Yabainika aliwasiliana na mkurugenzi wake mwaka 2001
SAKATA la Kampuni yenye utata ya Richmond Development LCC iliyoshindwa kuleta jenereta za kuzalisha umeme wa dharura, linazidi kuchukua sura mpya kila kukicha, Tanzania Daima Jumatano imebaini.
Baada ya sakata hilo kulitikisa taifa kwa zaidi ya miaka miwili sasa na hata kufikia hatua ya kusababisha aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa na mawaziri wengine wawili kujiuzulu Februari mwaka jana, sakata hilo sasa linaonekana kutaka kubadili mwelekeo na kuanza kumuandama Spika wa Bunge, Samuel Sitta.
Kubadilika sura kwa sakata hilo hivi sasa, kunatokana na kubainika kwa taarifa za kuwapo kwa mawasiliano ya barua yenye malengo ya kutaka kuja kuwekeza kwa kampuni hiyo hapa nchini, yaliyokuwa yakifanywa kati ya mkurugenzi wake, Mohamed Gire na Sitta mwaka 2001, wakati huo akiwa ni Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji nchini (TIC)!
Habari za kuaminika zinaeleza kuwa, kuvuja kwa taarifa hizi mpya ambazo tayari zimeshawekwa katika mtandao wa intaneti, kumepokewa kwa shangwe kubwa na kundi la majeruhi wa sakata la Richmond, ambao wanaiona hatua hii kuwa mwanzo wa ukweli halisi kuhusu sakata hilo, ambalo hatima yake ingali haijulikani hadi leo.
Kwa mujibu wa habari hizo, mawasiliano hayo kati ya TIC na serikali kwa upande mmoja na kinara huyo wa Richmond anayeishi Marekani, yaliwahi kusababisha ujumbe wa aliyekuwa Waziri Mkuu, Frederick Sumaye uliomjumuisha Sitta kwa wadhifa wake wa ukurugenzi wa taasisi yenye dhamana ya uwekezaji, kupata mualiko wa chakula cha mchana katika Jiji la Houston, Marekani katika kipindi cha kati ya mwaka 2001 na 2002.
Kuvuja kwa habari hizi, kwa mara ya kwanza kunathibitisha uvumi wa siku nyingi kwamba, Kampuni ya Richmond ilianza kupenya nchini hata kufikia hatua ya kufanya mawasiliano na viongozi wa juu wa serikali ya awamu ya tatu iliyokuwa ikiongozwa na Rais mstaafu Benjamin Mkapa, wakiwamo Sumaye na Sitta mapema mwaka 2001.
Maandishi yaliyoko katika fax iliyoandikwa na kusainiwa na Sitta mwenyewe, Oktoba 27 mwaka 2001 kwenda kwa Gire, yanaonyesha kuwapo kwa mawasiliano ya kabla kati ya watu wawili hao, ambayo pia yalimhusisha ofisa wa tatu wa serikali anayetajwa kwa jina moja tu la Sela, mtu ambaye kumbukumbu zinaonyesha alikuwa ni mmoja wa wasaidizi wa karibu wa aliyekuwa Waziri Mkuu, Sumaye.
Katika fax yake hiyo (ambayo imebandikwa ukurasa wa kwanza wa gazeti hili), Sitta anaonekana akimuelekeza Gire kuandaa barua ambayo itakuwa na maneno atakayochagua yeye mwenyewe, na akamwambia kuhusu kuwa na taarifa za mkurugenzi huyo wa Richmond kuwasiliana pia na Sela.
Hata hivyo, pamoja na Sitta kuonekana kuridhia uamuzi wa Sela kuendelea kulishughulikia suala wanalowasiliana na Gire kwa upande wake, bado katika sehemu moja anamtaka mkurugenzi huyo wa Richmond kuhakikisha kuwa anampa taarifa kuhusu mawasiliano yao.
Ingawa haielezwi katika barua hiyo ni mradi gani hasa wa uwekezaji, mkurugenzi huyo alikuwa akitaka kuwekeza akipitia TIC.
Kumbukumbu zinaonyesha kwamba, kabla ya kuonyesha dhamira ya kuwekeza katika umeme wa dharura, Richmond ilijaribu kuingia katika zabuni ya kufunga bomba la mafuta kutoka Dar es Salaam hadi Mwanza wakati wa serikali ya awamu ya tatu.
