Mbwa wa geti
Sehemu ya kumi na tano
Zedi akasimama mbele ya meza iliokuwa mle ofisini na kufanya kuwe na utenganisho baina yao.
‘naomba kujulishwa ilipo ofisi ya bwana Kamau' aliongea zedi huku macho yake yakiwa makini juu ya mwili wa meneja Kwasi.
“ooh aliacha kufika hapa ofisini wiki tatu sasa na ndio nikakaimu nafasi yake” alijijibu bwana Kwasi huku akiachia tabasamu la dhihaka na Zedi akajua anadhihakiwa makusudi
“hakuna taarifa zozote kumhusu!! Aliuliza tena Zedi
“Yeye ndie wa kutoa taarifa ofisini na si ofisi ijue taarifa zake” alijibu kijeuri Kwasi.
“ok naomba kujua taarifa za akaunti hii…”.(huku akitaja namba)
Kwasi akimtizama na bila kupepesa alimwambia hiyo ni ngumu kulingana na utaratibu wa kazi ulivyo ukizingatia Zedi sio mmliki wa akaunti ile na hapo tena Zedi akaongeza swali lingine
“Mzee matare na Kamau nasikia walikuwa wote ni wahudumu wa hii ofisi” hapo akaona msituko wa wazi kwa meneja yule japo alijitahidi kuuficha msituko ule na hicho ndicho alichokitaka Zedi.
Zedi hakuwa na pa kuanzia harakati zake za kuzima na kujua yaliojificha nyuma ya utafiti ule uliokuwa unateketeza mamia ya watu nchini Kenya na kuwanyima usingizi viongozi wazalendo na nchi yao,hivyo kwa kufauata maelekezo machache ya marehemu Matare alifanikiwa kupata kadi za bank ndani kwake na kuamua kwenda nazo huko ili japo aone mapokeo ya huko hivyo sasa akajua kuna mengi yamejificha nyuma ya kutekwa kwake na mzee Matare.
“Basi naondoka meneja ahsante kwa ushirikiano”alizungumza Zedi huku akianza kupiga hatua ili aufikie mlango,lakini akaona kundi la watu wakiwa kule mapokezi na kila mmoja alikuwa na bastola mkononi na walikuwa wanapokea maelekezo kutoka kwa Wambui huku akinyoosha kidole kuelekea kule kwenye mlango wa meneja.
Zedi akapagawa na haraka akageuka huku aliko meneja na hapo akapigwa na butwaa jingine.
Meneja alikuwa ameshika bastola double colt akiwa amemwelekezea huku tabasamu feki likiwa usoni pake.
Zedi hakuwa na pa kutokea hata dirisha lililokuwa mle halikutosha kupita mtu maana lilidhibitiwa kwa nondo imara kabisa.
Zedi akatazama juu ya dali la ofisi ile na hapo akatabasamu kimoyomoyo akatabasamu japo hakujua kwanini ofisi ile imejengwa kwa namna ile alioiona.
Watu wale haraka wakawa wanakuja kwa kasi na Zedi akawa bado amenyoosha mikono juu huku kila mara akipokea onyo kutoka kwa meneja Kwasi ya kuwa asijaribu kufanya ujinga wowote la sivyo angeliondoka na uhai wake.
Kitu kimoja meneja Kwasi hakujua ni kuwa bastola alioishika ilikuwa na umuhimu sana kwa Zedi maana hadi muda huo hakuwa na silaha yoyote zaidi ya mikono na akili yake .
Zedi akawa anamtazama meneja machoni tu na hapo akapata kuona alichokusudia kuona ndani ya macho ya meneja yule.
Meneja Kwasi alikuwa anatazama mlangoni huku akirudi kumtazama Zedi ni wakati macho yake yalipokuwa yakitizama mlangoni tena akashangaa kuona kitu cha ajabu.
Kule mapokezi kulikuwa kunafuka moshi kutokea chini kwenda juu huku watu wale waliokuwa wakijongea kwenda kwenye ofisi yake wakianza kurudi tena kule mapokezi kulikokuwa kunafuka moshi mzito huku sasa vingora vya tahadhari vikianza kulia jengo zima huku mashine za kumwaga maji kwa dharura ya moto zikianza kufunguka na kumwaga maji.
Zedi akaitumia vyema nafasi ile na kwa kasi ya ajabu kabisa akaruka na kutua juu ya meza huku mikono yake tayari ikiwa imekamata shingo ya meneja Kwasi na mkono wenye bastola ulikuwa umekamatwa na kuwekwa katikati ya miguu ya Zedi.
Mikono ilielekea kulia pamoja na shingo ya meneja huku miguu ikielekezwa kushoto na mkono wa meneja hivyo ikawa shingo imevunjwa na mkono umevunjwa na kisha bastola ikawa ndani ya himaya ya Zedi na hapo ndipo Zedi akaamua kutazama kule mlangoni japo sasa kioo cha mlango kilianza kufifia kuonesha upande wa pili kwa sababu ya moshi ule.
Zedi hakutaka kuhadaika kivile maana hakujua nani hasa kafanya vile maana kwa uzoefu wake alijua ule ni moshi wa smoke mashine na huwa unatumiwa maalumu na makomando watakapo kutoroka kwa adui na pia moshi ule ulikuwa na tabia ya kuwa kama unalevya kwa mtu awae karibu na kuuvuta.
Aliamini hakuna anaemjua pale Kenya hivyo hakutaka imani imweke matatizoni.
Haraka akasimama juu ya meza na kushika pangaboi lililokuwa linabembea juu kisha akabana pumzi kwa nguvu,hii ilimsaidia kupunguza uzito hivyo pangaboi lile likahimili kumbeba nae akalitumia na kujivuta kwa kasi huku mkono mmoja ukiwa umetangulia na akafanikiwa kugonga kijimlango kidogo kilichokuwa kule juu nacho kikafunguka huku kamba ikishuka chini na kwa haraka akaingia huko na kukifunga tena.
Ni wakati anamalizia kufunga na kugeuka ndipo akaona jambo lingine ambalo mwanzo alilitilia shaka.
Itaendelea