BRING BACK OUR GIRLS
SEHEMU YA 39
ILIPOISHIA SEHEMU ILIYOPITA
Ninawashukuru viongozi wa mataifa ya Afrka na wawakilishi wao kwa kukubali mwaliko wetu..Nawashukuru vile vile wageni wote kutoka Marekani,Karibean,Afrika na kwingineko kote duniani kwa kufika nchini kwetu.
Ninamshukuru kwa namna ya pekee kabisa mke wa rais wa Marekani Bi Gwen pring kwa kuja kutuunga mkono katika mkutano huu.Ninawashukuru pia viongozi mbali mbali waliokuja kuungana nasi kutoka katika serikali ya Marekani.Tunamshukuru raisi wa marekani kwa kuwatuma kuja kuungana nasi hapa.”
Hivi ndivyo alivyoianza hotuba yake mheshimiwa rais wa jamhuri ya muungano wa Tanzania akiwakaribisha viongozi wa mataifa na wageni mbali mbali waliohudhuria mkutano huu mkubwa wa Sullivan
ENDELEA…………………….
Ilikuwa ni hotuba ndefu iliyosheheni mambo mengi kuhusiana na Tanzania na mkutano ule kwa ujumla.
Wakati hotuba ya ufunguzi ya mheshimiwa rais ikiendelea katika jumba la kifahari la Sultani kikao kilikuwa kinaendelea.Mbele yao kulikuwa na runinga kubwa ambayo pembeni yake alisimama Abdulkhareem
“ Ndugu zangu leo tunafanya kikao cha mwisho.Yawezekana tusiwe na kikao kama hiki tena au tusionane tena .Lolote linaweza kutokea hapo kesho.Japokuwa mpaka hivi sasa tuna uhakika mkubwa kwamba bado tunayo nafasi kubwa ya kuweza kuutekeleza mpango wetu kwa ufanisi lakini hatuwezi kupingana na ukweli kwamba lolote linaweza kutokea .kwa maana hiyo basi kila mmoja wetu anatakiwa ajizatiti ipasavyo na afahamu kwamba kosa moja atakaloweza kulifanya litaweza kuuvuruga mpango huu wote ulioandaliwa kwa muda mrefu na kugharimu fedha nyingi” Akasema Abdulkhareem na kuwatazama wenzake waliokuwa kimya wakimsikiliza
“ Siku ya kesho ni siku muhimu na kubwa sana kwetu,ni siku ambayo naweza kuiita takatifu kwetu.Siku ambayo tutapeleka vilio duniani na hasa Marekani.Ni siku ambayo itaingia katika historia ya dunia kama ile ya September 11 ambayo hadi leo bado wamarekani wanakumbuka kilichotokea.Siku ya kesho kiongozi wetru ataachiwa huru.Nguvu ya Alshabaab itaonekana kesho” Akasema tena Abdulkhareem
“Nadhani kila mmoja wetu anafahamu nafasi yake na wajibu wake lakini pamoja na hayo sina budi kuwakumbusha tena nini tunapaswa kukifanya siku ya kesho.kama nilivyosema hapo awali kwamba sitaki kosa lolote litokee.” Akasema Abdulkhareem na kuiwasha runinga ile kubwa halafu ikatokea picha kubwa ya ramani ya jengo la KICC
“ Hii ni ramani ya jengo la KICC unamofanyika mkutano wa Sulivan.Kwa timu itakayo kuwapo pale KICC nadhani nyote tayari mnavyo vitambulisho vyenu vya kuwaruhusu kuingia mle ndani kama waandishi wa habari wa vyombo vya nje.Baada ya kuingia ndani kila moja atashika nafasi yake na wakati kikao kikiendelea Jamal ambaye ndiye mtu wetu tuliyemuweka pale ukumbini atawapeleka katika chumba cha sri ambako kumefichwa silaha zote mtakazozitumia .Mtachukua silaha na kukaa tayari na mara tu mtakapopata taarifa toka kwetu kwamba ni muda wa kuuteka ukumbi mtafanya hivyo haraka sana.Nafikiri tumekwisha fanya mazoezi ya kutosha kuhusiana na namna ukumbi utakavyotekwa ndani ya muda mfupi sana na kuwaweka watu wote mikononi mwetu lengo letu likiwa ni raia wa kutoka Marekani kwani kesho asubuhi kwa mujibu wa ratiba kuna majadiliano kuhusu ushiriki wa marekani katika masuala ya Afrika kwa hiyo nina imani wamarekani wote watakuwa hapo ukumbini.Baada ya kuuteka ukumbi mtafuata maelekezo yetu nini cha kufanya.Wakati wote huo tutakuwa tukiendelea kuwasilana.
Kutekwa kwa ukumbi wa KICC kutatanguliwa na kutekwa kwa wasichana wa shule ambao miongoni mwao atakuwemo mtoto wa rais na waziri mkuu.Hakutakuwa na huruma hata kidogo na laziam damu imwagike kesho ili kumpata kiongozi wetu.Baada ya wasichana kutekwa na ukumbi wa KICC kuwekwa chini ya ulinzi wetu,litafuata shambulio lingine katika hospitali ya Mount Meru .Hili ni shambulio la kibaolojia.Kirusi H5 kitaachiwa na kwa mara ya kwanza kitaleta maangamizi makubwa.Katika mipango ya awali tulipanga tuachie kirusi hiki katika hospitali mbili lakini tumebadili mpango na sasa tutakiachia katika hospitali moja tu ya Mount Meru.Watu wengi watapoteza maisha na baada ya hapo ndipo tutakaporusha video yetu tukitaka mkuu wetu aachiwe huru na na ili kuwatisha zaidi tutaanza kuwachinja wanafunzi tutakaokuwa tukiwashikilia.Nina hakika kwa mtikisiko huu serikaliya Tanzania itamuachiahuru kiongozi wetu.Nimeona niwakumbushe tu kwa mara nyingine tena kuhusu majukumu yetu ya hapo kesho. Vile vile tutumie kikao hiki kuagana kwani kwa wengine yawezekana tusionane tena lakini kumbukeni kwamba yeyote atakayepoteza maisha kesho atakuwa amekufa kishujaa na atakumbukwa na vizazi vyetu vyote” Akasema Abdulkhareem halafu wakaendelea na majadiliano mengine kuhusiana na siku ya kesho.
********************
Saa mbili za asubuhi ,jiji la Arusha lilikuwa katika heka heka kubwa.Geti kubwa la kuingilia jengo la KICC unamofanyika mkutano wa Sullivan lilionekana kuwa na vurugu zilizosababishwa na watu waliokuwa na vitambulisho maalum vya kuhudhuria mkutano ule ,kutaka kuingia pasi na kufuata utaratibu.Askari polisi walijitahidi kutuliza hali ile na watu wakatii amri wakaanza kuingia ndani kwa utaratibu bila kufanya vurugu.Wakati watu wakiendelea kuingia kupitia mlango mkuu geti la kusini lilitumika kwa ajili ya wageni waliotoka nje ya nchi.Mabasi maalum yaliyowabeba wageni toka katika mahoteli waliyofikia yaliendelea kuwasili.Mbali na mabasi hayo ,kulikuwa pia na magari mengine madogo yaliyokuwa yamekodishwa kwa ajili ya kutumiwa na wageni maalum ambao hawakutaka kupanda mabasi ya jumla. Geti la kaskazini liliwekwa maalum kwa ajili ya waandishi wa habari waliokuwa wakiingia na kutoka.Kulikuwa na ukaguzi mkali sana katika mageti yote .Kila aliyepita na kila gari lililoingia lilikaguliwa kwa vifaa maalum vya ukaguzi ili kuzuia watu wasiingie na silaha au kitu chochote cha hatari ndani ya ukumbi ule.Lango la mashariki lilitumiwa na viongozi wa kitaifa na wale wa kutoka mataifa mbali mbali.Kwa ujumla hali ya usalama ilikuwa ya kiwango cha juu sana mahala hapa.
Saa tatu za asubuhi rais wa jamhuri ya muungano wa Tanzania akawasili .Tayari viongozi karibu wote wa mataifa mbali mbali walikwisha wasili akiwemo mke wa rais wa Marekani ambaye aliongozana na mwenyeji wake mke wa rais wa Tanzania.
Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania akaingia ukumbini na kufungua rasmi kikao cha kwanza cha majadiliano kuhusu nafasi ya Marekani katika maendeleo ya afrika.Baada ya kufungua kikao kile mheshimiwa rais akaelekea katika ghorofa ya tatu ambako kulikuwa kunafanyika kikao cha pamoja kati ya wakuu wa nchi za afrika waliohudhuria mkutano huu na wafanya bashara wakubwa wa Marekani wenye asili ya afrika waliohitaji kuzijua fursa za uwekezaji zinazopatikana barani afrika.
Katika lango la kaskazini lililokuwa maalum kwa kupita waandishi wa habari,gari nyeupe aina ya Toyota VX ikawasili na kusimamishwa na walinzi kwa ajili ya ukaguzi.Kama ilivyokuwa taratibu,wote waliokuwa ndani ya ile gari walishuka kisha gari likaingizwa katika banda maalum lenye mitambo ya ukaguzi na likaonekana kuwa salama.
Wakati gari likiendelea kukaguliwa,waandishi wale nao walipita katika mtambo maalum wa ukaguzi.kamera pamoja na vifaa vingine vyote walivyokuwa navyo waandishi wale vilikaguliwa na hakukuonekana tatizo lolote wakaruhusiwa kuendelea na safari yao.Wakiongozwa na Jabir Hassan Jabir ambaye kitambulisho chake kilionyesha kwamba ni mwandishi wa habari wa kituo kimoja cha yelevisheni nchini Misri waliegesha gari katika maegesho na kushuka ,wakaingia ukumbini.Hakuna aliyefahamu kama wale hawakuwa waandishi wa habari bali magaidi.Wakati wakiendelea kuziweka sawa kamera zao akatokea mtu mmoja ambaye ni mwangalizi mkuu wa umeme katika jengo lile ,akasalimiana na Jabir kwa kupeana mikono na kumuachia vitu fulani mkononi kama vispika vidogo vya masikioni.Jabir akachukua kimoja na kukiweka sikioni halafu akawagawia na wenzake ambao nao wote waliviweka masikioni mwao.Kilikuwa ni kitendo cha haraka na wepesi mkubwa kiasi kwamba hakuna mtu aliyegundua wala kuhisi chochote.
Baada ya kumaliza kuziweka sawa kamera zao ,jabir akabonyeza kidude fulani katika kamera yake na taa ndogo nyekundu ikawaka halafu ikabadilika na kuwa ya kijani , akalipiga piga sikio lake kisha akasema kwa sauti ndogo
“ Tuko tayari”
“ Kazi nzuri sana jabir tumewapata vyema.Kaeni tayari na kusubiri maelekezo” ikasema sauti ya Abdulkhareem ambaye ndiye aliyekuwa akiongoza zoezi zima akitokea katika jumba la kifahari la Sultani.Mbele yao kulikuwa na runinga kubwa iliyokuwa ikonyesha kila kilichokuwa kinaendelea katika ukumbi wa KICC kupitia kamera za akina Jabir ambazo ziliunganishwa na kifaa fulani cha kielektroniki cha kurushia mawasiliano ambacho kilifungwa katika chumba cha siri kabisa bila ya mtu yeyote kufahamu.Kifaa hiki ndicho kilichowawezesha akina Jabir kuwasiliana na akina Abdul bila matatizo.
Mara tu baada ya kupokea taarifa toka kwa Jabir,Abdul akawasiliana na mtu ambaye alikwenda katika hospitali ya mkoa ya Mount Meru, akiwa na kirusi hatari cha H5 ambacho angekiachia mara tu atakapopewa maelekezo.Mtu yule aliyetumwa pale hospitali alimhakikishia Abdul kwamba hakukuwa na tatizo lolote na alichokuwa anakisubiri ni maelekezo toka ofisi kuu. Baada ya kujua hali ilivyo pale Mount Meru hospital,Abdul akawasiliana na timu nyingine iliyoko katika duka kubwa la kuuza bidhaa mbali mbali za kitalii na kiutamaduni sehemu ambayo mke wa rais wa Marekani pamojana mke war as wa jamhuri ya muungano wa Tanzania walitegemea kutembelea siku hiyo.Katika sehemu zote tatu ambazo walipanga kufanya mashambulizi hakukuwa na tatizo lolote na vijana walikwisha jipanga wakisubiri maelekezo.
“ Mpaka dakika hii kila kitu kimekwenda vizuri na hakuna tatizo lolote katika sehemu zote tatu.” Akasema Abdul huku akitazama saa kubwa ya ukutani ambayo ilizidi kusogeza mishale.Katika chumba kile kikubwa walikuwepo pia Sultani ,Safia pamoja na vijana watatu wataalamu sana wa mambo ya teknohama .Kazi yao kubwa ilikuwa ni kuhakikisha kwamba mawasilio kati ya sehemu zote tatu na ofisi kuu yanapatikana wakati wote.
Saa nne na dakika tatu wasichana zaidi ya Arobaini wa shule moja ya wasichana iliyoko nje ya jiji la wakiongozwa na mtoto wa rais wa jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakaelekea katika duka la kuuza bidhaa za kiutamaduni na utalii nje kidogo ya jiji la Arusha.
“ Msafara wa wasichana unaondoka kuelekea Kisongo” Hamidi akatuma taarifa kwa akina Sultani.Hamidi ni mtu ambaye alipandikizwa katika ukumbi huu wa KICC na mtandao wa Alshabaab na ambaye ndiye aliyefanikisha kwa kiasi kikubwa mpango mzima wa magaidi kuingia mle ukumbni.Akiwa kama fundi mkuu wa umeme wa jengo lile ,Hamidi alitumia nafasi hiyo kupenyeza silaha na kuzificha katika chumba chenye mitambo ya umeme chumba ambacho hakuna mtu mwingine asiyehusika anaruhusiwa kuingia..
“ Tumekusoma Hamidi.kazi nzuri.Tutarudi tena kwenu mara tu watakapofika Kisongo” akasema abdul akitokea ofisi kuu halafu akawasiliana na timu iliyokuwa Kisongo na kuwataarifu kwamba tayari msafara ulianza safari ya kuelekea kule kwa hiyo wajiweke tayari.
Iliwachukua dakika kama kumi na tano hivi kuwasili katika duka lile kubwa lililosheni bidhaa lukuki.Lango la kuingilia lilikuwa wazi na askari wa usalama barabarani aliyekuwapo pale akayaongoza magari na kuyaelekeza sehemu ya kuegesha na kisha wasichana wale wakashuka .Kitu cha kwanza walichokutana nacho na kuwafurahisha ni sanamu ya kuchonga ya morani wa kabila la masai akipambana na simba.Wasichana wale walionekana kufurahi sana ubunifu ule.Kijana ambaye kazi yake ni kupokea wageni katika duka lile ,aliwaelezea kwa ufupi maana ya sanamu ile ,maelezo ambayo yaliwafurahisha sana wasichana wale.Baada ya maelezo yale yaliyozifanya nyuzo zao zibaki na tabasamu wakaingia ndani ya duka ..Walizunguka sehemu mbali mbali za jengo lile na kushuhudia vitu mbali mbali vya kuvutia.Wakati wakiendelea na kutazama vitu vile ,kijana muongoza wageni aliwaeleza kuhusu kuwapo kwa sanamu kubwa ya mjusi mkubwa aliyewahi kuishi katika sehemu fulani ya Tanzania miaka mingi iliyopita,sanamu iliyotengenezwa na ustadi mkubwa mno.Wote walitamani kuiona sanamu hiyo.Kijana yule akawaongoza hadi katika chumba kikubwa kilichokuwa na sanamu ile kubwa.Wakati wakishangaa sanamu ile ya aina yake iliyofanana kwa kila kitu na mjusi yule mkubwa ghafla milango ikajifunga na taa zikazimika kukawa na kiza totoro.Wote wakapigwa na butwaa wasijue kumetokea nini ,walidhani labda ni hitilafu ya umeme. Mara moja hewa fulani kama moshi ikatoka mle ndani ya ile sanamu kubwa na wote waliokuwa mle chumbani wakaanza kuanguka mmoja baada ya mwingine.
TUKUTANE SEHEMU IJAYO……………………….