MAGNUM22 22
Sehemu 11
akainuka na kuuendea mlango mmoja wapo huku nyuma akifuatwa na Amata, wakaingia mahali pengine tofauti na ile ofisi ya kwanza. Huku kulikuwa na watu wachache wake kwa waume waliokuwa kwenye mazungumzo, tunaweza ita ya falagha kwa maana usingeweza kusikia wanachoongea ila ungewaona wanaongea. Mlango mwingine ukawafikisha nje kabisa kwenye bustani nzuri na ya kupendeza, yenye maua aina aina na vitu vizuri vya kuvutia.
“Sikiliza,” Perreira akamwambia Amata na nukta hiyo hiyo mwanadada mmoja aliyevalia bikini akafika mahala pale akiwa na kitunga mkononi mwake, hakuwa Mhindi wala Mwarabu ila alikuwa na nywele ndefu mpaka makalioni, akafungua kile kitunga na Perreira akachukua sigara moja kubwa na kuiwasha kisha akaipachika kinywani na kuibana kwa midomo yake miwili. Baada ya kupiga pafu tatu kubwa na kuutoa moshi hewani akamtazama Amata kwa mara nyingine.
“Mimi ni mtu mwema sana, huwa nasaidia serikali nyingi kwa mambo mengi, nasaidia makundi mengi ya huduma za kibinadamu kwa mambo mengi, ila kwa hilo ulilotumwa, Mr. Spark nina wasiwasi sana… Mimi sina mpango wa mauaji, ila nina taarifa ya mauaji, lakini sikai nayo hapa taarifa nyeti kama hiyo. Tazama kuleeeeee, unaona kile kisiwa?” akamwambia. Amata akatazama na kukiona vyema kabisa.
“Pale panaitwa Ilha da Canzaga, itakupasa uende utamkuta mtu mmoja anaitwa Oliviera, mwambie nimekutuma akupe hiyo kitu, na ukiishaipata kwa sababu wengi wanaitafuta, utatakiwa ufanye juu chini uondoke katika jiji hili kabla hujang’anywa. Maana kuna watu wengi wako hapa Luanda wanataka kitu hicho hicho,” Perreira akamwambia. Na mara ukasikika mlio wa boti, ikasimama mbele kidogo baharini, na opareta wa chombo hicho alikuwa ni yule mwanamke aliyeleta sigara kwa Perreira.
“Tutaonana baadae, all the best!” Fernandes akamuaga Amata. Kamanda alipotaka kumpa mkono, yeye akachukua sigara yake nakuendelea kuvuta huku akigeuza kurudi ndani ya jumba lile.
Amata akatembea harakaharaka na kuingia ndani ya boti lile na safari ikaanza. Kamanda alijiegemeza katika kiti cha nyuma huku mwanamke yule akiwa kwenye usukani mbele yake akiedesha chombo hicho kwa kasi huku amesimama na kumfanya kijana huyu kusisimkwa mwili kila alipomtazama. Kiu kilimshika, akasimama na kumwendea pasi nay eye kujua, akafika nyumayake na kumkamata kiuno.
“What!!!” yule mwanamke akapiga ukelele mara baada ya kuhisi kuwa ameshikwa bila ridhaa yake.
“Mh mhhhhh, endelea na kazi, u mrembo sana bibie!” Amata akamwambia huku kidevu chake akiwa kakiegesha begani kwa mwanamke huyo.
“Kaa kitini tafadhali,” akasema yule mwanamke.
“Nitakaaje wakati wewe umesimama?” akamuuliza.
“Kwa hiyo?”
“Tukae wote,” akamwambia huku akimbusu nyuma ya shingo. Yule mwanadada akajikuta kwenye wakati mgumu sana.
KISIWA CHA ILHA DA CANZAGA
Kijana mmoja akaondoa jicho katika lensi kubwa ya bunduki ndani ya jengo moja la ghorofa mbili katika kisiwa hicho.
“Vipi?” mwingine akauliza.
“Huyu jamaa inaonekana anajua nini kinampata!”
“Kwa nini?”
“Si amemkumbatia Alegria, sasa nakosa shabahsa sahihi,” yule kijana akamwambia mwenzake, naye akaja na kuweka jicho kuangalia.
“Mh!” akaguna.
“Vipi?”
“Mwache afike, tutafanya kazi hiyo hapa hapa,” akasema.
Wale jamaa wakaendelea kuiangalia ile boti ikizidi kuja katika jumba hilo.
Katika boti lile, Amata bado alikuwa nyuma ya Alegria, akimpapasa kimahaba sehemu za kiunoni na juu kidogo ambapo panatengeneza umbo halisi la mwanamke.
