Pigo kubwa na lenye madhara kwa Chama cha Walimu Tanzania

HaMachiach

JF-Expert Member
Dec 15, 2015
3,399
6,077
Chama cha Walimu Tanzania kimepitia misukosuko kadhaa ambayo isivyo bahati imekiyumbisha chama hadi kukiuka Katiba, kanuni zake na maamuzi mbalimbali ya vikao vya chama.

Hali hii imejitokeza baada ya kufariki kwa aliyekuwa katibu mkuu Alhaj Yahya Bakari Kilo Msulwa ambapo nafasi yake kwa mujibu wa katiba ilibidi ijazwe. Kwenye kikao cha baraza la taifa kilichofanyika ukumbi wa LAPF Dodoma, Deus Gracewell Seif kwa mshangao wa wengi alichaguliwa kuwa Katibu Mkuu akitokea Geita kama Afisa Elimu wa wilaya.

Kabla ya hapo Deus alikuwa mwenyekiti wa taifa cha chama kinzani cha CWT kikijulikana kama Umoja wa Maafisa Elimu Tanzania (UMET) Wakati wa uongozi wake ndani ya CWT ubadhirifu wa kutisha wa fedha na rasilimali nyingineza chama ulishuhudiwa pamoja na kushushwa vyeo kwa wafanyakazi kadhaa wa ngazi ya makao makuu na mikoa bila sababu, kuwapatia wengine vyeo kinyume cha katiba na kanuni za CWT na ajira za upendeleo.

Deus alifanikiwa kufika hapo kupitia nguvu ya baadhi ya wanasiasa waandamizi ambao lengo lao ilikuwa ni kupata fursa ya kujinufaisha na fedha za chama kupitia ada za wanachama za asilimia 2 na ada ya uwakala kwa wale wasio wanachama jambo ambalo walifanikiwa hadi Juni 2022.

Viongozi hao wameshatajwa mara kadhaa kwenye masakata yaliyokikabili chama hiki kwa nyakati tofauti na kwa kweli wamekua na influence kubwa kwenye maamuzi ya chama kwenye vyombo vyake mbalimbali ikiwemo vikao cya kamati ya utendaji ya taifa na baraza la taifa ambapo wajumbe kadhaa Deus amekuwa akiwanunua kwa fedha na taarifa lukuki za ufisadi huo ziko makao makuu ya TAKUKURU, Dodoma na maeneo mengine ambayo yamewanufaisha wao kwa kiasi kikubwa.

