GENGE
EP34
Of coz nimeshamwambia asubiri kwanza… nafikiri kwenye hizo kodi kuna siri nyingine kubwa,” Madam S akaeleza na Chiba akaitika kwa kutikisa kichwa, “kwa hiyo tunafanyaje?” akamwongezea swali.
“Nipe dakika chache,” Chiba akasema kisha akachukua simu yake na kuwasiliana na mtu mwingine.
* * *
Abigail Andrew, mwaDanada mahiri katika TEHAMA ndani ya kitengo cha siri cha kijasusi cha Israel aliipokea simu ya Chiba. Hakuuliza wala kushangaa, alimfahamu Chiba in and out na alijua mpaka kupiga simu basi kulikuwa na shida kubwa. Aliitazama simu yake, akatabasamu na kutikisa kichwa.
Amekamatika! Akawaza. Binti huyu aliyekuwa akihudumu ndani ya Mossad, shirika la kiintelijensia la Isarel, alikuwa mahiri sana katika Nyanja hiyo. Simu ile haikuongea chochote, akaelewa maana yake nini. Akachukua kitu kama waya na kuiunganisha na kompyuta yake kubwa ofisini hapo, kwa haraka akaifunga ili isiingiliane na mtandao mwingine wowote au kufukuliwa.
“Endelea,” akamwambia kwa lugha ya Kiebrania ambayo Chiba aliifahamu kwa kiasi kikubwa. Maelekezo kadhaa yakafuata na Chiba akaomba msaada wa kufunguliwa zile kodi pamoja na kupata maana zake.
Abigail, akazichukua na kuingiza katika mfumo wao wa utambuzi. Mfumo ulitumiwa na Mossad ulikuwa wa kisasa Zaidi kuliko wowote ule ulimwenguni. Haikuchukua hata dakika kumi kwa mwaDanada huyo kukusanya maelezo na kodi za QR zilizofichwa kwa namba maalumu. Hakuhitaji kujua ndani kuna nini, akazirudisha kwa Chiba mara moja ili kazi iendelee.
Chiba akazipokea taarifa zile ndani ya dakika thelathini tu. Akamshukuru mwaDanada huyo na kutazama kwenye zimu yake maelezo yote.
“Wanasemaje?” Madam akauliza kwa shauku ya kutaka kujua.
“Kazi imeisha mama,”
“Nini?”
“Kazi imeisha… hawa jamaa nafikiri hizi kodi za QR zitakuwa na maelezo Zaidi ngoja niziskani,” Chiba akajibu kisha akachukua zile Quik Response Code, na kuziweka kwenye mfumo wa kompyuta yake. Naam! Siri ikafichuka. Kodi moja kati ya hizo ilitoa maelezo stahiki kuhusu Kibwana Mtokambali, ubadilishwaji wake wa sura mpaka ile aliyoichagua.
“Madam!” Chiba akaita.
“Sema…”
“Haya hapa maajabu ya Mungu,” akachukua kompyuta yake na kuiunganisha na luning kubwa iliyokuwa ofisini hapo.
“Mama yangu! Kibwana huyu huyu?” akauliza.
Kwenye kioo kile ilionekana picha halisi ya Kibwana Mtokambali iliyopigwa miaka ya themanini ikiambatana na maelezo yote kuhusu yeye. Chini yake kulikuwa na maelezo na viambatanisho vya fomu alizojaza kukubali kufanyiwa upasuaji huo. Na sura aliyoichagua mwenyewe ilikuwa pale, jina lake jipya la Mc Tee lilijiandika na kumtambulisha kama raia wa Australia. Vivyo hivyo kwa James Msambamagoya maelezo yake yote yalikamilika, picha yake iliyopigwa miaka ya themanini ilionekana wazi pamoja na ile sura mpya atakayoonekana nayo mara baada ya upasuaji. Alikadhalika, jina lake jipya la Big J lilionekana wazi kabisa akiwa raia wa Mauritius.
Chiba na Madam S wakatazamana.
“Tumemaliza,” Chiba akasema. Madam S akatikisa kichwa kushoto kulia kuashiria kazi bado.
