Twiga Stars yachangiwa mil. 37
18 Dec 2007
By Somoe Ng\'itu
Jumla ya Sh. Milioni 37 juzi usiku ziliahidiwa kutolewa na watu mbalimbali kwa ajili ya kuipatia timu ya soka ya taifa ya wanawake, Twiga Stars ambayo imefanikiwa kusonga mbele katika mashindano ya kutafuta nafasi ya kucheza fainali za Mataifa ya Afrika kwa Wanawake.
Twiga Stars imefuzu hatua ya pili baada ya kuifunga Eritrea kwa jumla ya mabao 4-2 katika mashindano hayo.
Akitangaza ahadi hizo, mlezi wa timu hiyo ambaye ni mwenyekiti wa kampuni ya Noor Oil & Industrial Technology (T) Ltd, Madame Rahma Al Kharoos aliwataka wachezaji wa timu hiyo kuendeleza juhudi walizozianza na kusema kuwa mafanikio yao yatathaminiwa.
Madame Rahma alisema kuwa wote wanafahamu ugumu wa kuiandaa timu na yeye amekubali kuwa mlezi wa timu hiyo ili kuweza kusaidiana na viongozi wa Shirikisho la Soka Tanzania, TFF, kutafuta fedha zaidi.
Aliwataja walioahidi kutoa fedha hizo kuwa ni pamoja na Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Yusuph Makamba aliyeahidi Sh. Milioni 20, Superdol Sh. Milioni 3, Scandinavia Sh. Milioni 2, hoteli ya Paradise Sh. Milioni 2, familia ya Kapinga Sh. Milioni 1.5 na Mkurugenzi wa Masoko na Udhamini wa Vodacom Sh. 300,000.
Pia mlezi huyo ameahidi kuanzisha mfuko wa kuiandaa timu hiyo utakaoanza na kiasi cha Sh. Milioni 100 kabla ya kwenda katika mechi ya hatua ya pili dhidi ya Cameroon.
Mechi hiyo ya pili itachezwa mapema mwezi Februari mwakani na Twiga Stars wataanzia hapa nyumbani.
Rais wa TFF, Leodegar Tenga aliwapongeza wachezaji hao kwa ushindi huo na kuongeza kuwa walichokifanya ni wazi kuwa walikuwa wamefuata maelekezo ya walimu wao.
Wengine waliohudhuria sherehe hiyo ni pamoja na Kiongozi wa mabalozi wote, Balozi wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, Juma Mpango na katibu mkuu wa Shirikisho la Afrika Mashariki na Kati (CECAFA), Nicholas Musonye.
* SOURCE: Nipashe