Deus Seif aliyekuwa Katibu Mkuu na Abubakari Alawi aliyekuwa mwekahazina wa taifa walifanya ufisadi wa kutisha. Kati ya mambo yaliyowaathiri wanachama ni yafuatayo:
  1. Kusitisha mkono wa kwaheri (Golden Handshake) kwa kila mwanachama wa CWT anayestaafu sawa sawa na mabati 20. Maamuzi hayo yaliyofanywa na baraza la taifa tangu mwaka 2015 yalisitishwa wakati wa uongozi wa Deus.
  2. Ujenzi wa majengo ya ofisi za mikoa. Majengo yaliyokuwa yanaendelea kujengwa kwa ajili ya ofisi na vitega uchumi kwenye mikoa ya Simiyu, Geita, Songwe, Njombe na Katavi yalisitishwa baada tu ya Deus kuingia madarakani.
  3. Mchakato wa ujenzi wa ofisi za wilaya ulifanyika kwa upendeleo, mfano wakati Hayati Magufuli akiwa madarakani, viongozi hao walilighilibu baraza la taifa likajenge jengo la ghorofa mbili Chato jambo ambalo halikuwa na tija na muda uliamua, halikujengwa na uongozi wa wilaya uliomlamba Deus Miguu, walifadhiliwa kwa kujengewa majengo ya ofisi za wilaya walizokuwemo.
  4. Mwaka 2021 CWT ilikopa shilingi Bilioni 4 katika benki ya CRDB kwa ajili ya Tshirt na kofia za Mei Mosi huku CWT yenyewe ikiwa na Bilioni 2 kwa ajili ya kazi hiyo hivyo kuwa na mtaji wa Bilioni 6 kwa ajili ya Tshirt na kofia tu! robo tu ya tshirt hizo ilitengenezwa walimu wakazua taharuki nchi nzima na kesi iko TAKUKURU hadi leo bila kufanyiwa kazi.
  5. Juni 28 mwaka 2022 Deus Seif na Abubakari Alawi pasipo na shaka yoyote walitiwa hatiani na mahakama ya Kisutu na kuhukumiwa kifungo cha miezi 6 jela kwa kosa la wizi wa fedha za walimu kwa kuwa walitumia takribani shilingi Milioni 14 kwa ajili ya gharama za kusafiri kwenda Cape Verde kushangilia mechi ya kufuzu kombe la dunia baina ya Cape Verde na Taifa Stars, yaani fedha za walimu hawa maskini walizitumia kujistarehesha. Baada ya kuhukumiwa Kwa mujibu wa katiba ya CWT na kanuni zake, Mwalimu Japhet Maganga aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu alipitishwa na mkutano mkuu wa CWT kuwa Katibu Mkuu na Protas Magesa kuwa Kaimu Mweka Hazina Taifa kwa kipindi cha mwaka mmoja. Uongozi huu ulifanya yafuatayo ambayo uongozi wa awali haukuyafanya.
    1. Kudhibiti mapato na matumizi ya chama yaliyopelekea kuweza kuitisha na kuendesha mikutano mikuu miwili ya chama kwa fedha za chama bila kukopa (Kila mkutano una wajumbe zaidi ya 1500), wa kwanza Disemba 2022 na wa pili Machi 2023.
    2. Uongozi huu ulifanikiwa kuleta utulivu ndani ya chama hadi sasa hususani kwa wanachama wake ambao ni walimu waliokuwa wanaanza kupoteza imani na muelekeo kwa uongozi wa Deus Seif.
    3. Chama kuamua kurejesha utaratibu wa kuwanufaisha walimu ulioondolewa na uongozi wa Deus kwa kuwarejeshea walimu mkono wa kwa heri (Golden Handshake) ambapo kwenye kikao cha mkutano mkuu wa mwezi machi 2023 makatibu wa wilaya walielekezwa kupeleka orodha na taarifa sahihi za walimu wastaafu, wanachama na wale waliokuwa wanakatwa ada ya uwakala ili wapewe mkono huo mapema iwezekanavyo jambo ambalo hakuna chama hata kimoja nchini cha wafanyakazi kinachofanya jambo hilo. Hivyo basi chama kiliazimia kuwapa mkono huo wastaafu kuanzia Januari 2021, na wale wa 2020 kurudi nyuma mpaka pale utawala wa Deus na Alawi uliposimamisha utaratibu huo.
    4. Chama kimeendelea kurejesha asilimia 15 ya michango ya walimu kwenye ngazi za matawi (sehemu za kazi) ambazo matumizi yake huamuliwa na walimu wenyewe jambo ambalo utawala wa Deus na Alawi ulisitisha na haijulikani fedha hizo zimekuwa zikienda wapi kwa miaka yote waliyokuwa madarakani na ndio maana mara kadhaa tumeshauri kwenye kipindi cha viongozi hao, Serikali kwa kutumia vyombo vyake ifanye ukaguzi mahususi wa fedha na mali za chama (Forensic Audit) ili kubaini kiwango cha ufisadi uliofanyika maana hizi ni fedha za umma na pengine ushauri huu ulikua ukiangukia mikononi kwa wanufaika ndio maana haujawahi kuzingatiwa.
