HEKAHEKA - 19
Kitendo cha Jacob kushindwa kuongea kilimsikitisha zaidi Eve. Hivyo kwa haraka alirudisha vile vifaa masikioni mwa Jacob, kisha akarudi alipokuwa awali. Dakika chache baadaye kitu kama kengele kilitoa mlio. Eve akampungia mkono Jacob na kutokomea nje. Hapo hakuonekana mtu yeyote ndani ya chumba hicho hadi asubuhi siku iliyofuata. Ilikuwa ni siku ya sita kwa mpelelezi Jacob Matata kuwa katika kifungo hiki cha kutisha. Hakujua watu hawa walikuwa na lengo gani kwake, japo alianza kuhisi mauti.
* * *
Ilikuwa ni siku ya nne yenye mashaka na uchungu kwa mkuu huyu wa kitengo fukuzi. Mpaka wakati huu vijana wake walikuwa wameshafanya kila liwezekanalo kuhakikisha kuwa wanajua alipo mpelelezi mwenzao Jacob Matata. Lakini mpaka inafika asubuhi hii hakuna hata fununu walizokuwanazo juu ya Jacob. Kutokana na maiti walizozikuta nyumbani kwa Jacob siku Jacob alipotoweka, ilikuwa wazi vichwani mwao kuwa Jacob hakuwa amechukuliwa kwa heri. Ilikuwa hakika kuwa kabla ya kuchukuliwa yalikuwa yametokea mapambano makali yaliyopelekea kuuawa kwa watu hao. Jacob yuko hai au maiti? Kama yuko hai, atakuwa sehemu gani? Maswali haya yamekuwa yakijirudia rudia kichwani kwa Bi. Anita mkuu wa Ofisi Fukuzi.
Siku ile kabla ya kutoweka kwa Jacob, ofisi hiyo ilikuwa imeandaa operesheni kubwa ya kwenda kwenye jumba la mzee Harken Kalm. Operesheni hiyo ingeongozwa na Jacob Matata mwenyewe. Lakini kitendo cha kutoweka kwake ilikuwa ni wazi kuwa wasingeweza tena kwenda, kwani ni Jacob aliyekuwa akipajua mahali walipokusudia kwenda. Hivyo ofisi yote ilikuwa imekumbwa na ubaridi wa kutisha.
Mpaka kufikia siku hii, Bi. Anita alikuwa ameshapiga simu kila sehemu aliyodhani kungekuwa na tetesi. Lakini Jambo moja lilikuwa likija kwa mbali- Jacob yuko hai japo yawezekana kuwa katika shida.
* * *
Kila mmoja kwa lengo lake alikuwa katika jitihada zake. John Kificho alikuwa amekufa katika kumpenda msichana Regina, hivyo alikuwa katika jitihada za kuuteka moyo wa msichana huyo. Kwa sababu asizozijua, mpelelezi Jacob Matata alijikuta mikononi mwa John Kificho. Hakuwa anamjua Kificho lakini alikuwa katika hali mbaya na alitakiwa kufanya kitu ili kujinasua katika mikono hiyo hatari.
Regina alishatambua nia ya Kificho kumtaka, lakini hakujua kuwa Kificho hakuwa na lengo la kumsaidia Jacob Matata. Hivyo alianza kumuamini Kificho na kumchukulia kama mtu mwenye huruma ajabu. Pamoja na hayo, moyo wa Regina ulikuwa katika mapenzi mazito kwa mpelelezi Jacob Matata.
Mzee Harken Kalm kwa upande wake alikuwa amechanganyikiwa, kutoweka kwa Regina na kutoonekana kwa Jacob Matata aliona kuwa ni hatari kwa himaya yake. Hivyo alikuwa akifanya kila njia kuhakikisha anampata Jacob na Regina, ambao aliamini kuwa walikuwa na siri zake.
Bi. Anita mkuu wa kikosi cha siri cha ofisi fukuzi, ameamua kuacha ofisi na kuingia uwanja wa mapambano kuongoza kundi la vijana wake kuhakikisha wanampata Jacob na kusambaratisha himaya ya mzee Harken Kalm. Alikuwa makini kufuatilia na kutaka kujua Jacob yuko wapi, kwani aliamini kuwa kwa vyovyote Jacob yuko hai.