“Sipendi kushikwa namna hiyo tafadhali,” Alegria akamwambia Amata huku mikono yake bado ikikamata usukani mdogo wa chombo hicho.
“Katika jingo hilo ndipo tunakwenda?” akamuuliza.
“Ndiyo!” mwanake yule akajibu. Amata akamwacha mwanamke huyo na kuketi tena kitini, akachukua miwani yake maalumu na kuivaa. Miwani hii ilikuwa na uwezo mkubwa wa kukuza vitu vilivyo kilomita moja kwa umbali na kumfanya mvaaji avitambue kwa urahisi. Alipohakikisha imemkaa vyema, akazungusha vijinobu viwili vilivyo upande huu na mwingine. Kamanda Amata macho yake yakagongana na mtu anyeshusha darubini na pembeni yake kuna bunduki kubwa ya kudungulia. Tayari walikuwa kama mita mia mbili hivi kufika katika ghorofa hilo, Akili ya Amata ikafanya kazi haraka na kuamua kwa kasi ya ajabu, akainuka kutoka kwenye kiti na kukanyaga batani ya mwendokasi na kuifanya ile boti iongeze kasi kwa ghafla kiasi kwamba Alegria alishindwa kuiongoza na kumuangukia Amata. Kijana huyo akamdaka na kumkumbatia huku mguu wake bado ukiwa kwenye ile batani.
“Unafanya nini wewe?” yule mwanamke akapiga kelele na kumpiga kipepsi Amata. Maumivu aliyoyasikia hayakuwa ya kawaida katika moja ya mbavu zake.
“Tuliaaa mwanamke!” Amata akamwambia na kumtupia upande wa pili, mwanamke yule akajiinua na kumtandika pigo moja matata, Amata akaona asiwe mjinga kwa tayari aliijua azma ya wenyeji wake, akatoa mguu kwenye ile batani na kumpiga ngwala Alegria, akaanguka vibaya na kujikuta akitumbukia baharini. Kamanda akarudisha mguu kwenye batani na injini ya boti ikavuma na kunyanyua chombo hicho mara baada ya kugusa mchanga. Boti ile ilipaa na kutua kwenye dirisha moja la kioo, ikaingia nusu na kuning’inia. Amata akaruka haraka nje na kutua sakafuni, mara risasi chache zikapiga sentimita chache kutoka pale alipokuwa ameangukia, lakini tayari alikwishabingirita na kuhama eneo kusudiwa. Alipotulia tayari bastola ilikuwa mkononi na alipofyatua shabaha yake haikupotea bure. Mtu mmoja akaanguka kama mzigo, na Amata akamuwahi na kummalizia kwa guu moja zito la shingo.
“To the ground floor!!!!” sauti kutoka ghorofa ya juu ikasikika, Amata akajiweka tayari, bastola mkononi, akajibana sehemu akisubiri kuona hao wanaoamriwa kuja upande wake. Punde tu akamwona kijana mmoja akiteremka kupiti ngazi ya mzunguko inayounganisha ghorofa ya juu na ile ya chini. Kamanda Amata akajua mara hii ameingia kwenye domo la mamba, akainua bastola yake na kufyatua risasi moja, shabaha maridhawa. Kijana yule akapiga yowe moja na kuanguka vibaya sakafuni. Amata akahama kutoka pale na kwenda upande mwingine kulikokuwa na maboksi makubwa ambayo hata hakujua nini kipo ndani yake, akatulia kimya kabisa.
Oliviera, kijana mshupavu wa mwili anayeaminiwa na mkuu wake Pereira, aliteremka taratibu huku mkononi mwake akiwa Shot Gun matata sana. Akaangaza angaza macho yake huku na kule akitembea hapa na pale kwa hadhari kubwa, fulana aliyoubana mwili wake ilionesha jinsi gani alikuwa ‘baunsa’. Kamanda Amata akaendelea kusubiri ili kijana huyo afike kwenye ‘kumi na nane’ zake.
Simpigi kwa risasi! Akasema moyoni huku akijiandaa kumpa shambulizi la dharula. Oliviera, akatazama na kutazama, hakuna mtu! Akaiweka sawa bunduki yake na kupiga ‘burst’, risasi mfululizo zikamwagika na kumua maboksi yale, kisha ukimya ukatawala.
“Vieira! Vieira!” sauti ya mwanamke ikaita kutoka nje.
“Alegria, ingia ndani, mshenzi huyu ametufanya vibaya…” Olivieira akamwambia mwanamke huyo.
“Amejificha humu ndani au amekimbilia wapi, sijui….”
“Shiiiit! Kamuua Joao!” Alegria akiwa na vazi lile lile la bikini, akamwendea marehemu pale chini na kumtikisa tikisa.
