Sehemu ya 18*
Hata ungelibahatika kumuona ungelijua kabisa anapata tabu kufikiria namna ya kuukwea ukuta ule mrefu wa jumba la Papaa Deo Mukamba.
Koplo makame akasema na peke yake.
"Tutumie mbinu nyingine"
Akasikiliza kidogo kisha akahama eneo alilokuwa akaambaa na ukuta mrefu akafika nyuma ya kasiri lile,huko akakutana na koplo Ziga wakateta kidogo kisha kwa wepesi wa kustukiza Ziga akawa mabegani mwa Makame,na kitendo kilichofuatia ni koplo Ziga kutua taratibu ndani ya jumba lile la kifahari,akajipa utulivu wa kuyasoma mazingira.
Akakutana na miti mizuri ya maua iliokuwa imesimama mithili ya miti ya Azuni,akautazama mlango wa mbele wa jumba lile,hapo akaona walinzi wawili wakiwa wamesimama wima,upande wa kushoto mwake kulikuwa na magari kadhaa ya kifahari,akatazama kuuzunguka ukuta ule hapo akakutana na taa kali zilizokuwa zikimulika uwanja mzima,ina maana hakuna kitu ambacho kingekakatiza mbele bila kuonekana na walinzi,lakini pia nyuma ya kila taa kulikuwa na kamera ndogo.
Akajivuta kwa hatua za mtu anaeogopa kukanyaga moto.
Hatua ya kwanza,ya pili,akajikuta akitoa tusi kubwa la nguoni huku mguu mmoja ukiwa umebaki hewani bila kutua kumalizia hatua ya tatu,akaurudisha mguu ule hivyo akawa amebaki na hatua zilezile mbili.
Zilikuwa ni nyaya ndogo zilizokuwa zimetawanywa chini, nyaya hizi zilitumika kutoa tahadhari ndani kama zingeguswa na kiumbe yoyote.
Akaangaza kwa macho ya paka hapo akaona upande mwingine kukiwa na mitego kadhaa ya kunasia miguu au kiumbe ambae angeligusa pale,akatabasamu kisha akatoa vibati kadhaa kutoka mifukoni kwake,akatupia kimoja kwenye mtego ukafyatuka nae akarukia hapo hapo.
Akafika hadi karibu na dirisha kubwa akatazama ndani akaona watu watatu wakiwa wamezunguka meza wakizungumza,akafungua kioo kile polepole akawa anapiga hesabu za kuingia ndani kabla hakafanya hivyo akamwona mtu aliemfahamu.
Akaduwaa kwa sekunde kadhaa na akapoteza umakini kwa kumshangaa mtu yule,akiwa hivyo ametulia akawashuhudia watu wale wakisimama na kuondoka mle ndani akanong'ona kidogo kisha akatumia utalamu mdogo kioo kile kikaachia akazama ndani ya jumba lile huku kwa nje akisikia miungurumo ya gari kuashiria gari zilikuwa zikiondoka eneo lile.
Koplo Makame alipokea taarifa kutoka kwa koplo Ziga,punde akaona gari mbili za kifahari zikitoka pale,akapiga hesabu za kijeshi akaona umbali uliopo kati yake na usafiri wao uliowaleta Goma upo mbali,hivyo asingeliweza kuwahi gari zile akajipapasa akatoa kidude kidogo mfano wa betri ya saa kwa wepesi wa ajabu akakirusha kikaenda kukita nyuma ya gari moja wapo,kisha akageuka na kurudi kuendelea na harakati zake.
Ziga alinyata hadi karibu na korido ya kulia chakula,hapo akatulia kuyasoma mazingira ya nyumba ile,hakukawia kuziona ngazi zilizokuwa zikipandisha juu,pia upande wake wa mbele akaiona sebule pana iliopambwa kwa samani za kisasa,akajivuta baada ya kuhakikisha hakuna mtu kwenye sebule ile.
Wakati akikaribia kuifikia sebule ile akazisikia hatua za mtu akija kwa kasi akiwa anatokea kwenye vyumba vilivyojuu,akasimama punde akamwona mwanajeshi wa wa jeshi la Kongo akiifikia sebule ile na kuchukua kitu kwa haraka na kurudi juu haraka,hapo akagundua kuna watu upande huo.
Akaifikia sebule ile na kunyata akaziendea ngazi kwa hatua za haraka na bila kelele,akajikuta akikutana na uwazi mpana huku mbele yake kukiwa na milango mitatu iliopangana,akaisogelea milango ile ni wakati akitaka kujipa umakini wa kama wa popo akasikia nyuma yake.
"freezee"
Hakutaka kusubiri akaruka pembeni ni kama alijua alipotoka tu zikafuatia risasi tatu na zilipomkosa zikapiga mlango na mmoja wapo na kuwastua waliomo.
Ziga kwa wepesi ule ule akarusha kisu chake kikatua kichwani kwa mtu yule alietoka nyuma yake,alipogeuka nyuma akaona mlango ukifunguliwa na kutoka wanajeshi watatu wakiwa na silaha zao mikononi.
Akabiringita chini na kuzikwepa risasi kadhaa zilizovurumishwa na wanajeshi wale hakutaka kuwa mzembe akawahi kuipiga taa iliokuwa ikitoa mwanga ikazima kukabaki kiza ndani ya korido ile,na kwa kutumia tumbo akaanza kutambaa kisogea pembeni kulikokuwa na milango mingine.
Akiwa katika harakati hizo koplo ziga akajikuta akiguswa na kitu cha baridi upande wake wa kulia kisha akaamuliwa kusimama,ni wakati akisimama kukawaka taa za dharura mle ndani hapo akakutana na midomo minne ya bastola ikimtazama
Asalaaam Kudo