Tamaa. Ni tamaa iliyosababisha mzee Harken Kalm, apokee simu hii. Alikuwa ndani ya chumba maalum ndani ya himaya yake, akisubiri taarifa yoyote nzuri juu ya msako uliokuwa ukiendelea. Tangu kutoweka kwa Regina na kutoonekana kwa Jacob Matata, mzee huyu amekuwa hana amani huku akijiona hayuko salama kabisa. Kikosi cha Tai, kikosi cha Paka na kikosi cha Mbwa weusi vyote vilikuwa vimesambaa katika maeneo mbali mbali kuhakikisha Jacob na Regina wanapatikana.
Simu hiyo haikulia muda mrefu kabla mzee Harken Kalm hajainyanyua na kunong’ona
“Leta habari” Alisema hivyo akiwa na hakika kuwa huyu alikuwa ni mmoja wa vijana wake.
“Shikamoo mzee!” Ulisema upande wa pili. Mzee Harken Kalm hakuitikia, badala yake akasema.
“Siko kwa hilo, labda unalingine nikusaidie!” Kadhalika sauti ya mzee Harken Kalm ilitoka katika hali ya kunong’ona.
“Sihitaji msaada wako ila nipo kukupa msaada!” Ulijibu upande wa pili katika sauti nzito, tulivu ya raha.
“Shiit, unaweza nisaidia nini wewe? Kwanza umepataje hii namba?” Mzee Harken Kalm aliongea tena kwa kunong’ona. Aliongea hivyo huku akiwa anajiandaa kuweka simu chini. Hakuwa amependezwa na maongezi ya mtu huyu asiye mfahamu.
“Ni juu ya Jacob na Regina!!” Kwa ile sauti nzito, tulivu ya raha mtu wa upande wa pili alisema. Ilikuwa wazi kuwa mtu huyu alikuwa akisema maneno hayo kwa raha mno.
“Wamefanyaje?” Mzee Harken Kalm aliukumbatia zaidi mkono wa simu, huku ngozi yake ikibadilika na kuwa nyekundu.
“Najua walipo!” Ulisema upande wa pili.
“wako wapi?” Mzee Harken Kalm alinong’ona zaidi kana kwamba alikuwa na mtu chumbani humo.
“umeulizia hatua ya mwisho, kuna hatua kabla ya hilo swali” ulisema upande wa pili kwa sauti ya pozi.
“Una hakika na usemayo?” Harken Kalm alinong’ona
“asili mia moja!”
“hatua gani sijauliza”
“Pesa”
“Siyo pesa, nitakupa fedha. Sema uko wapi na nikupateje?” Mzee Harken Kalm aliongea huku akiminya kitufe fulani. Mara walikuja vijana wawili, walisimama wakisubiri amri zaidi toka kwa mzee Harken Kalm.
“Sawa, kesho asubuhi nitaenda benki kuangalia kama utakuwa umeniwekea hizo pesa au fedha kama unavyoita. Nikizikuta nitawaelekeza mahali mtakapo wachukua watu wenu” Ulisema upande wa pili, kisha mtu huyo alitaja namba za akaunti yake ya benki kisha akakata simu.
Simu ilipokatwa, mzee Harken Kalm aliwageukia vijana wake, kisha akanong’ona “Nataka kujua hii simu imepigwa kutoka wapi na habari kamili za mpigaji” alipomaliza alibonyeza kitufe fulani akapotelea ardhini. Jitihada zilifanyika kuhakikisha mpigaji wa simu hiyo anajulikana. Lakini masaa kadhaa yalikatika bila mafanikio, ilikuwa ni ujumbe tosha kwa mzee Harken Kalm kuwa mpigaji wa simu alikuwa mtu aliyejiandaa na si vinginevyo.
