SEHEMU-34
Lengo la Kachero Manu hakutaka kuacha hata chembe ya ushahidi kwa sababu alijua huko wanakokwenda kuna kufa au kupona. Hisia zake mpaka akaamua amfuatilie huyo Mzee wa kiarabu zilimtuma kuwa baadhi ya washirika wa "Al-shabaab" wameanza kutafuta maficho hasa baada ya nyaraka za siri zilizonaswa na Kachero Manu kule Simba Hoteli, Dodoma, zenye majina yao kutua mikononi mwa serikali. "Wewe Juma nakukubali aisee umejuana nae vipi mtu muhimu kama huyu, ambaye ana utajiri chekwachekwa" alidodoswa Juma na Kachero Manu wakati tayari ameshajaza mafuta pomoni kwenye tenki la pikipiki sasa walikuwa wanakata msitu kuelekea huko mashambani.
Juma Mavideo alikuwa analikimbiza pikipiki kwa mwendo wa kasi hakujibu swali la Kachero Manu, akawa anakanyaga mafuta na alikuwa analimudu ingawa alikuwa 'chordo chupa na kizibo chake' ananuka pombe ya ngomani balaa.
"Hapo mbele kwenye kona hapo pana mti wa msufi mkubwa, gari yao siku moja iliharibika, ilikuwa usiku kama saa 4 hivi sasa kuna fundi wao alitoka Mjini nikapewa kazi ya kumleta, kwa sababu mie hamna kijana anavijua vichochoro vyote vya Amboni kama mimi" alijibu Juma swali aliloulizwa kwa mbwembwe zote huku anaikamua pilipiki vilivyo.
Ghafla kutokea mbele yao ikawa inasikika sauti ya gari linakuja uelekeo wa kutokea mbele yao. "Ingiza porini haraka, huenda watu wabaya wanataka kutupora madini" alitoa amri Kachero Manu na Juma Mavideo akatii bila shuruti, wakalisweka pembeni haraka haraka, Juma akazima pikipiki yake na taa zake. Punde si punde likajitokeza gari linatembea mwendo wa pole pole limeshusha vioo, ndani kuna msichana amejifunga mtandio kichwani na mwanaume anayeliendesha gari. Waliweza kuwatambua vizuri kwa sababu dereva aliwasha taa ya ndani ya gari kana kwamba kwamba kuna kitu yule msichana alikuwa anatafuta ndani ya gari.
"Kaka kaka hili ndio gari lenyewe linalombeba yule mwarabu" alikuwa ananong'ona Juma kumwambia Kachero Manu, huku anatetemeka mwili mzima kule kichakani walipojisweka. Kachero Manu akatikisa kichwa kuonyesha kukubaliana nae huku ametingwa na ananakiri namba za gari hiyo ya polisi.
Baada ya gari lile kupita safari yao ikawa inaendelea tena, huku wanatumia matairi ya lile gari kama ndio dira ya wanaoelekea. Ilikuwa ni safari ya mwendo mrefu takribani masaa mawili, mpaka wakawa wamekaribia kufika. Juma akazima bodaboda ghafla pale yalipoishia yale matairi ya lile gari.
Akaanza sasa kumsomesha Kachero Manu, "sasa kaka yangu mpaka hapa ndio mwisho wa safari yangu, hapo mbele kuna nyumba moja nadhani ukiuliza hapo utapata jibu wapi anapoishi. Unajua analetwa na gari ya manjagu sasa wale jamaa hawana udugu wala urafiki unaweza bambikiziwa kesi ya wizi au mauaji ili wakufyedede vizuri".
Kachero Manu akabaki anatabasamu tu, akistaajabishwa na uoga wa Juma Mavideo wa ghafla, maana safari yao nzima akiongea yeye tu kujisifu ujanja, sasa ametepeta kama chapati za maji. "Mie nakupa nusu saa tu vinginevyo nasepa zangu, bado uhai naupenda mke wangu ndio kwanza nipo nae mwaka wa pili hata mahari yangu haijajilipa vizuri bado. Maadamu umeamua kujifunga bogi mie nakutakia kila kheri" aliongea kwa sauti kubwa Bwana Juma kusisitiza Kachero Manu asichelewe kurejea huko anakokwenda.
