SEHEMU YA 44...
“Wewe ni mpenzi wangu Tatiana, haiwezekani kuona ukiolewa na mtu mwingine, siwezi kuona harusi hii ikitokea,” ilisikika sauti ya mwanaume mmoja akiongea kwa hasira sana huku mkononi akiwa ameshika chupa ya pombe kali aina ya John Walker.
Mwanaume huyo alisimama katika mlango wa kanisa, alionekana kuwa mlevi, nywele zake zilikuwa timutimu. Kanisani hapo kulikuwa na watu wengi waliokuwa wamekuja kuhudhuria harusi iliyokuwa imetangazwa sana kati ya Tatiana na mwanaume wa Kizungu. Msichana Tatiana alisimama mbele ya kanisa hilo huku akiwa na mwanaume wa Kizungu aliyevalia suti nyeupe.
Ilikuwa ni siku ya harusi yake, mwanaume huyo wa Kizungu alikuwa Smith aliyekuwa kwenye mshangao mkubwa mara baada ya kumuona mwanaume huyo mlevi akiingia kanisani na kutaka mchungaji asifungishe ndoa, alikuwa Peter.
Kichwani akawa na mawazo, mwanaume yule alikuwa nani na alikuwa na uwezo gani wa kusimamisha ndoa ile isifanyike? Kila alipojiuliza, alikosa jibu kabisa.
Tatiana hakuzungumza kitu, alikuwa akimwangalia mwanaume yule huku akiwa kimya kabisa, kilio cha kwikwi kikaanza kusikika kutoka kwake, alikuwa kwenye kipindi kingine kigumu kuliko vipindi vyote maishani mwake.
Wazazi wake ambao walikuwa kwenye viti vya mbele kabisa walibaki wakimwangalia mwanaume yule aliyeonekana kuwa chakari kutokana na pombe kali alizokuwa akinywa.
Huku kanisa likiwa limetaharuki, mara mtu mwingine akaingia kanisani humo akiwa hoi, mwili wake ulijeruhiwa na alikuwa na bandeji kubwa mwilini mwake. Alipomuona, alimkumbuka vilivyo kwamba mwanaume huyo alikuwa Nathan, alisimama kule mlangoni na kuanza kuzungumza kwa sauti kubwa,
“Tatiana....” alianza kusema Nathan na kuendelea:
“Hata kama umenifanyia hivi, kuniua ili uolewe na huyu Mzungu wako, kumbuka ni jinsi gani ninakupenda, kumbuka ni jinsi gani tulivyokuwa pamoja,” alisema Nathan, watu wote waliokuwa kanisani wakabaki kimya.
Smith alionekana kuwa na hasira mno, kila alipokuwa akiwaangalia watu hao alishikwa na hasira zaidi hali iliyompelekea kuchomoa bunduki yake iliyokuwa kiunoni na kisha kuanza kuwasogelea watu wale.