Riwaya Mpya: Mpelelezi Ray Shaba katika

Mkuu kwanini hii stor usiwe unatupia tu hapa chini kuliko kuunganisha hapo juu? Kwa wenye simu watapata shida sana kuisoma hii stori
 
Kama nilijua sikuanza kuisoma hii hadithi manake ningeishia kwenye arostos!
 
SURA YA NNE



Fr. RENATUS KIKO ALIKUWA amemaliza kuadhimisha ibada ya Misa Takatifu katika Kituo cha Kiroho cha Agape nje ya Jiji la Dar-es-Salaam kama kilomita moja tu hivi toka barabara ya Morogoro karibu na kituo cha Kibanda cha Mkaa, maeneo ya Mbezi Mwisho. Fr. Kiko alikuwa ni Mkurugenzi Mtendaji wa kituo hicho cha aina ya pekee Tanzania chenye kutoa mafunzo ya kina ya Biblia, Ufuasi, na Uinjilisti katika Kanisa Katoliki Tanzania.

Makanisa mengi ya kipentekoste na kiprotestanti yalikuwa na shule na vyuo vingi vya uinjilisti. Wasabato walikuwa na Shule ya Kibidula, Mafinga Iringa na shule kama Mshewe ya Mbalizi kwa ajili ya waumini wa madhehebu ya Kipentekoste. Kabla ya Agape, Wakatoliki hawakuwahi kuwa na shule maalumu ya uinjilisti na biblia kwa walei ukiondoa seminari na vyuo vya makatekista.

Siku hiyo ya Jumapili pale Agape walikuwa wanamalizia semina ya wiki moja juu ya Misingi ya Kuwa Mfuasi. Baadhi ya wakufunzi wa semina hiyo walikuwa wanatoka Ghana akiwemo mhubiri maarufu wa Kikatoliki kutoka Ghana Dkt. Kwame Kuffor. Kwame alikuwa ameambatana na wakufunzi wengine kutoka visiwa vya Malta katika bahari ya Mediteranean lakini chenye historia ndefu. Mkufunzi mwingine alikuwa kutoka Ujerumani kituo cha kiroho cha Emmanuel kilichoko jimbo la Cologne ambacho kilikuwa kinatoa udhamini wa mafunzo hayo.

Fr. Kiko kama mwenyeji wao alikuwa pia ni mmoja wa wakufunzi wakishirikiana na wanajumuiya wasio mapadre au watawa wa Agape ambao walikuwa kituoni wiki hiyo. Hata hivyo kundi kubwa la wanajumuiya wakazi lilikuwa Shinyanga kwa ajili ya kuendesha semina za kiroho na mikutano ya Injili katika parokia na vigango mbalimbali. Ukiondoa Fr. Kiko wanajumuiya waliobakia alikuwepo Alex Mawenzi, Clara Morita, Mke wa Tadeo Nyoni na Celestina Mushi. Walikuwa na mgeni mmoja kutoka Tarime, Mara ambaye alikuwa ametumwa na Parokia ya Bikira Maria Malkia wa Shirati kujifunza juu ya mambo ya Uamsho wa Kikarismatiki wa Kikatoliki.

“Fr. Kiko” ilikuwa sauti ya Clara Morita iliyomshtua padre huyo wakati anaondoka kwenye jengo la kikanisa kidogo cha kituo hicho kuelekea kwenye makazi yake upande wa Mashariki wa kituo hicho. Ng’ambo ya pili yalikuwa ni majengo ya nyumba na shule ya Sekondari inayomilikiwa na familia ya Mzee Joseph Mishili.

“Nini tena Clara?” Fr. Kiko aliuliza akiwa amesimama; mkono wake wa kushoto ukiwa katika mfuko wa suruali; mkono wa kulia ukiwa umeshika simu yake ya mkononi.

“Baba kuna mgeni amefika tu na anahitaji kuonana nawe” Clara alisema. Clara alikuwa ni Mratibu wa Huduma za Wageni wa kituo cha Agape. Jukumu lake kubwa lilikuwa ni kupokea, kuandikisha na kuhakikisha wageni wanapata ukaribisho mzuri. Wenyewe pale Agape walisema alikuwa ana karama ya wageni. Clara alikuwa ni dada mfupi wa wastani ambaye alikuwa amechanganya damu ya Kichagga na Kiitaliano. Giovanni Morita babake na Clara hakujihusisha na lolote kuhusiana na bintiye kwani alikuwa na familia nyingine huko Italia. Nywele zake ndizo zilizofichua kwa kiasi kikubwa kuchangia damu. Mama yake alizaa na Muitaliano akiwa masomoni Roma na aliporudi Tanzania alikuja na mwanae ambaye alimpatia elimu na maisha Tanzania.

“Mgeni gani tena Jumapili hii?” aliuliza Fr. Kiko kwa udadisi. Hakuwa anatarajia mgeni yeyote siku ile ya Jumapili. Aligeu kuelekea eneo la kupokelea wageni kwenye jengo kuu la kituo hicho. Wakielekea huko walipishana baba mmoja, mkewe watoto wao wanne waliokuwa wanacheza cheza njiani wakitokea upande wa kanisani wakielekea eneo la kuegeshea magari. Walisimama kwa dakika chache kumsalimia Padre Kiko na kujuliana hali.

Ndani ya dakika kama kumi tu toka apate ujumbe Fr. Kiko alifika kwenye sehemu ya kupokelea wageni akiambatana na Clara ambaye alikuwa amemtangulia hatua chache mbele yake. Walipofika sehemu ya kukaa wageni palikuwa na mgeni mmoja tu aliyekuwa amewapa mgongo wakati huo akiangalia Televisheni ya kituo cha EWTN – Eternal Word Televsion Network – kutoka Marekani. Alipowasikia wakiingia mgeni yule aligeuka kusabahiana nao.

“Fr. Kiko” mgeni yule aliita huku akiangusha tabasamu la nguvu. Alikuwa amevaa suti ya rangi ya kijivu yenye vimistari vyembamba vya rangi nyeusi na shati jeupe, shingoni akining’iniza tai nyekundu ya damu ya mzee. Alipiga hatua mbili za haraka na kumfikia Fr. Kiko huku mkono wake kauelekeza kumsalimia. Clara alikuwa bado amesimama nyuma kidogo ya Fr. Kiko kumpisha asalimiane na mgeni wake. Alikuwa ni kijana wa makamo mwenye kila namna ya utanashati.

Fr. Kiko alinyosha mkono wake kumsalimia mgeni bila kuonesha amemtambua mpaka alipomsikia mgeni yule amemuita kwa jina lake ndio sura na sauti yake vikakubaliana.

“Raymond! Ah! Ah! Ah!” Fr. Kiko alisema kwa shauku huku akitingisha kichwa kwa kutokuamini. Mkono wake wa kushoto amekishika kidevu chake kwa mshangao; hakuweza kuyaamini macho yake mara moja. Aliyekuwa amesimama mbele yake alikuwa ni Raymond Shaba. Kama mtoto kwa baba yake Ray alimjongelea Padre Kiko na wakakumbatiana kwa furaha. Raymond alikuwa ni mmoja wa wanafunzi wake katika Seminari ya Soni Lushoto miaka kumi na nne iliyopita. Fr. Kiko alimkumbuka Raymond kama mmoja wa wanafunzi waliokuwa na kipaji sana darasani kati ya wanafunzi wengi ambao Fr. Kiko aliwafundisha kwa miaka karibu kumi aliyokuwapo seminarini pale kama Gombera yaani Mkuu wa Seminari.

Katika kumbukumbu ya Fr. Kiko hakukuwa na mwanafunzi mwingine aliyemkumbuka kwa undani kama ilivyokuwa kwa Ray. Miaka yake mingi ya upadre aliwafundisha vijana wengi waliopita na kwenda kuwa mapadre na wawili baadaye walikuja kupata Uaskofu akiwemo Askofu wa Jimbo la Lindi na Askofu wa Jimbo la Rulenge. Katika muda wote ambayo Kiko alikuwa pale Soni hakuna mwanafunzi aliyeacha alama katika mawazo ya Fr. Kiko kama Raymond Shaba. Umahiri wa Ray katika kinanda na Kilatini umeacha simulizi Soni hadi leo hii.

Tangu kidato cha kwanza hadi cha sita Raymond alikuwa akiongoza kwenye mitihani darasani. Baada ya matokeo ya kidato cha sita ambapo alifaulu na divisheni 1 ya pointi saba Ray hakuwa na mpango wa kuendelea na masomo ya Falsafa kujiandaa na upadre kama familia, marafiki na hata waseminari wenzake walivyotarajia. Kutokana na ushauri, uongozi, na msaada wa Fr. Kiko Ray alipata nafasi ya kwenda masomo ya juu huko Nairobi nchini Kenya kwenye Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Afrika ya Mashariki ambapo alisomea shahada ya Sheria.

“Samahani baba” Clara aliingilia kati kabla mazungumzo yao hayajanoga.

“Eh, Clara”

“Miye nawaacha mara moja sijui mnahitaji kitu chochote?” Clara aliwauliza.

“Ray unataka kinywaji chochote maana jua kali hili” Fr. Kiko alimuuliza mgeni wake.

“Maji ya baridi tu tafadhali” Ray alisema akimuangalia Clara ambaye alikuwa anasubiria majibu yao. Fr. Kiko naye akaomba maji vile vile. Clara akaaga na kuondoka. Baada ya dakika chache Clara alirudi na glasi za maji pamoja na jagi la maji likiwa na barafu ndogondogo. Aliwaaga tena na kuondoka.

“Fr. Kiko, huzeeki Baba” Raymond alimtania huku akikumbatiana naye kusalimiana.

“Wewe ndio haujabadilika kabisa ukiondoa huo mustachi wako” Fr. Kiko alimwambia huku akimcheka kidogo.

“Mustachi ndio fasheni baba” Ray alijibu akiendeleza utani.

“Unanikumbusha yule mcheza filamu wa Kimarekani wa enzi zile Fred Williamson” Kiko alisema na kusababisha waangushe kicheko kwa pamoja. Kwamba alikuwa amefanana na Fred Williamson haikuwa mara ya kwanza kusikia kwa Ray. Walichangamkiakana kama watu ambao hawakupishana umri sana. Kati yao hata hivyo kulikuwa na tofauti ya zaidi ya miaka thelathini.

“Ehe, hebu niambie kwanza umenipata pata vipi hapa maana ni muda mrefu sana sijakuona; mara ya mwisho nakumbuka ni graduation yako Nairobi” Fr. Kiko alisema huku akimuongoza Ray kwenye makochi. Wakati Ray anahitimu Nairobi Fr. Kiko alikuwa pale Chuoni kumalizia mwaka wake wa mapumziko wenyewe wanaita Sabbatical. Fr. Kiko alikuwa ni miongoni mwa watu ambao Ray alikubali kuwa walikuwa na kumbukumbu nzuri sana.

Siku ile ya Jumapili ilikuwa ni ya mvua na manyunyu ya hapa na pale hasa maeneo yote ya Kimara, kuelekea Kibaha. Mjini kwenyewe kulikuwa na mawingu tu yaliyotishia mvua. Wakati wa misa asubuhi ile ilinyesha mvua kubwa iliyoambatana na upepo mkali na dakika chache kabla ya Ibada kuisha mvua iliisha na kubakia manyunyu kidogo. Majani yalikuwa yamelala upande mmoja baada ya kupulizwa na upepo huku baadhi ya miti ikiwa imepukutisha matawi yake madogomdogo. Upepo bado ulikuwa unavuma si kwa kasi sana lakini ukiwa ndani uliweza kusikia madirisha yakipiga miluzi kama yakilalamika.

Kutoka pale walipokuwa wamekaa Ray na Fr. Kiko waliangalia eneo la bustani nzuri iliyopamba nje ya jengo hilo dogo la kukirimia wageni na ambalo lilikuwa pia na hosteli ndogo ya wanafunzi ikiwa imeunganishwa na jengo hilo. Kulikuwa bado na mawingu yametanda yakinyang’anyana anga na jua. Harufu ya udongo mkavu uliopigwa na mvua ilikuwa imetanda bado angani. Ndege na wadudu waliokuwa wamejificha wanakojua wenyewe wakati wa mvua walianza kujitokeza tena na kuimba tena. Sauti za viumbe wale ziliashiria tu kuwa kuwa hata kuwe na hali mbaya kiasi gani bado zipo sababu za kumsifu na kumshukuru Muumba.

Fr. Kiko na Ray walitumia dakika chache hivi kukumbushana habari mbalimbali za maisha yao tangu walipoonana mara ya mwisho kule Nairobi. Akijibu swali la jinsi alivyofanikiwa kumpata Fr. Kiko pale Agape Ray alimuambia kuwa alianza kwa kutafuta jina lake kwenye tovuti ya Jimbo la Tanga ambapo majina ya mapadre wa Tanga yalikuwepo na parokia au ofisi walizokuwa wanafanya kazi. Hata hivyo, jina lake halikuwepo na hivyo ikamsababisha kupiga simu mwenyewe makao makuu ya Jimbo la Tanga, pale Kanisa la Mt. Mtakatifu Antoni, Chumbageni.

