Rais Mwinyi mgeni rasmi katika Mjadala wa Demokrasia kuelekea uchaguzi wa Serikali za Mitaa, Vijiji na Vitongoji 2024 na Uchaguzi Mkuu 2025

Roving Journalist

JF Roving Journalist
Apr 18, 2017
2,913
12,189
Mkutano wa kitaifa wa wadau kujadili hali ya demokrasia nchini kuelekea uchaguzi mkuu wa serikali za mitaa, vijiji na vitongoji 2024 na uchaguzi mkuu 2025
1I2A4121.jpg

Mkutano umeandaliwa Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD) kwa lengo la kujadili hatua iliyofikiwa katika utekelezaji wa Maazimio ya Kongamano la Kitaifa la Maridhiano, Haki na Amani na kuimarisha mapendekezo ya awali yaliyotolewa na Wadau ili kuboresha Mazingira ya Kisiasa wakati wa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2024 na Uchaguzi Mkuu 2025

Mkutano unahudhuriwa na Mwenyekiti wa Kituo cha Demokrasia (TCD) Prof. Ibrahim Lipumba, Viongozi na Wawakilishi wa Vyama 19 vya Siasa, Viongozi kutoka Serikalini, Mabalozi na Wadau wa Demokrasia. Kwa siku ya pili (August 23) mgeni rasmi ni Rais wa Zanzibar, Dr Hussein Mwinyi.

Mwanzo wa Mjadala.

Wazungumzaji ni wawakilishi kutoka CCM, CUF, CHADEMA, NCCR-Mageuzi, ACT-Wazalendo, CHAUMMA, NEC, ZEC, Msajili wa vyama vya siasa. Mjadala ni kuhusu Nini kifanyike ili kuboresha Uchaguzi ujao(2024/25) ili ziwe huru na haki.

Mzungumzaji wa Awali ni Zitto Kabwe

Sheria ya Uchaguzi ihusishe Chaguzi zote
Ili uchaguzi uwe huru na haki inabidi mageuzi makubwa kwenye sheria zinazosimamia uchaguzi. Hata hivyo kumekuwa na mkwamo kwenye mchakato wa kupata katiba mpya. Hadi sasa hakuna hatua iliyotekelezwa ya kuwa na katiba mpya, hadi sasa hakuna kamati ya wataalamu ili kuanisha katiba ya sasa na rasimu ya Warioba ili kuja na kinachotakiwa.

Inawezekana mchakato wa katiba ukawa mrefu, lakini tunaweza kuwa na sheria mpya ya uchaguzi. Inawezekana katiba ikasema Rais wa JMT atateua wajumbe wasiozidi saba wa uchaguzi, lakini katiba haijasema atateuaje, kwa hivyo sheria ya uchaguzi itasema kuhusu Rais atateuaje bila kuvunja utaratibu. Kwamba mchakato wa jopo utakuwa wa watu kuomba na kutakuwa na usaili na kisha rais kuteua. Inachotakiwa ni wadau kukubaliana. Hii itafanya kusiwe na haja ya tume huru na uchaguzi.

Tukiendelea kuwa na mkwamo wa hoja tutakaa hadi 2025 na hakutakuwa na katiba mpya.

Zitto amesema hakuna sababu ya kwenda kuelimisha jamii kuhusu katiba, haina mantiki. Mchakato wa kutoa elimu kuhusu katiba kabla ya kubadili katiba umeundwa na serikali kupitia waziri wa katiba na sheria na utaanza mwezi Septemba 2023. Zitto amesema suala hilo linaleta utata kuhusu utayari.

Sheria ya uchaguzi inabidi iseme maafisa wengine wa uchaguzi watakavyopatikana.

Aidha, sheria ya uchaguzi ihusishe chaguzi zote. Suala la idara ya TAMISEMI kuendesha uchaguzi wa serikali za mtaa tuondokane nayo.


Mzungumzaji wa pili, Faustine Sungura, kutoka NCCR-Mageuzi.
Kama tunataka uchaguzi 2024/25 tumuulize Rais Samia kama anataka uchaguzi


Kilichofanyika 2019 na 2020 sio uchaguzi, suala hili hatuwezi kuwa na ubishani mkubwa. Swali je nini kifanyike ili kufanikisha uchaguzi wa 2024 na 2025. Sisi(NCCR-Mageuzi) tunasita kusema nini kifanyike, kwa kuwa rejea hazioneshi kama kumewahi kufanyika uchaguzi. Pia hatuwezi kuzuia 2024/25 isije, hatuwezi kuzuia kilichofanyika 2019/20 kutofanyika 2024/25. Lakini tunatamani mwaka 2024/25 kufanyike uchaguzi.

Ukitaka kufanya jambo lolote, muulize mwanaume. Lakini ukitaka jambo hilo lifanyike muulize mwanamke. Mazingira ya Tanzania ya sasa yanafanana na mazingira ya Magreth Sacha, na sasa rais wa Tanzania ni Mwanamke, hivyo tunaamini tukitaka kufanya uchaguzi mkuu wa 2025 utakaotanguliwa na uchaguzi wa mitaa 2024, hivyo mtu wa kumuuliza yupo. Nasema haya kwa sababu hata sheria za uchaguzi zilikuwepo hata kwa miaka iliyotangulia lakini jamaa(rais wa enzi hizo) aliamua kwamba hataki uchaguzi, hivyo tumuulize Rais aliyepo(Samia) kama anataka uchaguzi ufanyike.


