Mganga Shekhe Mbonde udhaifu wake mkubwa ulikuwa wanawake vibonge, tipwatipwa, wenye miili laini. Wakeze wote kwenye ndoa yake ya mitara aliowafanyia nikaha ukiwaangalia nyuma wamejazia msondo wa nguvu. Hajawahi kuoa tokea ujanani mwake mpaka uzeeni, mwanamke kimbaumbau mwiko wa pilau.
Na wote aliwapata kupitia kazi yake ya uaguzi, "kuku hula sawa na mdomo wake", hivyo wateja wake wanawake ndio walikuwa mboga yake rahisi kuwinda. Tayari Bi Mwantumu alishajiingiza kwenye rada za Shekhe Mbonde ilikuwa ngumu kwake kuchomoka.
"Sasa Bibie....njoo hapa karibu yangu, magoti yako yanatakiwa yaje yagusane na magoti yangu kisomo kiingie vizuri". Ilikuwa ni sauti ya kubembeleza ya mganga Shekhe Mbonde iliyobeba ulevi wa ngono uliotamalaki katika mishipa yake ya damu. Bi Mwantumu akawa anajongea huku anaogopa ogopa anatafuna kidole chake, huku macho yake anaangalia chini kama mwanamwali anayeletwa kutambulishwa kwa wakweze. Aibu ilimvaa hasa ukichukulia chumbani walikuwa wawili tu, na mlango umefungwa.
"Bibi acha uoga, utawakasirisha walimu wangu kichwani, hapa tupo kazini usiwaze mambo mengine, mimi umri wangu sasa miaka zaidi ya 80, mimi ni kisu kidugi hakina makali tena hakikati sina matamanio" aliongea kwa ukali Shekhe Mbonde kumtisha Bi Mwatumu. Bibi wa watu alinywea akawa mdogo hasa baada ya kusikia walimu wake mganga watakasirika, akajua majini hawana masihara watamteketeza, akajikalisha pwetepwete jirani na Shekhe Mbonde huku magoti yake yamegusana na magoti yake, mapaja yote nje.
"Sasa mahabubu tutaanza kuelewana maana ulishaanza kunikasirisha kwa kutonipa ushirikiano, walimu wameagiza ulete ngozi ya goromwe jike ukamkamate kwa mikono yako mwenyewe, ili tutengenezee hirizi utakayovaa kiunoni, na hirizi nyingine utaenda kuchimbia kwenye kizingiti cha mlango. Ukishachimbia saa nane za usiku utasimama kwenye kizingiti cha mlango na kuita jina la mwanao mara saba, atarudi baada ya muda mfupi" alitoa maelezo Shekhe Mbonde huku macho yake yamemtoka kama mjusi aliyebanwa na mlango kuchungulia matiti makubwa ya Bi Mwantumu yaliyojaza kifua mpaka yanataka kupasua sidiria yake ya mchina kutokana na kuelemewa na uzito. Bi Mwantumu alipigwa na taharuki mbili, kwanza kuitwa jina mahabubu, jina ambalo ni la kimahaba na pili ni ngozi ya goromwe huyo ndio mdudu gani!. Ikabidi aulize huyo goromwe ndio mdudu gani na atampata wapi.
"Ha... ha... ha....manti hofu manti hofu kidosho ondoa shaka, kula uliwe bibie, toa msaada usaidiwe, raha ya nyege kunyegezana. Huyo goromwe ni aina ya mjusi anayeishi mtini. Ila ukishindwa kumpata utasaidiwa na mwalimu, nawe utamsaidia anachokitaka" alitoa maelezo Shekhe Mbonde huku akionyesha kabisa lafudhi zake kuna ajenda ya siri ameikusudia kwa Bi Mwamtumu. Bibi wa watu masharti yalikuwa mlima mkubwa kwake kuupanda, kwanza huyo mende tu alikuwa anamuogopa kumuua sasa sembuse akamkamate mjusi tena juu ya mti na uzee wake, ni kutafuta kupanyuka msamba na kukiita kifo kwa makusudi.
Akaomba asaidiwe kupata hiyo malighafi adimu kwa ajili ya kushonewa hirizi itakayomrudisha mtoto wake kipenzi wa pekee mwanaume. Mganga akajitia amepandisha ruhani tena, kisha akatoa maelekezo hiyo ngozi ya goromwe wataipata makaburini saa saba za usiku watamletea. Hivyo ikabidi mipango ya kurejea Jijini Dar es Salaam siku hiyo ndio imekufa tena, inabidi alale hapo hapo kijiji cha Mkongo kusubiria kuletewa ngozi ya mjusi saa saba za usiku huko makaburini.

Ilipofika saa sita kamili juu ya alama, Bi Mwantumu aliamshwa na mpambe wa Shekhe Mbonde na kumpeleka makaburini kama alivyoelekezwa na Shekhe. "Sasa Bibi yangu, hapa masharti utatakiwa uende mpaka kwenye mbuyu ule pale, usaule nguo zote bila kubaki na chochote mwilini mwako, kisha unarudi kinyumenyume mpaka ufike kwenye kaburi lile pale la mtoto mdogo aliyezikwa jana, hapo sasa ukae kitako juu yake, ili mwanao nae afufuke upya. Utatakiwa ujifunike hili shuka jeupe ninalokukabidhi. Ufumbe macho usifungue kabisa baada ya nusu saa utasikia kivumo cha upepo hapo ndio ujue jini linalokuletea ngozi ya goromwe anakuja hivyo chochote atakachokufanyia kwako inatakiwa kuwa hewala tu, usimbishie, alitoa maelekezo na vitisho yule mpambe, huku Bi Mwantumu akitetemeka kwa uoga.
Moyo wake uligawanyika pande mbili, moja ya majuto, anajilaumu kwanini alikubali ushauri wa Bi Mwazani wa kuja kwa mganga. Hakutegemea kukuta masharti magumu namna hiyo yanayoendana kinyume na imani yake ya dini. Lakini upande wa pili wa moyo wake ukawa unamwambia nafasi pekee ya kumuokoa mtoto wake kipenzi "Maso Maso" na kujiokoa yeye mwenyewe ndio hii imewadia. Hivyo asilete masihara atajipoteza yeye mwenyewe na mtoto wake ndio atakuwa mwendawazimu nahaala wa laila.
Bi Mwantumu akafanya kama alivyoagizwa akawa sasa yupo juu ya lile kaburi jipya la mtoto mchanga, huku amejifunika gubigubi shuka nyeupe mithili ya sanda huku anatetemeka kwa uoga. Baada ya kupita kitambo cha takribani kama nusu saa tu, akaanza kusikia mvumo wa upepo mkali uliokuwa unatikisa miti yote ya pale makaburini. Upepo ambao ile shuka aliyojifunika ikawa kama inataka kupeperushwa na upepo.
Ghafla akashtukia kama kuna mtu anamfunua shuka yake anahema kwa nguvu, akaanza kumtomasa matiti yake. Akaanza kutaka kumlaza chini pale kwenye kaburi. Alikuwa hajafungua macho yake na hakumbishia kwa kuhofia kifo chake na kumpoteza mtoto wake Masoud. Wakati yule mtu anampapasa mapaja yake, akasikia kishindo kikubwa cha kama risasi iliyopigwa hewani. "Nyoosha mikono juu, upo chini ya ulinzi kibabu muasherati mkubwa wewe" ilikuwa ni sauti ya mmoja wa kundi la mapolisi, waliokuwa wamevamia makaburini saa saba za usiku kumkamata Shekhe Mbonde. Ilikuwa ni fedheha kubwa kwa Shekhe Mbonde na Bi Mwantumu.
"Wewe Bibi kavae nguo zako haraka sana, nawe upo chini ya ulinzi saa mbaya hizi za usiku makaburini unafanya nini, mpaka miaka hiyo yote uliyonayo na utu uzima bado tu unashinda kwa waganga. Huo ni umri wa kufanya toba kwa Mungu wewe unakuja kwa waganga ingebaki kidogo tu ungebakwa na huyu mganga. Kama hujui bibi huyu anaitwa jina la utani "kikaango", hakichagui mboga, uwe mke wa mtu, uwe bibi kizee maadamu umefungasha tu yeye twende kazi" aliongezea askari mwingine mwanamke, aliyekuwa anamuonea huruma Bi Mwantumu.
Bi Mwantumu akatamani ardhi ipasuke moja kwa moja aingie afukiwe, atoweke kwenye uso wa dunia hii tambara bovu, kukwepa aibu. Akajifananisha na hadithi ya punda kunyimwa pembe akapewa masikio, alipolia choyo akaongezewa mlio.
Ilikuwa ni aibu ya mwaka, habari zilisambaa kwa kasi kijiji kizima ndani ya muda mfupi umati wa watu ukafurika pale makaburini. Waandishi wa habari na makamera yao nao hawakubaki nyuma walikuwa wamefuatana na polisi wale waweze kuripoti tukio hilo. Wakiwa na hasira wananchi hao, wengine wakiwa wamebeba silaha za jadi kama mapanga, mashoka, mundu na zinginezo.
"Tuachieni hao walozi tumalizie kazi hapa hapa" alisikika mmoja wa wananchi mwenye hasira kali. "Biashara zetu haziendi vizuri, faida hatuzioni, hawa dawa yao ni kuchomwa moto tu, kijiji chetu ni kikongwe lakini tumebaki nyuma mithili ya koti, hatuna shule za maana hatuna hospitali bora, sababu ni hawa wanga wakubwa" alisikika mkuda mwingine. "Mke wangu Bi Chausiku alienda kutibiwa kwa hiki kibabu, tahamaki kumgeuza mke wake kimazingara ukimfata kumuhoji anatishia kukutupia majini" alilalama mwananchi mwingine.
Nchi nzima kulikuwa na kampeni ya kuwakamata waganga wa kienyeji wanaopiga ramli chonganishi katika jamii. Mbiu ya mgambo ilipigwa ikiwataka kila mwananchi mwenye taarifa za siri na za dhahiri za mganga anayejihusisha na kupiga ramli chonganishi ajitokeze kuleta taarifa. Serikali itampa ulinzi stahiki na itaficha majina na taarifa za wote walioleta taarifa hizo kulinda usalama wao. Jina la Shekhe Mbonde nalo likatajwa, hivyo akawa kwenye rada za wana usalama.
Bi Mwantumu baada ya kuhojiwa na kufanyiwa usaili wa kina alionekana hana hatia, ila alitakiwa awe shahidi namba katika kesi ya dhulma za kingono dhidi ya mganga feki Shekhe Abeid Mbonde. Baada ya kuachiwa yeye na shoga yake Bi Mwazani wakarejea Dar es salaam vichwa chini. Mambo yao yamekwenda mbagombago kinyume na walivyotarajia. Badala ya kupata faraja wamepata fedheha isiyoelezeka. Hadithi ya jipu kulipuka kugubua donda ikasadifu kwao.
Huku tukio lao zima likiwa limeripotiwa kwenye magazeti, redio na televisheni. Ilibidi amshukuru Mungu na akubaliane na matokeo tu kuwa mtoto wake Masoud Masoud ameshakuwa kichaa na amepotea. Hawezi tena kushindana na alilolikadiria Mola kwake, jitihada haiwezi kushinda kudura. Akawa ni mtu wa kujifungia ndani anaona aibu kutoka nje anahisi kila mmoja atakayeonana nae ameona picha zake za kukamatwa uchi makaburini usiku wa manane. Baada ya miezi kadhaa kupita akazoea akaanza maisha yake kama ya zamani siku zikaanza kusonga.