“Sawa, tumepata maelezo na kila utambulisho wao mpya… je yupi yupo Tanzania na yupo wapi, maelezo hayajadadavua…” Madam S akaeleza, “mwite Amata tukutane Shamba haraka iwezekanavyo,” akaamuru.
* * *
Katika ofisi kuu za TSA, Kigamboni, au kama panavyojulikana Shamba, Kamanda Amata alikuwa mbele ya Madam S na Chiba pembeni yake. Picha zile zilizotolewa kwenye lile kabrasha laini ndani ya mkufu wa Barbier zilikuwa mezani. Kamanda Amata alikuwa akiziangalia kwa zamu picha zile.
“Sawa!” akatamka, “hatruna haja ya kwenda India bali Mauritius… hawa jamaa ni mamafia aisee, yaani siri zao wanatembea nazo mwilini. Nikioanisha nay ale makabrasha niliyoyapata katika ile laptop ya Mwanachia kule Lisbon, nahisi sasa tunakaribia kupata mpango kamili,” akaeleza.
Madam S akatikisa kichwa juu chini, “tuna taarifa mbili, Rua Camarante na Saratov…” akasema.
“Yeah, na ukiziangalia, bado kuna vitu zinaficha, nafikiri bado kuna kabrasha lingine,” Amata akasema. Chiba akamkodolea macho TSA 1 kana kwamba hakuelewa kinachosemwa.
“Yaani…” akataka maelezo zaidi.
“Amata, jambo unalolizungumza nafikiri lina ukweli… unakumbuka taarifa ulizopata toka Brussels, zikatusaidia kufika Lisbon, ila kutoka Lisbon kwenda hatua nyingine tumepata tabu kwa sababu kulikuwa na Saratov,” Madam S akaeleza.
“Ndiyo,” Amata na Chiba wakajibu pamoja na kutazamana.
“Baada ya kumbana Dana katupa mwanga wa Saratov, na mzigo ndo huu, sasa hapa bila shaka kumebaki na taarifa mbili muhimu, kati yazo moja ni ya pili kutoka mwisho na nyingine ndo yenye kila kitu…” akaeleza Zaidi.
“Hiki kitendawili chepesi sana, James Msambamagoya, au Big J kwa jina jipya ametambulishwa kama raia wa Mauritius. Ina maana huyu Mtokambali au Mc Tee atakuwa hapa Tanzania… kazi imeisha,” Amata akasema.
Chiba akagonga meza, “inawezekana na vipi kama wametuzungusha tena katika hili wakitegemea kuwa ipo siku tungeweza kupata taarifa hii ili tuiamini na kumbe siyo?” akauliza.
“Negative,” Amata akatamka, “huyu mshenzi Ivan, kwa vyovyote alijuwa kuwa hatutaweza kuifikia hii taarifa, kwa hilo basi, hii ina ukweli,” akasema.
“Ok, kwa hiyo taarifa moja ipo Mauritius?” Madam akauliza.
“Fifty fifty Madam,” Chiba akadakiza.
Ukimya ukatawala kwa jozi la sekunde, watatu hawa, kila mmoja alikuwa akiwaza jambo lake kichwani mwake.
“Dana anahitajika tena?” Amata akatamka.
“Haswaaa!” Chiba akaunga mkono hoja.
“Pamoja na hayo lazima tufanye uchunguzi wa ndani nan je yaani huko Mauritius, na tukijua alipo, Amata, utatekeleza agizo. Nilikupa watu wanne, hujamaliza,” Madam akamwambia. Naye akajibu kwa kutikisa kichwa.
“Niachie mimi…” Amata akajibu huku ananyanyuka kitini.
“Tayari?” Madam akauliza.
“Ndiyo, naenda kumalizia hao wawili…”
“All the best!”
* * *
Kamanda amata aliwasili katika ofisi za jeshi la uhamiaji saa moja baada ya kikao na Madam S. Moja kwa moja akalifikia dawati analolihitaji. Katika dawati hilo kulikuwa na wanadada wawili waliokuwa wakiendelea kuhudumia wateja kwa kupokea simu, na kuwasikiliza ana kwa ana.
“Karibu kaka nikusaidie nini?” akaulizwa.
“Nahitaji kuonana na Lulu,” akamwambia.
Yule mwanadada, akainua simu na kubofya namba kadhaa akaiweka sikioni.