Taarifa kuwa vijana wake walishindwa kujua sehemu aliyokuwepo mtu aliyepiga simu na kutaka ampe pesa ili amuambie Jacob na Regina walipo, zilimfanya Mzee Harken Kalm apate hamu ya kusikiliza tena sauti ya huyo mtu. Akiwa kwenye chumba chake cha siri kilicho chini ya ardhi, alibonyeza kitufe fulani kilichokuwa pembeni ya redio yake, mara sauti za mazungumzo waliyofanya na huyo mtu kwenye simu zilitokea tena. Alisikiliza kwa makini tena na tena. Kilichomfanya arudie kusikiliza ni sauti ya mtu huyu aliyempigia, haikuwa ngeni masikioni kwa Harken Kalm.
"shiiiit, Banzi!!!!!!!!” Alisonya kwa hasira.
"Mshenzi huyu bado yuko hai?” alijisemea kwa mshangao. Mzee Harken Kalm baada ya hapo aliwasha Laptop yake. Humo alifunua mafaili kadhaa kisha akatulia huku akisoma taarifa fulani. Alichukua kijtabu chake kidogo akaandika vitu fulani kisha uso wake ukaonesha tabasamu fulani. akasimama na kutoka katika chumba hicho. Alipita vyumba kadhaa ambavyo vyote vilikuwa sehemu ya ardhini ambayo ni mzee Harken Kalm pekee aliyekuwa anajua namna ya kuingia huko. Alitembea hivyo hadi alipofika kwenye mlango uliokuwa umeandikwa ‘Contact the world’ hapo alibonyeza namba fulani mlangoni hapo na mlango ukafunguka. Chumba hiki kilikuwa kipana angavu na kilichosheheni vifaa mbali mbali vya mawasiliano. Hapo Harken Kalm, aliwasiliana na huyu akaacha, akampigia yule, akakunja uso akakata simu, akamtumia ujumbe huyu, ujumbe ulipojibiwa akatabasamu, akapiga na kupiga, akaandika ujumbe na kusoma mwisho akaonekana kuchoka...ni wakati anaelekea kutaka kutoka chumbani humo ndipo akawa kama aliyekumbuka kitu. Akachukua mashine fulani na kuingiza namba kadhaa. Mashine ilitoa milio...Ngriiiiiih ngriiiiii ngriiiiii, kama mara sita hivi.
“Old friend!!!” Harken Kalm alisema kwa sauti chovu iliyochanganyika na matumaini kwa mbali.
“Ben, umejichimbia wapi?” Harken Kalm alihoji baada ya upande wa pili kuwa kimya
“Najipa nafasi Harken Kalm!” Upande wa pili ulijibu.
“Nahitaji huduma yako Ben kama uko sawa!”
“Unajua kuwa wewe siwezi kukukatalia” Upande wa pili ulijibu kasha ukaongeza.
“Ndio Kalm nikusaidie nini?”
“Unaweza jua Banzi yuko wapi kwa sasa?” Kalm aliuliza.
“Kuna sehemu fulani anakula bata” Upande wa pili ulijibu.
"Sikiliza Ben, nilikuambia kuwa kuna kazi nataka nikupe, sasa nakupa kazi, alipo Banzi ndipo alipo Jacob Matata na Binti mmoja aitwaye Regina. Sasa nakupa kazi ya kuwamaliza wote watatu, utatumia njia gani na namna gani hiyo sitaki kujua, nataka ukinipigia simu uniambie kuwa kazi tayari nami nitafanya mambo yangu” Harken Kalm alisema huku sauti yake ikiwa na mchanganyiko wa uchungu na hasira kama ladha ya maziwa ya mgando yaliyo haribika.
“Hiyo kazi ni ngumu sana, unajua hapo unaniambia nifanye kazi ya kuwamaliza makomandoo wawili, unajua fika uwezo wa Banzi na Jacob, najua fika kwa sasa hawako pamoja, kwa vyovyote ilivyo Jacob atakuwa mateka wa Banzi. Wewe mzoefu wa mambo haya, bila shaka unajua itakuwa hatari kiasi gani, hivyo hilo lazima ulizingatie kwenye malipo la sivyo nikimaliza kuwaua wao utafuata wewe” Sauti ya upande wa pili iliongea, iliongea kwa kuunguruma na mikwaruzo kama kawaida yake.
“Ben mimi na wewe hatujakutana barabarani bana” Harken Kalm alisema.
