PUFDEA: Ni upatu au nini?

Mod unganisha hii thread na hiyo iliyowekwa DECI ingine yaja ( PUFDEA)

Zina ujumbe muhimu sana kwa wanaofuatilia. Maana tangu tumeweka hii sijui kama kweli vyombo vya serikali vimefuatilia. Tuliwawekea hadi adress ili wafanye kazi yao kabla ya madhara hayajatokea. Sasa naona yameshaanza, kesho utasikia vilio.
 
Naona vyombo vya Dola vimeamua kulifuatilia hili swala. Hongera jamiiforums kwa kuwakumbusha serikali what do do.!!



Deci mpya sasa yafikishwa polisi kwa uchunguzi
broken-heart.jpg
Ramadhan Semtawa na Fredy Azzah

BENKI Kuu ya Tanzania (BoT), imekabidhi taarifa za kampuni ya upatu ya Pufdia iliyojikusanyia mamilioni ya fedha kutoka kwa wananchi kwa vyombo vya dola ili izifanyie uchunguzi.

Kampuni hiyo ambayo inatoa ahadi ya kuwajengea nyumba, kusomesha watoto na mikopo isiyo na riba, imefungua matawi yake nchini kote na serikali ilianza kuifuatilia baada ya gazeti hili kuchapisha habari zake mwezi uliopita.

Hatua hiyo ya serikali imechukuliwa wakati sakata la Kampuni ya Deci iliyowatia hasara wananchi likiwa mahakamani huku vigogo wa asasi nyingine za aina hiyo wakisakwa.

Gavana wa BoT, Profesa Benno Ndulu alilithibitishia gazeti hili ofisini kwake wiki hii kuwa, ripoti ya kampuni hiyo ilishakabidhiwa kwa vyombo vya dola kwa sababu halihusiani na mambo ya kibenki.

"Tumekabidhi ripoti ya Pufdia katika vyombo vya dola ili wao waweze kufanya upelelezi wao na kuchukua hatua," alisema Profesa Ndulu.

Gavana alisisitiza kwamba, chombo hicho kimekuwa kikijiendesha kinyume na taratibu za kibenki kwani si benki, hivyo, vyombo vya dola vitajua hatua za kuchukua kisheria.

Hivi karibuni Waziri wa Fedha na Uchumi, Mustapha Mkulo, aliliambia gazeti hili kuwa, suala la kampuni hiyo limekabidhiwa kwa Gavana wa BoT kwa ajili ya uchunguzi zaidi.

Mkulo ambaye alionya kwamba, madhara ya kampuni hiyo yanaweza kuwa makubwa kuliko ya Deci, alisema uchunguzi wa suala hilo utakapomalizika taarifa yake itakabidhiwa serikalini.

Kwa mujibu wa uchunguzi uliofanya na gazeti hili katika baadhi ya matawi ya Pufdia, jijini Dar es Salaam ikiwemo makao makuu yaliyopo Manzese, umebaini kuwa bado kampuni hiyo inaendelea kusajili wanachama wapya ambao wanatakiwa kutoa kiasi fulani cha fedha kabla ya kuwa mwanachama.

Ingawa wahusika katika ofisi zote za kampuni hiyo hawasemi ni lini wanachama wao waliotangulia kujiunga watapata vitu walivyo vitegemea; lakini wanajitahidi kuwashawishi watu wanaotembelea ofisi zao kujiunga na kampuni hiyo kwa madai kuwa watafaidika baada ya muda mfupi.

Awali, baadhi ya wananchi ambao ni wanachama wa Pufdia na wengine waliosita kujiunga wamelieleza Mwananchi Jumapili kwamba, wanatilia shaka maelezo ya kampuni hiyo, jinsi inavyoendesha shughuli zake na namna itakavyopata fedha za kutimiza ahadi kwa wanachama wake.

Lakini wafanyakazi wa Pufdia walisema kampuni hiyo inafadhiliwa na Mtandao wa Kikristo Duniani unaoongozwa na Turko Simoni wa New York, Marekani.

Masharti ya uanachama wa Pufdia ni kutoa kiingilio cha Sh 30,000 endapo nia ya mteja ni kusaidiwa katika mradi mmoja, na kama akitaka msaada zaidi ya mradi mmoja atatakiwa kulipa kiingilio cha Sh 60,000.

Miradi ambayo mteja ataweza kujiunga nayo ni kujengewa shule, nyumba ya kuishi na kulipiwa ada kwa watoto au kwa mteja mwenyewe, kupewa mkopo bila riba, kupatiwa kazi baada ya mafunzo na kuwawezesha wakulima vijijini katika uzalishaji wa mazao na utafutaji wa masoko.

Kwa mujibu wa maelezo ya wafanyakazi wa kampuni hiyo, mwanachama atakayetaka kusomeshewa mtoto au kujisomesha mwenyewe atatakiwa kulipa Sh 100,000 kwa kila mtoto atakayetaka asomeshewe mbali na ada ya uanachama.

Kwa upande wa wateja walioomba kujengewa nyumba wanapaswa kulipa Sh 470,000 huku wale wanaotaka kujengewa shule wakitakiwa kulipa kiasi cha Sh 670,000.

Wanasema faida watakazopata wateja watakaojiunga na mradi wa kusomeshewa watoto ni pamoja na kulipiwa ada ya Sh 570,000 kwa muhula ambayo ni sawa na Sh 1,140,000 kwa mwaka kwa wanafunzi wa shule ya msingi hadi atakapomaliza darasa la saba.

Kwa wanafunzi wa sekondari, watafaidika kwa kulipiwa ada ya Sh 980,000 kwa muhula sawa na Sh 1,960,000 kuanzia kidato cha kwanza ndani au nje ya nchi hadi atakapomaliza kidato cha sita.

Kwa upande wa elimu ya juu taasisi hiyo itamsomesha mwanafunzi katika chuo chochote iwe ndani au nje ya nchi kwa ada ya Sh 5,280,000 kwa mwaka.

Kwa wale watakaochagua mradi wa kujengewa shule, watapewa kiasi cha Sh46.2 milioni huku wale waliojiandikisha kwa ajili ya kujengewa nyumba watapewa Sh6 milioni.

Miradi mingine ni pamoja na kutoa mikopo isiyo na riba, lakini mtu au kikundi kinapaswa kulipa asilimia 10 ya kiasi cha mkopo alichoomba.

Hivi karibuni kumeibuka asasi nyingi zinazojiendesha kwa mfumo wa benki, kinyume cha sheria bila kupata idhini ya BoT. Miongoni mwa asasi hizo ni pamoja na Deci na Malingumu, ambazo baadhi ya viongozi wake wamefunguliwa kesi mahakamani

Na Mwananchi ( www.mwananchi.co.tz)
 
Back
Top Bottom