Alipopiga simu huko aliambiwa kuwa Fr. Kiko alikuwa ameombwa na Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Dar-esSalaam Kardinali Polycarp Pengo kuwa Mkuu wa Kiroho wa Kituo cha Agape. Pengo na Kiko walisoma wote Seminari Kuu ya Kipalapala kuanzia 1965 hadi 1971. Padre Kiko alikuwa amebakiza mwaka mmoja tu kustaafu. Kwa vile bado alikuwa na nguvu alikubali kuchukua huduma hiyo kwani pamoja na mambo mengi, alikuwa ni miongoni mwa mapadre wachache waliojua kwa undani juu ya mwamko wa kikarismatiki ndani ya Kanisa Katoliki.

Mwaka 1985 Fr. Kiko alikuwa ni miongoni mwa mapadre wawili waliotoa semina kwa maaskofu kwenye mkutano wao wa mwaka juu ya uamsho huo na hivyo kufanya majimbo mbalimbali yaanze kuwakaribisha wakarismatiki. Miaka ya mwanzoni wanauamsho au kama walivyoitwa baadaye Wakarismatiki waliangaliwa kwa jicho la shuku kwani walionekana kama ni walokole fulani. Na wapo Wakatoliki wengi walioingia kwenye uamsho lakini baadaye wakaishia kuingia kwenye makanisa ya Kipentekoste kwani waliona kama uamsho ule ulikuwa bado unafungwa na Ukatoliki.

Haikuwa kazi kwa Shaba kufika Agape baada ya kupewa maelekezo kwani kituo chenyewe hakikuwa mbali na barabara ya Morogoro eneo la Mbezi ya Kimara; Kibanda cha Mkaa baada tu ya kwa Musuguri na Mbezi Temboni.

“Naona ushafunga na ndoa tayari, hongera bwana” Fr. Kiko alisema baada ya kuangalia kidole cha chanda cha Ray ambacho kilikuwa kimevikwa pete ya ndoa.

“Asante sana Father” Ray alisema huku vidole vyake vya mkono wa kulia vikiizungusha pete kidoleni kwa sekunde chache. Ni kule kuzungushazungusha pete ndiko kulimfanya Fr. Kiko ampe pongezi ya ndoa. Alionekana amepotea kwenye mawazo kwa sekunde chache wakati vidole vyake vikifanya hivyo; Fr. Kiko aliliona hilo lakini hakusema kitu mara moja.

“Ulijiunga na Jeshi la Polisi sivyo?”

“Ndiyo Father”

“Ehe, vipi kazini unaendeleaje?”

“Naendelea salama, changamoto za kawaida tu”

“Nina uhakika utakuwa na wadhifa mkubwa tu sasa; maana wasomi wa chuo kikuu nasikia mnatakiwa sana huko”

“Kwa kweli si mbaya sana; nimekuwa Mrakibu wa Polisi sasa”

“Ah, Superitendent bwana! Hongera sana Ray! I’m very proud of you bwana; ingawa nina uhakika ungekuwa Padre mzuri tu kama ungeendelea na wito wako” Fr. Kiko alisema kwa kucheka akimtupia Ray dongo kiaina.

“Hahahaha acha utani father, labda Kanisa lingekuwa limeruhusu kuoa kwanza” Ray alijibu na yeye akamrushia dongo jingine. Wote walicheka kwa pamoja.

“Huwezi kujua bwana si tuna Papa mpya! Ila kwa sisi wengine ndio imetoka hiyo” Alipokuwa Soni chini ya uangalizi wa Fr. Kiko Ray alikuwa alikuwa kinara wa mabishano ya mambo ya kidini na mara kadhaa aliitwa kwa Fr. Kiko kujieleza kuhusu mabishano yake hayo ambayo wengine walimuona kama mwanzilishi wa Kanisa la Kilutheri, Martin Luther kwa ubishi wake. Mara mbili Ray alijikuta akiitwa kwa Gombera baada ya kudakwa na walinzi akitokea nyumbani kwa mmoja wa wapishi wa pale Seminari. Mama yule alikuwa na binti wa sekondari ambaye walikuwa wamezoeana sana na Ray. Tetesi zilienea kwa waseminari wengine kuwa mahusiano yao yalikuwa ni zaidi ya ‘kuzoeana’ au kualikwa kula chakula cha mchana tu. Kulikuwa na tetesi kuwa Frateri Ray alikuwa anakula hata ambavyo hakupaswa kula kama mseminari.

Fr. Kiko alipomuangalia Ray alisahau yote yaliyopita; alijikuta amejawa na furaha na hisia ya fahari kama baba kwa mtoto wake. Hofu yake ya miaka mingi kuwa Ray angeweza kujikuta kwenye maisha ya siasa au mambo yakaenda vibaya ilimtoka. Alikuwa na furaha kuona mmoja wa vijana wake amefanikiwa hivyo na moyoni alijua kabisa kuwa Ray asingeuweza upadre. Kwa upande wake Ray alikuwa anajua kabisa kuwa kama wapo mapadre watakatifu na wenye kuchukulia wito wao kwa uzito mkubwa basi alikuwa ni Fr. Kiko. Kiko mwenyewe alikuwa ni mhubiri mzuri sana wa mwenye nguvu na licha ya hivyo alikuwa pia ni mtunzi wa nyimbo mbalimbali za misa ambazo zilijulikana kama Misa ya Kiko namba I hadi V. Wimbo wa Fr. Kiko wa Amejaa Huruma na Neema na ule wa Atakalowaambia Fanyeni zilikuwa ni nyimbo zilizopendwa sana nchini katika parokia mbali na vigango vingi. Zilipendwa sana kwa sababu zilifuata mahadhi ya nyimbo za Kisukuma na mdundo wake ulinoga zaidi ukipigwa kwa ngoma za kienyeji, chakacha na kinanda.

“Samahani baba” mazungumzo yao yalikatishwa tena na ujio wa Dada Clara tena kama wengi walivyomuita pale. Pale Agape mtu aliitwa “kaka” au “dada”. Clara alikuwa amebadili nguo kutoka alizokuwa nazo kanisani na kuvaa za nyumbani; juu yake amevaa aproni.

“Bila ya samahani Clara” Fr. Kiko alijibu na wote wawili walimuangalia Clara kusikiliza alikuwa na ujumbe gani.

“Chakula tayari father, tunawasubiri” Clara aliwataarifu na kuwakaribisha. Fr. Kiko aliangalia saa yake na kukuta kuwa muda umeshaenda inakaribia saa saba muda wa chakula cha mchana. Kwa kawaida wanajumuiya wote na wageni wao hushiriki chakula pamoja kwenye ukumbi mkubwa wa chakula pale kituoni.

“Sawa; Ray karibu ule na sisi, tutaendelea na mazungumzo baadaye”

“Asante father” Ray alijibu na wote wawili waliinuka wakitembea mita chache nyuma ya Clara huku wakiendelea na mazungumzo ya hapa pale. Ray alisifia sana ujenzi wa kituo na mwonekano wake. Bado kulikuwa na majengo mengine yalikuwa yanaendelea kujengwa na mengine yalikuwa yameanza kutumika kabla hata hayajakamilika kabisa.

Walipomaliza kula Fr. Kiko na Ray walishiriki kidogo kuosha vyombo kama ulivyo utaratibu wa jumuiya ya Agape kufanya hivyo watu wanapomaliza kula. Wakiongozwa na mapambio ya kusifu, vichekesho, na stori za hapa na pale wanajumuiya na wageni wao walishirikiana kufanya usafi wa vyombo na bwalo la kulia kabla hawajaenda kwenye mapumziko ya kama masaa mawili ya mchana. Baada ya kumaliza Fr. Kiko na Ray waliondoka kuelekea kwenye jengo lile la kupokelea wageni ambapo pia ilikuwepo ofisi ya Kiko.

Ofisi ya Fr. Kiko ilikuwa kubwa kiasi ikiwa na dirisha kubwa likiangalia upande wa Mashariki; kulikuwa na meza kubwa ya ofisi katikati na nyuma yake kulikuwa na kiti kikubwa cha kisasa cha rangi nyeusi. Mbele ya meza kulikuwa na viti viwili vya wageni. Upande wa kulia wa ofisi kulikuwa na kabati la vitabu ambalo lilikuwa limepambwa na vitabu mbalimbali vya kiroho na vya mambo ya kanisa. Kati yake kulikuwa na vitabu vya mfululizo wa mafundisho ya Mt. Thomas Akwino viitwavyo Summa Theologica, kulikuwa na vitabu vya Mt. Augustino vya City of God (Jiji la Mungu), Confessions of St. Augustine (Maungamo ya Mt. Augustino), On Grace and Free Will (Juu ya Neema na Utashi), Expositions on the Book of Psalms (Mafundisho Toka Kitabu cha Zaburi) pamoja na vitabu vya Sheria za Kanisa pamoja na mafundisho mengine mbalimbali ya kanisa.

Kulikuwepo pia na vitabu vya maisha ya kiroho, maisha ya upadre, Historia ya Kanisa, Upapa na vitabu vingine vingi vya historia. Fr. Kiko alikuwa pia ni mpenzi wa vitabu vya riwaya hasa za C.S. Lewis, G. H. Wells na waandishi wengine wa katikati ya karne ya ishirini. Kitabu kikubwa cha Jesus of Nazareth kilichoandikwa na Papa Mstaafu Benedict XVI kilikuwa kwenye meza yake.

Juu ya kabati hilo kulikuwa na tufe la ramani ya dunia, pamoja na picha za familia ya Fr. Kiko pamoja na chupa ya maua mazuri yaliyotoka kwenye bustani ya pale pale Agape. Kwenye ukuta kulikuwa picha kubwa ya kuchora ya Mlima Kilimanjaro na mbuga yake ambapo tembo, twiga na pundamilia walionekana wakila majani. Juu yake kulikuwa na picha ya Papa Francis, Askofu Mkuu wa Jimbo la Dar pamoja na Askofu wa Jimbo la Tanga. Pembeni ya picha hizo kila upande kulikuwa na picha ya Bikira Maria na picha ya Moyo Mtakatifu wa Yesu.

“Karibu uketi Ray” Fr. Kiko alimkaribisha na kumwelekeza upande wa kushoto wa chumba ambapo kulikuwa na makochi mawili yakitengenanishwa na meza ndogo ambapo Fr. Kiko alitumia kwa mazungumzo na wageni wake hasa ambayo hayakuhusiana na kazi zaidi au ya watu ambao walikuwa karibu naye. Siku ile Fr. Kiko alikuwa amevaa suruali nyeusi pamoja na shati la kipadre la rangi nyeusi pamoja na kola yake ya kichungaji. Kwa kawaida huwa anavaa koti juu ya shati hilo lakini akiwa pale kituoni alikuwa halivai. Kwenye mfuko wa kushoto wa shati lake kulikuwa na nembo ndogo ya ramani ya Tanzania ambayo ilikuwa na msalaba ukiigawa katikati ramani ambayo mapadre wengi wa majimbo Tanzania huvaa.

“Asante” Ray alijibu na kukaa kwenye kochi mojawapo.

“Ray unaonekana na mawazo sana na kuna jambo linakusumbua ni nini kijana wangu?” Fr. Kiko alimuuliza kwa sauti yake ya upole.

Ray alivuta pumzi kidogo na kuishusha, akamuangalia Fr. Kiko kidogo na kujifuta uso wake kwa mkono wake wa kulia kama anayenawa.

Is that bad eh?”

“Yeah, it is that bad”

“Haiwezi kuwa mbaya namna hiyo unanitisha”

“Ah kwa kweli sidhani kama ni mbaya kihivyo ila naona kama inaweza kuwa mbaya sana huko mbeleni ndio maana niliona mtu mzuri wa kupata ushauri wake ni wewe Father”

“Haya ni nini, Mambo ya kazini?” Fr. Kiko alijaribu kuanza kwa kuchokoza.

“Hapana, ni masuala binafsi; ya kazini I can handle that” Ray aliinuka kidogo na kuacha kuegemea kochi akijaribu kuketi vizuri.

“Haya nini sasa?”

Ray alivuta pumzi tena kidogo.

“Fr. Mimi na Sofia, mke wangu, naona tunaelekea kwenye mgongano ambao unaweza ukasababisha tutengane” Ray alisema. Alivyosema hivyo ni kama alikuwa ameanza kuutua mzigo mkubwa kutoka moyoni.

“Tumekuwa na matatizo ya muda kidogo lakini naona sasa tumefikia mahali ambapo hata hatusemezani; kila mtu anaingia na kutoka kama watu wasiofahamiana” Ray alisema sauti yake ikiwa inajitahidi kuficha uchungu na hasira. Alimuangalia Fr. Kiko ambaye alikuwa anamuangalia na yeye kwa umakini mkubwa tu akilichukua kila neno lililotoka kinywani mwa Ray moyoni mwake na akilini mwake kwa uzito wote unaostahili.

