RC Chalamila atangaza vita na malori kuegeshwa barabarani

BARD AI

JF-Expert Member
Jul 24, 2018
3,376
8,118
Baada ya leo kuripotiwa habari juu ya uegeshaji holela wa malori unavyosumbua wakazi wa Dar es Salaam, operesheni maalumu ya kuyaondoa malori hayo imetangazwa kuanzia kesho Jumanne Februari 6, 2024.

Wakati operesheni hiyo ikitangazwa kuanza, magari yao yameelekezwa kutumia sehemu maalumu zilizotengwa kwa ajili ya maegesho likiwemo eneo la Kibanda cha Mkaa, Mbezi.

Hayo yamesemwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila alipotembelea barabara ya Mandela eneo la Uhasibu kuangalia uegeshaji holela wa malori unavyofanywa, jambo ambalo pia linatajwa kuchangia uharibifu wa barabara.

Wakati operesheni hiyo ikitangazwa, Chalamila pia anatarajiwa kukutana na wamiliki wa bandari kavu kesho Jumanne, akiambatana na Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroad) na Jeshi la Polisi kikosi cha usalama barabarani.

Chalamila amesema kwa kawaida, kila mmiliki wa bandari kavu, lazima awe na eneo la maegesho ya magari, kwa sababu mtu hawezi kununua lori pasipo kuwa na eneo la kuliegesha na badala yake barabara ikatumika kwa kazi hiyo.

Amesema barabara hizo za dharura siyo za wamiliki wa malori bali kwa ajili ya matumizi ya Watanzania, huku akieleza kwa msongamano uliopo ndani ya jiji la Dar es Salaam si vyema barabara hizo zikazibwa.
“Hizi njia nazo zikijaa itafika wakati ambao mgonjwa anatakiwa kuwahishwa hospitali, tuna majambazi wamevamia mahali tunahitaji kuwakamata kwa foleni hizi na malori kuegesha ovyoovyo itafika kipindi tutashindwa,” amesema Chalamila.

Mbali na kushindwa kutoa usaidizi wa dharura unapohitajika, pia amesema kuendelea kuwapo katika eneo hilo kunaweza kutumika kama maficho ya watu wenye nia ovu.

“Tumieni maeneo yaliyopangwa kwa ajili ya kuegesha magari hayo na wale wenye maeneo yenu mpaki katika maeneo husika,” amesema mkuu huyo wa mkoa huku akieleza kuwa hivi karibuni utanuzi wa Barabaara ya Mandela utaanza ili kujenga njia za magari yaendayo haraka kuelekea Ubungo.

Hata hivyo, alipozungumzia suala hilo kwa simu leo, Katibu Mkuu wa Chama cha Wamiliki wa Malori Tanzania (Tamstoa), Issa John amesema mara nyingi wanaegesha malori katika maeneo hayo kwa ajili ya kusubiri kushusha mizigo jambo ambalo hawalipendi kwa sababu linawaongezea gharama.

"Sasa hivi wengi wanalazimisha kuegesha katika maeneo yenye bandari kavu, sehemu za kawaida hakuna na kesho (leo) tutakuwa na mkutano na idara zote za Serikali zinazohusika nasi ikiwemo Latra tutakapozungumza huko tutapata majibu mazuri," amesema John.

Naye Mkuu wa Idara ya Mipango wa Tanroads Dar es Salaam, Clever Akilimali amesema malori yanayopaki maeneo hayo yanatakiwa kuondoka ili kuruhusu watumiaji wengine kutumia barabara hizo.

Amewataka wenye malori yanayoingia mjini waegeshe maeneo maalumu, huku akieleza hatua za kisheria zitachukuliwa kwa watakaokamatwa, kwani barabara hizo zinatengenezwa kwa gharama kubwa.

“Lori linapoegeshwa linakuwa zito linaharibu barabara, hii imetengenezwa kwa ajili ya gari kupita na si kuegesha ndiyo maana sehemu za maegesho tunaweka zege. Mpaka sasa kuna eneo Kibanda cha Mkaa mtu anaweza kuegesha na tuko hatua za mwisho kukamilisha maegesho yanayoweza kuchukua magari zaidi ya 800 eneo la Kiluvya,” amesema Akilimali.

Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Sixtus Mapunda amesema tangu Novemba mwaka jana Tanroad ilisitisha vibali kwa ajili ya kutumia barabara kwa ajili ya maegesho.

“Bandari wameruhusu eneo la EPZA kutumika kama maegesho, eneo linaweza kubeba magari zaidi ya 350, sasa kwenye operesheni tunayokwenda kuanza kesho (leo) hatutarajii kuona lori lolote likiwa limeegeshwa pembezoni mwa barabara,” amesema Mapunda na kuongeza:

“Sehemu ya kupaki ipo, wenye bandari kavu waegeshe katika maeneo yao, gari tutakayoikuta barabarani tutaiona kama uchafu mwingine na tutaipeleka kwenda kuitupa kama uchafu,” amesema.

Katika hatua nyingine, Chalamila amesema wanatarajia kuja na mpango wa kuzuia shughuli za binadamu kandokando ya mito, kwa sababu inafanya mito kutanuka na mvua zinaponyesha inasababisha athari kwa miundombinu.

Hilo litaenda sambamba na mpango wa kuzuia watu kujenga kwenye mabonde ili kuondoa malalamiko ya kuhitaji msaada mafuriko yanapotokea.

“Nimekuwa nikisikika kuongea kama kwa utani lakini ipo siku baada ya utani kueleweka kwa kila mtu tutaanza operesheni maalumu ya kuondoa makazi yote kwenye mabonde, kwani athari zikija wanaanza kupiga kelele wanaomba msaada, mimi nilipiga kelele kuomba msaada kabla ya mvua,” amesema Chalamila.

Amesema mvua kubwa iliyonyesha jijini hapa ilimfanya kulala siku mbili katika maeneo yenye hitilafu huku barabara zaidi ya 13 zikihaaribiwa na maji na kufanya mawasiliano kukatika.

MWANANCHI
 
Back
Top Bottom