“Yeah, nadhani unajua ni kwa nini nafanya hivi, sihitaji pesa Harken Kalm, ila nahitaji kumuenzi baba yako. He was a good man” Upande wa pili ulisema.
Waliagana simu ikakatwa.
“Dawa ya moto ni moto, si maji, Ben ataumaliza mchezo” Harken Kalm alijisemea huku uso wake ukipata matumaini.
* * *
Baada ya mazungumzo na Harken Kalm, mwili wa Ben ulisisimka, alitabasamu, tabasamu baridi, picha ya Jacob Matata na Banzi zilimjia kichwani, aliwaangalia kila mmoja kwa zamu, kisha akaelekea kwenye friji na kutoa karoti moja akaanza kutafuna huku anazunguka sebuleni kwake.
Ben alikuwa Komandoo, komandoo kamili kwa maana ya kuhitimu. Mafunzo ya mtaani alipokuwa akingali mdogo, baadae alipojiunga na jeshi baada ya kufeli kidato cha nne, kisha kuwa miongoni mwa vijana kumi na tano waliochukuliwa kwenda Cuba kwa mafunzo baada ya urafiki wa Nyerere na Castro kuwa umekolea. Kwa vile alihitimu kwa kiwango cha kutisha, mwalimu wake wa kichina alimfanyia mpango wa kujiunga na shirika moja la siri nchini china ambalo lilikwa likitoa huduma ya uuaji ‘assassination service’. Alijiunga na shirika hilo kwa siri na kuwa miongoni mwa wauaji wa kuogopwa japo sura yake na jina lake halisi halikuwa likijulika. Watu wengi duniani hasa mashirika ya kijasusi na kigaidi yalimjua kwa jina moja tu – Kiroboto.
Mwaka 1995 alipata ujumbe wa siri kuwa alihitajika kwenda Siera Lione ambako mtu mmoja maarufu alikuwa katika harakati za kuuchukua urais wa nchi hiyo. Japo mtu huyo alikuwa mwanajeshi, lakini alitaka kuwa na mlinzi wake ‘special’ mbali na wanajeshi. Hivyo alikubali kulindwa na wanajeshi, lakini kwa sababu ambazo zilikubaliwa na waliokuwa wakitaka kumuweka madarakani, ilibidi atafutwe mtu special. Majina mengi yalipendekezwa ndani na nje ya bara la Afrika, lakini jina moja tu lilipita, nalo ni Kiroboto.
Moja kati ya masharti aliyopewa Kiroboto ili kupata kazi hiyo, ilikuwa ni kuua wazazi wake wote ili atakapokuwa katika kutimiza majukumu yake kitu muhimu kwake iwe ni huyo Rais mtarajiwa tu. Kwa Ben au Kiroboto kama alivyofahamika, mambo mawili yalikuwa muhimu sana kwake, pesa na wanawake. Alipenda pesa kama roho yake na pia alipenda wanawake kama mwili wake mwenyewe. Hivyo kwa kuzingatia kiasi cha pesa alichokuwa ameahidiwa kwa kazi ile, haikumpa shida kuja Tanzania na kuwamaliza wazazi wake wote wawili kwa risasi. Baada ya hapo akarejea Siera Lione na kuianza kazi yake ya kuulinda uhai wa aliyekuwa Rais mtarajiwa wa nchi hiyo wakati huo. Kweli alikuwa Kiroboto, kwani hadi mkataba wake ulipokwisha kila mmoja alinyoosha mikono kuwa jamaa alikuwa kiroboto. Cha mwisho kilichompa umaarufu zaidi duniani, ni pale mtu aliyemlinda kwa miaka mitano alipoona ameshachukua madaraka ya Urais, kwa siri alisitisha mkataba na Kiroboto. Kwa vile jeshi lilikuwa halimpendi na waliona tayari ameshakuwa na siri nyingi za nchi hiyo, hivyo wakaamuru auawe. Kikatumwa kikosi cha watu ishirini kufanya kazi hiyo. Ndani ya siku mbili watu wote hao waliuawa, tena si kwa risasi bali kwa mkono wa Kiroboto huku yeye mwenyewe akifanikiwa kuondoka nchini humo na kiasi kikubwa cha fedha na almasi ambazo alipewa kama zawadi na Rais aliyekuwa madarakani.
