MAGNUM 22
Sehemu 20
WATERLOO – SIERRA LEONE
Kamanda Amata na yule mwanamke waliangukia mtoni, ilimchukua kama sekunde kumi na tano hivi kuibuka juu ya maji na kuanza kuogelea kwa ufundi huku akimsaidia yule mwanake ambaye alionekana kutoyamudu maji hayo yaendayo kasi ya Mto Lofa. Kwa maelekezo machache aliweza kuijiokoa kisha wote wakatoka nje yam to huo.
“Asante sana, umeniokoa!” yule mwanamke akashukuru.
“Unaitwa nani?” akamuuliza.
“Relindis!” akajibu huku akitweta kama mbwa aliyekimbizwa.
“Ok, tuondoke hapa hapatufai,” Amata akamwambia na kuanza kumkokota na kupanda mlima kwenda juu walipoacha lile gari. Baada ya dakika kama thelathini hivi wakalifikia gari lao na kuingia ndani.
“Wapi tunaenda sasa?” Relindis akauliza kwa shauku.
“We unataka twende wapi?”
“Kwangu!”
“No! kazi inayonikabili ni kubwa na ngumu sana, sina budi kuondoka nje ya nchi hii,” Amata akamwambia huku akiwasha gari na kulirudisha barabarani kisha akaliondosha kwa kasi.
“Safari hii umefikia wapi?”
“Hata safari ile sikucheck-out, hivyo nipo Swizz Spirit,” Amata akamwambia wakati tayari akiwa barabara kuu kuelekea Freetown. Mwendo wake haukuwa wa kawaida kwa maana alikuwa akishindana na muda, wakati gari hilo liko katika kasi hiyo Relindis alikuwa kimya kabisa akimwangalia kijana huyo anavyobadili gia na kupanga na kupangua.
* * *
Mbele ya hoteli ya Swizz Spirit iliyojengwa katika viunga vya mji wa Freetown, Amata aliegesha gari mita kama mia tatu hivi, akamtazama Relindis ambaye bado alikuwa ametota kwa maji ya mtoni.
“So?” akauliza mwanamke yule.
“Nenda nyumbani kwako kaendelee na mapenzi yenu na yule gabacholi, nipigie baada ya saa tatu hivi…”
“Si kukupigia, ninaingia kazini muda huo…”
“Basi utanikuta! Si unajua kuendesha gari?” Amata akamwuuliza.
“Bila shaka!” mwanmke huyo akajibu na kufungua mlango, akazunguka upande wa derevana kuingia huku akimwacha Amata kasimama kando, akaondoka zake. Baada ya kuhakikisha gari lile limetoweka kabisa katika upeo wa macho yake, Kamanda akavuta hatua mpaka ndani ya hoteli ile na kuingia chumbani mwake pasi na kujulikana na mtu. Baada ya kuoga na kuwa katika hali nzuri, akaketi kitandani na kuchukua ile karatasi ambayo sasa ilikuwa imelowa, akaifungua taratibu ili isichanike na kuiweka mezani kisha akawasha taa ya kusomea na kuruhusu joto lake liifikie karatasi hiyo angalau inyauke kidogo.
‘Addis Ababa, yote yakamilike!’
Karatasi ile ilikuwa imeandikwa kwa mkono, na maneno hayo ndiyo yaliyosomeka japo kwa shida kutokana na mfifio wake, kisha kukafuatiwa na namba kadhaa za simu ambazo kwa Amata hazikumsumbua kujua kuwa ni za Ethiopia, namba hizo hazikuwa na majina, hilo halikumfanya kushindwa kujua kuwa ni za simu. Akakumbuka maneno ya yule dereva.
“… mmoja alikwishaondoka na wawili ndo sasa nimetoka kuwapeleka Uwanja wa Ndege…”
Akatikisa kichwa na kutazama tena saa yake, ikamwonesha kuwa ni saa mbili usiku, akapita hesabu zake kama waliondoka muda ule basi bila shaka wamekwishafika Addis.
Niko nyuma ya muda, shabash!!! Akawaza huku akianza kukusanya vitu vyake na kuvitia begini.
No time to waste! Akazidi kujikuta akiwaza, akili na mawazo yake yote yalikuwa ni kumtia mkononi Martin Gupter, Fredy na yule mwanamke wao ambao mpaka dakika hiyo walikuwa wakitikisa vichwa vya wanausalama wa Afrika. Baada ya kuhakikisha kila kitu kimekuwa sawa na kimehifadhiwa vyema begini, akachukua simu yake na kuiwasha, ikawaka, akaingiza namba anazozijua na kuzipiga.
“TSA 1!” akaita na upande wa pili simu ile ikapokelewa.
“Adui wetu amekwishafika Addis Ababa, narudia, adui wetu amekwishafika Addis Ababa!” Amata akaongea kwenye simu hiyo.
“Umesomeka, mpango ukoje upande wako?” sauti ya upande wa pili ikauliza.
“Naelekea Addis sasa!”
“Vyema! Na tukutane Addis!”
Simu ikakatika, Kamanda Amata akainua begi lake na kutoka nje, katika meza ya mapokezi akakamilisha taratibu zote za kuondoka.