Riwaya magnum22

Riwaya magnum22

Nmekuja mbio huku nikijua jamaa ameshatuma cha asubuhi kumbe bado!!! Uraibu wa riwaya hii ya Magnum 22 unanitesa vilivyo! Mkuu fanya fanya mambo utupie muendelezo huo... siku iende vyema!
Ikiwezekana leo fanya vipande vitatu kabisa, cha asubuhi, mchana na usiku.
 
MAGNUM22

Sehemu 16

USIKU WA MANANE
SIKU HIYO HIYO
Wakiwa wote wamelala, Kamanda Amata alitembea taratibu koridoni na kuelekea chumba maalumu chenye kila takataka ya mawasiliano, mkononi mwake alikuwa na vitu vitatu tu; kijitabu kidogo cha kumbukumbu, na kipande cha noti na mkanda wa kiunoni aliyopewa kule kaburini. Akaviweka mezani na kuchukua kile kijitabu cha kumbukumbu na kuanza kukisoma kurasa moja baada ya nyingine, lugha iliyotumika kuandika kumbukumbu hizo ilikuwa tatanishi, sehemu nyingine akaelewa na kwingine kukapita.
Hata huyu naye alikuwa anamsaka Martin Gupter! Akawaza na kuendelea kupekua kijitabu kile chenye mambo mengi. Katikati ya kijitabu kile akakutana na namba ambazo hazikuwa zikieleweka, akazikodolea macho asijue hata ni nini maana yake, akaanza kuingiza moja baada ya nyingine kwenye kompyuta lazkini hazikumpa maana, akaachana nazo na kuendelea kusoma vitu vingine. Kila alipokuwa akisoma kuna baadhi ya vitu alikuwa akiviandika pembeni kwenye karatasi nyeupe mpaka aliporidhika. Akaichukua ile noti na kutazama vizuri.
Kipande chake kiko wapi? Akajiuliza, akaona haina haja kuumiza kichwa maana si rahisi kujua, akajiegemeza kitini na kupitiwa na usingizi mzito.
* * *
Asubuhi kulipokucha akajikuta bado yupo palepale amekarti na kila kitu kiko vilevile, “Usingizi hauna adabu!” akajisemea kwa sauti ndogo na kukichukua kile kijitabu na kuendelea kurasa nyingine za mbele. Karibu na kurasa za mwisho akakutana na kifungu cha maneno ambacho kimezungushiwa kama kiboksi hivi kwa kalamau ya wino, na katika kifungu hicho kuna herufi zilizchanganywa na tarakimu na alama nyingine nyingine.
“Identity!” akajisemea, kwa kuwa alielewa kuwa huo ni utambulisho wa mwenye kijitabu hiko. Kamanda Amata akshusha pumzi kwa maana zaidi ya kusikia kikohozi na chafya na kuhisi mshiko wa mkono wa marehemu, hakuwahi kumwona sura mtu huyo kutoka na giza nene na zito ndani ya kaburi lile.
“Ni nani huyu?” akajiuliza huku akiinuka na kuiende kompyuta kubwa iliyo ndani ya chumba hicho akaiwasha. Mara nyingi kompyuta hii hutumiwa na Chiba katika maswala ya utambuzi na kadhalika. Akiwa katika kuiweka sawa ili afanye kazi yake, akasikia mlngo ukifunguliwa, akageuka na kukutana macho kwa macho na Chiba.
“Kamanda vipi?” Chiba akamuuliza.
“Kuna kitu nataka nikitambue hapa, sasa nimeona kukusmbua si fresh..!” akajibu.
“Aaaah, kitendo tu cha kuiwasha hiyo kompyuta mimi kule nimejua ndiyo maana nikaamka kuja kutazama kulikoni, isije kuwa tumevamiwa na mchwa,” Chiba akajibu huku akiwa tayari kafika eneo lile.
“No! si hivyo, ingiza hapo … enheee, sawa, bofya hapo kwenye scan … yes! Sasa subiri!” Chiba akamwelekeza Kamanda jinsi ya kufanya baada ya kugundua kuwa amekose katika kuingiza hizo. Baada ya dakika kama mbili hivi, Amata akajikuta katokwa na macho na kupigwa bumbuazi kwa maelezo yanayokuja juu ya kioo kile.
“Unamjua?” Chiba akauliza.
“Yes!” Amata akajibu, “Namjua vyema, huyu bwana anaitwa Costantine, ndiye niliyemwokoa dhidi ya mkono wa Pereira kule Angola, huyu naye kama mimi alikuwa katika harakati za kumsaka Martin Gupter… aisee, Costantine amekufa!” akaongeza kusema kisha chozi likamdondoka.
Chiba akampigapiga begani huku naye akisoma maelezo yaliyojitokeza katika kifaa hicho.