Kwa sasa Ben si mtu mwenye shida ya fedha, ila kuna kitu kinausumbua moyo wake, nacho ni kisasi, wala hakuwahi kuchukua kazi nyingine baada ya kupata utajiri ule toka Sierra Lione. Fununu za kuwa Harken Kalm ndio damu pekee iliyobaki toka kwa kingozi yule wa Sierra Lione zilimfikia Ben. Pia hakuchelewa kujua kuwa Harken Kalm alikuwa akifanya biashara haramu, lakini alijiapiza kumlinda kwa namna yoyote ile. Aliona hiyo ndio ingekuwa njia pekee ya yeye kulipa fadhila kwa kiongozi yule aliyempa utajiri alio nao sasa. Kwa siri sana Ben alijitambulisha kwa Harken Kalm, na kumwambia kuwa yupo kama atamuhitaji. Walitambuana. Hivyo simu hii ya kuomba msaada toka kwa Harken Kalm aliichukulia kwa uzito unaotakiwa. Alitamani kujikumbushia michezo yake, ila damu ilimsisimka zaidi alipotambua kuwa mchezo huu utamkutanisha na Jacob Matata na Komandoo Banzi. Ben and Jacob walikuwa miongoni mwa wale vijana waliokwenda Cuba. Wakati yeye alitoroshwa baada ya mafunzo kuisha, Jacob yeye alirejea Tanzania. Si kwamba Ben alikuwa mzuri zaidi ya Jacob, ila kilichomfanya mwalimu wa kichina amchukue Ben ni kwa vile alikuwa katili sana. Hivyo aliona kazi ya kuwa muuaji maalum wa kuajiriwa ingemfaa zaidi. Jacob alikuwa vizuri zaidi kimafunzo ila alikuwa na utu hivyo hakufaa kupelekwa kuwa muuaji.
Kila mmoja alishasikia sifa za mwenzake, Ben alijua kuwa Jacob Matata ni mpelelezi asiyeshindwa, na Jacob alishazisikia sifa za Kiroboto hasa ile habari ya namna alivyotoroka Sierra Lione ilimsisimua sana.
* * *
Huyu yeye anaitwa Gaucho, anamiliki kituo cha kufanyia mazoezi - Gym, maeneo ya Kimara Baruti. Leo hii hakufungua kituo chake. Si kwamba hakupenda kufungua au hakuwa na wateja, la hasha, alikuwa na wateja wengi, na wengi walishampigia kelele kwa nini huwa hafungui siku za Jumamosi. Jumamosi ingekuwa ni siku nzuri kwake kufungua kwa vile watu wengi ndio huwa na nafasi ya kufanya mazoezi, lakini asingeweza kufanya hivyo kwa sababu ya mtu mmoja tu, ndio mtu mmoja, mteja mmoja tu ndiye ambaye alisababisha Gaucho asiwe anafungua kituo chake siku ya Jumamosi.
Mteja huyo alijitambulisha kwa Gaucho kwa jina moja tu, Ben. Siku Ben amekuja ofisini kwa Gaucho hapo kwenye kituo cha mazoezi, alionekana kama mtu aliyepotea njia. Muonekano wake - mavazi, macho, usafi na uongeaji wake vilimfanya Gaucho atake kumuondoa haraka eneo hilo la ofisi yake. Walipoanza maongezi kidogo hali ikawa tofauti.
“Naitwa Ben.....” Sauti nzito iliyo na mikwaruzo ilisema huku macho makali yakiusanifu uso wa Gaucho.
“Sema nikusaidie nini” Gaucho alijibu kwa kukereka kidogo.
“Nahitaji sehemu ya kufanyia mazoezi.....”
“Mazoezi gani unayotaka kufanya wewe, ..na, ..na....unadhani hii sehemu ni muafaka kwako?”
Kabla ya kujibu, Ben aliminya vidole vyake, ule mlio wa vidole kuminywa ulitoka kwa fujo na kisha ukasika mlio huo huo toka miguuni.
“Sikiliza bwana....nani sijui?” Ben alitaka kujua jina.
“We sema tu shida yako” Gaucho akadharau hata kujitambulisha.