“Umesema mmekuwa na matatizo kwa muda; matatizo gani hasa? Kama hutajali sana kuniambia” Fr. Ray alianza kudodosa taratibu na kwa ustadi. Alikuwa kama ni daktari anayejaribu kupasua kichwa ili kuufikia ubongo.

“Father, kwa kweli si matatizo matatizo bali ni tatizo moja ambalo naona limezaa matatizo haya mengine” Ray alianza kufafanua bila kufikiria sana. Alikuwa ameshaungama mengi kwa Fr. Kiko huko nyuma na haya mengine wala hayafikii kwa uzito na usiri wake. Alijiona yuko huru kwani alikuwa ni mwanadamu pekee aliyeamini anaweza kutunza siri na anaweza kutoa ushauri bora na wa kumsaidia kwelikweli.

“Ehe” Fr. Kiko alichombezea. Kwenye meza iliyokuwa kati yao kulikuwa na chupa mbili za maji na glasi ambazo Clara alkuwa ameziandaa kwa ajili yao.

“Kwa kweli Padre ni suala la kuwa na watoto” alianza kuelezea. “Unajua tangu tumefunga ndoa imepita karibu miaka mitano sasa na hatujajaliwa kupata mtoto na mwenzangu naona kama anaanza kuwa na wasiwasi na kujisikia hatia” Ray aliendelea kumwelezea. Alimuelezea jinsi ambavyo Sofia alikuwa analalamika mara kwa mara kuwa anajiona kama siyo mwanamke kweli na anaona kama amemnyima Ray bahati ya kuwa na watoto kufikia mahali hata kumtaka Ray atafute watoto nje ya ndoa jambo ambalo Ray alilipinga vikali na kumhuzunisha.

Ray alielezea jinsi gani Sofia alihisi kuwa ndugu wa Ray walikuwa wanamng’ong’a kwa kushindwa kumpa kijana wao mtoto na hilo lilionekana kumuumiza sana. Ilifikia wakati Sofia hakuwa tayari kukutana na ndugu yeyote wa kina Ray kwa kuogopa masimango. Kila walipokutana na watoto wachanga Sofia alikuwa ni mtu wa kuzama kwenye mawazo na masononeko.

“Lakini watoto siyo haki ambao wanadamu wanaweza kuidai mbele za Mungu; ni neema tu Ray” Fr. Kiko alisema kwa namna ya swali hivi.

“Ndio Father, kiakili tunakubali hivyo lakini jamii yetu na tamaduni zetu zinatukuza sana ndoa zenye watoto na watu wakichelewa au kukosa kuwa na watoto basi maneno hayakosekani” Ray alielezea jambo ambalo Fr. Kiko alilielewa fika kutokana na miaka yake mingi katika utumishi wa uchungaji.

“Mmewaona madaktari kuona kama kuna jambo lolote la kiafya linalowafanya msiweze kupata mtoto?” aliuliza swali ambalo lilikuwa la kawaida katika mazingira ya mazungumzo hayo.

“Tayari tumeshaenda kwa madaktari mbalimbali na tumefika hadi kwa Dkt. Linus Ngonyani mmoja wa mabingwa wa Magonjwa ya Uzazi pale Muhimbili lakini wote hawaoni tatizo lolote kwangu au kwake la kwanini asiweze kutunga mimba” Ray alijibu huku akiinua glasi yake iliyokuwa na maji kidogo na kuyamalizia kabla ya kumimina mengine kutoka kwenye jagi. Alilamba kidogo midomo yake kuilanisha wakati maji baridi yakishuka taratibu kooni.

“Pole sana Ray; kwa kweli siyo jambo dogo hata kidogo” Fr. Kiko alisema akitafuta maneno ya kusema.

“Hilo ni sehemu tu ya tatizo lenyewe Father” Ray aliendelea kusema akimuacha Fr. Kiko akizama kwa sekunde chache katika mawazo ameshikilia glasi yake ya maji.

“Kuna tatizo zaidi?”

“Kwa kweli ni matatizo yanayotokana na hili sasa”

“Ehe!”

“Mwanzoni tuliposhindwa kupata tiba kwa madaktari mwenzangu aliamua kuanza kutumia mitishamba” Ray aliendelea kusimulia sauti yake ikiwa ni ya upole lakini kama ikihesabu kila sirabi iliyotoka mdononi mwake. “Mwanzoni ilikuwa mitishamba tu ya barabarani lakini mwisho sijui alipata ushauri wapi akaanza kusema twende kwa waganga wa kienyeji” Ray alisema na kukaa kimya kwa sekunde chache; aibu na hatia vilijiandika katika paji la uso wake. Kwa kijana msomi na mwenye nafasi kama yake kukiri kuwa ameenda kwa waganga wa kienyeji na kuwa anaamini katika ushirikina ilikuwa ni mashtaka makubwa kabisa ya kupotea kwa imani yake katika wema na huruma ya Mungu. Hivyo ndivyo alivyokuwa akijiambia mara kwa mara.

Fr. Kiko alimsoma Ray, “unajua siyo jambo la ajabu watu kujikuta wanalazimika kujaribu tiba za aina mbalimbali; huwezi kuamini wapo hata mapadre ambao walipokuwa katika majaribu ya udhaifu fulani wameenda hadi kwa waganga wa kienyeji!” alisema na kumfanya Ray atabasamu kidogo kiuvivu.

“Bila ya shaka hata huko hakukuwa na mafanikio aliyotarajia?” Fr. Kiko aliuliza swali ambalo jibu lake lilikuwa dhahiri.

“Ndiyo; hiyo ilikuwa mwaka jana; sasa ameamua kuachana na waganga wa kienyeji – na tumewazunguka kuanzia Bagamoyo, Morogoro, Tanga hata tulienda kwa yule Mbunge mganga wa kienyeji kutoka Korogwe” alisema Ray. Aliongeza kuwa “tatizo ni kuwa sasa ameanza kwenda kwenye makanisa mbalimbali kuombewa ili apate mtoto” alisema Ray kwa huzuni kama mtu aliyekata tamaa.

“Sasa hilo si ni jambo jema Ray, ameamua kumrudia Mungu?” Fr. Kiko alimuuliza

“Ingekuwa hivyo Father nisingekuja kukuona” Ray aliendelea huku aking’aka “ni kuwa huku kwenye makanisa nayo yamekuwa kama waganga wa kienyeji!”

“Kivipi tena?”

“Tangu mwezi Januari ameacha kabisa kwenda kwa waganga na kutupa madawa yote ya kienyeji na kuanza kwenda kwenye makanisa ya walokole kutafuta maombezi”. Ray aliendelea kusimulia huku Fr. Kiko akiendelea kusikiliza kwa makini. Wakati wanaendelea na mazungumzo pale kituoni ulishuka ukimya wa aina yake; watoto waliacha kucheza cheza, na watu wazima kila mtu alikuwa ameenda kujifungia chumbani au nyumbani kwake. Ulikuwa ni muda wa mapumziko. Sauti ya upepo na ndege wachache zilisikika zikikatishwa katishwa na sauti ya magari yaliyopita kwenye barabara iliyokuwa katikati ya eneo la Agape. Wageni wengine walikuwa wanaanza kuondoka na kurudi makwao kutoka Agape.

“Kama ni kuombewa tu hakuna madhara yoyote Ray” Fr. Kiko alijaribu kumshauri na kumtuliza.

“Ni kweli” Ray alidakia. “Inaonekana kama anajaribu kumshawishi Mungu kupitia haya makanisa ampe mtoto na yuko tayari kufanya lolote” Ray alimalizia.

“Mmh hili inaonekana ni zaidi ya kushawishi” Fr. Kiko alidakia tena. Maji kwenye glasi yake yalikuwa yameisha.

“Ni kweli father, katika kwenda kwenye haya makanisa Sofia amekuwa akitoa sadaka na michango mbalimbali ambayo sasa hivi inatishia uchumi wetu na hata ndoa yetu kwani karibu kila kanisa ambalo ameenda linasisitiza sadaka sana” Ray alisema na kwa sekunde chache alivingirisha tena pete yake kwenye kidole chake huku moyoni akichagua maneno aliyoyataka kuendelea nayo.

“Alianza kwa Mzee wa Miujiza Festo Kyaruzi, kaenda kwa Mch. Gwandi, na akaenda hadi kwa Mwingira na kwa Kakobe” aliendelea Ray Shaba kuorodhesha makanisa ambayo Sofia alikuwa ameyapitia.

“Kote huko baada ya muda anajikuta wanamhimiza kutoa sadaka za kila namna” Ray alisema. “Wenyewe wanaita ni ‘mbegu’ ambayo ili mtu avune sana inabidi apande mbegu kwa wingi na wakati mwingine mara kwa mara” alisema Ray huku sauti yake ikimsaliti kwani alionekana kama mtu aneyeungama kushindwa. Alijisikia vibaya kwani aliyekuwa anazungumza habari zake ni mke wake ambaye naye ni msomi wa kutosha tu – angalau kwa kuangalia suala la kuhitimu vyuo vikuu.

“Eh! Hayo sasa ni mambo ya hatari” Fr. Kiko alidakia na kuongezea

“Ndio namna ya kubarikiwa zaidi wenyewe wanasema”

“Yaani ili ubarikiwe lazima utoe?”

“Naam, na ili ubarikiwe zaidi inabidi utoe zaidi!”

“Unaposema kutoa michango, sadaka hiyo ni kiasi gani tunazungumzia?”

“Baba, hadi hivi sasa kwa miezi hii sita tu ya kwanza kwenye haya makanisa katumia karibu milioni karibu kumi na ushee” Ray alijibu.

“Sasa Ray nikuulize swali ambalo liko wazi kabisa” Fr. Kiko alisema.

“Kwamba, kwanini nimemuacha afanye hivyo?”

Exactly!”

“Mwanzoni kwa kweli sikuona madhara lakini siku zinavyozidi kwenda namuona anazidi kuzama kwenye haya mambo na sijui kama nasema anaonekana kuchanganyikiwa lakini ni kama yuko katika desperation ya aina fulani hivi” Ray alisema.

“Ehe”

“Ni hili nililolikuta wakati nimerudi kutoka nje hivi majuzi”” Ray aliendelea. Siku tatu nyuma Ray alikuwa amerejea nchini kutoka Cairo, Misri ambako alikuwa ameshiriki mkutano wa wapelelezi waandamizi wa Afrika.

“Kijana wetu wa shamba alinitumia ujumbe akinitaka tuonane mapema iwezekanavyo” Ray aliendelea kufafanua. “Jana nimeenda Kinyerezi na kukutana naye na amenishtua kwa kuniambia kuwa Sofia alikuwa ameuza Kinyerezi kwa Msomali mmoja hivi” Ray alisema huku sauti yake ikifichua hasira kidogo iliyokuwa inawaka moyoni mwake.

“Kauza shamba bila kuwasiliana na wewe?” Padre Kiko hakujali kama shamba liliuzwa kwa Msomali, Mndengereko au Mngoni. Lilomshtua kuwa uamuzi mkubwa wa namna hiyo unaohusisha mali za familia unaweza kuchukuliwa na mtu mmoja kwa namna hiyo.

“Hili shamba nilimnunulia na liko kwa jina lake; lakini ilikuwa ni mahali ambapo tulitaka kuanzisha miradi mbalimbali pale ya ufugaji na tayari tulikuwa tumeshajenga banda kubwa tu la ng’ombe na la kuku; ilikuwa baadaye mwezi Augusti tuanze kuingiza mifugo huko na yeye ndiyo angekuwa anasimamia miradi hiyo” Ray alisema kwa sauti yake nzito iliyochagua maneno vizuri, ikionesha jinsi alivyokuwa mtu wa kujipanga.

“Huwezi kuzuia au kwenda mahakamani kubatilisha?”

“Inawezekana lakini bado tatizo la msingi ndio linatusumbua kwani niliporudi nyumbani na kumuuliza kuhusu hili alianza kulia na kulalamika na nilipoulizia hizo fedha alizouzia shamba ziko wapi jibu lake ndio limenifanya nichague leo kuja kukuona.” Ray alimfafanulia Fr. Kiko ambaye toka waanze kuzungumza alikuwa bado hajanyanyua glasi ya maji. Na wakati huo Ray ndio aliamua kunyanyua glasi yake na kupiga mafundo mawili ya haraka haraka.

“Ni kweli nilikuwa nimetaka nikutafute nikujulie hali lakini hili lilinipa sababu nyingine ya kutaka kukutafuta Father” Ray alisema huku akionekana kujitetea kidogo. “Lakini tulipofikia nilihitaji kupata ushauri mapema vinginevyo ningejikuta nachukua uamuzi mbaya sana na wa hatari kwake na kwangu” Ray alisema kwa haraka haraka hasira yake ikiwa wazi kwa kugongagonga mkono wake kwenye meza ndogo iliyokuwa kati yao. Sauti ya glasi ilisikika zikidunda kidogo zilizisikika. Aliyaangusha macho yake chini kwenye sakafu kwa sekunde chache. Akatawala hisia zake.

