SEHEMU-43
[emoji3586][emoji3586][emoji3586][emoji3586][emoji3586][emoji3586][emoji3586][emoji3586][emoji3586][emoji3586][emoji3586][emoji3586][emoji3586][emoji3586][emoji3586][emoji3586][emoji3586][emoji3586][emoji3586][emoji3586][emoji3586][emoji3586][emoji3586][emoji3586]
Dr.Pesambili alitua barani Afrika nchini Tanzania kwa mara ya kwanza akiwa mtu mzima tokea achukuliwe akiwa ni mtoto mdogo kutoka kule nchini Kenya. Aliwasili Tanzania katika nchi ya asili ya wazazi wake, bila yeye mwenyewe kufahamu. Alikuwa amepata kibarua katika taasisi ya Afya yenye makao makuu nchini Marekani inayoitwa "The Centers for Disease Control and Prevention (CDC)", iliyo na matawi yake katika nchi mbalimbali duniani. Taasisi hiyo ilikuwa na miradi ya Afya nchini Tanzania, Mkoani Morogoro hivyo Dr.Trezguet au ukipenda Dr.Pesambili alikuwa ni mmoja wa Wafanyakazi kwenye taasisi hiyo. Alivyopangiwa kituo hicho kipya cha kazi, Dr.Pesambili alijawa na furaha sheshe. Furaha hiyo ilitokana na tamaa yake ya kwenda kuzuru nchi Kenya, sehemu ambayo alipewa taarifa na baba yake mlezi, Mr.Lorenzo kuwa ndipo alipochukuliwa kutoka kwenye kituo cha watoto yatima.
Dr.Pesambili baada ya kumaliza mafunzo yake ya vitendo alimzuru baba yake mlezi gerezani na kumdadisi vya kutosha kutaka kujua wapi ilipo asili yake. Ndipo Mr.Lorenzo bila kupepesa macho akamchana waziwazi kuwa alichukuliwa na msafara wa Papa John Paulo (II) kutoka kwenye kituo cha watoto yatima, Jijini Nairobi. Tokea hapo Dr.Pesambili akaanza kusaka nafasi za kazi kwenye Taasisi za Kimataifa kwa kutumia mtandao akilenga hasa maeneo ya nchi za Afrika Mashariki. Chambilecho mgaagaa na upwa hali wali mkavu, juhudi zake zikajibu akapata kazi nchini Tanzania. Furaha yake ya kupata kazi Tanzania ilitokana na kuwa kupitia somo la Jiografia alijua fika Tanzania na Kenya ni nchi majirani, wanaounda Jumuiya moja ya Afrika Mashariki, hivyo itamuwia wepesi kwake kukanyaga ardhi ya Kenya akitokea Tanzania, ili kuisaka asili yake. Taasisi ya "The Centers for Disease Control and Prevention (CDC)" mkoani Morogoro walikuwa wanajishughulisha na kutoa huduma za Afya majumbani, kwa kutumia magari maalumu, hospitali inayotembea kwa kuwapatia vipimo vya magonjwa bure na kuwapa matibabu. Nguvu kubwa ya hospitali inayotembea 'mobile hospital' ilielekezwa vijijini, sehemu ambazo kulikuwa na shida ya uwepo wa hospitali za kisasa.
Shirika la Afya Duniani 'WHO' kwa kawaida linapendekeza, daktari 1 atibu wagonjwa 300, lakini kwa Tanzania hali ilikuwa ni mbaya, daktari 1 huwa anatibu wagonjwa zaidi ya 20,000, hivyo Taasisi ya "The Centers for Disease Control and Prevention (CDC)" ikaonelea bora iwekeze nguvu vijijini kwenye upande wa kuboresha Afya. Kijiji alichokuwa anafanyia kazi Dr.Pesambili ndio kijiji ambacho alikuwa anaishi Mjomba Kobelo.
Mjomba Kobelo, alishahama zake kutoka kijiji cha Mikongeni na kuhamia kijiji cha Nyandira Mgeta wilaya ya Mvomero mkoani Morogoro. Mkewe yule mkorofi sana aliyekuwa haishi kumshushia vipigo shadidi na mateso Deborah alifariki kifo cha ghafla siku chache tu baada ya Mjomba Kobelo kupokea malipo yake ya fidia ya kuhamishwa eneo walilokuwa wanaishi. Alikufa kutokana na mshtuko wa moyo baada ya Mjomba Kobelo siku moja kurudi nyumbani amelewa akija na stori za kuibwa pesa zote za fidia. Baada ya maziko tu, haukupita siku nyingi Mjomba Kobelo akahama kijiji na binti zake pamoja na dada yake mgonjwa, mama Deborah kuhamia kijiji kipya. Ndipo Dr.Pesambili katika mapito yake ya shughuli za kikazi akajikuta anafika katika nyumba ya Mjomba Kobelo. Akafanikiwa kumuona mama Deborah akiwa kwenye hali mbaya ya kupooza mwili. Dr.Pesambili kwa jinsi alivyokuwa na uchungu wa kukosa mama, alihuzunika sana kumuona mama Deborah wamemtelekeza, hapati huduma stahiki. Hima hima akamuanzishia matibabu, na kumuanzisha pia mazoezi ya viungo. Baada ya miezi kama mitatu (3), mama Deborah taratibu akaanza kuimarika afya yake. Kutokana na huduma mbovu nyumbani kwa Mjomba Kobelo, ikabidi Dr.Pesambili ajitolee kukaa nae mgonjwa wake nyumba moja na yeye.