“Nataka nitumie kituo chako kwa ajili ya mazoezi, na nikifanya mazoezi sihitaji mtu mwingine awe ndani.... nahitaji kuwa peke yangu siku nzima......”
“Hilo halitawezekana bwana......” Gaucho alimkatisha Ben.
“Ben” Ben alimsaidia Gaucho kukumbuka jina lake.
“ndio Bwana Ben, haiwezekani kufunga kituo kwa ajili yako, yaani niwashe umeme, viyoyozi vyote vifanye kazi na mashine zote ziwe zimewashwa halafu ukumbi wa mazoezi uwe wewe tu Ben, huo ni ukichaa mkubwa.......” Gaucho alitaka kuendelea lakini alikatizwa na Ben.
“Miye nitakulipa mara mbili ya hela ambayo huwa unakusanya kwa siku” Sauti ile nzito yenye mikwaruzo ilitamka na kmfanya Gaucho ashituke kidogo.
“Wewe unaweza kufanya hivyo?” Gaucho aliuliza kwa dhalau.
“Sema ni shilling ngapi?” Ben alisisitiza.
“shillingi laki moja na nusu kwa siku” Gaucho alisema huku akiwa anataka kuinuka maana alijua mwisho wa maongezi yao ulikuwa unafika.
“Basi mie nitakupa laki nne kwa kila siku nitakayokuja kwenye mazoezi” Ben alisema huku akijitengeneza kitini.
Hicho ndicho kilimfanya Gaucho awe tayari kutia pamba masikioni kila wateja wake walipomsihi awe anafungua kituo siku ya Jumamosi.
Gaucho hakuwa anaamini macho yake pale Ben alipokuwa akianza mazoezi. Alikuwa ni kama anayeangalia filamu za wapiganaji wa kichina. Ben alikuwa anabadilika kabisa na kuwa kiumbe mwingine, staili zake za maozezi ya kupigana, kunyanyua vitu vizito na utumiaji wa vifaa ndani ya ukumbi wa mazoezi vilimfanya amuogope sana na kufuta mtazamo aliokuwa nao juu ya Ben. Aliamini huyu Ben kama si Ninja basi ni Komandoo.
Ben mwenyewe alilidhika na hilo, alihitaji siku moja ya mazoezi badala ya kuulaza tu mwili wake nyumbani akiwa anashinda akiangalia filamu mbali mbali. Haikutokea tu Ben akaamua kuanza mazoezi, laah. Ujumbe aliopokea siku nne zilizopita toka kwa Harken Kalm ndio uliomfanya aende kwa Gaucho kuomba kituo cha mazoezi. Ile simu kuwa anatakiwa awamalize Jacob na Banzi ndio iliyomfanya Ben au Kiroboto aanze mazoezi hayo ya kuweka mwili safi.
********
Tofauti na Banzi ambaye aliyepiga simu kwa mzee Harken Kalm, kumtaka pesa, huyu yeye alikuwa amejaa tamaa ya mapenzi. Mapenzi yalimfanya Eve awe katika harakati za siri za kutaka kumtorosha mpelelezi Jacob Matata toka katika himaya hii ya John Kificho. Alikuwa ameshaangalia kila namna ya kufanya lakini hakuwa amefanikiwa. Alikuwa na hakika kuwa siku ambayo angefanikiwa kutoroka katika himaya hiyo akiwa na Jacob Matata basi angeanza maisha mapya na Jacob.
Ni tamaa ya kutaka kumtorosha Jacob ilimfanya atengeneze urafiki na komandoo Banzi. Maana jamaa huyo ndiye aliyemtorosha Regina toka katika jumba la mzee Harken Kalm na ndiye pia aliyemfuata Jacob Matata kumleta katika jumba hili la John Kificho. Kutokana na uwezo alionao katika kupigana, Komandoo Banzi anaheshimiwa sana na John Kificho.
“Mambo Eve?” Banzi alisabahi wakiwa katika sehemu ya kulia chakula ya John Kificho ndani ya jumba hili.
“Poa tua…… nani sijui?”
“Banzi, Komandoo Banzi!”
“Oooh Komandoo!!! Kwa maana ya kufuzu jeshini au wa sifa fulani, maana siku hizi kuna makomandoo wengi?”
