RIWAYA : MKONO WA CHUMA.
MTUNZI : ALEX KILEO.
SEHEMU YA THELATHINI NA SITA.
"nini tatizo?" Dokta Smith aliuliza huku akimtazama yule mgonjwa,
"huyu alivunjwa vunjwa kila kiungo cha mwili, sasa mimi nimemtibu vilivyokuwa vinawezekana, ila Kuna vilivyonishinda" Dizonga alijibu,
"na wewe ni Dokta?" Dokta Smith alimuuza Dizonga,
"ndio, mimi ni Dokta, tena Dokta mzuri sana wa jeshi" Dizonga alijibu,
"umeegemea katika matibabu ya nini na nini?" Dokta Smith alimuuliza Dizonga,
"moyo zaidi" Dizonga alijibu,
"Sasa ilikuwaje ukaacha utabibu na kuwa kiongoz wa serikali?" Dokta Smith aliuliza,
"mzee endelea kuwa na mimi, utajua mengi sana, ila kifupi mimi sio Mfanyakazi wa serikali, ila niliamua kujifanya vile ili nikupate, kuna mtu mkubwa zaidi ya serikali ndio alinituma nije nikufuate" Dizonga aliongea maneno mengi na kufanya Dokta Smith ashtuke,
"lengo la kufanya yote haya ni nini?" Dokta Smith aliuliza,
"utajua tu zinavyozidi kwenda, kwanza ebu anza kumuangalia mgonjwa wangu" Dizonga aliongea na kumfanya Dokta Smith atikise kichwa tu, kisha akaanza kumuangalia X soldier kwa kumshika shika baadhi ya maeneo mwilini, na kugundua Kuna sehemu za mwili zimevunjija, hasa mguu wa kulia, ila maeneo ya mbavu na kichwa kulikuwa na maumivu tu.
"hayo maumivu ya kichwa, ni vyema tukamcheki kwenye X ray" Dokta Smith aliongea,
"huyu jamaa hawezi kutoka nje, hatakiwi kuonekana" Dizonga aliongea,
"Sasa tutajuaje tatizo lake?" Dokta Smith aliuliza,
"Dizonga, ni bora nipelekwe tu hospital, kuendelea kujificha humu naweza kufa" Sajenti Minja aliongea,
"na kwanini unajificha?" Dokta Smith aliuliza,
"taratibu utajua tu, si tupo wote kila siku?" Dizonga alimwambia Dokta Smith,
"yasije kuwa kama yale yaliyonikuta msituni, natibu mtuhumiwa alafu nakuja kupewa kesi nzito" Dokta Smith aliongea,
"hata usijali Dokta, mtu aliyekutoa gerezani ni zaidi ya sheria, yaani yeye ndio anayeziamrisha sheria, ana uwezo wa kumgeuza mtuhumiwa na kuwa hana tuhuma" Dizonga aliongea,
"Sasa kama ni hivyo, mbona mgonjwa wake huyu anaogopa kwenda hospitali wakati mtu wake ana nguvu za namna hiyo?" Dokta Smith aliuliza,
"huyu sio mgonjwa ambaye amefanya umeachiwa, yupo, yupo utamuona" Dizonga aliongea na kuzidi kumchanganya Dokta Smith,
"Sasa kama yupo, kwanini usingenipeleka moja kwa moja kwa huyo mgonjwa?" Dokta Smith aliuliza,
"huyo mgonjwa hawezi kumuona hovyo, kila kitu kina taratibu zake, hapa nasubiri kupigiwa simu ili nikupeleke kwa huyo mgonjwa" Dizonga aliongea na kuzidi kumvuruga Dokta Smith,
"lakini hata mimi ni mgonjwa" Sajenti Minja aliongea,
"ndio, ila sasa ili utibiwe, tunatakiwa tujue tatizo kwa undani, ili tatizo lijulikane, ni lazima uende hospital" Dokta Smith aliongea kwa upole,
"sawa, kesho nitaenda hospital, maana nimechoka kukaa kitandani kila siku" Sajenti Minja aliongea,
"X soldier sasa hospital utaendaje, huoni ni kujipa mitihani tu" Dizonga aliongea,
"nitaenda tu, hata ukunikatalia kunipeleka, nitaenda hata kwa kutambaa" Sajenti Minja aliongea na kipindi hicho simu ya Dizonga ilikuwa ikiita, akaipokea,
"nambie" Dizonga aliongea baada ya kuipokea simu
"tayari tumeshampeleka yule mwanamke kwa Ray, sasa unaweza kumpeleka Dokta" Sauti ya upande wa pili iliongea,
"sawa" Dizonga aliongea na kukata simu, kisha akamgeukia Dokta Smith,
"twende sasa uko sehemu husika, na tukifika hutakiwi kuzungumza chochote kuhusu huyu mgonjwa wangu hapa" Dizonga alimuonya Dokta Smith,
"nitafanya hivyo" Dokta Smith alijibu,
"X soldier baadae, acha nimpeleke Dokta" Dizonga alimwambia Sajenti Minja,
"poa D" Sajenti Minja aliongea,
"Kijana, jitahidi uende hospital, alafu nitajua nianze wapi kukutibu" Dokta Smith aliongea,
"usijali, nitaenda kesho" Sajenti Minja aliongea,
"sawa, ugua pole" Dokta Smith aliongea huku akitoka na Dizonga, wakamuacha Sajenti Minja akiwa anajigeuza kitandani.