Kwa Mjomba Kobelo kiroho safi akakubali, kwake ikawa ni nafuu kubwa kitendo cha Dr.Pesambili kumchukua mama Deborah na kuishi nae chini ya paa moja. Mgonjwa zamani hali yake ilikuwa mbaya sana kutokana na kukosa faraja toka kwa wauguzi wake. Lakini sasa chini ya mikono ya Dr.Pesambili alikuwa anapata lishe bora, huduma bora za afya na ushauri nasaha wenye kumpa matumaini mapya katika maisha yake. Baada ya kupita miezi sita (6) mama Deborah akaanza kutembea kwa kuchechemea kwa msaada wa fimbo. Ila kitu kibaya zaidi, homa ile ya kupooza ilimfanya mama Deborah asahau kumbukumbu nyingi sana maishani mwake.
Ilikuwa inakadiriwa kuwa itamchukua kama muda wa mwaka mmoja na nusu kuweza kufanikiwa kurudisha kumbukumbu zake za miaka ya nyuma. Mbaya zaidi Mjomba Kobelo akahama tena toka kijiji kile na kutokomea kusipojulikana huku Binti zake wote wakiwa wameshaolewa wanaishi na waume zao, kila mtu na lake bila hata kumpa taarifa Dr.Pesambili. Maendeleo ya Kiafya ya mama Deborah kila uchao yalikuwa yanampa faraja kubwa sana Dr.Pesambili, sasa mama Deborah kwake akageuka ndio kama mama yake mzazi. Akaajiri mtumishi maalumu wa kumpa huduma zote mama Deborah. Lakini Dr.Pesambili alikuwa anamlea mama yake wa kambo bila kufahamu. Mama Deborah nae alikuwa hajui kitu chochote kama Dr.Pesambili huyu mfadhili wake na daktari wake, mama yake mzazi ni Recho, ambaye ndio hasimu wake mkubwa, aliyemdhulumu mali za marehemu mumewe Bosi Minja na kumsababishia msongo wa mawazo uliosababisha mpaka apooze mwili. Mungu aliamua kumtumia Dr.Pesambili kumfanyia wema mama Deborah ili kufuta ubaya wa mama yake mzazi alioufanya kwa mama Deborah.
Mkataba wa kazi ulipoisha, Dr.Pesambili hakutaka kuongeza tena kandarasi yake. Aliamua rasmi makazi yake kuyafanya yawe Jijini Dar es Salaam. Alipolipwa mafao yake tu akanunua nyumba maeneo ya Mikocheni na kuhamia rasmi akiambatana na mama Deborah, ambaye kadri siku zilivyokuwa zinasonga alikuwa anazidi kuimarika kiafya. Sasa rasmi akazindua harakati za kumtafuta mama yake mzazi, kwa udi na uvumba. Ikabidi apange safari ya kuelekea Jijini Nairobi, Nchini Kenya kwenye kituo cha kulelea watoto yatima cha Cheryls Childrens Home and Learning Centre. Kituo hicho kinachomilikiwa na mtu binafsi, Mr.Ochieng kilikuwa kipo Katika mtaa wa Dagorretti Corner hatua chache kutoka barabara ya Ngong, Jijini Nairobi. Wakaagana vizuri na mama Deborah huku mama Deborah akimtakia kila la heri kwenye safari yake hiyo. Miadi walipeana kuonana baada ya wiki 2, ndipo Dr. Pesambili atarejea Jijini Dar es Salaam, hivyo akamuacha nyumbani na mtumishi wa kumpa huduma.
[emoji3586][emoji3586][emoji3586][emoji3586][emoji3586][emoji3586][emoji3586][emoji3586][emoji3586][emoji3586][emoji3586][emoji3586][emoji3586][emoji3586][emoji3586][emoji3586][emoji3586][emoji3586][emoji3586][emoji3586][emoji3586][emoji3586][emoji3586]
Alex na Deborah baada ya kumaliza mambo ya kesi, sasa walikuwa wanapika na kupakua pamoja, wanalala kitanda kimoja, wakijifunika shuka moja. Walikuwa ni wapenzi rasmi wapendanao 'Love Birds' wasiojificha tena, kila kitu hadharani. Muda wa kazi ulikuwa unapoisha tu, basi popote utakapomuona Alex basi Deborah yupo nae sako kwa bako. Wale wenye vijiba vya Roho, mahasidi wasiopenda kuona watu wakipendana mapenzi ya kweli, roho zao zilikuwa zinakaribia kuwachomoka kwa wingi wa chuki katika mioyo yao.
Chuki zilianzia Ofisini kwake Alex, wapo wasichana waliokuwa wanajiona wana sifa na vigezo vya kuwa wapenzi wa Alex kutokana na uvaaji wao nadhifu wa nguo za gharama na namna wanavyojua kwenda na wakati, lakini tahamaki Alex kadondokea kwa Deborah. Mwanamke ambaye kwa mtazamo wao ni mshamba, nywele zake anasuka mtindo wa twende kilioni. Magauni yake ya mshono wa mfuko wa mashineni kama muimba kwaya kanisani, na ngozi yake ya asili haipakwi cha ziada zaidi ya mafuta ya mgando. Walichokuwa hawakifahamu ni kuwa Alex alikuwa anatafuta mke mwema na sio gubegube linalojishebedua kwa uzuri wake.