Baada ya Deus na Alawi kumaliza vifungo vyao kwa msukumo wa wanasiasa waandamizi waliamua kwa kutumia mbinu na mikakati mbalimbali kuupiga vita uongozi wa chama ulioko madarakani ambao unakubalika kwa wanachama ili kuweka viongozi ambao watawanufaisha wafungwa hao na viongozi hao wa kisiasa. Ufuatao ni mtiririko wa matukio na harakati za Deus Seif, Abubakari Alawi na baadhi ya wanasiasa waandamizi kuipiga vita CWT ili wanufaike.
  1. Deus Seif na Abubakari Alawi kupitia mahakama kuu Dodoma walifungua kesi namba 17 ya mwaka 2022 ya Deus Seif na Abubakari Alawi dhidi ya Chama cha Walimu Tanzania kupinga majina yao kujadiliwa kwenye mkutano mkuu wa CWT Disemba 2022. Katika kesi hiyo mahakama iliamua Deus na Alawi wasijadiliwe. Hata hivyo wakati wa kesi hiyo Mahakamu kuu haikuihabarisha ofisi ya CWT makao makuu na iliridhia kinyume cha kanuni za mahakama kusikiliza upande mmoja (expert hearing) inashangaza kwa sababu ofisi ya CWT makao makuu iko Dodoma, mkutano mkuu ulikua unafanyikia Dodoma kwenye tarehe hizo hizo. Hata hivyo stop order ilipofikishwa ofisini mkutano mkuu ulikwisha malizika na maamuzi yake. Kwa kuwa CWT haikutekeleza amri hiyo, Deus na Alawi walimshtaki Maganga kama mtu binafsi kwa kesi namba 3 ya 2023 ili naye afungwe miezi 6 na kupoteza nafasi yake na nafasi kwenye utumishi wa umma.
  2. Machi 2023, Deus na Alawi walifungua kesi nyingine kumtaka katibu mkuu Maganga aondoke kwenye nafasi ya ukatibu mkuu. Hiyo ilikuwa ni kesi ya kupinga uchaguzi wa Machi 2023 kujaza nafasi ya Katibu Mkuu na Mwekahazina wa taifa. Mahakama kuu ya Dodoma iliamua nafasi hiyo isijazwe japo la kushangaza ni kwamba nafasi hiyo haikuwa moja ya nafasi zilizopaswa kujazwa kwenye uchaguzi huo kwa kuwa Katibu Mkuu alikuwepo kwa mujibu wa Katiba ya CWT. Hii yote lengo ikiwa ni Deus na Alawi kujaribu kurejea kwenye nafasi hizo.
  3. Kumpandikiza Joseph Misalaba. Kwa kuwa katiba ya CWT iko bayana, kikao cha mkutano mkuu cha Tanga cha tarehe 17 Machi 2023 kilipaswa kumchagua Naibu Katibu Mkuu. Deus, Alawi, na wanasiasa wachache wenye uroho na fedha za CWT walimpandikiza Joseph Misalaba na kwa kweli Tanga Rushwa ilitembea kwa kiwango cha kuhuzunisha na kama ulikuwa mfuatiliaji mzuri wa mitandao ya kijamii taarifa juu ya matukio ya rushwa zilisambaa mpaka kwenye vyombo vya serikali. Misalaba alishinda na alitakiwa kukidhi maelekezo ya Deus na Alawi na genge la baadhi ya wanasiasa waandamizi wanaotazama uchaguzi mkuu wa 2025 na wanaotegemea fedha hizo kuwanufaisha.
  4. Kikao batili cha kamati ya utendaji ya taifa cha tarehe 6 Juni 2023 kilichoongozwa na Joseph Misalaba na kufadhiliwa na genge tulilolibainisha hapo juu, kiliwakusanya viongozi 18 kati ya 32 wa Kamati ya utendaji ya taifa jijini Dodoma. Wajumbe hao waasi walifanya kikao haramu nje ya ofisi ya makao makuu CWT Dodoma chini ya miti na kutangaza kumuondoa madarakani Japhet Maganga kama katibu mkuu bila kugusa nafasi nyingine. Wakati wa kikao hicho Japhet Maganga alikuwepo ofisini akiendelea na shughuli za utendaji. Misalaba akaanza kufanya mawasiliano na ofisi mbalimbali za serikali na zisizo za serikali kwa kutumia headed paper zake na mihuri yake ya kughushi, pia akaita waandishi wa habari kutanganza kwamba Japhet Maganga sio tena Katibu Mkuu bali yeye ndiye anayetambulika kama Kaimu Katibu Mkuu jambo lililoleta taharuki na mkanganyiko kwa wanachama, serikali na wadau wengine. Ikumbukwe kwamba ilikuwa ni miezi mitatu tu tangu Joseph Misalaba aingie kwenye