SURA YA PILI
"Maso Maso, mwehu mtaani"
"Maso Maso.....Msela toka Sinza kwa wajanja, nimezaliwa Ocean Road nitazikwa Kisutu inshallah..... sijaja Mjini kwa mbio za mwenge wala kwa ajili ya kufuata shule, mie ni "Born Town" bana, born here here ha..... ha......haa...teh.... teh....teh.. Haya haya tunaendelea elimu kitaa bila twisheni, nyie akina dada mnanunua magari mazuri sana lakini kila tatizo hata dogo tu unaita fundi, mnaliwa pesa zenu mnapunguza bajeti za pipi za wajomba zangu nyumbani.
Leo nawafundisha kudili na gari yako ikikataa kuwaka. Ukiona haiwaki kwanza kuna uwezekano mkubwa kwamba betri imekufa. Kuna sababu nyingi ya hii kutokea, zikiwemo, labda uliacha taa zikiwaka kwa muda mrefu. Sababu inaweza kuwa nguvu ya betri haiendani na nguvu gari, au betri imeingia maji. Wakati mwingine betri ni ya muda mrefu na imechoka. Woyo Woyo Woyoooooo.....! Huyo alikuwa ni Masoud Masoud mtoto wa Bi Mwantumu akiwa mitaa ya Posta, mwehu amekwisha kazi.
Ilishapita nusu mwaka sasa tokea atoroke wodi ya wagonjwa akili katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili. Mama yake alishakubali matokeo kuwa mwanawe ni kichaa sasa. Alikuwa amevaa shati lililoraruka kila kona, na suruali yake msurupwete wenye viraka vya kutosha. Mguuni amevalia ndula saizi kubwa kuliko miguu yake. Mkononi amebeba sanduku la chuma la mafundi gereji lililoshiba spana zote muhimu kwa fundi magari.
Kichwani nywele zake zikikuwa hazijapitishwa chanuo yapata miezi sita. Ulikuwa ukimuona tu hauhitaji kuuliza mtu kuhusiana na afya ya akili yake. Alikuwa amejipatia umaarufu maeneo ya Posta yote mpaka kijiwe chake mtaa wa Ghana. Hapo ndio palikuwa kijiwe chake jirani na Wizara ya Mambo ya Ndani pamoja na Makao Makuu ya Polisi.
"Unajua huyu kichaa anazungumza vitu vya ukweli kabisa kuhusu magari, mimi fundi magari nimemkubali sana muda mchache tu niliomsikiliza" alisema mmoja wa watu waliokaa kwenye benchi la fundi viatu karibu kabisa na aliposimama mwehu "Maso Maso" anapomwaga sera zake. "Huyu kijana ni balaa, akili zake zikitulia wanakujaga hapa mafundi magari wa gereji kubwa kubwa hapa mjini kumuuliza maswali" alichangia mada fundi viatu anayejulikana kwa jina la Peter huku akichapa kazi kwa kuvifua viatu vyake vya sabuni, kabla ya kuvipaka dawa ya viatu.
"Kwanini sasa ndugu zake wasimtafutie tiba apone, huyu kijana ni hazina kwa taifa akipona akafunguliwa gereji ataweza kuajiri mamia ya watu" alichangia mada muuza magazeti aliyekuwa anafuatilia mazungumzo yale.
"Nasikia wamehangaika bara na pwani, kwa waganga na waganguzi lakini wameambulia patupu, nasikia katupiwa jini mbaya sana" alizungumza fundi Peter ambaye alikuwa anapenda sana mada za kuchangamsha kijiwe chake ili pavutie wateja waje kupiga kiwi viatu vyao.
"Itakuwa kweli katupiwa jini, maana huyu kijana mie namfahamu vizuri sana tulikuwa tunakaa nae jirani Sinza-A. Huyu alifaulu vizuri sana katika mitihani yake ya kidato cha sita. Alikuwa anasoma shule ya watoto wenye vipaji maalumu vya akili, Mzumbe sekondari. Matokeo yake alipata daraja la kwanza pointi tatu, akaongoza nchi nzima. Alikuwa anasoma mchepuo wa Fizikia, Kemia na Hesabu. Kuna mwarabu mmoja nasikia alipopata taarifa za za kuwa ni yatima, amebaki na mama yake tu naye ni mtu mzima akampa ufadhili wa kusomea Uhandisi huko nchini Uingereza. Sasa toka amerudi huko ndio akaanza kuwa haeleweki eleweki" alichagiza mada hiyo mmoja wa wanunuzi wa magazeti aliyekuwa pia anamfuatilia majinuni "Maso Maso".
"Isijekuwa alitembea na mke wa mtu huko Arabuni wakamtengeneza, maana kuna wakati huwa akikaa hapa pembeni ya duka langu anaimba mashairi yake ya lugha ya kiarabu huwa naambulia ubeti anaourudia mara kwa mara utamsikia "Hoor-ain uhibukki Hoor-Ain I love you, Hoor Ain nakupenda.. " alichangia mada muuza duka anayeitwa Soni ambaye muda mwingi majinuni "Maso Maso" anaketi kivulini kwenye pembe ya kibanda lake la biashara. Mchango wa Soni katika kujadili mada ya uchizi wa "Maso Maso" uliamsha kicheko cha kikwakwa baraza zima, sasa likachangamka.
Wakati mjadala juu yake unaendelea ghafla geti la Wizara ya Mambo ya Ndani likawa linafunguliwa likatoka gari moja aina ya "Land Cruiser v8" rangi ya buluu yenye kibao cha namba za gari "PT" kujulisha ni gari ya polisi. "Maso Maso" alivyoliona tu lile gari akachomoka mbio mbio kulikimbilia, akalipiga mkono likatii amri na kusimama. Akaanza kuongea na yule kigogo wa polisi aliyekaa upande wa siti ya abiria, akachomoa noti ya elfu kumi akampa. "Maso Maso" alivyopewa tu hata hakuaga mbio mbio dukani kwa Soni hata hakukumbuka hata kushukuru. "Naomba mtindi paketi moja, Cocacola moja na maandazi matatu" alitoa oda "Maso Maso" uso wake ukiwa na bashasha.
Alivyopewa tu akachukua bakuli lake chafu chafu akachanganya soda yake, mtindi na akakatia maandazi akaanza kula bila kujali kunawa mikono wa kuosha sahani yake ya chakula. "Masooo..... wewe kiboko aisee mpaka vigogo wa polisi wanakupa saluti, nimeona umepigwa na msimbazi" alitania Soni kumtania mwehu "Maso Maso" baada ya kumpa mahitaji na kuanza kula.
"Wewe mimi sio wa nchi hii, hata Trump Rais wa Marekani atanipigia saluti, hata nyinyi bendera hufuata upepo mtaniimba sana tu tena huku mnalia, nitakuwa maarufu kwenye kila kinywa cha Mtanzania, jiandae tu kunipigia kura kwa hiari au kwa lazima" alijibu "Maso Maso" huku anashushia tumboni mwake mtindi uliochanganywa na soda.
MAMBO YANAANZA KUNOGA INSPEKTA WA POLISI ANAMPA PESA MWEHU KUNANI HAPO?? ENDELEA KUFUATILIA RIWAYA HII
ITAENDELEA
 
RIWAYA: MSAKO WA MWEHU
MTUNZI: Badi .M. Bao
MWASILIANO. 0625920847, ( whatsap )
E- mail: badi.bao11@gmail.com
Dar es Salaam

SEHEMU YA NNE

"Wewe mimi sio wa nchi hii, hata Trump Rais wa Marekani atanipigia saluti, hata nyinyi bendera hufuata upepo mtaniimba sana tu tena huku mnalia, nitakuwa maarufu kwenye kila kinywa cha Mtanzania, jiandae tu kunipigia kura kwa hiari au kwa lazima" alijibu "Maso Maso" huku anashushia tumboni mwake mtindi uliochanganywa na soda.
" Unaambiwa yule Inspekta wa polisi anamheshimu sana "Maso Maso", ile gari aliyopanda "v8" wakati imefika ndio ina wiki tu ilipata hitilafu, mafundi wa jeshi la polisi wote walichemka. Ndio mwishoni wakamkumbuka "Maso" kuwa anajua ufundi magari. Walimfata hapa, aliwaletea madahiro kweli kweli maana baadhi ya polisi walikuwa na tabia ya kumpiga piga wakimuona hapa getini. Huyu Bosi wao aliyempa elfu kumi alimbembeleza mpaka akakubali ndani ya dakika 5 tu gari ikawaka na kupona kabisa. Tokea hapo wanamuacha afanye anavyotaka, siku akiamka vizuri anaweza kuingia mpaka kule karakana yao akawasaidia kutengeneza magari. Na siku kichaa chake kikimpanda atamwaga matusi, hamna anayeweza kumsogelea," alieleza fundi Peter tukio la ukaribu wa "Maso Maso" na kigogo wa polisi.
Soga za hapa na pale zikaendelea ili mradi siku imalizike kwa usalama. Mpaka jua likazama, hayo ndio yalikuwa maisha mapya ya Masoud Masoud, maisha ya kuwa punguwani wa akili asiyejua kesho yake itakuchaje, asiye na uhakika wa kula yake wala afya yake. Analala vibarazani, mbu wake, baridi yake. Wapo waliomsikitikia kwa tatizo lililompata na wapo waliompuuza na kumbeza kuwa kayataka mwenyewe kutembea na mke wa mtu, wakatoa hukumu bila kufahamu chanzo chake ni nini!.

Kikao kizito ofisini kwa Inspekta Haroub
Ofisini kwa Inspekta Haroub Farouq, mmoja wa vigogo wa Jeshi la Polisi kulikuwa na kikao kizito kinachoendelea baina ya maafisa wa ngazi za juu wa Polisi Makao Makuu na wale wa kutoka Wizara ya Mambo ya Ndani na Ustawi wa Nchi. Ni kama kikao cha baba na mtoto kwa sababu hawa wote walikuwa ofisi zao zipo pua na mdomo na wanatumia geti moja na majukumu yao ya kikazi yanashabihiana. "Nimewaiteni kikao hiki kifupi cha kabla ya kuanza kazi, ili kukumbushana majukumu yetu mazito yalioyopo mbele yetu. Kama mnavyofahamu tunatarajia kupata ugeni mzito wa Mabalozi wawili toka Marekani na Canada." Akapumzika kidogo mazungumzo yake na kumeza mate kisha akaendelea. "Wanakuja kutukabidhi msaada wao wa vifaa walivyotoa kwa Jeshi la Polisi. Vifaa hivyo ni magari ya doria idadi yake 50, pamoja na kompyuta zaidi ya 1000. Ni msaada ambao umetufikia katika wakati muafaka hasa ukichukulia bado vituo vyetu vya Polisi Tanzania nzima tunaandaa mashauri ya watuhumiwa kwa kutumia mtindo wa karne za ujima wa peni na daftari.
Pia tuna uhaba mkubwa wa magari ya kufanya doria hasa nyakati za usiku. Huko nje ya Miji, majambazi yanajitawanya kwa mapana na marefu. Sio jambo zuri kwa Jeshi la Polisi, ni dalili ya kuwa tumeshindwa kwa kila njia na jiha kudhibiti uhalifu nchini Tanzania. Sasa anapotokea mhisani wa kutupa magari 50 ni jambo la kupongezwa sana.
Sasa maandalizi ya mkutano huo wa makabidhiano yapambe moto, kila mwenye jukumu lake alitekeleze kwa ufanisi mkubwa. Habari nilizopata ni kuwa mgeni rasmi atakuwa Waziri wa Mambo ya Ndani na Ustawi wa Nchi Mheshimiwa "Ngaiza Jacob Ngaiza", na pia baadhi ya vigogo wa serikali watahudhuria hafla hiyo wakiwemo Wabunge wetu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Tengenezeni naizesheni yenu vizuri kabisa kila kitu kiende kama tulivyopanga. Uzembe wowote utakaosababisha aibu na izara mbele ya wageni wetu, tutahesabu ni uzembe kazini na unaweza kukupelekea kufukuzwa kazi, hivyo tekelezeni wajibu wenu, kumbukeni cheo ni dhamana, ahsanteni sana" akawa Inspekta Haroub ameshafunga kikao kifupi cha kulishana yamini ya utendaji kazi uliotukuka.
Kila Afisa akawa anatawanyikia ofisini kwako kichwa chini kwenda kujipanga vyema kutimiza majukumu yake. "Koplo Michael njoo hapa" ulikuwa ni wito wa Inspekta Haroub kwa fundi mkuu wa karakana ya Jeshi la Polisi. "Naam afande" aliitikia wito huku akigeuka na kupiga saluti maana tayari alishakishika na kunyonga kitasa cha mlango wakutokea. Ikabidi akiache kitasa na kupiga hatua mbili tatu za kurejea karibu na Bosi wake.
"Uzembe kama wa kipindi kile cha kushindwa kutengeneza v8 sitaki ujirudie tena mpaka anakuja kukusaidieni kichaa nyie wenye akili timamu mnaolipwa mishahara na posho mpo mpo tu mnapigwa ubwete! "alizungumza kwa kufoka Inspekta. "Samahani Afande kosa halitojirudia tena" alijibu Koplo Michael kwa unyenyekevu akiwa amekakamaa hatikisiki. "Kama mtamhitaji yule mwehu "Maso Maso" tena mie namuweza sana yule atakusaidieni hasa ukichukulia baadhi ya magari yamekaa bandarini muda mrefu na yatajaribiwa pale kama yanafanya kazi, sasa inaweza kuja aibu ya mwaka, au unasemaje"? aliuliza swali la mtego Inspekta Haroub.
"Itakuwa vizuri sana, unajua sasa pale karakana wenzetu wawili wapo likizo na mmoja amefiwa na mzazi wake sasa, ukaguzi wa magari yote ni shughuli pevu bora "Maso Maso" aje tu kama utamdhibiti asilete Ukichaa wake" akajibu Koplo Michael ili kumridhisha Bosi wake asije kukataa msaada likazuka la kuzuka akatimuliwa kazi.
"Haya niachie mimi hilo jukumu kesho tu utamuona karakana" akajibu Inspekta Haroub, wakaagana akaendelea na majukumu yake mengine.

SURA YA TATU
Hafla ya makabidhiano ya vifaa kwa Jeshi la Polisi
Ilikuwa ni siku ya Ijumaa majira ya kuanzia saa nane mchana jua lilikuwa bado linatoa miale yake yenye kuchoma mwili, kadamnasi ya watu ilikuwa imekusanyika mbele ya jengo la Wizara ya Mambo ya Ndani. Kulikuwa na hafla kubwa ya makabidhiano ya vifaa vya kazi vikiwemo magari na kompyuta kwa Jeshi la Polisi. Vifaa hivyo vilikuwa ni msaada kutoka nchi ya Marekani na Canada kwa ajili ya kuboresha utendaji wa jeshi hilo.
Bendi ya Jeshi la Polisi ilikuwa inatumbuiza nyimbo yao mpya ya kusifia ushirikiano mwema wa kidugu baina ya Tanzania na Marekani. Bendi hii ya "Polisi Jazz Band" ni moja ya bendi kongwe nchini iliyozoeleka miaka ya 70's-80's kwa mtindo wao wa "vangavanga". Pia wakaanza kuimba nyimbo zao zilipendwa kama "Naamua kurudi kijijini","Halima" na "Baba yupo wapi" nyimbo ambazo zilisuuza roho za watu wazima waliohudhuria ambao walikuwa wanakumbushwa enzi wapo vijana. Ilimradi hafla nzima ilikuwa imefana sana kila mtu alikuwa ana furaha sheshe.
Ilipofika saa kumi alasiri, shangwe, hoihoi, nderemo na vigeregere vikaibuka kisha watu wakatulia vitini raha mustarehe kama Sultan bin Jerehe. Nderemo hizo zilikuwa ni kuashiria kuwasili kwa Waziri wa Mambo ya Ndani Mheshimiwa Ngaiza Jacob Ngaiza akiwa ameambatana sambamba na wageni wake watukufu Mabalozi wa Marekani na Canada. Wakakaribishwa meza kuu huku viongozi wengine wa chama na serikali wakiwa wameshachukua viti vyao. Zikaanza hotuba mbalimbali za wageni hao wakiwa wameambatana na Maofisa wao wa kutoka Ubalozini. Kisha ukafika wakati adhimu wa kukabidhiana vifaa hivyo. Wakaitwa mbele ya kadamnasi wageni wa heshima wote wakasogelea yale magari na kompyuta. Wakaanza kuzungukwa na wanahabari kwa ajili ya kuchukuliwa picha na video za kutosha kwa ajili ya vyombo vyao vya habari.
Balozi wa Marekani na Balozi wa Canada wakapanda kwenye magari pamoja na Waziri wa Mambo ya Ndani kwa ajili ya kuyajaribisha. Waziri wa Mambo ya Ndani, Mheshimiwa Ngaiza, alipopachika funguo kwenye swichi ili awashe gari alipowasha tu, gari linataka kuwaka kisha likagoma kwa kuzimika. Ghafla moshi mzito ukaanza kufuka mbele ya boneti la gari, kabla hawajafahamu kinachendelea ukalipuka mlipuko mkubwa wa bomu kwenye lile gari haujapata kusikika tokea Jiji la Dar es salaam ligeuzwe jina kutoka kuitwa Mizizima. Kishindo kikubwa hicho kikazusha taharuki na tafrani eneo zima la Posta Mpya kila mtu akawa anakimbilia upande wake kuokoa roho yake. Ajali nyingi zilitokea barabarani siku hiyo kwa magari kugongana yenyewe kwa yenyewe na watu kugongwa kwa sababu ya hofu iliyotokana mlipuko huo uliotokea jioni hiyo.