Mpelelezi binafsi! Akawaza.
Amata akainua kichwa na kutulia kimya, “Ni vipi kama asingekuwa yeye, ningekuwa hai leo? Si kwamba nalia kwa sababu amekufa, no, kufa ni ratiba ya kila mja, ila ninalia kwa sababu nakumbuka maneno ya wahenga ‘wema hauozi’,” akamwambia Chiba kisha akaendelea kusoma maelezo yale vizuri na kumjua vyema rafiki huyo aliyemtoroka kule Angola..
Alikuwa anajua ni wapi Gupter anapatikana! Akawaza huku akiendelea kuchambua yale maandishi na mwisho wa yote akakutana na ramani ndogo, akaitazama vizuri na kuielewa akisaidia na Chiba.
“Hii ni ramani ndogo ya Waterloo!” Chiba akamwambia Kamanda Amata.
“Ina maana Costantine alitumia ramani hii kufika mahalia haswa alipo Martin Gupter!” Amata akamwambia Chiba huku akiiprinti ramani ile katika karatasi. Alipohakikisha anayo tayari mkononi, akaendelea kuchambua kama atakutana na vingine vya kumfaa. Alipojiridhisha kuwa hakuna akafunga kompyuta na kubaki katulia kimya huku kile kijitabu kikiwa mkononi mwake pamoja na kile kipande cha noti.
“Bado nitajua moja baada ya jingine!” akasema huku akitoka ndani ya chumba kile na kurudi katika chumba chake cha kulala na kujibwaga kitandani akiwa na mawazo mengi.

WATERLOO
Katika jumba kubwa lililotengwa na makazi ya watu na kujengwa mbali kidogo ila pembezoni mwa Mto Lofa, Martin Gupter alikuwa na kikao cha dharula na swahiba wake yaani Amanda na Fredy. Aliwaita kwa mazungumzo mara baada ya kupata ujumbe kuwa sasa anasakwa kwa udi na uvumba kila kona ya Afrika.
“Tupo matatani,” akawaambia, “kuna timu ya wapelelezi imesambazwa, Angola, Tanzania na Ivory Coast kwa ajili ya kutusaka,” akaongeza.
“So?” Fredy akauliza.
“Lazima tuwe na tahadhari kubwa sana tutokapo nje, tuwasome kila tunaowaona, tutakayemtilia shaka tu lazima tumtie mkononi,” akamjibu.
Ukimywa sekunde kadhaa ukajidai katikati ya watatu hawa.
“Sina wasiwasi!” Amanda akasema.
“Kwa nini?” Martin akauliza.
“Kama kuna mtu nilikuwa na mwogopa na kumhofu ni huyu wa Tanzania, kwa sababu ni yeye tu ambaye tunaweza kusema tumepambana na anajua wapi tupo,” akasema.
“Aaaaah huyo anongea na babu zake saa hii…”
“Kama ni hivyo, siwezi kuviogopa vimburu vingine hivi, vikimtia mguu hapa tunavitenganisha roho na mwili,” Amanada akajibu. Wakiwa katika mazungumzo hayo simu ikaita kwa nguvu na fujo, Martin akampa ishara Amanda akaipokee, naye akafanya hivyo.
“Yes!” akaitikia na kumsikiliza mtu wa upande wa pili.
“(…)”
“Ok, copy that!” akajibu na kukata simu kisha akaja kwa wenzake na kuketi pale pale alipokuwa ameketi mwanzoni.
“Vipi?” Martin akauliza.
“Subiri nukushi inaleta habari sasa hivi, nafikiri inabidi tufanye hesabu za kuto sasa,” akawaambia na sekunde chache tu, mashine ya nukushi ikapata uhai na kuanza kupiga kelele zilizofuatiwa na karatasi kama mbili hivi. Amanda akainuka tena na kuziendea, akazinyofoa na kurudi nazo kitini, akampa Martin kuzisoma.
… najua kuwa mna miezi miwili ya kumaliza kazi yenu, hapa nataka kuwapa nafasi nyingine pekee ambayo mnaweza kuitumia kukamilisha kazi yenu kabla ya wakati na kupokea pesa zenu mbaki mnatwanga maisha mtaani.
…Kutakuwa na kikao cha dharula katika Jiji la Addis Abbaba, kikao hiki kita kitahuduriwa na marais wachache na viongozi wengine wa Baraza la Usalama, lengo ni kufanya tathmini ya uchunguzi wao na pia wanataka kutoa tamko la mwisho juu ya mzozo huu wa Somalia.
… kwa hiyo kuna mambo mawili, ama wakubaliane na matakwa ya Jaffery Bakhar au wakatae, tayari wamemtumia taarifa ya yeye kufika Addis kwa ajili ya mazungumzo ya swala hilo. Je; mwaweza kuitumia nafasi hiyo?