“Kuna mgeni wako, nimruhusu?” akamuuliza mtu wa upande wa pili. Baada ya kupata jibu, akakata ile simu na kumwonesha Amata mlango wa kuingia.
Lulu, mwanausalama mwenye kifuniko katika idara ya uhamiaji ya Tanzania, mara nyingi aliwasaidia TSA katika kazi mbalimbali hasa walipokuwa wakihitaji kujua kuhusu wageni au nani kaingia nchini na nani katoka. Miaka kadhaa nyuma alikuwa akihudumu katika Uwanja wa ndege wa Julius Nyerere na mara hii alihamishiwa katika ofisi za makao makuu, jingo la Wizara ya Mambo ya ndani.
“Waoh! Amata!” Lulu alifurahi kumuona kamanda. Akainuka na kumkumbatia kwa nguvu, “karibu Amata, za siku nyingi…”
“Salama, naona sasa upo kwenye kiyoyozi, umeachana na kelele za ma boeing…”
“Kabisa,”
“Nisipoteze muda nimekuja nina shida,”
“Shidika kaka yangu,”
Kamanda Amata akachukua kadi mmweko na kumpatia msichana huyo, “fungua hiyo nikuoneshe kitu,” akamwambia.
“Mtu kazini?” Lulu akauliza.
“Yap!”
Lulu akaipachika ile kadi kwenye kompyuta yake, sekunde kadhaa ikaonesha picha za watu kama sita hivi.
“Enhe…”
“Huyo mwanaume, huyo mtu mzima…”
“Huyu?” akasogeza panya kwenye picha hiyo.
“Yes!”
“Enhe,”
“Nataka nijue kwenye kumbukumbu zenu za ofisi, mtu huyu yupo hapa nchini?” Amata akauliza. Lulu akafanya mambo yake kwenye mtandao huo takriban dakika tano hivi. Akamgeukia Amata.
“Anaitwa Christopher…” Lulu akasema.
“Christopher?”
“Christopher McTee…” akamalizia. Kamanda Amata akatikisa kichwa juu chini.
Christopher McTee! Amata akawaza. “Maelezo Zaidi…”
“Mzaliwa wa Australia…”
“Sihitaji hayo, nataka kujua yupo hapa nchini?”
“Oooh ok…” Lulu akajibu na kuendelea kuchakata kompyuta yake akizidi kuingia ndani kabisa ya mtandao wa uhamiaji, ambao ni wachache wanaweza kuuingia.
“Alikuja nchini mwaka 1999 mwezi September kupitia uwanja wa ndege wa Kilimanjaro…” Lulu akaeleza. Amata akafungua masikio kusikia zaidi kuhusu mtu huyo. “Sikiliza Lulu, nataka kujua Zaidi kuhusu huyu mtu,” akamwambia.
“Christopher McTee kama nilivyokwambia, alikuja nchini mwaka ’99 kwa nia ya kuwekeza kadiri ya taarifa zilizopo hapa, japo zipo kwa uchache. Viza yake ilikuwa ya kibiashara…” Lulu akaeleza.
“Sawa! Asante sana Lulu… sina zaidi,” Amata akasema na tayari alikuwa keshainuka kutoka kwenye kiti chake.
“Ndo unaenda?”
“Ndiyo… nilichotaka nimepata. Kuna zaidi?” akamuuliza.
“Hakuna…” Lulu akajibu.
“Ok!”
Kamanda Amata akaagana na Lulu na kutoka katika ile ofisi, akateremka ngazi za mlango mkubwa na kulifikia gari lake. Akaingia na kuketi. Akachukua kitabu chake cha kumbukumbu na kuandika mambo kadhaa.
Nitamjua tu, nan itajua yuko wapi! Akajiwazia na kuwasha gari. Akatoka eneo hilo na kuchukua barabara ya Ohio kuitafuta ile ya Ali Hassan Mwinyi mpaka daraja la Salenda. Akautafuta ufukwe wa Coco na kunyoosha na barabara hiyo mpaka Msasani.