“Umefanya vizuri sana kuja kuniona; na ni uamuzi vizuri kwa sababu mambo kama haya yanaweza kuishia mahali pabaya sana. Sasa fedha kazipeleka wapi?”

“Nilipombana sana alikiri kuwa amezipeleka kwa kanisa jingine la Mavuno kama mbegu yake kwa ajili ya kupata baraka ya mavuno kutoka kwa Mungu” Ray alisema kwa mara nyingine kwa sauti kama yenye kejeli isiyoamini katika mavuno.

“Kiasi gani kama hutajali mimi kuulizia”

“Milioni mia mbili”

“Yaani, zote kazipeleka huko?”

“Alikuwa amebaki na shilingi milioni ishirini tu kwenye akaunti”

“Au ana miradi mingine?”

“Ambayo miye sijui si itakuwa tatizo kubwa zaidi!”

Fr. Kiko na Ray waliendelea kwa muda kidogo kuzungumza kuhusiana na suala hilo na maamuzi ya kuchukua. Akiwa na uzoefu wa muda mrefu wa kazi za kichungaji Fr. Kiko alimshauri Ray wapange kukutana tena wiki moja toka siku hiyo na ikiwezekana aende na Sofia. Ray alijisikia unafuu kidogo moyoni na amani akilini. Alimshukuru Fr. Kiko na kumuaga akiahidi kurudi na mkewe wiki moja baadaye.

Ray aliondoka pale akiwa anajisikia mwepesi kidogo lakini pia akiwa bado na mawazo. Hakujutia uamuzi wa kwenda kumuona Fr. Kiko. Tatizo lake bado lilikuwa ni jinsi gani anaweza kuiokoa ndoa yake na kumfanya mkewe atambue kuwa njia ambayo ameichagua ni njia itakayomletea majuto baadaye.
 
SURA YA TANO


MTUMISHI WA MUNGU Ndondo alikuwa amemaliza kikao chake cha kwanza na wasaidizi wake kwenye majira ya saa tano na alikuwa anajiandaa kwa kikao kingine cha Wainjilisti wa Kanisa lake nusu saa baadaye. Kikao hicho cha kwanza kilikuwa ni cha kufanya tathmini ya mkutano wake ule mkubwa wa siku saba uliomalizika siku ya Jumapili iliyopita. Kikao hicho kilikuwa kinafanyika siku ya Jumanne kwenye ofisi yake pale pale Mavuno. Baada ya kulipa gharama zote za kuendesha mkutano huduma ya Ndondo ilikuwa imebakiwa na shilingi milioni mia tano na nusu kama faida. Kiasi chote cha fedha kilikuwa kinaingizwa kwanza kwenye akaunti ya mchungaji huyo.

Na kutoka huko yeye mwenyewe aliandika hundi ya shilingi milioni mia mbili hamsini kwenda kwenye akaunti ya kanisa lake. Fedha za sadaka za ibada za jumapili asilimia sabini ilienda kwenye akaunti yake ya kanisa na asilimia thelathini ilienda kwake. Asilimia ile sabini ndiyo ilitumika kulipia gharama mbalimbali za umeme, maji, usafi na kadhalika. Hata hivyo kwenye fedha za mikutano ya Injili asilimia zaidi ya themanini ilienda kwake na ile ishirini ilienda kwenye huduma ikiwemo kulipa kwaya, watumishi mbalimbali na gharama za mkutano. Askofu alikuwa anaingiza hela kutokana na mauzo ya DVD, vitabu, gazeti la Mavuno ya Mwisho na ada mbalimbali alizolipwa kuzungumza kwenye taasisi au mikutano mbalimbali ya kimataifa aliyoalikwa.

Karibu kila mwezi Ndondo alikuwa anaingiza kwenye akaunti yake si chini ya shilingi milioni mia tano akishalipa gharama zote za uendeshaji wa kanisa na huduma yake. Ndondo alikuwa ni tajiri, na labda neno tajiri halielezei kwa usahihi ukwasi aliokuwa nao mhubiri huyo namba moja nchini. Pamoja na magari ya kifahari ambayo zilikuwa ni “baraka za Bwana” Ndondo alikuwa anamiliki pia ndege ndogo ya kifahari ya Gulfstream 450 au maarufu kama G-IV. Ndege anayotumia Rais wa Tanzania ni kubwa kidogo ya Gulfstream 550. Pamoja na ndege na magari Askofu Ndondo alimiliki pia boti ya kisasa ya anasa ya Miromutu kwa ajili ya kuwaburudisha watu mashuhuri au watu ambao angependa kuwe nao katika hali ya upekee. Boti hiyo ya kisasa ilitengenezwa na kampuni ya kutengeneza boti hizi za kisasa ya Riva ya nchini Italia. Ukipata bahati ya kualikwa na Askofu Ndondo ama kwenye ndege yake au kwenye boti yake basi wewe ni miongoni mwa watu muhimu sana au kuna kitu muhimu sana anakihitaji kutoka kwako.

Kutoka katika ukwasi wake alikuwa na uwezo wa kuwakaribisha wahubiri wengine wa Injili ya Mafanikio kutoka sehemu mbalimbali duniani. Kinyume na makanisa mengine mengi ambayo hufadhiliwa wanapopata wageni, Ndondo alikuwa anawalipa wahubiri hao na kuwagharimia kila kitu. Miongoni mwa wahubiri maarufu waliowahi kufika nchini na kuhubiri katika kanisa la Mavuno ni pamoja na Askofu Keith Butler kutoka Kanisa la Word of Faith jijini Detroit, Michigan; Mchungaji Jesse DuPlantis kutoka New Orleans, Lousianna na mara mbili Mchungaji Benny Hinn kutoka Florida naye alishahubiri pale. Kanisa lilikuwa linajiandaa pia kwa ujio wa Mchungaji maarufu sana Joel Osteen kutoka Houston, Texas Marekani ambaye alikuwa anatarajiwa kuhubiri ibada tatu mwezi Juni. Mwaka uliopita alimkaribisha mtu ambaye alimuona kama mlezi wake katika huduma Askofu David Oyedepo kutoka Nigeria.

Baada ya kikao hicho cha tathmini ya mkutano kulikuwa na kikao cha kawaida cha uongozi wa kanisa lake ambapo alikuwa anafuatilia mambo mbalimbali na kufanya maamuzi. Mwili wake ulikuwa kwenye vikao hivyo lakini moyo wake ulikuwa ukitangatanga kwa mawazo ya matamanio ya vile vilivyokatazwa. Alikuwa anasubiria kukutana na mwimbaji Skola Kanuti ambaye alikuwa amemuomba wakutane saa tisa alasiri pale pale ofisini. Wazo hilo kila lilipomjia, moyo wake ulimpasuka.

Ofisi ya Askofu Damien ilikuwa inaendana kwelikweli na hadhi yake na ujiko wake kama kiongozi mashuhuri zaidi wa kiroho nchini. Waliwahi kuwepo wachungaji na wahubiri wengine waliowahi kulitikisa taifa na kuwa na wafuasi lakini hakuna aliyemfikia Askofu Damien Ndondo kwa ujiko wake, mbwembwe zake na kwa hakika kwa umahiri wake anapokuwa jukwaani. Kina Moses Kulola, Dunstan Maboya, Mwalimu Christopher Mwakasege, Geor Davie, Mwingira, Gwajima na wengine wengi hawakumfikia Askofu Damien. Hawa wote walikuwa na ujiko lakini Ndondo alikuwa na maujiko. Kama alivyoimba Diamond Platnumz, hawa wengine wote walikuwa “zilipendwa”.

Jengo la ofisi ya Askofu lilikuwa ni sehemu ya mkusanyiko wa majengo matatu ambapo yote yaliunganishwa na madaraja ya juu kwa juu maarufu kwa Kimombo kama skywalk. Madaraja hayo yalimwezesha mtu kutoka jengo moja kwenda jingine akipita juu kwa juu. Kanisa lake kubwa lilikuwa ndio kitovu cha eneo lote pale. Upande wa Mashariki wa kanisa kulikuwa na jengo la hoteli na hosteli za kisasa kabisa za nyota nne. Upande wa Magharibi ndiko kulikuwa na ofisi yake na majengo mengine ya kiutendaji yakiwemo ambayo yamekodishwa kwa makampuni mbalimbali.

Ofisi ilikuwa kwenye jengo la gorofa kumi na tano pembeni tu kidogo ya Kanisa lake kubwa. Jengo hilo lilikuwa limewekwa vioo kwenye kuta zote za nje na kulifanya liwe kama jengo la vioo vitupu. Pale maeneo ya Ubungo hakukuwa na sehemu nyingine iliyokuwa imejengwa na kukusanya majengo ya kisasa namna ile ukiondoa yale ya Chuo Kikuu cha Dar-es-Salaam. Tangu kufunguliwa kwa Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano na Makongamano wa Mavuno basi mikutano mingi ya Kimataifa ambayo ilikuwa inafanyika Arusha au Ukumbi wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere ilianza kuhamia pale. Kituo kile cha mikutano ya kimataifa kilikuwa na vyombo vya kisasa kabisa vya kuendesha mikutano yenye hadhi ya kimataifa, uwepo wa hoteli na burudani mbalimbali mubashara.

Saa tisa juu ya nukta, Skola Kanuti alikuwa anatoka kwenye lifti ndani ya jengo la ofisi ile akiwa anatazamana na sehemu ya mapokezi ambapo alichangamkiwa kwani alikuwa anatarajiwa.

“Bwana Asifiwe Da’Skola” alisalimia binti aliyekuwa pale mapokezi.

“Amen Regina, za masiku?”

“Nzuri tu dada”

“Pole na kazi”

“Asante dada, umependeza Da’Skola, Halleluyah!” alisema Regina sauti yake ikificha wivu fulani lakini akionesha tabasamu lililofichua mwanya mdogo.

“Amen dada, utukufu kwa Mungu” Skola alitabasamu kwa sekunde. Hakutaka kuendeleza maneno ya umbeya. Alikumbuka maandiko katika Zaburi ya kwanza yanasema wazi kuwa kuwa ana heri mtu yule asiyeketi barazani pa wenye mizaha. Alielekezwa na Regina kuelekea kwenye ofisi ya Askofu. Regina alibonyeza kitufye cha bluu kumuashiria Askofu ofisini kwake kuwa kuna ugeni unaelekea kule. Kwa namna fulani alimwelekeza si kwa furaha sana lakini kama mtu mwenye wivu wa aina yake. Kati yake na Skola hakukuwa hata na haja ya ushindani. Regina alijikuta anatamani kama Mungu angempa umbo kama lile la Skola na asilimia moja ya uimbaji wake.

Kama ngamia anayeshiriki mashindano ya urembo Skola alielekea taratibu ofisini kwa Askofu Mkuu. Hatua zake zilikuwa kama za kuhesabu na mwendo wake kama anayeogopa kukanyaga ardhi, lakini akiwa amejaa kujiamini. Sauti ya mchuchumio wake tu ndio ulisikika, tap tap tap. Ofisi ya Askofu Damien kwa makusudi kabisa ilikuwa imetanguliwa na vyumba viwili vikubwa vya mikutano upande huu na ule ambavyo vilifuatia tu eneo la mapokezi. Ukumbi wa mkono wa kulia ulikuwa umeandikwa juu mlangoni VIP Conference Room na ule wa kushoto uliandikwa Executive Room. Huo wa ER ulikuwa mahsusi kwa ajili ya wageni wakubwa wa kimataifa au wale wa kitaifa. Ulikuwa unaweza kuchukua watu 18 tu. Ule wa kulia ulikuwa na uwezo wa kuchukua watu thelathini tu; kumbi zote zikiwa na vyombo vya kisasa kabisa vya mawasiliano ya TV na kurusha kupitia mtandao wa intaneti.

Skola alikuwa amevaa sketi ndefu ya rangi ya bluu angavu iliyomfikia karibu kabisa na nyayo zake. Sketi hiyo ilikuwa na maua maua madogomadogo ya rangi nyekundu yakianza kwa wingi kutoka juu lakini yakipungua kuelekea magotini. Sketi ilipasuliwa upande wake wa kulia hadi kwenye magoti. Alikuwa amevaa viatu vya mchuchumio vya rangi nyeupe vikiwa na kamba zilizozunguka visigino hadi kwenye ugoko. Juu alivaa blauzi nyeupe iliyombana ya mikono mifupi. Ni wazi alikuwa ni binti ambaye alikuwa anafanya mazoezi ya kujenga mwili kwani mabega yake yalionesha misuli kama ile ya Michelle Obama. Alikuwa amemechisha bangili, mkufu pamoja na hereni zake vyote vikiwa ni vya dhahabu. Siku hiyo Skola alikuwa amefumua nywele zake na kuziachilia huru kichwani kwake na kumfanya aonekane kama mrembo ambaye anapaswa kutokea kwenye mojawapo ya kalenda za Victoria’s Secret au kwenye picha zinazouza mbuga mbalimbali kwa watalii. Nywele zilianguka pande mbili za mabega yake kama farasi jike aliyetunzwa vizuri.