Pamoja na maelezo mengi, haya nayo yalikuwa ndani ya nukushi hiyo. Martin akashusha pumzi na kuwapa wenzake ile karatasi nao wakaisoma kwa zamu. Baada ya wote kumaliza ikawekwa mezani.
“Vipi, tutumie nafasi hii?” Fredy akauliza.
“Siku saba zinatosha kufanya maandalizi? Maana mkumbuke kupanga mashambulizi si kitu kidogo!” Amanda akasema.
“Huu ni mchezo wa hatari sana, kwa nini wamemwita Bakhari? Siyo mtego huu?” Martin akawauliza wenzake, “isije kuwa wanataka kummaliza ili kelele hii iishe,” akaongeza kusema.
“Hapa kuna utata, tunaweza kwenda tukatiwa mbaroni kirahisi sana,” Fredy akasema.
“Acha uoga Fredy, tuitumie nafasi hii, inaweza ndo ikawa bahati pekee kwetu, na ninafikiri, safari hii sintotumia bunduki kuua…”
“Utatumia nini?” Amanda akauliza.
“Siwezi kukwambia ila utajua mtu atakapokufa,” Martin Gupter akawaambia swahiba zake.
“Hapo ndipo ninapokupendea, hupendi kuweka wazi mipango yako…” Amanda akamwambia Gupter.
“Nilizoea kutumia bunduki moja tu, na nimeishi nayo miaka kama ishirini hivi, ilikuwa kama mwanangu, na imenifanyia kazi nyingi sana, sasa mshenzi yule akafanikiwa kuitoa mikononi mwangu… nina kazi ngumu ya kupata nyingine kama ile, kwa sasa nitamaliza kazi zangu kwa mikono na sumu tu basi,” Martin akasema.
Martin Gupter katika kazi yake yote ya mauaji aliizoea sana bunduki hii ‘Magnum 22 riffle’, haikuwa maalumu ya kudungulia ila yeye alipenda kuitumia kwani aliiamini kuwa ina nguvu za kutosha katika kummaliza adui yake. Haikuwahi kutoka mikononi mwake kwa takribani miaka ishirini lakini sasa ni Kamanda Amata aliyeharibu utaratibu huo na kufanikiwa kuipata bunduki hiyo kisha kuihifadhi Shamba. Japokuwa ilikuwa ni pigo kwake, bado Gupter aikuwa mtaalamu sana katika maswala ya uuaji, aliweza kuua kwa mitindo mbalimbali na kwa ustadi wa hali ya juu sana na ndiyo maana alikodiwa na watu mbalimbali waliotaka kutekelezewa kazi kama hizo.
Martin Gupter alikuwa kwenye orodha ya watu hatari, akioneshwa na CIA kwa sura kama hamsini tafauti, akinaswa kwa sauti nyingi tafauti, MOSSAD walimwelezea kama Shetani mwenye bunduki ya kizamani, kila shirika la kijasusi ambalo ndani ya nchi yao kijana huyu keshafanya maangamizi walimpachika jina wanaloona linamfaa. Aliamini kuwa kwa kuweza kuzitoroka ngome ngumu kama hizo za kijasusi za Ulaya na Mashariki ya mbali asingeweza kutikiswa na Afrika, alijua atachukua kazi na atamaliza kwa wakati bila hata kipingamizi. Kila anapokwenda alikuwa na timu yake anayoiamini sana, Amanda na Fredy, wao nao kama makachero watoro kwenye nchi zao walimsaidia vyema sana Martini kuweza kufanikisha mauaji yake katika ngome yoyote ile duniani.
Haikuwa mara ya kwanza kwa Jaffery kumpa kijana huyu kazi, alimwamini na ndiyo maana hata safari hii, kwenye kazi ya kuipigania nchi yake alimtafuta na kumfanya kama kifaa cha kuushinikiza Umoja wa nchi za Afrika kuigawa Somalia vipande viwili ili Kusini kutawaliwe na tajiri huyu kwa madai kuwa ni ardhi ya mama zake.
“Tunaingia kazini! Ngoja niwasiliane na tajiri, ila jiwekeni tayari,” Martin akawaambia swahiba zake huku akiiendea simu ya mezani na kupiga namba fulani, akaweka sikioni kifaa kile na kusikiliza upande wa pili. Baada ya mazungumzo kama ya dakika kumi na moja hivi akakata simu na kurudi kwa wenzake.
“Jaffery anasema tutumie nafasi hiyo kama loope hole ya kuwamaliza, ila sharti lake ni lile lile, asipokuwepo yeye basi atamtuma binamu yake kwenda kwenye kikao hicho na kuwa msemaji badala yake. Wakikubali matakwa yake basi tuweke silaha chini, wakikataa tutekeleze mbinu ya mwisho na tayari jeshi litaivamia Somalia na kuendesha vita isiyo na mwisho…” Martin akaeleza.