Australian Honorary Consulate! Kibao chenye hayo maandishi kikamkaribisha. Amata akaweka vizuri koti lake. Akaitazama ile closed-circuit television camera iliyokuwa mbele yake, juu ya kiambaza cha jengo hilo. Akajiweka tai vizuri, na kuvuta hatua kuelekea katika lango la ofisi hizo. Mbele ya walinzi, akajitambulisha kama afisa uhamiaji na kuruhusiwa kuingia.
Ndani ya ofisi hiyo, Amata akakutana na afisa anayehusika na uhifadhi wa taarifa zote za raia wa nchi hiyo wanaoingia nchini.
“Karibu sana,” akakaribishwa. Amata akaketi kwa utulivu kabisa huku macho yake nay a yule bwana yakiwa yanasomana, yakaelewana.
“Naitwa Mr. Spark,” akajitambualisha na kuonesha kitambulisha chake.
“Karibu sana Mr. Spark. Naitwa Mr. Peterson…naweza kukusaidia …” akamwambia. Amata akaingiaza mkono ndani ya koti, mara hii akatoa picha na si kadi mmweko kama kule kwa Lulu.
“Mwaka 1999, mwezi wa tisa, bwana Christopher McTee aliwasili nchini akitokea Australia. Pasipoti yake na viza vimemtambulisha kama raia wa nchi hiyo. Katika kufanya tafiti juu ya watu wanaoishi nchini kinyume na taratibu, huyu amekuwa mmoja wao. Nimekuja kwenu kujua kama mna taarifa zozote za mtu huyu…” Amata akaeleza.
Peterson, akaichukua ile picha na kuitazama kwa makini, akakusanya yale maelezo na kuingiza kwenye kompyuta yake. Akaitisha taarifa ili kujua chochote juu ya mtu huyo. Dakika sita hivi baadae, akashusha pumzi ndefu na kugeuza kiti chake kumtazama mgeni wake.
“Spark!” akaita. Kamanda Amata akamtazama kwa macho makali yaliyokuwa yakimwambia
‘sema nakusikiliza’.
“Christopher McTee, mwenye surah ii, alikwishakufa. Na hata hapa kwenye mtandao wetu wa utambuzi, imejiandika ‘Deceased’”. Peterson akaeleza.
Kamanda Amata akashusha pumzi ndefu na kujiegemeza kitini.
“Amekufa!” akasema.
“Yeah!”
Peterson akamwonesha na tarehe na mwezi na hospitali gani mtu huyo alipofia. Kamanda Amata akasukuti kwa jozi la sekunde, akili yake ikafanya kazi kwa haraka kidogo. Akamtazama tena yule bwana.
“Sasa … huyu aliyeingia Tanzania mwaka huo ni nani? Hebu tazama pasipoti namba hiyo imekatwa lini?” Amata akauliza.
“Swali lako lipo sawa… tarahe ya kuja kwake, na tarehe za pasipoti zote zimefanyika baada ya kifo chake,” akaeleza. Sasa wote wawili vichwa vikawagonga.
“Huyu bwana kaingia nchini, na hakuna maelezo yoyote kuwa amekwishaondoka… ina maana yupo hapa hapa,” Amata akasema. “Nashukuru sana Mr…”
“Mr. Peterson!”
Kamanda Amata akainuka, kabla hajavuta hatua kutoka akazuiwana kauli.
“Mr Spark, maada nina hii taarifa, nitakujulisha kama nitapata lolote,” akamwambia. Amata akachomoa kadikazi yake na kumpatia. Akaondoka.
Ndani ya gari lake, aliketi kimya kabisa akifikiri nini cha kufanya. Akajikuta akipiga ngumi usukani wa gari hiyo na kutoa tusi la nguoni. Akatia injini moto na kuondoka eneo lile.
* * *
Dakika kama thelathini zilizofuata, Amata akaegesha gari katika makutano ya barabara ya Ohio na Garden. Akateremka na kuliendea jengo mojawapo lililobeba ofisi za ubalozi wa Mauritius. Hapa hapakuwa na maswali mengi kama alikotoka. Akapandisha mpaka ghorofa ya sita na kuzipata ofisi azitakazo. Makaribisho yaliyojawa kila aina ya ukarimu yalimlaki kijana huyo mtanashati pindi tu alipolifikia dawati la mapokezi. Mara baada ya kueleza shida yake, akaongozwa moja kwa moja kwenye ofisi inayohusika na kazi iyo ya kuratibu raia wan chi hiyo wanaoishi nchini.