“Keshakufa,” Olivieira akasema.
“Kwa nini hamkumuua tangu tunakuja kama kawaida?” Alegria akamuuliza Olivieira.
“Huyu mshenzi ni mjanja, alijificha nyuma yako…”
“Hakikisha tunaitoa roho yake, maana kama akipata anachotaka ataharibu mambo!” mwanamke huyo akasema huku akichukua Shot Gun ya yule marehemu na kuikamata vyema. Muda wote huo, kamanda Amata alikuwa akiwatazama kutoka nyuma ya maboksi, pale alipo ni risasi kadhaa zilimpita karibu sana, kilichomuokoa ni kuwahi kulala chini. Kwa wakati huu alikuwa akisikiliza mazungumzo yote ya wawili hao, akajua kuwa marehemu anaitwa Joao, na pia kuwa anachokitaka kipo hapa.
Kumbe! Akawaza na kujiweka tayari kutoa shambulizi la dharula.
Hapa lazima mmoja afe na mwingine apate kipigo kitakachomlazimu kunipa kila kitu, shenzi sana! Akajisemea moyoni kisha akaanza kuchagua nani afe na nani abaki. Akimtaza Alegria, jinsi alivyoumbika hakutamani kabisa kumuua, lakini akajiuliza kama akibaki hai je aianajua kila kitu kilipo? Hakuoma haja ya kujiuliza hilo. Akaigiza mkono mfukoni na kutoa goroli tatu, akazirusha mja upande huu nyingine ule na nyingine katikati kwaribu kabisa na miguu yao, kisha yeye akahama haraka na kuelekea upande mwingine.
“Aaaaaaaaaaaaaiaiiiiiiiiiihhhhhhgggggghhhhh!!!!!” Oliviera akapiga kelele huku akimiminia risasi upande ule kwa minajiri ya kuua tu. Mwanamke yule naye akaungana naye kwa kufyatua risasi vilevile. Baada ya kama sekunde ishirini hivi, Olivieira akanyosha mkono na risasi zikakoma, kilichobaki ni harufu ya baruti tu. Oliviera akampa ishara ya mkono Alegria akimtaka kupita upande wa pili huku yeye akipita upande huu waibukie nyuma ya mabaoksi hayo. Kamanda Amata akajua wakitawanyika tu pale waliposimama itakuwa ngumu kuwashambulia. Akatumia nguvu zake zote na kuruka kutoka juu ya maboksi yale huku miguu yake ikimchangua mmoja baada ya mwingine. Oliviera alishtuliwa na kishindo cha Amata kuanda maboksi akatazama juu na kujikuta akikanyagwa na guu la uso, akayumba na kwenda kando wakati Alegria akienda chini na bunduki kumtoka mikononi.
Mara alipotua chini, Oliviera tayari alikwishajiweka imara, akamshushia konde moja zito, Amata akayumba kwa nyuma na kujikwaa kwenye mwili wa Joao na kuajikuta akitaka kuanguka kinyumenyume lakini akajiwahi. Oliviera alikuwa akimfuata Amata kwa kasi lakini alipomfikia tayari alijikuta kapoteza, kwani pigo moja la pili la tatu, yote ya karate yakamwacha hana hali. Jamaa huyo akainua pipa lililo karibu na kulirusha kwa nguvu, Amata akaruka sarakasi na kuliacha likipita chini. Alegria alijiokota kutoka pale chini kuokota ile bunduki, hata hakufanikiwa kuishika kwani alijikuta akiangukiwa na mtu juu yake.
“Tulia! Kahaba wewe!” Amata akaunguruma huku bastola ikiwa mkononi tayari ilikwshammaliza Oliviera.
“Nipe ninachohitaji haraka!” akamwamuru.
Alegria akarembua macho yake ili kumteka mwanaume huyo. Kama alifikiri Amata hudanganywa na wanawake kirahisi basi alikosea, risasi moja ikachimba milimita kama tatu hivi kutoka mguuni mwa mwanamke huyo.
“Nipe ninachotaka haraka kisha unirudishe kwa bosi wako,” akamwambia huku akimfuata taratibu. Mwanamke huyo mwenye bikini akajikuta hana kingine cha kumlaghai jamaa huyu.
Huyu ni nani? Akajiuliza.
“Huku, nifuate!” Alegria akamwambia Kamanda, kisha wakafuatana na Alegria akamzungusha mpaka upande wa nyuma.
“Inabidi twende bondeni,” akamwambia Amata.
“Bondeni wapi?” akamuuliza.
“Hicho unachokitaka, kipo bondeni,”
“Sitaki maneno, nipe ninachotaka,” Amata akasisitiza.