“Sasa nimepata mbinu, tunachotakiwa kufanya ni kuwa pale lakini kuwa wapole sana, hata kikao kikiisha sisi tusifanye lolote ili Martin utekeleze kazi yako kimyakimya nasi tutakulinda,” Fredy akaongeza.
“Ndiyo, na huo ndo ujanja sasa ambao nataka tuutumie. Unajua wataimarisha ulinzi, wakijua tupo, sasa sisi hatutumii nguvu sana kama mwanzoni, mlengwa wetu ataamka akiwa marehemu basi!” Martin akawaeleza.
“Kwa hiyo!” Amanda akatamka.
“Tuingie kazini, siku saba kabla, yaani ikiwezekana kesho Amanda utangulie au mjipange wenyewe,” akawaambia.
 
keshokutwa ifike tu mda huu vinginevyo ni mateso makubwa kwa tunaoikosa riwaya hii....!!!
 
MAGNUM22

Sehemu 17


SEHEMU FULANI HUKO SOMALIA
KIKOSI cha vijana kama elfu moja waliovalia nguo za kijeshi na kujifunga vitambaa vichwani mwao na wengine wakiwa wamevaa soksi usoni, kila mmoja alikuwa na bunduki kubwa ya kisasa yenye nguvu mkononi mwake, walikuwa wamesimama kimya katika vikosi vya watu mia moja mia moja huku kila kikosi kikiwa na bendera nyeusi. Licha ya kuwa na silaha hizo nzito, kila mmoja alikuwa na sime kiunoni mwake.
“TUNAUTAKA UMOJA WA NCHI ZA AFRIKA KUIGAWA JAMHURI YA SOMALIA NA KUWA NCHI MBILI HURU!” alisikika mtu mmoja aliyekuwa amesimama mbele yao juu ya kijukwaa kidogo, akiwa na kipaaza sauti mkononi mwake.
“MAZUNGUMZO YA MWISHO YATAFANYIKA WIKI MOJA IJAYO, HIVYO WAKIKUBALI, ARDHI HII TULIYOSIMAMA ITAKUWA NCHI YETU, WAKIKATAA TUTAANZISHA VITA ISIYO NA MWISHO!” akawaambia na wao kwa kutii agizo hilo, wakainua bunduiki zao na kupiga risasi juu mara tatu.
Baada ya taarifa hiyo wanajeshi hawa wakatawanyika na kuingia katika maficho yao ya kila siku. Fadicky Al – Habib aliteremka kwenye kile kijukwaa na kuvuta hatua huku akifuatwa na vijana wengine wanne ambao nao walivalia kijeshi kama wale wanajeshi.
“Unafikiri watakubaliana na matakwa yetu?” mmoja wa wale vijana akamuuliza.
“Wasipokubali ndipo watakuwa wamefungulia bomba la damu katika ardhi hii,” akasimama na kumwambia yule kijana, “Jaffer anahitaji kitu kimoja tu, ardhi ya mama zetu, hivyo wasipoitoa kidiplomasia wataitoa kwa mtutu wa bunduki,” kisha akaendelea kutembea na kuingia ndani ya hema ndogo yenye ulinzi mkali kwa nje. Wakaketi katika zuria kubwa na la kisasa, wanadada wawili warembo wakapiga magoti huku na huku wakimkandakanda mabega.
“Yusra, jiandae, weka watu wako vizuri, siku isiyojulikana tutaondoka hapa kuelekea Addis!” akamwambia yule kijana.
* * *
DAR ES SALAAM
OFISI YA MUDA YA BARAZA LA USALAMA LA A.U
Kikao cha wajumbe wale wale kilikutana tena katika afisi hii iliyoteuliwa kuhifadhi nyaraka zote za kiusalama kwa kipindi hiki. Usiku huu kama walivyoitwa na Mwenyekiti wa baraza hilo walifika na akidi ilitimia. Madam S alikuwa ameketi katika kiti chake kile kile na wajumbe wengine nao vivyo hivyo.
“Kama tulivyoelekezana kuwa kwa kazi hii tutaitana muda wowte hata kama ni usiku wa manane kama leo hii … nimekuitena kwa sababu kuna jambo ambalo limejitokeza na lazima lifanyiwe kazi. Kikao cha dharula cha wadau wa AU baada ya kukutana jana pale Addis, kimeamua kwamba ufanyike mkutano wa mazungumzo kati ya AU na huyu Bwana Jaffery Bakhary ili kufikisha mwisho mgogoro huu…” akalieleza jopo hilo ambalo lilikuwa kimya kabisa likifuatilia nini mkuu huyo anataka kusema.