ITAENDELEA
KUPATA KITABU KUANZIA JUMAMOSI IJAYO NICHEKI KWA NAMBA
0625920847
 
RIWAYA: MSAKO WA MWEHU
MTUNZI: Badi .M. Bao
MAWASILIANO. 0625920847, ( whatsap )
E- mail: badi.bao11@gmail.com
Dar es Salaam

SEHEMU YA TANO


Jumamosi nyeusi iliyotanda huzuni
Kulipokucha kila kona ya nchi katika siku hiyo ya Jumamosi gumzo lilikuwa ni tukio la mlipuko wa jana yake kwenye jengo la Wizara ya Mambo ya Ndani. Magazeti yote yalitoa taarifa ya tukio hilo kwa ufasaha kabisa. Televisheni zote za ndani ya nchi zilisitisha vipindi vya burudani na michezo wakawa wanaripoti juu ya tukio hilo la kishenzi na kinyama mfululizo.
Mpaka kufikia saa sita mchana wa siku hiyo ya Jumamosi ilithibitika watu 50 walifariki dunia huku zaidi ya 100 wakilazwa hospitalini Muhimbili kama wahanga wa kisanga hiko cha kigaidi. Miongoni mwa waliofariki dunia walikuwa ni Mabalozi wote wawili wa Marekani na Canada, pamoja na Waziri wa Mambo ya Ndani. Pia Wabunge 10 nao walipoteza maisha yao, hivyo ilikuwa ni misiba iliyogusa Tanzania nzima. Kama hukufiwa na Mbunge wako, basi utakuwa umepoteza Mjomba, Shangazi, Rafiki, Baba, au Mama ili mradi kila mtu aliguswa kwa namna moja au ingine.
Amiri Jeshi Mkuu, Rais wa Nchi alizungumza mubashara na wananchi kupitia vyombo vya habari vya redio, televisheni na mitandao ya kijamii. Alitangaza maombolezo ya kitaifa ya wiki moja na bendera ya taifa itapepea nusu mlingoti. Pia aliwataka wananchi kuwa watulivu wakati vyombo vya usalama vinawasaka wahusika ili wafikishwe mahakama. Akawahakikishia kuwa serikali yao ipo makini kuhakikisha inavitumia vyombo vyake vya ulinzi na usalama na wananchi kukabiliana na tishio la makundi ya kigaidi dhidi ya Tanzania.
Ikapangwa Ijumaa ijayo kuwa ni ya mazishi ya kitaifa. Ambapo Wabunge waliofariki watapelekwa Dodoma Bungeni kuagwa kwa heshima zote kisha maiti zao zitapelekwa Majimboni kwao kwenda kuzikwa. Miili ya Mabalozi wa Marekani Na Canada ilisafirishwa kwenda nchini kwao kuzikwa. Pia serikali ya Marekani ikawataka raia wake wote waliopo Tanzania warejee nyumbani mara moja mpaka tishio la kigaidi dhidi yao litakapokoma. Wingu jeusi lilitanda katika nchi ya Tanzania kwa upande wa kidiplomasia. Ilishachafuka kimataifa sifa yake ya kuwa kisiwa cha amani na usalama, ikapotea na kuanza kuonekana kuwa sio sehemu salama tena bali ni kisiwa cha mauti na machafuko.
Vyombo vya usalama vilikuwa sasa vinaanza mkesha wa usiku na mchana kwa ajili ya kuwasaka wahusika wa tukio hilo la kigaidi.

SURA YA NNE
"Magaidi wajianika dhahiri shahiri"
Vyombo vya Dola vilichanganyikiwa havikufahamu lengo la magaidi kufanya shambulio hilo kwa nchi ya Tanzania. Mashushushu wakatawanywa kila mtaa wanahaha na kunusanusa kutafuta penyenye za watu waliokula njama za kulipua mabomu kwenye Jengo la Wizara ya Mambo ya Ndani, Ijumaa iliyopita.
Ilipofika siku ya Jumapili asubuhi fumbo la makusudio ya shambulio hilo likateguka, likawa hadharani kweupe. Vipeperushi viliokotwa vimesambazwa mitaani maeneo yote ya Jijini kuanzia Posta Mpya mpaka Kariakoo. Mbagala kuu mpaka Bunju, hakuna kichochoro, wala kinjia ambacho vipeperushi hivyo havikufika. Kipeperushi hicho kilisomeka kama ifuatavyo :
"TUNATAKA NCHI YA TANZANIA IKATE MAHUSIANO YA KIDIPLOMASIA NA MAADUI ZETU NCHI YA KENYA MARA MOJA. TUNATOA MUDA WA SIKU TATU TU BALOZI WA TANZANIA AWE AMERUDISHWA TANZANIA, MWISHO JUMATANO IJAYO, VINGINEVYO KISHINDO KINGINE KIKUBWA KINAKUJA MJIANDAE KUCHIMBA MAKABURI MENGI ZAIDI"
احب الحور العين
Ujumbe huo ulioishia na chata ya maandishi ya lugha ya kiarabu ulizusha kizaa upya na kupandikiza hofu mpya miongoni mwa wananchi. Hapo kila mtu akawa anajiuliza "hao walioandaa kipeperushi ni watu gani, mbona hawajajitaja!". Wale watu waoga wenzangu na mimi wakaanza wakakacha kwenda Mjini tena, na wengine wakarudi Mikoani kwao kabisa kupisha upepo mbaya upite.
Magaidi walishafanikisha walichokikusudia, nacho ni kupandikiza hofu na taharuki miongoni mwa wananchi na kudhoofisha uchumi wa nchi. Pia watalii wakaanza kuogopa kuitembelea Tanzania. Kwa watu wa usalama kwao haikuwa shida kutambua kuwa hivyo ni vitisho toka kundi la kigaidi la "Al-shabaab", walihitaji muda tu kuthibitisha dhana yao hiyo. Adui aliyetangaza vita ya hadharani na nchi ya Kenya ni kundi la kigaidi la "Al-shabaab". Kundi hilo lilikuwa linaendesha mapambano ya ulipizaji kisasi dhidi ya Jeshi la Kenya ambalo katika miaka michache iliyopita lilijiunga na "Vikosi vya Umoja wa Afrika" (AMISON) kwa lengo la kuwaondoa wapiganaji wa kundi hilo katika Miji mikubwa na midogo nchini Somalia. Hivyo vipeperushi hivyo sasa vilionyesha "Al-shabaab" wanakusudia kuifanya Kenya ni kisiwa, iwe nchi iliyotengwa na majirani zake wa Afrika Mashariki. Mipango ambayo walijua fika kama itafanikiwa itadhoofisha Umoja wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na Afrika kwa ujumla. Hivyo kuzima ndoto za viongozi waasisi wa Afrika akina Kwame Nkurumah wa Ghana na Mwalimu Julius Kambarage Nyerere wa Tanzania. Ndoto yao ya kutamani uwepo wa Umoja wa Afrika wenye nguvu ya kisiasa, kiuchumi, kiutamaduni na kila nyanja ya kimaendeleo. Magaidi tayari walileta kishindo cha mtego kilichowanasa wakazi wa Tanzania.


Vibaraka wa Al-shabaab wakabidhiwa mikononi mwa Kachero Manu

Ofisi za Usalama wa Taifa kitengo maalumu cha Ujasusi, zilikuwa zipo katika jengo la "Benjamin William Mkapa Pension Tower" roshani ya tano katika mtaa wa Azikwe. Zamani jengo hili lilikuwa linaitwa "Mafuta House". Zilikuwa ni ofisi za siri ambazo mtu wa kawaida huwezi kujua kazi wanazofanya watu hao. Ilikuwa ni Ofisi yenye Makachero bobezi wasiozidi watano, pamoja na Mkuu wao wa kazi mpya Bwana Omega Mtanika na Katibu Muhtasi wao dada Kokunawa.

Siku hiyo ya Jumatatu asubuhi Makachero wawili 'Manuel Yosepu maarufu kama "Kachero Manu" na Kachero wa kike Yasmine Abeid walikuwa wameitwa ofisini kwa Mudiru wao wa kazi Bwana Omega Mtanika ili wapewe jukumu jipya la kikazi.
Kachero Manu alikuwa ndio kwanza bado mpya mpya hajamaliza hata fungate lake la ndoa aliyoifunga hivi karibuni na mpenzi wake wa siku nyingi, tokea akiwa Chuo Kikuu, Bi Faith Magayane. Alipigiwa simu jana yake Jumapili saa sita mchana, akiwa yupo "Hotel Verde", Zanzibari na Katibu Muhtasi wa Mudiru wake kuwa anatakiwa arudi ofisini mara moja.

Mara baada ya vipeperushi vya magaidi wa "Al-shabaab" kusambazwa kwenye kila kona ya Jiji. Idara ya Usalama wa Taifa ikaona kuna haja ya Jeshi la Polisi kupigwa jeki na Kachero Manu, ambaye ametabahari katika fani ya Ukachero. Maji yalishazidi unga kwa Jeshi la Polisi, mapambano dhidi ya magaidi walio na uthubutu wa kufanya shambulio katika Makao Makuu ya Wizara ya Mambo ya Ndani yalikuwa ni mapambano kabambe. Ilikuwa ni patashika ya nguo kuchanika, mtoto hatumwi dukani, ngoma inogile mpaka kieleweke.

Kachero Manu kumuelewesha mkewe kuwa anavunja fungate kwa sababu ameitwa ghafla kazini, ilikuwa ni kazi nzito kueleweka. "Kama kazi yenyewe hiyo ambayo inakukosesha hata muda wa kutulia na mke wako katika kipindi muhimu kama hiki cha fungate bora uache kazi tu. Huu ndio muda adhimu tuliotakiwa kama wanandoa wapya kujenga mustakabali wetu mpya wa namna ya kuendesha maisha yetu" yalikuwa ni maneno makali yaliyoropokwa na mke wa Kachero Manu akiwa amefungwa na joto la hasira kooni mwake.

"Sasa mke wangu nikiacha kazi hii nitafanya kazi gani? " aliuliza Kachero Manu swali la mtego kwa sauti ya kubembeleza huku amemkazia macho mkewe. "Utajiajiri tu, utafute shamba Bagamoyo unalima mbogamboga na matunda na huku unafuga ng'ombe na kuku maisha yatajipa tu" aliweka msisitizo kwa sauti ambayo inaonyesha anamaanisha kile anachokizungumza hatanii japo chembe.

"Mke wangu, uhondo wa ngoma ingia uicheze, usizuzuke na ile michanganuo ya kilimo sijui cha matikiti au ufugaji wa kuku inayokufikia mezani kwako pale benki kwenye idara yako ya mikopo ukajua basi kilimo na ufugaji kinalipa sana.

Michanganuo mingi inakolezwa matokeo kuliko uhalisia ulivyo, mie imani yangu naamini kila Mtanzania mkubwa kwa mtoto ana Diploma ya Usanii hata kama hajasomea sanaa kule chuo cha TASUBA, Bagamoyo. Utaletewa mchanganuo wa kilimo cha matikiti uelezwe ekari moja itakuzalishia milioni sita, lakini ukienda kukifanya hicho kilimo au kuangalia hali halisi ya uchumi wa wakulima hao wa matikiti hauendani na michanganuo yao uliyoisoma. Kilimo na ufugaji Tanzania bado kuna changamoto kubwa ya masoko, bei duni, pembejeo feki, na zinginezo kibao. Labda serikali yetu siku za mbele ije na sera ya kulinda bei ya wakulima wa mbogamboga na matunda na bidhaa za mifugo kama mayai, maziwa na nyama. Vinginevyo bado haujanishawishi mke wangu kucheza pata potea na ya kuacha kibarua changu kinachonipa jeuri Jijini" alimalizia maelezo yake Kachero Manu bila kupindisha maneno kwa mkewe ili kumuweka sawa.

"Mhhh....haya bana ngoja tukomae na ajira za mkoloni za maofisini, ambazo zinatubana mpaka tunashindwa kufurahia maisha ya kifamilia, muda wote tunatenganishwa na majukumu ya kikazi tu" alijisemesha kwa manung'uniko mke wake huku akionekana ameshakubaliana na maelezo ya mumewe kwa shingo upande.

