*PENZI LA UMAUTI-04*
Wakati huo bado nilikuwa nimeishikilia picha huku machozi yakiendelea kunidondoka lakini ghafla! mke wangu Julieth akatokea, akanikuta nikitokwa na machozi.
“Mume wangu kuna nini kimetokea?” aliniuliza Julieth kwa sauti iliyogubikwa na upole wa hali ya juu, alionekana kushangazwa na hali aliyonikuta nayo kwa wakati ule.
“Hakuna kitu,” nilimjibu huku nikiyafuta machozi yangu kisha nikairudisha ile picha ukutani.
“Hakuna kitu na wakati nimekukuta unalia?” aliniuliza huku akionekana kutoelewa lolote lile. Naam! Ni kweli alikuwa hajui lolote lililokuwa limetokea hata hivyo sikutaka kumuweka wazi, niliamua kumficha ukweli, niliamua kufanya hivyo ni kutokana na hali ambayo alikuwa nayo.
“Hakuna kitu nipo sawa,” nilimwambia kisha nikajaribu kutengeneza tabasamu pana katika uso wangu, nilifanikiwa kutabasamu.
“Mbona unalia?” aliniuliza wakati huo alinisogelea kisha akaanza kunifuta machozi kupitia viganja vyake, nilipomtazama alionekana kuonyeshwa kuguswa na tukio lile japo hakuwa akijua ni nini hasa kilichokuwa kimetokea.
“Nimemkumbuka marehemu baba yangu laiti kama angekuwepo naamini hata yeye angefurahia kwa tukio hili lililotokea, angefurahi kuwa babu mtarajiwa,” nilimwambia maneno ya uongo ambayo yalijitunga ghafla!
kichwani. Muonekano wangu wa majonzi ukichanganya na hayo maneno niliyomwambia yakasaini ukweli ambao alikuwa akiutaka kuufahamu japo ulikuwa ni ukweli wa kutunga.
“Mume wangu usiseme hivyo utakufuru,” aliniambia huku akionekana kuniamini kabisa ila ni kama alikuwa akiwaza kitu na mara baada ya kukiwaza akaamua kuniambia.
“Halafu nimesahau kukwambia,” aliniambia huku akionekana kufurahi.
“Umesahau kuniambia nini?” nilimuuliza huku nikimtazama, wakati huo machozi yalikuwa yamekoma kunidondoka.
“Nimeongea na mama,” alinijibu.
“Mama yupi?” nilimuuliza.
“Kwani wewe una mama wangapi?” aliniuliza.
“Wawili,” nilimjibu.
“Yupi na yupi?” aliniuliza tena swali ambali likanifanya nitabasamu.
“Mama Julieth mzaa chema na Mama Dominick, sasa sijui wewe umeongea na mama yupi hapo?” nilimjibu kwa kumuuliza swali.
“Nimeongea na Mama Dominick,” alinijibu.
“Anasemaje?” nilimuuliza.
“Amefurahi tu! kusikia kuwa nina ujauzito ila ameniambia kuna zawadi anataka kunipa.”
“Zawadi gani tena.”
“Hata sijui mume wangu ila amefurahi huyo,” aliniambia Julieth huku uso wake ukiwa katika tabasamu pana, tabasamu ambalo likazidi kuniweka katika bumbuwazi, kichwani likanijia swali.
Lilikuwa ni swali juu ya huyo Mama Dominick ambaye alikuwa akiniambia alifurahishwa na taarifa hizo kiasi kwamba ikafikia wakati wa kutaka kumpa zawadi.
Ni zawadi gani hiyo ambayo anataka kumpa mke wangu?
Na je huo upendo anaouzungumzia mpaka akafurahishwa na taarifa za ujauzito wake ulitokea wapi?
Nikazidi kuwa katika kizungumkuti, sikujua ni nini kilichokuwa kinakwenda kutokea katika ndoa yangu. Nikakumbuka yale maneno aliyoniambia Mama yangu pamoja na ule ujumbe alinitumia, vilikuwa ni vitu viwili tofauti na yale maneno ya Julieth aliyokuwa akiniambia kwa wakati huo.
“Unasema umeongea na Mama Dominick, Mama yangu!” nilimuuliza Julieth huku nikionekana kushangazwa na maneno yake.
“Ndiyo nimeonge na Mama yako,” alinijibu huku akionekana kutokuwa na tatizo lolote, alikuwa akijiamini na jibu lake.
“Vipi na Mama yako pia umemwambia?”
“Ndiyo niliwaambia wote ila kwa ufupi hakuna tatizo lolote mume wangu.”
“Una uhakika?”
“Ndiyo mbona umeshangaa?” aliniuliza.
“Hapana hakuna kitu,” nilimjibu.
Nilizidi kuwa katika fumbo zito, nisijue ningeweza kulifumbua vipi kwani tayari akili yangu ilikuwa imechoka. Nikazidi kubaki kujiuliza maswali lukuki ambayo hayakuweza kupata majibu, kiufupi nilitawaliwa na mawazo.
“Ina maana Mama yangu alikuwa akinitania au?” nikajiuliza tena hapo nilikuwa nikijichekesha kama mwendawazimu, sikutaka kumuonyesha tofauti yoyote mke wangu.
Maisha yaliendelea huku nikiendelea kubaki na siri moyoni mwangu, ilikuwa ni siri ile ya maneno aliyoniambia Mama yangu, aliniambia kuwa sikutakiwa kuendelea kuishi na mke wangu hasa katika kipindi kile cha ujauzito hivyo nilitakiwa kumrudisha nyumba kwao kwa ajili ya kuilea mimba mpaka pale ambapo angeweza kujifungua ndiyo nilitakiwa kumrudisha na kuendelea kuishi naye. Hilo lilizidi kuniumiza sana akili yangu.
Dominick mimi fundi simu wa Kariakoo sikushindwa kutafuta pesa ya kuweza kuihudumia mimba, sasa kwanini Mama yangu aniambie nilitakiwa kumrudisha kwao, kwani ameona nini?
Lilipotoka swali hilo likajitunga swali lingine basi ikawa ni tafarani tu! nikazidi kujiona kuwa mjinga wa kuendelea kuificha siri ambayo mwisho wa siku ningeweza kuzikwa nayo.
Baada ya wiki moja kupita niliamua kumueleza ukweli mke wangu, nilimuelezea kila kitu kilichokuwa kimetokea, sikutaka kumficha lolote, nilimwambia kwa kuwa nilimuamini, alikuwa ni msikivu hivyo sikutegemea tofauti yoyote ambayo ingeweza kujitokeza.
“Mume wangu,” aliniita mara baada ya kumuelezea kila kitu tulipokuwa nyumbani.
“Naam,” nilimuitikia huku nikimtazama, hakuonekana kubadilika kwa lolote lile, sura yake ya kitoto bado iliendelea kuwa katika vazi lake la upole.
“Mama ameongea kitu cha umuhimu sana,” aliniambia Julieth kwa sauti ya upole.
“Cha umuhimu kivipi?” nilimuuliza.
“Ameona mbali,” alinijibu.
“Kivipi?”
“Wewe hautaweza kunihudumia kwa kila kitu, kuna vingine utashindwa wakati utakapokuwa kazini ni bora niende nyumbani tu! kule watakuwa karibu sana na mimi hasa katika hiki kipindi cha ujauzito wangu.”
“Kwahiyo unataka kuniambia umekubaliana na Mama mkwe wako?”
“Ndiyo tena ameongea kitu cha umuhimu sana,” aliniambia Julieth huku akionekana kuwa sawa, hakuonyesha kukasirika kwa lolote lile.
Nilijaribu kumkatalia lakini lilipokuja suala la king’ang’anizi kwa kweli nilishindwa, Julieth hakutaka kuona wazo la Mama yangu ninalipuzia.
“Mama ni mama Dominick embu tusimpuuzie yeye ni mtu mzima,” aliniambia Julieth.
“Lakini mke wangu.”
“Hakuna cha lakini, kilichobaki hapo wewe nipe nauli niende nyumbani,” aliniambia Julieth.
****
Baada ya siku ya tatu kupita niliamua kwenda kumkatia tiketi ya basi Ubungo mke wangu ambapo siku iliyofuata alitakiwa kusafiri kwenda mkoani Kilimanjaro na basi la KIMOTKO.
Ilikuwa ni moja kati ya safari iliyoniacha katika wakati wa maumivu sana, nilimzoea sana mke wangu, alikuwa ndiyo kila kitu katika maisha yangu.
Hatimaye siku ya safari ikawadia, Julieth mke wangu akaweza kusafiri kuelekea nyumbani kwao Kilimanjaro. Nakumbuka nilipokuwa Ubungo nikimuaga machozi yalikuwa yakinilengalenga mwisho yakaanza kunibubujika.
“Nakupenda sana mke wangu, nitakukumbuka sana,” nilimwambia nilipokuwa nikimuaga.
“Hata mimi nitakukumbuka sana mume wangu, huwezi kuamini yani natamani nisiondoke lakini sina jinsi acha niende nikailee mimba yako nikirudi nitakuletea furaha ya maisha yako,” aliniambia Julieth maneno aliyoyatamka kwa hisia.
Nilishindwa kujizuia nikaamua kumkumbatia, akatulia vyema katika kumbato langu.
“Niambie kitu kimoja kabla hujaondoka,” nilimwambia nilipokuwa nimekumbatiana nae.
“Nakupenda sana na ninakuahidi nitamlea vizuri mwanao,” aliniambia huku akilipapasa tumbo lake. Nilimtoa katika lile kumbato kwa wakati huo muda wa kuondoka basi ulikuwa umefika. Nikamsindikiza kwa zawadi ya mabusu huku moyoni nikiahidi kumtunzia thamani yake kama mke wangu wa ndoa.
****
Nilianza kuyaamini maneno ya Mama yangu, niliamini alikuwa sahihi kuniambia maneno yale ya kunikaripia. Hakika nilijiona kuwa mjinga sana hasa kwa kujaribu kupingana na maneno ya Mama yangu, Mama aliyeniweka miezi tisa tumboni mwake kisha akanizaa kwa uchungu.
Nilihisi kuwa mkosaji na niliamua kwenda kumuomba msamaha kwa yale yote yaliyokuwa yametokea.
Alinisamehe lakini ulikuwa ni msamaha wa masharti.
Alikuwa amenitafutia mwanamke mwingine ambaye alihitaji nimuoe haraka iwezekanavyo na kila kitu alikuwa ameshakiandaa kama maandalizi ya kumuoa mwanamke huyo ambaye alijulikana kwa jina la Evelyne.
Hakutaka kunipa nafasi ya kujielezea lolote kwa wakati huo alipokuwa akinieleza kuhusu Evelyne, alijua fika nisingeweza kukubali kirahisi hivyo aliamua kutumia cheo chake kama Mama katika kunikandamiza.
“Dominick ukitaka nikusamehe na haya yote yaishe yaani nisiwe na kinyongo chochote basi kubali umuoe Evelyne, roho yangu itaridhika,” aliniambia Mama kwa msisitizo.
*Je, nini kitaendelea?*
Tukutane kesho mahali hapahapa.