BRING BACK OUR GIRLS
SEHEMU YA 33
ILIPOISHIA SEHEMU ILIYOPITA
“nani wewe unayegonga mida hii?Sauti toka ndani ikauliza.
“Frank ni mimi Ithan.”
“Ithan ?? Umefuata nini usiku wote huu? Frank akasema
“Kuna matatizo yametokeandugu yangu naomba ufungue mlango tuongee ni kuhusu zamu ya kesho asubuhi.” Ithan akasema na baada ya muda mfupi komeo ya mlango ikasikika ikifunguliwa,mlango ukavutwa kwa ndani na akatokeza mtu mmoja mfupi mwenye kitambi .
“Frank karibu nda……………………..” hakumaliza sentensi yake akajikuta akisukumwa ndani na kuelekezewa bastora kichwan\i.Kwa sauti ndogo Rahim akamuamuru.
“Usithubutu kupiga kelele ama la nitakufumua kichwa chako kwa risasi.Taratibu na bila kelele ongoza nje.”
Huku midomo ikimtetemeka Frank akaongoza nje na moja kwa moja wakaingia garini na kuondoka maeneo yale haraka.
ENDELEA................................
Ni saa kumi na moja na nusu za alfajiri katika chumba kilichokuwa na mitambo mingi Ithan akiwa katika sare za kazi alikuwa ameketi mezani akipewa maelekezo.Frank alikuwa amefungwa katika moja ya chumba na lengo kuu likiwa ni kumzuia asiingie kazini ili nafasi yake ichukuliwe na Ithan.
“Kifaa hiki ndicho utakachoingia nacho katika chumba cha kuongozea kamera.Ukisha ingia pale ndani,nyuma ya kompyuta kuna kifaa kimekaa mfano wa pembe tano na kimeandikwa CF – TR.54 .Katika kifaa hicho kuna nyaya tano.Chomoa nyaya zote tano na uzichomeke katika kifaa hiki kila waya mahala pake .Ukisha zichomeka nyaya hizo bonyeza hapa halafu taa ya kijani itawaka na kuzima halafu taa ndogo nyekundu itawaka .Baada ya hapo utachukua tena kifaa hiki kingine ambacho kinaweza kukaa mahala popote kwa sababu kina gundi nyuma yake na kukibandika ukutani na kisha utabonyeza kidude hiki hapa cha katikati.Hapo utakuwa umemaliza kazi na utaelekea katika chumba cha Tonny.Sisi tutakuwa umbali wa mita kadhaa toka hapo gerezani na tutakuwa tukiangalia kila unachokifanya kupitia kompyuta zetu ambazo zitaunganishwa na kifaa kile utakachokuwa umekichomeka , hivyo usijaribu kufanya ujinga wa namna yoyote ile.Tutakuwa tukikupa maelekezo ya nini cha kufanya.Ukishamaliza hapo katika chumba cha kamera utatoka haraka na kuelekea katika chumba cha Tonny.Ukifika utampatia zawadi hii ndogo.Ndani ya boksi hili kuna keki tamu na nzuri na nina imani Tonny ataifurahia sana kwa sababu ni muda mrefu hajapata vitu vizuri kama hivi .Mshawishi ale na akisha kula kaa usubiri kwa dakika kama tano halafu tutakupa maelekezo mengine na utaondoka pale gerezani haraka sana na mpaka hapo utakuwa umemaliza kazi yako na familia yako itakuwa huru.Kumbuka kwamba ukijaribu kufanya ujinga wa namna yoyote ile basi familia yako yote tunaiteketeza kwa risasi.Usijaribu kumweleza mtu yeyote kuhusu jambo lolote.Kifaa hicho tulichokuwekea sikioni ndicho tutakachokuwa tukikitumia kuwasiliana na wewe.Tumeelewana Ithan? Rahim akamuuliza .Mwili ulikuwa ukimtetemeka na kwa wasiwasi mwingi akasema
“Tumeelewana”
“umeelewa nini unachotakiwa kwenda kufanya?