"Magaidi wamelipua Wizara ya Mambo ya Ndani na kusababisha vifo vya viongozi kadhaa, hivyo hamna mtu anaweza kuwafunza adabu magaidi kama mimi serikali ndio imeona hivyo, ngoja nikatoe jasho na damu yangu kwa ajili ya nchi yangu. Nchi ikichezewa na magaidi wakafanya wanavyotaka wao watakuja kutupangia mpaka muda wa kulala na kuamka" aliendelea kukizalendo kwa mkewe ili kumjenga kuwa ameolewa na mpambanaji katika medani za kivita, ambaye anaweza hata kuiacha familia yake miaka miwili mtawalia anaipigania nchi. Alitaka atambue kabisa kuwa hajaolewa na mwanamuziki ambaye anabembeleza mpenziwe kwa nyimbo, vilio na chakula cha nyuki, zawadi ya mauaridi.

Kachero Yasmine Abeid nae alijumuishwa kwenye jukumu hili kutokana na sababu mbili kubwa. Kwanza yeye ndio aliyefanikiwa kuzima mashambulio ya mabomu yenye viashiria vya ugaidi yaliyokuwa yanarindima Zanzibar kila kukicha katika miaka ile ya 2012-2013. Pia alikuwa ni fasaha sana katika bahari ya lugha za Kiarabu na Kisomali, hivyo huenda kuna nyaraka zinaweza kupatikana za siri yeye ndio atakuwa mtarujumani wa lugha kwa Kachero Manu. Alihamishiwa kikazi kuja bara kutokea Zanzibar yapata mwaka na nusu sasa.
 
RIWAYA: MSAKO WA MWEHU
SEHEMU YA SITA


"Mbwa koko wamejileta wenyewe wapeni mfueni wa nguvu"
"Vijana wangu, nimewaiteni kikao kifupi sana cha kupeana majukumu ya kutekeleza. Sisi kazi yetu ni vitendo zaidi, kuupepeta mdomo tumewaachia Wanasiasa huko kwenye majukwaa yao na Wachungaji na Mashekhe huko kwenye nyumba zao za ibada. Nadhani mnafahamu tukio lililotokea Ijumaa iliyopita...!" alisimamisha maongezi yake kwa muda Bosi Omega Mtanika akavua miwani yake na kuwaangalia usoni kwa kuwakazia macho yake makali Kachero Yasmine Abeid na Kachero Manu. Wote kwa pamoja wakatikisa vichwa vyao kuashiria wanajua tukio lililotokea siku ya Ijumaa. Alipoona wameafikiana na alichowauliza, akavaa tena miwani yake na kuendelea na maongezi yake.
"Sasa nimekutupieni zigo hilo mlibebe, kama mie nilivyotupiwa na wanene huko juu, mzigo mzito wabebebeshe wanyamwezi, sasa sisi ndio tumebebeshwa. Ujumbe wangu kwenu upo wazi mbwa koko, vibaraka wa "Al-shabaab" wamejileta wenyewe wapeni mfueni wa nguvu, wakawasimulie vizuri Mabwana zao wanaowatuma huko Somalia, mfuasi wa nzi daima hula uvundo wameyataka wenyewe" akaonyesha kuwa kamaliza maongezi yake.
Ukapita ukimya wa dakika kadhaa, kisha Kachero Manu akavunja ukimya huo kwa swali. "Je ameshajulikana nani atakuwa Mgeni rasmi katika mazishi ya Kitaifa ya Wabunge wetu hiyo siku ya Ijumaa, Dodoma?".
"Makamu wa Rais anategemewa kuongoza mazishi hayo ya Kitaifa" alijibiwa kwa ufupi na Mudiru wake Bwana Omega Mtanika. "Mkuu tunakuahidi utendaji uliotukuka, wewe chapa usingizi kwa raha zote, tuachie kazi sisi" aliongea Kachero Yasmine baada ya kuwa kimya kwa muda mrefu. "Ha ha ha ha.....nimefurahi Kachero Yasmine unanipa matumaini mazuri, hasa nikipitia kazi yako nzuri uliyoifanya Zanzibar, ambayo ilibaki kidogo tu igeuke kuwa Somalia ndogo" alijibu Bwana Mtanika kwa kuanza na kicheko, akifurahishwa na ujasiri wa Kachero wake. "Ameacha kula urojo wa Zenji sasa yupo Bara anakula ugali wa dona kwa mandondo ndio maana amekuwa mkakamavu kila siku ananiambia mikono inamuwasha anatamani kazi " alitania Kachero Manu, wote kwa pamoja wakafa kwa kicheko.
Wakaagana na kutawanyika, huku Kachero Manu akifuata guu moja na Kachero Jasmine kwenda kujipanga kwa kazi nzito iliyopo mbele yao.

Hamna kulala Jogoo limewika kumekucha
Siku hiyo hiyo baada ya kikao chao kwisha tu, waligawana majukumu. Kachero Yasmine alitakiwa haraka atangulie Dodoma kuangalia mazingira ya usalama wa viongozi watakaohudhuria siku ya Ijumaa kwenye mazishi ya Kitaifa. Hasa ukichukulia kipeperushi cha "Al-shabaab" kilichimba mkwara mzito wa kuleta maafa mengine kwa Taifa.
Kachero Manu yeye akaelekea moja kwa moja Wizara ya Mambo ya Ndani sehemu lilipotokea tukio la mlipuko wa mabomu kwa ajili ya kuanza taftishi yake ya awali. Alipowasili alikuta kikosi cha mbwa wa kutegua mabomu wametawanywa wananusa eneo la tukio kama kuna mabomu yamebaki yaweze kuteguliwa kwa haraka. Pia kulikuwa na magari makubwa ya kubeba yale magari ya msaada ambayo yamethibitishwa kuwa yapo salama, hayakupata athari ya milipuko ili yaanze kusambazwa yakafanye kazi iliyokusudiwa. Hali aliyokuta mahalo hapoilikuwa inasikitisha sana. Zile picha za majengo ya kule Somalia, Afghanistan, Syria zinazoonyeshwa kila leo kwenye runinga, zilifanania na jengo hilo. Sehemu kubwa ya jengo hilo hasa upande wa kushoto ambao yale magari yaliegeshwa kuliharibika vibaya sana.
Mubashara akaingia Ofisi ya Mapokezi akajitambulisha na kutoa kitambulisho chake cha kazi. Akaomba kuonana na mhusika wa Usalama wa Jengo. "Karibu sana Kachero karibu ukae, nipo tayari kukupa ushirikiano unaouhitaji toka kwangu" yalikuwa ni maneno ya ukarimu toka kwa Inspekta Chacha kwa Kachero Manu, akiwa amekaa ofisini kwake. "Ahsante sana" akajibu huku anavuta kiti na kukaa. Akachomoa peni yake, peni ambayo inauwezo wa kurekodi kwenye mfuko wa shati lake akafungua kidaftari chake kidogo na kuanza mahojiano na Inspekta Chacha;
Kachero Manu: "Kwanza poleni na matatizo, unaweza kunielekeza ni uharibifu kiasi gani umetokea"?
Inspekta Chacha: "Tumepoa tayari, uharibifu kwa haraka haraka siwezi kutoa makadirio, lakini ni mkubwa baadhi ya majengo yameporomoka kama ulivyoona na samani za ofisi na nyaraka kuharibiwa"
Kachero Manu: "Kuna mtu yoyote wa ndani mnamshuku kuhusika na tukio hili na mmefikia wapi kwenye upelelezi wenu? "
Inspekta Chacha: "Hapana hamna mtu yoyote ninayemtuhumu kwa tukio hili. Mpaka sasa tumekamata watu zaidi ya 200 na tunawashikilia na kuwahoji lakini hamna matumaini yoyote ya kumpata mhusika. Tunawashikilia tu ili mradi wananchi huko nje waone tunashughulikia suala hilo la ugaidi lakini hatuna ushahidi wa kutosha kuwabandika tuhuma hizo"
Kachero Manu: "Je naweza kupata picha na video za CCTV-Kamera za siku ya tukio"?
Inspekta Chacha: "Kama nilivyokueleza kuna uharibifu mkubwa wa samani ikiwemo vifaa vya hizo kamera nazo zimeharibika vibaya hatukuambulia kitu"
Kachero Manu: Ahsante sana kwa ushirikiano wako, kama nitakuhitaji tena sitosita kuja tena kutaka msaada wako
Inspekta Chacha: "Karibu hamna shida tupo pamoja mkuu".
Wakapeana mikono na kuagana na mwenyeji wake. Kachero Manu wakati anaweka vizuri vitu vyake kwenye brifkesi lake dogo la rangi nyeusi ili aondoke zake, akaonyesha kuna kitu amesahau kuuliza. "Samahani kuna wafanyakazi wowote wa hapa hasa wa kwenye karakana ya magari ambao hawajafika kazini"? alitupa swali Kachero kwa Inspekta ambaye nae alionyesha dalili za kujiandaa kutoka nje ya ofisi. "Kwa haraka haraka siwezi kukujibu, ngoja niende idara ya rasilimali watu nikapate majibu, nipe kama robo saa, nisubiri hapo kitini" alijibu Inspekta Chacha huku akifanya haraka kuondoka kwenda kuchukua taarifa anayohitaji mwenyeji wake.
Baada ya kitambo cha dakika 10, Inspekta Chacha alirudi na orodha ikiwa na majina ya askari 5 ambao hawakufika kazini. Karatasi ilikuwa imeorodhesha majina yao, vyeo vyao, na majukumu yao ya kazi na sababu ya wao kutokufika kazini na maeneo wanapoishi. Ripoti hiyo Ilieleza kuwa wawili walikuwa akina mama ambao wapo likizo ya uzazi, na wawili akina baba walikuwa wapo likizo zao za mwaka na mmoja hakutokea kazini kwa utoro tu na hana sababu yoyote, na kwenye simu yake ya mkononi hapatikani hewani.
Kachero Manu akaisoma ile karatasi kwa umakini mkubwa kisha akatabasamu, akaisunda kwenye brifkesi yake ile karatasi akaaga tena kwa mara ya pili na kutokomea nje ya ofisi. Alipotoka nje ya geti tu akavuka barabara na kwenda pale kwenye kijiwe cha jirani na Wizara wanapokaa watu, maarufu kwa fundi viatu Peter. Alikumbuka hajanunua gazeti lolote la michezo tokea asubuhi. Kachero Manu alikuwa ni mdau na mpenzi sana wa kabumbu, akiwa ni shabiki wa kutupwa, tena yule kindakindaki. Akachagua magazeti yake kadhaa ya michezo anayoyataka akalipia kwa kutoa noti ya Sh.10,000/=. Akawa anasubiria chenji yake toka kwa muuzaji aliyekwenda kuitafuta chenji hiyo. Kama ujuavyo masikio hayana pazia, ndipo akasikia mazungumzo toka kijiweni kwa fundi viatu jirani na muuza magazeti.
Mazungumzo ambayo kwake aliyatilia umuhimu mkubwa sana kutokana na yanayozungumzwa kuvuta hisia zake. Walikuwa wanajadili tukio la mlipuko wa mabomu siku ya Ijumaa iliyopita. "Ebana eeeh....., kifo kinatisha sana, jamani yule mwehu "Maso Maso" anayependaga sana kukaaga pembeni ya kiduka cha Bwana Soni nae alitimka mbio, baada ya kishindo kile sikumuona tena" alisema mmoja wa wana kijiwe hapo huku akionyesha kusikitishwa na tukio hilo.
"Na tokea mlipuko ule hajakanyaga tena eneo hili, labda atafuata furushi lake analoliachaga hapo kwa Soni chini ya meza yake, usicheze na kifo wewe mpaka mwehu anakiogopa". Maongezi hayo ya mporoto yalisababisha mapigo ya moyo ya Kachero kwenda matiti. Tayari alishaanza kunusa harufu ya sehemu ya kuanzia upelelezi wake. Alipotupa macho yake pembeni ya hicho kiduka jirani na aliposimama akaona kweli kuna furushi linalozungumziwa lipo ndani ya eneo la mmiliki, ila duka limefungwa.
ITAENDELEA
 