nafasi hiyo jambo linalothibitisha nia ovu ya genge hilo ambayo tulitahadharisha tangu awali(rejea maandiko yetu ya awali) Kikao hiki kilikuwa batili ambacho kilimuondolea majukumu katibu mkuu kinyume cha katiba ya CWT hivyo mapinduzi hayo yalishindikana. Kufuatia ukiukwaji huu wa katiba Baraza la taifa la CWT kama chombo kikubwa cha maamuzi lilikaa kikao tarehe 18 Juni 2023 na kuazimia kuwawajibisha wajumbe 18 wa kamati ya utendaji ya taifa akiwemo aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu Joseph Misalaba hivyo kuenguliwa kwenye nafasi zao. Baada ya maaumuzi hayo ya baraza Deus na kundi lake walikimbilia wizara ya kazi ili kutengua maamuzi ya baraza la taifa wakiwa na uhakika wa usaidizi wa aliyekuwa Katibu Mkuu kwenye wizara hiyo, Katibu Mkuu aliitisha kikao cha pande tatu. Uongozi wa chama, Joseph Misalaba na Protas Magessa wenye uungwaji mkono na genge la Deus na upande wa tatu ni wizara ya kazi akiwemo msajili wa vyama vya wafanyakazi. Msajili wa vyama vya wafanyakazi ambaye ni mlezi alionesha bayana kwa kupitia katiba ya CWT na kanuni zake kwamba wajumbe 18 wa Kamati ya Utendaji ya taifa walifanya kikao haramu, pia kwamba kikao cha Baraza la Taifa kilikuwa halali na maamuzi yake pia.
  5. Hukumu ya Kesi namba 7 ya mwaka 2023 Joseph Misalaba dhidi ya Japhet Maganga mahakama kuu ya Dodoma katika maamuzi ya kushangaza ilitoa amri ya kumrejesha Misalaba kwenye nafasi yake ya Naibu Katibu Mkuu ili aendeleze mapinduzi kwa msaada wa Deus Seif, Abubakari Alawi na baadhi ya wanasiasa waandamizi. Lengo likiwa ni kupata fursa ya kufisidi fedha na rasilimali nyingine za chama cha CWT ambazo ni mali ya walimu inayotokana na michango yao. Kesi ya msingi imepangwa kusikilizwa tarehe 24 Septemba 2023 Mahakama kuu Dodoma hivyo hakimu alihukumu kesi ndogo hata kabla ya kesi ya msingi haijaanza hata kusikilizwa. Baada ya kugundua hila hiyo, Chama kiliomba revision ya kesi hiyo namba 651/03/2023 mahakama ya rufaa ili kuona haki inatendeka.
  6. Deus Seif na genge lake waliona kwamba moja ya silaha muhimu za kukidhoofisha chama zilizobakia ni kuzuia mtiririko wa fedha za CWT ili chama kisiwe na fedha ili isababishe mtafaruku ndani ya chama chenye wafanyakazi zaidi ya 400 na wanachama zaidi ya 280,000. Katika kukamilisha hilo Wakili wa Joseph Misalaba alipeleka zuio benki ya MCB kuzuia fedha zote kwenye benki hiyo zisitolewe bila saini ya Joseph Misalaba na Protas Magesa ambao wote ni genge la Deus na Alawi. Uongozi wa benki ukawaelekeza kwamba walete muhtrasari wa kamati ya utendaji ya taifa kuhalalisha hilo lakini cha kushangaza baadae uongozi wa CWT ulizuiwa kutoa fedha bila kuwepo saini ya Joseph Misalaba na Protas Magesa, ambapo kwa mujibu wa maamuzi ya baraza Protas Magesa ukaimu uweka hazina wake ulikua unaishia Juni 2023. Lengo kubwa la mkakati huu ni kumkwamisha Katibu Mkuu Mwalimu Maganga na uongozi ulioko madarakani ili ionekane kwamba ameshindwa kuendesha chama. Hili limefanikiwa kutokana na uswahiba mkubwa wa muda mrefu kati ya Deus Seif na Abubakari Alawi kwa upande mmoja na Richard Makungwa Mkurugenzi mtendaji wa benki ya walimu ambaye ameendelea kumkumbatia Deus Seif kama mjumbe wa bodi ya Benki kabla, wakati na hata baada ya kumaliza kifungo chake gerezani. Lengo ni kuhakikisha kwamba anaendelea kuiba fedha za benki na anaongezewa mwaka mmoja wa ajira baada ya kustaafu Septemba 2023. Kukwamisha malipo ya benki ya MCB kwa CWT kuna madhara yafuatayo.
    1. Michango ya Bima za wafanyakazi wa CWT 432 wenye wategemezi 4 kila mmoja yanasimama
    2. Asilimia 8 za fedha za mikoani zinasimama, asilimia 30 za fedha kila wilaya zinasimama na asilimia 15 za fedha zinazorudi kuwasaidia walimu mashuleni/matawini zinasimama, fedha za mkono wa kwaheri nchi nzima zinasimama, michango kwenye mashirika ya kikanda na kimataifa inasimama, kazi zote za chama kwa ujumla zinasimama, uendeshaji wa ofisi unasimama, hata mtumishi wa chama akifariki mwili wake hauwezi kurejeshwa kwao. Hapa unajiuliza faida ya Benki ya mwalimu ambayo wakati wa uanzishwaji wake mtaji ulikuwa ni Bilioni 35 na sasa ni Bilioni 15.6 na masharti ya BOT ni kwamba mtaji haupaswi kupungua Bilioni 15. Je MCB ina mustakabali gani kwa walimu walioitazama kama mkombozi wao na wana hisa zao humo. Iweje inatumika kuwahujumu walimu na Mkurugenzi anayetumika ana lengo gani?
  7. Harakati za kuhakikisha kuwa Katibu Mkuu huyu ndugu Japhet Maganga anayekwamisha upigaji wa genge la Deus na Alawi anaondolewa kwenye nafasi ya ukatibu mkuu na hatimaye kurejeshwa kwa mwajiri wake ili kupandikiza watu wao. Baada ya mikakati iliyokwisha ainishwa hapo awali kushindikana na hata kumtoa kafara aliyekuwa msajili wa vyama vya wafanyakazi aliyesimamia kikamilifu na kiuadilifu Katiba na kanuni za vyama vya wafanyakazi kwa kuondolewa kwenye nafasi yake kwa uadilifu wake. Silaha ya mwisho iliyobaki hadi sasa ni kutokumpa kibali kingine mwalimu Japhet Maganga cha kuendelea kuazimwa na chama kutoka kwa mwajiri wake Mkurugenzi wa Manispaa ya Temeke bila sababu yoyote ili kutokuendelea kukitumikia chama cha walimu Tanzania. Tangu chama hiki kimeanza tarehe 1 Novemba 1993 sio Anatory Rwehumbiza, wala Yahya Msulwa waliwahi kunyimwa vibali vya kuendelea kukitumikia chama. Kumnyima kibali mfanyakazi wa chama cha wafanyakazi aliyekitumikia ni ubaguzi kwa mujibu wa sheria ya ajira na mahusiano namba 6 ya 2004 kifungu cha 9 (1) hadi (5). Hii haijawahi pia kutokea kwa wafanyakazi lukuki wa serikali ambao wamewahi kuazimwa na chama kusitishiwa vibali. Kwa nini mara hii itokee kwa Maganga peke yake, ametenda dhambi gani, je kusimamia kikamilifu fedha na rasilimali za chama ndio kumemponza? au ni mikakati thabiti kwa maslahi ya walimu inayowachefua wapigaji? Sasa kwa taarifa ya uhakika yenye ushahidi tuliyonayo genge la Deus na baadhi ya wanasiasa walafi wamekwishafanya mipango yote na imekamilika ya kumpatia Japhet Maganga barua kutoka idara ya utumishi ya kumrejesha kwa mwajiri wake na barua tunayo na kumbukumbu namba za barua hiyo na nakala yake tutazitoa kwa mamlaka husika. Hivi batili inaweza kushinda haki? Ni vema wanachama wa chama cha walimu Tanzania, wadau wa elimu yakiwemo mashirika ya kitaifa na kimataifa na watu wote wenye mapenzi mema na walimu na elimu ya nchi hii, Serikali na vyombo vyake ikiwemo mamlaka ya juu kuona kwamba walimu na elimu ya nchi hii haihujumiwi na mafisadi. Cha kujiuliza ni kwamba, kwa nini Maganga aonewe, kama amefanya ufisadi vyombo na mamlaka kumbaini kwa uhalifu kama ameutenda vipo, kwa nini wasifanye hivyo? Au mkono wa genge la wahalifu hao ni mrefu kwa kiasi hicho kiasi cha kupofusha haki kama ilivyomtokea msajili wa vyama vya wafanyakazi wa awali. Ni imani yetu kwamba kwa kila mzalendo atakayepata taarifa hii zikiwemo mamlaka kadhaa watalifanyia kazi. Wahuni hawa wanaweza kumpa barua ambayo ipo tayari ili arejee kwa Mwajiri, je ni upi utakua mustakabali wa walimu ambao kwa muda mrefu wamekua wakilalamikia ubadhirifu uliofanywa na uongozi uliopita wa Deus Seif. Je maamuzi hayo yakitekelezwa hayataupa umma ujumbe wa vitisho kwamba yeyote anayesimamia haki atakutana na mkono wa genge hili la viongozi walafi? Iwapo Katibu Mkuu atarejeshwa kwa mwajiri, itawapa walimu ujumbe kwamba haki haina nafasi katika kipindi na bado waendelee kubakia kwenye utumwa wa Deus Seif na genge lake.
 
Mkuu tuhuma hizo dhidi yake ni nzito sana na za kutisha!

Jaribu "kwa njia moja ama nyingine" kuzifikisha sehemu zenye macho na meno ya kung'ata.

Wee ni mtu mzima siwezi kukuelekeza, unazijua, ili hatua stahiki ziweze kuchukuliwa dhidi ya huyo fisadi papa.

Kumwaga mtama kwenye kuku wengi kama ulivyofanya, haiwezi kuwasaidia sana wavuja jasho unaowasemea, ama saazingine kwa wasiokuwa na uwezo wa kuyapima mambo sawa sawa, watakuona kama ni mpiga majungu, mwenye wivu wa kike na roho ya kutu yenye kupinda kama korosho.
 
Mimi kama mdau wa elimu, ninachofahamu ni kwamba; Viongozi wote wa CWT ni wezi tu. Hakuna mwenye unafuu hata mmoja.

Na kwa kushirikiana na serikali ya CCM inayonuka rushwa na ufisadi; mnaendelea kuwaibia walimu hela zao kila mwezi kupitia makato yenu ya 2% kwenye mishahara yao kiduchu.

Ahueni siku hizi kuna mwizi mpya anayeiba walimu walau elfu 5 kila mwezi (Chakuhawata). Hivyo walimu baadhi wameanza kukimbilia huko ili kuokoa chochote kitu kutoka kwa nyinyi majizi sugu CWT.
 
Mimi kama mdau wa elimu, ninachofahamu ni kwamba; Viongozi wote wa CWT ni wezi tu. Hakuna mwenye unafuu hata mmoja.

Na kwa kushirikiana na serikali ya CCM inayonuka rushwa na ufisadi; mnaendelea kuwaibia walimu hela zao kila mwezi kupitia makato yenu ya 2% kwenye mishahara yao kiduchu.

Ahueni siku hizi kuna mwizi mpya anayeiba walimu walau elfu 5 kila mwezi (Chakuhawata). Hivyo walimu baadhi wameanza kukimbilia huko ili kuokoa chochote kitu kutoka kwa nyinyi majizi sugu CWT.
Dah!! Kwahiyo majizi ni mawili sasa hivi??
 
Dah!! Kwahiyo majizi ni mawili sasa hivi??
Sahihi kabisa. Moja ni jizi sugu (CWT). Hili linakula kimasihara tu 2% ya basic salary ya mshahara wa mwalimu aliyeko serikalini kila mwezi. Na hili jizi kwa miaka nenda limekuwa likilindwa na serikali ya ccm!

Kajizi kengine ni hako ka Chakuhawata. Haka ni kajizi kapya kabisa! Mana kameingia rasmi kwenye ulaji mwaka huu wa 2023 kama sijakosea. Na walau haka kajizi kapya kanapendwa na walimu walio wengi, kwa sababu kenyewe kanaiba 5000/= tu kila mwezi kwenye basic salary ya mwalimu mnyonge wa nchi hii.
 
Back
Top Bottom