“Nimeelewa nini mnataka nifanye.Msiwe na wasi wasi nitafanya mnavyotaka nifanye lakini tafadhali nikishamaliza kazi yenu muwaache huru mke wangu na mwanangu” Ithan akasema
“Ok vizuri.twende ukawaage mkeo na mtoto wako kwani iwapo utakwenda kinyume na tunavyotaka sisi basi itakuwa ni mara yako ya mwisho kuwaona.” Rahim akasema na kwa pamoja wakaongozana kuelekea katika chumba ambacho rebeka mke wa Ithan na Vanesa mwanae walikuwa wamefungiwa.
“Baba Vamessa kitu gani kimetokea? Hawa watu ni akina nani? Umewafanya nini watu hawa ? Rebeka mke wa Ithan akauliza huku akitoa machozi akiwa amemkumbatia mwanae Vanessa kwa nguvu.
Ithan akapiga magoti akamkumbatia mkewe na mwanae kwa pamoja .
“Usiogope mama Vanessa.Hawa jamaa mimi siwajui lakini kuna kazi wanataka nikawafanyie na baada ya hapo tutakuwa huru.” Akasema Ithan
“Kazi gani wanataka ukawafanyie ? Una uhakika watatuacha salama hawa watu baada ya kuwafanyia hiyo kazi yao ? Mimi nawaogopa sana.Wanaonekana ni watu hatari”
“Sikiliza mke wangu ,huna haja ya kuogopa..Nimekubali kufanya kazi wanayotaka niwafanyie ili tuwezekuwa huru.Nisipofanya hivyo wanaweza wakatuua wote.Jitahidi kumtuliza Vanessa ,nitarudi hapa kuwachukua muda si mrefu” akasema Ithan huku akimbusu mkewe na kuinuka akaondoka mle chumbani akiwa ameongozana na Rahim.
“Mkeo mzuri sana Ithan “ Rahim akasema huku akitabasamu.Ithan hakujibu kitu
“Usiwe na wasi wasi Ithan ,ukishaifanya kazi hii kikamilifu sisi tutakuacha wewe na familia yako.Hatuna sababu ya kuendelea kuwashikilia mkeo na mwanao wakati kazi yetu itakuwa imekamilika.” Akasema Rahim wakati wakitoka mle ndani ya nyumba na kuelekea mahala yanakoegeshwa magari .
Gari moja lenye muundo wa Fuso lilikuwa tayari lieandaliwa maalum kwa ajili ya shughulii hii.Milango ya nyuma ikafunguliwa na Ithan na Rahim pamoja na watu wengine wanne wakaingia.Mle ndani ya ile gari kulikuwa na mitambo mingi na kompyuta tano.Ithan akashangaa sana na kuzidi kujiuliza maswali mengi kuhusiana na wale watu.Walionekana ni watu ambao wamejiandaa mno.Taratibu gari lile likaondoka Mwili wa Ithan ulikuwa ukitetemeka na alikuwa na woga mwingi.
“Najuta ni kwa nini nilikubali kumsaidia Tonny kuchukua ujumbe ule na kuupeleka mahala alikonituma.Kama nisingekubali kufanya vile mambo haya yote yasingetokea.Lakini ujumbe ule wenye maandishi ya ajabu ajabu ulikuwa una husiana nini na watu hawa kiasi kwamba hawa jamaa waseme una hatari kwao? Je watu hawa ni akina nani? Wanashughulika na nini? Kitu gani wanataka kukifanya manake nimewasikia wakiongea wao kwa wao kwamba Tonny ni hatari kwa mpango wao.Ni mpango upi huo? Ninahisi kuna jambo la hatari linaloendelea na inaonekana Tonny ameligundua.Watu hawa ni watu hatari sana.Hiki kifurushi wanachosema kuna keki ambayo natakiwa nikampatie Tonny nina uhakika kwamba wanataka kumuua Tonny.Lazima keki hiyo wanayotaka Tonny aile itakuwa na sumu.Masikini sina namna nyingine ya kufanya.Iwapo nikiamua kutokumpa Tonny ile keki ale nitakuwa nimehatarisha usalama wa familia yangu.Kijana wa watu atakufa nikimuona.Nitawezaje kuishi maisha yangu na dhambi hii kuibwa moyoni mwangu?” akawaza Ithan huku akihisi kijasho chembamba kikimchuruzika.