Pale aliposimama Alegria, pakafunguka na kuacha uwazi katikati, wakateremka na katika chumba walichopita, Amata akashtuka kukuta kuna mtu kafungwa minyororo miguuni na mikononi akining’inia.
“Shiit! Mfungue huyu!” akamwambia Alegria.
“Sina funguo, hiyo loki hufungwa kwa namba na namba hiyo anaijua Oliviera pekee, sasa si umeshamuua, kwa hiyo no way!” Alegria akajibu kwa dharau, Amata akavuta hatua moja na kumpiga kwa kitako cha bastola katikati ya paji la uso na kumpasua.
“Mfungue!!!” akamwambia. Alegria akajipapasa katika paji la uso, akashika damu inayotiririka, kisha akamtazama Amata.
Kama kuna kitu ambacho Kamanda Amata hakuwa anakipenda ni kuoneshwa dharau na mtoto wa kike. Akairudisha bastola mahala pake, kumfuata mwanamke huyo. Lakini kabla hajafanya atakalo, yule mwanamke akaliamsha dude kwa mapigo ya kutosha ya karate. Amata akayapangua yote kisha akamshushia moja la kilo nyingi na kumpeelka sakafuni. Kamanda akamuwahi huku tayari mkononi ana kisu kidogo amekwishakikunjua, akakididimiza kwenye nyama ya paja.
“Aaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaahhhhhh!!!!” Alegria akatoa yowe lililomstua yule mateka.
“Mfungue!!!” akamwambia na wakati huo tayari mkononi ana kisu kingine. Alegria akainuka kwa taabu na kutembea kwa kuushika ukuta huku damu ikimwagika kwenye paja lake, akaingia kwenye kile kuwazi na kubonya namba fulani kwenye kifaa maalumu, ile minyororo ikalegea na yule bwana akawa huru.
“Huyu ni nani?” akamuuliza.
“Mpumbavu kama wewe!” Alegria akajibu.
“Sawa, nioneshe ninachotaka,” akamwambia tena na mwanamke yule akaendelea kujikongoja mpaka kwenye mlango mwingine wenye kufuri.
“Hapa!” akamwambia Amata, naye hakufanya ajizi, akachukua bastola yake na kuifumua kisha mlango ukawa wazi. Kulikuwa na shelfu ya vitabu na kabrasha kadhaa. Amata akaingia ndani na kijichumba hicho na kuvuta hili na lile.
‘SECRET ASSASSINATION’ moja ya makabrasha lilikuwa limeandikwa hivyo.
“Thank you very much!” Amata akamwambia Alegria kisha akamwongoza kutoka nje wakampitia na yule bwana mwingine, Amata akamsaidia kumkokota mpaka pale kwenye boti lililonasa dirishani. Amata akalisukuma kutoka upande wa ndani nalo likajikita chini kwa upande wa nyuma, akatoka na kulivuta kwa nje, akalisukuma mpaka majini kwani hapakuwa mbali, kisha akamtaka mwanamke yule kushika usukani. Watatu hao wakaondoka taratibu na kutokomea baharini kurudi Condominio Bela Vista.
Palepale alipopandia boti ndipo liliposimama tena na Bwana Pereira akatoka nje kuwalaki. Mkononi mwa Amata kulikuwa na ule mkoba ambao ndani yake kuna lile kabrasha, akashuka nalo na kusimama wima. Kisha akageuka kwa Alegria na kuchomo kile kisu kutoka pajani. Pereira akaendeela kutazama Amata anavyomchomo kile kisu. Akakipangusa na kwa kitambaa kutoka mfukoni mwake na kukirudisha ndani ya koti la suti aliyoivaa.
“Umefanya nini?” Pereira akamwuulia Amata.
“Nashukuru kwa wema wako nimepata ninachokitaka, na nimempata rafiki yangu pia, good bye and see you soon!” Amata akamuaga na kuondoka na yule jamaa aliyechoka ambaye kwa mateso alibaki na nguvu aliyopewa na Mungu tu.
* * *
Kamanda Amata moja kwa moja alikwenda na mtu wake katika kliniki moja maarufu sana ambayo mzee yule, dereva wa taksi alikuwa anaijua na ndiye aliwapeleka. Katika kliniki hiyo, Amata akakutana na daktari mwanamama mtu mzima mwenye asili ya Kihindi, akamkabidhi mgonjwa huyo huku akimtaka asiruhusu kuonekana na mtu yeyote.
“Wala usiondoke, subiri hapahapa, ni masaa kama mawili au matatu tutakupa jibu na utaweza kwenda na mtu wako,” yule daktari akasema.