Walitoka mpaka nje, Dizonga akachukua gari yake na kisha Dokta Smith akaingia upande wa pili wa gari, siti za mbele, Dizonga akaondoa gari.
"huyu unaemuita X soldier alipata matatizo gani, maana haiwezekani mtu aumie mwili mzima, hata ajali hakuna ya namna hiyo, hiyo labda kwa mwizi ndio inaweza kutokea, kwa sababu wananchi wakianza kumpiga mwizi hawachagui pa kupiga, wanapiga kila sehemu" Dokta Smith aliongea,
"huyo alitakiwa afe, yaani kipigo alichopewa kilikuwa kipigo cha kifo, alipoteza fahamu siku tatu" Dizonga aliongea,
"kwanini alipigwa?" Dokta Smith aliuliza,
"ni mambo ya kijinga tu, utayajua mbele siku zinavyozidi kwenda" Dizonga aliongea,
"na imekuwaje amepona wakati tangu amepigwa hujawahi kumpeleka hospitali, na hapo ulisema alizimia siku tatu?" Dokta Smith aliuliza kwa mshangao,
"huyu jamaa alipigwa na kufungwa kwenye gunia, kisha akatupwa baharini, na kati ya watu walioshiriki kumtupa baharini, mimi nilikuwepo, ila sasa huyu jamaa mimi nilikuwa namfahamu juu juu tu, kwa kuwa huyu ni mwanajeshi, kwa hiyo baada ya kupigwa na kutupwa baharini, mimi nilienda duka la dawa na kununua dawa na bomba la sindano, kisha nikawaambia wenzanu nimesahau kitambulisho katika gunia tulipomuweka huyu mtu, kwa hiyo tukarudi baharini na mimi mwenyewe ndio niliingia baharini kwenda kuutoa mwili wa huyu jamaa na uko uko nilimchoma sindano ya kushtua mapigo ya moyo, wenzangu hawakuweza kugundua kitu kwa kuwa nilikuwa mbali sana na nchi kavu, kwa hiyo nilifanya kila kitu kwa utaratibu sahihi. Baada ya kumchoma sindano, mapigo ya moyo yalianza kupiga, basi nikambeba na kumpeleka nchi kavu, kisha ndipo nikajifanya kufungua gunia alilofungwa na kutoa kitambulisho changu, nikauacha mwili nchi kavu, kisha tukarudi kwa mkubwa aliyetutuma, tukarudisha report kwa mkuu, baada ya hapo tukatawanyika, ndipo niliporudi baharini na kumchukua huyo X soldier na kumpeleka nyumbani kwangu, kisha nikampigia mkuu mmoja wa jeshi na kumueleza kuhusu habari za huyu jamaa kutaka kuuawa, akanambia niendelee kumuhifadhi huku nikiendelea kumchunguza, kwa maana alikuwa na tuhuma za kumtorosha muarifu, mpaka sasa hakuna aliyethibitisha hilo" Dizonga aliongea,
"kwa hiyo X soldier ni Mfanyakazi wa jeshi, na wewe ni Mfanyakazi wa jeshi. Jeshi lipi sasa, la polisi au la ulinzi na usalama?" Dokta Smith aliuliza,
"hilo hupaswi kujua" Dizonga alijibu,
"sawa, je na huyo mgonjwa mwingine ninayeenda kumtibu, nae amevunjwa kama X soldier?" Dokta Smith aliuliza na kumfanya Dizonga amtazame,
"huyo ugonjwa wake ni tofauti, ila pia hatibiwi kwa nia njema" Dizonga aliongea,
"kwanini unasema hivyo?" Dokta Smith aliuliza,
"huyo anatakiwa atibiwe ili afe" Dizonga aliongea,
"bado sijakuelewa" Dokta Smith aliongea huku akimgeukia Dizonga,
"hujaelewa nini sasa?" Dizonga aliuliza,
"kuwa anatibiwa ili afe, yaani kivipi?" Dokta Smith aliuliza,
"huwezi kunielewa kwa kuwa tunazungumza lugha moja ila vichwa vyetu vinajenga picha tofauti" Dizonga aliendelea kuongea,
"unaongea mafumbo sana" Dokta Smith aliongea,
"sio mafumbo, ninachoongea ni ukweli halisi, ngoja ufike tuendapo na uzoee mazingira, huenda utajua ninachoongea leo, maana ukishazoea mazingira ya pale, huenda tukawa tunajenga picha moja na kuongea lugha moja" Dizonga aliongea na kumfanya Dokta Smith akae kimya tu,
"ila endapo nitamkuta mgonjwa yupo katika hali kama ya X soldier, hapo ndipo nitaamini unyama upo" Dokta Smith aliongea,
"hivi pale X soldier unamuona ana hali mbaya? Je ungemkuta ndio nimetoka kumuokoa, si ungelia kabisa wewe" Dizonga aliongea na kukohoa,
"tusiishi kwa mazoea, mimi ninachokushauri, ni vyema utumie mbinu yoyote ile, uhakikishe X soldier anafika hospital kufanyiwa X Ray, vinginevyo unaweza kumsababishia ulemavu usiokuwa na maana, kwa maana ule mguu ambao umevunjika, eneo ulipovunjikia ni pabaya sana, sasa kwa umri wa X soldier, mifupa yake haikui tena, endapo utamchelewesha zaidi, mnaweza shangaa mnampoteza.