“Hivyo basi siku saba zijazo kutafanyika kikao hicho ndani ya ukumbi mdogo wa mikutano katika jingo letu la AU Headquaters. Dhumuni la kikao hiki sasa ni kwamba sisi kama baraza la usalama la jumuia hii tunatakiwa tuandae ullinzi wa kutosha kuwalinda viongozi wetu siku hiyo. Sasa nakaribisha mawazo yenu ni jinsi gani tutaweka ulinzi eneo hilo,” akamaliza na kuzima kifaa chake cha kuzungumzia.
“Tupo kwenye harakati za kuwasaka hawa jamaa wanaofanya mauaji ya viongozi … sasa na tena tunaandaa kikao cha viongozi hao hao, Mwenyekiti huoni kama tunaweza kuwa tunarahisisha kazi kwa wauaji kutekeleza mpango wao?” mjumbe mmoja akauliza.
“Lakini je, huoni kuwa inawezekana kuwapata wauaji kirahisi kama watakuja mahalia hapo, na najua kwa vyovyote watakuja kwa sababu ni wafuasi wa mtu huyu, nsiyo maana nataka tujadiliane jinsi ya kuweka ulinzi huu na kuhakikisha tunamtazama kila mtu,” yule mwenyekiti akasema. Ukimya ukajidai kwa nukta chache kisha mjumbe mwingine akakohoa.
“Kwa hiyo tunafanyaje? Vijana tuliowasambaza tunawarudisha na kuwapeleka Addis au tunaunda kikosi kazi kingine?” mwingine akauliza.
“Ndiyo nataka tuone pamoja kama tunawapa kazi hawahawa au hawa tuwaache na misheni yao kule waende wengine…. Tuweke mawazo pamoja!” mwenyekiti akaeleza.
“Mjue mnapambana na nani!” Madam S akawaambia, “wale au yule kama ni wauaji au muuaji mwenye profesheno yake katika kazi msifikiroi atajileta kirahisi hivyo au atatumia mbinu ile ile. Tazameni alivyoua Angola sivyo alivyoua Ivory Coast … alipojaribu kutumia mbinu ileile hapa Tanzania tukampa ambush ya nguvu hata silaha yake akaicha hapa, sasa unafikiri kama atakuja Addis atatumia mbinu hiyo hiyo?” akawaacha kwa swali.
“Sure! Anachosema Madam pale ni sahihi kabisa, inabidi tutanuke na tunuse katika kila kitu ikiwezekana tupenyeshe watu wetu kwenye kona zote muhimu, ili waangalie kila kitu kwa ukaribi zaidi…” mjumbe mwingine akasema.
Kikao kikaendelea na mipango mingi ikasukwa kwa ajili ya siku hiyo, wakatakiwa kukusanya wana intelijensia kutoka sehemu tafauti za Afrika ili kuwapenyeza kwa siri katika Jiji hilo kuweka usalama. Lakini katika uteuzi wote huo haikuguswa idara nyeti ya TSA, kwa kuwa ilisemwa kuwa Tanzania imeshindwa kuongoza operesheni hiyo tangu awali, hata Madam S alipotaka kutetea hilo hakusikilizwa,”
“Kwa kuwa hawa washenzi walitaka kutekeleza mauaji ndani ya nchi hii, vijana wangu wataendelea kuwasaka popote walipo katika dunia hii bila kujihusisha na kikosi cha AU…” Madam S akazungumza kwa hasira.
“Sasa mjumbe kutoka Tanzania, kumbuka kijana wako unayemtegemea sana mpaka sasa hajulikani alipo, utampelekea nani tena huko, hili swala liache, tutalifanyia kazi kama kamati…” mwenyekiti akasema.
“Sina kijana mmoja, ninao zaidi ya mia tano wazuri kuliko yule. Ninachotaka nikwambie ni kwamba, siridhiki na mwenendo wa kamati hii, kuna ulakini hapa, leo sintosema lakini nitakuja kuwaambia bado nafanya uchunguzi wangu… si ajabu kuna watu au mtu anajua kila kinachoendelea lakini anajifanya msafi…” Madam akazungumza huku tayari anataka kuondoka.
“Mjumbe, naomba utangue kauli yako… ina maana humu ndani kuna msaliti, unamaanisha hivyo? Yaani sisi wenyewe ndiyo tufanya mauaji ya viongozi wetu?” akaongea kwa ukalia.
“Mi sijasema hivyo, ila hayo umesema wewe…”
“Wewe lazima ushughulikiwe, we mwanamke wewe lazima ushughulikiwe na kamati ya nidhamu,” Mwenyekiti akaongea huku kijasho kikiwa kinamtoka, akaketi na kushuhudia mwanamke huyo akiishia nje ya jengo.