Mzunguzaji kutoka CHADEMA - Reginald Munisi.


Kuwe na chombo cha kufanya reference check (reference group) baada ya uchaguzi, chombo hicho kiundwe na CSO, Viongozi wa dini na viongozi wa serikali. Pia tunapendekeza, kama tunaenda kufanya kura za maoni tuwe na chombo huru cha kusimamia kura za maoni, au tubadili katiba. Uhuru wa tume kwanza uweze kutafsiriwa na katiba ili kujua mchakato mzima wa teuzi za viongozi wa uchaguzi kwa kuwa mchakato sio rafiki.

Sidhani itawezekanaje kupeleka mapendekezo ya sheria kwa wakati mmoja lakini tunaweza kufanya mabadiliko ya katiba yatafanya mabadiliko katika sheria nyingine zote.

Tunahitaji kuhakikisha tume ya uchaguzi ina uwezo wa kujisimamia, pia turuhusu waangalizi wa uchaguzi wa ndani na wa nje. Kwa yaliyotokea uchaguzi uliyopita watu hawana imani na tume ya kusimamia uchaguzi, na kama kikiendelea hivi kwa uchaguzi ujao watu hawataona umuhimu wa kupiga kura, hivyo ni muhimu kwanza kutoa elimu ya uraia kuhusu uchaguzi. Ili watu wajitokeze kugombea, kupiga kura na kujua umuhimu wa mchakato wa uchaguzi.


Kwa Ufupi alichokisema: Chama tulipendekeza tutengeneze Chombo cha Kusimamia Mchakato wa Katiba kitakachoitwa Reference Group itakayoundwa na Rais, Viongozi wa Chama, Viongozi wa Dini, Asasi ya Kiraia na Sekta Binafsi ili kuhakikisha safari hii mchakato haikwami na penye tatizo lolote tunajua tuna chombo cha kukiendea

Ameongeza kuwa kwa mapendekezo ambayo tulitoa na tumekuwa tukijadiliana na Serikali kama Muswada ungepelekwa mwezi wa 9 Bungeni, mchakato ungekamilika na tungepata Tume Huru na namna itakavyopatikana na mambo mengine ambayo tungeyataka

Munisi anafafanua kuwa kwa mazingira ya sasa ya Uchaguzi, nikienda kuchukua Fomu nikanyimwa tayari nimeondolewa nafasi ya kwenda Mahakamani kushtaki na matokeo ya kuhojiwa ni ya Wabunge tu, ya Rais hayahojiwi, hivyo kuna migongano ya kurekebisha kwenye Katiba kabla ya SheriaMzungumzaji kutoka CCM- Anamringi Macha
Kwanza sikubaliani na swali la nini kifanyike, inakuwa ni kama hakuna kitu kimefanyika kwahiyo ni muhimu tujadili nini kiendelee kufanyika. Kwa sababu hata kukutana hapa ni jambo, hadi kukutana hapa vyama tofauti maana yake kuna jambo limefanyika.

Pia watu wote hapa tumeafiki kuwa tuna refa tunayemuamini, yaani rais wa JMT, Samia Suluhu. Kwa hiyo ni wajibu wetu kufanya mazoezi katika kutafuta suala la kushika dola. Kwa hiyo cha kufanyika ni kuonesha dhamira ya kweli na utashi wa kisiasa. Ili tutoke hapa tukiwa wakweli lazima turidhiane. Mfano hivi viao viwe vya mara kwa mara ili kujadili na kuwa na makubaliano maana hakuna maridhiano bila majidiliano.

Hata kwenye mchakato wa katiba kuna mkwamo kwa kuwa hatukuridhiana, kuna wengine walisema kuna watu wamekuja na katiba yao mfukoni nk.nk. Mchakato wa katiba ni tofauti na kitabu cha hadithi hivyo utachukua muda. Lakini tumekubaliana kufanya mabadiliko ya katiba ili kukidhi mahitaji ya uchaguzi, hata hivyo baadhi ya hayo tayari yamefanyika kama kuondoa zuio la kufanya vyama vya siasa.

Pia utashi wa kisiasa uwe katika kila chama, elimu ya uraia inabidi ifanyike kwa wote. Suala la nani atoe elimu linaweza kuwa mjadala lakini hatuwezi kubishana kuhusu elimu kutolewa kwa wananchi.

Mimi najua utashi wa kisiasa upo, kinachotakiwa ni kama ilivyo kwa elimu kuwa haina mwisho hivyo kunakuwa na umuhimu wa watu kuelimishwa kuhusu utashi wa kisiasa. Elimu ya uraia kuhusu katiba isijekuonekana kama ni elimu inayotaka kukwamisha mchakato wa katiba, kwa kuwa ni muhimu watu waelimishwe.


Aliyosema Hamad Masoud Hamad-CUF
Zanzibar imefanya chaguzi 6, ni chaguzi mbili tu hazikuwa na mauaji
Mimi katika suala uchaguzi nina haya ya kusema. Kwanza watu wote waliokatika panel hii wanazungumzia uchaguzi wa muungano, mimi nataka nizungumzie uchaguzi wa Zanzibar ili yanayozungumzwa hapa yafike Zanzibar.

Kitu cha kwanza ambacho ni muhimu ni good political will, hakuna ayeyote aliyeko madarakani atapenda aondoke madarakani. Kwa hiyo cha kwanza cha kufanyika kipo ndani ya nafsi ya mtu. Zanzibar tumefanya chaguzi 6 katika chaguzi 6 ni chaguzi mbili tu hazikuwa na mauaji ambayo ni 2015 na 2010. Hii ni mojawapo ya vitu vya msingi, hivi viti vilifanya na Karume na Maalim Seif, wakawa na makubaliano.

Kwa Zanzibar, sheria ya uchaguzi iliyotumika 2010 na 2015, inaweza kuwa ndio hasa ya kipi kifanyike ili haya mambo yasiweze kutokea.

Kuhusu uchaguzi wa muungano. Wengi wanazungumzia kubadili sheria na kadhalika lakini uchaguzi zaidi ya 80% unasimamiwa na CCM. Mkuu wa wilaya na Mkuu wa Mkoa hajatajwa kokote kwenye sheria ya uchaguzi, sasa anakuja kwenye uchaguzi anafuata nini.


Aliyozungumza Hamis Issa Hamis - ZEC

Nimekuwepo tangu jana na madongo mengi yanapelekwa kwenye tume ya uchaguzi, lakini sitajibu. Wapiga kura wa Zanzibar wanapiga kura tano, ambapo kura mbili zinahusu muungano na kula tatu zinahusu Zanzibar lakini kwetu sheha anateuliwa, kwa hiyo hakuna uchaguzi wa serikali za mitaa.

Nini kifanyike: Sisi kama tume, tunasema uchaguzi ni mchakato endelevu, unapoisha uchaguzi mmoja tunaanza uchaguzi mwingine. Utoaji wa elimu kwa wapiga kura ni mchakato ambao huwa hauishi, hausiti, kwa Zanzibar tunaendelea. Kwa sasa tunatumia TV Kkuwaelimisha wananchi kuhusu Uchaguzi.

Sheria zinataka tuandae mpango kazi na bajeti na vyote tumeshaandaa. Kuanzia mwezi Novemba tutaanza kuandikisha wapiga kura wapya kwa kuwa serikali imeshakubaliana na bajeti yetu, pia mwakani zoezi la kuandikisha wapiga kura litaendelea. Kutokana na sensa kuna ongezeko la watu hivyo tutafanya mapitio ya majimbo.

Kama hakutakuwa na marekebisho tutaendelea na ratiba hii kwa kuwa tunafanya kazi kwa mujibu wa sheria.


Kutoka kwa ofisi ya msajili wa vyama vya siasa - Sisti Nyahoza

CHANGAMOTO ZA UCHAGUZI ZIPO NDANI YA VYAMA NA NJE YA VYAMA

Aliyoongea: Changamoto za uchaguzi zinatokana na maneno wanayosema hao wanaoshiriki uchaguzi. Uchaguzi ni ushindani. Hivyo hapa tumesikia maneno ya shukrani au changamoto na hapa tumesikia yote.

Katika Uchaguzi, changamoto ni ziko nne ambazo ni
1. Uelewa wa demokrasia na kuamini demokrasia. Wengi huingia kwenye uchaguzi bila kujua au kuamini kuhusu demokrasia. Ukishindwa uchaguzi usikatae, kwa sababu kanuni ya demokrasia ni wengi wapi, ukiona haupigiwi kura usilete vurumai

2. Sheria. Chaguzi zote zinaendeshwa kwa sheria lakini sheria zinaweza kuwa na upungufu ambao unaweza kurekebisha.

3. Utendaji. Hii ni changamoto ambayo inaweza kuwekwa sawa kwa kuonyana, mathalani unaenda kuchukua fomu mtoa fomu hajafungua ofisi. Hii inataka watu wachaguliwe wenye maadili.

4. Rushwa. Hii ni changamoto inayofanya tusiwe na uchaguzi wa huru na haki.

Hizi changamoto ziko ndani ya chama na kati ya chama na chama. Na mambo mengi huwa yanaanza ndani ya vyama kama tulivyojadili kwenye suala la wanawake, hivyo ndani ya vyama inabidi wafundishane kuhusu demokrasia ndani ya vyama. Ambapo uchaguzi baina ya vyama utakuwa mzuri.

Hivyo tunashauri sheria zirekebishwe na tupambane na rushwa ili kuhakikisha uchaguzi unakuwa sawa. Wala tusikimbilie suala la katiba kwenye masuala ya uchaguzi bali marekebisho ya sheria na kuwa na watendaji wazuri, kuwa na uwazi.
 
Back
Top Bottom