Hapa alikutana na kijana mwingine mrefu, mwembamba mwenye kichwa kisicho na nywele.
“Karibu bwana…” akamkaribisha kwa Kiswahili.
“Asante sana, nimekaribia,” Amata akajibu na kisha wote wakaketi baada ya kusalimiana.
“Naitwa Mr. Spark,” akajitambulisha na kumpa mkono yule bwana.
“Karibu sana Mr. Spark… naitwa Hamadou Hassan,” naye akajitambulisha kisha wote wakaketi chini.
“Yes Mr…”
“Mr. Spark,” Amata akamalizia.
“…naweza kukusaidia?”
“Ndiyo Mr Hamadou… nimekuja kutoka Wizara ya mambo ya nje, mimi ni afisa uhusiano wa Wizara,” akaeleza. Akatoa kitambulisho kingine na kumwonesha. Yule bwana akakitazama na kutikisa kichwa. Akamrudishia. Kamanda Amata akatoa picha nyingine na kumuwekea mezani yile bwana.
“Utanisamehe, wizara inahitaji kumtambua huyu mtu raia wa Mauritius ambaye ameomba ajira katika ofisi zetu pale. Kabla ya kumpa jibu lake, tunapenda kujiridhisha kuhusu yeye,” Amata akamwambia. Uongo mtupu. Hamadou akaichukua ile picha na kuitazama, kisha akamtazama Amata.
“Jina lake…”
“Aimer Jonathan,”
Yule bwana akaingiza yale majina kwenye kompyuta yake na kusubiri kidogo. Kama dakika tatu hizi akaanza kuandika tena vitu kadhaa kwenye kompyuta hiyo. Dakika chache zilizofuata, akainua simu na kupiga moja kwa moja Mauritius kuuliza taarifa za mtu huyo. Baada ya kuongea na mtu wa upande wa pili, takribani dakika tano hivi, akakata simu na kumgeukia Amata.
“Mr. Spark… kuna utata wa mtu unayehitaji taarifa zake. Kwanza tumepata watu wengi sana wenye jina kama hilo katika Mouritius. Wamefikia watu sitini na tisa. Lakini katika hao wote hakuna anayeoana na picha hii,” akaeleza. Amata akaonesha mshituko bandia.
“Inawezekanaje?”
“Hapa kuna mambo mengi sasa, inawezekana ameghushi taarifa na si mtu wa Mauritius,”
“Na ndiyo maana nikaja hapa kuhakikisha kwa kuwa haya mambo ya kidiplomasia, tusije kuingia kwenye matatizo ya kimahusiano baina ya nchi na nchi kwa kuajiri jasusi la nchi nyingine,”
“Haswaaa hapo sasa panatufanya na sisi kumtafuta huyu mtu…” Hamadou akamwambia Amata. Wakiwa bado katika mazungumzo hayo ile simu ikaita.
“Samahani…” Hamadou akamtaka radhi Amata na kuinyakuwa ile simu. Dakika mbili zilizofuata akaitua na kumrudia tena Amata.
“Unaona bwana,” akatulia kidogo, baadae nukushi ikaingia, akachomoa lile karatasi na kumpatia Amata.
Alipoipokea, akaisoma. Karatasi ile ilimweleza mtu mwenye picha hiyo kuwa ni Farouk AlFakry, raia wa Djibout na isitoshe tayari amekwishakufa miaka mitano ilopita.
“Asante kwa taarifa hii. Naomba niifikishe panapohusika halafu sisi na ninyi tutaona la kufanya,” Amata akamwambia Hamadou, wakaagana na kuachiana kadi kazi zao.
Mara baada ya mazungumzo yale, Kamanda Amata akashika njia mpaka kwenye gari lake. Akaingia na kuketi nyuma ya usukani. Akaitazama ile picha na ile ya kwake. Zinashahabiana kwa asilimia tisini na tisa.
Washenzi wamejificha nyuma ya sura za marehemu! Akawaza. Kisha akaziweka kwenye kiti cha kando yake. Akawasha gari na kuondoka.
* * *
ITAENDELEA