“Aaaaaaggghhhh!!!! Ameniuzi kabisa bullshit!” akang’aka na kuinuka kitini, akaingia katika mlango mwingine na kujifungia maliwato kwa dakika kadhaa, kisha akarudi kuungana na wengine na kikao kikaendelea.
* * *
USIKU HUO HUO
Katika makutano ya Barabara ya Morogoro na Bibi Titi, Madam S alikuwa akikatisha usiku huo kuelekea ofisi ndogo. Mara kutoka barabara ya upande wa pili alisikia sauti kali ya gari, akageuka na kuona Land Rover nyeusi ikiwa mita mbili kutoka kwake, kabla hajafanya lolote, kishindo kikubwa kikasikika. Lile Land Rover likaipamia gari la Madam S na kulisukumia pembeni, likatupwa na kubingirita upande mwingine, lile Land Rover likakaa barabarani vizuri na kuendelea na safari kwa kasi kuelekea upande wa Mahakama ya Kisutu.
Usiku huo kulikuwa na watu wachache sana barabarani, hawakuzidi hata kumi, wakawahi kufika katika lile gari na kushuhudia uharibifu mbaya. Madam S alikuwa amebanwa na mkanda wa kiti alichokaa, hakuweza kutoka, damu zilikuwa zikimwagika kichwani. Kazi kubwa ilikuwa ni kumnasua mama huyo ili angalau wamweke pembeni apate upepo. Vibaka nao hawakuwa mbali aliyechukua simu akafanya hivyo aliyenyofoa redio haya.
Dakika kama thelathini baadae, gari la polisi likawasili eneo hilo, itifaki za kusalama zikaendelea na kumkimbiza mwanamama huyo Muhimbili, mpanga dakika hiyo hakuna mtu aliyemgundua majeruhi huyo.
Na huko Shamba TSA members walikuwa wakiendelea na shughuili zao, kila mmoja akiwa katika jukumu lake analopaswa kufanya. Simu ya mezani ikaanza kuita kwa fujo, haikuwa mbali sana na pale ambapo Chiba alikuwa ameketi.
Nani anayepiga hii simu? Akajiuliza huku akisukuma kiti chake kidogo ili kuifikia. Kila mmoja alishangaa kwa mwito huo maana simu hiyo inaweza ikakaa hata miezi miwili isitumike nah ii ni kwa sababu ni ya siri sana, njia zake zimefungwa kitaalamu kiasi kwamba haziingiliani na simu za kawaida. Ikiita ama inatokea Ikulu, Makao makuu ya Usalama wa Taifa na watu wachache wenye namba hiyo wasiozidi wane Tanzania nzima. Wote wakaikaribia wakati Chiba akiinyakuwa na kuiweka sikioni huku tayari kitufe cha kurekodi kikiwa kinafanya kazi.
“… umesema? … nheee…. Usiku huu au?” Chiba alionekana kuhamanika kwa simu aliyokuwa ameipokea. Baada ya hapo akakata na kuiweka mahala pake, akageuka na kukutana na macho nane yakimtazama.
“Vipi?” Amata akwa wa kwnza kuuliza.
Chiba hakujibu zaidi ya kuwatazama tu.
“Chiba nini?” Gina akadakia kuuliza.
“Madam S amepata ajali usiku huu kama saa moja au dakika arobaini na tatno zilizopita,” Chiba akawaeleza.
“What?”
Amata akang’aka na kuwaacha wenzake, dakika chache baadae akarudi akiwa keshavaa koti lake, “Simu imepigwa na nani?” akauliza.
“Inspekta Simbeye!”
“Smbeye?” akauliza na kuchukua simu yake, akapiga namba za inspekta huyo na kuzungumza naye machache kisha akaitua na kuitia mfukoni.
“Ok! Dkt. Jasmine, Scoba na Chiba nendeni Muhimbili haraka sana mkaweke mambo sawa, Mimi na Gina tunaenda eneo la tukio. Dakika ya tisini tuwasiliane,” Amata aatoa maagizo na kila mmoja akatawanyika tayari kwa kazi aliyopewa.