Kachero Manu akawa anatokomea kwenye uoni wa upeo wa Juma kuelekea alipoelekezwa, kikubwa alichoshukuru hawakukanyaga chechele wakapotea njia bali wamefika salama wanapopakusudia. Jukumu la Juma lilishaisha tayari, sasa imebaki kazi yake.
[emoji3586][emoji3586][emoji3586][emoji3586][emoji3586][emoji3586][emoji3586][emoji3586][emoji3586][emoji3586][emoji3586][emoji3586][emoji3586][emoji737]
Kachero Manu akaanza kutembea kupita kwenye mafukutu ya nyasi zilizoshonana kwa msaada wa mbalamwezi huku akichukua tahadhari kubwa. Mpaka alivyotembea kama dakika 5 akaanza kuona mwangaza kwa mbali unatoka kwenye nyumba iliyoonekana kuwa ni ya kibanda cha miti, iliyokaa kiungani kwa kujitenga.
Akazidi kukisogelea kibanda kile kwa umakini mkubwa. Mbele yake akauona mti mkubwa ulio karibu na nyumba ile. Akajificha kwenye mti mmoja huku akitafuta mbinu ya kuingia kwenye kibanda kile. Alipoona kimya hamna michakato yoyote inayoendelea pale akachomoka kwa kasi kwa mwendo wa kunyata kuzungukia upande wa kushoto wa nyumba. Akafanikiwa kufika mlango wa nyuma. Akaweka sikio lake kwenye uwazi mdogo sana wa baina ya mbao na mbao pale mlangoni. Akawa anasikilizia kama kuna lolote linaloendelea. Akaona kimya kimetamalaki kwa kiasi kikubwa.
Giza la nje lilikuwa msaada mkubwa kwake, mwanga uliokuwa unaangaza ni wa mbalamwezi tu. Akaachana na mlango na kuanza kuzunguka na kiambaza kuchungulia kwenye madirisha ya chumba tofauti tofauti. Chumba zote tatu zilikuwa vina giza isipokuwa kimoja tu kulikuwa na mwangaza wa koroboi.
Kilikuwa ni chumba kina pipa moja kubwa la plastiki lilikuwa lina maji kiasi. Pia kulikuwa na vyombo vichache vya kupikia. Akaamua aingilie kupitia dirisha hilo. Haikuwa kazi ngumu kulinyofoa dirisha hilo kutokana na kuwa ilikuwa ni nyumba ya udongo na miti. Akachidikia chumbani, wakati anashangaa mle chumbani anafikiria kitu cha kufanya, akasikia michakato ya viatu ya mtu anayekuja kwenye kile chumba.
Kachero Manu akafanya maamuzi ya kupiga mbizi kwenye pipa lile la maji. Kweli Bwana yule mtu aliingia chumba kile kile akaenda mpaka vyombo akaviparanganyua na kuchukua kitu anachokitaka, akajifanya anaondoka zake na kufunga mlango. Kachero Manu alipiga mbizi kwa zaidi ya dakika 10, kisha akaibuka na kuruka nje ya pipa hilo. Ile anatua chini tu, akapigwa na gunia zito la mchanga kisogoni mwake. Lilikuwa ni pigo takatifu ambalo kama angepigwa mtu tefutefu asiye na mazoezi kama Kachero Manu lazima angefuata njia ya marahaba, malaika wangempokea kaburini. Akaanza kuyumbayumba kama mlevi aliezidiwa na pombe, kisha akaanza kuona nyota nyota na huku kuna watu warefu wasio na mwisho wamevaa nguo nyeupe wengi sana.
Ambao wanaimba nyimbo za mapambio huku wakimzunguka duara. Akajiona mwishoni anazama kwenye shimo refu sana yenye kiza kinene. Alichokuwa hakifahamu Kachero Manu ni kuwa kulikuwa na mlinzi mmoja yupo juu ya mti anafanya doria ya eneo zima, kwa bahati mbaya hakumuona na huyo ndio aliyepanga shambulizi dhidi yake. Kachero Manu akapoteza fahamu akiwa ndani ya nyumba ya mtu asiyemfahamu.
[emoji3586][emoji3586][emoji3586][emoji3586][emoji3586][emoji3586][emoji3586][emoji3586][emoji3586][emoji3586][emoji3586][emoji3586][emoji3586][emoji737]