Alipokaribia mlango wa ofisi ya Askofu Damien, mlango ulifunguka wenyewe na alikaribishwa na Askofu Damien mwenyewe akiwa amesimama pembeni tu ya mlango.

“Karibu Skola” alinyosha mikono yake kumkumbatia kirafiki.

“Asante Baba Askofu, Bwana Asifiwe” alimsalimia

“Karibu karibu sana” alisema Askofu Damien huku akimshika mkono kumuelekeza kwenye eneo lililokuwa na sofa na meza ndogo ya kahawa. Japo hiyo ilikuwa ni mara yake ya pili kuingia ofisini hapo Skola bado alikuwa ameachama mdomo wake katika hali ya kushangaa ukwasi uliokuwepo ndani hapo. Ilikuwa ni ofisi kubwa mno hasa kama ni kwa mtu mmoja. Zipo ofisi duniani halafu zipo OFISI. Ofisi ya Askofu Damien ilichukua nusu ya gorofa ikiwa imegawanywa sehemu tatu zote kubwa kabisa. Ukiingia tu kutokea mlangoni kama alivyofanya Skola unatazamana moja kwa moja na meza ya rangi ya kijivu iliyowiva ya Askofu Damien; juu yake kukiwa na kompyuta mpakato ya Mac ikiwa na rangi ya dhahabu; inaaminiwa kompyuta hizo ziko tano tu duniani zikitengenezwa kwa oda maalum.

Watu wanne wengine waliopata hadhi au ujiko wa kuwa nazo ni masheikh wa mafuta wa Saudia, Oman na Falme za Kiarabu pamoja na Rais wa Marekani Donald Trump. Kulikuwa na taa ya kusomea pamoja na simu ya ofisini. Hakukuwa na faili lolote pale mezani; kama Askofu alikuwa anafanya kazi yoyote yenye kuhusisha makaratasi basi alikuwa na sehemu nyingine au wanaosimamia ofisi wanajua anapenda usafi sana kiasi kwamba akimaliza kazi yoyote kila kitu kinarudishwa na kufanya ionekane tena kama ofisi mpya. Hata harufu ya ofisi ilikuwa ni harufu ya upya upya fulani.

Nyuma ya meza kulikuwa na kiti kikubwa cheupe cha ofisini kikiwa kimenakshiwa kwa dhahabu. Na nyumba ya meza hiyo na kiti kwenye ukuta kulikuwa na kabati kubwa ambalo lilikuwa limewekwa mapambo mbalimbali yakiwa yamepangwa vizuri kabisa pamoja na vitabu vichache ikiwemo Biblia kubwa. Kulia kwa meza ile karibu na ukuta kulikuwa na kabati dogo ambalo juu yake kulikuwa na mapambano ya maua pamoja na chupa za mapambo za rangi ya bluu. Na juu yake ukutani kulikuwa na picha kubwa ya pundamilia wawili wakitazamana.

Upande wa kulia wa meza ya Askofu kulikuwa na sehemu ya kukalia wageni. Upande huo kulikuwa na madirisha makubwa ya kioo yaliyoanza toka juu hadi chini. Kulikuwa na seti ya makochi makubwa ya rangi nyeusi matatu yakiwa yamezunguka ile meza ndogo ya kahawa ambayo juu yake kulikuwa na chupa kubwa yenye maua mekundu ya waridi.

“Unataka kinywaji chochote Skola?” Askofu Damien alimuuliza akielekea kwenye friji la vinywaji lililokuwa pembeni kidogo ya sehemu hiyo ya kukaa.

“Hapana Baba Askofu, asante” Skola alijibu na kuchagua mojawapo ya sofa na kuketi baada ya kuiweka sketi yake vizuri. Ofisi nzima ilikuwa ina ubaridi mzuri uliokuwa unatoka kwenye viyoyozi na kuhakikisha kuwa karaha ya joto la Dar havimsumbui Mtumishi wa Mungu. Skola alikuwa kama ua lililokuwa limekosekana ndani mle, manukato ya Tom Ford Tobacco Vanille aliyokuwa amejipulizia kabla ya kuja hapo kwa Askofu na taratibu yalifunika ile harufu ya upya.

“Hongera sana kwa huduma wiki iliyopita kwa kweli mlihudumu vizuri sana” Askofu alisema na kukata ukimya huku mkononi akishikilia glasi ya kinywaji kikali. Skola hakutaka kuamini kuwa Askofu alikuwa anatumia kileo.

“Baba Askofu unakunywa pombe!?” Skola alisema kwa mshangao kidogo lakini ni kama hakukusudia kwani ilikuwa ni kama kumhoji mzazi wake. Skola alimheshimu sana Askofu Damien; na labda neno heshima halikutosha kwa jinsi alivyokuwa anamheshimu; ni kama alimtukuza. Kumuona ameshikwa kinywaji kikali kulimshtua moyoni.

“Hapana, si unajua biblia inasema kwa maradhi ya tumbo?” alisema na kucheka kidogo kwa dharau fulani. Alienda kukaa kwenye kochi jingine la karibu na Skola lakini akiwa upande wa kulia wa Skola.

“Mmh” ndicho pekee Skola alichothubutu kusema na mara moja alijiona hakupaswa kuwa pale. Mwenyewe angeweza kusema kuwa alijihisi Roho Mtakatifu alikuwa anamshuhudia aondoke pale.

“Samahani Baba Askofu, nina miadi mingine jioni hii kwa hiyo uniwie radhi kama nitaonekana nina haraka kidogo”

“Bila ya shaka haitachukua muda mrefu; nashukuru kwa kuitikia wito” alisema Askofu Damien. Alimuangalia Skola kwa sekunde kadhaa na yale mawazo machafu yalimjia tena kama wimbi katika bahari ya takataka; alitamani mikono yake ingekuwa inamgusa na kumpapasa dada yule kwa namna ambayo malaika mbinguni wangeziba macho yao kwa aibu. Pamoja na ujanja wake wote Askofu Damien hakuwahi kujiona dhaifu mbele ya mwanamke kama alivyojisikia saa na wakati ule. Lakini alikuwa ni mtu mwenye ukwasi na hakuna mwanamke ambaye alimtaka ambaye hakumpata. Hilo lilimpa ujasiri wa uovu.

“Bila ya shaka Skola” Askofu alijibu. Alienda pembeni kidogo ya walipokaa ambapo kulikuwa na meza ndogo yenye madroo na kutoka huko alichukua bahasha kubwa nyeupe. Alirudi alipoketi Skola na kumkabidhi. Alipoipokea mikononi mwake Skola aliiminya kidogo na hakuwa na shaka kuwa ndani yake kulikuwa na kiasi cha fedha; swali ni alilobakia nalo lilikuwa ni kiasi gani na kwanini anapewa kwani tayari alishalipwa baada ya wiki ile ya Mkutano wa Injili.

“Mikononi mwako ni dola hamsini elfu kama shukrani yangu binafsi kwa kazi yako nzuri ambayo umekuwa ukifanya huduma kila tulipokuhitaji” alisema. Alama kubwa ya kuuliza ilisomeka kwenye uso wa Skola. Hakujua kama aseme asante au vipi; lakini machale ya kiroho yalikuwa yanamcheza kwa jinsi ambavyo Askofu alikuwa anamuangalia. Tangu aingie mle ofisini aliona jinsi gani Askofu alikuwa anamuangalia kwa namna ambayo haikumpasa mtumishi wa Mungu. Macho ya Askofu yalikuwa yanampapasa Skola kuanzia kichwani, yakitua kwa sekunde kifuani, miguuni na kiunoni; na labda yalifanya vitu vingine zaidi ambavyo dada huyo wa kilokole hakuwa tayari kufanyiwa na mtu huyo; vitu ambavyo mtu pekee aliyekuwa na haki navyo ni mumewe wa ndoa.

Ulipita ukimya wa sekunde chache. Skola aliiweka ile bahasha pembeni yake. Alikuwa amekunja mikono katika hali ya kutaka kuondoka mahali pale.

“Jambo la pili Skola naomba lisikukwaze hata hivyo” aliendelea Askofu Damien, “Skola nimetokea kukupenda sana na nimejaribu kujizuia lakini nimeshindwa. Natamani sana kuwa na wewe kimapenzi hata kama ni mara moja tu” alisema Askofu akimwimbisha Skola kama malaika kutoka kuzimu. Maneno yake yalisemwa kwa mpangilio, pumzi yake ikitoka kama mtu aliyekuwa ametoka kukimbia na anajaribu kuzungumza. Tamaa ilianza kumuwaka na kuamsha vitu vilivyokuwa vimelala chini ya suruali yake. Wazo la Skola kuwa mikononi mwake lilimfanya ajisikie hadi maumivu katika mishipa ya viungo vyake. Alijihisi damu inapwitapwita hadi kwenye viganja.

“Eh Askofu, unathubutuje kuniambia maneno kama hayo?” Skola aliamua kumtolea uvivu Askofu. Aliamua kusimama kabisa na kushika pochi yake aliyokuwa ameipakata. Hasira ilimshika lakini zaidi ni aibu ya kutoamini kama alikuwa anasikia maneno yale kutoka kwa Mtumishi wa Mungu.

“Kwanini nini jipya Skola? Mimi ni mwanamme na nimekiri udhaifu wangu kwako” alisema Askofu kwa upole lakini ndani yake kukawa na hifadhi ya radi ya tamaa.

“Yaani, kuna vitu vingi naweza kusema Askofu lakini” Skola alikatisha na kuamua kuanza kuelekea mlangoni walipoingilia. Kuufikia mlango ilimpasa ampite Askofu kwani alikuwa amesimama upande huo huo. Askofu alikuja mbele yake na kuweka mikono yake miwili kwenye mabega ya Skola. Skola alijaribu kujinasua lakini alisikia maumivu kidogo kwani Askofu alikuwa amemminya kwa nguvu. Kijasho chembamba kilianza kumtoka, hofu ilimuingia na moyo ulianza kumuenda kasi. Alipojaribu kumuangalia Askofu machoni alijawa na hofu zaidi kwani macho ya Askofu yalikuwa mekundu, yenye kutisha kama simba aliyekuwa tayari kumrarua swala.

“Skola, utanipa penzi lako leo hii na sasa hivi” sauti ya Askofu ilikuwa imebadilika, Maneno hayo machache aliyasema kwa haraka kama chereheani. Halikuwa ombi.

“Hapana baba Askofu siwezi, Yesu nisaidie” Skola alisema huku machozi yakianza kumlenga. Aliliitia jina la Yesu na kuomba aingilie kati. “Baba Askofu hii ni dhambi siwezi na hata wewe unawezaje hata kufikiria kitu kama hicho wakati una mke mzuri kweli jamani” alinung’unika. Kauli yake hiyo ilijaribu kumfanya Askofu ajisikie hatia na aibu. Lakini ilikuwa ni kama kujaribu kusafisha ndani ya jiwe kwa maji ya sabuni. Askofu alikuwa katika ulimwengu wa peke yake.

Skola alijaribu kutumia nguvu zaidi kujinasua na ndivyo hivyo hivyo Askofu naye alivyozidi kumbana kwa nguvu. Skola aliangalia kama akipiga kelele labda Regina angeweza kusikia lakini isingewezekana kwani palikuwa na umbali wa kutosha kati ya ofisi ya Askofu na eneo la mapokezi na ile ofisi ilikuwa imejengwa kuzuia sauti kutoka. Alitumia nguvu zaidi na kumsukuma Askofu nyuma na kufanikiwa kujinasua na Askofu aliserereka hadi karibu na meza yake na alifanikiwa kujishikiza kwenye kiti chake mbele ya meza yake.

Askofu kwa haraka aliingiza mkono kwenye droo ya upande wa kushoto wa meza yake. Alipoinuka alikuwa ameshikwa na hasira zaidi na mkononi alikuwa ameshikiliza bastola ya Glock G23. Alifura kama kifaru aliyejeruhiwa.

Skola alikuwa ameufikia mlango na anajaribu kuulazimisha ufunguke. Mlango ulikuwa umetiwa komeo la umeme na namna pekee ya kufungua ilikuwa kitufye kwenye meza ya Askofu. Mlango ulikuwa umetengenezwa kumlinda Askofu ndani na kuzuia mtu kukimbia au kuingia kwa nguvu ofisini. Ilikuwa ni mfumo wa usalama. Lakini pia alikuwa anasimamia mwenyewe nani anaingia au kutoka kama inavyodaiwa kufanywa na Matt Lauer yule mtangazaji wa Kimarekani kwa wanawake waliofanya kazi chini yake. Alijaribu tena kutikisa kitasa cha mlango bila mafanikio yeyote. Aligeuka taratibu katika hali ya kukata tama. Miguu yake ikipoteza nguvu zake. Alijikuta anasalimiana na na mdomo wa bastola. Alifungua kinywa chake kujaribu kupiga kelele lakini hakuthubutu kwani Askofu alikuwa ameweka kidole chake mdomoni kumuashiria asijaribu kupiga kelele.

