Mbwa wa geti
Sehemu ya kumi na tatu
Ila ni kwa kuwa hawakujua na laiti wangejua!!!!!!
****
Burizozo alikuwa amekaa kwenye sofa akitizamana na Tausi,huku kushoto kwao kukiwa na mtoto mdogo umri wa miaka kama mitano ama sita hivi
Tausi alikuwa akimtizama Burizozo kwa chuki kubwa sana.
Tausi alitaka kusema kitu lakini alikatishwa na sauti ya mtoto aliekuwa karibu yake ,mtoto alilalama njaa ,alitaka kunyanyuka ili ampe walau chai ahsubuhi ile lakini akapata onyo kutoka kwa Burizozo
“usimpe chai ama kitu cha moto,atakufa maana ametoka kutema mzigo sasa hivi….”
Kilifuata kilio kutoka kwa Tausi,alilia kwa kuona mwanae amegeuka kuwa mbeba madawa ya kulevya.
Na hapo akamatazama tena mwanae yule na Kama ndio anamwona kwa mara ya kwanza,akaona vile mtoto amedhoofu,akamfunua shati alilokuwa amevaa na hapo akaona kovu kubwa lililokuwa tumboni kwa yule mtoto mdogo.
Tausi hakutaka kujiuliza lile kovu ni la nini,tayari alishajua hutumika kutolea tembe zinazosalia tumbobi baada ya kushindwa kutoka kwa njia ya haja .
Tausi alilia na kama mtoto mdogo lakini kilio chake hakikufika mbali wala hakikuwa na thamani zaidi kilimwamsha Kabah aliekuwa kalala juu gorofani na akashuka kwa kasi na kipensi tu na kuwakuta Tausi na mwanae wamekumbatiana,hakujali.
Kwa kasi akamfikia Tausi na kumvuta juu na haraka akamchapa makofi kama sita mfululizo na kumchana usoni kisha akamsukuma kwa nguvu na kumtupa juu ya sofa na bila huruma akanyoosha mkono ili amtandike kofi mtoto aliekuwa amesimama kando akitizama mama yake akisulubiwa,lakini konde lile halikufika likadakwa na Burizozo,
“We need him more than you think” alisema kwa lugha ya kusihi na maneno yakamwingia Kabah akagairi kutoa kipigo kwa mtoto aliefanana na Zedi kwa kila kitu.
Hasira zake bado zilikuwa kwa Tausi na akaendelea kumshushia makonde na kufanya damu zijae kwenye sura ya mwanamama yule sura ambayo ilikuwa imeanza kutota kwa utumizi wa dawa za kulevya.
Kabah alipoona roho yake imesuuzika kwa kipigo alichotoa akaanza kumburuta Tausi kuelekea kwenye chumba ambacho huwa hakifunguliwi mara kwa mara na huko akamtupia humo kama mzoga kisha akakifunga kwa nje.
Tausi alijikunyata kama mtoto mdogo huku kilio kikiwa ni kwikwi,alijuta kwa alioyafanya na alijuta kwa kumsaliti mwanaume aliempenda kuliko kitu chochote.
Mara nyingi Tausi akiwa katika hali kama ile hujituliza kwa dozi ya sindano ama mnuso wa cocaine.
Na tayari mwili ulikuwa unahitaji kupata hicho kitu,lakini hakuwa na wa kumpa ndani ya chumba kile cha giza totoro.
Matanio yalizidi uwezo,akanyanyuka,lakini hakupiga japo hatua mbili akawa yupo chini maumivu ya kipigo yalikuwa yapo kila sehemu,tena ni bora angelikuwa amepigwa na mtu kama mimi au wewe ambao hatujui hata silaha inashikwa vipi,lakini huyu alikuwa amepigwa na komando la waasi wa huko Somalia,tangu utoto hadi ujana wake anacheza na roho za watu tu.
Tausi hamu ya kuvuta unga ilimzidia,akajongea hadi kwenye mlango,akaugonga mara kadhaa na punde ukafunguliwa ila alieufungua hakuwa msemaji akafanya alichoagizwa,akamwaga maji ya baridi ndani ya chumba alichomo Tausi kisha akaufunga ule mlango na kumwacha Tausi akiwa anaelea juu ya maji ya baridi.
Kwa kiasi chake ilimsaidia kumwindolea zile hisia za uhitaji wa kuvuta unga,lakini nafuu ile haikudumu kamwe.
Tausi akawa anayapitia mateso ya kujitakia!!!
****
Ziga alikuwa anaikata kona ya nkuhungu chama na akapunguza kidogo mwendo kulingana na ukali wa kona ile.
Safari yao ilikuwa ya ukimya,haikuwa safari ya mbwembwe kama walivyokuwa wamezoea wawapo wa wili ndani ya gari.
Mbele kidogo ya mtaa wa nkuhungu vibandani Ziga alikata kulia na kupita pembeni kidogo ya ukuta wa nkuhungu sekondari kisha akasogea mwendo wa mita mia mbili na kisha akasimisha gari mbele ya geti kubwa jeusi.
Ziga akapiga honi kadhaa lakini hakuna alietoka kufungua,ikabidi Mina ashuke na kulisogelea geti lile na hapo akaona kitu kilichoamsha hisia mbalimbali ndani ya kichwa chake.
Kimuonekano tu ilionekana eneo lile halijakaliwa na watu kwa muda mrefu kidogo.
Mina akalisogelea zaidi lile geti na kujaribu kusukuma na hapo mshangao mwingine ukamvaa geti la nyumba ya Zedi lilikuwa wazi na kwa tahadhari kabisa akaingia ndani ya uzio wa geti lile nako akazidi kupigwa na butwaa.
Palionekana kutofanyiwa usafi kwa muda mrefu hali iliopelekea kuote majani marefu huku uchafu wa kila aina ukiwa umejaa pote .
Mina akazidi kujongea kuingia ndani ya nyumba ya Zedi na huko akapigwa na mshangao ambao hakuutegemea.
Ni wakati anaingia ndani ya nyumba ya Zedi,mlangoni tu akakutana na matone ya damu yalioganda na Kukauka kabisa na yalionesha ni ya muda mrefu kidogo na pia mlangoni kulionesha kumeparazwa na kitu kama risasi hivi.
Akausukuma mlango na kuingia ndani kabisa kwa mwendo wa tahadhari kabisa.
Hakuwa mgeni wa matukio na moja kwa moja akajua kabisa pale ndani palitokea ugomvi wa aina yake na wapambanaji walionesha wanaujua mchezo,Mina akabaki akishangaa na kujiuliza kulikoni kimemkuta nini Zedi.
***
Ziga akiwa ndani ya gari aliona vile Mina alivyokuwa ananyata kuingia ndani na hapo akajua kabisa huko si salama nae akataka kushuka ili aungane na Mina.
Ni wakati alipokuwa akikaribia kufungua mlango wa gari akili yake ikamtuma atazame kwenye kioo na hapo hakuwia kugundua hawapo peke yao pale,kuna macho ya watu wawili yalikuwa yanawatizama,na sio kuwatizama tu yalikua yanawatizama kwa husda.
Itaendelea