Kamanda Amata akasubiri. Baada ya saa mbili, kweli mtu yule alikuwa sawa, akitembea mwenyewe bila kushikiliwa, aliyeonekana kuwa na nguvu haswa.
“Na hizi ni dawa ambazo atatakiwa kunywa kwa wiki moja,” muuguzi akamwambia Amata kisha akazilipia na kuchukua majibu ya vipimo mbalimbali. Mtu huyo akatakiwa kurudi siku ya pili kwa matibabu zaidi au tuseme ya kina. Baada ya kutoka hapo, Amata na mtu wake wakaelekea mpaka Hoteli ya Alvalade ambako alimpangia chumba na kumpatia huduma zote ikiwamo mavazi na nyingine za kukandwa na kadhalika ili kumrudisha katika hali ya ubinadamu.
Baada ya saa mbili kupita, yule mtu akawa mwingine kabisa si yule aliyemwokoa kule kisiwani. Hakuwa kijana bali mtu wa makamo, mwenye mvi chache kichwani na ndevu zilizonyolewa kiufundi sana. Suti safi ya gharama ilitulia mwilini mwake, yote haya yalifanywa na Kamanda Amata lakini mpaka dakika dakika hii hakuna aliyemjua mwenzake, ni mtu huyu tu ambaye aliisikia japo sauti ya Amata lakini mwenzake hakusikia chochotebkutoka kwa mtu huyo.
* * *
Katika chumba namba 720, ndani ya Hoteli ya Alvalde, mtu huyu alisimama mbele ya kioo kikubwa akijitazama mwili wake uliositiriwa kwa suti ya gaharama.
“Ni nani huyu aliyeniokoa?” akajiuliza kwa sauti ndogo. Hakukuwa na wa kumjibu, akajitazama vidole vyake na kugundua kuwa kimoja kimekatika, hakipo kabisa, akatikisa kichwa.
“Walinikata kidole!” akajisemea tena. Akajaribu kutikisa mguu, unaweza kidogo japo bado una uzito au tuite ganzi.
“Miezi mine chini ya himaya ya washenzi hawa, bila Mungu wangeshaniua…” akajisemea.
Maneno yote haya aliyazungumza peke yake akiwa kasimama mbele ya kile kioo, mtu huyu aligundua udhaifu mkubwa wa mwili wake katika utendaji kazi. Jamaa hawa walimweka katika himaya yao kwa takribani miezi mine ilhali alikotoka walikuwa wakimtafuta na kusaidki kuwa kapotea au kafa kabisa. Akajaribu kuvuta kumbukumbu ya jinsi alivyoingia katika himaya ya washenzi hao hakukumbuka. Ubongo wake ulikuwa ukimleta mpaka anaingia kwenye gari, zaidi ya hapo ni giza na ukiwa.
Ngoh! Ngoh! Ngoh! Mbisho wa hodi ukamshtua kutoka katika mawazo yake. Akautazama mlango huo kwa chati huku kichwani mwake akijiuliza kama afungue au la.
Liwalo na liwe! Akajisemea na kuuendea mlango, akaufugua na macho yake yakagongana nay a Amata. Hakuongea kitu akajikuta akigwaya tu kwani hakumwona mtu huyo kutabasamu tangu alipomwokoa.
“Tunatakiwa kuondoka! Haraka!” Amata akamwambia.
Yule mtu hakujali kujiuliza imani yake yote ililala kwa kijana huyu ambaye ukiwaweka pamoja inaoneka wazi kuwa huyu ni mkubwa kama miaka mine au mitano kwa Kamanda. Akatoka na kumfuata Amata katika njia ya ngazi, kisha wakaachana na ngazi na kuchukua ukorido mrefu uliowatoa upande wa kumbi za mikutano huko wakateremka kwa ngazi nyingine mpaka chini kabisa, wakajikuta nyuma ya hoteli. Hawakujisumbua kuzunguka mbele, wakapita kwenye kijimlango kilichjengwa katika wigo wa hoteli hiyo na kuibukia barabarani, Amata akafungua mlango wa gari na kuingia ndani huku yule mtu akifuatia kisha wakaondoka kwa kasi.
Taksi ya akina Amata, ikawasili katika Nyumba ya Wageni ya Chicala iliyojengwa katika ghuba ya Total Angola.
“Hapa patatufaa!” akasema huku akitangulia kushuka na kuchukua mkoba wake kutoka katika siti ya nyuma. Hakujali kama mtu wake huyo anaelewa au haelewi. Kisha akamtazama yule mzee mwenye taksi ambaye mpaka dakika huyo hata yeye alikuwa akipelekwa pelekwa tu hajui nini kinaendelea.