“Nenda pale kwenye kochi” Askofu alimuagiza Skola akiwa hatua mbili tu kutoka kwake. Skola alikuwa anatetemeka mwili mzima. Vinyweleo vya mwili mzima vilisimama. Katika maisha yake kama binti alikuwa anaishi na hiyo hofu ya kuja kubakwa. Lakini katika maisha yake yote haijawahi kumtokea. Hata baada ya kuolewa kama wanawake wengine wengi alikuwa anaishi na hofu ya siku moja kukutana na uovu huo lakini hakuwahi kufikiria ingeweza kutokea kwa mtu ambaye alimheshimu sana na tena katika mazingira ya kutoweza kupata msaada wowote. Hakujua kuwa takwimu zinaonesha wanawake wengi wanaobakwa wanabakwa na watu wa karibu yao na wengine wapenzi wao.

“Askofu please don’t do this” Skola alisema huku machozi yakianza kububujika.

“Shut Up!” Askofu Damien alinguruma. Paji lake la uso la lilikuwa limetanda jasho licha ya ubaridi uliokuwemo mle chumbani. Alifungua vifungo vya shati lake huku akiwa anamuelekeza Skola kwenye kochi. Kwa kila kipimo Askofu alikuwa ni kama treni lililopoteza breki zake likiwa limeshindwa kupanda kilima cha Salanda. Alianza kufungua mkanda wa suruali yake. Skola aliangalia suruali ilivyokuwa inafunguliwa, aliona jinsi gani Askofu alikuwa katika hali mbaya ya mfadhaiko, mfadhaiko ambao alikuwa ameamua kuupigia magoti na kujisalimisha kwake. Moyo ulimuenda mbio, sauti ilimtoka kwa shida.

“Baba Please, please” alibembeleza kwa sauti iliyotetemeka, iliyopoteza ujasiri wote. Machozi aliyokuwa amejitahidi kuyazuia yalianza kutiririka bila ruhusa yake. Aliinamisha kichwa chake kama binti wa kifalme aliyenyang’anywa taji na watumwa.

“Unajiona mzuri sana kwamba huwezi kuwa na mimi; mbona wanawake wengi tu hawana maringo kama ya kwako” Askofu alimkandia Skola kwa maneno machafu, tena kwa kufoka.

“Vua nguo zako mwenyewe!” alimuamuru. Mtutu wa bastola ukiwa umewekwa pembeni ya kichwa cha Skola. Ubaridi wake ulimfanya Skola kujua kuwa hakukuwa na njia ya kutokea hapo. Hakukuwa na malaika kutoka mbinguni aliyeshuka kuingilia kati. Alikuwa peke yake. Askofu alikuwa amebakia na nguo ya ndani na vesti nyeupe.

Mungu wangu! Skola alijisemea moyoni. Miguu ilikuwa inamtetemeka kama majani ya mitende yakipigwa na maji mtoni. Hakuwa na uthubutu wa kutii agizo la Askofu. Macho yalikuwa hayawezi kuona kutokana na wingi wa machozi yaliyokuwa yakibubujika. Na siyo machozi tu, pua zake nazo zilikuwa ni mifereji. Hakuthubutu kuinua vidole vyake.

“Unataka nikusaidie kuzivua” Kwa sauti ya kukoroma tena huku akihema Askofu alimgutusha tena. Skola aliangalia kila namna hakuona jinsi, hakuna namna ya kukwepa tukio hilo, alikuwa amekamatwa kama kwenye mtego wa mwindaji.

“Kama umeamua kunifanyia hivi Askofu, ufanye utakalo lakini kwa hiari yangu sivui!” Ndio kauli pekee ya kijasiri ya mnyonge iliyoweza kutoka kinywani mwa Skola huku ikisindikizwa kwa kwikwi. Askofu hakufanya ajizi, hakufikiria mara mbili, hakuuliza tena wala kubembeleza. Alifanya kama vile ilikuwa ni mali yake. Hakujali uchungu au maumivu aliyoyasababisha, wala hakujali kama angeweza kumpa mimba mke wa mtu; au gonjwa na magonjwa.

Yesu nisaidie.

Mungu nisamehe.

Mume wangu, Simon. Jamani mume wangu.

Skola alifumba macho yake, hakuweza kupiga kelele. Maumivu ya shambulizi lile la aibu yalipasua mwili wake na kuuchoma moyo wake. Alimlaani askofu, alilaani siku yake ya kuzaliwa, alijuta kumfahamu Askofu Mkuu, Nabii, Mtumishi wa Mungu, Damien Ndondo.
 
SURA YA SITA


ALIPOAMKA KICHWA KILIKUWA kinambamiza kwa maumivu. Alijishika kichwa na kukitukania mamake. Alijaribu kukitikisa tena taratibu na kikamgonga zaidi. Alijikuta ameng’ata meno kwa ghafla. Alifumbua macho taratibu na kuangaza mle ndani wakati fahamu zikimjia taratibu. Alijihakikishia kwa macho yake kuwa hakuwa katika chumba chake, na kwa hakika hakuwa katika kitanda chake. Alijitambua mara moja kuwa chini ya zile shuka alikuwa mtupu kama alivyozaliwa. Alijaribu kukumbuka starehe ya usiku uliopita, hakuweza kukumbuka kila kitu. Anakumbuka jinsi walivyojirusha kwa muziki wa kina P-Square na kina Neyo, miziki ya kuchangamsha damu ya kina Gwen Estafan na miziki ya kina Ali Kiba na Diamond. Akakumbuka wimbo wa Ndi Ndi Ndi wa Lady Jay Dee hakuweza kukumbuka kilichofuatia baadaye.

Alichokumbuka ni kuwa wakati wimbo huo unaanza alikuwa amefuatwa na mbaba mmoja wa makamo. Alijaribu kumkumbuka na ndipo fahamu zilipomjia kuwa pembeni kitandani alikuwepo mtu mwingine ambaye hata jina halikumjia mara moja. Mzee yule wa makamo alikuwa ni mmoja wa wazee wanaofahamika sana Jijini Dar kwa kujirusha na vibinti vidogo vidogo. Mabinti waliopita kwenye kiuno chake walimuita “Babu Powa”. Alikuwa ni mmojawapo wa Wakurugenzi Waandamizi Makao Makuu ya Mamlaka ya Mapato Tanzania. Pamoja na ajira yake iliyompa kipato kizuri alikuwa na “vimiradi” vingi karibu kila kona ya nchi. Kuna watu walikuwa wanasema alikuwa kwenye mashindano na bosi mwingine pale ambaye alikuja kutimuliwa Rais mpya alipoingia madarakani.

Mabinti walikuwa wanamtaja kwa furaha kwani wengi waliweza kuishi mjini kwa ajili yake. Na hapo ni wale wa Dar tu; alikuwa na mabinti wengine Mwanza, Mtwara, Arusha na Mbeya. Na alikuwa na binti wa kiarabu Darajani Zanzibar. Hapo wale aliowapitia mara moja katika safari zake sehemu mbalimbali hawakuhesabiwa.

Fela alikumbuka kuwa rafiki yake mmoja walioenda naye kwenye ile tafrija ndiye aliyemtambulisha kwa mzee yule usiku ule. Mzee alimchangamkia kwa kumsifia alivyovaa na hakuchelewa kuanza kumshika mkono, mara kiuno mara hivi mara vile kama mbwa anayedai umiliki wa mfupa wake. Alijaribu kumnong’oneza maneno matamu lakini Fela hakuyakumbuka. Anakumbuka waliletewa vinywaji ambavyo vilikuwa vimeagizwa na Mzee yule na baada ya hapo hakuweza kukumbuka tena.

Alimuangalia mzee yule pembeni yake akiendelea kukoroma na mara jina lake likamjia; aliitwa Godlisten Shayo. Kwa sura mzee yule alikuwa na changamoto ya kudumu, lakini vingine alikuwa navyo. Alikuwa mtundu kitandani utadhani kijana wa miaka ishirini na mitano. Na wasichana walisifia hilo “game” lake kama wenyewe walivyoita. Na enzi zake za ujana ni utundu huo uliompatia wanawake kiasi kwamba hakujua idadi halisi ya watoto wake. Hofu yake ya mara kwa mara ilikuwa ni siku akifa watoto wake watakuja kukutana msibani. Ni hofu ya wazee wengi inakisiwa.

“Oh umeshaamka darling” Shayo alishtuka na kutabasamu akimuangalia Fela katika utupu wake; moyo wake ukiwaka tamaa tena. Mzee alitaka raundi nyingine.

Fela hakuweza kusema kitu, ila alikuwa amejaa aibu. Aliinuka huku akivuta shuka moja na kujizuia nayo kifuani. Aliokota nguo zake zilizokuwa zimezagaa sakafuni na kuelekea bafuni kubadilisha. Alipotoka hakuweza hata kuthubutu kumuangalia mzee Shayo. Alisema kwa aibu kidogo kuwa alipenda kurudi nyumbani. Shayo alichukua paketi ya sigara iliyokuwa pembeni kwenye meza ndogo pembeni ya kitanda na kuchomoa sigara moja na kuiwasha kwa kiberiti cha gesi kilichokuwa pembeni ya paketi hiyo ya sigara.

Shayo alichukua simu yake iliyokuwa hapo hapo ilipokuwepo paketi ya sigara na kubonyeza namba moja na akazungumza na mtu kumuagiza kuwa mgeni wake alikuwa anatoka na ampeleke hadi nyumbani kwake.

“Dereva atakuwa hapa kama dakika ishirini tu kukupeleka nyumbani. Nitafutahi sana kama nitaweza kukuona tena Fela” Shayo alisema kwa sauti nzito yenye mikwaruzo na lahaja nzito ya Kichagga. Fela hakusema lolote aliangusha macho kwa aibu tu na tabasamu la uongo na kweli. Moyoni alikuwa anajisikia kinyaa na hasira. Lakini ndio mjini alivyoishi. Alivuta pumzi na kujilazimisha kuitikia ombi.

“Nitafurahi pia” alisema kwa sauti ya kinyonge. Mzee Shayo alivuta kidroo kidogo kwenye ile meza ya pembeni na kuchukua bahasha. Alimkabidhi Fela huku akimwambia kuwa akimhitaji tena atamtafuta. Fela aliitikia akichukua makorokocho yake kwenda bafuni kujimwagia maji. Alipotoka usafiri ulikuwa tayari chini. Aliondoka hapo baada ya kumuaga Shayo huku akiapa hatokaa kitandani na bwana huyo tena. Isingekuwa msururu wa magari angefika nyumbani kwake dakika ishirini tu; lakini kwa vile ni Jiji la Dar ilimchukua dakika arobaini na tano.


Alipofika nyumbani kwake Fela alijihisi kama kizunguzungu kikimjia mara tu baada ya kuingia ndani na kufunga mlango. Ile fedha na aibu ambayo alikuwa nayo tangu atoke kwa Shayo iliongezeka mara kumi zaidi. Alijihisi kichefuchefu kikimjia kwa nguvu; alikimbia moja kwa moja bafuni bila hata ya kuvua viatu. Alirusha mkoba wake sebuleni wakati akifanya hivyo. Alipoingia bafuni alijaribu kutapika kwenye sinki lakini hakuna chochote isipokuwa mate tu; alikumbuka kuwa hakuwa amekula chochote jana yake zaidi ya vile vinywaji vikali. Machozi yalianza tena kububujika. Alijihisi ni mchafu; hakuamini aliuachia mwili wake uguswe na kuchezewa na mtu kama Shayo; lakini hakuwa Shayo tu aliyeugusa na kuuchezea mwili wake. Walipitia wengi; kulikuwepo Waziri, Naibu Waziri, Mkuu wa Wilaya moja ya Arusha asiyekosekana kwenye TV kwa kutafuta ujiko, Padre mmoja, Wakufunzi kadhaa wa chuo kikuu cha UDSM, na wengine ambao hakuwakumbuka hata majina. Hata shehe mmoja kutoka BAKWATA naye alishauonja mwili wake. Alipojaribu kukumbuka wanaume hao alijihisi tumbo likimuuma na kumbana. Alinawa usoni na kujipangusa.

Alipojiangalia kwenye kioo hakupenda alichokiona. Fela alijikuta akijichukia. Alichukia kila alichokiona kikiakisiwa kwenye kioo kile. Hakupenda nywele zake, hakupenda midomo yake, hakupenda macho na sura yake kama vile ambavyo hakupenda kuangalia kifua chake. Vitu vyote hivyo vilikuwa ni kivutio kwa wanaume wa kila kona; lakini kwake vilikuwa ni sababu ya laana na fedheha; ilikuwa ni tiketi ya kutumikishwa katika mapenzi.