Baada ya miezi mitatu (3), majibu ya Deborah ya kidato cha 6 yakatoka, huku akiwa amepata ufaulu wa daraja la kwanza. Alikuwa amechaguliwa kujiunga Chuo Kikuu cha Dar es Salaam 'UDSM' kusomea Uhandisi wa Chakula 'Food Engineering'. Alijawa na furaha chekwachekwa kwa kuchaguliwa kozi hiyo ambayo ingempa wigo mpana wa kujiajiri mwenyewe kwa kufungua kiwanda cha kusindika vyakula hasa katika zama ambazo ajira rasmi zilikuwa ni finyu sana. Lakini furaha yake hiyo ilitumbukia nyongo baada kutokupata mkopo toka Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi Tanzania 'Higher Education Student's Loan Board'(HESLB). Vigezo vyote vya kuweza kupatiwa mkopo alikuwa anakidhi lakini Mrs.Tonny ndio aliyechafua hali ya hewa. Kumbuka alimpa ahadi ya kumfadhili kwenye elimu ya juu hivyo Deborah katu hakujishughulisha na kujaza fomu za maombi ya mkopo huo. Lakini mpenzi wake Alex akatekeleza msemo wa ukipenda boga penda na ua lake, hivyo akajivika rasmi mzigo wa kumsomesha. Alex hakutaka kufuata maneno ya mtaani ya kuwa mchumba hasomeshwi utakuja kulia kilio cha kusaga na meno. Alimuamini Deborah zaidi ya hata anavyoiamini nafsi yake, ya kuwa hawezi kamwe kuja kumgeuka pindi atakapohitimu masomo yake ya Chuo Kikuu.
Kwa kutumia mshahara wake, Alex akakopa pesa za kumlipia ada Deborah na matumizi ya kujikimu chuoni. Muda wa kuripoti Chuoni ulipowadia, Alex akamsindikiza Deborah mpaka Chuoni. Wakakamilisha taratibu zote za Chuo zinazohitajika na Deborah akapangiwa kuishi Hosteli za Mabibo zilizopo barabara ya Mandela jirani na eneo la Ubungo. "Mpenzi Deborah, nakutakia masomo mema, kikubwa kumbuka kulinda ahadi yetu, ya kuwa tutakuja kuoana pindi utakapomaliza Chuo. Jitahidi kujilinda na vishawishi vya kila aina. Upo ndani ya Jiji la Dar es Salaam lenye watu wa kila sampuli, wenye uwezo hata wa kukuhonga nyumba na magari ili mradi wavuruge penzi letu. Lakini kumbuka pia maisha ya Chuo ni matamu sana lakini ni mafupi mno, ukivuruga muelekeo wako ndani ya miaka 4, utakuja kujutia maisha yako yote, hivyo akili kumkichwa chako" alizungumza Alex kwa hisia kali, nasaha ambazo zilimtoa machozi Deborah pindi walipokuwa wanaagana hapo Mabibo Hosteli.
Deborah hakuwa na maneno mengi zaidi ya kushukuru kwa hisani ya kusomeshwa na mpenzi wake, kipindi ambacho aliona kabisa ndoto yake ya kielimu inataka kutoweka. "Nakuahidi sitokuangusha, nitalilinda penzi letu kwa hali na mali, na nitasoma kwa bidii ili kuhakikisha ninapata maarifa stahiki. Nakuahidi pindi nikimaliza Chuo nitafungua kiwanda cha kusindika nyanya kule kule Mzumbe, na hutojuta kwa pesa ulizonilipia ada, tutakuwa matajiri wakubwa tu. Nataka siku moja tukae meza moja na hasimu wetu Mrs.Tonny tukiwa tunaongea lugha moja ya uwezo wa kipesa" aliongea Deborah kwa furaha huku akimpa matumaini makubwa mpenzi wake Alex.
Wakaachana, siku zikaanza kusonga, miezi kadhaa ikakauka, huku Deborah akijihesabia kuwa yupo sasa yupo salama salimini, ndani ya mikono ya mtu makini kama Alex. Likizo ndogo zote alikuwa lazima arejee Mzumbe kwa Alex. Nae Alex kwa upande wake, majukumu ya kazi yaliongezeka hivyo kumfanya muda mwingi awe anautumia ofisini. Akitoka saa 1 asubuhi kurudi kwake ni saa 1 usiku. Sana sana mapumziko yake rasmi yalikuwa ni siku ya Jumapili, hali ambayo ilimlazimu kuajiri mtumishi wa kike wa kuja na kuondoka kwa ajili ya usafi wa nyumba, kufua nguo na kupika chakula. Kabla ya kuajiri mtumishi huyo, alipata baraka zote za Deborah hasa baada ya kuthibitisha uzito wa majukumu aliyo nayo mpenzi wake hivi sasa.
Lakini kama ujuavyo ya kuwa Deborah ni mtu wa mikosi, daima hawezi kupata starehe ya kukesha mpaka che, lazima tu kitokee kitu cha kuchafua hali ya hewa, akajikuta anaingia kwenye mgogoro wa mapenzi na Alex. Mgogoro ambao ulisababisha penzi lao lisambaratike vipande vipande, na kumuacha Deborah yupo njia panda hajui cha kufanya.
Mgogoro wao ulianza wakati wa likizo ndogo ya karibu na mapumziko ya Sikukuu ya Pasaka, Deborah akiwa ndio kwanza amerejea toka Chuoni, ghafla yule dada wa kazi za ndani akatoweka bila taarifa. Simu yake ikawa kila ikipigwa ili kufahamu ana tatizo gani lililomfanya asije kazini ikawa haipatikani. Wakakubali matokeo kuwa huenda kazi imemshinda au kapata sehemu nyingine yenye maslahi zaidi ya hapo.
Asubuhi yake iliyofuatia, wakati Alex yupo kazini hana hili wala lile, Deborah akiwa kwenye harakati za usafi wa nyumbani akaifuma barua iliyokuwa imesokomezwa chini ya sofa ukumbini. Kichwa cha habari juu ya bahasha ya barua hiyo, alipokisoma tu kilimpa mshtuko mkubwa Deborah. Jasho jekejeke likaanza kumtiririka mwilini mwake huku mapigo ya moyo wake yakienda mbio. Akajikuta anaishiwa nguvu na kuamua kukaa kitako chini ya sakafu ili aisome vizuri barua hiyo mbaya. Akajikuta ghafla anatetemeka mwili mzima kama mgonjwa aliyepigwa na homa kali. Vidole vya mikono vilikuwa vinamtetemeka mithili ya mnywaji gongo aliyekubuhu. Kwa ufupi Deborah alijihisi kufa kufa.
Hakuamini mtu aliyemwamini na kumthamini kama Alex angeweza kumtenda kiasi hicho. Kilichokuwa kinampa mawazo ni kuwa ataiweka wapi sura yake kwa mashosti zake wa Chuoni ambao kutwa kucha alikuwa anawatambia kuwa amepata mpenzi mwenye kujiheshimu na anayempenda kwa dhati. Licha ya wenzake kumtahadharisha kuwa asiweke matumaini asilimia 100% kwa mwanaume, lakini Deborah alikuwa anamkingia kifua Alex. Sasa leo kupitia barua hiyo alikuwa anaonjeshwa asali kwa ncha ya kisu. Deborah akajikaza Kisauni na kujitutumua kuifungua barua hiyo.
Barua ambayo juu ya bahasha kulikuwa na maandishi ya herufi kubwa, "KWAKO MPENZI ALEX". Ndani ya barua sasa kulikuwa kunasomeka kama ifuatavyo; "Mpenzi Alex, nimeamua kukuachia ujumbe huu kama nilivyokuelekeza kwenye meseji ya simu yako kuwa utaukuta chini ya sofa lako unalopenda kukalia. Nimeamua kupotelea kusipojulikana kutokana na shinikizo lako la kutaka nitoe mimba uliyonipa ili mchumba wako asijue kama nina mimba yako. Nakutakia kila la heri katika maisha yako na huyo mchumba wako unayempenda sana kuliko mtoto wetu aliye tumboni mwangu. Nitamlea peke yangu bila kuhitaji msaada wako wowote lakini hesabia huna mtoto na mimi". Deborah alipomaliza kusoma barua hiyo alijikuta anajiona anaishiwa nguvu na kujilaza kwenye zulia la pale sebuleni. Kifua chake kilikuwa kinafukuta fukuto la joto la hasira dhidi ya Alex. Mawazo lukuki yalimvamia kichwani mwake, huku Ibilisi akimpandia kichwani na kumshadidia ajiondoshe uhai wake. Alijilaumu sana kukubali kuwa mpenzi wa Alex bila hata kupata nafasi ya kumchunguza tabia zake kiundani.
"Ina maana kipindi chote nipo Chuoni, huyu dada wa kazi alikuwa ndio alikuwa anajinafasi, ama kweli paka akitoka panya hutawala" alijisemea kimoyomoyo Deborah na kuamua kuinuka pale alipojilaza. Akili yake ilimuambia aifiche ile barua, ili aone mwisho wa sinema hiyo mpya kwake ya mapenzi baina ya Alex na dada wa kazi. Deborah akiwa hana hili wala lile, akashtukia mlango wa barazani unafunguliwa kwa kishindo, kisha Alex akaingia ndani ya sebule. Bila kuzungumza na mtu yoyote akaenda kukaa kwenye sofa lile lile aliloelekezwa kuna barua yake.
"Kulikoni mbona salamu unatuvamia, umepatwa na maswaibu gani mwenzangu mbona unanitisha..!" alisema Deborah huku akijikaza kutokumuuliza chochote kuhusiana na barua ile ili amuone kama atakuwa mkweli na kueleza kinagaubaga bila mficho. "Aaaah....take easy hamna kitu nimekuja kunywa chai tu, tayari umepika..?" aliongea Alex huku akilazimisha tabasamu. "Tayari ipo mezani, ingawa hukunipa taarifa kama utakuja kunywa chai nyumbani maana huna kawaida hiyo ukiwa kazini" Deborah alizidi kumfunga Alex ili kumtengenezea mazingira ya kuelezea kitu kinachomsumbua. "Hapa si nyumbani kwangu? usiwe na mashaka nimeamua tu kukufanyia surprise..twende basi tukapate wote staftahi" alijibaraguza Alex huku ameuviringisha mkono wake kwenye kiuno cha Deborah. "Ahsante mpenzi, lakini mie nimeshakunywa, sasa naenda kujipumzisha chumbani sijisikii vizuri, nimekunywa dawa za kutuliza maumivu " alisema Deborah huku akiutoa mkono wa Alex kiunoni mwake na kuelekea moja kwa moja chumbani kwao. "Pole sana, kapumzike unono..." alisema Alex huku akimuangalia Deborah namna anavyomalizikia kuelekea chumbani kwao.