“Sina namna nyingine ya kufanya kuweza kumsaidia Tonny.” Ithan aliendelea kuwaza na gari ikiendelea kwenda kwa kasi
“Ithan kifaa hiki ndicho utakachokwenda kukiweka mle katika chumba cha kamera. Unakumbuka malekezo niliyokupa namna ya kukichomeka? Rahim akauliza huku akimkabidhi Ithan kifaa kilichokuwa ndani ya mfuko wa nailoni
“nakumbuka Rahim “ Ithan akajibu kwa sauti yenye kitetemeshi
“Vizuri kama bado unakumbuka.Ukisha chomeka nyaya zile utawasha hapa na kisha utachukua kifaa hiki kingine utakibandika ukutani na kukibonyeza hapa kati kati.Baada ya hapo kompyuta yetu itaunganishwa na kamera za hapo gerezani na tutakuwa tukitazama kila kitu. .Kwa maana hiyo usitubutu kufanya jambo lolote la kipuuzi.Upuuzi wowote utasababisha umkose mkeo mzuri na mwanao .Mara tu kamera za gereza zikishaunganishwa na mtandao wetu kupitia vyombo hivyo tulivyokupatia ,utakuwa ukipokea maelekzo toka kwetu.Kifaa hicho tulichokuwekea sikioni ndicho tutakachokitumia kuwasialiana nawe.Tumeelewana? Rahim akauliza
“Nimekuelewa Rahim.Nitafanya kama unavyotaka nifanye lakini tafadhali naomba nkishamaliza kazi yenu muiachie huru familia yangu”
“Usijali kuhusu hilo Ithan.Jitahidi kuifanya kazi yetu tunavyotaka na familia yako itakuwa huru.” Rahim akamweleza Ithan.
Gari liliingia katika kivuko na kuvushwa kuelekea kigamboni.Tayari kulikwisha pambazuka na watu wengi wa kigamboni walikuwa wakiwahi katika shughuli zao .Mita mia tano toka gereza la Uwangwa gari lile likasimama
“Ithan sisi safari yetu inaishia hapa .Tutakuwa hapa tukikusubiri ukamilishe kazi yetu.Nadhani unakumbuka maelekezo yote tuliyokupa.Kumbuka kwamba kosa moja tu ,utakalolifanya,familia yako yote hutaiona tena.Jitahidi ufanye tunavyotaka ili uweze kuiokoa familia yako” Rahim akamuonya Ithan kwa mara nyingine tena.
“Rahim ninaelewa ninachotakiwa kukifanya .Siwezi kufanya jambo lolote la upuuzi wakati familia yangu mmeishikilia.” Akasema Ithan
“Nafurahi kusikia hivyo Ithan.Unaweza ukashuka sasa “ Rahim akasema huku akitoa ishara mlango mkubwa wa gari ufunguliwe na Ithan akashuka.
Akiwa pale nje ya gari aliweza kuliona gereza .Akasimama akafikiri kidogo na kuanza kupiga hatua kuelekea gerezani.
“Sina namna nyingine ya kukwepa kufanya wanavyotaka.Inanibidi nifanye watakavyo kwa ajili ya kuiokoa familia yangu” akawaza
Ithan akapita geti kuu na kuwasalimu askari wenzake waliokuwa pale.Hakuna aliyeweza kumtilia maanani kwa sababu kwa asubuhi hii huwa ni kipindi cheye pilika pilika nyingi za askari kubadilishana zamu na wale waliochukua zamu huwa katika pilika za kuanza kazi.
Moja kwa moja baada ya kuingia gerezani Ithan akaelekea katika ofisi ya kiongozi wa zamu wa wiki hiyo ili kusaini kitabu cha mahudhurio na kuchukua silaha.Kwa kawaida askari waliokuwa wakilinda zile sehemu zilizokuwa na watu waliodhaniwa kuwa ni hatari wote walikuwa wakichukua silaha.
“Ithan leo hauko katika orodha ya watu watakaoingia.Uko mapumzikoni anatakuiwa aingie Frank badala yako” akasema Meja Sadick ambaye ndiye aliyekuwa mkuu wa zamu ya wiki hii.Akiwa amesimama kwa ukakamavu kuoyesha heshima mbele ya mkuu wake Ithan akasema
“Afande, Frank amepatwa na dharura ya kuuguliwa na akaniomba niingie asubuhi ya leo badala yake ili aweze kupata nafasi ya kumpeleka mkewe kwenye matibabu”
“kwani familia yake si inapata matibabu katika hospitali ya gereza? “ Meja Sadick akauliza
“Afande ugonjwa wa mke wake si ugonjwa wa kutibiwa hospitali.Anampeleka kushughulikiwa na wataalamu wa tiba za asili.” Akadanganya Ithan.
“Hata mimi mke wangu amekuwa akistuka stuka sana usiku na kuongea mambo ya ajabu ajabu.Ninafikiria hata mimi kumpeleka kwa wataalamu wa jadi ili wamtibu” akasema Meja Sadick huku akilisogeza daftari la kusaini kwa Ithan.
“Uwasiliane naye na akwambie atachukua muda gani huko alikoenda ili hata kama akiuliziwa na wakuu niwe na jambo la kumtetea.” Akasema meja Sadick
“Aliniambia kwamba leo hii hii atarejea” Ithan akajibu
Ithan akasaini na kukabidhiwa bunduki kisha akaondoka mle ofisini.
“kazi ya kwanza nimeimaliza.Kinachofuata kwa sasa ni kueleka katika chumba cha kamera.” Akawaza akiwa ameinamisha kichwa chini.
“Katika chumba kile kuna watu watatu ambao huwa wanaingia kwa zamu ya asubuhi.Nitawezaje kuingia na kukichomeka kifaa hiki? Lazima nitumie njia yoyote ile niweze kuingia mle chumbanii na kukichomeka kifaa hiki” akawaza huku akipiga hatua ndefu kuelekea katika chumba chenye mitambo ya kuongozea kamera za ulinzi. Kupitia kile kifaa alichokuwa amewekewa sikioni akasikia sauti ya mtu akimuita
“Ithan unanipata ? Mara moja akagundua sauti ile ilikuwa ya Rahim.Akapumua kwa nguvu na kusema kwa sauti ndogo
“nakupata Ithan.tayari nimekwisha saini na sasa hivi ninaelekea katika chumba cha kamera”
“Ok .kazi nzuri.” Akajibu Rahim
Ithan alikuwa akifahamika sana hapa gerezani hivyo hakuna mtu yeyote ambaye aliweza kushuku kitu chochote kibaya kwa kuonekana kwake akitembea maeneo yale.Kila aliyepishana naye alijua Ithan alikuwa katika moja wapo ya majukumu.
“Najua baada ya kukamilisha kazi hii nitakuwa na kesi ya kujibu lakini ni afadhali nifungwe kuliko kuiacha familia yangu iteketezwe na hawa jamaa.Ninafanya jambo hili kwa ajili ya familia yangu” akawaza Ithan huku akiukaribia mlango wa kuingilia chumba kile .
Mlango ulikuwa wazi akaingia.Watu watatu waliokuwa wamekaa vitini kila mmoja akiwa na kompyuta yake hawakusumbuka kugeuza nyuso zao na kuangalia ni nani aliyeingia.
Hallo Jimmy” akasema Ithan akimsalimu mmoja wa wale jamaa
“Ouh Ithan .karibu sana kaka.Muda mrefu haujatutembelea huku kwetu.” Akasema Jimmy akiendelea na kazi zake.Ithan akaivua ile silaha na kuishika mkononi .Mlio wa vyuma vya bunduki aliyokuwa ameishika Ithan ukawastua wote mle ndani na kuwafanya wageuke na wote hawakuamini macho yao walipojikuta wakitazamana na mtutu wa bunduki.
“Ithan acha utani na silaha” akasema Jacob
“Si utani.nawaomba wote muinuke hapo vitini” Ithan akasema kwa ukali huku akiangalia nje kama kuna mtu yeyote aliyekuwa akija pande zile.
“Nimesema Inukeni vitini haraka sana.Nitawafumua kwa risasi kama hamtatii ninavyowaambia.” Akafoka Ithan.
Wote wakainuka vitini.Walianza kuamini kwamba ule haukuwa utani tena.
Jimmy chukua ule waya na uwafunge wenzako mikono kwa nyuma “ akaamuru Ithan.Bila ubishi Ithan akachukua waya na kuanza kuwafunga wenzake mikono kwa nyuma.
“Wafunge na miguu na kisha chukua ule mkasi pale mezani chana mashati yao na uyajaze midomoni mwao” akamuru tena na bila ubishi Jimmy akawafunga miguu kwa waya halafu akachukua mkasi mdogo akachana shati la Jacob na kuchukua vipande na kuvijaza midomoni mwao..
“Fungua huo mlango wa hicho chumba kidogo na uwaweke wenzako humo ndani” Ithan akaamuru tena.
Jimmy akafungua mlango wa chumba kidogo kilichokuwa pemBeni akawavuta wenzake na kuwafungia ndani ya kile chumba.
“Nieleze chumba anachofungwa Tonny kinatumia kamera gani? Ithan akauliza
“ namba kumi na mbili.”
“ Nikitaka kukifungua chumba cha Tonny ninafanyaje?
Jimmy akamuelekeza Ithan namna ya kufanya ili kufungua mlango wa chumba cha Tonny na ghafla kama umeme Ithan akampiga na kitako cha bunduki akaanguka na kupoteza fahamu.Akamfunga mikono na miguu kwa waya halafu akamvuta na kumfungia katika chumba kile pamoja na wenzake.
Haraka haraka akakitafuta kile chombo alichoelekezwa akitafute.Jasho lilikuwa likimtoka na alikuwa akitetemeka.
“Chombo chenyewe ni hiki hapa.” Akaongea kwa sauti ndogo baada ya kukipata chombo alichokuwa akikitafuta.Akachomoa nyaya na kuzichomeka katika chombo alichopewa na Rahim na kufuata maelekezo yote.Alipomaliza akachukua kile kifaa kingine akakibandika ukutani na kukiwasha. Sekunde kama tano hivi akasikia akiitwa kupitia kile chombo kilichowekwa sikioni kwake.
“Kazi nzuri Ithan .Kwa sasa kamera zote zimeunganishwa na kompyuita zetu kwa hiyo tutakuwa tukiziongoza kutokea hapa katika gari.Ondoka sasa hapo chumbani na kwa haraka nenda katika chumba cha Tonny” Ilikuwa ni sauti ya Rahim.
Ithan akachukua bunduki yake na kutoka mle chumbani.Akaufunga mlango wa chumba kile kwa namba maalum na kwa haraka akaondoka katika chumba cha Tonny .
“Mungu atanisamehe kwa sababu nilichokifanya ni kitu kibaya sana .Ninakwenda kumuua mtuhumiwa niliyekabidhiwa jukumu la kumlinda na kuhakikisha yuko salama.Mungu anisamehe kwa sababu ninalazimika kufanya hivi kwa ajili ya kuinusuru familia yangu.” Ithan akawaza huku akikimbia kuelekea katika chumba cha Tonny.
Alihisi miguu kuisha nguvu baada ya kukifikia chumba cha Tonny.Mara akasikia sauti ya Rahim katika kile kifaa kilichokuwa sikioni
“Ithan nimekushakuona.Kazi nzuri sana.Tafadhali usijaribu kufanya jambo lolote la kipuuzi.Rudi nyuma hatua tano na unielekeze jinsi mlango wa chumba hicho unavyofunguliwa .Tutaufungua mlango huo na kisha utaingia ndani na kumpatia Tonny hiyo keki na kumshawishi aile haraka Akisha kuila utasubiri kwa dakika tano halafu tutakupa maelekezo ya mwisho kabla haujatoka hapo gerezani” Rahim akamuamuru Ithan ambaye alimpa maelekezo yote kama alivyokuwa ametaka halafu akatembea taratibu na kuelekea katika mlango wa chumba cha Tonny akasimama pale na baada ya dakika mbili mlango ukafunguka.Tonny alikuwa amekaa kitandani na mlango ulipofunguka akastuka baada ya kumuona Ithan.
“Ithan !! akaita Tonny .Hakuwa ametegemea kama angemuona Ithan asubuhi ile.
“Tonny,habari za toka jana? akasema Ithan huku akiingia mle chumbani na kwenda kuketi katika kitanda cha Tonny
“Vipi ujumbe wangu uliufikisha? Tonny akauliza
Kupitia chombo alichovaa sikioni Ithan akasikia sauti ya Rahim akimuelekeza namna ya kumjibu Tonny
“Mwambie kwamba uliufikisha ujumbe ule na umepokelewa na mkurugenzi”
“Ndiyo niliufikisha kama ulivyonielekeza na tayari umepokelewa na mkurugenzi” Ithan akasema
“nashukuru sana Ithan.Kuna jambo lolote walikueleza au ujumbe wowote walikupa uje unipatie? Tonny akauliza
Rahim akasikika tena akimwelekeza Ithan
“Mwambie kwamba wameahidi kuja kukuona ili waweze kupata maelekezo zaidi “
“Ujumbe niliopewa nikupatie ni kwamba watakuja kukuona muda si mrefu ili waweze kupata maelekezo” Ithan akasema
“Nashukuru sana Ithan .Umenisaidia sana.Naanza kuwa na matumaini ya kutoka humu gerezani.” Akasema Tonny kwa furaha huku akimpa Ithan mkono.
“Tonny nimeomba nifunguliwe geti mara moja ili niweze kukupa taarifa hizo ambazo nina imani ni za muhimu sana kwako na vile vile nimeona nikuletee keki hii.Tafadhali naomba uile keki hii mara moja ili mkaguzi akipita asiweze kuikuta kwani inaweza kuniweka matatani.Si ruhusa kuingiza gerezani vitu kama hivi bila kibali maalum cha mkuu wa gereza.” Ithan akasema na kumkabidhi Tonny boksi lile lenye ile keki nzuri.
“Ni muda mrefu sana sijaona vitu vizuri kama hivi.Ithan nashuru sana kwa kunikumbuka “.Akasema Tonny huku akiimega keki ile kwa mkono wake wa kulia.
“kazi nzuri Ithan,endelea kukaa hapo hapo mpaka atakapomaliza kuila hiyo keki” Rahim akamweleza Ithan kupitia kile chombo maalum walichokuwa wakikitumia kuwasiliana. Ithan moyo ukamwenda mbio ,jasho jembamba likamtoka.
" Ouh Mungu wangu Tonny anakwenda kufa akila hii keki..Nitafanya nini mimi wakati wameizuia familia yangu? Mungu atanisamehe sana kwa kosa hili lakini ni kwa ajili ya kuiokoa familia yangu." akawaza Ithan
USIKOSE SEHEMU IJAYO.............