SEHEMU YA 75...
Huo ndiyo ulikuwa ukweli, Smith hakupunguza neno wala kuongeza neno, kila kitu alichokuwa amekihadithi kilikuwa sahihi kabisa kwamba msichana huyo alikuwa amebadilika kwa asilimia mia moja.
Tatiana akawa huru, kitendo cha kuachana na Smith kilimpa nafasi kubwa ya kuishi kama alivyokuwa akitaka,. Alikulia katika maisha ya dini, alikwenda sana kanisani na hata kuimba kwaya lakini mara baada ya kupata fedha na umaarufu, kila kitu kikabadilika, Tatiana yule wa kipindi cha nyuma hakuwa huyu.
Akajifunza kunywa pombe kwani ndiyo aliamini kwamba kilikuwa kitu pekee alichokuwa amekibakiza katika maisha yake. Kadiri maisha yalicyokuwa yakisonga mbele, Tatiana aliendelea kuharibikiwa zaidi kiasi kwamba akasahau alipotoka.
“Tatiana,” aliita rafiki yake, alikuwa amelewa mno.
“Unasemaje?”
“Naomba niendeshe gari.”
“Hapana! Nitaendesha mimi, gari hii ni yangu,” alisema Tatiana.
“Hapana! Haiwezekani kuendesha na wakati umelewa,” alisema rafiki yake huyo.
Hiyo ilikuwa ni usiku wa saa saba, walikuwa wanatoka katika Klabu ya Casanova iliyokuwa katikati ya Jiji la New York. Siku hiyo Tatiana alikuwa amekunywa pombe nyingi, alilewa chakari huku akiwapa nafasi wanaume kushika maungo yake.
Japokuwa alikuwa amekunywa kiasi kikubwa cha pombe, bado alihitaji kuendesha gari kitu kilichokataliwa na rafiki yake huyo. Huku akibisha, Tatiana akaingia garini, rafiki yake hakuwa na jinsi, naye akaingia na kuanza kuondoka mahali hapo huku watu wakiwaangalia kwani hapo nje bado kulikuwa na wengi waliokuwa wakimpiga picha.
“Puuuuuuuu......!!” ulisikika mlipuko mkubwa wa bomu, watu wakshtuka, wengine wakaanza kukimbia huku na kule, gari alilokuwa amepanda Tatiana likalipuka na kuanza kuteketezwa kwa moto.
Sauti za wasichana wawili zikaanza kusikika wakipiga kelele, moto mkubwa ulikuwa ukiliteketeza gari lile jambo lililowafanya watu wengi kushtuka, hawakuelewa kile kilichokuwa kimetokea, badala ya kuanza mishemishe ya kuuzima moto ule, walibaki wakiangalia kwa mshangao mkubwa huku kelele za Tatiana na rafiki yake zikiendelea kusikika ndani ya gari hilo.