RIWAYA: MSAKO WA MWEHU
SEHEMU YA SABA

SURA YA TANO
"Kachero Yasmine anawasoma kinagaubaga Al-shabaab"
Usiku wa siku ya Jumatatu kuamkia Jumanne Kachero Yasmine akiwa tayari ameshatia nanga Jijini Dodoma, alikesha kusoma lundo la nyaraka na vitabu mbalimbali vitakavyomsaidia kwenye jukumu lake la kuwatia mbaroni magaidi waliohusika na milipuko. Alibeba nyaraka za siri toka 'C.I.A" na "F.B.I" zinazoelezea kundi la Al-shabaab kiundani.
Humo akadurusu kuwa "Al-shabaab" ni kifupi cha neno la kiarabu "Harakat ash-Shabāb al-Mujāhidīn" kifupisho "HSM"; kwa Kisomali, inatamkwa "Xarakada Mujaahidiinta Alshabaab" maana yake kwa Kiswahili ni "Tapo la Vijana wa Jihad". Ni kundi la waislamu wenye itikadi kali lililoanzishwa nchini Somalia mwaka 2006 kutoka kwenye kundi la Muungano wa Umoja wa Mahakama za Kiislamu "Islamic Courts Union" (ICU).
Mara baada ya kupinduliwa kwa Rais wa Somalia dikteta Mohammed Siad Barre, mwaka 1991, dikteta ambaye aliyedumu madarakani kwa muda wa miaka 22, Somalia ikaingia kwenye mzozo wa vita vya wenyewe kwa wenyewe.
Katika mapigano hayo ya wenyewe kwa wenyewe kikundi cha Muungano wa Umoja wa Mahakama za Kiislamu "ICU" kikafanikiwa kujipachika madarakani nchini Somalia tarehe 6/06/2006 na kuleta utulivu ya muda mfupi nchini Somalia. Utawala huo wa "ICU" haukudumu madarakani kwa zaidi ya miezi 6. Ilipofika tarehe 27/12/2006 wakafurushwa madarakani. Ulipoangushwa utawala huo wa Kundi la Muungano wa Mahakama za Kiislamu ndipo "Al-shabaab" wakaibuka kwa kasi wakijimegua kutoka kwenye kundi la "ICU" wakiongozwa na muasisi wao Bwana Ahmed Godane.
Mwaka 2012 kundi hilo lilijiunga na kundi kubwa la kigaidi la Al-Qaeda ili kuimarisha nguvu zake. Mpaka kufikia mwaka 2014, Wanamgambo wa Al-Shabaab walikadiriwa kuwa 7,000 - 9,000, wakiwemo wageni wengi, hasa kutoka Yemen, Sudan, Kenya, Tanzania, Afghanistan, Saudi Arabia, Malaysia, Pakistan na Bangladesh wote wakidai kuwa na lengo la kuigeuza Somalia kuwa nchi ya Kiislamu itakayoongozwa kwa sheria za Allah na sio za kutungwa na binadamu kwenye Bunge.
Alivyomaliza kujisomea taarifa za "Al-shabaab" akaanza kuandaa dhana na kuzitafutia majibu mepesi mepesi ili kuzipanua fikra zake katika uwanda mpana. Akatengeneza dhana ya kwanza "Kitu gani haswa kinamfanya kijana ajiunge na makundi hatari ya kigaidi?".
Akajipa majibu yeye mwenyewe, kuwa huenda ni sababu za kiuchumi, anashawishika kwa ndururu za kujikimu mahitaji yake kama kijana hasa ukichukulia kuna changamoto kubwa ya ukosefu wa ajira Afrika na duniani kwa ujumla. Wapo wanojiunga kwa sababu za kidini, wamepata mafundisho potovu yanayowahimiza wakubali kufa kwa ajili ya kutetea dini yao. Wapo pia wanaojiunga kwa kuchukizwa na vitendo vya kikatili wanavyofanyiwa watu wanyonge akina mama na watoto, huku mashirika ya haki za binadamu wamefungwa midomo kupaza sauti zao. Mfano mabomu yanayotupwa na jeshi la Marekani kule Syria, Afghanistan, Iraq na kwingineko duniani yanasababisha kuzalisha kizazi cha magaidi wenye lengo la kulipiza kisasi.
Na wapo wanaoingia kwa kulazimishwa kwa nguvu, wanakuwa hawana jinsi ya kukataa. Kwenye maeneo ambayo magaidi wamesimika utawala wao kila kijana anawajibishwa kujiunga na jeshi. Akaanza kutengeneza dhana mbalimbali za namna ya kuzuia ugaidi. Waswahili wanasema kinga ni bora kuliko tiba, hivyo ni vizuri ikaandaliwa mipango mkakati ya kuziba mianya ya ugaidi.
Kwanza watawala waumize vichwa kubuni miradi itakayozalisha ajira kwa vijana. Pia taasisi za dini na majumba ya ibada yote lazima yasajiliwe na viongozi wake pia watambulike kisheria na wafuatiliwe nini wanachokifundisha kwa wafuasi wao.
Baada ya kumaliza tafakuri yake, Kachero Yasmine akajisomea vitabu mbalimbali vya lugha ya kiarabu na kisomali vinavyowachambua vizuri sana "Al-shabaab". Akajikuta amepata mbinu mujarabu ya kuwatia mbaroni Al-shabaab kiulaini sana. "Hawa punda wa-al-shabaab kasoro mkia hawachomoki kwa mbinu hii ninayoiandaa kwao" aliwaza Kachero Yasmine huku akijiamini kwa kazi yake, huku akifunga makabrasha yake.

"Kigogo wa Polisi anayetumia PT3001 ni mshukiwa wa Ugaidi"
Kachero Manu alipotoka Mwananyamala Kisiwani alikanyaga mafuta kisawasawa kuendesha gari yake kuharakia mlo wa mchana maeneo ya Ferry, Kigamboni kwa Mama Nitilie maarufu kwa jina la Bi. Mwajuma, anayesifika kwa ujuzi wa mapishi na upimaji wake ni shazi la chakula cha kushiba.
Huyu Bi Mwajuma inasemekana kuwa wali wake akikupikia ulikuwa unakolea nazi vilivyo. Wateja wake walikuwa wanamtania kuwa "kwenye mchele kilo moja anatia nazi saba". Bi. Mwajuma alikuwa anamjulia mteja wake Kachero Manu chakula gani anachokipenda. "Mwanangu leo wali mchafu au mweupe, karibu sana" aliuliza Bi Mwajuma kwa uso wa bashasha mujarabu akimaanisha anataka kula pilau au wali mweupe. "Shusha wa kushiba mweupe kwa mchuzi wa samaki na mandondo ya nazi tafadhali".
Alipoletewa tu akaanza kukisokota chakula kutokana na njaa kali iliyomshika. Akala fyuu kisha akashushia na maji baridi ya kwenye mtungi, akalipa pesa Sh. 2,500/= tu, akaaga kwa ajili ya kurudi ofisini kuendelea na harakati za ujenzi wa taifa.
Alipofika ofisini akaandaa ripoti fupi ya alipofikia kwenye upelelezi wake mpaka sasa na anachotarajia kukifanya kukamilisha kazi yake. Akazama kwenye dimbwi la uandishi wa taarifa zake. Kisha baada ya hapo akaamua kutuma taarifa ya maombi rasmi ya picha na video za picha za CCTV-Kamera kutoka majengo ya jirani na Wizara ya Mambo ya Ndani iliyolipuliwa. Alituma maombi katika jengo la Tume ya Katiba ile ya Warioba, pia na jengo linalotumiwa na Tume ya Uchaguzi na pembeni yake kuna jengo la yalipo makao makuu ya "Exim Bank".
Kuja kuangalia saa yake ya mkononi baada ya kumaliza kazi zake zote, muda ukawa unasoma ni saa kumi na mbili kasorobo ikabidi akurupuke mbio mbio kushuka chini ili aelekee mtaa wa Ghana jirani na yalipo Makao Makuu ya Wizara ya Mambo ya Ndani.
Akaamua aache gari yake atembee tu kwa miguu kwa kupenya katikati ya majengo ya ofisi za Posta Mpya. Ilimchukua takribani dakika 10 tu kufika mpaka dukani kwa Soni, alipokaribia zaidi akatoa miwani yake yenye uwezo wa kurekodi matukio kwa njia ya video na sauti kwa muda usiozidi saa mbili.
Kwa bahati ile anafika tu ndio anamuona Soni anafungua geti la mbele la chuma la kiduka chake. "Mr.Soni habari yako, pole sana na matatizo ya msiba" aliwahi kusalimiwa na Kachero Manu. "Ahsante kaka yangu tumeshapoa tumezika salama, nashukuru". Alijibu Soni, huku anaharakisha kufungua walau apate riziki yake aliyopangiwa na Mola wake kwa jioni hiyo.
"Samahani, nataka nifanye mahojiano mafupi sana na wewe nikiwa kama Afisa Usalama" alijitambulisha Kachero Manu huku akivaa uso wa kazi. Soni alivyosikia ule utambulisho akaanza kutetema mpaka za funguo za geti zikamdondoka chini. Kachero Manu akamuokotea huku anatabasamu akamkabidhi kisha akamshika bega lake.
"Ondoa hofu, ni maswali ya kawaida tu kuhusiana na kadhia iliyotokea Ijumaa iliyopita" alimtoa wasiwasi ili apate ushirikiano. "Naogopa nimeshikwa na fadhaa unajua rafiki zangu hapa nimefika tu sasa hivi wananipa taarifa kuwa kuna kigogo mmoja wa polisi ananitafuta kwa udi na uvumba, wanasema anakuja mpaka hapa anaangalia kibanda changu kisha anaondoka kana kwamba ananitaka mimi" alijibu Soni huku uso wake ukinywea kwa uoga mkubwa uliomtawala.
"Yeah labda mpelelezi mwenzangu, je wanamfahamu kwa sura?" alizuga wanafahamiana na huyo kigogo wa polisi ili kumuondolea hofu Soni. "Walivyonielekeza hata mimi namfahamu sana wajihi wake, lakini gari anayoitumia leo ni gari binafsi hamna anayeifahamu, gari yake ya kazini anayotembelea ni rangi buluu 'v8' namba zake za gari ni PT 3001" alielekeza kwa ufasaha.
Wakazunguka nyuma ya kibanda kwenye maboksi na uchafu wa dukani na kilipo kifurushi cha mwehu "Maso Maso". Kachero Manu akakalia kiti cha mbao kichakavu huku Soni akikalia juu ya dumu tupu, lenye rangi ya manjano la lita 20 la mafuta ya kula. Mahojiano yakaanza kama ifuatavyo;
Kachero Manu: "Unamfahamu vipi Maso Maso?"
Soni: "Kumfahamu kivipi ningeomba ufafanuzi "
Kachero Manu: "Hivyo hivyo unavyomjua" alijibu Kachero Manu kwa sauti yenye hasira ila hakutaka kujijulisha.
Soni: "Maso Maso", ni mwehu ambaye amezoea kukaa hapa dukani kwangu, pembeni hapo ulipokaa ndio kikazi chake. Iwe mvua iwe jua hapo ndio maskani yake, wanasema watu kapigwa kipapai"
Kachero Manu: "Ana muda gani tokea awe anakita kambi dukani kwako hapa?"
Soni:"Sikumbuki vizuri sana ila haizidi miezi sita"
Kachero Manu: "Kuna vitu labda alikuwa anaongea ongea na wewe? "
Soni: "Hapana, mara nyingi alikuwa anautumia kuimbaimba nyimbo zake na kuandika andika kwenye kidaftari chake, mara chache ndio alikuwa anaongea lakini maongezi yasiyo na mtiririko maalumu ya kiwehuwehu"
Kachero Manu: "Unaweza kunionyesha hilo furushi lake nione hicho anachokiandika!". Soni akajibu swali kwa vitendo kwa kwenda kubeba fuko lenye vitu vya chizi "Maso Maso" akalibwaga mbele ya Kachero Manu. Kachero Manu akasitisha mahojiano kwa muda akaanza kazi ya kuchakurachakura kwenye lile fuko la mwehu. "Kweli hili fuko la chizi, mpaka chupa za mikojo zimo! " alijisemea kimoyomoyo Kachero Manu. Kulikuwa na vikorokoro vya simu mbovu, taa mbovu za kuchaji za Mchina, karatasi zilizochanika za aya za Qu'ran, viwembe vilivyotumika, mabakuli na vikombe na kila aina ya takataka zinazostahili kuwemo kwenye furushi la chizi.
Alipokuwa anakaribia kukata tamaa akashika kitu kigumu,

MAMBO MOTO KACHERO KASHIKA KITU KIGUMU KWENYE FURUSHI LA MWEHU.....