ENEO LA TUKIO
Gina aliegesha gari kando kando ya wigo wa Chuo Cha Ufundi Dar es salaam (Dar Tech) na wote wakateremka na kuelekea eneo hilo ambalo lilizungukwa na askari wa usalama barabarani na wale wa kawaida ambao walikuwa na silaha mikononi mwao. Amata na Gina wakawasabahi askari hao na kusogea pale lilipokuwa gari lile. Askari wenye silaha wakawazuia kwa kuwa tayari breakdown lilikuwa kwenye mchakato wa kuinua na kuivuta mpaka kituo cha polisi. Mazungumzo ya sekunde chache yakafanyika na Amata akaruhusiwa kusogea eneo lile, moja kwa moja akazunguka upande wa mlango wa dereva na kupenyeza mkono kwa upande wa chini, alipoutoa alikuwa na vitu viwili mkononi mwake; bastola ndogo ambayo haraka aliipachika kiunoni na kitu kingine kama pakiti la sigara lakini hiki kilikuwa cheusi, akakitia mfukoni na kutoka eneo hilo. Kando akakutana na askari mmoja mwenye sare nyeupe aliyekuwa na faili mkononi mwake na kuonekana akiandikaandika vitu fulani.
“Mmefanikiwa kuona gari lililosababisha ajali?” akamuuliza.
“Hapana! Inaonekana hawakusimama, kwani sisi tumefika kwa kuchelewa kidogo,” akajibu. Amata akatulia kidogo.
“Una undugu na huyu mama?” yule askari akamuuliza.
“Ndiyo, ni mama yangu…”
“Oh pole sana, wahi Muhimbili, hali yake sijui kama atapona,” sentesnsi hii ya mwisho iliufanya moyo wa Amata kupaa kwa hofu, haraka akarudi garini na kuketi kitini, akashusha pumzi ndefu.
“Vipi?” Gina akamtupia swali.
“Hali ya mama ni mbaya,” akajibu huku akichukua simu yake na kabla hajabofya namba yoyote ikaita, akaichukua na uiweka sikioni.
“Chiba!” akaita.
“Mama yupo mahututi,” Chiba akamwambia Amata.
“Nipo njiani kaka!”
Gina akawasha gari na safari ya Muhimbili ikachukua nafasi, “Ni ajalia au?” Gina akauliza.
“Siwezi kujua kwa sasa, lakini nitachekecha vizuri akili tutajua tu, hata gari iliyofanaya ajali itapatikana tu,” Amata akajibu wakati gari likiiacha Barabara ya Umoja wa Mataifa na kuchukua Mtaa wa Mindu kuelekea katika hospitali hiyo.
Hatua za harakaharaka zikawafikisha katika jengo la wagonjwa mahututi, wakaingia kadiri ya utaratibu wa wodi hiyo. Ndani ya chumba cha pekee Madam S alikuwa amelala kimya huku mashine ya oksijeni ikiwa puani mwake na ile ya kufuatilia mwenendo wa moyo nayo ilikuwa ikionesha mapigo hafifu. Daktari Jasmini alikuwa hima hima na madaktari wengine wakijaribu kufuatilia kila kinachoendelea kwa mgonjwa wao.
“Tunafanyaje?” Chiba akamuuliza Amata wakati tayari wakiwa nje ya jingo hilo, saa ya mkononi mwa Amata ilionesha saa nane usiku.
“Tutulie tu na tufuatilie kila kitu kwa ukaribu, ila kwa sasa tuzuie kila baya kama lipo, tutafanya hivi; Gina tunakuacha hapa na Scoba, muangalie usalama wa Mama kama mnahisi au mnamhisi yeyote kutaka kufanya baya, hakikisheni mnashughulikia. Madam S asiguswe na mtu yeyote kitandani iwe kuchomwa sindano au kufanyiwa tiba yoyote zaidi ya Dkt Jasmine, muwe macho. Mimi na Chiba kuna mambo tunayaweka sawa kisha tutawasiliana…” akatoa maagizo.
“Sawa, umesomeka mkuu…” Gina akajibu.
Chiba na Amata wakaingia garini na kutokomea zao. Breki ya kwanza ilikuwa katika kituo polisi kati, hapo wakakutana na Inspekta Simbeye ndani ya afisi yake chakavu ambayo hata haina mpangilio vizuri.
Mzee huyo aliyebwaga moyo wake kitini huku miguu yake mifupi ikiwa juu ya meza, aliwakaribisha wageni wake na kisha akaketi vizuri kwa mazungumzo.
“Tumekuvamia!” Amata akamwambia.
“Na nilijua mtakuja,” Simbeye akawajibu, “kwanza poleni sana kwa yaliyotokea…”
“Asante sana, tunasikitika sana na tunamhitaji huyo aliyefanya hivi, kwa akili yangu mbaya najua wazi kuwa si ajali ya kawaida,” Amata akamwambia Simbeye.
“Ndiyo, upo sawa, Kamanda … mnazungukwa! Naanza kung’amua kitu…” Simbeye akasema.
“Utu uzima dawa, nambie baba labda utaifungua akili yangu iliyolala,” Amata akamwambia simbeye huku akijiweka sawa kitini. Inspekta Simbeye, hakuzungumza kitu, akachukua simu yake na kumpatia Amata, naye akatupia jicho juu ya kioo na kuusoma ujumbe uliyoandikwa.