Alex alivyomuona Deborah ameshamalizikia kuingia chumbani akarudi kwa kasi pale sebuleni mpaka kwenye sofa lake analopenda kukalia. Akalinyanyua kuitafuta barua aliyoelekezwa na mtumishi wake aliyetoweka. Alex tokea alipopata ujumbe wa kwenye simu ya mkononi, alikosa amani kabisa ya kuendelea kufanya kazi ofisini. Alijutia kitendo cha kumkubalia kuwa mtumishi wake wa nyumbani, mpaka akamuingiza kwenye mtego uliosababisha atembee nae kimapenzi. Siku ya kwanza Alex kumuona dada huyo alivyokuwa kuomba kazi hakuamini kama kweli dada huyo anatafuta kazi za ndani hasa kutokana na urembo wake wa shani. Urembo ambao ulimbabaisha Alex vilivyo na kumkubalia ombi lake, huku akijifanya kuomba ushauri kwa mpenzi Deborah ili kuondosha fikra potofu. Mpaka anavyopokea ujumbe huo wa simu alishakuwa ametembea nae si chini ya mara mbili. Lkini anachokumbuka ni kuwa mara zote alizofanya nae mapenzi alitumia kondomu, hakufanya ngono uzembe sasa mimba hiyo amepataje, ni kitu kilichokuwa kinamfanya achanganyikiwe vilivyo.
"Kama Deborah aking'amua nitambeba na mbeleko gani apate kunielewa kuwa ni shetani tu amenipitia..! " alijisemea peke yake Alex kimoyomoyo huku akiwa anaendesha lile sofa alilonyanyua. Deborah mchezo wote anaoufanya Alex wa kuitafuta barua chini ya sofa alikuwa anaushuhudia kupitia upenyo wa mlango wa chumbani. Alipojifanya anaenda kulala, ilikuwa ni janja ya nyani tu, ili kumpa nafasi Alex ya kujitawala sebuleni. Deborah akajithibitishia mubashara bila chenga kuwa Alex ni kweli kambandika mimba dada wa kazi kutokana na juhudi zake za kutaka kuinyakua barua hiyo. Deborah akajikokota kinyonge mpaka kitandani na kujitupa kama furushi la mwizi. Macho yake yalikuwa yanabubujikwa machozi bila ukomo, huku akiwaza na kuwazua maamuzi ya kufanya juu ya penzi lao. Mawazo mengine yakimshawishi aachane na Alex aanze maisha yake upya katika ulimwengu wa huba, lakini kikwazo kikaja kwenye suala la kusomeshwa, nani atakuwa tayari kumlipia ada ya Chuo Kikuu na gharama zingine kama anavyofanya Alex. Akajiona kabisa analazimika kuwa mtumwa wa Alex kwa sababu tu za kiuchumi lakini tayari alishamfuta thamani kwenye moyo wake.
[emoji3586][emoji3586][emoji3586][emoji3586][emoji3586][emoji3586][emoji3586][emoji3586][emoji3586][emoji3586][emoji3586][emoji3586][emoji3586][emoji3586][emoji3586][emoji3586][emoji3586][emoji3586][emoji3586][emoji3586][emoji3586][emoji3586][emoji3586][emoji3586][emoji3586][emoji3586][emoji3586]
"Koh...Koh....Koh....Koh....fungua mlango...!" ilikuwa sauti nzito iliyoshiba ikishinikiza yeyote aliyekuwa ndani ya nyumba ya Alex afungue mlango. Deborah akiwa jikoni anakarangiza maakuli ya jioni, wito huo ukamshtua kidogo. Akawa anasikilizia wito huo akijaribu kutaka kutanabahi sauti hiyo ni ya nani. Alipozidi kusikia wito huo ukitaka mlango ufunguliwe, ikabidi akurupuke na kanga moja kwenda kufungua mlango huo kujua kulikoni. Alipoufikia mlango huo na kuufungua mshtuko wa ghafla ulimshika. Alihisi mapigo ya moyo wake kama yanataka kusimama kwa ghafla. Akajikuta miguu yake haina ushirikiano na sehemu ya juu ya mwili wake, ikaanza kushindwa kuhimili uzito wake, akajikuta anachegama mlango huo ili kupata msaada wa kuegemeza mwili.
Alimuona Alex akiwa amefungwa pingu za mikononi huku machozi yanamtiririka machoni mwake. Deborah alikuwa anatamani afungue mdomo wake aulize kulikoni lakini akajikuta anapatwa na gagaziko la ulimi hawezi kuongea chochote. "Ingia ndani, unatuchelewesha fisadi mkubwa wewe" aliongea yule mtu mwenye sauti nzito aliyekuwa anagonga mlango. Walikuwa ni askari kanzu wawili wameambatana na Mtendaji kata wakimleta Alex nyumbani kwake. Majirani nao waliokuwa wamebakia nyumbani muda huo nao wakaanza kujongea kutaka kujua kulikoni.