ITAENDELEA
 
RIWAYA: MSAKO WA MWEHU

SEHEMU YA NANE

Wakazunguka nyuma ya kibanda kwenye maboksi na uchafu wa dukani na kilipo kifurushi cha mwehu "Maso Maso". Kachero Manu akakalia kiti cha mbao kichakavu huku Soni akikalia juu ya dumu tupu, lenye rangi ya manjano la lita 20 la mafuta ya kula. Mahojiano yakaanza kama ifuatavyo;
Kachero Manu: "Unamfahamu vipi Maso Maso?"
Soni: "Kumfahamu kivipi ningeomba ufafanuzi "
Kachero Manu: "Hivyo hivyo unavyomjua" alijibu Kachero Manu kwa sauti yenye hasira ila hakutaka kujijulisha.
Soni: "Maso Maso", ni mwehu ambaye amezoea kukaa hapa dukani kwangu, pembeni hapo ulipokaa ndio kikazi chake. Iwe mvua iwe jua hapo ndio maskani yake, wanasema watu kapigwa kipapai"
Kachero Manu: "Ana muda gani tokea awe anakita kambi dukani kwako hapa?"
Soni:"Sikumbuki vizuri sana ila haizidi miezi sita"
Kachero Manu: "Kuna vitu labda alikuwa anaongea ongea na wewe? "
Soni: "Hapana, mara nyingi alikuwa anautumia kuimbaimba nyimbo zake na kuandika andika kwenye kidaftari chake, mara chache ndio alikuwa anaongea lakini maongezi yasiyo na mtiririko maalumu ya kiwehuwehu"
Kachero Manu: "Unaweza kunionyesha hilo furushi lake nione hicho anachokiandika!". Soni akajibu swali kwa vitendo kwa kwenda kubeba fuko lenye vitu vya chizi "Maso Maso" akalibwaga mbele ya Kachero Manu. Kachero Manu akasitisha mahojiano kwa muda akaanza kazi ya kuchakurachakura kwenye lile fuko la mwehu. "Kweli hili fuko la chizi, mpaka chupa za mikojo zimo! " alijisemea kimoyomoyo Kachero Manu. Kulikuwa na vikorokoro vya simu mbovu, taa mbovu za kuchaji za Mchina, karatasi zilizochanika za aya za Qu'ran, viwembe vilivyotumika, mabakuli na vikombe na kila aina ya takataka zinazostahili kuwemo kwenye furushi la chizi.
Alipokuwa anakaribia kukata tamaa akashika kitu kigumu, alipokivuta akakuta ni daftari. Akashikwa na tashiwishi ya kulifungua na kujua kilichoandikwa. Ikadondoka kikaratasi chakavu cha maandishi ya Kiarabu, akakihifadhi sehemu salama. Kisha alipozidi kulifungua daftari hakuona chochote cha kumsaidia zaidi ya namba za simu kochokocho.
Kachero Manu: "Je siku ya mlipuko, Maso Maso alikuwepo au hakufika kabisa?". Akaendeleza mahojiano yake baada ya kulifunga furushi vizuri.
Soni: "Ndio alikuwepo alikaa hapo hapo, ila siku hiyo alikuwa kama mgonjwa hakuwa mchangamfu na hakula chochote tokea asubuhi, ulipotokea ule mlipuko, taharuki iliyokuwepo siku hiyo kila mtu aliingilia upande wake, na hajaonekana tena eneo hili mpaka tuna wasiwasi kama amesalimika na kifo"
Kachero Manu: "Ahsante sana kwa ushirikiano wako, nikikuhitaji tena nitakuja na samahani kwa kukuchelewesha na biashara yako"
Soni: "Hamna shida karibu tena, ngoja nifungue duka langu sitaki kula mate " aliongea kwa sauti ya hasira huku uso wake umebeba mawimbi ya ndita kuonyesha kuchukizwa kwa kuhojiwa muda wa biashara. Kachero Manu hakujali akaondoka zake huku akiwa amechukua kila kiratasi na kile kidaftari cha "Maso Maso" huku akishukuru kwa kupata majibu yaliyomkifu kifaya.
Muda sasa ulikuwa umeenda harijojo, ilikuwa imeshafika saa moja kasorobo magharibi. Akapitiliza moja kwa moja mpaka kwenye geti la Wizara ya Mambo ya Ndani kwenda kukagua namba za hiyo gari v8 PT3001 aliyotajiwa na Soni kuwa kigogo anayeitumia hiyo gari anamsaka .
Kachero Manu alikuwa tayari kasharuhusiwa na walinzi wa eneo hilo kufanya ukaguzi wake wa gari anayoitafuta. Alikuta v8 zaidi ya 18 rangi ya buluu zimejipanga. Hayo yote yalikuwa ni magari yanayotumiwa na Vigogo wa Wizara na Polisi Makao Makuu. Akaanza kufanya spenkesheni yake kwenye yale magari. Alirudia zaidi ya mara tatu halikuona lile gari alilotajiwa jina namba zake na Soni, PT3001.
Kijasho chembamba kikaanza kumvuja mpaka kwenye meno. Uso wake ukala debe akaanza kukata tamaa ya kuikosa gari hiyo. Akaamua awashe na mwangaza wa tochi ya simu yake ya mkononi kusaidia mwangaza wa eneo lile. Alipofika kwenye gari lenye namba 'PT1003' akasimama kwa muda akiikagua. "Namba hili zinafanana na zilizotajwa PT3001 tofauti ni mpangilio wa namba tu, labda zinachezewa" aliwaza Kachero Manu.
Akaanza kuchezea kile kibao namba za gari, akakikuta kibao kimeungwaungwa kiufundi mkubwa huwezi kugundua kwa haraka. Katika kupekenyua akakuta kuna nyaya zimepita kwenye namba tatu na moja. "Shabaaaashiii......kuna mchezo mchafu unafanyika, inaelekea gari ikitoka geti kuna kitufe kinabinywa kuzichezea namba za mwishoni zinapishana ndio maana mtaani linasoma PT3001, lakini humu ndani linasoma PT1003, kwisha kazi ujanja wake upo uchi" alijisemeza yeye mwenyewe.
Haraka haraka akawa anarudi pale getini kuulizia jina la kigogo anayetumia lile gari lenye namba za utata.
Alipofika wakati anaandikiwa jina la kigogo anayeitumia hiyo gari, tahamaki mtaani karibia na getini ikasikika milio ya risasi mbili zilizopigwa mtawalia, na kufuatiwa na risasi moja iliyobutuliwa juu, halafu ikasikika mseleleko mkali wa gari lenye kwenda kwa mchepuo wa kasi. Akajua mambo yameshaenda segemnege huko nje. Akafanya haraka kuchukua ile karatasi aliyopewa na kukimbilia nje ya geti huku mkononi tayari kachomoa bastola yake.

"Muuza duka Soni ameuliwa kinyama kibandani kwake"
Mamia ya watu walikuwa wamekusanyika karibia na kiduka cha Soni, huku giza lilikuwa tayari limeanza kushitadi angani katika usiku huo mbichi. Kila mmoja akijiuliza kulikoni mpaka muuza duka Soni ameuliwa kikatili namna ile. Hali ya hewa ilishachafuka kifo cha Soni kilizua tenge tahanani eneo hilo jirani na Wizara ya Mambo ya Ndani.
Maiti ya Soni ilikuwa imelala chali, damu zinamtiririka huku matundu ya risasi yakionekana dhahiri shahiri kwenye paji lake la uso na shingoni.
"Mie nimeshuhudia kila hatua ya tukio hili, walikuja watu wawili kwenye gari rangi ya kijivu aina ya "Brevis", mtu mmoja mrefu amevaa koti la kujikinga na mvua na kofia akashuka akaenda mubashara kwenye kiduka. Sikumfuatilia nikajua ni mteja wake tu anahitaji vitu vya dukani. Baadae nikaona kama kuna furushi kalibeba tokea kule anakohifadhia marehemu Soni takataka zake akalirusha ndani ya gari. Nae akaingia ndani ya gari kwa kuharakisha, lakini hawakuliondoa gari. Halafu baada ya kupita kitambo kama cha dakika 10 akashuka mmoja akakaribia tena kama meta 3 akanyanyua bastola yake na kumfyatulia risasi mbili za kichwani, ikabidi nijifiche nyuma ya kabati la fundi viatu jirani pale. Mpigaji akakimbilia kwenye gari kwa haraka. Alivyoona tumeanza kujikusanya wakadhani tunataka kuwapiga kipopo, mmoja wao akapiga risasi moja hewani, kisha wakatimka na gari lao wakala matu kwa umahiri mkubwa. Wakaingilia hiyo barabara ya mtaa wa Ohio na gari lao na kutokomea kusikojulikana" alielezea tukio hilo kwa ufasaha mkubwa mmoja wa mashuhuda wa tukio hilo.
Kachero Manu alivyoona umati wa watu umejikusanya akaamua kuirudisha silaha yake kwenye ala yake, akasogea karibu na eneo la tukio. Alikuwa ni mmoja wa wale waliosikiliza kwa umakini kabisa maelezo ya yule shuhuda. Baada ya hapo akaisogelea maiti ya Soni, akaona tayari kashaaga dunia, ameshaelekea jongomeo zamani.
Akajiona ni mtu mwenye bahati ya mtende kuwahi kuzungumza nae Soni muda mchache kabla hajapoteza maisha yake na kupata maelezo yaliyompa mwangaza wa upelelezi wake. Akatumia fursa ya watu kushuhudia mwili wa marehemu kuzunguka kule nyuma ya kiduka kwenye matakataka kuangalia kama furushi la chizi "Maso Maso" lipo au ndio limebebwa na wauaji!. Alipopiga jicho, akaona hamna kitu limepotea. "Kumbe furushi la mwehu, ni dili kama dhahabu linasakwa kwa udi na uvumba" alijiwazia peke yake Kachero Manu huku anatabasamu. Alishaanza kuunganisha matukio mbalimbali yatakayofanikisha upelelezi wake na hatimaye kuwatia mbaroni wahusika wa matukio ya ugaidi uliotekelezwa kwenye jengo la Wizara ya Mambo ya Ndani, Ijumaa iliyopita.
Askari kanzu wakawa wameshafika na kuanza kutawanya watu huku wakizungushia uzio eneo la tukio. Kachero Manu akaona isiwe tabu akaanza kuondoka mdogo mdogo kwa miguu kurejea ofisini, kufungasha vitu vyake arejee nyumbani kwake, tayari kwa safari ya Dodoma kesho kutwa yake.
Alipanga kwenda kumuongezea nguvu Kachero Yasmine. Lakini tukio la kuuliwa kwa kijana Soni kulimpa msongo wa mawazo wa kutaka kufahamu "je kuna uhusiano kati ya mauaji ya Soni na msako wa walipuaji wa jengo la Wizara? "

ITAENDELEA
KUPATA HARDCOPY NICHEKI
0625920847
 
RIWAYA: MSAKO WA MWEHU

SEHEMU YA TISA

SURA YA SITA
Kachero Manu uso na uso na Kigogo wa Polisi anayetumia gari PT3001
Siku ya Jumatano saa 12:00 asubuhi na mapema, kibaridi cha asubuhi kinapuliza, Kachero Manu alikuwa yupo ndani ya ndege ya shirika la ATCL aina ya Bombadia akielekea Jijini Dodoma. Alikuwa anahudhuria taazia ya marehemu waliokufa kwa mabomu yaliyolipuka katika jengo la Wizara ya Mambo ya Ndani, Ijumaa iliyopita. Alikuwa ametinga usoni miwani yake nyeusi na suti ya rangi buluu bahari, huku chini akiwa amevalia viatu vyake vyeusi. Muda wote wa safari alijifanya ametingwa na kusoma magazeti lako ila ilikuwa zuga tu.
Kila wakati alikuwa anamkodolea macho kwa kuibia, mbaya wake kigogo wa gari tata v8 PT1003 analohisi ndio mhusika wa mauaji ya Soni. Anamshuku kuwa anahusika kwa sababu ndio mtu wa mwisho kumtafuta Soni kutwa nzima na magharibi yake tu kijana wa watu akauliwa.
Yule Afisa alionekana ni mtu mwenye wasiwasi kama koo la kuku anayetaka kutaga. Uso ulionyesha kuwa ni mtu ambaye kichwani mwake ana mlima mzito wa mawazo ameubeba. Waliposhuka tu kwenye ndege, Kachero Yasmine alishakuja tayari uwanja wa ndege kumlaki Bosi wake. "Habari za asubuhi Bosi wangu, pole na safari... " zilikuwa ni salamu za Kachero Yasmine kwa Kachero Manu. "Fuata gari lile haraka sana" badala ya kujibu salamu, Kachero Manu akawa anatoa maagizo kwa mwenzake ya kumfuatilia kigogo huyo wa polisi. Kachero Yasmine akatekeleza amri ile kwa vitendo kwa kuitoa gari yake kwa haraka akiifuta taksi iliyombeba kigogo yule.
Kachero Yasmine alimjua vizuri sana Bosi wake kuwa akiwa ametingwa na jambo kuongea kwake ni tabu hata kula yake ni kwa manati. Baada ya dakika chache wakawa wapo nyuma yake mara walipotoka tu nje ya geti la uwanja wa ndege. Taksi ile iliyokuwa inafuatwa na Kachero Yasmine ilikuwa inaelekea barabara ya Arusha kama inaelekea njia ya ilipo kambi ya jeshi ya JKT-Makutupora.
"Inaonyesha anaenda Hoteli ya nje ya Jiji nadhani" alivunja ukimya Kachero Yasmine kwa kumzungumzisha Kachero Manu huku amemtupia jicho akitegemea kumsikia Bosi wake akitia neno. "Nadhani anatafuta eneo lenye utulivu " alijibu Kachero Manu kimkato. Ghafla gari wanayoifuatilia ikawasha indiketa ya taa ya kulia kuonyesha anaingia Simba Hoteli.
Ilikuwa ni Hoteli nzuri na tulivu iliyopendezeshwa kwa marumaru nyeupe kwa nje. Pia kulikuwa na bango kubwa kwa nje limeandikwa Simba Hoteli huku kukiwa na picha ya mnyama simba. "Sasa mie niache na huyu mjuba bado kuna vitu navihitaji kutoka kwake kabla sijamkamata, wewe endelea na yako" alisema Kachero Manu. "Sawa usisahau kunipa mzigo toka furushi la mwehu uliloniahidi toka juzi kuniletea" alijibu Kachero Yasmine na kukumbushia akabidhiwe karatasi iliyochukuliwa kutoka kwenye zigo la "Maso Maso".
"Hii hapa tena nashukuru kwa kunikumbusha, nilishasahau" alijibu Kachero Manu, huku mkononi amekamatia bahasha ya rangi ya kaki akimkabidhi. Kachero Yasmine hakuwa na simile pale pale akaipokea na akaitatua bahasha ile ya kaki na kukutana kikaratasi kidogo kichakavu kina maandishi ya lugha ya kiarabu. Akaanza kukisoma kiratasi hicho chenye maandishi yafuatayo ;
امتي قد لاح فجر فارقبي النصر المبين"
دولة الاسلام قامت بدماء الصادقين
دولة الاسلام قامت بجهاد المثقين
قدموا الاواح حقا بثبات ويقين
ليقام الدين فيها شرع رب
أحب الحور العين
Baada ya kumaliza kusoma Kachero Yasmine, akatabasamu, uso wake ukala mbwende kisha akamuangalia Kachero Manu ambaye nae alikuwa amemkodolea macho kwa hamu kumsubiria Yasmine aseme chochote kitu nafsi yake ipate faraja.
"Malizana na huyo mjuba wako kigogo wa Polisi anayekula kivuli cha Jeshi la Polisi, tuanze kumsaka huyu mwehu Maso Maso ana mengi sana ya kutueleza, ushahidi wa kimazingira umeanza kumfunga kuwa anahusika na mlipuko uliotokea Wizarani". Kachero Manu akajenga tabasamu la furaha usoni mwake akashuka haraka na kuagana nae, kisha akafanya haraka kuingia ndani ya hoteli na moja kwa moja akaelekea mapokezi.
"Karibu sana mgeni wetu, malazi yapo tumebakiwa na "single room" na "mini deluxe room" tu" alikaribishwa Kachero Manu kwa unyenyekevu mkubwa na mhudumu kisura wa mapokezi katika hoteli ile. "Ahsante sana, naomba nivione baadhi ya hivyo "Mini Deluxe Room" nione ubora wake" akajieleza Kachero Manu. "Usiwe na mashaka kabisa ubora wake ni wa kutukuka, vigogo wengi wa serikali hapa ndio nyumbani kwao, na hivi tunavyoongea na wewe kimebaki kimoja tu, chumba kingine kimechukuliwa na mteja ameingia sasa hivi punde tu" alijifaragua kwa maringo yule dada wa mapokezi.
"Any way no problem, nipe hiko chumba kilichobakia nisije kukosa mwana na maji ya moto" alisema Kachero Manu huku akiombea wawe jirani na huyo mgeni, hasimu yake. Akapewa daftari la wageni la kujaza taarifa zake. Akalifungua na kuanza kujaza taarifa zake lakini akawa anajaza huku anatabasamu pana sana. "Ushindi unanukia kiulaini kabisa" alijiwazia moyoni. Alichokuwa anafurahi ni kuona huyu kigogo huyo, Inspekta Haroub Farouq kaweka moja ya namba ya simu iliyopatikana kwenye daftari la kichaa "Maso Maso". "Inaonekana hii ni namba walikuwa wanapigiana wakiwa na mawasiliano ya faragha" aliwaza Kachero Manu.
Kwenye lile daftari la "Maso Maso" kulikuwa na namba zaidi ya 20 ambazo Kachero Manu zote alizihifadhi kichwani na kuweza kuziimba kwa kichwa. Na zote namba hizo walipofuatilia TCRA zilionekana zimefungwa hazitumiki. "Inaonyesha wana mtandao mpana mpaka kwenye kampuni za simu, wakitaka kuongea siri zao wanazifungulia kwa muda kisha zinafungwa na kufutwa mazungumzo ya siri yaliyorekodiwa" aliendelea kuwaza Kachero Manu.
Alipomaliza kujaza taarifa akasindikizwa na mhudumu yule mpaka chumbani kwake akiwa amesaidiwa kubebewa brifkesi yake ndogo nyeusi. Walipofika tu chumba namba 10B, wakamuona Inspekta Haroub Farouq anatoka kwenye chumba kinachotazama namba 10A huku akiwa amevalia sare zake za jeshi la polisi zikiwa zimechafuka vyeo mabegani mwake kama uchafu vile.
"Dada hiki chumba sitaki watu wa usafi au mtu yoyote aingie mpaka siku nitakapoondoka pia funguo nitakuwa nazo mwenyewe" alisema yule kigogo wa polisi ikiwa ni amri na sio ombi huku anatokomea zake kwenye korido za hoteli ile kutoka zake nje, huku akitembea kwa mwendo mzofafa kwa kiburi cha cheo chake kikubwa. "Huyu mteja wenu anaonekana mtata sana eeeh" alichokonoa Kachero Manu, akibahatisha huenda akaambulia chochote anachokijua huyu dada juu ya Inspekta Haroub Farouq.
"Simfahamu kwa kweli maana mie ni mgeni hapa kazini, kesho kutwa ndio natimiza mwezi kamili anajitia hanjamu mwenyewe wala hanipi presha mie " alijibu yule dada kwa nyodo huku analiweka brifkesi la Kachero juu ya meza, akaaga na kuondoka zake. Kachero Manu akazuga kama anajifungia chumbani kwake yule binti mhudumu ilivyopotea tu michakato ya nyayo zake masikioni mwa Kachero Manu, akafungua mlango wake na kutoka nje ya chumba chake.
Akatoa mfukoni mwake kibati kidogo mithili ya ATM-kadi ya benki akasogelea chumba alichotoka kigogo yule, akabonyeza namba za mlango wa chumba kile akakiingiza kibati kile mlango ukajimanua wenyewe bila kokoro zozote. Akaingia haraka na kuufunga tena kama iliyofungwa. Alivyoingia chumbani kwa Inspekta Haroub bila kupoteza muda akaenda moja kwa moja kwenye kabati la ukutani la chumbani kwa bahati lilikuwa limeegeshwa tu. Akavuta mlango wake ukafunguka, lilikuwa ni kabati lenye nafasi ya kutosha kukiwa na chemba nne, juu kulia na kushoto mbili na chini hivyo hivyo. Chemba za juu zinajitegemea mlango wake mmoja na chemba za chini nazo zinajitegemea mlango wake. Chemba ya chini kushoto alikuta ndipo alipohifadhi begi lake kubwa la nguo. Hakukuta zaidi ya begi hilo. Akarudi mezani alipoangalia chini ya meza akakuta kuna mkoba wa rangi nyeusi umetunatuna umefungwa kwa zipu tu. Akautoa chini na kuufungua, akakuta kuna makaratasi mengi mengi, ila akavutiwa na mafaili madogo mawili yaliyohifadhi nyaraka kimpangilio. Akaanza kuzipiga picha kwa kutumia simu yake ya kisasa zile nyaraka ambazo kwa haraka haraka aliziona zitamsaidia kwenye kazi yake.
Lilikuwa ni zoezi lisilozidi dakika 5 tu, akawa ameshamaliza kupiga picha. Wakati anafunga na kujiandaa kuelekea kwenye kabati afungue begi akasikia sauti ya mitembeo ya viatu vya kipolisi inakaribia kuishia mule chumbani alipo. Haraka haraka akafunga mkoba vizuri na kuurudisha mahali pake kisha akakimbilia kwenye kabati akafungua chemba ya upande wa kulia na kujificha kisha akairudishia.
Hisia zake zilimtuma sahihi kwa zaidi ya asilimia 100%. kuwa Inspekta Haroub Farouq alikuwa amerejea tena chumbani mwake ghafla huku anaongea kwa simu kwa sauti ya jahara, inayosikika wazi kabisa.
ITAENDELEA
 