“Sasa, we waweza kwenda, mimi nikikuhitaji nitakwambia, bado nina siku kama tatu hapa Luanda. Mtu yeyote akikuuliza kama niko wapi usimpe habari zangu sanasana nitumie meseji kwa siri na meseji hiyo aundike K.A, mi nitaelewa kuwa kuna mtu anakuuliza juu yangu. Akampa pes iliyotakata na kuagana naye.
Haikuwa Gesti ya hadhi kubwa ila si mbaya sana, wakapata chumba kiimoja chenye vitanda viwili na choo ndani. Ukikaa ndani ya chumba hiki na kutazama diridhani unakutana na Bahari ya Atlantiki na Kisiwa cha Ilha Da Canzaga unakiona kwa mbali sana ila kwa chombo kama darubini unaweza kukiona uzuri kabisa. Kamanda Amata akafunga mlango na kutupia mkoba wake kitandani kisha akaketi na yule mtu naye akaketi upande wa pili, yaani kwenye kitanda kingine. Kutoka katika meza ndogo pembeni yake, akanyakua simu iliyowekwa hapo na kuzungusha namba kadhaa kisha akaiweka sikioni. Baada ya kupokelewa upande wa pili, akaagiza whisky na bilauri mbili na kigudulia cha barafu. Haikupita muda mlango ukagongwa, akaufungua na mwanadada mfupi kibonge akaingia na kuweka kinywaji kile mezani kisha akaondoka zake. Amata akafunga mlango na kuketi huku akifungua kile kinywaji, moja ya bilauri akajimiminia na ile nyingine akampa rafiki yake ambaye hajawahi hata kusikia sauti yake.
Baada ya nusu saa ya kila mtu kupiga kama bilauli tatu hivi, Amata akafungua kinywa na kumuuliza, “ Wewe ni nani?”
Yule jamaa akamtazama Amata kana kwamba haelewi anachoambiwa.
“Naitwa Costantine!” akajibu kwa sauti ya kukwaruza sana kiasi kwamba Amata akajua wazi kuwa huyo jamaa ana shida kwenye mfumo wake wa sauti hasa kooni.
“Costantine?” Amata akarudia kwa kuuliza.
Mara hii kabla hajajibu akakohoa kwanza na kutikisa kichwa chake, “Yes! Costantine,” akajibu. Ukimya ukapita tena kwa jozi la sekunde, mara hii Amata akajua kwa nini mtu huyo hapendi kuongea kwani alihisi ana maumivu sana kwenye koo.
“Mimi naitwa Mr Spark kutoka Zambia…”
“Oooh Mr. Spark!”
Koh! Koh! Koh! Akakohoa mfululizo kisha akaendelea kusema, “Happy to know you… mimi nilikuwa nakufa polepole,” koh! Koh! Koh! “…lakini nashukuru umenileta tena duniani, umenipa nafasi ya pili ya kuishi,” akaongea kwa kirefu.
“Obrigado!” akamshukuru.
Costantine akainuka na kuelekea dirishani, akasimama na kuangalia upande wa baharini, kisha akachukua darubini ya Amata iliyokuwa juu ya meza, akatazama tena baharini.
“Ilha Da Canzaga!” akatamka. Kamanda Amata akainuka alipoketi na kumwendea pale dirishani, wakasimama pamoja.
“Unapaona vizuri?” akamuuliza.
“Yes!”
Kishapo, Amata akachukua simu yake na kufungua program fulani katika hiyo, wakati wote Costantino alikuwa akimwangalia anachofanya. Na mara mlipuko mkubwa ukaonekana kule kisiwani.
“Kila kitu kimeanguka!” Amata akasema. Costantine akatazama kisini na kushuhudia moto na moshi mzito, akageuka kwa Amata na kumtazama, akamwona akiirussha ile simu kitandani na kisha ye mwenyewe kujibwaga hapo na kujimiminia kinywaji.
“Who are you?” Costa’ akamuuliza.
“Mr. Spark… mwokozi wa wanyonge,” akamjibu.
“Kazi yako ni nini hasa hapa Angol?” Costa akaanza kumhoji Amata.
“Nilikuja kuiangusha Ilha Da Canzaga, bahati nzuri nimekuokoa na wewe lakini pia nilikuwa nahitaji hii…” akachomoa kabrasha lake mkobani na kumwonesha kwa mbali.
“A secret assassination!” akasoma.
“Yes! Sasa sikiliza, mimi nimemaliza na hatuna budi kuagana, lakini marafiki lazima wajuane kwa kina….”
“…Ndiyo, bila shaka…”
“Ulikuja kufanya nini Angola?” akamuuliza.
