*PENZI LA UMAUTI-07*
Nilipanga kumueleza ukweli mke wangu wala sikutaka tena kumficha, maneno ya Chrispine yaliiingia vilivyo mpaka nikajiona kuwa nilikosea. Nilianza kwa kumuomba msamaha kwa kosa nililokuwa nimelifanya, akaonekana kushangazwa na msamaha wangu, alinitazama kama mtu aliyekuwa katika mshangao wa kuitazama sinema ya kutisha. Nilifahamu nilikuwa nimemuacha njia panda hasa baada ya kumuomba msamaha wa kosa ambalo sikulikiri mbele yake.
“Unaniomba msamaha kwani umenikosea nini mume wangu?” aliniuliza huku akiendelea kunishangaa, sikutaka kumuacha aendelee kuwa katika mshangao ule sajari na hali ya sintofahamu iliyokuwa imemkumba ghafla! nikaamua kumuelezea kila kitu kilichokuwa kimetokea.
Hakutaka kuamini hata kigogo kwa kile nilichokuwa nikimueleza kuhusu Mama yangu na mambo aliyokuwa akinifanyia, akabaki akiwa ameyatoa macho yake mithili ya mtu aliyekuwa katika kabali nzito baada ya kusikia kuwa nilitafutiwa mwanamke ambaye nililazimishwa nimuoe kipindi kile ambacho alikuwa nyumbani kwao akiilea mimba.
Kama ilivyokuwa kawaida yake machozi hayakuwa mbali, yalianza kumdondoka huku midomo yake ikionekana kumchezacheza, alikuwa na maneno ya kuniambia lakini yalikwamishwa na kilio kilichomkumba ghafla! Nikapata kazi ya kumbembeleza mpaka pale alipotulia ndipo alipoweza kuzungumza.
“Dominick kwanini mama yako ananichukia kiasi hiki nimemkosea nini mimi?” aliniuliza kwa sauti dhaifu iliyokaribisha kilio kingine, akaanza kulia tena, nikamsihi anyamaze huku nikimfuta machozi yake.
“Dominick hivi nimemkosea nini mimi mama yako?” aliniuliza huku machozi yakiendelea kumbubujika mashavuni mwake. Nilipomtazama alinisikitisha mno, nikajikuta maumivu yakianza kunichoma katika moyo wangu.
“Hapana mke wangu usiseme hivyo,” nilimwambia kwa kumkataza, sikujua hata nilikuwa namkataza nini wakati ukweli nilikuwa tayari nimeshamueleza.
“Dominick mama yako hanipendi, hampendi hata huyu mwanao hivi unafikiri tutaishi vipi?” aliniuliza huku machozi yakiwa yamemjaa katika macho yake.
“Julieth mke wangu najua Mama yangu hakupendi lakini mimi ndiye ninayekupenda hivyo naomba usijisikie kuwa mnyonge, umesikia mke wangu,” nilimwambia lakini hakunijibu lolote, alibaki kuwa kimya huku akiwa ameyaelekeza macho yake chini, machozi bado yalikuwa yanaendelea kumbubujika.
Haikuchukua sekunde chache akainua kichwa chake kisha akanitazama, maneno yangu yalionekana kumuumiza sana.
“Dominick najuta hata kumzaa huyu mtoto,” aliniambia huku akiyafuta machozi yake.
“Mke wangu ndiyo maneno gani hayo unanayoniambia kwanini hutaki kuwa mwelewa, nimekwambia usijali lolote,” nilimwambia.
“Hivi kwa haya yote uliyonieleza bado niendelee kuishi na wewe kweli au unasubiri mama yako aje aniue ndiyo ufurahi?”
“Julieth mke wangu.”
“Naomba uniache,” aliniambia huku akionekana kujawa na hasira, hakutaka hata nizungumze lolotr, hakuwa tayari kunisikiliza tena.
Nilianza kujilaumu kwa uamuzi ule niliyokuwa nimeuchukua wa kumueleza ukweli mke wangu, moyo wangu ukaanza kumchukia Chrispine, nilimuona kuwa kama adui mwingine wa ndoa yangu yani ushauri kwa wake badala uiokoe ndoa yangu ndiyo kwanza ulienda kuiharibu na kwa wakati ule nilikuwa katika ugomvi na mke wangu.
Nilijitahidi kuomba msamaha lakini hakukuwa na msamaha, nilichukiwa ghafla! na mke wangu hata ile furaha ambayo ilikuwa imetawala katika maisha yetu ikapotea, hakukuwa na aman tena.
“Kwanini hutaki kunielewa mke wangu?” nilimuuliza wakati huo nilikuwa nimepiga magoti.
“Nikuelewe nini Dominick we nenda kamuoe huyo mwanamke aliyekutafutia mama yako,” aliniambia huku hasira pamoja na wivu vikiwa vimemtawala.
“Nakupenda wewe mke wangu huyo mwanamke kama ningekuwa nina nia ya kumuoa ningemuoa tangu ulipokuwa nyumbani lakini sikuwa tayari kufanya hivyo, nakupenda mke wangu,” nilimwambia.
