Posho za vikao ni dhuluma dhidi ya kodi za wananchi
Juzi Waziri Kivuli wa Fedha ambaye pia ni mbunge wa Kigoma Kaskazini kupitia Chadema, Zitto Kabwe, alisema kuwa kambi ya upinzani inapendekeza kufutwa kwa posho za vikao kwa wabunge na hata katika mikutano ya watumishi wa serikali ili kuokoa fedha zitakazoelekezwa kwenye mambo mengine muhimu kwa maendeleo ya nchi.
Katika mkakati huo, ni dhahiri serikali itaokoa mabilion ya shilingi ambazo zitasaidia katika maeneo ambayo kwa muda mrefu yamekosa fedha kwa sababu ya visingizio vya ufinyu wa bajeti, sekta ambazo zimekuwa zikiyumba kwa sababu ya ufinyu wa bajeti ni pamoja na elimu, afya, nishati na ujenzi wa miundombinu kama barabara na reli.
Kwa mwaka wa fedha ujao, yaani 2011/2012 serikali inatarajiwa kuwa na bajeti ya Sh. trilioni 12.8 ikiwa ni juu kwa Sh. trilioni 1.2 ikilinganishwa na bajeti inayomalizika ya mwaka 2010/2011 ambayo serikali ilikadiria kutumia Sh. trilioni 11.6.
Kama ilivyokuwa mwaka huu wa fedha unaomalizika, ambao kiasi cha Sh. trilioni 7.7 kilitumika kwa matumizi ya kawaida (ulaji tu) na Sh. trilioni 3.8 kwa shughuli ya maendeleo, mwaka ujao hali itakuwa mbaya zaidi kwani kiasi cha Sh. trilioni 8.8 kinatazamwa kama matumizi ya kawaida, wakati Sh. trilioni 4 tu ndizo kwa ajili ya maendeleo.
Kwa vyovyote itakavyoangaliwa bajeti ya namna hii ni ya kula, yaani theluthi mbili ni kwa shughuli za kulipana mishahara na posho nyinginezo wakati maendeleo yakiambulia theluthi moja tu. Huu umekuwa ni ugonjwa wa taifa hili kwa miaka mingi, nguvu nyingi sana zinaelekezwa kuhemea chakula, maendeleo yanapewa kipaumbele kwa uzito mdogo sana.
Katika mfumo wa namna hiyo si jambo la ajabu kusikia mbunge akishauri sasa posho za vikao zipigwe marufuku kwa sababu mbali ya kugharimu fedha nyingi za walipa kodi, pia zimejenga utamaduni wa kuishi kwa udanganyifu. Kazi hazifanyiki watu wakifukuzana na posho hizi, ufanisi unashuka katika sehemu za kazi kwa sababu kwa kawaida nguvu nyingi zinaelekezwa kusaka posho za vikao.
Kwa mtindo huo, kwanza serikali inashiriki kwa kusaidia watu kukwepa kulipa kodi kwa sababu mapato yote ya posho hayakatwi kodi, wanaokamuliwa ni watu ambao hawana nafasi ya kunufaika na vikao vya posho; lakini la pili ambalo ni kubwa na baya zaidi, posho hizi zinajenga mfumo wa malipo mara mbili kwa watumishi wa serikali na hata kwa wabunge.
Kama serikali inaweza kulipa posho za vikao vyote hivi, ni kwa nini inakuwa na kigugumizi cha kuboresha mishahara ya watumishi wake wote, ili iwe bora, na hivyo kuwa chachu ya uchapakazi na uwajibikaji uliotukuka na kwa njia hiyo kuwa na uwazi juu ya vipato halisi vya watumishi wa umma kuliko ilivyo sasa ambako asilimia kubwa ya mapato ya watumishi wake yamefichwa kwenye posho ambazo hata hivyo ni siri kati ya mtumishi na mtumishi; kati ya idara moja ya wizara na nyingine lakini pia kati ya wizara na wizara.
Kama ilivyo katika sekta binafsi, kila anayeajiriwa anajua wazi nini mapato yake, yameanishwa kwenye mkataba, hatarajiwi kuishi kwa ujanjaujanja, anapimwa utendaji wake kulingana na mkataba kwa kuwa hana kisingizio, kama ni mshahara ni mzuri kama ni mazingira ya kazi ni mazuri na mwisho wa yote kama ni kodi za serikali zinakatwa moja kwa moja kwenye mshahara wake ambao uko wazi.
Tunaamini na kwa kweli huo ndio ukweli, serikali ama kwa makusudi au kwa kutokujua imekuwa ikishiriki katika kulea utamaduni wa kukwepa kulipa kodi, mfano halisi ni ulipaji wa posho za vikao; haya ni mapato ambayo yanajulikana wazi kabisa. Kwa mfano wabunge wanajua kwamba kwa mwaka wana mikutano minne, Februari, Aprili, Juni na Novemba; mikutano yote hii ina vikao kadhaa kulingana na urefu wake, hivyo si jambo la kubahatisha, mbunge anafahamu vilivyo kila mwaka mapato yake kutokana na posho za vikao ni kiasi gani, si kitu cha kubahatisha hata kidogo.
Hali hii ya uhakika wa posho za vikao si kwa wabunge tu, watumishi wa ngazi fulani serikalini nao wanajua vilivyo kila mwezi hawawezi kukosa mapato ya kiwango fulani kutokana na vikao vingi vikiwa ni sehemu ya kazi zao za kawaida kabisa.
Katika hali hii tunashindwa kujua ni kwa nini wabunge wanalipwa posho za vikao ambavyo ndiyo msingi wa kazi ya ubunge, kadhalika hatuelewi inakuwaje watumishi wa umma nao wanalipwa posho wanapokuwa wanatekeleza wajibu wa ajira zao kwa kufanya kazi ambazo ndizo zinawapa mshahara mwisho wa mwezi. Kwa macho ya kiungwana na bila kutafuna maneno tunaamini kuwa malipo ya posho za vikao ni aina nyingine ya ulipaji ujira mara mbili kwa kazi moja.
Inawezekana ukawa ni ufisadi uliorasimishwa. Serikali ni lazima sasa ianze kujiondoa katika mitego hii mibaya kama kweli inataka kusonga mbele katika kuwaletea wananchi maendeleo ya kweli, si kuandaa bajeti ya kula mwaka baada ya mwaka.
CHANZO: NIPASHE