MKE WA RAIS
SEHEMU YA 73
Akageukaaa.. Lakini hakufika katika usawa sahihi. Akasikia sauti ya mwanadada ikinguruma kutoka nyuma yake. Sauti ambayo haikuonyesha masihara. Sauti ambayo haikuwa na utani ndani yake. Sauti ya Amri, sauti ya kukulazimisha kutii hata kama haupo tayari. Jenipher akatii bila kuonyesha ubishi wowote. Hakujua aliyekuwepo nyuma yake ni nani lakini akiusikia mdomo wa bastola Ukiigusa ngozi yake. Akatulia kama maji mtungini, akatulia kanakwamba ameogopeshwa na tukio lile. Hata pale alipokuwa akiamriwa atembee kuelekea alipotakiwa alifanya hivyo. Alifanya bila wasiwasi wowote, alifanya akiamini Ummu Yupo Sehemu Sahihi akimuangalia na akishudia kile kilichomtokea. Kitu hicho kikampa imani kubwa, imani iliyomfanya atulie bila wasiwasi. Hivi sasa walikuwa wakiiacha Hongera Bar na kutaka kuivuka barabara kuiendea gari yao ambayo ilishageuzwa kurudi ilipotoka. Wakatizama kulia na Kushoto kama kuna watu wanatizama, hawakuliona hilo. Kilichofuata ni kupiga hatua kuvuka barabara; muda wote bastola ilikuwa ipo mgongoni kwa Jenipher. Hatua ya kwanza ikapita bila chochote. Hatua ya pili akaenda pasipokutokea chochote, hatua ya Tatu haikupita wala haikupigwa popote, pikipiki ikaonekana kuja kwa kasi, pikipiki ambayo haikuwa ikiendeshwa na mlevi wala mvuta bangi. Bali alikuwa Ummu, Ummu Sammy bastola mkononi mwake.
Jenipher alikisoma kile kitendo na hata Neema Alikitambua mapema sana. Licha ya Neema kutambua lakini hakuweza kujiandaa katika hilo, hakuweza kuzuia kile ambacho kilipangwa kitokee. Muda mfupi alikuwa amepaa Hewani na sekunde ya pili alikuwa akianguka katikati ya barabara akiwa hana uhai tena. Risasi tatu kutoka kwenye Bastola ya Jenifer iliweza kumnyamazisha Neema. Hakuujua wepesi wa Jenipher pale alipokuwa akimuongoza. Hakuiona bastola ambayo ilikuwa katika mfuko wa Siri wa Jenifer. Hata pale alipoiona pikipiki ikija kwa kasi kisha yeye kugeuka kuangalia kule, hakuweza kumuona Jenipher alivyoichomoa bastola bali alikuja kushangaa pale kitu cha baridi zaidi ya kimoja kikipenya kifuani kwake.
Hata pale Ummu Sammy alipokuja kufika maeneo yale hawakutaka kujiuliza bali waliondoka kati mwendo ambao uliwashangaza wapita Njia Wachache hasa pale Jenipher alipochupa kisha kutua kwenye pikipiki, na muda ule ule pikipiki kuondoshwa. Hakukuwa na kushangaa wala hapakuwa na msikilizano, Maiti ya mwanadada Neema Mtobwa Ilikuwa Chini katikati ya Barabara damu ikichuruzika taratibu na kuweka kidimbwi kidogo. Ingawa ulikuwa usiku lakini mlipuko ule wa bastola Uliwafikia watu wachache. Kati ya Watu hao mmoja wao alikuwa ni Mohamedi. Ndio kwanza alikuwa amefika maeneo yale baada ya kutorokwa na Wakora katika mapambano yaliotokea Muda Mfupi uliopita. Ingawa alikuwa na Haraka Ya kuutafuta mwili wa mwanamke uliotoroshwa na Neema. Hiyo haikumzuia kwenda sehemu ya tukio. Sehemu ambayo alirakiwa na Watu waliozunguka kitu kama Mwili wa mwanamke. Licha ya watu hao lakini pia kulikuwa na polisi Wengi kutoka Kijitonyama polisi na pia walikuwepo Mashushushu kutoka Idara Ya Usalama wa Taifa.
Mohamedi akaendelea kusogea akiwapita watu mmoja baada ya Mwingine. Hakufanya hivyo kwa kupenda bali alivutiwa na mavazi aliovaa mwanamke Yule aliyekuwa amelala katikati ya Dimbwi la Damu. Mavazi ambayo muda mfupi Uliyopita yalivaliwa na mwanadada Shupavu Neema Mtobwa. Hilo likamvutia na kumfanya asogee. Kweli alisogea na kusogea na hata alipoupita Utepe uliozungushiwa na Polisi Hakuna aliyemuuliza. Wote walikuwa wakimuangalia kwa mshangao, mshangao ambao haukudumu sana baada ya mtu wanayemshangaa kuonyesha kuguswa na kifo cha mwanamke aliyelala katika dimbwi la damu. Naam, Mohamed alikuwa akimtizama Neema Mtobwa. Mwanamke aliyemtoroka Muda mfupi uliyopita tena akiondoka na mwili wa mwanamke ambaye alikuwa na sura ya bandia yenye kufanana na Sura ya mke wa Rais. Neema ambaye angepatikana angeweza kueleza alikuwa akimtumikia Nani katika mpango Huu. Aliuangalia Mwili wa Neema Mtobwa kwa muda mrefu bila kufanya kitu chochote kile. Lakini Muda mfupi baadae mikono Yake ilikuwa nddani ya mifuko ya Marehemu Yule akiangalia hiki na kuangalia kile. Hapo akakutana na Simu ya Marehemu akaichukua na kuiweka mfukoni mwa koti lake. Baada ya hapo akachukua vitu vingine ambavyo aliviona ni Muhimu kisha akainuka na kuanza kuondoka huku akiacha maagizo kadha wa kadha kwa askari wale ambao wengi walitii ingawa hawakumjua. Hata pale alipotoweka katika Upeo wa macho Yao Hakuna aliyemuona Zaidi ya kujikuta wakiongeza Mshangao katika hilo.
Mohamed alijitokeza pale makusudi akiamini kuwa palikuwa na watu sehemu wakimtizama. Na hilo ndilo ambalo alilitaka, alitaka wamtizame na wamjue ili waanze kumfuatilia. Alitaka kufuatiliwa ili aupate ukweli, ukweli Juu ya Mapinduzi, Ukweli Juu Ya Mpango Ovu kutoka kwa mtu ambaye bado nikitendawili. Alitembea akiamini kuna macho mahala yakimtizama na kuna watu sehemu wakimfuatilia. Naam Hakukosea na Hakuwa mbali na Ukweli.