"Dada habari yako, sisi tumekuja kufanya upekuzi nyumbani kwa mtuhumiwa huyu Bwana Alex kutokana na tuhuma za kuomba rushwa ya ngono kwa mwanafunzi wake. Hivyo tumekuja kukagua mitihani ya wanafunzi wake aliyosema amehifadhi nyumbani kwake ili wana usalama iwasaidie kwenye taftishi yao dhidi ya mhadhiri Alex. Hivyo kuwa na amani kwa sababu tumekuja kisheria" alisema Mtendaji Kata nia na madhumuni ya ujio wao pale nyumbani. "Sawa hamna shida, kwani amefanyaje mpaka mnamtia pingu kama jambazi? " alijitutumua Deborah kuuliza kwa tabu akitaka adadavuliwe kwa undani tuhuma hizo. "Dada usichoelewa kitu gani, huyu jamaa yako tumemkata ofisini kwake leo saa 9 alasiri akijiandaa kufanya mapenzi na mwanafunzi wake ofisini kwake..! " aliongea yule askari kwa kufoka huku akimhimiza Alex asonge ndani ya nyumba hiyo akaonyeshe mahali anapohifadhi nyaraka za wanafunzi wake. Deborah akabaki amesimama mlangoni amebung'aa kwa mshangao anawasindikiza kwa macho. Alex wakati wote alikuwa anatikisa kichwa kuonyesha hakubaliani na tuhuma hizo, ukweli halisi wa tukio hilo alikuwa anaujua Alex na huyo mwanachuo aliyetoa taarifa kwa vyombo vya dola juu ya kusumbuliwa rushwa ya ngono ili apewe maksi za kumfaulisha kwenye somo analofundisha Alex.
Baada ya nusu saa ukaguzi wao ukakamilika huku wakiondoka na mitihani ya wanafunzi waliyoikuta nyumbani kwa Alex. "Naomba umfahamishe mama yangu mzazi tukio lote..!" aliongea Alex kumpa maagizo Deborah huku akikwepesha macho hataki kuangaliana uso kwa uso na Deborah. Alichofanya Deborah ni kuitikia kwa kichwa, kuonyesha kuwa atatekeleza maagizo hayo. "Mshahara wa dhambi ni mauti, umeumbuka Alex, umempa mimba dada wa kazi na leo leo kabla jua halijakuchwa unapigwa kofi lingine la rushwa ya ngono, Ahsante sana kwaheri..!" alisema Deborah baada kulisogelea gari la wazi lililotumika kumbeba Alex kwa upande wa nyuma. Alex hakuwa na kitu cha kujibu, soni ilimjaa usoni kwake, macho yake yamemwiva wekundu.
"Kumbe barua chini ya sofa kaichukua Deborah..!, ama kweli siku ya kufa nyani miti yote" hizo zilikuwa ndio fikra za Alex wakati huo. Gari hilo likaondoka eneo hilo kwa manjonjo likiwaacha majirani midomo wazi kila mtu anasema lake. Deborah haraka haraka akaingia ndani ya nyumba na kujifungia kwa komeo. Alijua majirani wale habari kuuzwa ndio wakati wao muafaka wa kuja kuchokonoa mambo ya watu. Watamuingia kwa gia za kumpa pole kisha waanze kumdadisi undani wa tukio la Alex. Alipoingia ndani Deborah akatuma meseji kwa mama yake mzazi Alex akimuelezea tukio zima kisha akazima simu yake kukwepa maswali, baada ya hapo akaanza kupanga nguo zake na vifaa vyake mbalimbali kwenye begi lake la safari. Alishajua penzi lake na Alex ndio limekufa rasmi, kwani lazima atafungwa jela kwa kosa la kuomba rushwa ya ngono.
Moyoni mwake aliyakinisha asilimia 100% kuwa Alex amehusika hasingiziwi hasa akirejea tukio la kumtundika mimba dada wa kazi. Pia hata kama angeendelea kukaa hapo lazima angetimuliwa katika nyumba na Uongozi wa Chuo cha Mzumbe ili kupisha watumishi wengine wasio na makazi. Kilichokuwa kinambangua kichwa ni kuwa anaelekea wapi akitoka hapa nyumbani kwa Alex, na nani atamlipia ada Chuoni na kumpa pesa za matumizi hali ya kuwa ni kesho kutwa tu Chuo kinafunguliwa. Chakula chake alichokuwa anakipika jikoni hakuwa na hamu nacho tena, akakitekeleza huko huko. Akiwa na begi lake pembeni akaa juu ya sofa sebuleni anatafakari. Muda ulikuwa inayotoka, magharibi ilikuwa inakaribia, muda muafaka aliopanga kuondoka huku kukiwa na kigizagiza kukwepa fedheha mbele ya majirani. Ghafla bin vuu akakurupuka kwenye sofa na kuanza kufungua begi na kuchambua vitu vyake pembeni ya begi kana kwamba kuna kitu anatafuta. Akaunda tabasamu jepesi baada ya kukiona kitu alichokuwa ananitafuta. Alikuwa anatafuta kadi yenye anuani na namba za simu za mfadhili wake mpya Timammy alizompa siku alipomchomoa mikononi mwa Mrs.Tonny kule mahakamani kwa kumuwekea dhamana. Tokea siku ile alipomtafuta mara moja na hakumpatana hewani hakujisumbua tena kumtafuta. Lakini leo alikuwa ametumbukia kwenye dhiki yenye kuhitaji utatuzi wa haraka hakuwa na jinsi zaidi ya kumtafuta tena, kama ujuavyo mficha ugonjwa mauti humuumbua. Sakata lake lilimfikisha mahali pa kuchagua kusuka ama kunyoa, hivyo ampige pande Timammy afukuzwe Chuo kwa kukosa ada au amtafute Timammy amuombe tena msaada wa kusomeshwa ili aweze kuhitimu Chuo.