Tanzania Daima Jumatano ilipowasiliana na Mkurugenzi Mtendaji wa TIC, Emmanuel ole Naiko ofisini kwake jijini Dar es Salaam na kumuonyesha nakala ya barua inayodaiwa kutumwa kwenda kwa Gire na iwapo walikuwa na nakala ya mawasiliano hayo, mbali ya kukiri kuitambua sahihi ya Sitta na namba ya simu inayoonekana kuwa ni ya kwao, alisema ni jambo gumu kusema haraka haraka iwapo kulikuwa na nakala hapo kwao.
Ninachoweza kusema hapa ni kwamba, sijaziona taarifa hizi katika mtandao, ila sahihi ninayoiona hapa ni kweli ni ya Sitta, hata lugha iliyotumika inaonekana kuwa ni yake, kwani unajua alikuwa bosi wangu hapa kwa miaka mingi, alisema Ole Naiko ambaye alilazimika kufanya kwanza mawasiliano na wasaidizi wake kadhaa kabla ya kuthibitisha kwamba hata namba ya fax ilikuwa ni ya hapo ofisini.
Juhudi za gazeti hili kuwasiliana na Sitta mwenyewe na kupata maelezo yake kuhusu kuwapo kwa mawasiliano kati yake na mkurugenzi huyo wa Richmond hatimaye zilifanikiwa jana, baada ya kukwama kwa wiki nzima iliyopita.
Akizungumza kwa simu jana asubuhi, Sitta alikiri kuwa na kumbukumbu za kuwahi kuwasiliana kwa njia ya fax na Gire na kwamba wakati huo mkurugenzi huyo wa Richmond alikuwa anakusudia kuwekeza katika bomba la mafuta akiwakilishwa na wakala wake aliyemtaja kwa jina moja tu la Muro.
Mbali ya hilo, Sitta alisema wakati huo ulikuwa ni wajibu wake kama mkurugenzi mtendaji wa TIC kufanya mazungumzo na watu mbalimbali waliokuwa wakionyesha nia ya kuja kuwekeza hapa nchini, akiwamo huyo Gire kwa nia njema na si kwa malengo ya kifisadi.
Nakumbuka kuwasiliana naye...wakati ule alikuwa akijifanya akitaka kuwekeza katika bomba la mafuta na agent wake alikuwa Mr. Muro... Mazungumzo na mawasiliano yote tuliyafanya kwa nia njema kabisa ya uwekezaji, alisema Sitta alipoulizwa iwapo ni kweli taarifa za kwenye mtandao wa intaneti na nakala ya barua yenye sahihi yake vilikuwa ni vyake.
Mbali ya hilo, Sitta alikiri pia kuwapo kwa mawasiliano hayo kati ya Gire na Ofisi ya Waziri Mkuu, wakati huo Sumaye, na kwamba alikuwa hana kumbukumbu sahihi iwapo kampuni aliyokuwa akitaka ije kuwekeza ilikuwa ni Richmond au nyingine.
Siwezi kukumbuka iwapo wakati huo huyo Gire alikuwa akitumia jina la Richmond au la. Unajua wakati huo kwa mwaka tulikuwa tukizungumza na makampuni ya uwekezaji hadi 500, hivyo si rahisi kukumbuka details ndogo ndogo, alisema Sitta.
Akiendelea alisema, ni jambo lisiloingia akilini kwa maadui zake kutaka kuyatumia mawasiliano aliyoyafanya na Gire wakati huo, tena kwa nia njema, na kuyahusisha na ufisadi kwa sababu tu ya jambo baya alilokuja kulifanya miaka saba baadaye.
Sitta alikiri pia kwamba, wakati akiwa katika msafara wa Waziri Mkuu Sumaye (wakati huo) kwenye ziara yake ya Marekani, Gire alikuwa miongoni mwa kikundi cha Watanzania 30 waliokwenda kuwapokea uwanja wa ndege wakati walipofika Houston.
Alisema wakiwa nchini humo kwa ziara ya kuhamasisha uwekezaji nchini, Gire ambaye hivi sasa hawezi hata kumkumbuka kwa sura wakikutana, aliwaandalia chakula cha mchana kwa ajili ya Sumaye na ujumbe wake.
Tukiwa pale Houston, Gire nadhani alitu-offer (alituandalia) ujumbe wa Waziri Mkuu, ambao mimi nilikuwa miongoni mwao chakula, sikumbuki kama ni cha usiku au cha mchana... No kilikuwa ni chakula cha mchana. Na mazungumzo pale yalikuwa ni ya kawaida tu. Ni makosa kuunganisha vitu vilivyofanywa kwa nia njema na ufisadi, alisema Sitta.
Source: Tanzania Daima