RIWAYA: MSAKO WA MWEHU
SEHEMU YA KUMI NA MOJA

Mara moja Kachero Manu akatoa maagizo kwa Afisa Usalama wa Taifa wa Mkoa wa Dodoma awatafutie sehemu salama Wabunge wote wanaokuja kwenye hitimisho la maombolezo, kwenye nyumba maalumu za Usalama wa Taifa 'Safe House' na wapewe ulinzi mkali. Kisha wakaanza kupanga mipango sasa wa kuwatia mbaroni kwa pamoja usiku wa leo Inspekta Haroub Farouq na mwehu "Maso Maso" watakapokuwa pamoja chumbani.
Walipomaliza mipango yao tayari, wakaelekea mgahawani hapo hapo hotelini kupata mlo wa mchana wa nguvu kisha wapumzike. Wakati wapo mgahawani kwenye simu yake Kachero Manu ikaonyesha alama ya kutumiwa barua pepe. Alipoifungua na kuisoma akakuta Katibu Muhtasi wao Kokunawa kamtumia picha na video za CCTV-Kamera za majengo jirani na sehemu kulipotokea mlipuko walizohitaji. Wakarudi tena chumbani kwa mara ya pili kuanza kuzichambua picha kwa umakini. Wakawa wanaona namna "Maso Maso" anavyoingia na kutoka kama chumbani kwake katika jengo la Wizara ya Mambo ya Ndani utasema ni chooni kwake. Wakayakinisha asilimia 100% kuwa "Maso Maso" alikuwa hakauki ndani ya jengo la Wizara kipindi chote cha kabla ya milipuko ya kigaidi.
Wakaamua wajipumzishe, kwa ajili ya kuirudishia miili yao nishati yake asilia. Kachero Yasmine akatandika mito chini ya zulia la chumbani mule mwa Kachero Manu, akiwa anajiandaa kujipumzisha. Kachero Manu akiwa amebaki kitandani peke yake akamchombezea utani kachero Yasmine, "Ndio tatizo la kufanya kazi na watoto wa Mashekhe kutwa wao mawazo yao kuogopa kuoga janaba tu, unajitesa bure kulala chini wakati kitanda kikubwa hiki ni futi 6*8, uje hapa kitandani tulale mzungu wa nne".
"Ha ha ha ha...sumu haipimwi makali yake kwa ncha ya ulimi, safari moja huanzisha nyingine, usije kunitia vishawishini, na majaribuni nikashindwa kuhimili ukanitia dhambini ukanivunja kizinda changu bure nikakosa kuvikwa kisarawanda siku ya ndoa yangu kwa kupoteza usichana wangu kwa jitu la ajabu na katili kama wewe, ambaye anapata pesa za kutambia Mjini kwa kutoa roho za watu" alijibu Kachero Yasmine kwa utani. "Nawe kweli mtu wa Zenji Kijukuu cha Sultani bin Jerebi, sasa hiyo kisarawanda ndio nini maana yake, umenitoa kapa"?, aliuliza Kachero Manu.
"Ha... ha... ha...ndio shida ya kufanya kazi na Mmwera, watu wa tunumba tunumba sana na kujishebedua kama wanajua kumbe wanaungua jua tu, kisarawanda ni nguo nyeupe anayovikwa mwanamke bikira kiunoni siku ya ndoa yake anaposindikizwa kupelekwa kwa mumewe" alijibu Kachero Yasmine kwa uso wa bashasha huku akisubiria dongo maridhawa toka kwa mkuu wake wa kazi.
"Kwa hiyo unataka kuniambia umri huo huo ulionao wa miaka yako 28 bado unayo yenyewe au Mchina tu ha ha ha? unataka kumshughulisha mpenzi wako akupe tunu na tamasha usiyostahili! aliuliza Kachero Manu huku akiwa anatabasamu pana, swali ambalo halikupata jibu la moja kwa moja toka kwa Kachero Yasmine zaidi ya kicheko na kurushiwa mito kitandani alipokaa, kuonyesha hataki utani wake ule wa kuulizwa swali la uhalisia wa ubikira wake.
Kisha wote wakaendeleza utani wa hapa na pale mpaka wakapitiwa na usingizi mwepesi huku wanapulizwa na kiyoyozi chenye sentigredi 15. Miili yao ikipata nguvu mpya tayari kwa mshikemshike wa usiku wa kumtia mbaroni Inspekta Haroub na kichaa wake feki "Maso Maso The Duduman".

ITAENDELEA-USIKU SAA 3
 
MSAKO WA MWEHU
SEHEMU YA KUMI NA TATU

SURA YA NANE
Kisengerenyuma hadi 23/09/2014
Masoud Masoud alikuwa ndio anaripoti chuo kikuu cha "Stanford University" akiwa kama mwanafunzi wa kitivo cha Uhandisi wa Mitambo "Mechanical Engineering". Kukanyaga kwake Ulaya kwa Masoud Masoud akitokea mitaa ya uswahilini Sinza ilikuwa ni kama ndoto ya alinacha tena ya mchana wa saa sita, jua limesimama dede, alikuwa haamini kabisa.
Majumba ya kifahari, magari ya kisasa, mabasi ya mwendokasi na treni za umeme aliyokuwa anayashuhudia tu kwenye filamu na televisheni sasa alikuwa anayaona mubashara kwa mboni za macho yake. Wiki ya kwanza ya mwelekeo "Orientational Course", haikuwa na durusu za darasani. Ilikuwa ni wiki ya kufanya usajili wa chuo, kuonyeshwa benki ilipo ili kufungua akaunti, kuelekezwa maduka ya kununua bidhaa, na sehemu zote muhimu kwa mahitaji ya mwanadamu.
Ilipoanza wiki ya pili, ndio masomo yakaanza rasmi. Shule ilikuwa ngumu kama ilivyo kawaida ya shule ya uhandisi, haitopata kuwa rahisi hata siku moja mpaka dunia itakavyotoweka. Ndio maana wahandisi wanapenda sana watambulike kama Injinia fulani ili kujimwambafai kidogo kufidia machungu ya ugumu wa shule.
Masoud Masoud licha ya ugumu wa masomo alikuwa anaweza kwenda nayo sambamba, huku akiwagaragaza vibaya watoto wa kizungu. Baadhi ya wanafunzi wenzake wakampachika jina "Maso Square The Duduman" kuonyesha kukubali utabe wake katika masomo. Lakini baada ya masomo kwisha darasani alijikuta yupo mpweke kupitiliza hana sehemu ya kwenda, hana mtu wa kumtembelea wala kumjulia hali. Vyakula vya nyumbani kama ugali, wali wa nazi, mihogo ya kuchemsha, magimbi na mengineyo mengi akawa anayakosa. Akaanza kutamani kurejea nyumbani, Tanzania, Waingereza wanasema alipatwa na "Home Sickness".
Mwanachuo mwenzake aliyekuwa mkubwa kwake kiumri, kijana wa kutoka Sudani, kwa jina anaitwa Mudrah Mudriki, aliyekuwa anasomea Shahada ya Sheria. Ambaye ni chotara wa baba Msudani na mama Mzanzibari akatumia hiyo fursa ya upweke wa "Maso Square The Duduman" kumzoea kwa haraka sana, na akafanikiwa.
"Kwanza rafiki yangu Masoud tuanze kwa kuwekana wazi usione matreni ya umeme, ukaona majumba mazuri ukaona Mahoteli na Mikahawa mikubwa mikubwa au ukaona mabenki makubwa huku Ulaya ukadhani Waafrika kwa Wazungu wote wanaishi kwa raha. La hasha ni wachache sana, maisha ya Ulaya yamejaa msongo wa mawazo ambao siyo wa kawaida na kuna wakati hasa wageni wanaingia katika majaribu mbalimbali hata ya kutaka kujinyonga. Ndio maana kama umefuatilia vyombo vya habari jana Waziri Mkuu wa Uingereza kamchagua Waziri wa Upweke. Miongoni mwa malengo ya kuwekwa Wizara ya Upweke ni kukabiliana na upweke unaowakabili watu wazima, wale waliopoteza wapendwa wao, wale wasio na watu wa kuzungumza nao ama hata kugawana fikra na uzoefu" yalikuwa ni maneno ya nasaha ya Mudrah kwa rafiki yake Masoud ya kumfanya asijisikie mpweke. "Sawa nakuelewa rafiki yangu, lakini lakini kwanini sasa kule nyumbani Tanzania hata kwenu Sudani watu wanatamani kuzamia Ulaya kuja kutafuta maisha bora, wakati huku hamna starehe yoyote ya maisha?" aliuliza "Maso Square The Duduman" kwa rafiki yake aliyemsafishia nia na kumuamini.
"Tatizo nadhani ni lile lile tu la kuzuzuka na maroshani wanayoyaona yameota kama uyoga, na vitu vya anasa wanavyoviona. Laiti wangefahamu haya yanayotukuta, Balozi zao za nchi za Ulaya kule nyumbani Afrika wangefugia kuku kwa kukosa watu wanaokimbilia kuomba visa", alijibu kwa umakini Mudrah swali aliloulizwa na rafiki yake Masoud.
Kutokea hapo wakawa wapo kama mapacha, utasema ni "Sunche" na "Kapeto" unapomuona Mudrah ndio umemuona Maso, ukimuona Maso basi ndio umemdiriki Mudrah.
Kidogo kidogo "Maso Square The Duduman" akaanza kuizoea hali ya Uingereza. Wakawa sasa wapo bega kwa bega kila mahali, mambo yao wanayafanya kwa mkono mmoja, sio kwenye kuangalia mechi za kandanda ligi ya Uingereza, sio kwenda muziki, na kwenye kila aina ya starehe.
"Maso Square The Duduman" alimuona rafiki wa kweli ni Mudrah kwa sababu alijitoa wakati yupo kwenye taklifu ya kuyazoea maisha ya Ulaya. Wakawa kama kijibwa na mwanawe, lakini kwa kiasi kikubwa "Maso Maso" alikuwa ameshajenga utegemezi mkubwa kwa Mudrah, na hilo ndio jambo Mudrah alikuwa analitaka, na kulitamani litokee nalo likajipa.
Ikajitokeza ghafla tu Mudrah kakata mguu kwa rafikiye Maso bila taarifa yoyote. Akawa sio wa kumpigia wala kupokea simu ya swahiba wake Maso, wala si wa kujibu barua pepe anayotumiwa na rafiki yake. Hiyo hali ilidumu kwa muda wa si chini ya wiki mbili.
Mbaya hata akienda chumbani kwa Mudrah hapatikani, mlango umefungwa. Na akiwaulizia sanjali wenzake wa kozi ya sheria nao wanasema hawamuoni daima dawamu darasani. Maso akaanza kupata upweke wa mwanzoni, ukamrudia kwa kasi. Akapatwa na daka la roho kwa kumkosa bila taarifa rafiki yake kipenzi walioshibana. Akaanza kupatwa na msongo wa mawazo, na kuanza kupoteza hamu ya kula mpaka akaanza kuwa gofu la mtu mithili ya mgonjwa UKIMWI.
Mwaka wa masomo kuhitimisha muhula wa pili ulikuwa ndio unakaribia kwisha, akawa anajifikiria ndio kwanza anamaliza mwaka mmoja na bado miaka mitatu mbele yake. Masharti ya mfadhili wake ni kubakia Ulaya mpaka amalize Chuo ndio atarudi nyumbani Tanzania. Mbaya zaidi huku nyumbani kwao mama yake alipigwa mkwara na mfadhili kuwa asimsumbue kabisa mtoto wake masomo ni magumu, mtoto wake akifeli hata somo moja tu hatomlipia tena gharama za masomo na maisha.
Ikabidi Bi. Mwantumu awe anawasiliana kwa nadra sana na mtoto wake, jambo ambalo lilizidi kumuongezea upweke kipindi ambacho alikuwa anahitaji mfariji. Ghafla bin vuu, siku moja usiku akiwa amekaa nje ya bustani za hosteli maalumu kwa Wanachuo, akiwa ameshakata tamaa ya kuishi Ulaya, anatafakari kitu cha kufanya. Akajitokeza rafiki yake Mudrah Mudriki katika uoni wa macho yake kama mzuka vile.