Fela alijikuta akipata donge kooni kwani alijiona kuwa hakuwa na tofauti na machangudoa wanaojiuza kila usiku kwenye mitaa ya Dar-es-Salaam. Alifikiria labda siku moja mambo yakiwa magumu anaweza kweli kujikuta anafanya hivyo kwani tayari mara kadhaa ameshaenda kukutana na watu kimwili kwa sababu ambazo aliogopa kuzifikiria na alijua uwezekano wa kufanya hivyo tena ulikuwepo kama ulivyo uwezekano wa yeye kupumua tena. Alivua nguo zake zote alizokuwa ametoka nazo kwa Shayo na kuzitupa pembeni karibu na mlango. Alikaa chooni kwa dakika chache akijaribu kujisafisha alikodhania kumechafuka sana. Hakuridhika. Kwa mara nyingine tena alijikuta anataka kuoga tena. Aliingia bafuni baada ya kujaza sinki la bafu maji na kuweka sabuni ya mapovu.

Mwili wake ulipogusana na maji yale ya vuguvugu ilikuwa ni kama aliyekumbatiwa na mamaye; alijiachia na kujiegemeza bila kufanya lolote huku mawazo yake yakimpeleka mbali, yalimbeba na kumpeleka siku ile akiwa anahitimu elimu ya kidato cha nne. Siku ambayo iliacha donda kubwa kwenye moyo wake na kumvuruga katika mahusiano yake ya mapenzi.

Alipomaliza kuoga alijisikia kuchangamka kidogo; alienda chumbani na kubadili nguo na kuvaa suruali yake ya jeans na blauzi ya rangi nyeusi iliyoandikwa maneno ya I Love You. Alikuwa na hamu ya kitu chenye utamu wa sukari. Alifungua friji yake na kuchukua juisi ya machungwa na kujaza glasi na kukaa chini kunywa taratibu huku akiangalia TV asubuhi hiyo.

Bila hata kupenda au kuombea alijikuta kwa mara nyingine tena mawazo yake yalimvuta kama kwa mnyororo kurudi kule ambako hakutaka kwenda. Mawazo yake yalimrudisha kule Iringa Girls kwenye ile siku ya mahafali ya kidato cha nne. Kwa kadiri alivyojitahidi kukwepa kufikiria ndivyo kumbukumbu zilivyo kuwa zinamjia kwa nguvu. Akaona isiwe shida akaamua kwenda kutafuta dawa ya kushughulikia kumbukumbu hiyo mbaya.

Ilikuwa ni siri yake nyingine, siri yake kubwa ya pili. Hata marafiki zake wengi walikuwa hawaijui. Aliingia chumbani kwake na kwenda kwenye droo ya chini kabisa kwenye meza yake ya kujipodolea iliyokuwa karibu na kitanda chake. Droo ya chini mwisho kulia baada ya kupangua chupi zake alikuta vifurishi vidogo vidogo viwili kama vya dawa za mganga wa kienyeji zikiwa na unga unga mweupe. Alichukua kimojawapo na kukiweka mezani pale.

Alikaa mbele ya meza na kujiangalia mbele ya kioo kikubwa kilichokuwa kimeshikimana na meza ile. Alipojiangalia uso wake macho yake yalikuwa yamevimba. Alifungua kile kifurushi kidogo na kumwaga kidogo ule unga mweupe. Kilichobaki alikifunga tena na kukirudisha chini kwenye droo. Alichukua kiwembe kilichokuwa kwenye kibakuli kidogo chenye vifungo na sindano na nyuzi za kushonea nguo. Kama mtaalamu anayejua anachofanya aligawa ule unge kwa kiwembe kile katika mafungu matatu madogo yaliyokuwa yanaonekana kama mstari mweupe hivi; yalikuwa kama matuta madogo ya unga mezani. Alikumbuka ile bahasha aliyopewa na Shayo ilikuwa bado iko sebuleni aliirusha kwenye meza ya kahawa wakati ameingia ndani tu kabla ya kwenda bafuni. Aliiendea mara moja na kuingia nayo chumbani na kuketi nayo pale kwenye meza na kuifungua. Ndani kulikuwa na noti kumi na tano za shilingi elfu kumi kumi.

Alichukua mojawapo na kuivingirisha mkononi na kutengeneza kama mrija mdogo. Aliinamia ule mstari wa kwanza wa unga wake, huku akifunga tundu moja la pua kwa kidole cha mkono mmoja aliingiza upande mmoja wa ule mrija wake wa noti ya shilingi elfu kumi kwenye tundu jingine la pua. Alivuta pumzi ya nguvu wakati anaupitisha mrija ule juu ya ule unga na kuuvuta kama mashine zinazotumika kuvuta vumbi ndani ya nyumba. Mstari mmoja ukaisha kama utani. Alijisikilia dawa ile ya Cocaine ikipenya kwenye matundu ya pua yake na kumpa hisia kali kwenye damu yake.

Akakata mwingine kwa wembe wake na kurudia; alifanya hivyo mara tatu na kujikuta yuko katika ulimwengu mwingine. Alijipangusa usoni na kujisafisha pua yake wakati unga ule ukianza kufanya kazi mwilini mwake kumpa kile alichoamini kuwa ni starehe kupita kiasi. Alijihisi mwili umechangamka na furaha ya ajabu. Hofu yote na kumbukumbu zote mbaya zilimpita. Alijihisi amekuwa kama mtu mwenye nguvu za ziada tena za ajabu.

Hakutaka kufanya kitu kingine chochote isipokuwa kulala kwanza huku akijisikiliza kile alichoamini ni uhondo kupita kiasi. Alianza kuona viumbe wa ajabu ajabu vikielea ndani ya chumba chake, wengine walikuwa ni kama vipepeo wenye mapembe, na wengine walikuwa ni kama sisimizi wenye ukubwa wa punda, alijisikia raha na wakati huo huo alijihisi mwenye wasiwasi. Ilikuwa ni mchanganyiko wa utamu na uchungu vyote vikiwa na ladha ya pekee katika mdomo wake. Fela alikuwa anaelea katika mbingu aliyojiundia mwenyewe.
 
SURA YA SABA

WIKI ILIYOFUATIA SIKU ya Jumapili Ray aliambatana na mke wake hadi kituo cha Agape kama walivyokuwa wamekubaliana na Padre Kiko wiki moja kabla. Jumapili hiyo ilikuwa ni ya jua kali siyo kama ile iliyotangulia. Kama ilivyokuwa wiki moja kabla safari hii tena walifika wakati ambapo ibada ya misa ilikuwa imeisha na tayari watu walikuwa wameshakula na kwenda kwenye mapumziko ya mchana. Sofia alikataa kushiriki ibada ya Kikatoliki japo alilelewa utotoni katika ukatoliki hadi alipoamua kuanza kwenda kwenye makanisa ya Kilokole.

Waumini wanaokaa maeneo ya jirani na pale Agape walikuwa tayari wametawanyika na pale kituoni palikuwa panaelekea katika hali ya ukimya. Ray alikuwa amevaa suruali ya jeans na shati la rangi nyekundu lililokuwa na miraba miraba ya rangi nyeusi. Shati lile jepesi liliweza kuonesha vesti nyeupe aliyokuwa ameivaa chini na hivyo kuonesha ni jinsi gani Ray alikuwa ni kijana wa miraba mine. Walipofika walipokelewa kwa ukarimu wote kama ilivyokuwa kawaida ya Agape na kwa vile walikuwa wanatarajiwa basi walielekezwa moja kwa moja ofisini kwa Padre Kiko ambaye alikuwa anawasubiria kwa hamu.

Pd. Kiko kwa upande wake alikuwa amevaa kanzu yake nyeupe ya kichungaji ikiwa na mkanda wake mweusi ambao unajulikama kama fascia ambao huwa unaning’inizwa upande wa kushoto pembeni kidogo tu ya usawa wa paja la kushoto. Kama kawaida yake alikuwa kihuduma zaidi. Ilikuwa ni nadra sana kumkuta Kiko akiwa hajavaa aina yoyote ya mavazi ya kichungaji.

“Karibuni sana” Fr. Kiko aliwakaribisha huku Ray akimtambulishe mkewe kwa Padre Kiko.

“Asante sana Father, Tumsifu Yesu Kristu” Ray alimsalimia Padre Kiko.

“Milele Amina”

“Mke wangu Sofia, Sofia huyu ni Padre Kiko mwalimu wangu nikiwa seminari” Ray aliwatambulisha huku akitumia mkono wake kuwaashiria.

“Shikamoo Padre, nashukuru kukufahamu” Sofia aliitikia utambulisho lakini hakutaka kutumia salamu ya kikatoliki.

“Mimi vile vile, karibu sana” Padre Kiko alimpa mkono Sofia na kuwakaribisha.

Sofia hakuweza kusema tu lakini ukweli ni kuwa hakutaka kuwepo pale na ni kwa vile mumewe alimlazimisha tu ndio maana alikubali. Kilichomtibua zaidi ni wazo la kwenda kwa Padre wa Kikatoliki kutafuta ushauri wa ndoa kwa mtu ambaye hajawahi kuoa. Hilo lilimtibua zaidi kuliko kuliko hata matatizo aliyokuwa nayo na mumewe.

Haikuchukua muda mrefu baada ya kupata vinywaji vya soda na biskuti kabla hawajaanza kuingia kwenye mazungumzo yaliyowaleta pale. Aliyeanzisha mjadala alikuwa ni Padre Kiko mwenyewe aliyemkaribisha Sofia kwa kuelezea kwa ufupi mkutano wake na Ray wiki iliyotangulia. Alielezea manung’uniko na hofu ya Ray juu ya kile kinachoendelea hasa masuala ya imani ambayo inaonekana kama Sofia alikuwa ameyapeleka katika ngazi nyingine kabisa. Kwa kadiri Fr. Kiko alivyokuwa akizungumza alizidi kuona jinsi gani uso wa Sofia uliokuwa ukikunja ndita. Lakini Fr. Kiko aliendelea kwa utulivu na kwa kuchagua maneno taratibu.

“Sofia, wewe unaonaje kuhusu aliyoyasema mwenzako” Fr. Kiko alimuuliza Sofia huku akimkazia macho.

Sofia bado alikuwa ameinamisha kichwa chake kama kwa aibu fulani hivi ya mtoto wa kike anayezungumza na babake. Taratibu kama asiyetaka lakini aliyelazimika alijiinua na kukaa huku akiegemea kiti kwa upande kidogo kama anayegoma. Alivuta pumzi ndani kwa sauti kidogo kidogo halafu na kuishusha taratibu. Aliiuma midomo yake kidogo na kuguna kama mtu ambaye alikuwa na hasira lakini asiye tayari kusema kitu. Mikono yake alikuwa ameituliza kwenye magoti yake huku vidole vikiwa vimeshikana. Kwa sekunde kadhaa hivi alikuwa anaiminyaminya mikono yake taratibu; alimuangalia kwanza Ray kwa jicho la pembeni halafu akayarudisha macho kwenye mikono yake.

“Mimi kwa kweli sina la kusema; sijaelewa tu kwanini matatizo yetu ya nyumbani ameyaleta kwako” alisema Sofia kwa sauti ya kiburi kidogo na yenye kutoa shutuma ndani yake. Sauti yake ikitetemeka.

“Kwani kuna ubaya gani?” Ray aliunguruma na yeye hakuficha hasira yake. Sauti yake ilitoka kwa nguvu kidogo na kumshtua hata Fr. Kiko pale. Kiko alijua mara moja nini kinaweza kutokea kama hatodhibiti mazungumzo hayo.

“Taratibu Ray, taratibu!” Fr. Kiko aliingilia kati akimuashiria kwa mkono wake wa kulia. “Ngoja tumsikilize mwenzako halafu kila mmoja atatoa maoni yake, lengo ni kuelewena na kujua mtazamo wa kila mmoja. Hakuna sababu ya kugombana au kubishana” aliendelea Fr. Kiko kwa sauti iliyokuwa imetulia isiyoonesha hisia zake. Miaka karibu arobaini ya uchungaji ilimuandaa kwa mambo mengi na aliyasikia mengi katika maisha yake yale ya kichungaji na katika chumba cha maungamo. Hili la Ray na Sofia lilikuwa ni moja tu. Tofauti ni kuwa Ray alikuwa ni kama mtoto wake wa kumzaa mwenyewe. Fr. Kiko alikuwa akijiambia mara nyingi kuwa kama angekuwa amezaa mtoto wa kiume basi angeona fahari sana angekuwa kama Ray.

“Ehe endelea Sofia” Kiko alimuashiria Sofia kuendelea.