"kuhusu hilo nitalifanyia kazi" Dizonga aliongea huku akisimamisha gari mbele ya geti la nyumba ya Ray Charles,
"ndio hapa?" Dokta Smith aliuliza na kipindi hicho Dizonga alikuwa akipiga honi mfululizo, baada ya muda geti likafunguliwa, Ray Charles akasimama mlangoni, akamkata jicho kali Dizonga,
"mambo vipi Ray?" Dizonga alimsalimia Ray,
"unajua mimi sipendi kelele, hizo upigie kwako, ukifika hapa simama getini na ungoje ufunguliwe, haina haja ya kupiga honi au kugonga geti" Ray Charles aliongea kwa hasira, Dizonga akatabasamu tu na kuingiza gari ndani ya uzio. Walipofika ndani ya geti, Dizonga akazima gari na kisha wakatelemka, wakawa wanamngoja Ray afunge geti. Ray alimaliza kufunga geti na kuwapita huku akiingia ndani ya nyumba yake, Dizonga nae akaamua kumfuata kwa nyuma huku wakiambatana na Ray Charles. Ray Charles alitembea mpaka katika chumba kimoja na kufungua mlango,
"Dokta ingia" Ray Charles aliongea kisha Dokta Smith akampita dizonga na kuingia ndani, Dizonga nae akawa anataka kuingia, Ray Charles akamzuia kwa kumuwekea mkono kifuani,
"wewe ulitakiwa uishie nje ya geti, ndio kazi yako iliishia pale, hukupaswa kuingia humu" Ray Charles aliongea na kumsukuma Dizonga, Dizonga akatabasamu na kuondoka huku akitikisa kichwa kwa masikitiko.
Dokta Smith alipoingia akapigwa na butwaa kumuona mgonjwa mwenyewe ni BQ,
"siwezi kumtibu huyu, maana huyu ndio amesababisha nikawa gerezani" Dokta Smith aliongea,
"ila huyu huyu ndio amefanya uwe huru tena" Ray Charles aliongea,
"unachotakiwa kufanya ni kutii amri, mimi sio mtu salama kwako, kwa hiyo usinilazimishe nikuoneshe upande wangu mbaya" Ray Charles aliongea na kumfanya Dokta Smith awe mpole.
Dokta Smith akamsogelea BQ na kumpima joto, akashtuka, sura yake ikahamaki,
"nipishe kidogo" Dokta Smith aliongea huku akihema haraka haraka, alikuwa na hofu mno, Ray Charles akaondoka na kwenda kukaa sebuleni.
Dokta Smith akafungua begi lake na kutoa vipimo kadhaa, akaanza kumpima BQ, ila kila kipimo alichokuwa anampima BQ, kilikuwa kinagoma, kinaleta majibu yasiyoridhisha, Dokta Smith akaamua amfunue macho BQ kwa kidole, akakuta macho yameshakuwa meupe, Dokta Smith akaanza kulia,
"kwisha kabisa, ni unyama huu" Dokta Smith aliongea huku akilia kwa uchungu, Ray Charles akasikia kilio cha Dokta Smith, akaja haraka ndani,
"Kuna nini?" Rav Charles aliuliza,
"mmenileta nitibu mtu au nifufue mtu?" Dokta Smith aliuliza kwa uchungu huku akilia, Ray Charles akamsogelea BQ na kumuangalia kwa umakini,
"unamaanisha amekufa?" Ray Charles alimuuliza Dokta Smith,
"muda sana" Dokta Smith alijibu huku akiendelea kulia,
"basi, hakuna hasara, jiandae nikurudishe gerezani" Ray Charles aliongea huku akitoka katika kile chumba....
*********ITAENDELEA**********
the Legend☆