TUJIKUMBUSHE......
Porokwa na Lowassa wana siri moja
Na Saed Kubenea
Imechapwa 09 June 2010
DANIEL ole Porokwa, amenaswa na nyavu za mbunge wa Monduli, Edward Lowassa. Polokwa wa zamani siyo wa leo. Wanasema amefaulu kumeza ndoana. Kama ni matatizo yatatokea tumboni lakini siyo kooni. Mwanachama huyo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), aliyekuwa ameahidi kumpokonya kiti Lowassa, sasa anasema hatagombea ubunge.
Ni zaidi ya miaka miwili sasa tangu Porokwa atambe kuwa atagombea ubunge katika jimbo la Monduli, mkoani Arusha; lakini sasa amevunja ahadi yake. Aliwaambia waandishi wa habari Dar es Salaam, Jumapili iliyopita, kuwa amefikia uamuzi huo wa kujitoa katika kinyang'anyiro baada ya kushauriwa na wazee wa kimila kutoka kabila la Wamasai ambao hufahamika kwa jina la Malaigwanani.
Porokwa ametaja sababu tatu anazosema zimemfanya kuchukua uamuzi wa kutogombea ubunge jimboni mwake.Kwanza, amesema amefanya hivyo baada ya kutambua kuwa Lowassa ndiye kiongozi mkuu wa kimila wa wazee wa kimasai – Malaigwanani.
Hivyo basi, akiwa kijana aliyelelewa vizuri na anayezitambua mila za kabila lake, hakuona busara kushindana na kiongozi wa kimila – Lowassa.
Pili, Porokwa amesema ameamua kuachia ngazi kutokana na kutambua kwamba chini ya uongozi wa Lowassa, jimbo la Monduli limepiga hatua kubwa kimaendeleo na kwamba safari hii ndiyo itakuwa ngwe ya mwisho kwa Lowassa kuwatumikia wananchi wa Monduli.
Tatu, amesema amefikia uamuzi huo kutokana na upendo mkubwa alionao kwa familia yake, hasa mke wake ambaye tangu alipotangaza azima ya kugombea ubunge wa Monduli, amekuwa mtu wa majonzi kutokana na kutotaka mume wake (Porokwa) agombee ubunge.
Sababu hizo tatu zimezua mjadala mkubwa. Sababu ya pili inaonekana moja kwa moja kuwa alikabidhiwa aitaje; siyo yake.
Sababu ya kwanza inaonekana kuwa kisingizio tu, kwani Porokwa amekuwa Mmasai miaka yote ya maisha yake. Hawezi kudai kuwa leo ndio anagundua kuwa anastahili kuheshimu wakuu wa kabila lake.
Sababu ya tatu ndiyo inazaa utata zaidi. Kitu gani kinafanya mke wake apende Lowassa aendelee kuwa mbunge kuliko yeye (mume wake), hasa katika mazingira ya mafao?
Siyo rahisi sana kumbishia Porokwa kwa sababu alizotoa; lakini hapa kuna kila sababu ya kujenga mashaka.
Kwanza, si kweli kwamba Porokwa amejiondoa katika harakati za kuwania "ubunge wa Lowassa" kwa sababu ya kutambua kuwa Lowassa ndiye kiongozi Malaigwanani. Ni Porokwa huyuhuyu anayesema amejiondoa kuwania ubunge Monduli, kwa kuheshimu mila za Kimasai, ambaye alikuwa anahubiri hadharani kuwa Lowassa si Mmasai. Amenukuliwa mara nyingi na vyombo vya habari akisema Lowassa hastaili kuwa kiongozi wa Wamasai kwa kuwa Lowassa siyo Mmasai. Mara zote Porokwa amekunuliwa akisema Lowassa anatoka kabila la Wameru.
Ni Parokwa huyu aliyetaka kupeleka kundi la waandishi wa habari jimboni kwa Lowassa kuthibitisha madai kwamba Lowassa ni Mmeru na kwamba umasai anaojipachika ni wa "kuchonga."
Alisema wazazi wa Lowassa walihamia Monduli miaka mingi iliyopita na kwamba hata jina la Lowassa linadhihirisha madai yake; si miongoni mwa majina ya Kimasai. Sasa kama hili ndilo alilolisema huko nyuma, hiki anachikisema leo kimetokana na msukumo upi?
Kama si hivyo, madai yake ya awali yalilenga nini; kumchafua Lowassa au kulikuwa na ukweli ndani yake? Kama alilenga kumchafua, nani alimlipa kwa kazi hiyo na alilipwa kiasi gani kufanya kazi ambayo leo hii anaikana?
Sasa amebadilika. Amezaliwa upya katika imani tofauti inayolenga kumpigia debe Lowassa. Tayari wengi wanauliza: Amenunuliwa? Hapa ndipo suala la kulipwa au kutolipwa linapopoteza maana: kulipwa ili uchemke na kulipwa ili upoe? Kwa gharama ipi, kwa kiasi gani cha shilingi mtu aweza kujikana mbele ya mke, watoto na jamii yake?Kwa kujua hili, Porokwa aliharakisha kuwaambia waandishi wa habari kuwa hakuhongwa kufanya alichofanya. Vyovyote itakavyokuwa, wengi watabaki wakijiuliza ni kitu gani ambacho kimeleta mabadiliko katika akili ya Porokwa na kufanya uongo anaokana kuwa ukweli anaotaka tuamini.
Hoja ya Porokwa kuwa ameamua kuachia ngazi baada ya kutambua kuwa chini ya uongozi wa Lowassa, jimbo la Monduli limepiga hatua kubwa kimaendeleo, haingii akilini. Ni kijana huyu aliyetuhumu Lowassa kuwa hajafanya kitu chochote cha maana Monduli.
Katika mkutano wake na waandishi wa habari mwishoni mwa mwaka jana, alinukuliwa akisema, "Lowassa hajafanyia kitu wananchi wa Monduli, zaidi ya kutumia mgongo wa wananchi wa Monduli kujinufaisha binafsi."
Alisema hata ule uwaziri mkuu aliokuwa anashikilia, haukusaidia wananchi wa Monduli. Alidai uwaziri mkuu huo, ulimsaidia Lowassa na familia yake tu. Kama haya ndiyo alitamka hadharani wakati huo, mangapi ambayo ameyatamka kwa siri na ambayo wale aliowaeleza bado wanayakumbuka?
Kwa mara nyingine, siyo rahisi kutilia mashaka majonzi ya mke wa Porokwa kila mumewe anapotaka kuchukua "ubunge wa Lowassa."
Hii ina maana tangu mwaka 2005, Porokwa alipotaka kugombea, mkewe amekuwa kwenye "majonzi makubwa" kuona mume wake anataka kupokonya kiti cha Lowassa. Majonzi ya "mama" katika vita hivi vya panzi wa kisiasa, yaweza kuthibitishwa na mama huyohuyo; si Porokwa au hata Lowassa. Bali kama ni kweli, majonzi hayo yaweza kuthibisha mvuto na mguso wa kisiasa wa aina yake hata kwa wasio na fursa ya kupanda jukwaani.
Kuna madai kwamba Parokwa aliondoa jina lake katika kinyang'anyiro cha 2005 baada ya kuahidiwa na Lowassa kuwa atapewa nafasi ya "mkuu wa wilaya." Hata hivyo, hakufanikiwa kupata nafasi hiyo kwa madai kuwa hakuwa na elimu inayohitajika kwa nafasi hiyo. Badala yake Parokwa aliibukia Chuo cha Maendeleo ya Jamii cha Tengeru, mkoani Arusha ili kupata elimu ambayo inadaiwa ndiyo Lowassa alitaka. Lakini wakati anamaliza masomo yake Tengeru, Lowassa alikuwa tayari ameshapoteza uwaziri mkuu wake. Hii ilifuatiwa kuhusishwa kwake katika kashfa ya mkataba wa Richmond. Hapa ndipo ndoto ya Porokwa ilionekana kufunikwa na wingu jeusi ambamo alifurukutia kwa madai ya "Lowassa siyo Mmasai."
Kimsingi hakuna anayelalamika kwa hatua ya Parokwa kuvunja ahadi yake ya kugombea ubunge Monduli. Hata andishi hili haliwasilishi malalamiko, bali linatoa sura nyingine ya wanaozaliwa upya kisiasa. Kijana huyu wa Monduli atakumbukwa kwa kuwasilisha malalamiko mbele ya rais, akituhumu Katibu Mkuu wa CCM, Yusuph Makamba kumuondoa katika nafasi yake ya katibu msaidizi wa CCM, wilayani Hanang.
Hii ilifuatia madai ya Porokwa kuwa Makamba alinukuliwa akimueleza George Mkuchika, naibu katibu mkuu wake kwamba "mwenyekiti (Jakaya Kikwete) amekasirika sana."
Kauli hiyo ilihusishwa na kuteuliwa kwa Porokwa kuwa katibu Hanang na kwamba Kikwete hakupenda uteuzi huo. Je, katika hali hiyo, wale waliokwenda kwa rais kumtetea Parokwa, anawaweka katika mazingira yapi mbele ya Lowassa? Bali mnofu wa kauli za Porokwa umo katika maneno haya: "…nimeamua kuachia ngazi baada ya kuona kuwa hii ndiyo itakuwa ngwe ya mwisho kwa Lowassa kuwatumikia wananchi wa Monduli." Amepata wapi ushahidi wa jambo hili kama siyo kwa Lowassa? Je, inawezekana amekutana na Lowassa na wakaahidiana "kitu" katika siku za usoni?
Tangu Porokwa aseme kuwa hii ni mara ya mwisho kwa Lowassa kuwa mbunge wa Monduli, Lowassa hajakana. Je, Lowassa atagombea nini mwaka 2015 kama "msemaji wake" anasema hatagombea ubunge? Je, atagombea urais?Hivi Porokwa ana uhakika gani kuwa Lowassa atashinda nafasi anayotaka kugombea? Amemhakikishia vipi kuwa iwapo atashindwa hatarudi kutaka ubunge wake?
Kwa hiyo kama Lowassa na Porokwa waliteta na kukubaliana, lolote laweza kufanyika – kwa Lowassa kutorudi Monduli au kurudi iwapo mipango yake ya masafa marefu haikufanikiwa. Jambo moja litabaki kuwa chungu. Majonzi ya mke wa Porokwa hayataisha hadi ithibitike kuwa Porokwa hampingi Lowassa. Hilo nalo ni somo.
Porokwa ambaye pia ni Mwenyekiti mstaafu wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (VCCM) mkoani Arusha,Alisema tayari ameanza kufanya maandalizi ya kumtafuta Lowassa, ili amuombe radhi.