“Komandoo wa vyote, maisha, jeshini, shida na……?” Banzi alisita kabla hajaendelea.
“Mbona hujamalizia?” Eve alisahili.
“wa mambo mengi kama nilivyosema!! Ha ha ha ha! Basi” alisema kwa kicheko huku akimuangalia Eve kifuani.
Kimya kilipita kila mmoja akionekana kutafakari yake. Kisha Eve alinyanyua uso wake na kumuangalia Banzi huku akitengeneza nywele zake.
“Huonekani kama wewe ni Komandoo wa chochote kati ya ulivyovitaja!” Eve alichokoza.
“Ungependa kuona alama gani ya ukomandoo?”
“ukomandoo wa jeshi ningetegemea kuona mtu sugu, wa kutisha na mwenye tabia za ajabu ajabu tu, lakini si kama wewe Banzi. Kadhalika ukomandoo wa shida huonekana hata usoni tu japo si rahisi kuelezea lakini huonekana” Eve alieleza kabla ya kuuliza.
“Kwani nini kinakufanya useme wewe ni komandoo wa shida?”
“Kwa sababu nadhani nimefuzu na naendelea kupambana nazo” Banzi alijibu.
“Mmmmmmh, unapambana nazo? Lakini kama umefuzu basi hazikupi shida na ni sehemu tu ya burudani zako!!!!”
“Aha ha ha ha ha tse tse!!!” Wote walicheka.
“Kila mtu ana shida ila kuna mambo yanayosababisha kuwe na utofauti katika kuzikabili.” Eve lisema kwa utulivu huku akimeza funda la juisi aliyokuwa akitelemshia chakula.
“Una maanisha nini?” Banzi alihoji.
“Kuna shida za kujitakia na kuna shida za kusababishiwa” Eve alifafanua.
“Mmmmh, naona u mwalimu mzuri!” Banzi alisifia.
“Kwa nionavyo mimi, shida za kujitakia ni nzuri kulikuo za kusababishiwa”
“Hebu elezea kidogo, maana sioni shida nzuri, shida zote ni mbaya.”
“Hapana kuna shida ambazo hufundisha na shida ambazo zinaua” Eve alizidi fafanua.
“Mmmmmm, naona muda wangu unanitaka kuwa mahali fulani, ila nimependa mada hii, natamani tungepata nafasi ya kuijadili zaidi, naomba pia tujaribu kutafakari tofauti ya shida na changamoto” Banzi alisema huku akinyanyuka. Huu ndio ukawa mwanzo wa mazoea ya Eve na Banzi.
Siku nyingine wakiwa katika mijadala yao kama hii Eve alileta mambo mapya.
“Banzi, hivi una umri gani rafiki yangu?”
“Duuuh, leo naona una mada nyingine mpya, mwezi wa kenda natimiza miaka 39!”
“Hongera sana kwa umri na unaonekana unatunza mwili wako vizuri!”
“Asante, japo nadhani nastahili pole au kupewa tahadhari”
“Kwa nini Banzi?”
“Umri wangu na mambo yangu haviendani?”
“Sijakuelewa”
“Jana nilikuwa naongea na mama yangu ambaye yuko taabani hospitali, alikuwa analalamikia kitendo cha mimi kutokuwa na mke wala watoto, anasema naishi kama ndege”
“Lakini hilo si suala la kukulaumu sana, kwani inawezekana unakamilisha mipango yako ili ufanye hivyo!” Eve alijibu kwa kusisitiza.
“Ingekuwa hivyo nadhani mama asingekuwa ananisema, lakini naweza sema mie ni kama mtu ambaye naishi tu na kutimiza malengo ya watu wengine kama John Kificho” Hapo ndipo mjadala mkali ukazuka wa jinsi watu wengine wanyotumiwa na taaluma za kufikisha malengo ya watu wengine ilhali wao wakiachwa kuwa wahanga wa gharama za mafanikio ya hao watu. Ni mjadala huu ndio uliowafikisha kugundua kuwa Eve na Banzi walikuwa na shida mbili tofauti. Wakati Banzi akiwa na shida ya fedha za kujenga maisha yake, Eve yeye hakuwa na shida ya fedha bali mpenzi. Walivyojiangalia, hakuna ambaye angeweza kuwa jibu la mwenzie, ila jambo moja walikubaliana baada ya mjadala mrefu, nalo ni kuwa kila mtu ana ufunguo wa kuelekea kutatua shida ya mwenzie.