“Nilikuja kumsaka mtu mmoja muuaji anayetafutwa kila kona ulimwenguni, lakini mtandao wake ukahi kunitambua na wakaniteka na kujikuta nipo kule, hata sikuwa najua kama ni kisiwani mpaka nilivyoona tulipokuwa tunatoka,” Costa akasema.
“Muuaji?” Amata akauliza.
“Yes, muuaji mmoja profesheno… katika kumtafuta nikagundua kuwa ana misheni ya kufanya hapa Angola …”
“Lini ilikuwa atekeleze misheni hiyo….?” Amata akamkatiza kwa swali.
“Aaaaannnhhh huu ni mwezi gani, samahani!” Costa akauliza, kumbe hata hakuwahi kujua tarehe na miezi inakwendaje.
“September!” akajibiwa
“September?” khooo – kho! Akakohoa, “ina maana nimekaa miezi mine mateka?” akasema.
“Ni miezi mine iliyopita… huyu bwege anaitwa Martin Gupter ila hutumia majina mengi sana na sura nyingi za bandia kujificha, yeye hutumiwa na mitandao mikubwa ya mauaji ijapokuwa naye anatimu yake ya watu wawili wenye weledi mkubwa wa mbinu za kigaidi na mauaji, hayawajawahi kukamatwa wala kujulikana kwa majina halisi,” akamwambia Amata.
Akili ya Kamanda ikaanza kuunganisha matukio, akachekecha na kuchekecha, akaona kwa vyovyote vile kuna uwezekano mkubwa wa misheni yao kuwa moja ila ikatofautiana maudhui.
“Miezi mine ilopita, aliuawa rais wa Angola,” Amata akasema.
“Come on! Walifanikiwa? Hawa ni washenzi…” Costa akaongea kwa hasira kidogo.
Ina maana huyu jamaa anajua mengi juu ya hili! Amata akawaza na kubaki kimya kwa sekunde kadhaa akimtazama mtu huyo. Baada ya muda kidogo, Costantine akainua uso na kumtazama Amata.
“Martin Gupter ni muuaji hatarai sana, yeye amebobea katika assassination iwe ya moto au ya baridi. Anatafutwa, natafutwa na watu wengi ikiwamo mimi, nilipata siri ya kuwa wanakuja huku Angola ili kutekeleza mauaji ambayo wenyewe waliyaita ‘Mauaji ya Kihistoria’, nikiwa hapa nikawafuatilia sana mpaka nikajua ni wapi watafanyia shabaha yao, siku nilipokuwa nimepanga kumaliza mchezo nikajikuta matatani, nilikuwa nachukua gari kwenda eneo la tukio, ghafla nikapigwa na kitu kama bomba la chuma kichani, nikapoteza fahamu na kujikuta ndani ya chumba kile. Wao nao wakanitesa na kunipiga sana ili niwaambie ni nani kanituma…”
“Kwa hiyo ni hicho tu kilichokuleta Angola?” Amata akamuuliza.
“Hicho tu! Namhitaji Gupter nimtoe roho yake, nilishahesabu nimeshindwa lakini wewe umenipa nafasi nyingine na kwa nafasi hii lazima nimmalize,” akasema, “na wewe huna haja na huyu shetani?”
“Sina, ila ninachotaka sasa ni kukamilisha uchunguzi kama mtu aliyetaka kufanya mauaji Dar es salaam ni huyo huyo au la…”
“Tena?”
“Ee ila hakufanikiwa na risasi ikamuua mtu mwingine, sasa nataka kuhakikisha je muuaji huyu wa Angola na yule wa Dar es salaam ni mmoja? Amata akamwambia huyu mtu bila kumzungusha.
“Hiyo kazi ndogo, nitakupeleka kwa mtu mmoja ambaye anaweza kukusaidia kujibu maswali ya shida yako, kwa vyovyote atakuwa anajua nini kinaendelea”.
“Twende hata sasa!” Amata akasema huku akiwa tayari amekwishainuka.
Wakatoka nje na kufunga mlango kisha wakachukua taksi mpaka mtaa mmoja wa kimya sana, ni majumba makubwa na machache yaejipanga upande huu na ule.
“Tuache hapa!” Costantine akasema na lile gari likaingia pembeni, wakashuka na kulipa kisha likaondoka, wakalitazama kwa kulisindikiza mpaka lilipoishia kwenye upeo wa macho yao.
Kutoka hapo wakavuka barabara, na Costantine akaongoza njia mpaka katika jumba moja la kifahari. Muda wote huu, Costantini ndiye alikuwa mbele huku Amata akifuatia kwa karibu maana hakujua hata ni wapi kiukweli alikuwa akipelekwa.