Maso akiwa amepigwa na butwaa na kushikwa na gagaziko la ulimi, hayaamini macho yake "Assalaamu Aleikum rafiki yangu kipenzi wa moyoni" aliwahiwa kusalimiwa na Mudrah huku wakikumbatiana. Badala ya kujibu salamu, Maso haraka haraka akamtupia swali, "ulipotelea wapi ulinipa wahaka wa moyo usiomithilika kubeba nisiyoyaweza kifuani mwangu, kitu gani nilikukera uniambie kabla wakati haujazidi kwenda matiti nikuombe radhi tusameheane turudi kuwa washirika wa chanda na pete kama zamani". "Maso Square The Duduman" alikuwa anaongea kwa hisia za ndani ya moyo mpaka machozi yalikuwa yanamlengalenga.
Alikuwa ndio kwanza anatimiza miaka 21 bado anahitaji muongozo na faraja ya watu wa karibu. Mudrah Mudriki rafiki mkia wa fisi ukimshiriki atakufilisi alikuwa anafurahi kimoyomoyo kuwa lengo lake linakaribia kutimia muda sio mrefu la kumtumbukiza Maso kwenye shimo refu ambalo kuchomoka kwake itahitajika kudra za Rabana tu.
Kiuhalisia Mudrah Mudriki alikuwa Mwanachuo feki, alitumwa kazi maalumu ya kumuingiza "Maso square The Duduman" kwenye kundi la kigaidi la "Al-shabaab". Mchongo wote ulichongwa na mwarabu mmoja Mfanyabiashara na Mkandarasi maarufu nchini Tanzania 'Hafeedh Abdullah', ambaye ndio aliyemrubuni Bi.Mwantumu kuwa anataka kumsaidia kumsomesha mtotowe Uhandisi huko Ughaibuni ili aje kumuajiri kwenye kampuni zake zilizosambaa Arabuni na Afrika. Akamzuga ameamua kumsomeshea mwanawe kwa sababu yeye ni mwanamke mjane na pia kutokana na mtoto wake kufanya vizuri kwenye mitihani yake ya Kitaifa. Akamuingiza kingi kuwa Mwenyezi Mungu katika vitabu vya dini amesisitiza sana kuwajali wajane na mayatima kama Maso. Mfanyabiashara huyo Hafeedh Ibn Abdullah alikuwa ana ushirika na kampuni za Ukandarasi wa majengo nchini Sudani tokea mwaka 1989.
Hivyo Osama Bin Laden alivyokuja kuishi nchini Sudani kuanzia mwaka 1991-1996 alivyotafuta washirika wake wa kufanikisha ajenda zake za kigaidi siku za usoni akamsajili kibopa Hafeedh Ibn Abdullah kuwa ndio msimamizi mkuu wa shughuli za "Al-qaeda", Ukanda wa Afrika Mashariki. Chambo chao cha udaga kilikuwa kinakaribia kumnasa samaki muhimu kwao katika karata ya ugaidi.
Walitambua kabisa ugaidi katika karne ya 21 unahitaji watu wenye ubongo unaochemka sana kama "Maso Maso" ambaye alikuwa amemaliza shule katika sekondari ya watoto wenye vipaji maalumu vya kiakili, Mzumbe Sekondari. Mapambo yoyote dhidi ya adui yako katika zama za sayansi na teknolojia zilikuwa zinahitaji akili nyingi kuliko nguvu nyingi.
"Rafiki yangu samahani sana nimeipata njia ya kunikurubisha kwa Mola wangu. Mie nimeamua kujitenga na wewe kwa sababu Mwenyezi Mungu anasema kwenye Qur'an Surat Mujaadalah, surah ya 58 aya namba 22; "Hutokuta watu wanaomuamini Allaah na Siku ya Mwisho kuwa wanafanya urafiki na kuwapenda wanaompinga Allaah na Rasuli Wake, japo wakiwa ni baba zao, au watoto wao, au ndugu zao, au jamaa zao. Hao (Allaah) Amewaandikia katika nyoyo zao iymaan, na Akawatia nguvu kwa Ruwh (Wahyi) kutoka Kwake, na Atawaingiza Jannaat zipitazo chini yake mito ni wenye kudumu humo. Allaah Ameridhika nao, nao wameridhika Naye. Hao ndio kundi la Allaah. Tanabahi! Hakika kundi la Allaah ndio lenye kufaulu". Akapumzika kuongea baada ya kumaliza kusoma aya. Akachomoa hanchifu yake mfukoni, akaanza kufuta machozi yake yaliyokuwa yanabubujika kama maji, kujionyesha amejawa na mapenzi ya Allah moyoni mwake kumbe bosheni tu, kisha akaendelea na mahubiri yake.
"Sasa kwa msingi huo mie nakuacha rasmi kwenye maisha yako ya kumtumikia Shetani, mimi sasa nimempokea Allah na kumfanya kuwa taa ya maisha yangu. Sasa wewe bado unahudhuria muziki, bado unaangalia kandanda wakati wachezaji wake wamevaa nusu uchi na dhunubu kibao ambazo zinamchukiza Allah na Mtume wake, hivyo nakuaga rasmi urafiki mimi na wewe basi, kwaheri" akaaga, akageuka akawa anajifanya anaondoka.
"Maso Square The Duduman" akawa anaona sasa anaachwa solemba moja kwa moja, hata onana tena na swahibu wake. Kuachana kwao urafiki inamaanisha hana nguzo tena ya kujishikia atakapopatwa na shida ugenini. Ndugu yake mwenye asili ya nyumbani Zanzibari, Tanzania aliyemtegemea sasa anamuacha kwenye mataa. "Mudraaaaah Mudraaaaaah....pliiiiiiz my friend don't leave me, let's talk pliiiz..!! " ilikuwa ni sauti ya kubembeleza ya Maso ikimtaka rafiki yake Mudrah arejee wayajenge. Furaha ya Mudrah moyoni mwake ilikuwa kama amepaa yupo juu ya mwezi, ndio kitu alichokuwa anakitarajia. Alikuwa tayari ameshakaribia kutaka kupotea kwenye upeo wa Maso ndio akasikia sauti inayomuita kwa nguvu zote.
Akajifanya anatikisa kiberiti kwa kujichelewesha kidogo, akasikia tena sauti ya Maso inamuita. Kiunyonge akajifanya anarudi alipo Maso. Alipofika wakakumbatiana na rafiki yake, huku anajifanya kulia kifaurongo. "Sasa inabidi nikupeleke msikitini ukatubu dhambi zako usilimu upya"
Wakakubaliana wapitiane saa kumi na nusu usiku kuelekea msikitini kwa shekhe Dawoud El-jabeer. Shekhe ambaye durusu zake za masomo ya dini baada ya sala ya alfajiri zilikuwa zinavutia vijana wengi wa Ulaya hususani nchini Uingereza. Huyo Shekhe ndio alikuwa bomu maalumu lililotegwa na Al-qaeda kuwapika magaidi wapya kwa kutumia kasumba ya Uislamu wa itikadi kali. "Maso Square The Duduman" alikuwa anaenda kulishwa itikadi kali ya kiislamu iliyopotoshwa makusudi ili kuwapotosha vijana wasio na hatia wajitoe muhanga kwa kujivika mabomu.


"Maso Square The Duduman" amesajiliwa rasmi kuwa gaidi.
Ulikuwa ni usiku wa giza nene lililoenea kila mahali. Nuru pekee iliyoangaza nchi ilikuwa ni ya nyota tu zilizoko angani ambazo zilimeremeta kwa utulivu. Watu wengi walikwisha jilalia zao usingizi wa pono kutokana na uchovu wa mihangaiko ya kimaisha ya mchana kutwa. Wakati fulani sauti za wazururaji wa usiku na walevi wenye kupenda ugomvi ilisikika mbali kabisa na karibu na kambi ya siri ya magaidi wa "Al-shabaab" iliyopo katika Milima inayoitwa 'Jabar Marrah', Magharibi mwa Jimbo la Darfur, nchini Sudani. Walevi hao walikuwa wanajiiba tu kutimiza hawaa za nafsi zao kwa kunywa pombe katika nchi ambayo inafuata utawala wa Sharia za Kiislamu, ambapo ukikamatwa umekunywa pombe unapigwa mboko hadharani.
"Maso Square The Duduman" usiku huo alikuwa amejisokota kwenye kichaka kilichopo kwenye Milima hiyo akiwa amevaa sare maalumu za "Al-shabaab", kombati za rangi ya kijani mpauko. Ghafla bin vuu bila kutegemea, katika mazingira ya ukame wa jangwani, mvua ya kidindia ikaanza kunyesha mfululizo. akaanza kulowana na akatota chapachapa mwili mzima.
Hakuwa na jinsi bali kuendelea kubakia pale pale alipohitajiwa kuwepo na wakufunzi wake. Alikuwa yupo doria ya kambi katika siku yake ya mwanzo kabisa akiwa kambini hapo kwa ajili ya mafunzo ya muda mrefu yatakayompika aje kuwa gaidi mahiri duniani. Alishakacha masomo kitambo na kutorokea nchini Sudani bila familia kung'amua. Siku ambazo ilikuwa hamna kulala mchana na usiku kwa muda wa miezi miwili mtawalia. Ilikuwa ni mwendo wa kunyanyua vitu vizito na kutembea navyo umbali kadhaa, kubiringika, kupiga pushapu, skwashi, kutambaa na kifua, kukimbia na kunyoosha viungo. Kambi ya 'Jabbar Marrah' ilikuwa ni pacha wa kambi kuu ya kigaidi ya "Al-qaeda" iliyopo katika mashamba ya 'Tarnak' huko 'Kandahar', Afghanistani. Hiyo ndio kambi aliyokuwa anaishi gaidi mkuu Osama Bin Laden, enzi za uhai wake wakati amejichimbia nchini Afghanistani.
Wakufunzi wake wote kijana "Maso Maso" walitokea huko 'Tarnak' wakitumia mitaala ya huko huko Kandahar iliyoachwa na muasisi wa Al-qaeda, Osama Bin Laden. Wakufunzi wa "Maso Maso" walikuwa ndio wale wale wakufunzi mahiri waliowafunza vijana hatari kwa ugaidi duniani, "Mohammed Atta" na "Ziad Jarrah". "Mohammed Atta" raia wa Misri na "Ziad Jarrah" raia wa Lebanoni wakiwa wamemaliza elimu yao ya Chuo Kikuu jijini Hamburg, nchini Ujerumani, hawa ndio walioshiriki mashambulizi ya kujitoa mhanga kwa kutumia ndege ya tarehe 11/09/2001, maarufu kwa "September 11" yaliyotokea nchini Marekani.
ITAENDELEA
 
Kitabu pia kipo mtaani
IMG-20200611-WA0020.jpg
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom