RIPOTI: Mapendekezo 19 ya Kikosi Kazi cha Rais Samia kuhusu uendeshaji Siasa nchini

BARD AI

JF-Expert Member
Jul 24, 2018
3,376
8,118
1. Kuhusu Mikutano ya Hadhara na Mikutano ya Ndani ya Vyama Vya Siasa,

Kikosi Kazi kinapendekeza Sheria ya Vyama vya Siasa ifanyiwe marekebisho ili:

a) kulipatia Baraza la Vyama vya Siasa mamlaka ya kuishughulikia suala la uvunjifu wa maadili ya Vyama vya Siasa kupitia Kamati yake ya Maadili;
b) Msajili wa Vyama vya Siasa awe na mamlaka ya kuandaa mwongozo wa uchaguzi wa ndani ya Vyama vya Siasa;
c) kuweka masharti kwamba idadi ya jinsi moja katika vyombo vya maamuzi vya chama cha siasa isipungue asilimia 40; na
d) kukitaka kila chama cha siasa kuwa na sera ya ushirikishwaji wa watu wenye ulemavu katika shughuli za chama husika.

2. Kuhusu Ruzuku Kwa Vyama Vya Siasa

Kikosi Kazi kinapendekeza kuwa:

a) mfumo wa sasa wa kugawa ruzuku ya Serikali kwa Vyama vya Siasa uendelee, isipokuwa asilimia 10 ya fedha za ruzuku kwa Vyama vya Siasa zilizotengwa katika bajeti ya Serikali ya mwaka wa fedha husika, igawiwe sawa kwa vyama vyote vya siasa vyenye usajili kamili kwa mujibu wa vigezo na masharti yafuatayo:

(i) chama kiwe na usajili kamili;
(ii) chama kiwe kimefanyiwa uhakiki na Msajili wa Vyama vya Siasa na kuthibitishwa kwamba, kinakidhi vigezo vya usajili kamili;
(iii) chama kiwe kimeshiriki Uchaguzi Mkuu angalau mara mbili tangu kupata usajili kamili;
(iv) katika mwaka wa fedha uliopita, chama husika kisiwe kimepata Hati Chafu ya Mahesabu kutoka kwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali; na
(v) ruzuku itumike kwa shughuli za kuendesha Ofisi ya Makao Makuu, Ofisi Ndogo au Ofisi Kuu ya Makao Makuu ya chama cha siasa husika.

b) Sheria ya Vyama vya Siasa itamke kuwa, asilimia ishirini (20%) ya fedha za ruzuku kwa Vyama vya Siasa inayotolewa na Serikali katika mwaka wa fedha, igawiwe kwa Vyama vya Siasa vyenye Madiwani wa kuchaguliwa katika kata, kwa mujibu wa uwiano wa idadi ya Madiwani hao ambao kila chama kinao, kwani kwa sasa sheria haijatamka kiwango chochote bali imempa mamlaka Waziri Mwenye dhamana kuamua;
c) fedha za ruzuku zigawiwe kwa Vyama vya Siasa kwa mujibu wa idadi ya kura za ubunge na idadi ya wabunge ambao chama cha siasa kinao kwa wakati husika; na
d) Serikali iongeze fedha za bajeti ya Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, kwa ajili ya uendeshaji wa shughuli za Baraza la Vyama vya Siasa, ili liweze kutekeleza majukumu yake ipasavyo, ikiwemo jukumu linalopendekezwa la kusimamia Maadili ya Vyama vya Siasa.

3. Kuhusu Mfumo wa Uchaguzi

Kikosi Kazi kinapendekeza kuwa:

a) Mfumo Mseto wa Uchaguzi (Mixed Electoral System) uendelee kutumika kwa uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani. Aidha, katika uchaguzi wa Rais ili mgombea ashinde uchaguzi iwe ni lazima apate zaidi ya asilimia hamsini ya kura zote halali zilizopigwa;
b) uchaguzi wa wabunge, madiwani na uchaguzi wa Serikali za Mitaa uendelee kutumia Mfumo wa Mshindi kwa Kura Nyingi; na
c) Mfumo wa Uwiano wa kura uendelee kutumika kupata wabunge na madiwani wa viti maalum vya wanawake.

4. Kuhusu Uhuru wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi

Kikosi Kazi kinapendekeza yafuatayo:

a) Tume ya Taifa ya Uchaguzi isilazimike kufuata amri au maagizo ya mtu yeyote, idara yoyote ya Serikali, maoni ya chama chochote cha siasa, taasisi au asasi yoyote; na
b) utendaji wa Tume ya Uchaguzi uruhusiwe kuhojiwa kwenye Mahakama ya Juu pale itakapoanzishwa ili kuongeza uwajibikaji wa Tume.

5. Kuhusu Uteuzi wa Wajumbe wa Tume ya Uchaguzi

Kikosi Kazi kinapendekeza kuwa, utaratibu wa kumpata Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti na wajumbe wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi uboreshwe, ili kuongeza uwazi katika upatikanaji wao, Utaratibu huo uwe ifuatavyo:

a) kuwe na Kamati ya Uteuzi ya Wajumbe wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi itakayokuwa na wajumbe wafuatao:

i) Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye atakuwa ni Mwenyekiti;
ii) Jaji Mkuu wa Zanzibar ambaye atakuwa Makamu Mwenyekiti; iii) Kamishna wa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma ya Tanzania Bara;
iv) Mwenyekiti wa Tume ya Maadili ya Viongozi wa Umma ya Zanzibar;
v) Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu; na vi) wajumbe wengine wawili watakaoteuliwa na Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, baada ya kupendekezwa na Chama cha Wanasheria Tanganyika na Chama cha Wanasheria Zanzibar.

b) angalau wajumbe wawili wa Kamati ya Uteuzi wawe wanawake;
c) sifa za mtu kuwa Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti na mjumbe wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi ziainishwe;
d) nafasi ya mjumbe wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi itangazwe na Mtanzania yeyote mwenye sifa aruhusiwe kuwasilisha maombi kwa Kamati ya Uteuzi ya kuwa mjumbe wa Tume;
e) Kamati ya Uteuzi ifanye usaili wa watu waliowasilisha maombi ya kuwa wajumbe wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi na kupendekeza kwa Rais majina ya watu wanaostahili kuteuliwa
kuwa wajumbe wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi;
f) Kamati ya Uteuzi itawasilisha kwa Rais majina manne (4) zaidi ya idadi ya nafasi zinazohitajika kujazwa;
g) Rais ateue wajumbe wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi miongoni mwa majina yaliyowasilishwa kwake na Kamati ya Uteuzi; na
h) Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi ambaye anapaswa kuwa ni Jaji wa Mahakama Kuu au Mahakama ya Rufani aliye madarakani au mstaafu na Makamu Mwenyekiti ambaye anapaswa kuwa na sifa ya kuwa Jaji wa Mahakama Kuu au mstaafu, wateuliwe na Mheshimiwa Rais bila kufuata utaratibu wa kuomba na kusailiwa na Kamati ya Uteuzi.

6. Kuhusu Matokeo ya Uchaguzi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kutohojiwa Mahakamani


Kikosi Kazi kinapendekeza kuwa, matokeo ya uchaguzi wa Rais yahojiwe kwenye Mahakama ya Juu mara itakapoanzishwa.

7. Kuhusu Watendaji wa Tume ya Uchaguzi

Kikosi Kazi kinapendekeza kuwa:

a) Tume iendelee kutumia watumishi wa umma kusimamia uchaguzi;
b) watumishi wa umma wawajibike moja kwa moja kwa Tume ya Uchaguzi kwa masuala yanayohusu shughuli za uchaguzi kwa mujibu wa sheria;
c) wasimamizi wa uchaguzi wazingatie sheria, weledi, maadili, uwazi na ushirikishwaji wa wadau wakati wa kufanya kazi zao; na
d) wasimamizi wa uchaguzi watakaokiuka sheria na utaratibu wawajibishwe kwa mujibu wa Sheria.

8. Kuhusu Bajeti ya Tume ya Uchaguzi

Kikosi Kazi kinapendekeza kuwa, Tume ya Taifa ya Uchaguzi ipewe fedha zilizotengwa katika bajeti kwa wakati, hata baada ya uchaguzi, ili kuiwezesha kutekeleza majukumu yake ipasavyo wakati wote.

9. Kuhusu Usimamizi wa Uchaguzi

Kikosi Kazi kinapendekeza kuwa:

a) kasoro zilizojitokeza katika uchaguzi uliopita zifanyiwe kazi; na
b) Serikali ifanye utafiti wa kina kuhusu namna bora ya kusimamia Uchaguzi wa Serikali za Mitaa ili kuufanya uwe wa kidemokrasia zaidi.

10. Kuhusu Sheria Zinazosimamia Masuala ya Uchaguzi

Kikosi Kazi kinapendekeza kuwa:

a) itungwe sheria ya kusimamia shughuli za Tume ya Taifa Uchaguzi;
b) kuwepo na sheria moja ya uchaguzi itakayotumika kusimamia uchaguzi wa Rais, wabunge na madiwani, badala ya kuwa na
sheria mbili ambazo ni Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, Sura 343 na Sheria ya Uchaguzi wa Madiwani, Sura 292; na
c) maafisa wa Tume ya Uchaguzi watakaowaengua wagombea kushiriki katika uchaguzi bila kuzingatia sheria na weledi wawajibishwe kwa mujibu wa sheria.

11. Kuhusu Matumizi ya TEHAMA Katika Uchaguzi

Kikosi Kazi kinapendekeza kuwa:

a) matumizi ya TEHAMA katika mchakato wa uchaguzi yahamasishwe na kiwango chake kiongezwe;
b) zitayarishwe Kanuni mahsusi za kuratibu matumizi ya TEHAMA kwenye mchakato wa uchaguzi; na
c) kuwepo na uwekezaji wa kutosha kwenye miundombinu ya TEHAMA na usalama wake wakati wa uchaguzi.

12. Kuhusu Ushiriki wa Wanawake katika Siasa, Demokrasia na Uongozi

Kikosi Kazi kinapendekeza kuwa:

a) Sheria ya Vyama vya Siasa irekebishwe ili:

i) kuweka sharti la kila chama cha siasa kuwa na sera ya jinsia na ujumuishi wa makundi maalum katika jamii;
ii) kuweka sharti la kisheria kwamba idadi ya jinsi moja katika vyombo vya maamuzi ndani ya chama cha siasa isipungue asilimia 40;
iii) Kanuni za Usajili na Ufuatiliaji wa Vyama vya Siasa za Mwaka 2019 ziwe na vigezo vya ufuatiliaji ili kupima utekelezaji wa Sheria, katiba na kanuni za vyama vya siasa, kuhusu masuala ya jinsia na ujumuishaji wa makundi maalum ya jamii katika chama na uchaguzi; na

b) katiba za vyama ziwe na Ibara zinazoshughulikia masuala ya ukatili wa jinsia ikiwemo udhalilishaji wa wanawake;

c) kila chama cha siasa kiwe na programu maalumu kwa ajili ya kuwajengea uwezo wanawake kugombea ubunge, uwakilishi na udiwani, ikiwemo kuwa na mipango na mikakati ya kufikia usawa wa kijinsia;

d) Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa na kila chama cha siasa kiwe na dawati la jinsia litakalofanyia kazi masuala ya jinsia ndani ya vyama vya siasa;

e) utaratibu wa kuwa na viti maalum vya Wabunge, Wawakilishi na Madiwani wanawake uendelee, isipokuwa sheria ziboreshwe kuweka ukomo wa miaka kumi kwa mtu kuwa Mbunge, Mwakilishi au Diwani wa viti maalum vya wanawake. Uwakilishi huu uwe ni njia ya kupata uzoefu na kisha kupisha wanawake wengine wenye nia ya kuongeza ujuzi wa masuala ya siasa na uongozi.
f) kuwepo na mwongozo wa kisheria wa uteuzi wa wagombea na uchaguzi wa viongozi ndani ya Vyama vya Siasa, ikiwemo wabunge wa viti maalum ili kusaidia uteuzi na uchaguzi huo kuwa wa haki, uwazi na huru;

g) kila chama cha Siasa kiweke mkakati wa kuongeza idadi ya wanawake wanaogombea katika majimbo na kata za uchaguzi; na

h) kwa kuwa idadi ya wanawake ni ndogo katika Baraza la Vyama vya Siasa aongezwe mjumbe mmoja mwanamke kutoka kila chama cha siasa kuwa mjumbe wa Baraza la Vyama vya Siasa;

iv) Wabunge wa Viti Maalum vya Wanawake waitwe Wabunge wa Taifa na Madiwani, waitwe Madiwani wa Wilaya, kwa sababu wabunge hao wanatokana na kura za nchi nzima na Madiwani wanatokana na kura za Wilaya. Aidha, Sheria ya Mfuko wa Jimbo ifanyiwe marekebisho ili itambue Wabunge wa Taifa kuwa miongoni mwa Wabunge wanaofaidika na fedha za Mfuko huo.

13. Kuhusu Ushiriki wa Watu Wenye Ulemavu katika Siasa, Demokrasia na Uongozi

Kikosi Kazi kinatoa mapendekezo kuwa:

a) sheria zisizozingatia ujumuishwaji wa Watu Wenye Ulemavu na zile zinazokwamisha ushiriki wao katika siasa, demokrasia na uongozi ndani ya vyama siasa zifanyiwe maboresho;

b) Vyama vya Siasa viweke mazingira rafiki yatakayowawezesha Watu Wenye Ulemavu kufanya shughuli za kisiasa bila vikwazo;

c) kila chama cha siasa kianzishe dawati la kushughulikia masuala ya Watu Wenye Ulemavu;

d) kuwepo na nafasi maalum kwa Watu Wenye Ulemavu katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Baraza la Madiwani. Viti vya uwakilishi wa Watu Wenye Ulemavu Bungeni viwe katika uwiano utakaozingatia jinsi. Suala hili lifanyiwe kazi katika mchakato wa kutungwa kwa Katiba Mpya ili lifanyike kwa ufanisi. Hata hivyo, kwa kuanzia kila chama cha siasa kitumie utaratibu wa sasa wa viti maalum vya Wanawake kujumuisha Watu Wenye Ulemavu;

e) Sheria ya Vyama vya Siasa irekebishwe ili:

i) iweke sharti kwamba chama cha siasa kiwe na nakala ya Katiba na Kanuni zilizo katika maandishi ya breli. Aidha, katika mkutano mkuu wa chama taifa, awepo mkalimani wa lugha za alama;
ii) katazo la ubaguzi kwa Watu Wenye Ulemavu katika vyama vya siasa lililopo katika kifungu cha 9 (1)(c) cha sheria ya vyama vya siasa liwahusu pia viongozi wa vyama vya siasa; na
iii) katiba ya chama cha siasa iwe na ibara inayokitaka chama husika kiwe na programu za kuwajengea uwezo watu wenye ulemavu kushiriki kikamilifu katika michakato ya kisiasa, demokrasia na uongozi ndani na nje ya chama.

f) zitungwe Kanuni za utekelezaji wa Kifungu cha 6A (2) cha Sheria ya Vyama vya Siasa kinachoelekeza chama cha siasa kuzingatia suala la ujumuishwaji wa Watu Wenye Ulemavu katika masuala ya vyama vya siasa na demokrasia;

g) vyombo vya habari viandae vipindi maalum vya elimu ya uraia vinavyoeleza haki na mahitaji ya Watu Wenye Ulemavu;

h) Serikali iboreshe Makazi maalum ya Wazee na Watu Wenye Ulemavu;

i) suala la kuondoa ombaomba mitaani lifanyiwe kazi kwa ufanisi, kwani linaleta taswira kuwa Watu Wenye Walemavu ni maskini; na

j) elimu kuhusu masuala yote yanayohusiana na ulemavu na madhara yake ikiwemo afya ya uzazi, kinga kwa ajali, maradhi na njia bora za utabibu iongezwe ili kupunguza idadi na madhara
ya ulemavu.

14. Kuhusu Ushiriki wa Vijana katika Siasa, Demokrasia na Uongozi

Kikosi Kazi kinapendekeza kuwa juhudi zinazofanywa na Serikali kuhusu ushiriki wa vijana katika siasa, demokrasia, uongozi, uchumi, ulinzi na usalama wa nchi yetu ziendelee na mikakati mipya ibuniwe ili kuongeza ufanisi na tija.

15. Kuhusu utoaji wa Elimu ya Uraia ikiwemo elimu ya mpiga kura nchini

Kikosi Kazi kinatoa mapendekezo yafuatayo:

a) Serikali iandae mwongozo wa kitaifa, mpango kazi na mikakati ya utoaji elimu ya uraia, ili utoaji wa elimu hiyo uzingatie vipaumbele vya taifa na kuwa na uelewa wa pamoja wa walengwa;

b) elimu ya uraia ikiwemo elimu ya mpiga kura ifundishwe katika ngazi zote za mfumo wa elimu kuanzia shule za awali mpaka katika vyuo vya elimu ya juu. Aidha, mtaala wa elimu ujumuishi masuala ya elimu ya uraia;

c) Serikali na wadau wengine waongeze kiwango cha ufadhili katika kutoa elimu ya uraia ikiwemo elimu ya mpiga kura, ili kukabiliana na upungufu wa rasilimali, watu, fedha na vifaa katika kutoa elimu hiyo;

d) elimu ya mpiga kura itolewe kipindi chote siyo cha uchaguzi pekee, ili kuongeza muda wa kutoa elimu hiyo kuwezesha kuwafikia walengwa wengi zaidi; na

e) uratibu na ufuatiliaji wa elimu ya uraia unaofanywa na taasisi mbalimbali kwa mujibu wa sheria uendelee, isipokuwa ufanywe katika hali isiyokwamisha juhudi za kuwafikia watanzania wengi kupata elimu hiyo.

16. Kuhusu suala la Rushwa na Maadili katika siasa na uchaguzi

Kikosi Kazi kinapendekeza kuwa:

a) suala la rushwa litamkwe katika Katiba, ili wananchi watambue kuwa vitendo vya rushwa havitavumiliwa wala kuonewa muhali. Pendekezo hili lifanyiwe kazi katika mchakato wa kutungwa kwa Katiba Mpya ili litekelezwe kwa ufanisi;

b) Sheria ya vyama vya Siasa Sura 258 irekebishwe ili:

i) kuweka sharti kwamba, katiba ya chama cha siasa iwe na adhabu ya kumwondoa katika mchakato wa uchaguzi, mtia nia au mgombea aliyedhaminiwa na chama, endapo atathibitika kujihusisha na vitendo vya rushwa;
ii) Msajili wa Vyama vya Siasa apewe mamlaka ya kuandaa mwongozo wa kufuatilia mchakato wa uteuzi wa wagombea na uchaguzi wa viongozi, ndani ya Vyama vya Siasa; na
iii) kukitaka kila chama cha siasa kuwa na Kanuni za Maadili, zitakazodhibiti ukiukwaji wa maadili ndani ya chama, ikiwemo mwanachama kujihusisha na vitendo vya rushwa. Kanuni hizo ziweke utaratibu wa kushughulikia ukiukwaji wa maadili na adhabu, ikiwemo onyo, karipio, faini, kuvuliwa
ujumbe wa kikao husika, kutoruhusiwa kugombea uongozi ndani ya miaka kumi tangu alipopatikana na hatia, kusimamishwa au kufukuzwa uanachama.

c) Sheria ya Gharama za Uchaguzi irekebishwe ili:

i) kutoa adhabu kwa mgombea atakayeshindwa kufanya marejesho ya gharama za uchaguzi badala ya kukiadhibu chama cha siasa;
ii) vitendo vinavyokatazwa katika sheria hiyo kuwa na sifa ya kuwa kosa la jinai;

iii) nyaraka za uthibitisho wa matumizi ya gharama za uchaguzi zibaki katika chama cha siasa husika badala ya kuwasilishwa kwa Msajili wa vyama vya siasa; na
iv) kuondoa upungufu mwingine wowote ambao ni kikwazo katika kuzuia na kupambana na rushwa katika mchakato wa uchaguzi;

d) Sheria ya Ushahidi, Sura ya 6 irekebishwe kutambua Ushahidi wa mazingira (Circumstantial Evidence), ili uweze kutumika Mahakamani kuthibitisha makosa ya rushwa;

e) Sheria za Uchaguzi zirekebishwe kuweka masharti kwamba, mgombea atakayethibitika kujihusisha na vitendo vya rushwa aondolewe sifa ya kugombea katika uchaguzi wowote kwa miaka 10 mfululizo;


f) Sheria ya Watoa Taarifa na Ulinzi wa Mashahidi Sura ya 446 ifanyiwe marekebisho ili kuongeza kinga kwa mtoa taarifa wa siri;

g) Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa irekebishwe, ili kumwajibisha pia mtu anayetoa rushwa ya ngono. Aidha, adhabu zinazotolewa katika sheria hiyo kuhusu kosa la rushwa ya ngono ziendane na zile zilizopo katika Sheria ya Makosa ya Kujamiiana (SOSPA),

h) mitaala katika shule za msingi na sekondari iwe na moduli ya rushwa, badala ya kutajwa kama mengineyo kwenye somo la uraia;

i) matumizi ya teknolojia katika kuzuia na kupambana na rushwa yaongezwe, ili kuibua ushahidi uliojificha kwa kutumia utaalam wa utambuzi (exhumation of hidden evidence through forensic expertise);

j) Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa isiingiliwe kisiasa wala kiutawala kinapotimiza majukumu yake ilhali kinafuata sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa kisheria;

k) kujenga silka na hulka ya uadilifu kwenye kaya (familia) hadi ngazi ya Taifa kwa njia zifuatazo:

i) kuwa na mpango na mkakati mahususi wa kitaifa wa kukuza uadilifu;
ii) kudhibiti utandawazi ili kuepusha wananchi kuiga mambo ya nchi nyingine ambayo hayaendani na utamaduni na mazingira ya nchi yetu;
iii) kuheshimu na kufuata mila na desturi za asili zinazofaa; iv) viongozi wa dini waendelee kutekeleza majukumu yao ipasavyo;
v) familia na shule ziweke mkazo katika malezi ya watoto kimaadili.
vi) shule za msingi na sekondari za umma na binafsi ambazo siyo seminari zitakiwe kuwa na vipindi vya dini, ili kuruhusu watoto kupata elimu ya dini ambayo kimsingi ni njia ya
kujenga uadilifu; na vii) maisha ya kifamilia yapewe kipaumbele na msisitizo
wakutosha;

l) Somo la uraia na maadili linalofundishwa shule za msingi na sekondari liwekewe mkazo wa kutosha na lifundishwe katika ngazi zote za elimu.

17. Kuhusu mfumo wa maridhiano ili kudumisha haki, amani, utulivu na umoja wa kitaifa nchini

Kikosi Kazi kinatoa mapendekezo kuwa:

a) kuanzishwe utaratibu wa mijadala kila mwaka (Annual State of Politics Conference) itakayohusisha viongozi wakubwa wa kitaifa wa dola na Vyama vya Siasa ambapo mjadala utalenga kutazama hali ya ushindani wa kisiasa na kuimarisha mshikamano miongoni mwa wanasiasa na Vyama vya Siasa. Mkutano huo ufanyike katika Siku ya Demokrasia nchini;

b) mahakama iwe na mamlaka ya mwisho ya kuamua pale maridhiano yatakapokuwa yamekwama kwa pande husika; na

c) kwa kuwa nchi yetu ina amini katika Utawala wa Sheria na utoaji wa haki, hivyo, vyombo vinavyosimamia utatuzi wa migogoro kama Mahakama, Tume ya Haki za Binadamu, Tume ya Maadili na Kamati ya Amani ya Kitaifa ya Viongozi wa Dini na viongozi wa dini mbalimbali, ni lazima vifanye kazi kwa uadilifu na uaminifu wakati wote na hasa wakati wa migogoro inapotokea kupitia utaratibu huu wananchi watajenga imani kwa vyombo hivyo kama watoaji wa haki katika migogoro.

18. Kuhusu mawasiliano kwa umma, vyombo vya habari na siasa

Kikosi Kazi kinatoa mapendekezo kuwa:

a) wanahabari wenyewe waunde chombo cha kusimamia maadili ya wanahabari na vyombo vya Habari;

b) uwekwe utaratibu wa kusimamia utekelezaji wa Sheria husika, ili vyombo vya habari vya umma vitoe fursa sawa ya Kutangaza habari za wagombea na Vyama vya Siasa wakati wa uchaguzi bila upendeleo;

c) ziandaliwe Kanuni zitakazoelekeza vyombo vya habari kuheshimu maadili ya taaluma ya uandishi wa habari, ikiwemo mwanahabari kuhakikisha anahakiki habari aliyoipata kutoka pande zinazohusika, kabla ya kutangaza au kuchapisha habari husika;

d) wagombea, viongozi na wanachama wa Vyama vya Siasa waepuke kutumia lugha za kuudhi, kejeli, uchochezi na matusi kupitia vyombo vya habari au mikutano ya hadhara;

e) sheria husika irekebishwe, ili kuondoa mamlaka ya Mkurugenzi wa Idara ya Habari Maelezo kufungia vyombo vya habari bila kuwepo mchakato wa wazi wa kuviwajibisha;

f) ili kuruhusu wananchi kushiriki ipasavyo katika shughuli za maendeleo na kuwafikia wananchi wengi zaidi wakati na baada ya uchaguzi, ni vyema wanasiasa wakafanya siasa kupitia vyombo vya habari kwa kufanya mahojiano, vipindi maalum, kushiriki mijadala na mazungumzo kama ilivyokuwa katika nchi nyingi duniani; na

g) sheria zinazoratibu uhuru wa habari ziboreshwe ili kukuza uhuru wa Habari na demokrasia nchini.

19. Kuhusu Katiba Mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Kikosi Kazi kinapendekeza kukamilishwa kwa mchakato wa kupata Katiba Mpya ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia hatua sita zifuatazo:

Hatua ya Kwanza: Mjadala wa Kitaifa ili kupata Muafaka katika Masuala ya Msingi

Kuanzishwa kwa mjadala wa kitaifa katika masuala ya msingi, ili kupata muafaka wa kitaifa kabla ya kuanza mchakato wa kuandika Katiba mpya. Mjadala huu ufanyike kwa ushiriki mpana wa wananchi. Masuala ya msingi yanajumuisha muundo wa Muungano, madaraka ya Rais, mfumo wa uchaguzi, madaraka ya Serikali za Mitaa, rushwa na maadili na mengineyo yatakayojitokeza.

Hatua ya Pili: Kuhuisha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba na Sheria ya Kura ya Maoni

Kuhuisha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba na Sheria ya Kura ya Maoni ili kuweka mahitaji ya sasa, yakiwemo kuainisha muda wa mchakato mzima, kutambua kuanzishwa kwa Jopo la Wataalam na kuainisha misingi ya kuzingatiwa katika mchakato wa mabadiliko ya Katiba. Aidha, kuwepo na ushirikishwaji mpana wa wananchi katika mchakato wa kuhuisha Sheria hiyo, kwa kufuata taratibu za utungaji wa sheria nchini.

Hatua ya Tatu: Kuundwa kwa Jopo la Wataalam Baada ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba kuhuishwa,

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kushauriana na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi aunde Jopo la Wataalam, litakalopitia na kuoanisha Katiba Inayopendekezwa na
Rasimu ya Pili ya Katiba iliyoandaliwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba ya Mwaka 2011 na kuandaa Rasimu ya Katiba Mpya itakayowasilishwa Bungeni.

Kikosi Kazi kinapendekeza kuwa, katika utekelezaji wa majukumu yake, Jopo la Wataalam lizingatie masuala yafuatayo:

a) kufanya mapitio ya Katiba Inayopendekezwa ya Mwaka 2014, kwa kuzingatia hali ya sasa ya kisiasa, kiuchumi na kijamii;

b) kurejea nyaraka zifuatazo, Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mwaka 1977, Katiba ya Zanzibar ya Mwaka 1984, Rasimu ya Pili ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba ya Mwaka 2011 na Ripoti ya Serikali kuhusu masuala muhimu ya kitaifa yaliyojadiliwa katika mjadala wa kitaifa wa Katiba; na

d) masuala muhimu ya kitaifa ambayo ni:

i) mfumo wa kiutawala wa kijamhuri;
ii) uwepo wa Jamhuri ya Muungano;
iii) uwepo wa Serikali, Bunge na Mahakama;
iv) uwepo wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar;
v) uwepo wa umoja wa kitaifa, amani na utulivu;
vi) uwepo wa uchaguzi wa kidemokrasia katika vipindi maalum na
kuzingatiwa kwa haki ya kila mtu mwenye sifa ya kupiga na kupigiwa kura;
vii) uhifadhi wa Haki za Binadamu na utawala wa sheria;na
viii) uwepo wa Serikali isiyofungamana na dini.

Hatua ya Nne: Rasimu ya Katiba Mpya Kupitishwa na Bunge

Baada ya Jopo la Wataalam kukamilisha kazi ya kuandaa Rasimu ya Katiba, itawasilishwa katika Bunge la Jamhuri ya Muungano kwa ajili ya kujadiliwa na kuipitisha kuwa Katiba Inayopendekezwa. Majukumu ya Bunge yatabainishwa katika Sheria ya Mabadiliko ya Katiba.

Hatua ya Tano: Elimu ya Uraia kuhusu Katiba Mpya

Kutoa elimu ya uraia kuhusu Katiba Inayopendekezwa kabla ya kupigiwa kura, ili wananchi waifahamu Katiba husika na kuwaandaa kupiga kura ya maoni kwa amani na utulivu.

Hatua ya Sita: Kura ya Maoni

Wananchi kupigia kura ya maoni Katiba Inayopendekezwa.
 
Tume ya uchaguzi: rais asichague bali atangaze yule aliyeshinda usability.
Bunge liwe bunge maalum la wananchi na sio la jamhùri, wanasiasa wakirudi 25%.
Katiba mpya: muda umefika kuingiza swala la serikali za majimbo kusogeza huduma na maamuzi majimboni badala ya kutegemea dodoma/raisi kwa maamuzi yote.
 
... mbona hawajazungumzia suala la mgombea binafsi?
... sijaona suala la vyama kuungana - muhimu sana hili.

Kikosi Kazi kimekaa kichama zaidi kuliko kuwa huru!
 
Naona mapungufu kadhaa kwenye hiyo ripoti.

- Hapo kwenye mikutano ya vyama vya siasa, naona kabisa hivyo vilivyopendekezwa vinaenda kuingilia uhuru/mamlaka ya vyama husika yaliyowekwa kikatiba na msajili wa vyama akayapitisha kutumiwa na vyama husika.

Mfano wa hili, ni pendekezo la kikosi kazi kumtaka msajili wa vyama kuandaa muongozo wa uchaguzi kwa vyama husika.

- Pia, kikosi kinasema mchakato wa kumpata Mwenyekiti na M/mwenyekiti wa tume ya uchaguzi uboreshwe, lakini hakijasema huyo mwenyekiti na makamu wake watapatikana vipi, wao wamekimbilia tu kuonesha vipi wajumbe wa hiyo tume wapatikane.

- Zaidi, naona kikosi kazi kimefeli kabisa pale kilipopendekeza watumishi wa umma kuendelea kusimamia uchaguzi, hao watumishi wa umma ambao ni waajiriwa wa serikali ya chama kilichopo madarakani hawawezi kuvitendea haki vyama vingine vya siasa, kwa kupenda wenyewe, au kushurutishwa, mifano ya hili ipo.

- Mwisho, kikosi kazi kimezungumzia "Mahakama ya Juu" ambapo hii imetakiwa kusikiliza kesi ya kupinga matokeo ya Urais, na majaji wake pia kutakiwa kuhusika kuteua wajumbe wa Tume ya Uchaguzi.

Hata hivyo, hii ripoti ya Kikosi Kazi imeshindwa kutuambia, hao majaji wa hiyo mahakama watapatikana vipi, ili tuone kama mchakato wa kupatikana kwao hautaingiliana na majukumu ya Rais aliyepo madarakani, ambaye kimsingi nae ni mwenyekiti wa chama cha siasa.
 
Utitiri wa vyama vya siasa ni usanii na utapeli mwengine kwa wananchi ambao tume haikuja na suluhisho lake.
 
Mapendekezo ya tume kimsingi yanalenga kudhibiti kila chamq cha siasa kiwe chini ya chama tawala kupitia msajili na baraza la vyama. Kuongeza mzigo kwa wananchi yaani qsilimia kumi ya bajeti iende kuliwa na vyama huku wanafunzi wakikaa chini kwa ukosefu wa madawati, hospitali hazina dawa za kutosha, hakuna maji safi kwa wananchi wote hasa vijijini n.k. Fikiria kwa bajeti ya trilioni 40, trilioni nne (=10%) zipewe vyama ili wqjanja watanue huku wananchi wakiteseka halqfu tunaambiwa hakuna fedha tuchangie huduma! Ruzuku inatakiwa ifutwe kabisa kila chama kijitegemee.

Mgombea binafsi wamekwepa kumzungumzia na tume kuwa na wafanyakazi wake wenyewe wamepinga..
 
Tusubiri utekelezaji wa kilichopendekezwa, maana hata tukiibua mapya wakati yalipendekezwa hatujua kama yamekubaliwa ni kujilisha upepo tuu, Hii ni afrika makaratasi na vimemo ni vingi kuliko ukamilishaji wa tunayoyatarajia.
 
Back
Top Bottom