Kelele za mbwa akibweka zilisikika ndani ya wigo wa jumba hilo, na kabla hata hawajabonyeza kitufe cha kengele, mlango ukafunguliwa na mtu mmoja wa makamo aiyevalia jinzi na fulana mchinjo akatoka na kulifuata geti hilo kwa mwendo wa haraka kidogo. Bila kuongea neno lolote akafungua geti na kuwapa ishara ya kuingia, wakafanya hivyo na bwana huyo akawaongoza mpaka sebuleni wakaketi.
“Yes! Nashindwa niseme nini, ni wewe au?” yule bwana akamuuliza Costantine, wala hakuwa na muda na Amata.
“Yes! Ni mimi, nilikuwa mikononi mwa mbwa kwa miezi karibu mine kwa mujibu wa kalenda,” Costa’ akaeleza.
“Nilijua umekufa, tumekutafuta sana, mpaka kwa waganga tumeenda, mwisho tukakubali kushindwa…”
“Mlikubali tu kushindwa, ila sikufa…” akamjibu kwa kumkatiza kile alichokuwa akiongea. Yule jamaa akampa ishara ya kumwita pembeni ili wazungumze machache.
“Hamna shida, ongea hapahapa!” Costa akasema huku akimtazama Amata, “Najua sijakutambulisha, huyu ni rafiki yangu, anaitwa Spark!” akamtambulisha Kamanda kwa mwenyeji wake kisha akafanya hivyo kwa Kamanda Amata, wakafahamiana na kupeana mikono.
“Nasikia mzee katunguliwa,” akaanzia hapo na Amata akawa kimya akaisikiliza tu.
“Yes! Tumeshasahau ila bado tuna kazi ngumu kwani baada ya kufanya uchunguzi na kuweka tafutishi zote pamoja lile kabrasha likaibwa, mpaka sasa badala ya kumsaka muuaji tunatafuta kabrasha,” akaeleza.
“Oh shit! Hamjapata chochote? Ni Gupter au ni nani?” Costa akauliza.
“Hatujang’amua ni nani mpaka sasa tumemwita jina ‘sweet killer’ kwa sababu anaua na hapendi kuacha chochote nyuma yake, bahati nzuri tu niliokote kitu hiki…” akainuka na kuiendea droo, akafungua na kuchukua kijimfuko cha plastiki akaenda nacho mezani na kukifungua ndani, akamwaga vitu viwili … “ganda la risasi lakini ni mita kama mia tatu kutoka eneo tunalolihisi muuaji alikuwako,” akaeleza.
“Naweza kulishika?” Amata akauliza.
“Yes, ila usitumie mkono tupu,”
“Sawa!” Amata akajibu na kutoa soksi za mikononi kutoka katika suti yake akavaa na kuinua lile ganda, akaligeuza kwa nyuma na kujikuta anapigwa na bumbuwazi.
Magnum 22 riffle! Akasoma kilichoandikwa kisha akampasia Costantine, naye akalipokea na kuatazama vizuri.
“Martin Gupter! Huyu ni Gupter, siri ya jamaa huyu ni kutumia aina moja ya bunduki, Magnum 22 riffle, nimepita kwenye kesi zake kama tatu hivi kati ya hizo wachunguzi wamegundua aina hii ya bunduki kutumika,” Costa akaeleza.
“Ungekuwa umefanikiwa kumpata, ungetusaidia sana, sasa utafanya nini, kwa ujumla si kwamab tumemkosa ila ni kazi sana kumpata,” yule jamaa akasema.
“Mh!” Costa akaguna, “Jerry! Huyu bwana naye anamtafuta Gupter naweza kusema hivyo,” akamwambia.
“Huyu? Mr Spark?” akauliza. Ni mara hii Jerry alimtazama Amata, akaondoa miwani yake na kuiweka kitini, akatikisa kichwa, “Unamtafuta Gupter, the sweet killer?” akamuuliza.
“Si kwamba namtafuta Gupter, kwa sababu mpaka sasa inabidi nijiridhishe kama ndiye ninayemtafuta. Si unajua kilichotokea Tanzania siku nne zilizopita!”
“Yes! Najua, na ninafuatilia kujua nini Tanzania inafanya kwa sababu tunaiamini sana kwenye maswala ya kijasusi, ila hatujasikia chochote,” Jerry akasema.
“Ninaanza kuona kuwa ni huyu aliyetaka kutekeleza mauaji ya Dar es salaam…”
“Kwa nini??” hii ‘kwa nini’ ikatoka kwa Jerry na Costa’ kwa mara moja. Kamanda Amata akaingiza mkono mfukoni na kutoa kijimfuko cha plastiki na kuweka mezani ganda la risasi kama lile lile.
“Shiiiiit!” Jerry akang’aka kwa kulitazama tu, kisha akamtazama Amata na kisha Costa.