‘Usiku huu nitafanya msilolitegemea, free Somali Land’
Baada ya kuusoma ujumbe huo akatazama saa ngapi ulitumwa, akagundua kuwa haikupita hata saa tatu ni saa mbili na dakika kadhaa. Tofauti kati ya muda wa ajali na muda was ms ile ni dakika kama ishirini na nne hivi.
“Nini hiki?” akauliza huku akimpa Chiba simu ile.
“Utashangaa kwa kuwa hujui hili, huu si ujumbe wa kwanza ni wa tatu sasa, na namba ndiyo hii, ‘unknown’, Chiba pale anajua na imemtesa sana kuifuatilia,” Simbeye akasema. Amata akamtazama Chiba kana kwamba anamuuliza, ‘ni kweli?’
Namba zake zimefungwa kwa code ngumu sana, nimejaribu mara kadhaa lakini nimeshindwa kumpata mtumaji…”
“Na umeamua kuacha?” Amata akauliza.
“Si kuacha ninamsaka bado, nitamtia nguvuni tu, na asije kujaribu siku akapiga simu ndiyo utakuwa mwisho wake,” Chiba akazungumza kwa uchungu.
“Simbeye, mimi naweza kuichukua ajali hii kama hujuma katika sakati ambalo tunadili nalo kwa sasa, kwa mbali ninaanza kuona nini kinajiri, nakuhakikishi, huyu mpumbavu nitamleta hapa umle nyama,” akasema na tayari akawa wima kwa safari.
“Unaenda wapi?” Simbeye akamuuliza.
“Nataka niwe karibu na Madam S, ili akiamka tu anambie nini kimemsibu,” akajibu.
“Good! Hata mimi nipo kwenye kumtafuta juha huyu, nikipata fununu nitakwambieni, ila kwa sasa tuondokeni wote kwenda Muhimbili,” akawaambia kisha wote watatu wakatoka na kuingia garini. Safari ya kuelekea Muhimbili ikaanza, wakapita barabara ya Bibi Titi ili makusudi kufika eneo la tukio, wakati huu kulikuwa kimya hakuna mtu.
“Walizamilia kumuua,” Chiba akasema.
“Na hawatampata!” Chiba akajibu huku tayari wakiingia katika uwanja wa hospitali hiyo, haraka haraka wakateremka na kuliende jengo la wagonjwa mahututi. Wakiwa hatua chache kabla ya kulifikia lango kuu wakakutana na watu kama wane hivi waliokuwa wakizungumza kwa lugha ya Kifaransa, Amata akasimama na kuwatazama, kisha akamtazama Chiba.
“Vipi unawajua?” akamuuliza.
“Hapana, isipokuwa mmoja wao kama nimewahi kukutana naye vile,”
“Wapi?”
“Sikumbuki, ila nimewahi kukutana naye,” akajibu kisha wakaingia ndani na kumkuta Scoba na Gina wakiwa katika ulinzi madhubuti. Gina akaamka mara moja na kumuendea Amata.
“Vipi Kamanda… tetesi yoyote?”
“Hakuna kitu, mbingu bado nyeusi!”Amata akajibu huku akimshika mkono na kumvutia pembeni, kisha kwa sauti ndogo ya kuwatosha wao akamnong’oneza.
“Kuna watu wamekuja hapa kumwona mama?”
“Ndiyo wamekuja, lakini tumewakatalia kuingia, kwani hamjapishana na watu fulani hapo nje?”
“Ndiyo maana nimekuuliza…” Amata akamwambia. Wakati wao wakijifanya kuongea peke yao kumbe Inspekta Simbeye amewasiki vyema kabisa, na Amata alipachana na Gina na kurudi kuungana na wengine, Simbeye akamwambia.
“Ina maana we wale huwajui?”
“Hapana, ila mmoja nimeshawahi kukutana sehemu…”
“Wajumbe wa Baraza la Usalama la AU ambao wameweka kambi hapa Dar kwa ajili ya kuendesha oparesheni ile ya kumsaka muuaji shetani,” akamwambia.
Muda huo huo, Dkt. Jasmin akaungana nao, haraka, Simbeye na Amata wakamdaka juu kwa juu na kumvutia pembeni kwa mazungumzo.
“Vipi, mmegundua nini huko?” Amata akawa wa kwanza.
“Madam hajaumia yaani kupata majeraha, ila inaonekana amejipiga kichwani ndo maana amepoteza fahamu..”
“Ndani ya kichwa hakuna tatizo kubwa?” Simbeye akauliza.
“Hapana, hajapata tatizo lolote baya, na ataamka tu, tunaamini atakuwa na kumbukumbu zake sahihi kabisa,” Jasmine akawajibu na kila mtu moyo wake ukatua.
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom