Riwaya: Bring back our girls

Riwaya: Bring back our girls

BRING BACK OUR GIRLS

SEHEMU YA 34

ILIPOISHIA SEHEMU ILIYOPITA
“Nashukuru sana Ithan .Umenisaidia sana.Naanza kuwa na matumaini ya kutoka humu gerezani.” Akasema Tonny kwa furaha huku akimpa Ithan mkono.
“Tonny nimeomba nifunguliwe geti mara moja ili niweze kukupa taarifa hizo ambazo nina imani ni za muhimu sana kwako na vile vile nimeona nikuletee keki hii.Tafadhali naomba uile keki hii mara moja ili mkaguzi akipita asiweze kuikuta kwani inaweza kuniweka matatani.Si ruhusa kuingiza gerezani vitu kama hivi bila kibali maalum cha mkuu wa gereza.” Ithan akasema na kumkabidhi Tonny boksi lile lenye ile keki nzuri.
“Ni muda mrefu sana sijaona vitu vizuri kama hivi.Ithan nashuru sana kwa kunikumbuka “.Akasema Tonny huku akiimega keki ile kwa mkono wake wa kulia.
“kazi nzuri Ithan,endelea kukaa hapo hapo mpaka atakapomaliza kuila hiyo keki” Rahim akamweleza Ithan kupitia kile chombo maalum walichokuwa wakikitumia kuwasiliana. Ithan moyo ukamwenda mbio ,jasho jembamba likamtoka.
" Ouh Mungu wangu Tonny anakwenda kufa akila hii keki..Nitafanya nini mimi wakati wameizuia familia yangu? Mungu atanisamehe sana kwa kosa hili lakini ni kwa ajili ya kuiokoa familia yangu." akawaza Ithan


ENDELEA......................


Ngumi nzito iliyoupiga mkono wa Tonny ilimfanya aiachie keki aliyokuwa ameishika mkononi ikaanguka chini na kwa haraka Ithan akaikanyaga kwa mguu wake.Tonny alibaki ameduwaa kwa kitendo kile alichokifanya Ithan .Wakati akiwa katika mshangao ni kwa nini Ithan alifanya kitendo kile kwa kasi ya aina yake akavutwa mkono na kupelekwa hadi korido la chumba cha pemBeni ambacho hakikuwa na kamera ya ulinzi.Ithan jasho lilikuwa likimtiririka na kwa mbali macho yake yalikuwa yamelengwa na machozi.
“ Ithan nini kimetokea? Mbona sielewi kumetokea kitu gani? Tonny akauliza akiwa bado na mshangao.Ithan hakujibu kitu akaegemeza kichwa chake ukutani.Machozi yalikuwa yakimtoka.Tonny akamsogelea na kumshika mabega akamuuliza
“Ithan niambie kuna tatizo gani? Umenishangaza mno kwa kitendo ulichokifanya” Tonny akasema.Ithan aliendelea kulia kwa kwikwi.Ghafla akaingiza kidole sikioni na kukitoa kifaa kilichokuwa kimewekwa sikioni kwake kwa ajili ya kuwasiliana na akina Rahim akakitupa chini na kukikanyaga kanyaga kwa hasira. Tonny akabaki amesimama akimuangalia asielewe nini kilichokuwa kimetokea.Ithan akasimama ameshika kiuno chake huku akihema kwa hasira.Tonny akamsogelea na kumshika mkono
“Ithan niambie una tatizo gani? Nini kimetokea?
Huku akifuta machozi Ithan akasema
“Tonny ! familia yangu……familia yangu” akasema kwa uchungu mwingi
“Familia yako imefanya nini?
“Tonny familia yangu inakwenda kuuliwa…familia yangu inateketezwa…ouh Rebecka mke wangu…..” Ithan akachuchumaa na kuinama chini akilia
Tonny akamuangalia kwa makini sana na kisha akainama na kuuinua uso wa Ithan
“Ithan tafadhali naomba futa machozi na unieleze ni kitu gani kimekutokea.Nieleze familia yako imefanya nini ?
Ithan akafuta machozi akamtazama Tonny na kusema
“Tonny nimeshindwa kutekeleza walivyonituma.Familia yangu yote inakwenda kuuawa”
“Ithan hebu njoo huku” Tonny akamshka mkono na kumvuta ili warudi katika ile seli ya Tonny
“hapana Tonny.Tusiende huko wananiona katika kamera” Akasema Ithan na kuzidi kumduwaza Tonny
“Ok Ithan nakuomba uvute pumzi ndefu na uwe huru” Tonny akamweleza Ithan huku akimsaidia kuirejesha akili yake katika hali yake ya kawaida.
“Good.You are ok now.Just calm down …ok…ok..Good..sasa naomba unieleze kwa ufasaha nini kimetokea.Ni nani wanaokutazama katika kamera na familia yako imefanya nini? Tonny akamwambia Ithan ambaye akavuta pumzi ndefu na kusema
“Jana usiku nikiwa nyumbani nilivamiwa na watu ambao siwafahamu.Watu hao waliokuwa wamezifunika nyuso zao walinichukua mimi na familia yangu na kutupeleka mahala ambako sipafahamu ni wapi.Tulipelekwa katika jumba moja kubwa,mimi nikatenganishwa na mke wangu na mwanangu.Mtu mmoja ambaye alijitambulisha kwangu kama Rahim ambaye kwa muonekano wake ana asili ya kiarabu alianza kunihoji maswali kuhusiana na barua ile uliyonituma jana..”
Tonny aliposikia kuhusu barua ile akahisi kama baridi ikimuingia mwilini.Akahisi nywele zikimsisimka
“Walikuuliza maswali gani kuhusiana na barua ile niliyokupa?
“Rahim ambaye aliyeonekana ndiye mkubwa wao alitaka kujua kwamba ujumbe ule ulihusu nini,nikamwambia kwamba sijui ujumbe ule ulihusu nini kwa sababu sikuelewa lugha iliyokuwa imeandikwa katika ule ujumbe.Akaniuliza tena kama kuna maagizo yoyote ulinipatia tofauti na ile barua nikamwambia kwamba hukunipa maagizo yoyote yale na halafu akataka kufahamu kama kuna mtu mwingine yeyote ambaye nilimweleza kuhusiana na ujumbe ule nikamwambia kwamba hakuna mtu mwingine niliyemweleza kwa sababu ujumbe ule sikuuelewa na haukuwa na maana yoyote kwangu.Baada ya kuridhika na majibu niliyompa,Rahim akaniambia kwamba nisiwe na wasi wasi kwa sababu yeye hana tatizo na mimi ila dhumuni la kuniteka mimi na familia yangu ni kwa sababu wanataka niwafanyie kazi yao ndogo na kisha wataniacha huru mimi na familia yangu.” Ithan akanyamaza kidogo akameza mate.Tonny damu ilikuwa ikimchemka kwa maelezo aliyoyapata toka kwa Ithan.
“Alinitaka leo hii niingie kazini.Nikamweleza kwamba leo hii ni siku yangu ya mapumziko lakini akasema kwamba kama ninaijali familia yangu ni lazima niingie kazini ili niweze kuwafanyia hiyo kazi yao.Akaniuliza ni nani ambaye anaingia kazini badala yangu siku ya leo nikamwaeleza ni Frank.Akaniuliza kama ninapafahamu mahala anapoishi frank nikamwambia ndiyo napafahamu akanipakia katika gari na kuelekea nyumbani kwa Frank ambaye walimchukua na kwenda kumfungia katika jumba lao na kisha wakaanza kunielekeza kazi wanavyotaka niifanye hiyo .Rahim alinieleza kwamba ujumbe ule ambao ulinituma niupelekea katika zile ofisi ulikuwa ni hatari sana kwao na ulikuwa na lengo la kuutibua mpango wao mzima ambao hakunieleza ni mpango gani.Akanieleza kwamba nikifika leo asubihi niende katika chumba cha mitambo ya kamera kisha niunganishe chombo Fulani na kukiwasha na baada ya hapo nije kwako na nikupe ile keki halafu nisubiri kama dakika tano kisha nitoke na baada ya hapo familia yangu ingeachiwa huru.Leo asubuhi nilikuja nao na hivi unavyoongea wameegesha gari lao mita chache toka hapa gerezani.Sikioni waliniwekea chombo hicho nilichokiharibu haribu ili kuwasiliana nami.Kwa kuwa bado kulikuwa na giza giza sikuweza kuzisoma namba za lile gari.Niliingia kazini na kufanya kama walivyotaka .Nikiwa na silaha nikawaweka chini ya ulinzi askari waliokuwa katika chumba cha kamera na kuwafunga mikono na miguu kwa waya na kisha kuwafungia katika chumba kidogo na baada ya hapo nikaunganisha vile vifaa walivyonipa ambavyo viliunganisha moja kwa moja kamera za hapa gerezani na mtandao wao na hivyo wakawa wakiangalia kila kitu kilichokuwa kikiendelea hapa gerezani.Baada ya kamera za gereza kuunganishwa na mtandao wao wakaniamuru nije katika chumba chako na wakalifungua geti na hata maswali uliyoniuliza walikuwa wakinielekeza majibu ya kukupa.Keki ile ambayo walisema nikupe ilikuwa na sumu kali sana ambayo ingekuua baada ya muda mfupi .Nilikuwa nimedhamiria kufanya vile kwa ajili ya kuiokoa familia yangu lakini mawazo yakanijia kwamba wewe ni mtu muhimu sana kwa taifa na hukustahili kufa bila kosa lolote.Sikuona tena sababu ya wewe kufa kwa sababu kama ungekufa basi hakuna mtu ambaye angeweza kuwafahamu watu hawa na kuwazuia jambo wanalotaka kulifanya.Watu wale si watu wazuri hata kidogo kwani wana kila namna ya silaha na mitambo ya kisasa inayotumia teknolojia ya hali ya juu sana.Kuna kitu ambacho wanataka kukifanya ambacho si kitu kizuri kwa nchi yetu na unayekifahamu kitu hicho ni wewe pekee na ndiyo maana wameamua kukuua kwa gharama yoyote ile..Baada ya kuwaza mambo hayo ikanilazimu kuiweka familia yangu nyuma na kuyaweka maslahiya wengi mbele .Nilipata picha kwamba hata kama nikitekeleza kila kitu walichonituma kamwe hawataweza kuniacha mimi na familia yangu hai.hivyo nikaamua kuiweka kando familia yangu na kukuokoa usife ili uweze kutafuta namna ya kuwafichua watu hawa.Ninasikitika sana kwa sababu baada ya kushindwa kutekeleza kazi waliyonipa niifanye ,najua tayari familia yangu itakuwa imeangamizwa……” Ithan akashindwa kuvumilia akangusha machozi.Tonny akavuta pumzi ndefu na kusema
“Nyamaza kulia Ithan.Ulifaya vizuri sana.You are so brave.Ahsante sana kwa uzalendo huo mkubwa ulio nao kwa taifa lako.Nashukuru sana kwa kuyaokoa maisha yangu. Bila wewe hivi sasa ingekuwa marehemu.Katika maisha yangu sintakusahau kwa hilo” Tonny akamwambia Ithan huku akimpiga piga mgongoni ili kumpa moyo
“Tonny nasikitika sana familia yangu yote inakwenda kuteketezwa.” Akasema Ithan kwa uchungu mkubwa
“Ithan nakuomba tafadhali usihofu kuhusu hilo.Ulichokifanya ni kitu kikubwa sana kwa nchi hii na siku moja watanzania watakukumbuka.Sasa naomba nikuulize mambo machache .Ile barua niliyokupa ulimkabidhi nani?
“Niliipeleka katika zile ofisi ulizonielekeza,nikaambiwa kwamba mkurugenzi hayupo hivyo kama nina ujumbe wowote niuache pale getini ambako kulikuwa na askari wawili waliokuwa wamevalia mashati meupe na suruali za bluu.kwa hiyo sina uhakika kama ujumbe ule ulimfikia mhusika ama vipi”
Taa nyekundu ikawaka kichwani mwa Tonny akafikiri kidogo na kisha akasema
“hao jamaa umesema kwamba waliegesha gari lao mita chache kutoka hapa gerezani?
“Ndiyo Tonny.Walikuwa si mbali sana na hapa gerezani.”
“Ok nimekuelwa Ithan.Usiwe na wasi wasi kuhusu familia yako.Ninachokihitaji kwa sasa ni ushirikiano wako ili tuweze kuiokoa familia yako angali mapema.Ninachokitaka kwa sasa naomba ukimbie ukamuite mkuu wa gereza haraka sana uje naye hapa.Baada ya hapo nitakueleza nini cha kufanya” Tonny akamwambia Ithan ambaye bila ubishi akaanza kukimbia kuelekea katika ofisi ya mkuu wa gereza.kabla hajafika mbali Tonny akamuita
“Ithan mbona umesahau bunduki yako?
Ithan akarudi akaichukua bunduki yake na kisha akatoka mbio kuelekea katika ofisi ya mkuu wa gereza.Tonny alibaki amesimama akivuja jasho
“mambo yameanza.Monica alikuwa sahihi kabisa kwamba kuna jambo zito litatokea katika mkutano huu wa Sullivan kule Arusha.Kinachoniumiza akilini kwamba watu hawa wamejuaje kwamba kuna ujumbe nimeutuma katika ofisi zetu? Nina wasi wasi ni lazima kuna mtu ambaye wanamtumia katika kupata taarifa katika ofisi zetu.Nafahamu namna mitandao ya kigaidi na kijasusi inavyofanya kazi zao.Ili waweze kutekeleza shambulio lao ni lazima wawe na taarifa za kutosha na za mara kwa mara za kiusalama .Ni lazima watakuwa wamemuweka wakala wao pale ili kuwapatia taarifa muhimu.kama ni hivyo idara yetu si mahala pa kuaminika tena.Kwa muda mrefu nimekaa humu gerezani na sikuwa tena na hamu ya kutaka kujiingiza katika namna yoyote ile ya shughuli za usalama wa nchi.Lakini kinachonisikitisha ni kwamba kila ninavyojitahidi kutokujiingiza tena katika mambo haya ya kijasusi najikuta nashindwa na siwezi kuyakimbia tena majukumu yangu kwa nchi yangu japokuwa sithaminiki hata kidogo.Itanilazimu kurudi tena kwa mara nyingine katika uwanja wa mapambano na kuweza kuiokoa nchi yangu dhidi ya mashambulio ya hawa magaidi.Swali gumu ni kwamba nitawezaje kufanya hivyo hali nimefungwa humu gerezani? Jibu lake ni jepesi kwamba sintaweza kabisa kufanya jambo lolote lile kuzuia shambulio hilo lisitokee. Pamoja na yote waliyonifanyia ikiwa ni pamoja na kunitelekeza gerezani lakini najisikia kama nina wajibu mkubwa wa kuweza kulizuia shambulio hili.Nitajitahidi kwa kadiri nitakavyoweza kwanza kuiokoa familia ya Ithan ambaye ameyaokoa maisha yangu na pili kuwatia nguvuni watekaji hao ambao watatusaidia katika kulizima shambulio lolote kutokea.” Tonny akastuliwa kutoka katika mawazo mengi na watu wawili walioingia kwa kasi mahala alipokuwa amejificha ili asiweze kuonekana na kamera za ulinzi.
“Kitu gani kimetokea hapa? Mbona Tonny yuko hapa badala ya kuwepo katika seli yake? Nani kaufungua mlango wa chumba cha Tonny? Salvatory Mpimwe mkuu wa gereza la Uwangwa akauliza maswali mfululizo huku naye akishangaa
“Afande,kilichotokea ni kitu chenye kuhitaji maelezo marefu kidogo.Kama hutajali tunaweza kwenda kuongelea ofisini kwako? Tonny akasema na kumfanya Salvatory kuhamaki akamgeukia Ithan na kusema kwa ukali
“Ithan kuna kitu gani kimetokea hapa.Nini kinaendelea hapa? Ni kwa nini Tonny yuko nje ya chumba chake?
“Afande kuna mambo yametokea ambayo unapaswa kuyafahamu” Ithan akasema kwa kutetemeka.
“Afande tafadhali naomba unipe nafasi niweze kukuelezea na kukufafanulia kwa kina “ Tonny akasisitiza.
“Ithan tafadhali naomba mrudishe Tonny chumbani kwake haraka sana.Umefanya kosa kubwa mno kumuacha mfungwa kama Tonny akae hapa nje bila aina yoyote ya ulinzi.Kwa kosa hili unastahili adhabu kali sana.”
“Afande……………..” Ithan akataka kuongea jambo lakini tayari Salvatory alikuwa amekwisha ghafirika.
“Sitaki kusikia chochote kutoka kwako Ithan.Umenifuata na kunieleza kwamba kuna tatizo kubwa katika seli ya Tonny.Nimefika mwenyewe mpaka hapa lakini hakuna tatizo lolote na umemuacha Tonny akiwa huru kitu ambacho ni hatari sana .Kwa hili sintaweza kukusamehe hata kidogo Ithan,.Umevunja taratibu za gereza na nitahakikisha unapata adhabu kali sana” Salvatory akatamka kwa ukali huku Ithan akimshika mkono Tonny na kuanza kumrudisha katika seli yake Tonny akausukuma kwa nguvu mkono wa Ithan na kisha akapiga hatua kumsogelea Salvatory ambaye alianza kuingiwa na wasi wasi akaitoa bastora yake.

USIKOSE SEHEMU IJAYO………………………..
 
BRING BACK OUR GIRLS

SEHEMU YA 35

ILIPOISHIA SEHEMU ILIYOPITA
“Ithan kuna kitu gani kimetokea hapa.Nini kinaendelea hapa? Ni kwa nini Tonny yuko nje ya chumba chake?
“Afande kuna mambo yametokea ambayo unapaswa kuyafahamu” Ithan akasema kwa kutetemeka.
“Afande tafadhali naomba unipe nafasi niweze kukuelezea na kukufafanulia kwa kina “ Tonny akasisitiza.
“Ithan tafadhali naomba mrudishe Tonny chumbani kwake haraka sana.Umefanya kosa kubwa mno kumuacha mfungwa kama Tonny akae hapa nje bila aina yoyote ya ulinzi.Kwa kosa hili unastahili adhabu kali sana.”
“Afande……………..” Ithan akataka kuongea jambo lakini tayari Salvatory alikuwa amekwisha ghafirika.
“Sitaki kusikia chochote kutoka kwako Ithan.Umenifuata na kunieleza kwamba kuna tatizo kubwa katika seli ya Tonny.Nimefika mwenyewe mpaka hapa lakini hakuna tatizo lolote na umemuacha Tonny akiwa huru kitu ambacho ni hatari sana .Kwa hili sintaweza kukusamehe hata kidogo Ithan,.Umevunja taratibu za gereza na nitahakikisha unapata adhabu kali sana” Salvatory akatamka kwa ukali huku Ithan akimshika mkono Tonny na kuanza kumrudisha katika seli yake Tonny akausukuma kwa nguvu mkono wa Ithan na kisha akapiga hatua kumsogelea Salvatory ambaye alianza kuingiwa na wasi wasi akaitoa bastora yake.

ENDELEA…………………………….

“tafadhali Tonny naomba usinisogelee ama sivyo nitakupiga risasi”akaonya Salvatory.Alionyesha uoga wa dhahiri
“Ithan nimekwambia mrudishe Tonny ndani mara moja ,na kama huwezi nitaita askari wengine wa kuifanya hiyo kazi” akasema kwa ukali Salvatory
“Huna haja ya kuninyooshea bastora Mr Salvatory.Mimi si mtu mbaya kama unavyofikiri na wala sina nia ya kutoroka au kufanya jambo lolote baya.Kama ningekuwa ninahitaji kutoroka humu gerezani ningekwisha toroka hapa gerezani muda mrefu sana.Hakuna ulinzi wa kunizuia mimi kutoroka.Niko hapa gerezani kwa sababu sioni sababu ya kutoroka .Nitakaa hapa mpaka siku ambayo walioniweka humu wataamua kwa hiari yao wenyewe kunitoa.Kwa maana hiyo kuwa na amani Mr Salvatory ,weka bastora yako mfukoni na unisikilize kile ninachotaka kukueleza.” Tonny akasema na kumuangalia Mr Salvatory kwa makini.
“tafadhali naomba unisikilize Mr Salvatory.Ninalotaka kukueleza ni jambo kubwa sana kwako na kwa taifa zima.” Tonny akasisitiza.salvatory akafikiri na taratibu akaushusha chini mkono wake uliokuwa na bastora .
“Ahsante sana Mr Salvatory,sasa naomba unisikilze kwa makini.” Tonny akamweleza Salvatory aliyekuwa akihema kwa nguvu.
“Askari wako Ithan yuko katika matatizo makubwa sasa hivi.Hivi tunavyoongea familia yake yote imetekwa ikiwa ni pamoja na askari wako aitwaye Frank ambao kama hakutakuwa na juhudi zozote za kuwaokoa basi muda si mrefu toka sasa watauawa.Tunatakiwa kufanya kila juhudi ili kuweza kuwaokoa” Tonny akasema na kumfaya Salvatory astuke kidogo.
“Unasema nini Tonny mbona sikuelewi?
“Mr Salvatory ,juzi nilimtuma Ithan anisaidie kupeleka barua katika ofisi zetu.Ilikuwa ni barua niliyomuandikia mkurugenzi wetu.Kwa bahati mbaya barua ile iliangukia katika mikono isiyo salama .Jana usiku Ithan na familia yake wamevamiwa na kutekwa wakapelekwa mahala ambako hakujulikani .Ithan alipewa kazi ya kufanya ambayo ukamilifu wake ndio ungepelekea familia yake kuwa salama.Kwa kuwa leo haikuwa zamu ya Ithan kuingia kazini iliwalazimu watekaji hao kumteka pia Frank mtu ambayealitakiwa kuingia kazini leo badala ya Ithan na hivyo kumfanya Ithan kuingia badala ya Frank.Kazi waliyompa ya kwanza ni kwenda katika chumba cha kuongozea kamera na kuweka vyombo ambavyo vingeunganisha kamera za hapa gerezani na mtandao wao hivyo wangeweza kuona kila linaloendelea hapa gerezani.Baada ya hapo walimtaka Ithan anipatie keki ambayo ilikuwa imefungwa vizuri ambayo ndani yake mlikuwa na sumu kali ambayo ingeniua baada ya muda wa dakika tano tu.Ithan ameniokoa nisife baada ya kunizuia kuila keki ile Ameamua kuyaweka rehani maisha ya familia yake kwa manufaa ya Taifa.Kwa maana hiyo bila kupoteza muda kuna mambo mawili ya kufanya.Jambo la kwanza ni kuwazuia watekaji hao wasiendelee kumiliki na kuziongoza kamera za ulinzi za hapa gerezani.jambo la pili ni kuwatafuta na kuwakamata kwa sababu hawako mbali na hapa gerezani” Akasema Tonny
Mr salvatory alikuwa akitetemeka midomo .Alishindwa aseme kitu gani
“Mr Salvatory suala hili ni zito sana na ninaomba tafadhali tushirikiane sote katika kulitatua.Naomba uniamini na tushirikiane.Nimekuwa jasusi wa kutumainiwa na nchi hii kwa muda mrefu na ninaomba tafadhali uniamini na uutumie ujuzi na uzoefu wangu kwa siku hii ya leo ili kuweza kulitatua jambo hili kwa haraka” Tonny akamwambia Salvatory ambaye akamtazama kwa makini na kisha akasema.
“Unashauri tufanye kitu gani?
“Kitu cha kwanza ni kama nilivyokwambia kwamba tunatakiwa tuawazuie hawa jamaa wasiendelee kuunganishwa na kamera zetu Kwa sasa bado wanaendelea kufuatilia kila kitu kinachofanyika hapa gerezani .Hii ni hatari sana kwa usalama wa gereza.Hauwezi kujua wana lengo gani lingine” Tonny akasema na kumfanya Salvatory ainame akafikiri kidogo na kusema
“Tonny umenilazimisha nikuamini .kwa mara ya kwanza ninavunja sheria ya gereza na ninakuomba tusaidiane ili tuweze kulitatua jambo hili ambalo ni la hatari kwetu sote.”
Kwa kasi wakakimbia kuelekea katika chumba cha kuongozea kamera za ulinzi.Askari walikuwa wakiwashangaa na kujiuliza kumetokea kitu gani kwani halikuwa jambo la kawaida kuwahi kutokea..
Haraka haraka wakaufungua mlango wa chumba cha kamera ,Ithan akawaonyesha vifaa alivyokuwa ameviweka.Tonny akavichomoa na kurudisha kila kitu kama kilivyokuwa awali.Wakati Tonny akiendelea na kurudisha mambo yake sawa Ithan alikuwa akiwafungua wale jamaa aliokuwa amewafungia katika chumba kidogo.
“Ithan kwa hili sintaweza kukusamehe hata kidogo” Akasema Salvatory wakati akishuhudia Ithan akiwafungua wenzake nyaya walizokuwa wamefungwa mikononi na miguuni.Kwa haraka akaagiza gari la wagonjwa lifike pale na kuwachukua askari wale na kuwapeleka katika zahanati ya gereza kwa huduma ya kwanza na kuwatibu majeraha.
“Afande kila kitu kiko shwari hapa na hawawezi tena kuunganishwa na kompyuta zenu.”
“Umejaribu kujua ni akina nani hao? Salvatory akauliza
“Ni jambo ambalo litachukua muda kulifanyia uchunguzi kwa sababu watu hawa ni wataalamu na mambo yao wanayafanya kwa umakini mkubwa.Unachotakiwa kufanya kwa sasa naomba uwasiliane na kituo cha polisi Kigamboni ili waweze kukizuia kivuko na kulifunga daraja kwa muda ili watu hawa wasiweze kuvuka ng’ambo ya pili na hivyo kuweza kuwanasa.Afande na askari wako tukiongozwa na Ithan twendeni tukawafuate hao jamaa mahala walikoegesha gari lao”
“Tonny hiyo si kazi yetu.Ni kazi ya jeshi la polisi.Tuwataarifu na kuwaacha waifanye kazi yao”
“Salvatory kwa sasa hii ni kazi yetu sisi.Hatuna muda wa kulisubiri jeshi la polisi.Chukua vijana wako wenye silaha tunakwenda kuwakabili hao jamaa kabla hawajaondoka mahala walipo” Tonny akasema na Salvatory akakubaliana na mawazo yake akaagiza vijana nane wenye silaha na kwa haraka wakaingia garini wakaondoka kuelekea mahala ambako akina Rahim walikuwa wameegesha gari.
“Gari lao lilikuwa limeegeshwa hapa.Tayari wameshaondoka” Ithan akasema kwa kukata tamaa.
“Una uhakika ni hapa walipokuwa wamesimamisha gari? Akauliza Tonny
“Nina uhakika ni hapa.Alama za matairi hizi hapa bado zipo” akasema Ithan akiwaonyesha akina Tonny alama za matairi ya gari la akina Rahim
“Salvatory wasiliana na askari polisi wa hapa kigamboni na uwaeleze waendelee kufanya uchunguzi wa eneo lote la Kigamboni kuanzia sasa hivi ili kuona kama wanaweza wakalipata gari hilo japokuwa sina uhakika sana kwa sababu jamaa hawa wanafanya mambo yao kwa umakini mkubwa sana.”
Salvatory akawasiliana na jeshi la polisi kigamboni na kuwaomba wafanye msako wa kulitafuta gari hilo kisha wao wakarejea gerezani.
“Tonny vipi kuhusu familia yangu? Ithan akauliza huku akilengwa lengwa na machozi
“Ithan usife moyo .Familia yako itakuwa salama.naomba uniamini.Tutafanya kila juhudi ili kweza kuikomboa familia yako pamoja na afande frank.”Tonny akasema.
“Tumewakosa watu hawa , nini kinafuata baada ya hapa Tonny? Kwa nini tusiwakabidhi jeshi la polisi ili waifanye kazi hii ya kuwasaka hao jamaa? Salvatory akamwambia Tonny.
“hapana Mr Salvatory.Suala hili ni suala pana sana tofauti na unavyoliona kwa sasa.Ninaomba nikaongee nawe ofisini kwako tafadhali “ Akasema Tonny wakiwa ndani ya gari wakirejea gerezani.
Baada ya kushuka garini Salvatory akaamuru Ithan awekwe chini ya ulinzi na apelekwe katika seli maalum kwa ajili ya askari.Kwa haraka akafungwa pingu na kuanza kupelekwa katika seli .Alimuangalia Tonny kwa uchungu mwingi..
“It’s ok Ithan.Naomba uniamini kwamba nitaikomboa familia yako” Tonny akamwambia Ithan ambaye alikuwa ameonyehsa dalili za kukata tamaa
“Tonny naomba ufanye kila uwezalo kama ulivyoahidi ili uweze kuiokoa familia yangu.Nimeyaokoa maisha yako naomba uisaidie familia yangu” Ithan akasema kwa uchungu huku akiongozwa na askari wenzake kwenda katika seli .Tonny na Salvatory wakaingia ofisini
“Tonny samahani kuhusu Ithan lakini sina namna nyingine ya kufanya zaidi ya kufuata sheria.Jambo alilolifanya ni jambo la hatari kubwa sana na ambalo lingeweza kuleta madhara makubwa hapa gerezani.Hapa gerezani kuna wafungwa wengi wakiwemo wafungwa wanaotuhumiwa kwa makosa mbali mbali ya kivita toka nchi mbali mbali kwa hiyo kwa kuwaacha hao jamaa waziongoze kamera zetu za ulinzi ilikuwa ni kuwapa nafasi waufahamu mfumo mzima wa gereza na kuna hatari wangeweza hata kuwatorosha watuhumiwa.Jambo hili ni zito sana na linaloweza kutuletea matatizo sisi sote.Lazima Ithan ashikiriwe kwanza wakati ninaangalia nini nifanye cha haraka ikiwa ni pamoja na kubadili mfumo mzima wa kamera na ulinzi kwa ujumla.” salvatory akasema akiwa ameegemea kiti chake cha ofisini.Jasho likimtoka .
“Salvatory ninachoweza kukisema ni kwamba ,ni kweli Ithan alifanya makosa lakini kwa mtu yeyote yule angekuwa katika nafasi yake angefanya kama alivyofanya Ithan.Sina lengo la kutetea jambo alilolifanya Ithan lakini sina budi kumshukuru kwa kuyaokoa maisha yangu.Aliamua kuiweka familia yake pemBeni kwa ajili ya maslahi ya taifa.Naomba tafadhali kama kuna lolote unaloweza kumsaidia ili asiweze kupata adhabu kali naomba umsaidie kijana huyu ambaye bado familia yake inashikiliwa na watekaji tusiowafahamu.” Tonny akamwambia Salvatory
“Nitaangalia nini cha kufanya “ akajibu Salvatory
“nafurahi kusikia hivyo Mr salvatory.Sasa naomba unisikilize kwa makini.Nimefanya kazi katika idara ya ujasusi kwa muda mrefu sana.Nimefanya mambo mengi makubwa ambayo hakuna mtu anayekumbuka leo hii na badala yake nimeachwa niozee gerezani.Nikiwa hapa gerezani nilipata taarifa za kuwepo kwa mpango wa kutokea shambulio la kigaidi katika mkutano wa Sulivan unaoanza kesho jijini Arusha.Kwa kulipa uzito suala hilo niliandika barua na kumpa Ithan ampelekee mkurugenzi wangu Mr Meshack Jumbo”
“Tonny naona huna taarifa.Mr Meshack Jumbo alikwisha staafu kazi muda mrefu.Kwa sasa idara ya ujasusi ina mkurugenzi mpya mwanamama ambaye silifahamu jina lake” Salvatory akamfahamisha Tonny na kumfanya abaki mdomo wazi
‘Ndiyo maana mambo yamekuwa hivi…….” Akasema Tonny huku akisikitika
“Ok tuachane na hayo.Katika barua ile niliyompa Ithan aipeleke katika ofisi zetu nilikuwa nimetoa angalizo kwamba kunaweza kutokea shambulio la kigaidi katika mkutano wa Sullivan.Sina hakika kama barua ile ilimfikia mkurugenzi wetu lakini kuna mtu ndani ya idara anayetumiwa na watu hawa ambaye aliwapa taarifa kwamba kuna barua imetumwa kutoka kwangu.Hii ndiyo sababu iliyopelekea Ithan atafutwe na kulazimishwa afanye vile alivyofanya leo.Wamekwisha fahamu kwamba kuna jambo ninalijua kuhusu mpango wao hivyo wakaona njia bora ni kuniua.Mr Salvatory suala hili ni suala zito kwa sababu linahusu usalama wa taifa.Tuna kila sababu ya kunganisha nguvu ili tuweze kuzuia shambulio hili lisitokee.” Tonny akasema na kumtazama Salvatory ambaye alikuwa amezama katika mawazo mengi
“Tonny suala hii ni suala zito sana kama unavyosema .Bado ninarejea ile kauli yangu niliyokwambia mwanzo kwamba kwa nini tusilikabidhi suala hili kwa jeshi la polisi? Wao wana mtandao mkubwa nchi nzima na wanaweza wakaifanya kazi hii kwa ukamilifu mkubwa.Sisi wawili hatuwezi kupambana na magaidi.”
“Mr Salvatory nakuomba unisikilize kwa makini.Suala hili ni suala nyeti sana na ambalo haliwezi kutangazwa kwa kila mtu.Huwezi kufahamu nani wa kumuamini kwa sasa.Hata katika idara za serikali watu hawa wana mawakala wao ambao huwapa taarifa za kiusalama.Kulipeleka suala hili katika jeshi la polisi ni kuharibu kila kitu.Lengo hapa ni kuzuia shambulio na kuwakamata magaidi na ndiyo maana suala kama hili linatakiwa lishughulikiwe na vyombo vinavyohusika na vyenye wataalamu waliopata mafunzo ya kukabiliana na ugaidi..Mr salvatory naomba tafadhali uniamini na unipe nafasi ya kuweza kulifanyia kazi suala hili.Masuala kama haya yanayohusu usalama wa nchi mara nyingi huwa yanakuwa ni siri kubwa na hii ndiyo sababu niko hapa gerezani sasa hivi kwa sababu nilikuwa nikifahamu jambo zito linalohusiana na usalama wa nchi na sikuliweka wazi kwa vyombo vya usalama. “ Tonny akamweleza Salvatory ambaye alimuangalia kwa makini na kusema
“Tonny nimekuelewa lengo lako.Unaposema nikupe nafasi una maana nikuachie huru .Siwezi katu kufanya jambo kama hilo.Hata kukaa nawe hapa nimefanya kosa kubwa sana.Nimevunja sheria kukutoa katika seli yako na kukaa nawe hapa.Ni kosa kubwa na kama wakuu wangu wakilifahamu ni lazima nichukuliwe hatua kali sana za kinidhamu.Naomba tafadhali tusiendelee na mjadala wa kuhusu suala hili kama huafikiani nami kuhusu kulifikisha suala hili katika jeshi la polisi.Jeshi la polisi ndicho chombo pekee ambacho kinaweza kulishughulikia suala hili kwa ukamilifu.Unaponiambia kwamba tusiitaarifu polisi unanifanya nisiamini kuhusu jambo uliloniambia na badala yake unanifanya niamini kwamba ilikuwa ni moja ya janja yako ya kutaka kutoka gerezani.”
“Mr salvatory naomba tafadhali uniamini ninayokueleza ni ukweli mtupu .Suala hili ni suala zito sana na linalohitaji umakini wa aina yake.Si kwamba siliamini jeshi la polisi lakini naomba ufahamu kwamba tofauti na idara yetu ambayo ina watu wenye mafunzo maalum ya kupambana na ugaidi hakuna idara inayoweza kulishughulikia suala hili kikamilifu” akasema Tonny
“Tonny naona hakuna jambo la maana la kuongea mimi na wewe tena.Kwa sasa utarejea katika seli yako .Ahsante kwa msaada wako uliotusaidia “
“Mr Salvatory tafadhali usifanye hivyo.Nipe nafasi nilishughulikie suala hili.Mamia ya watu watakufa kama suala hili lisipozuiwa.Ninakuahidi kwamba sintatoka nje ya gereza hili .Nina watu wangu ambao nina imani kwa maelekezo yangu wataifanya kazi hii kwa ufanisi na kuzuia shambulio lolote lisitokee .naomba uniamini Salvatory” Tonny akasisitiza
“Tonny we’re done here.Muda wa mchezo umekwisha sasa ni muda wa kazi” akasema kwa ukali Salvatory huku akipiga simu na mara wakaingia polisi wanne wenye silaha wakamfunga pingu Tonny na kumuongoza kurudi katika seli yake.
“Salvatory kama huniamini naomba basi unipe walau nafasi niweze kufanya mikakati ya kuiokoa familia ya Ithan .Nilimuahidi kuwa nitahakikisha familia yake inakuwa salama”
“Tonny kila kitu kitashughulikiwa na jeshi la polisi.” Salvatory akasema kwa ukali huku akiinama na kukishika kichwa chake.Alikuwa na mawazo mengi mno.
" Umefanya kosa kubwa sana Salvatory ..utaikumbuka siku hii ya leo" akasema Tonny lakini Salvatory hakumuangalia tena.
Tonny akarudishwa katika seli yake na kwa mara nyingine kusudio lake la kutaka kulizuia shambulio la kigaidi lisitokee likagonga ukuta.Alisikia uchungu moyoni kwa kutoitimiza ahadi yake aliyompa Ithan kwamba atahakikisha familia yake inakuwa salama.

USIKOSE SEHEMU IJAYO...................
 
BRING BACK OUR GIRLS

SEHEMU YA 36

ILIPOISHIA SEHEMU ILIYOPITA
“Tonny we’re done here.Muda wa mchezo umekwisha sasa ni muda wa kazi” akasema kwa ukali Salvatory huku akipiga simu na mara wakaingia polisi wanne wenye silaha wakamfunga pingu Tonny na kumuongoza kurudi katika seli yake.
“Salvatory kama huniamini naomba basi unipe walau nafasi niweze kufanya mikakati ya kuiokoa familia ya Ithan .Nilimuahidi kuwa nitahakikisha familia yake inakuwa salama”
“Tonny kila kitu kitashughulikiwa na jeshi la polisi.” Salvatory akasema kwa ukali huku akiinama na kukishika kichwa chake.Alikuwa na mawazo mengi mno.
" Umefanya kosa kubwa sana Salvatory ..utaikumbuka siku hii ya leo" akasema Tonny lakini Salvatory hakumuangalia tena.
Tonny akarudishwa katika seli yake na kwa mara nyingine kusudio lake la kutaka kulizuia shambulio la kigaidi lisitokee likagonga ukuta.Alisikia uchungu moyoni kwa kutoitimiza ahadi yake aliyompa Ithan kwamba atahakikisha familia yake inakuwa salama.

ENDELEA..............................................

Baada ya Ithan kushuka katika gari la akina Rahim na kuanza kupiga hatua kuelekea gerezani Rahim na timu yake wakageuza gari na kuvuka ng’ambo ya pili ya bahari.Hawakutaka kukaa karibu na gereza lile kwa sababu walikuwa na wasi wasi kwamba lolote linaweza likatokea hivyo ikawalazimu kuchukua tahadhari mapema.Wakiwa katika ng’ambo ya bahari waliweza kumfuatilia Ithan kupitia mitambo yao iliyokuwa katika lile gari.
Ithan alipoingia katika chumba cha Tonny na kumkabidhi keki , walilitazama tukio hilo katika runinga kubwa iliyokuwamo garini na kila mmoja akabaki kimya akisubiri Tonny ale ile keki
“C’mon Tonny eat that cake” Rahim akanong’ona akiwa ameuweka mkono wake mdomoni .Ghafla kikatokea kitu ambacho hawakuwa wamekitegemea kama kingetokea.Ithan aliupiga ngumi mkono wa Tonny uliokuwa umeishika ile keki na kwa kasi ya ajabu Ithan akamvuta Tonny kutoka katika kile chumba na hakuweza tena kuonekana katika kamera.
“bastard !!! Rahim akasema kwa hasiara huku akiipiga meza kwa mkono wake
“Ithan umefanya nini tena? Rahim akauliza kwa ukali
“Ithan….Ithan…Itha…………..” Rahim akaendelea kuita lakini ghalfa mawasiliano yakakatika.
Huku akitweta kwa hasira akavua spika za masikioni alizokuwa amevaa akazitupa mezani.
" Bastard !!!!..." akafoka Rahim
“Rahim tunafanya nini sasa ..? akauliza mmoja wa vijana wake
Rahim akafuta jasho lililoanza kumtirrika usoni na kusema
“Sielewi tunafanya nini tena.Ithan amebadili maamuzi.Ameamua kumuokoa Tonny asife.Nina uhakika atamueleza Tonny kila kitu na hiyo inaweza ikasababisha kuanza msako mkali wa kututafuta.” Akasema Rahim huku akihema kwa kasi.
“Jamal ,funga kila kitu tulichokiunganisha na kamera zao kule gerezani tuondoke zetu haraka sana hapa.Muda si mrefu wataanza kutusaka.” Akaamuru Rahim na kwa haraka vijana wake wakaanza kazi ya kufunga kila kitu .Baada ya dakika tano kila kitu kikawa tayari na Rahim akamuamuru dereva kuliondoa gari haraka.
“Sikutegemea kama Ithan angeweza kufanya kitendo cha namna hii.” Rahim akasema .Alihisi kuchanganyikiwa.Akaitoa simu yake na kuwapigia wakuu wake jijini Arusha.
“Hallo Rahim.Nipe taarifa za maendeleo.Kazi imekwenda vizuri? Akauliza Sultan.
Rahim akasita kidogo kuongea .Hakujua aseme kitu gani
“Rahim nini kinaendelea huko ? Zoezi la kumuua Tonny limekamilika? Akauliza tena Sultan
“ Sultan …aah….” Rahim akashindwa kuongea.
“Rahim kuna tatizo gani? Akauliza Sultan kwa ukali kidogo
“Sultan..kuna tatizo limetokea.Zoezi lile limeshindikana.” Akasema Rahim kwa sauti ya upole.
“Zoezi limeshindkana? C’mon Rahim how could that happen? Sultan akauliza kwa mshangao
“Kila kitu kilienda kama tulivyokuwa tumepanga na Ithan akafanikiwa kuingia gerezani na akafanya kila tulichokuwa tumemuelekeza .Tulikuwa tukifuatilia kila jambo alilokuwa akilifanya Ithan pale gerezani.Tulihakikisha amempa Tonny keki ile yenye sumu lakini kitu cha kushangaza kilichotokea ni kwamba kabla Tonny hajaitia mdomoni keki ile Ithan alimuwahi akaupiga mkono uliokuwa umeishika ile keki ikaanguka chini na kisha akamtoa Tonny mle chumbani na baada ya hapo mawasiliano na Ithan yakakatika.Hakuweza tena kuonekana katika kamera.Kwa ajili ya usalama wetu ,tumeamua kuondoka eneo tulilokuwa tumejificha.I’m sorry Sultan,I failed you “ rahim akasema na kisha kikapita kimya kifupi.
“Nimekuelewa Rahim.Inaonekana Ithan aliamua kuzuia Tonny asife kwa sababu maalum.Inaonekana alikwisha gundua kwamba hata kama angetekeleza kila kitu mlichomtaka atekeleze,isingekuwa rahisi kumuacha huru na ndiyo maana akaamua kuiacha familia yake na kuamua kumuokoa Tonny.Kwa kuwa alichagua kumuokoa Tonny badala ya familia yake ni wazi atamueleza kila kitu kilichokuwa kimetokea.kwa maana hiyo wanaweza wakaanzisha uchunguzi kuhusiana na suala hilo.Kwa kutegemea suala kama hilo linaweza kutokea mnatakiwa mfanye hivi,msiwafanye lolote familia ya Ithan kwa sasa.Lengo la kuwafanya hivyo ni ili kulifanya jeshi la polisi kuelekeza nguvu zake katika kuitafuta familia ya Ithan na kutupa sisi wasaa wa kutekeleza shughuli yetu hapa Arusha bila vikwazo.Suala hili badi halinipi shida kwa sababu mtandao wetu ni mkubwa na kila kitu kimepangwa kwa umakini mkubwa sana.Kwa hiyo endeleeni kuishikilia familia ya Ithan hadi hapo baadae mtakapopata maelekezo mengine.Kwa sasa msifanye kazi yoyote ile ila kaeni tayari tayari kwani muda wowote inaweza ikatokea kazi ya kufanya “ Sultan akamwambia Rahim na kukata simu.

**************************

Tonny alikuwa ameketi kitandani baada ya kurudishwa katika seli yake.Jasho lilikuwa likimtiririka.Akasimama na kuzunguka zunguka mle chumbani akakaa tena kitandani
“Nimeponea tundu la sindano.Bila Ithan ningekuwa nimekwisha fariki muda mrefu.Kwa sasa ninaamini kweli kuna jambo linakwenda kutokea Arusha.Watu hawa tayari wana mtu wao katika idara yetu ya ujasusi na ndiyo maana kwa haraka hivi tayari wanataarifa kwamba ninafahamu mpango wao na ndiyo maana walifanya juu chini ili waniue.Kinachoniuma ni kwamba ninafahamu kinachokwenda kutokea huko Arusha lakini sina namna ya kufanya kuweza kulizuia shambulio hilo nikiwa humu gerezani.Serikali niliyoitumikia kwa muda mrefu na kwa uadilifu mkubwa hainitambui tena.Viongozi wangu kwa sababu wanazozijua wao wenyewe waliamua kunitelekeza hapa gerezani.Ninaozea hapa gerezani bila msaada wowote na sielewi nitatoka lini .Kama nisingekuwa nimefanyiwa hivi walivyonifanyia ningeweza kutafuta namna ya kuweza kulizuia shambulio hili lisitokee lakini kila nikikumbuka jinsi nilivyotelekezwa humu gerezani najikuta sina tena hamu ya kufanya jambo lolote lile .” Akawaza Tonny kisha akainama akaitazama keki ile iliyoletwa na Ithan ambayo ilikuwa na sumu
“Ithan ameyaokoa maisha yangu leo.Nasikitika kwa sababu sina uwezo wa kuweza kumsaidia kuiokoa familia yake ambayo inashikiliwa na hawa magaidi.Baada ya Ithan kushindwa kutimiza matakwa yao hawatakuwa na manufaa na familia yake hivyo watawatekeza wote.Inauma sana lakini sina namna ya kufanya kuzuia hilo lisitokee.”
Wakati akiwaza hayo mara mlango ukafunguliwa na akaingia mkuu wa gereza Mr Salvatory akiwa na maafisa wanne wa polisi.Watau kati yao walikuwa na wamevaa sare na mmoja hakuwa amevaa sare
“Tonny hawa ni maafisa toka jeshi la polisi ambao wamekuja kuchukua maelezo yako kuhusiana na tukio lililotokea leo.Watakuuliza maswali machache kuhusiana na kilichotokea leo.Naomba uwape ushirikiano mzuri ili kwa pamoja tuweze kusaidia kuiokoa familia ya Ithan” akasema Salvatory .
“Bwana Tonny ,tumepata taarifa kutoka kwa askari magereza ajulikanaye kwa jina la Ithan akidai kwamba ulimtuma apeleke barua katika ofisi ambazo ulikuwa ukifanya kazi kabla hujawekwa humu gerezani.” Akauliza afisa wa kwanza ambaye alikuwa na cheo cha mkaguzi wa polisi.
Tonny akawaangalia maafisa wale kwa zamu na kusema
“Ndiyo nilimtuma”
“Unaweza ukatueleza ujumbe huo uliomtuma ulihusu nini?
Tonny akafikiri na kusema
“Niliwaandikia ujumbe ule kuwakumbusha kwamba washughulikie suala langu kwani miaka inazidi kwenda na sielewi ni lini nitatoka gerezani.” Akadanganya .Salvatory akamuangalia kwa macho makali ya mshangao
“Una hakika hicho ndicho ulichokiandika Tonny? Akauliza Salvatory hukuakimkazia macho
“Ndiyo Mr Salvatory .Hicho ndicho nilichokiandika” akasisitiza Tonny
“Jana usiku watu wasiojulikana wamemvamia Ithan nyumbani kwake na kumteka yeye na familia yake na kuwapeleka mahala kusikojulikana na kisha wakamuamuru Ithan aingie kazini na ili familia yake iwe huru alitakiwa kutekeleza yale yote watakayomuamuru.Kwa ajili ya kuiokoa familia yake ilimlazimu kufanya kila walichomtaka kukifanya.Maelekezo waliyompa ilikuwa ni kuhakikisha kwamba anafanikiwa kukufikia na kukupa keki ambayo inasemekana kuwa na sumu na lengo la watu hao lilikiwa ni kukuua kwani kwa mujibu wa maelezo yao hao jamaa ni kwamba kuna mambo unayoyafahamu ambayo hukupaswa kuyajua.Unaweza ukatuambia ni mambo gani hayo unayoyafahamu yaliyopelekea mtiririko huu wa matukio ya utekaji nyara na wewe kutakiwa kuuawa?
Tonny akawatazama maafisa wale wa polisi halafu akatabasamu na kusema
“Ndugui zangu nadhani nyote mnafahamu kazi niliyokuwa naifanya.Katika kazi kama hii ni wazi lazima utafahamu mambo mengi sana na siri za watu mbali mbali .Ni muda mrefu sasa nimekuwa humu gerezani na siwezi kukumbuka ni jambo gani hasa ninalolifahamu ambalo linaweza likawafanya watu hawa wapange mpango wa kuniua .Ninachofahamu ni kwamba kazi hii ya ujasusi inakufanya uwe na maadui wengi sana wa ndani na nje ya nchi kwa maana hiyo inawezekana watu hao wakawa ni maadui zangu na wana lengo la kulipiza kisasi.” Tonny akaendelea kudanganya.Salvatory akaghafilika
“C’mon Tonny.Hebu sema ukweli wako.Muda ule wakati unataka nikupe nafasi ili uweze kuiokoa familia ya Ithan ulisema kwamba kuna jambo kubwa unalolifahamu na ambalo limepangwa kufanywa na watu hao walioiteka familia ya Ithan lakini nikakukatalia na kukwambia kwamba suala hilolinatakiwa kushughulikiwa na vyombo vya usalama.Nakushangaa unapotoa taarifa za tofauti kwa maafisa wa polisi.Maafisa hawa wamekuja hapa ili kupata mwanga wa nini kinachoendelea na kuanza mchakato wa kuiokoa familia ya Ithan na hatimaye kuzuia hicho unachosema kinaweza kutokea.Tafadhali Tonny,kama kuna jambo lolote unalolifahamu ambalo ni hatari kwa usalama wa nchi tafadhali naomba uliweke wazi kwa maafisa hawa wa jeshi la polisi ambao watalifanyia kazi.” Akasema Salvatory
Tonny akamtazama tena Salvatory na kusema
“Salvatory mambo yote niliyokuambia hayakuwa ya kweli.Nilikudanganya ili niweze kupata nafasi ya kutoroka gerezani.Hakuna hata suala moja lililokuwa na ukweli.Samahani sana kwa hilo” akasema Tonny na kuzipandisha hasira za Salvatory
“Bastard !!…. Kumbe muda wote huu ulikuwa na unanichezea akili yangu? Akasema kwa hasira Salvatory ikamlazimu afisa mmoja wa polisi amtulize
“Tonny ,kama kuna jambo lolote unalolifahamu linaloweza kutusaidia kuiokoa familia ya Ithan pamoja na askari magereza ambaye naye anashikiliwa na watu hawa tafadhali tueleze.Kumbuka kwamba ni Ithan ndiye aliyeyaokoa maisha yako leo hii.Tafadhali tunaomba ushirikiano wako” akabembeleza mkaguzi yule wa polisi
“Afisa,namshukuru sana Ithan kwa kuyaokoa maisha yangu.Nina deni kubwa kwake .Laiti kama ningekuwa nikifahamu lolote ambalo lingesaidia katika kuipata familia ya Ithan ningewasaidia lakini kwa sasa sina chochote ninachokifahamu.Mnaweza kuniruhusu kupumzika tafadhali? Akasema Tonny.
Maafisa wale wa polisi wakiongozwa na mkuu wa gereza la Uwangwa Mr Salvatory wakaondoka mle chumbani kwa ahadi ya kwenda kuendelea na uchunguzi wa jambo lile na kuahidi kurejea tena baadae kama kungekuwa na jambo lolote ambalo wangehitaji ufafanuzi kutoka kwa Tonny
“ Nimemuudhi sana Salvatory lakini nilifanya vile kwa sababu maalum.Suala hili ni gumu na linapaswa kushughulikiwa na vyombo vinavyohusika na ugaidi.Sina maana kwamba jeshi la polisi hawana uwezo wa kushughulikia suala hili lakini kuna vyombo mahsusi vyenye watu wenye mafunzo ya hali ya juu katika kukabiliana na mambo kama haya ya kigaidi.Kwa kuwa idara ya ujasusi wameamua kulipuuza onyo langu sioni tena kama kuna haja yoyote ya kuendelea kuumiza kichwa kuhusiana na kinachokwenda kutokea.” Akawaza Tonny halafu akajilaza kitandani.
Akiwa amejilaza kitandani mlango ukafunguliwa tena na akaingia mkuu wa gereza akiwa amefura kwa hasira
“Tonny nimerudi tena safari hii nikiwa mwenyewe.Naomba unieleze ni kwa nini uliamua kuichezea akili yangu kwa kunidanganya na kunifanya nihatarishe usalama wa gereza? Iwapo ningekupa nafasi kama ulivyokuwa ukiomba halafu ukatoroka unahani ningekwua wapi mida hii? Nilikwisha anza kukuamini lakini baada ya kukiri kwamba ulikuwa ukinidanganya kwa dhumuni la kutoroka nilipatwa na hasira kali sana .Kwa nini uamue kufanya hivyo Tonny? Kwa nini uamue kunidanganya? Tonny naomba unipe majibu haraka sana “ akasema Salvatory akiwa amevimba kwa hasira
“Mr Salvatory ,nakufahamu wewe ni mtu makini na mwerevu.tafadhali punguza hasira na unisikilize kwa makini” Tonny akasema.
“I didn’t lie to you.” Akasema Tonny
“Yote niliyokueleza yalikuwa ni mambo ya kweli. Taarifa nilizonazo ni taarifa nyeti sana ambazo zinahusiana na usalama wa taifa kwa maana hiyo siko tayari kumweleza kila mtu na kama unavyojua kwamba kwa sasa sioni mtu yeyote wa kumuamini kwa sababu tayari kuna mawakala karibu kila idara nyeti ya serikali ambao wanadaka kila taarifa na kuzipeleka kwa watu wao .”
“Damn you Tonny..kila mara unasema una taarifa nyeti..kwa nini sasa hutaki kuziweka wazi tarifa hizo ili zifanyiwe kazi? Akafoka Salvatory
“Mr Salvatory ningependa sana kuzitoa tarifa hizi ili zifanyiwe kazi lakini ninasita kufanya hivyo kwa sababu sioni mtu wa kumwamini kwa sasa.Nimejaribu kuitaarifu idara yangu lakini kupitia huko ndiko taarifa hizi zimevuja na kusababisha tukio la kutekwa kwa familia ya Ithan.”
“Tonny kama huna mtu mwingine unayeweza kumuamini tafadhali naomba uniamini mimi.Start with me” akasema Salvatory
“Salvatory naomba unisikilize kwa makini sana.” Akasema Tonny huku akimsogelea Salvatory
“jambo ninalolifahamu linalokwenda kutokea ni jambo zito na halitasahaulika kwa vizazi hadi vizazi.Napenda nikuhakikishie kwamba hakuna mtu anayeweza kuzuia jambo hilo lisitoke zaidi yangu.Ni mimi pekee ambaye nina uwezo wa kulizuia suala hilo kwa sababu ninafahamu wapi pa kuanzia na nini cha kufanya.Waluioniweka hapa ndani walisahau kwamba bado taifa hili linanihitaji.Angalia haya maajabu mimi niliye gerezani nina taarifa nyeti sana za usalama wa taifa hili lakini wao walioko huru hawaelewi chochote. Kwa bahati mbaya sana sintaweza kufanya jambo lolote la kuzuia jambo hilo baya kwa taifa letu lisitokee kwa sababu ninaozea humu gerezani na hakuna hata mmoja anayeukumbuka mchango wangu kwa taifa hili.Kama watakuwa wakiutambua na kuuthamini mchango wangu kwa taifa hili basi huu ni wakati wangu wa kuniachai huru” akasema Tonny
“Tonny naomba ufahamu kwamba kuwa na taarifa muhimu inayohusu usalama wa nchi na ukashindwa kuiwasilisha kwa vyombo husika ili ifanyiwe kazi ni kosa kisheia na kama kutatokea tukio lolote la umwagikaji wa damu basi damu yote itakayomwagika itakuwa juu yako.Damu za watanzania zinakulilia Tonny.Tafadhali waokoe na jambo hilo linalokwenda kutokea.”Salvatory akasisitiza
“Damu ya watanzania haitakuwa juu yangu mimi bali itakuwa juu ya wale walioamua kuniweka humu gerezani kwa manufaa yao wenyewe na kusahau mchango wangu kwa taifa hili.Sikufichi salvatory kinachokwenda kutokea hakitaweza kufutika kwa vizazi na vizazi vya nchi hii” Tonny akasema
“C’mon Tonny tell me what to do to stop that !! Akasema Salvatory kwa ukali
‘You want to know what to do to stop what’s going to happen? Get me prime minister..nahitaji kuongea na waziri mkuu uso kwa uso..Kama ikishindikana kuongea na waziri mkuu basi jiandaeni kwa msiba wa kitaifa” Tonny akasema
“Tonny ngoja nijitahidi nione nitakachoweza kukifanya ili kumpata waziri mkuu”
akasema Salvatory huku akitoka mle chumbani kwa kasi
“Ninamfahamu vizuri mheshimiwa waziri mkuu .kama nikimueleza vizuri kuhusiana na suala hili anaweza akanisikiliza na kunitoa humu gerezani.Kama hawatakuwa tayari kunitoa humu gerezani sintaweza kuwasaidia kwa lolote lile.Wajiandae kwa msiba wa kitaifa.” Akawaza Tonny.


*********************

Saa sita na dakika kumi na saba za mchana ndege ya kwanza iliyowabeba wageni wanaokuja kuhudhuria mkutano wa Sulivan wakitokea nchini Marekani ikatua katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Kilimanjaro. Ulinzi mkali ulikuwa umeimarishwa uwanjani hapo. Kila kona ya uwanja huu askari walikuwa wakizunguka na kuhakikisha kwamba hakuna tukio lolote lenye kuhatarisha amani linaweza kutokea.Wageni walianza kushuka ndegeni na kila aliyeshuka alikuwa akitabasamu.Wengi wa wageni hawa ilikuwa ni mara yao ya kwanza kuigusa ardhi ya Tanzania.Vikundi mbali mbali vya ngoma za asili vilikuwepo uwanjani kwa ajili ya kuwaburudisha wageni ambao hawakusita kuonyesha furaha yao na wengine walioshindwa kujizuia wakajiunga na wenyeji wao katika kucheza ili mradi ikawa ni furaha kubwa hapo uwanjani.Mabasi manne yalikuwa yameandaliwa kwa ajili ya kuwabeba wageni na kuwapeka katika hoteli walizokuwa wameandaliwa.Msafara wa magari hayo ulitanguliwa na piki piki ya polisi ili kuongoza njia na nyuma kabisa kulikuwa na gari mbili za wanausalama.Kila mahala walikokuwa wakipita wageni hawa walikuwa wakiwapungia mikono wenyeji na kuonyesha furaha yao ya kukanyaga tena ardhi ya Afrika kwani wote waliamini kwamba afrika ndilo bara la asili yao.
Safari yao ikaishia katika hoteli ya kimataifa ya Arusha green Valley ambayo ndiko wageni wengi walipangiwa kukaa.pale nje kulikuwepo vikundi mbali mbali vya ngoma za kiasili vilivyowatumbuiza wageni na kuwafanya wazidi kufurahi.

***************

Saa saba za mchana mlango wa chumba cha Tonny ukafunguliwa na akaingia Salvatory mkuu wa gereza.Alikuwa na uso uliosawajika sana Bila kupoteza muda akasema
“Tonny ninaufahamu mchango wako katika nchi hii.Umefanya mambo mengi sana mazuri kwa nchi hii.Kusema ukweli sifahamu ni kwa kosa gani umefungwa hapa gerezani na ndiyo maana siku zote nimekuwa nikihakikisha kwamba unapata kila aina ya huduma unayoitaka hapa gerezani.Ninaamini maneno yako kwamba kuna jambo ambalo unalifahamu linakwenda kutokea na ninapenda kukuhakikishia kwamba niko nawe bega kwa bega katika kuhakikisha kwamba suala lako linamalizika haraka iwezekanavyo na unaruhusiwa kutoka gerezani ili ukashughulikie jambo hilo .Nimejaribu kufanya kila linalowezekana ili kumpata waziri mkuu kama ulivyokuwa umeomba lakini jibu nililolipata linakatisha tamaa sana” akasema Salvatory
“Umepata jibu gani? Akauliza Tonny
“Nimempata waziri mkuu katika simu na nikamueleza kila kitu akadai kwamba kama kuna kitu unakifahamu kuhusu jambo lolote lile linalohusu usalama wa taifa basi uniambie ili niweze kuliwasilisha sehemu husika.Amedai kwamba hana muda kwa sasa ametingwa na shughuli nyingi za kiserikali”
Huku akitabasamu Tonny akasema
“nashukuru sana Salvatory kwa kuniamini .Kama waziri mkuu naye amekataa kuja kunisikiliza basi hakuna tatizo lakini nina imani siku moja watanifuata wao wenyewe humu gerezani lakini watakuwa wamekwisha chelewa sana.Ahsante sana kwa msaada wako Mr Salvatory” akasema Tonny kwa kukata tamaa.
“Juhudi zote za kunitoa humu gerezani zimeshindikana kabisa.Ninamuachia Mungu suala hili pengine siku moja nitafanikiwa kutoka humu gerezani” akawaza Tonny akiwa ameinamisha kichwa akiwaza.

USIKOSE SEHEMU IJAYO........................................
 
Wakuu nawakubusha kumjali Mtunzi wa Riwaya hii
Kumbukeni ndie mtunz wa Paniela,queen Monika pamoja na hii na zinginezo nyingi

Kiukweli ni Mtu mwenye moyo sana na mwenye upendo na Wasomaji wake
3bc18ff08ac01d3088efb618444e5f52.jpg
 
BRING BACK OUR GIRLS
SEHEMU YA 37
ILUIPOISHIA SEHEMU ILIYOPITA
“Umepata jibu gani? Akauliza Tonny
“Nimempata waziri mkuu katika simu na nikamueleza kila kitu akadai kwamba kama kuna kitu unakifahamu kuhusu jambo lolote lile linalohusu usalama wa taifa basi uniambie ili niweze kuliwasilisha sehemu husika.Amedai kwamba hana muda kwa sasa ametingwa na shughuli nyingi za kiserikali”
Huku akitabasamu Tonny akasema
“nashukuru sana Salvatory kwa kuniamini .Kama waziri mkuu naye amekataa kuja kunisikiliza basi hakuna tatizo lakini nina imani siku moja watanifuata wao wenyewe humu gerezani lakini watakuwa wamekwisha chelewa sana.Ahsante sana kwa msaada wako Mr Salvatory” akasema Tonny kwa kukata tamaa.
“Juhudi zote za kunitoa humu gerezani zimeshindikana kabisa.Ninamuachia Mungu suala hili pengine siku moja nitafanikiwa kutoka humu gerezani” akawaza Tonny akiwa ameinamisha kichwa akiwaza.

ENDELEA…………………………..

Rahim akiwa na vijana wake wakarejea katika maskani yao wakiwa na nyuso zilizojaa hasira kubwa baada ya kazi kubwa waliyoifanya kushindwa kufanikiwa.Kitendo cha Ithan kugeuka katika dakika za mwisho bado kiliendelea kumtesa sana Rahim kwani hakuelewa wakuu wake wa kazi wangemchukulia vipi.Katika kazi zote ambazo aliwahi kupewa ni kazi hii moja ambayo imeshindwa kukamilika.Jambo hili lilimuumiza sana kichwa chake
Baada ya kuwasili maskani kwao moja kwa moja Rahim akaelekea katika chumba alimokuwa amewekwa Rebeca mke wa Ithan.Rebeca ambaye alikuwa amekaa chini amemkumbatia mwanae Vanessa akastuka baada ya mlango kufunguliwa na Rahim akaingia .Rebeca akaogopa kwa namna Rahim alivyokuwa akimtazama kwa hasira .
“Tayari mume wangu ameshawafanyia kazi yenu? Kama tayari tuachieni huru tuondoke tafadhali” akasema Rebeca kwa ujasiri mkubwa.Rahim akamuangalia kwa macho makali akavuta kiti na kuketi
“Mume wangu yuko wapi? Akauliza tena Rebeca
“Jina lako nani? Akauliza Rahim
“Rebeca” .
Rahim akamuangalia tena Rebeca kwa macho makali na kusema
“Rebeca wewe ni mwanamke mzuri sana lakini sifahamu ni kwa nini ulianguka kimapenzi kwa mtu kama Ithan.”
“Mume wangu yuko wapi? Mlisema akiwafanyia kazi yenu mtatuachia huru” Rebeca akasema
“Rebeca una bahati mbaya sana kwa kumpata mtu kama Ithan kuwa mume wako.Siku zote amekuwa akikudanganya kwamba anakupenda lakini ukweli ni kwamba hana hata chembe moja ya upendo kwako.”Rahim akasema
“Hufahamu chochote kuhusu mambo yetu ya ndani.Ithan ananipenda sana na mimi ninampenda na ni mwanaume mwenye roho nzuri ya upendo” akasema Rebeca na kumfanya Rahim acheke kicheko kikubwa
“sikiliza Rebeca,Ithan amekuwa akikudanganya kwamba anakupenda nawe ukakubali kudanganyika.Ukweli ni kwamba mumeo hakupendi hata chembe”
“kwa nini unasema kwamba mume wangu hanipendi? Rebeca akauliza
“Kama angekuwa akikupenda kweli basi asingekubali kukutelekeza wewe na mwanao”
“ Ithan hawezi kunitelekeza mimi na mwanangu hata siku moja.Ninamfahamu vizuri yuko tayari hata kuupoteza uhai wake kwa ajili ya kunilinda mimi na mwanangu na ndiyo maana amekubali kuifanya kazi yenu ili kutuokoa mimi na mwanangui” Rebeca akasema
“Kwa taarifa yako ni kwamba Ithan amekwenda kinyume na makubaliano yetu.Ameshindwa kuifanya kazi tuliyomtaka aifanye na akakimbia.Makubaliano yetu naye yalikuwa kwamba atufanyie kazi yetu tunayoitaka halafu tutawaachia huru wewe na mwanao lakini iwapo atashindwa kutekeleza kazi yetu basi familia yake yote itateketezwa.Rebeca ,sisi siyo watu wabaya lakini kwa sababu Ithan amekwenda kinyume na makubaliano yetu basi hatuna haja kutimiza ahadi yetu ya kuiteketeza familia yake.Kwa maana hiyo jiandae kwani muda wowote kuanzia sasa wewe na mwanao tutawapiga risasi kwa sababu hatuna matumizi na nyie tena.Tuliwashikilia na kuwaweka hapa kwa lengo moja tu la kumfanya Ithan aweze kutufanyia kazi yetu lakini kwa kuwa ameshindwa basi hatutakuwa na jambo lingine la kufanya zaidi ya kuwaua.Nasikitika sana kwa kitendo alichokifanya Ithan lakini sina namna nyingine ya kuweza kuwasaidia.Jiandae wewe na mwanao muda wowote kuanzia sasa “ Rahim akasema na kumfanya Rebeca kuangua kilio.
“Jamani naomba msituue mimi na mwanangu.Tumewakosea nini? Mtatuua bure sisi hatufahamu jambo lolote lile” akalia Rebeca huku akimkumbatia mwanae
“Usinililie mimi.Mlilie mumeo ambaye amekubali wewe na mwanao mfe ili yeye apone.” Akasema Rahim kwa ukali huku akiinuka na kuufunga mlango.
“Ithan mume wangu kwa nini lakini umeamua kufanya hivi? Kama ni kweli umeamua sisi tufe sintakusamehe milele.Ee Mungu tuokoe katika jambo hili,tunakufa bila hatia.Hakuna jambo lolote lile ambalo tumewakosea watu hawa.” Rebeca akaendelea kulia kwa nguvu

***************


Saa mbili za usiku ndege ya nne iliyowabeba wageni toka Marekani wanaokuja kuhudhuria mkutano wa Sullivan ikawasili katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Kilimanjaro.Wageni wapatao mia moja na arobaini na sita walikuwamo katika ndege hii.Kama ilivyokuwa katika kila kundi la wageni waliowasili walipokelewa na viongozi mbali mbali wa kiserikali waliokuwepo pale uwanjani wakati ule wakIongozwa na mkuu wa mkoa wa Arusha na kisha kupelekwa katika hoteli maalum walizokuwa wameandaliwa chini ya ulinzi mkali sana wa jeshi la polisi .Kundi hili lilikuwa ni kundi la mwisho kuwasili kwa siku hii.
Wakati kundi la mwisho la wageni likiwasili jijini Arusha , kikao kizito kilikuwa kinaendelea katika jumba kubwa la mfanyabiashara mkubwa wa madini ya Tanzanite aliyejulikana kwa jina la Sultan.Ni katika jumba hili mipango yote ya utekelezaji wa shambulio kubwa kuwahi kutokea katika historia ya Tanzania ilikuwa ikiandaliwa.Tayari viongozi waliokuwa wakiratibu shambulio hilo kutoka katika mtana vikundi hatari vya Alshabaab na Boko haram walikwisha wasili toka siku iliyotangulia.Kikao hiki kilikuwa na watu wapatao thelathini na sita
“ Taarifa tulizozipata muda si mrefu ni kwamba kundi la mwisho la wageni kwa siku ya leo limewasili muda mfupi uliopita na tayari wamekwisha pokelewa na kupelekwa katika hoteli walizoandaliwa.Idadi ya wageni ni sawa na ile ambayo tuko nayo ila tumepata taarifa nyingine kwamba kuna ndege nyingine mbili zinategemea kuwasili kesho saa tatu na saa sita mchana.kwa maana hiyo idadi ya wageni itaongezeka .Tayari katika sehemu zote walizofikia wageni hawa kuna watu wetu ambao wamekuwa wakifuatilia kwa karibu nyendo za hawa wageni pamoja na hali nzima ya kiusalama ilivyo na kutupa taarifa za mara kwa mara.Kwa taarifa tulizozipata mpaka hivi sasa toka kwa wawakilishi wetu ni kwamba mpaka sasa hivi hakuna dalili au tetesi zozote za kuweza kufahamika kwa mpango wetu au hata kutiliwa shaka kwamba kuna mpango unaoandaliwa chini kwa chini.Ni huyu kijana Tonny ambaye alitaka kuharibu hali ya mambo baada ya kuonekana kupata fununu za kuwepo kwa shambulio.Bado tunaendelea kufanya uchunguzi ili tuweze kufahamu taarifa hizi alizipata wapi.Pamoja na kujitahidi kutoa tahadhari kuhusiana na kuwepo kwa tukio hili tunashukuru kwa sababu taarifa yake haikupewa uzito unaostahili.Lakini hii haiwezi kutuhakikishia kwamba hali ni salama kwa asilimia mia moja kwa maana hiyo itatulazimu kuendelea kuchukua tahadhari kubwa hasa kwa siku ya kesho ambayo mkutano utafunguliwa rasmi “ Abdulkhareem kutoka nchini Iran ambaye ndiye mratibu mkuu wa mpango huu akatulia kidogo na kisha akaendelea.
“Mke wa rais wa Marekani atawasili kesho kama ratiba inavyoonyesha na jioni ya kesho yeye pamoja na rais wa Tanzania watafungua rasmi mkutano wa Sullivan.Siku itakayofuata ndiyo itakuwa siku yetu ya kuibadii historia ya dunia.Tunataka.Mtaalamu wetu wa silaha za kibaolojia bi Safia Alwadhir amekwisha kamilisha kuweka sawa mambo yake na kirusi hicho kipo tayari kwa matumizi .Tutakitumia kirusi hiki ambacho kitasababisha maangamizi makubwa .Siku ya leo sina maneno mengi ya kusema .Nilihitaji kuwapa taarifa kwa ufupi ya wapi tumefikia mpaka sasa hivi.Kama kutatokea mabadiliko ya aina yoyote tutafahamishana mara moja.Sina haja ya kurudia rudia kuwakumbusha juu ya wajibu wa kila mmoja wetu katika kufanikisha tukio hili muhimu.Yangu mimi yalikuwa hayo machache kwa leo ,mengi zaidi tutaelekezana kesho.Kwa sasa nawakaribisha kila mwenye maoni au jambo lolote lile la kusema” akamaliza Abdulkhareem .
Majadiliano yaliendelea hadi ilipotimu saa sita za usiku.Kikao kikafungwa na wote wakatawanyika kwenda kupumzika.

*******************

Kumekucha tena katika jiji la Arusha na hali ya asubuhi hii ni ya kiubaridi kama ilivyo kawaida ya jiji hili mashuhuri barani Afrika.Pilika pilika za wakaazi wa jiji hili zilikuwa nyingi kama kawaida lakini kwa siku hizi chache kuelekea mkutano wa Sulivan jiji la Arusha lilionekana kuwa na pilika zaidi hasa kutokana na watu wengi kuwasili kutoka ndani na nje ya Tanzania.Mkutano kama huu uliwahi kufanyika katika jiji hili kwa hiyo wakazi wa Arusha na watanzania kwa ujumla wanafahamu umuhimu na faida za mkutano huu ndiyo maana wamehudhuria kwa wingi sana katika mkutano huu unaofanyika kwa mara ya pili jijini Arusha.Hoteli zote za jiji la Arusha zilijaa wageni waliotoka katika mikoa mbali mbali na nchi za jirani na Tanzania waliokuja kuhudhuria mkutano huu mkubwa.Mpaka kufikia siku hii ya leo ilikuwa ni vigumu sana kuweza kupata nafasi katika nyumba za kulala wageni jijini Arusha.Wageni wengine iliwalazimu kwenda kutafuta nafasi katika nyumba za wageni zilizokuwa nje kidogo ya jiji la Arusha na hadi mjini Moshi.Jiji la Arusha lilikuwa limefurika watu.
Siku hii ni siku ya ufunguzi wa mkutano huu wa Sullivan unaotarajiwa kufunguliwa na rais wa jamhuri ya muungano wa Tanzania ambaye ndiye mwenyekiti wa mkutano huu.Katika mkutano huu ambao unahudhuriwa na marais zaidi ya kumi toka katika nchio mbali mbali za afrika,ulitegemewa kuhudhuriwa pia na mke wa rais wa Marekani Bi Gwen pring ambaye ni mmarekani mweusi akiambatana na binti yake Theresa waliotegemewa kuwasili saa nne za asubuhi katika uwanja ndege wa kimataifa wa Kilimanjaro.
Eneo lote kuzunguka ukumbi utakamofanyikia mkutano huu wa Sullivan lilikuwa na pilika pilika nyingi za kuhakikisha kwamba kila kitu kinakwenda kama kilivyopangwa.Ulinzi pia ulikuwa mkali sana eneo hili.Kulikuwa na askari wengi waliokuwa wamewekwa kulizunguka jengo lile wengine wakiwa na silaha .Walikuwepo pia askari wa kikosi cha mbwa na farasi na vile vile kulikuwa na idadi kubwa ya askari kanzu .Katika mitaa ya jiji la Arusha askari wa doria walikuwa wakizunguka ili kuimarisha ulinzi .Angani helkopta mbili za polisi zilikuwa zikizunguka na kufanya doria ya angani.Usalama ulikuwa mkubwa sana kiasi kwamba ungeweza hata kulala mlango wazi bila kuwa na hofu yoyote.Ukiweka kando kundi hilo kubwa la askari lililoimarisha ulinzi katika ukumbi ule na mji wote wa Arusha walikuwepo pia maafisa usalama maalum toka kutoka Marekani waliokuwa wakisaidiana na askari wetu katika kuimarisha ulinzi.Serikali ya marekani iliamua kuwatuma askari wake ili kuhakikisha kwamba raia wake pamoja na baadhi ya viongozi wake wote waliokuja kuhudhuria mkutano wa Sullivan wanakuwa salama na kurejea nyumbani salama..Kwa ulinzi uliokuwepo eneo hili ilikuwa vigumu sana kuamini kwamba kuna sambulio lolote la kigaidi lililokuwa likipangwa kutokea
Wakati maandalizi ya mwisho mwisho ya mkutano wa Sullivan yakiendelea ,nje kidogo ya jiji la Arusha katika nyumba moja kubwa mithili ya kasri kubwa la kifalme mipango ya shambulio kubwa ilikuwa ikiendelea .Katika kasri hili ndipo Alshabaab wakishirikiana na wenzao toka kundi la Boko Haram walikuwa wakiratibu shambulio kubwa la kigaidi kuwahi kutokea katika eneo hili la Afrika mashariki.Abdulkhareem ndiye aliyekuwa mratibu mkuu wa operesheni hii.Asubuhi hii walikuwa wote wamekaa katika ukumbi wao mdogo wakijaribu kupitia tena mpango mzima na kuangalia iwapo kila kitu kinakwenda kama kilivyopangwa.Katika meza kuu Abdulkhareem alikuwa amekaa na Sultan mmoja kati ya wafanya biashara wakubwa sana wa madini ya Tanzanite jijini Arusha ambaye ndiye mmiliki wa jumba hili kubwa ambalo linatumika kuratibu mashambulio.Pembeni yao alikuwa ni mwanamke mmoja ambaye kwa sura alionekana bado ni msichana mbichi na anayevutia sana Bi safia Alwadhir ambaye ni mtaalamu mkubwa wa silaha za kibaolojia aliyetengeneza kirusi hatari sana cha maangamizi ambacho walipanga wakitumie kwa mara ya kwanza siku hii.
" Mpaka dakika hii bado kila kitu kinakwenda kama tulivyopanga.Japokuwa kulitaka kutokea mushkeli kidogo baada ya huyu kijana Tonny kupata taarifa za kuwepo kwa mpango wa shambulio ,lakini nashukuru kwamba mpaka dakika hii kila kitu kinakwenda vizuri.Pamoja na hayo kuna jambo nilikuwa nikilijadili na Sultani asubuhi hii ya leo.Jaribio la kutaka kumuua Tonny gerezani lilishindikana kwa hiyo kuna kila uhakika kwamba polisi wanaweza wakalifanyia uchunguzi suala lile na kutaka kuufahamu ukweli.Tumefikiria kufanya kitu kimoja..kwa kuwa ndani ya jeshi la polisi kuna watu wetu basi tutawatumia hao ili kuweza kufanya uchunguzi wa jambo hili kuchelewa au kutokufanyika kabisa ili kutupa sisi nafasi ya kuweza kutekeleza shambulio letu hiyo siku ya kesho.Tayari tumekwisha wasiliana na viongozi watatu wa juu wa jeshi hili na tayari tumekwisha watumia kiasi cha shilingi millioni mia moja kila mmoja kwa ajili ya kulishughulikia suala hilo yaani kuhakikisha kwamba hakuna uchunguzi wowote utakaofanyika kwa siku za hivi karibuni.Huyu kijana Tonny anaonekana kuwa ni kijana hatari sana lakini kwa sasa hatuna shaka naye kwani tayari amekwisha dhibitiwa na hakuna mtu yeyote atakayeruhusiwa kuonana naye." Abdulkhareem akawatazama wajumbe wa mkutano ule kisha akaendelea.
" Leo hii saa nne za subuhi mke wa rais wa Marekani akiambatana na binti yake watawasili katika uwanja wa kimataifa wa Kilimanjaro.Ratiba yake inaendelea vile vile kama ilivyokuwa imepangwa na hakuna kitu kilichobadilishwa. Pale uwanjani atapokelewa na mke wa rais wa Tanzania Bi Devotha Simanga akiambatana na baadhi ya viongozi wa serikali akiwemo waziri wa mambo ya nje wa tanzania.Kisha pokelewa ataelekea katika ikulu ndogo ambako atakuwa na maongezi na rais wa Tanzania na baada ya hapo ataelekea Tandala International hotel ambayo ndiyo hoteli atakayofikia kwa kipindi chote atakachokuwa hapa Arusha.Pale Tandala Hoteli tayari tunao watu wetu watatu wanaofanya kazi kama wahudumu kwa hiyo tunauhakika mkubwa wa kupata taarifa za uhakika .Jioni ya leo mkutano wa Sullivan utafunguliwa rasmi na rais wa Tanzania akishirikiana na baadhi ya viongozi kadhaa wa taasisi hii ya Sullivan .Siku ya leo itakuwa kimya sana na hakuna kitu chochote kitakachofanyika kama ratiba yetu inavyotuongoza." Abdulkhareem akanyamaza kidogo na kuendelea.
" Siku ya kesho ndiyo siku ya kazi.Siku ya kuibadili historia ya dunia.Nadhani nyote mnafuatilia mwongozo wa shughuli zote kama unavyoelekeza.Naomba kila mmoja afahamu nafasi yake tafadhali.Mpango huu umeandaliwa kwa muda mrefu sana na ni mpango uliogharimu pesa nyingi sana hadi kufika hapa kwa hiyo hatutaki kuona kosa lolote likitokea.Kosa lolote dogo linaweza likasababisha mpango mzima kuharibika.Narudia tena nawaomba muwe makini sana siku ya kesho.Nina uhakika mkubwa kati yenu hakuna yeyote ambaye anaweza akaharibu kazi.Siku ya kesho tutaachia kirusi chetu hatari katika hospitali ya Mount Meru na katika hospitali ya Serian sina hakika kama nimetamka sahihi jina hili majina ya kitanzania ni magumu sana lakini tutaachia kirusi pia katika soko kuu la mji wa arusha.Hizi ni sehemu zenye mikusanyiko mikubwa ya watu.Hili litakuwa ni shambulio letu la kwanza kabisa ambalo litaamsha taharuki miongoni mwa jamii na kuilazimisha serikali kuhamaki na kuelekeza nguvu nyingi katika kutaka kuokoa maisha ya watu watakaokuwa wakiangamia ndani ya muda mfupi.Hakuna dawa ya haraka ya kuweza kukizuia kirusi hiki ambacho husambaa kwa njia ya hewa.Baada ya nguvu zote za serikali kuelekezwa katika maeneo haya basi sisi tutapata nafasi nzuri ya kuweza kutekeleza mipango yetu mingine bila ya kukabiliwa na nguvu kubwa.
TUKUTANE SEHEMU IJAYO………………
 
Back
Top Bottom