Deborah alijawa na matumaini kuwa atamuelezea kila kitu Timammy kuwa Mrs.Tonny ndio alimuingiza chaka asiombe mkopo kwa kujimwambafai kuwa atamsomesha akaishia kumtelekeza machakani. Akatoa simu yake kwenye pochi la mkononi, na kuanza kuingia namba kwa ajili ya kuipiga simu ya Timmamy. Bila mafanikio yoyote namba zote za Timammy zilizokuwa zimeorodheshwa kwenye kadi ile zilikuwa hazipatikani. Jasho jekejeke likaanza kumvuja Deborah huku machozi yakianza kumlengalenga upya machoni mwake. Matumaini yake aliyaona kabisa mithili ya mshumaa uliowashwa kwenye uelekeo wa upepo mkali. Akaanza kuvuta tafakuri jadidi ya maisha yake upya tokea azaliwe mpaka leo yupo Chuo Kikuu akajiona kabisa hajawahi kabisa kuishi maisha ya kula bata kama walivyo wenzake, yeye kila siku kidagaa kinamuozea yeye tu. Machozi sasa yakaanza kumtiririka kwa wingi bila kizuizi na kilio cha kwikwi. Ghafla akanyamaza kulia, akatoa hanchifu yake kwenye pochi yake na kujifuta machozi yote. Akachomoa noti ya sh.5,000/= na kufungua mlango wa sebuleni atoke nje. Alipanga kwenda duka la dawa kununua vidonge ili avibugie afilie mbali. Alishakata tamaa ya kuishi, hakuona tena thamani ya maisha ya dunia, kwake aliona bora awafuate wazazi wake waliotangulia jongomeo. Kabla hajanyonga kitasa cha mlango, simu yake ikaanza kuita kwa fujo. Akairudia alipoangalia ilikuwa ni namba binafsi 'private number' akaikata na kuizima simu kabisa kisha akairudisha kwenye kipochi tena.
Akachomoka mbio mbio kuelekea duka la dawa, bila kutanabahi kuwa ile simu aliyoikata ni ya mfadhili wake Timammy aliyekuwa anamtafuta kwa udi na uvumba muda mchache uliopita. Ama kweli hasira hasara, Deborah alikuwa kama vile anapiga teke furushi la pesa, anapishana na ngekewa. Baada ya dakika takribani 10 Deborah akawa anarejea akiwa na tembe zake mkononi. Akiwa meta chache kabla ya kufika nyumbani akashtuka kuona gari la kifahari aina ya 'Vanguard' limeegeshwa upenuni kabisa mwa nyumba ya Alex. Akasita kwenda mbele akasimama, akiwa ameshtushwa roho yake kuwa huenda amekuja kukamatwa yeye sasa. Akiwa bado amepigwa na mzumbao akaliona lile gari limeamshwa linageuzwa na kuanza kuja uelekeo wake pale aliposimama. Deborah hakuwa na simile tena, akageuka, akavitupa vile vidonge na kutaka kuanza kutimua mbio, tayari alikuwa ameshachanganyikiwa, anaona kabisa penzi lake na Alex linampiga pute furaha yake katika maisha. Kichwa chake kilikuwa ni kama dampo ya mawazo machafu ya kila aina. Tahamaki lile gari likawa limefunga breki karibia kabisa na miguu yake, Deborah akaanguka mpaka chini kutokana na kiwewe cha hofu iliyomsonga moyoni mwake. Akaharakisha kunyoosha mikono yake juu anahema kwa kutweta kuonyesha kuwa anahitaji amani amesalimu amri. Lile gari lilifungwa vioo vyeusi lisivyoruhusu kumuona aliyekuwa ndani ya gari. Kioo cha gari upande wa siti ya mbele ya abiria kikaanza kushushwa taratibu mpaka aliyekaa siti ile akaonekana dhahiri.
"Deboraaaah.....usikimbie ni mimi Timammy nimekufuata...!" aliongea mtu aliyekuwa amekaa siti hiyo akiwa amevaa miwani yenye vioo vyeusi. Akaivua miwani yake na kufungua mlango wake akashuka chini na kumsogelea Deborah pale alipokaa kwenye mchanga. Akanyoosha mkono wake mrefu kutaka kumpa msaada Deborah wa kuinuka toka ardhini. Deborah alinyoosha mkono wake lakini kwa wasiwasi bado akiwa amepigwa na butwaa kaachwa mdomo wazi. Hofu yake ilikuwa haamini kama kweli huyu ni Timammy alidhania labda ni mzuka wake Timammy. "Haiwezekani mtu niliyempigia simu robo saa iliyopita tena sikumpata hewani ghafla awe amefika mpaka kwenye nyumba ninayoishi" aliwaza Deborah. "Najua unajiuliza maswali kibao na hupati majibu kuhusu ujio wangu, kwa ufupi sakata la mchumba wako kuomba rushwa ya ngono limetangazwa mapema sana kwenye redio na televisheni, na mie nilikuja kijiji cha Mlali hapo jirani na Mzumbe nikiwa kwenye harakati za kutafuta eneo la kufungua kiwanda cha kusindika nyanya ndio nikaonelea nichepuke mara moja kuja kuangalia usalama wako..! " aliongea Timammy kwa kujiamini bila kupepesa macho wala kutafuna maneno, kauli ambayo kidogo iliondosha hofu katika moyo wa Deborah. Kama ujuavyo ukiwa kwenye dhiki na shida hata akili inapunguza uwezo wake wa kuchanganua mambo kwa upana. Mtu mwenye njaa anafikiria kwa msaada wa tumbo lake, kichwa chake kinaenda likizo.