Eve alikuwa na jukumu la kumpa Banzi wazo la kumsaidia kupiga bingo, ili hali Banzi alikuwa na kazi ya kutumia ukomandoo wake kufanikiwa kutekeleza wazo la Eve na kumsaidia Eve.
Eve alikuwa na shida ya kumpata na kummiliki Jacob Matata ilhali komandoo Banzi alitaka kutumia hali iliyopo kujinufaisha kwa kupata fedha nyingi.
“Sikiliza Banzi, mzee Harken Kalm anamtaka Jacob na Regina kwa udi na uvumba, John Kificho anakutegemea katika ulinzi na kutekeleza mipango yake ya siri. John Kificho anakulipa fedha kidogo sana tofauti na kazi unayomfanyia. Fanya kitu! Ila hakikisha nampata Jacob Matata akiwa hai”
“Huo ni mpango mgumu sana ila naona unamanufaa, ngoja nijaribu kubuni vitendo vyake nione utafanyaje kazi” Banzi alisema huku akikuna kichwa kwa tafakari.
* * *
Banzi ni Komandoo kama alivyomuambi Eve, si Komandoo wa kujiita bali ni wa kutunukiwa baada ya kufuzu mafunzo ya juu kabisa yanayomfanya mtu kuitwa jina hilo. Amewahi kufanya kazi nyingi za hatari, japo nyingi zikiwa ni nje ya nchi kama vile Holland, Ugiriki na Cambodia. Kwa sasa hakuna kitu anahitaji zaidi ya pesa, ndo maana serikali ilipomtaka baada ya kuhitimu mafunzo alikataa na kusema atakuwa anafanya kazi binafsi.
Ili kutekeleza mawazo aliyokuwa amepewa na Eve, simu ya kwanza kupiga ilielekea ofisini kwa mzee Harken Kalm, ikimtaka pesa ili apate taarifa za walipo Jacob Matata na Regina. Ni simu hiyo ndio ilimfanya mzee Harken Kalm atume vijana wake watafute wapi alipo mtu aliyepiga hiyo simu bila mafanikio.
Simu ya pili kupiga iliingia moja kwa moja ofisini kwa mkurugenzi wa ofisi fukuzi, Bi. Anita.
“Ennhe niambie habari uliyonayo?” Bi Anita alimuuliza Banzi.
“Ni kuhusu rafiki yangu Jacob Matata, najua alipo, kama hutajari napenda kuwa kwenye oparesheni itakayokwenda kumchukua”
“Banzi! Umesahau kanuni namba nne?”
“Samahani mama si unajua uzee. Kwa hiyo?”
“Cover 9” Alijibu Bi. Anita.
“Assurance?” Banzi alisema.
“asilimia mia!”
Jibu la mwisho ndilo lilimfanya Komandoo Banzi aende posta saa nane na dakika saba usiku ili kuangalia sanduku lake la barua kwa maelekezo toka ofisi fukuzi. Na kweli alikuta karatasi yenye mistari minne tu. “BANZI FANYA MNADA KWA AJILI YA KUFILISI MALI YA MDAIWA JACOB, BANKI ITALIPA SHS 716”. Komandoo Banzi alikunja hiyo karatasi na kuiweka mfukoni. Akaangaza angaza kama anayetafuta sanduku jingine la barua, alipoona namba 716 alifungua kwa kutumia funguo zake malaya na kuweka karatasi nyingine tofauti na ile aliyokuwa amechukua toka sanduku lake.
Aliondoka haraka eneo hilo la kuchukulia barua na kurudi alipokuwa ameegesha gari lake. Aliingia ndani ya gari na kutia moto, lakini gari haikuwaka. Wakati anataka kutafuta nini kimetokea alipigwa na kitu kama nyundo ya kilo tano kichwani akapoteza fahamu papo hapo.
Itaendelea