“Nimesema Dominick naomba uniachee,” aliniambia.
“Kumbuka tuna mtoto hivi kama tukianza kugombana wakati huu unafikiri mtoto atakuwa katika misingi ipi?”
“Dominick sitaki kukugombanishe na Mama yako nende ukamuoe huyo mwanamke ili umridhishe mimi niache na maisha yangu.”
“Hiyo ndoto isiyoweza kutimia, siwezi kukuacha wala siwezi kuruhusu ukapotea katika maisha yangu, wewe ni mke wangu tafadhali naomba unielewe.”
“Nikuelewe nini?”
“Nakupenda.”
“Na mama yako je?”
“Mama yangu asikuumize kichwa, sisi tuishi maisha yetu kama yeye hataki basi ila sisi ndiyo tumependana na tayari tupo katika ndoa hivyo hawezi kufanya lolote,” nilimwambia.
“Niahidi,” aliniambia hapa alikuwa tayari ameshaacha kulia.
“Sitokuacha kamwe katika maisha yangu mpaka mwishi wa pumzi zangu,” nilimwambia.
“Kweli?” aliniuliza.
“Namaanisha,” nilimwambia.
Tuliendelea na Maisha yetu huku huku mawazo ya mama yakiendelea kufutika, sikutaka Mama yangu aendelee kuwa kikwazo cha ndoa yangu, nilifanya kila niwezalo ilimradi ndoa yangu iendelee kuwa salama.
Baada ya kupita mwaka mmoja nilihisi kuwa na kila sababu ya kubadilisha kazi, majukumu yaliongezeka na kama unavyojua tena swala la kulea mtoto siyo kazi ya mzahamzaha. Pale Kariakoo nilipokuwa nikifanya kazi yangu ya ufundi simu haikuwa ikinilipa sana kama hapo awali, maisha yalibadilika na kila siku ilikuwa ni afadhali ya jana.
Kuna kipindi tulikuwa tukishindia uji siku nzima huku pesa niliyokuwa nikifanikiwa kuipata nilikuwa nikiichanga kwa ajili ya kulipa kodi ya chumba. Maisha yalikuwa magumu sana, ukichanganya na uwepo wa mtoto tuliyekuwa naye ndiyo kwanza kichwa kilizidi kuniuma.
Nilimueleza mke wangu juu ya mpango wangu wa kubadilisha kazi akaonekana kuniunga mkono lakini pia hakuacha kunishauri,
“Kwanini usiangalie kazi ambayo inalipa ndiyo uifanye?” aliniuliza.
“Ni kazi gani hiyo?” nilimuuliza.
“Kuna biashara nimeifikiria,”aliniambia.
“Biashara gani hiyo?”
“Kwanini usifanye biashara ya kuuza mitumba nasikia inalipa,” aliniambia mke wangu.
Kwa kweli biashara hiyo ya kuuza mitumba ilionekana kuniingia akilini, nilitabasamu baada ya kusikia hivyo, sikuacha kumshukuru mke wangu ambaye ndiye aliyenipa wazo lile, hakutaka kunishukuru zaidi aliniambia kuwa lile lilikuwa ni jukumu lake kama mke kuhakikisha nafanikiwa katika maisha.
“Hivi mtaji wake ni shilingi ngapi?” nilimuuliza.
“Inategemea na uwezo wetu ila kwa kuanza itabidi ukanunue mzigo pale Ilala sokoni kwa bei rahisi halafu utakuwa unaenda kuwauza wateja mitaani mpaka pale ambapo tutapata mtaji kisha na sisi tutakuwa tukinunua kwa jumla na kuziuza kwa upana,” aliniambia mke wangu maneno ambayo niliyapitisha katika serikali ya ubongo wangu.
****
Niliamua kufanya rasmi biashara ya kuuza nguo za mitumba mitaani, biashara ambayo ilifanya watu wengi wanishangae kipindi ambapo nilikuwa nikianza hata rafiki yangu Chrispine alinishangaa sana na kuniona kuwa nilifanya maamuzi ya kukurupuka bila kuhitaji ushauri.
Kama walivyosema wahenga kuwa katika wengi kuna mengi pia ndivyo ilivyonitokea kipindi ambapo naanza kufanya biashara yangu ya kuuza nguo za mitumba mitaani.
Nilianza kusikia maneno ya watu wakisema kuwa nilifilisika kiasi kwamba niliamua kuacha kazi yangu ya ufundi simu Kariakoo nikawa muuza mitumba. Kila mtu alikuwa na lake la kusema.
Miongoni mwa maneno ambayo siwezi kuyasahau katika maisha yangu nayakumbuka mpaka leo katika kumbukumbu zangu ni siku moja nilisikia watu wakinizungumzia vibaya, walikuwa wakisema kuwa nililogwa na mke wangu ambaye alikuwa hana kazi yoyote Ati! Limbwata la mke wangu ndiyo lilikuwa linaniongoza niende kufeli katika maisha yangu ili tuwe sawa.
Je, nini kitaendelea?