Deborah akajinyanyua ardhini na kujikung'uta mavumbi kwenye sketi yake. Baada ya maongezi mafupi ya kusafiana nyoyo baina yao, Deborah akaingia ndani kufuata begi lake aweze kuondoka na Timammy. Moyo wa Timammy ulijawa na furaha fokofoko kutokana na kukaribia kutimiza ndoto yake ya kumfanya Deborah awe mke wake wa kufanya nae maisha. Msichana ambaye amemsubiria kwa zaidi ya miaka 6 na ushee ili aweze kumtia kwenye himaya yake. Timammy ndio aliyeandaa mipango yote ya maangamizi kwa Alex bila Alex na Deborah kutanabahi kuwa ni adui yao. Baada ya Timammy na dereva wake kumkosa Deborah kule shuleni na kuelekezwa kuwa yupo Morogoro. Katika juhudi zao za kumsaka wakafanikiwa kuelekezwa kuwa anafanya kazi dukani kwa Mrs.Tonny. Walipofika hapo dukani ndio wakapata hadithi ya Deborah kuwekwa ndani rumande kwa kosa la wizi wa vito vya thamani. Kwa jinsi Timammy anavyomfahamu Deborah kwa tabia zake njema, moja kwa moja akajua ni zengwe tu lililosukwa na Mrs.Tonny, mwanamke ambaye anamjua kinagaubaga kuwa ni tajiri lakini ana tabia za kikhabithi sana.
Uzuri wake Mrs.Tonny alikuwa anamuogopa vibaya sana Timammy kutokana na mtifuano mkali waliowahi kuzozana katika kugombea tenda mbalimbali zenye ulaji serikalini. Ndio maana ikawa rahisi kwa Timammy kumaliza kesi ya Deborah kiulaini kama kumsukuma mlevi. Kikwazo pekee kilichokuwa kimebakia mbele Timammy alikuwa ni Alex. Akaitafuta mbinu iliyoenda shule ili kumchomoa Deborah kwa Alex, hakutaka kutumia mbinu ambazo Deborah zitamfanya amgundue yeye kama ndio mpishi faraka katika penzi lake na Alex kwa kutumia kuni za fitina. Timammy Kwa ujuba wake uliotopea angeweza kumuua Alex au kumtia kilema chochote ili ajitwalie kirahisi Deborah ila akaamua kutumia njia za kisayansi ambazo itakuwa ngumu Deborah kugundua kuwa yeye ndio mhusika wa matatizo ya Alex.
Akatumia fursa ya upweke wa Alex pindi mpenziwe alipokuwa Chuoni kumpenyeza dada wa kazi ambaye ni mrembo wa haja kumtia mtegoni Alex, akafanikiwa kunasa. Ndipo ukasukwa mpango yule dada ajisingizie amepata ujauzito na apotee kimoja ila ahakikishe taarifa zinavuja kwa Deborah. Ramani ya tukio zima ikachorwa kiustadi mkubwa kuwa siku hiyo hiyo inayovuja habari ya ujauzito wa dada wa kazi kabla jeraha la moyo wa Deborah halijakauka, atoneshwe tena ili amchukie kimoja Alex. Ndipo akapangwa msichana mrembo, mmoja wa wanafunzi wa Alex aingie ofisini kwa Alex kisha askari kanzu wavamie wamkamate Alex kwa kigezo cha kuomba rushwa ya ngono. Waandishi wa habari na wapiga picha wakapewa chao kuhakikisha wanaripoti tukio la Alex kiufasaha na kwa kuongeza chumvi zaidi ili kuzidi kuchafua hali ya hewa. Sasa mipango ya Timammy ilikuwa inakaribia kutimu, Deborah anaingia kwenye himaya yake kiulaini mithili ya mbwa mbele ya chatu.
Punde si punde Deborah akatoka na begi lake, kisha akaacha funguo za nyumba ya Alex kwenye nyumba ya jirani huku akimpa maelekezo kuwa mama yake Alex atakuja kuufuata ufunguo hapo, kisha akaingia kwenye gari la Timammy na kutokomea zao, usiku mbichi huo wa saa moja na robo usiku. Deborah mchezo aliokuwa anaucheza wa kutaka auni toka kwa Timammy ilikuwa ni kama kurudisha tende Manga, kamwe asingepata faraja anayoitarajia. Auni iliyokuwa inatolewa na Timammy kwa Deborah ilikuwa ni kwa malengo maaalumu.
[emoji3586][emoji3586][emoji3586][emoji3586][emoji3586][emoji3586][emoji3586][emoji3586][emoji3586][emoji3586][emoji3586][emoji3586][emoji3586][emoji3586][emoji3586][emoji3586][emoji3586][emoji3586][emoji3586][emoji3586][emoji3586][emoji3586][emoji3586][emoji3586][emoji3586][emoji3586]