“Padre, kusema ukweli mimi sijafurahia. Kila mtu kwenye ndoa ana matatizo yake ya aina mbalimbali na watu huzungumza huko na kujaribu kuyatatua” Sofia aliendelea pale alipoishia kabla Ray hajaingilia sauti. “Sasa nimeshangaa mwenzangu kaja huku wakati miye nimemuomba mara kadhaa twende kwa Askofu Ndondo lakini amekataa kabisa” alisema huku akimrudishia tuhuma mmewe.

“Siwezi kwenda kwa tapeli Father!” Ray alirukia baada ya kushindwa kujizuia. Hasira na dharau zake zikiwa wazi kabisa. Hakusema kwa sauti bali alikuwa ameamua kuchomekea tu, akirusha mkono pembeni kama kupuuzia.

“Yeye ni mtumishi wa Mungu, unajua watu wangapi wamebarikiwa kwa huduma yake? Unajua kina mama wangapi wamejaliwa kupata watoto na mafanikio ya kila namna kwa kuombewa naye? Askofu Ndondo ni kama T.B. Joshua kabisa wa Tanzania” Sofia alimtetea Askofu Ndondo kama mtu aliyekuwa analipwa kumtetea.

“Kwa hiyo sababu kubwa ya kwenda huko ni kwa ajili ya kutaka kuombewa?” aliuliza Fr. Kiko.

“Ni zaidi ya kuombewa, miye ninabarikiwa sana kule! Siyo kama huku kwa Wakatoliki! Kule, tunamuabudu Mungu kwa uhuru, na Mungu anafanya miujiza mikubwa kila siku” Sofia aliamua kuwatolea uvivu; aliamua kuwapiga gombo. Aliendelea kuwahubiria “na kule kwa Mtumishi wa Mungu Ndondo watu wanaishi kwa Neno kweli kweli” Sofia alirusha mishale yake kama kutoka kwenye podo la mwindaji mahiri. Hakujali nani inamgusa au nani anaumia. Alitumia mikono yake kujieleza kama mwalimu wa shule ya msingi.

“Na unaona kuwa kule kwa Ndondo kuna chakula kizuri zaidi cha kiroho” alisema tena Fr. Kiko kama kumfanya Sofia aendelee kutiririka.

“Kweli kabisa!” alidakia Sofia na kuendele akiombea moyoni labda Padre Kiko anaweza kukubali hoja zake. Alifafanua kuhusu manufaa anayoyapata kinamna akilinganisha na yale yanayopatikana kwenye Kanisa Katoliki “chakula cha kiroho ni kipya kila siku. Kuna mafundisho ya kila namna na yanamjenga mtu kiroho. Jumatatu wanakutana vijana, Jumanne ni huduma ya kuombea wagonjwa na wenye matatizo mbalimbali” hakusimama kupumzika maana alikuwa anazungumza kama hotuba ya mshindi wa tuzo ya Oscar. “Jumatano ni masomo ya Biblia, Alhamisi kina mama tunakutana na kufanya intercession na Ijumaa ni kufunga. Jumamosi wanakwaya wanakutana na Jumapili ni siku ya ibada” aliendelea kuzungumza bila kuvuta pumzi. Hoja yake ni kuwa maisha ya kiroho yalikuwa yanalelewa vizuri zaidi kwa Ndondo kuliko kwa Wakatoliki.

Alipofika mwisho hapo alimeza fundo kubwa la mate na kushusha pumzi. Alichukua glasi ya maji na kupiga mafundo mawili. Ingekuwa kwenye umati mkubwa wa watu wangesimama kumpigia makofi. Ray na Fr. Kiko walikuwa wanamsikiliza kwa makini kabisa. Fr. Kiko alijua Ray amepata mshindani kwenye masuala ya kujenga hoja. Ray mwenyewe kwa namna aliona fahari kwa jinsi mke wake alivyokuwa anajiamini. Ingekuwa mazingira mengine Ray angempongeza mkewe.

“Na unaona Ray hashiriki katika mambo hayo ya kiroho?” Kiko alimgongelea kwa swali jingine kama mwendesha mashtaka akimuongoza shahidi muhimu kizimbani.

“Siyo tu hashiriki, ananipinga kwa kila kitu” Sofia alijibu kwa sauti ya juu kidogo. Aliposema maneno hayo alikaa viizuri na kumuelekea mumewe moja kwa moja. “Tuna miaka mingapi hii hatujajaliwa mtoto; tumeenda kwa kila daktari hapa nchini lakini hakuna mafanikio, mwenzangu yeye ameweka mkazo wake huko kazini sijui anataka kuwa nani katika nchi hii. Na mimi umri ndio unaenda hivyo” alisema huku sauti yake ikipanda kufichua hasira iliyojificha ndani yake. Macho yake yalianza kutengeneza madimbwi. Alivyomeza fundo lile la mate na machozi yakamdondoka. Fr. Kiko alimpa tishu nyepesi ya kujipangusia machozi.

“Ray unasemaje kuhusu aliyoyasema Sofia hapo?” Fr. Kiko alimuuliza Ray ambaye alikuwa anamuangalia mke wake kama mtu aliyekuwa anashuhudia mwigizaji aliyebobea. Upande mmoja hata hivyo alijikuta anaona huruma lakini upande mwingine akijua kabisa ni nini kilicho kwenye matatizo baina yao. Fr. Kiko alijiinua kidogo kujikalisha vizuri kwenye kochi lake kumsikiliza kijana wake.

“Fr. Kiko, tatizo langu na mke wangu siyo mtoto - at least not from where I stand” alianza kujieleza kuwa yeye alivyoona tatizo halikuwa kupata mtoto. “Tatizo letu ni mahusiano na kutosikilizana. Mtoto kwa kadiri ninavyofahamu mimi siyo haki ambayo unaweza kumdai mwenzako kana kwamba naye ana uamuzi wa mwisho wa kumtoa mtoto” alijieleza kwa sauti kavu, iliyochagua maneno herufi kwa herufi, kituo kwa kituo. “Tumekuwa tukijaribu miaka yote lakini hatujajaliwa, sote tumeenda kwa madaktari na hawaoni matatizo yoyote; miye simlaumu yeye na sijilaumu mwenyewe maana kama kujaribu tunajaribu sana!” Alisema na kuweka msisitizo kwenye neno sana na kumfanya Kiko aelewe amemaanisha nini.

Baada ya kumeza fundo la mate aliendelea “Sasa kama njia za kisayansi zote zimeshindikana huku kwingine tunaenda kutafuta mambo ya kishirikina tu na baadaye kujiletea matatizo”

“Kwani kuombewa ni ushirikina?” alidakia Sofia akionesha hakuwa tayari kuburuzwa. “Nilikuwa naenda kwa waganga wa kienyeji wa kila sehemu na wengine niliwaleta hadi nyumbani, mwenzangu akagoma kabisa na kuwafukuza, sasa nimeamua kujaribu kwa mambo ya sala bado yeye anaona ni ushirikina!” alisema kwa sauti ya juu kidogo akiona kama amekata tamaa.

Ray naye hakuwa tayari kusalimu amri; “Ni aina ya ushirikina hasa kwa hawa wahubiri uchwara ambao unaenda kwao, watu wanataka utoe sadaka sijui za kila namna gani ili ati mtu abarikiwe; sasa wana tofauti gani na waganga wa kienyeji wanaotaka watu wapeleke mbuzi, kuku na bata” alisema sauti yake ikizidi kuonesha hasira. Midomo yake ilikuwa imeanza kumkauka, akachukua na yeye glasi yake ya maji na kupiga fundo moja na kujilamba kidogo.

“Siyo ushirikina ni imani na…” Sofia alijibu mapigo kutetea imani yake.

“Ushirikina ni imani vile vile” Ray alimkatiza bila kufikiria.

“Twende taratibu” Fr. Kiko aliamua kuingilia kati kwani aliona sauti zinazidi kupandiana juu kama ngazi. “Sasa hili suala la fedha na viwanja ni vipi Sofia maana inaonekana hapa ndipo hasa mwenzako anaona kama ndio msingi wa hofu yake kwamba unaweza kuleta umaskini kwenye nyumba hasa unapofanya maamuzi kama haya bila kumshirikisha au kukubaliana na mwenzako?”

“Kwa mtu alivyo hivi ningemwambia natakiwa kutoa sadaka unadhani angekubali?” Sofia alijaribu kuelezea kwa sauti ya kejeli kidogo. Aliamini ametoa sababu ambayo ilikuwa ina mantiki ya aina fulani hivi. “Inawezekana nilikosea na hapo naomba msamaha lakini tayari imefanyika siwezi kwenda kwa Askofu na kumdai tena” alisema huku sauti yake ikiwa imebeba aina fulani ya kutokuaminika na yeye mwenyewe akigeuza macho yake kuangalia dirishani.

“Lakini vipi kuhusu kuachana na hilo kanisa?” Kiko alimuuliza moja kwa moja bila kuzungusha maneno.

“Ah, sasa mambo ya imani Father ni imani ya mtu, kama yeye anaamini katika ukatoliki na kaja hapa kwako na mimi nina haki ya kuamini ninavyoamini” alisema Sofia. Wote wawili Fr. Kiko na Ray walikosa majibu ya moja kwa moja kwani kweli Sofia alikuwa na hoja hapo. Kiko alijua kuwa kwa kuzungumza tu Sofia alikuwa na kipaji kwani ni miongoni mwa vitu vilivyomvutia Ray hata kufikia kumtongoza, kuchumbia na hatimaye kumuoa. Sofia alikuwa na shahada ya pili katika uandishi wa habari na wakati anakutana na Ray alikuwa ameanza kazi Televisheni ya Taifa kama Mhariri Mwandamizi Msaidizi.

Kama fahari wawili waliokuwa wameshikana mapembe wakigomeana ushindi, Ray na Sofia walikuwa wamekamatana. Hawakuwa na mengine ya kusema isipokuwa kwa siku ile waliamua kukubaliana kutokukubaliana na kupingana bila kupigana. Jioni ilikuwa imeanza kuingia na Fr. Kiko alikuwa ana kikao cha kupanga wiki ya waombeaji ambayo Agape walikuwa wanaiandaa kwa wale wenye huduma ya kuombea wengine. Ni huduma kama ya kanisa la Ndondo ambapo watu wenye karama ya kuombea walikuwa wanakutanika kufanya maombezi. Makanisa mengi ya Kipentekoste yana vikundi vya waombeaji na Wakarismatiki wa Kikatoliki nao walikuwa na vikundi kama hivyo hivyo.

Waliagana na Fr. Kiko aliwasihi kuwa itakuwa vyema wakitafuta muda mwingine mzuri zaidi waje tena kuzungumza naye. Aliwapa maongozi mengine ya kiroho na kimaisha kama baba kwa watoto wake. Ray aliyashika moyoni lakini Sofia yaliingia sikio moja na kutokea kwingine, tena yakitoka mkuku.

Walipoondoka pale Agape hawakuzungumza kabisa. Sofia alikuwa anaangalia nje ya dirisha la gari. Majaribio yote ya Ray kumsemesha yalikuwa kama kujaribu kukinga mikono kusubiria mvua jangwani. Moyoni Sofia alikuwa amekasirishwa sana lakini pia aliamini kabisa kuwa mume wake alikuwa na mapepo na hakuwa tayari kumpa shetani nafasi kwani aliamini shetani alikuwa hataki afanikiwe. Alikuwa ametulia moyoni anakemea mapepo yale na alidhamiria kabisa kuwa akipata nafasi tu atafanya mpango akazungumze na Askofu wake kumueleza matatizo yake.

Kutokana na sadaka zake na kujitolea kwake kwenye shughuli mbalimbali za kina mama pale kanisani Sofia alikuwa anajulikana na Askofu Ndondo na viongozi wengine wa kanisa. Hata hivyo, hajawahi kuwa na muda hasa wa kuzungumza na Askofu matatizo yake au mambo yake au hata kuweza kukaribishwa katika ofisi za Askofu ukiondoa zile zilizopo ndani ya jengo la kanisa. Askofu alijua tu kuwa Sofia alikuwa ni mke wa afisa wa polisi, hapo hakujua undani wa cheo na shughuli za ofisa yule.

Ray hakuwa anaelewa kwanini mke wake ambaye mwanzoni alikuwa anamsikiliza, na wanazungumza vizuri tu na kushauriana mambo mbalimbali alikuwa kama mwenye mapembe yaliyochongoka kama mbilimbi. Kila walipokuwa wakijaribu kuzungumza ilikuwa ni kama kondoo wanagonganisha vichwa. Walipofika nyumbani hata chumbani hawakulala pamoja; haikuwa mara ya kwanza Ray kujikuta anajilaza kwenye makochi kwani mkewe aliingia chumbani na kufunga mlango. Aliamua tu kumwacha aendelee na mambo yake na yeye aendelee na kazi zake. Kutokana na majukumu yake asingeweza kuachilia matatizo ya nyumbani yamtawale mawazo kiasi cha kushindwa kufanya majukumu yake ya kiusalama kwani Taifa na jamii ilikuwa inamtegemea.
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom