Penzi bila maumivu

Penzi bila maumivu

SEHEMU YA 21...
Hakukuwa na kipindi ambacho Peter alikuwa kwenye presha kubwa kama kipindi hicho, kila siku alikuwa mtu wa kusikilizia kama barua aliyokuwa akiihitaji ilikuwa imeingia au la. Yeye ndiye aliyemwambia baba yake kwamba katika kipindi ambacho atakuwa hapo nyumbani, basi apewe ufunguo wa posta ili aweze kuwa nao.

Hilo halikuwa tatizo, kila siku ilikuwa ni lazima aende kuangalia kwenye sanduku la posta ili kuona kama ametumiwa barua na msichana huyo au hakuweza kuandika kwa kuwa alikuwa kipofu.

Baada ya wiki moja, alipokwenda kufungua sanduku la barua, macho yake yakatua katika bahasha moja ndogo, ilikuwa na karatasi huku kwa juu ya ile bahasha kukiwa na jina lake. Moyo ukamlipuka, hakuamini kama ile barua alikuwa ametumiwa yeye au aliona vibaya, akaichukua na kuanza kuiangalia vizuri, liliandikwa jina lake.

Hakutaka kuchelewa, nyumbani alipaona mbali, alichokifanya, hapohapo akaifungua barua ile, kitu cha kwanza kukutana nacho ilikuwa ni harufu nzuri ya manukato yaliyoichezesha pua yake na kumfanya kusahau kama alikuwa posta kulipokuwa na watu wengi.

“Mungu wangu! Mpaka kopa,” alisema Peter huku akiwa ameifungua bahasha ile na kukutana na mchoro wa kopa.
Nyumbani kulikuwa mbali, hakutaka kwenda kuisoma barua hiyo nyumbani kwao, alichokifanya ni kwenda pembeni na kisha kuifungua.

“Naweza nikanyeshewa na mvua au kugongwa na gari na barua nisiiisome, ngoja niisome hapahapa,” alisema Peter na kukaa chini, pembeni kidogo na sehemu iliyokuwa na masanduku yale ya posta.
Kwako Peter.

Nashukuru kwa barua yako iliyonisisimua, imenifanya kujiona nikiingia kwenye ulimwengu mpya ambao sikuwa nikiutarajia kwamba ningeingia. Siwezi kuandika mengi, ila kila kitu tumshirikishe Mungu kwani yeye ndiye wa kutufanya tuje kuoana.
Nakutakia maisha mema, nakupenda.
Tatiana Sangiwa.

Peter akashusha pumzi nzito, japokuwa mwandiko ulikuwa umepinda kidogo lakini aliyaelewa vizuri maneno yaliyokuwa yameandikwa. Pasipo kutarajia akajikuta akiibusu barua ile huku akiwa amekenua meno yake.
 
SEHEMU YA 22...
Alijisikia kuwa mtu mpya, aliyepewa tumaini jipya la kuishi, hakukuwa na siku ambayo alijisikia kuwa na furaha kama siku hiyo. Akasimama na kuanza kuondoka mahali hapo, kila mtu aliyepishana naye, alikuwa akimsalimia kutokana na furaha kubwa aliyokuwa nayo.

Kuanzia siku hiyo, akapata msichana ambaye aliamini kwamba angempenda maisha yake yote. Ulipofika muda wa kurudi shule mkoani Shinyanga, akarudi kuendelea na masomo.
“Nitakwenda kwao tu, siwezi kuvumilia,” alijisema Peter.
Masomo hayakupanda hata kidogo, kichwa chake kilichanganywa na uwepo wa Tatiana, kila siku akawa mtu wa kuliandika jina la msichana huyo huku akionekana kama mtu
aliyechanganyikiwa na mapenzi makubwa.

Hakuwa na siri, alijaribu kuwaambia marafiki zake kuhusu Tatiana. Wengi walimshangaa, ilikuwaje amchague mwanamke kipofu katika maisha yake? Wengine wakapuuzia kwa kuona kwamba Peter alikuwa akiwadanganya.
“Msichana kipofu?”
“Ndiyo!”
“Anaitwa nani?”
“Tatiana.”
“Acha masihara Peter, unahisi leo ni Siku ya Wajinga Duniani?”
“Hapana, nipo siriasi, ninampenda Tatiana,” alisema Peter.
Peter aliwaambia marafiki zake wote kwamba alikuwa na msichana aliyekuwa akimpenda kwa mapenzi ya dhati, hakutaka kumficha mtu yeyote yule kwani aliamini kwamba msichana huyo ndiye angekuja kuwa mke wake hapo baadae.

Aliendelea kusoma huku mara kwa mara akiwasiliana na Tatiana kwa njia ya barua, kitu pekee alichokuwa akimwandikia ni kwamba angeweza kumuoa na mwisho wa siku kuishi kama mke na mume.
“Nitakuja huko likizo,” aliandika Peter kwenye mmoja wa mistari katika moja ya barua aliyokuwa akiituma.
Aliona siku zikienda taratibu sana kuliko siku nyingine. Macho yake yalikuwa na kiu mno ya kumuona msichana huyo aliyekuwa akimpenda kwa mapenzi ya dhati kuliko msichana yeyote yule. Kila alipokuwa akilala usiku, usingizi haukumjia kama siku nyingine, ulikuwa usingizi wa mang’amung’amu mpaka alfajiri.

Siku zilikatika zaidi mpaka siku ile ambayo walifanikiwa kufunga shule na hatimaye kuondoka shuleni hapo. Hakutaka kuelekea Mwanza, kitu alichokifanya ni kuelekea katika Kijiji cha Chibe kwa ajili ya kumuona Tatiana tu.
 
SEHEMU YA 23...
Njiani, alitamani kuliendesha gari lile kwani alimuona dereva akiendesha taratibu mno. Njia ilikuwa na mashimo mengi lakini hiyo haikuonekana kuwa sababu ya kutosha kumwambia Peter kwamba gari lilitakiwa kuendeshwa hivyo hasa barabara inapokuwa mbaya.
“Nikuulize swali kaka?” alimuuliza jamaa aliyekuwa naye pembeni.
“Swali gani?”
“Umeoa?”
“Ndiyo! Kwani nini?”
“Hivi siku ya kwanza kwenda kuonana na mpenzi wako ambaye ndiye mkeo kwa sasa, ulijisikiaje?” aliuliza Peter huku akiachia tabasamu.
“Kwa nini unauliza hivyo?”
“Nataka kujua tu.”

“Nilijisikia furaha sana kwa kuwa alikuwa mwanamke pekee niliyempenda kwa dhati,” alijibu mwanaume huyo.
“Asante sana kwa majibu yako,” alisema Peter na kuyapeleka macho yake nje huku tabasamu pana likiendelea kuwepo usoni mwake.
Gari lilichukua masaa mawili hatimaye kufika katika Kijiji cha Chibe ambapo Peter akateremsha mabegi yake na kuanza kuelekea ndani ya kijiji kile. Japokuwa hakuwa amezoeleka kijijini pale lakini alikuwa na uhakika kwamba angepokelewa vizuri kwa kuwa tu baba yake alikwishawahi kufanya mkutano wa Injili kijiji hapo.

Alipofika, hatua ya kwanza kabisa ilikuwa ni kwenda nyumbani kwa mzee Sangiwa, alipofika hapo, akapokelewa vizuri na kukaribishwa.
“Karibu sana Peter,” alisema bi Frida huku uso wake ukiwa kwenye tabasamu pana.
“Nashukuru mama.”

Mgeni alikuwa amefika nyumbani, kila mmoja alikuwa na furaha kumuona, chumba kikaandaliwa kwa ajili yake. Alipewa heshima kubwa kwa kuwa alimuahidi mtoto wao mambo makubwa kwamba angemuona na kuwa mke wake wa ndoa hata kama alikuwa kipofu.
Upendo wa Frida kwa Peter ulikuwa mkubwa, hata mzee Sangiwa alipoambiwa kuhusu Peter, bila kupenda akajikuta akianza kumpenda kijana huyo.
Peter alitulia sebuleni, macho yake yalikuwa yakimwangalia kila mtu aliyekuwa akipita mbele yake. Mtu ambaye alitaka kumuona kwa wakati huo hakuwa mwingine bali Tatiana ambaye alimkumbuka mpaka kuhisi kuumwa.

Itaendelea.
 
SEHEMU YA 24...
Alikaa zaidi ya masaa mawili, hakufanikiwa kumuona Tatiana au hata kuisikia sauti yake jambo lililomfanya kuwa na wasiwasi mwingi kwamba kulikuwa na tatizo limetokea kwani kama angekuwepo, angekuwa amekwishaitwa mbele yake kwa ajili ya kuzungumza naye.

“Mama...” aliita Peter.
“Unasemaje mwanangu?”
“Siwezi kulala usiku wa leo pasipo kumuona Tatiana. Yupo wapi?” aliuliza Peter, bi Frida akashtuka.
“Eeeh! Kwani hakukwambia?”
“Kuniambia nini?”
“Kwamba alikuwa anasafiri?”
“Anasafiri? Kwenda wapi?”
“Marekani!”
“Marekani?”
“Ndiyo!”

“Hapana! Hakuniambia, ilikuwaje?” aliuliza Peter huku akionekana kuchanganyikiwa.
“Alifuatwa na kwenda Marekani.”
“Alifuatwa na nani?” aliuliza Peter huku akionekana kuwa na presha kubwa, akahisi mwili wake ukinyong’onyea na nguvu kuanza kumuisha. Kijasho chembamba kikaanza kumtoka.

Itaendelea.
 
SEHEMU YA 25...
Alikuwa miongoni mwa matajiri wakubwa nchini Marekani ambao walimiliki mali nyingi huku akiwa na kiasi cha dola bilioni arobaini katika akaunti yake. Mwanaume huyu aliyekuwa na mke mmoja aitwaye Posh, alibahatika kupata watoto watatu tu katika maisha yake.
Alikuwa na kila kitu alichokuwa akikihitaji, aliendesha magari ya kifahari na kununua nyumba zilizokuwa na hadhi ya kukaliwa na watu wenye fedha nyingi kama yeye.

Mzee huyu aliyejulikana kwa jina la Garrett Warrenalikuwa mfanyabiashara mkubwa aliyekuwa akijiingiza mamilioni ya dola kila siku. Maisha yake yalikuwa ya kifahari na alipendwa na watu wengi kwa kuwa tu alikuwa mtu wa kuisaidia jamii.
Alimpenda Mungu, alivisaidia vyuo vingi vya dini, aliwasaidia watoto yatima na hata wale waliokuwa wakiishi katika maisha ya kimasikini. Katika mambo yote aliyokuwa akiyafanya, aliamini kwamba hakukuwa na mtu ambaye alifilisika baada ya kuwasaidia watu.

Baada ya miaka mingi kupita huku akijihusisha na biashara mbalimbali, ndipo alipopata wazo moja kwamba ilikuwa ni lazima aanzishe kipindi maalumu kwenye luninga ili aweze kuwatafuta waimbaji bora nchini Marekani na kuwashindanisha huku mshindi akijinyakulia kitita cha dola milioni moja ambazo ni zaidi ya shilingi bilioni moja kwa fedha ya Kitanzania.
Wazo hilo likapitishwa, akamwambia mkewe ambaye alimpa jina la shindano hilo liitwe American Pop Idol.Alichokifanya, kupitia televisheni yake, akaanza kutangaza kwamba waimbaji walikuwa wakihitajika huku kiwango hicho cha fedha kama zawadi kikiwekwa wazi kitu kilichowachanganya watu wengi na hivyo kujisajili.

Sehemu ambayo fainali ilitakiwa kufanyika ilikuwa jijini California ila mashindano madogomadogo yalitakiwa kufanyika katika kila jiji nchini Marekani. Ndani ya siku saba tu, tayari watu zaidi ya milioni moja walikuwa wamejiandikisha hivyo mchakato kuanza.

American Pop Idol likawa shindano lililomuingizia kiasi kikubwa cha fedha kupitia matangazo na wadhamini, utajiri wake uliongezeka huku shindano hilo likichukua miezi sita na hatimaye mshindi wa shindano hilo kupatikana huku yeye kama yeye akiwa ameingiza kiasi cha dola bilioni tano.

Itaendelea.
 
SEHEMU YA 26...
“This is good business, I thank God for giving me this idea,” (Hii ni biashara nzuri, asante Mungu kwa kunipa wazo hili) alisema bwana Warren huku akiangalia kiasi cha fedha kilichoingizwa ndani ya akaunti yake.

Hakuishia hapo, bado alihitaji kutengeneza fedha zaidi, kila mwaka akawa na kazi ya kuandaa shindano ambalo lilimfanya kuwa maarufu huku likimuingizia fedha nyingi. Mwaka wa tano ulipofika baada ya mchakato wa usajili wa shindano hilo kuanza, hapo ndipo alipoamua kwenda nchini Tanzania.
Alikwenda huko huku lengo lake kubwa likiwa ni kupanda mlima Kilimanjaro na kutembelea mbuga za wanyama pamoja na familia yake wakiwemo watoto wake, Laurent, Jessica na kaka yao mkubwa Smith.

Walipofika huko, wakafanya kama walivyokuwa wamepanga na hivyo kutaka tena kusafiri mpaka Butiama, Musoma kwa ajili ya kuangalia makumbusho ya Mwalimu Julius Nyerere aliyezikwa huko.
“Tunakwenda huko, lakini nina wazo,” alisema bwana Warren, alikuwa akimwambia mkewe huku safari ikiendelea.
“Wazo gani?”

“Tumejitahidi sana kufanya shindano la American Pop Idol nchini Marekani kwa kuwashirikisha Wamarekani, hivi hatuwezi kuwatafuta Watanzania wenye uwezo nao wakaenda huko kushindana?” aliuliza bwana Warren.

“Inawezekana, lakini tutawapataje hao washiriki kutoka huku?”
“Hakuna tatizo, nahisi tunaweza kwenda makanisani, huko, kuna waimbaji wengi tu, nahisi hatutoshindwa, halafu shindano letu litakuwa la kihistoria,” alisema bwana Warren.
“Na mimi nina wazo.”
“Lipi?”
“Kwa nini tusiwashindanishe Wamarekani na hawa Waafrika waliopo huku?” aliuliza bi Stellah.

“Wazo zuri sana, tuanze mchakato.”
Hicho ndicho walichokifikiria kwa wakati huo, walichokifanya mara baada ya kufika Musoma, moja kwa moja wakaanza kutembelea makanisani kutafuta waimbaji ambao waliwaona kustahili kushindana katika shindano lao.
Ilikuwa kazi kubwa ambapo baadae wakaamua kuwaachia watu ili waendelee kuwatafuta waimbaji wengine wengi kwa ajili ya mchakato huo huku matangazo yakianza kutangazwa nchini Marekani kwamba shindano la American Pop Idol mwaka huo lingekuwa la aina yake kwani Wamarekani wangepata nafasi ya kushindana na Waafrika, kila mmoja akalisubiria kwa hamu.
 
SEHEMU YA 27...
“Do you really want best singers?” (Hivi kweli mnahitaji waimbaji bora?) aliuliza jamaa mmoja, alikuwa akizungumza na bwana Warren.
“Yes, we do. Do you know anyone who can sing?” (Ndiyo, tunahitaji. Unamfahamu yeyote anayeweza kuimba?) aliuliza bwana Warren.

“Just wait,” (Subirini) alisema kijana yule na kusogea pembeni.
Alichokifanya ni kuchukua simu yake na kupiga sehemu fulani, baada ya sekunde kadhaa, alikuwa akizungumza na mtu simuni. Alikuwa akimuuliza kuhusiana na muimbaji mmoja ambaye kwake alimuona kuwa bora zaidi, muimbaji huyo alikuwa Tatiana.

Alipoambiwa kwamba msichana huyo alikuwepo kijijini, akawaambia Wazungu wale kwamba muimbaji huyo ambaye alikuwa bora kwa kipindi hicho, alikuwa kijijini. Safari yao ya kwenda Butiama ikasitishwa hivyo kuanza safari yakuelekea Shinyanga.
Hawakuchukua masaa mengi wakafika huko ambapo wakaanza kuelekea katika Kijiji cha Chibe. Ilikuwa safari ndefu na ya kuchosha mno lakini hawakutaka kukata tamaa, walihitaji kumuona muimbaji huyo ambaye aliendelea kusifiwa na kijana yule kwamba alikuwa na sauti nzuri mno.

Walipofika Chibe, moja kwa moja wakaingia ndani kabisa ya kijiji kile na kijana yule kuwapeleka mpaka kwa mzee Sangiwa. Hapo, akaanza kuwaambia wazazi wa Tatiana kwamba wale walikuwa wageni wao na walikuwa hapo kwa kuwa walihitaji waimbaji wazuri.

“Ila umewaambia kwamba binti yangu ni kipofu?” aliuliza mzee Sangiwa.
“Hapana, sasa wewe si ndiyo uwaambie.”
“Sasa kwani mimi najua Kizungu? Waambie wewe,” alisema mzee huyo na kijana huyo kuwaambia.

“Wamesema hakuna tatizo, wanataka kusikia jinsi anavyoimba.”
Hapohapo Tatiana akaitwa na kuanza kuambiwa juu ya ugeni ule, hakuamini kama kweli alisimama mbele ya Wazungu waliotaka aimbe ili kama atakuwa yupo vizuri basi wamchukue na kwenda naye Marekani, akafanya hivyo.

Sauti yake kali ilimfanya kila mtu kutokuamini kama sauti ile ilikuwa ikiimbwa na mtu, walikwishazoea kuzisikia sauti zile kutoka studio ambazo zilichanganywa na mashine, lakini siku hiyo, wakakutana na msichana aliyekuwa akiimba kiasi kile.
 
SEHEMU YA 28...
Hawakutaka kupoteza muda, Tatiana akaonekana kustahili kushirikia shindano hilo, walichokifanya ni kuomba kumchukua, hilo wala halikuwa tatizo.
“Naomba wasimuuze binti yangu,” alisema bi Frida.
“Hakuna tatizo, hakiwezi kutokea kitu kama hicho.”
“Sawa. Tunakuamini.”

Hakukuwa na cha zaidi mahali hapo, kwa kuwa walikuwa wamekwishakubaliana, walichokifanya ni kumwambia Tatiana ajiandae tayari kwa kusafiri na kuelekea nchini Marekani kushiriki shindano hilo lililoendelea kujinyakulia umaarufu huku kwa wakati huo, mshindi alitakiwa kuvuna dola milioni tano, zaidi ya bilioni kumi za kitanzania.

Tatiana hakuonekana kuwa na raha, moyo wake ulikuwa ukimuwaza Peter tu. Alijua ni kwa jinsi gani mwanaume huyo alikuwa akimpenda, alimthamini japokuwa alikuwa kwenye hali ya upofu.
Alijua fika kwamba angeumia mno endapo angemwambia ukweli kwamba alitakiwa kusafiri kuelekea nchini Marekani, hivyo alichokifanya ni kubaki kimya tu.

Baada ya mwezi mmoja wa maandalizi kufanyika, bwana Warren na mkewe, Stellah wakafika kijijini hapo na kumchukua Tatiana kwa ajili ya kuelekea nchini Marekani. Tatiana hakuamini kile kilichokuwa kikitokea, katika maisha yake yote hakuwahi kutoka nje ya kijiji kile, aliyapenda mazingira ya hapo lakini kitendo cha kuambiwa kwambaalitakiwa kuondoka, kilimsononesha mno.
“Nakutakia ushindi mwema Tatiana,” alisema mama yake.

“Asante mama. Naomba msimwambie Peter, akiniulizia, mwambieni ninampenda sana na hakuna zaidi yake. Namuahidi kuwa naye maisha yangu yote,” alisema Tatiana huku akilia.
“Nitamwambia tu.”
“Nitashukuru mama. Mwambie kwamba ninampenda....please mama mwambie kwamba ninampenda,” alisema Tatiana.
“Nitamwambia kila kitu.”

Hakukuwa na cha kupoteza mahali hapo, walichokifanya ni kuanza safari kuelekea Dar es Salaam ambapo huko wangechukua washiriki wengine watano na kukamilisha idadi ya washiriki ishirini kutoka mikoa mingine.

Mchakato huo haukufanyika Tanzania tu bali kwenye kila nchi huku Waafrika elfu moja waliokuwa na uwezo wa kuimba vizuri wakitakiwa kwenda nchini Marekani kitu kilichoonekana kuwa faraja kwa familia zao, na wote hao waliwaombea watoto wao ushindi mkubwa kwani waliamini kwamba maisha yao yangebadilika.
 
SEHEMU YA 29...
“Tunakwenda Marekani sasa, wewe unaitwa nani?” aliuliza msichana mmoja aliyekuwa amekaa na Tatiana.
“Naitwa Tatiana, wewe?”
“Mimi naitwa Maria. Nimefurahi kukufahamu,” alisema Maria.
“Na mimi pia nimefurahi kukufahamu.”
“Nikwambie kitu Tatiana?”
“Niambie, kitu gani?”
“U msichana mrembo sana, sijawahi kuona. Una sura nzuri mpaka nakuonea wivu,” alisema Maria.
“Kweli?”
“Hakika.”
“Utukufu kwa Mungu,” alisema Tatiana, muda huo walikuwa kwenye ndege wakielekea jijini Dar es Salaam.


*****
Kwa jinsi uso wa Peter ulivyokuwa tu, tayari alionyesha kwamba mudawowote ule machozi yangeanza kumbubujika. Bi Frida akaanza kumuelezea kile kilichokuwa kimetokea mpaka binti yake kuchukuliwa na kuelekea nchini Marekani.
Moyo wa Peter ulikuwa kwenye maumivu makali, hakuamini kile alichokisikia lakini kutokana na hali ilivyoendelea, hakuwa na jinsi kuamini kila kilichokuwa kikielezwa mbele ya masikio yake.

Moyo wake ulinyong’onyea huku kipindi kingine akihisi kwamba huo ndiyo ungekuwa mwisho wa kuwa na msichana huyo mrembo, hata nguvu ya kuendelea kukaa kijijini hapo hakuwa nayo tena.
Angewezaje kukaa kijijini na wakati yule aliyemfanya kuwa mahali hapo hakuwepo? Kila alipofikiria kwamba ni kwa jinsi gani angeendelea kukaa kijijini hapo, akakosa jibu.
“Kwa hiyo atarudi lini?”
“Bado hatujajua, nahisi mpaka atakapotoka kwenye mashindano,” alijibu bi Frida.

Kwa kuwa muda ulikuwa umekwishakwenda sana, Peter hakuwa na jinsi, siku hiyo akalala hapohapo kijijini japokuwa muda mwingi kitandani alikuwa na mawazo tele juu ya mpenzi wake huyo.
Hakupata usingizi kwa haraka kama ilivyokuwa siku nyingine, alibaki akibimbirika kitandani tu, kila alipogeuka, taswira ya uso wa Tatiana ilikuwa ikionekana kichwani mwake jambo lililomfanya kukosa usingizi mpaka ilipofika saa kumi alfajiri.

“Ninataka kuondoka,” alisema Peter, alikuwa ameamka asubuhi huku mwili wake ukiwa umechoka mno.
“Mbona mapema?”

“Sina amani kukaa hapa, Tatiana hayupo, unafikiri nitaendeleaje kuishi hapa mama?” aliuliza Peter.
“Sawa, hakuna tatizo. Ila siku ya mwisho alivyoondoka alisema nikwambie kwamba anakupenda, anakupenda na kukupenda sana anataka umuoe na muishi pamoja,” alisema bi Frida.
 
SEHEMU YA 30...
“Kweli?”
“Ndiyo! Huo ndiyo ujumbe pekee alioniambia kuhusu wewe,” alisema mwanamke huyo.
“Nashukuru, ninampenda pia.”
Siku hiyo Peter hakutaka kuendelea kubaki kijijini hapo, alichokifanya ni kuondoka. Njiani alikuwa na mawazo tele, bado alimkumbuka Tatiana, lengo lake kubwa la kwenda kijijini kule lilikuwa ni kuonana naye, akae naye na kumuahidi mambo mengine mengi ambayo angejitahidi kuyafanya pamoja naye likiwepo suala la kumuoa na kuishi naye mpaka kifo kiwatenganishe.

“Tatiana, ninakupenda mpenzi, naomba urudi haraka nchini Tanzania, hakika sitoweza kukusaliti, nakuahidi kuwa nawe maisha yangu yote,” alisema Peter huku akiangalia nje, mawazo juu ya Tatiana yalikuwa mengi mno.

Itaendelea......
 
SEHEMU YA 31...
Ndege iliendelea kukata mawingu huku msichana Maria akiendelea kumsifia Tatiana kutokana na uzuri mkubwa aliokuwa nao. Sifa zile zikaendelea mpaka zikaonekana kumchosha Tatiana kwani kwenye kila sentensi kumi alizokuwa akiziongea Maria, aliingizia suala la uzuri wake.

Safari iliendelea zaidi mpaka walipoingia Dar es Salaam ambapo wakapelekwa katika Hoteli ya Kilimanjaro na kisha kuambiwa kwamba walitakiwa kusubiri kwa wiki mbili mpaka mchakato wa kuwakusanya waimbaji wengine kutoka mikoa mbalimbali utakapokamilika.
Huko, kila siku walikuwa wakichukuliwa na kupelekwa ufukweni ambapo walikuwa wakifanya mazoezi ya kuimba ili kujiweka sawa hata kabla ya kwenda nchini Marekani kwa ajili ya mashindano.
Uzuri wa Tatiana ulikuwa gumzo mno, japokuwa alikuwa kipofu lakini alionekana kumvutia kila mtu. Mbali na uzuri wake, sauti yake ilikuwa nzuri ambayo ilizitetemeza ngoma za masikio ya kila mtu aliyekuwa akiisikia.

Tatiana alikuwa kama kiongozi, kila walipokuwa wakiimba, yeye ndiye aliyechaguliwa kuwapanga wenzake na mpangilio wa sauti ukiwa sauti ya kwanza, ya pili, ya tatu mpaka besi.
Maandalizi hayo yaliendelea kufanyika kila siku, asubuhi na mapema waliamka na kwenda katika ufukwe na kufanya mazoezi hapo. Kila mmoja alionyesha uwezo wake huku hata walimu ambao waliitwa mahali hapo mara kwa mara waliwapa mazoezi mazito ya sauti huku wakiamini kwamba mshindi wa shindano hilo angetoka mahali hapo.

“Namfundisha mshindi wa shindano hili hapa,” alisema mmoja wa walimu ambaye alionekana kuwa mchangamfu mno.
“Natumaini mshindi wa shindano hili atatoka hapa. Jamani, kuna siku mtanitafuta na kuniambia kweli mwalimu Luciana utabiri wako ulikuwa mkubwa. Mnakwenda Marekani, huko, wala msiogope, wale hawazaliwagi na vipaji, wale wanaingia darasani na kujifunza, ila nyie, niaminini, mna vipaji vya kuimba, na mshindi yupo kati yetu,” alisema mwalimu Luciana maneno yaliyomfariji kila mmoja.
Mazoezi yaliendelea kila siku, badala ya wiki moja kama walivyoambiwa walichukua wiki mbili mpaka kumaliza mazoezi hayo huku wale waimbaji kutoka mikoa mbalimbali wakiwa wamekwishafika na kujumuika pamoja.
 
SEHEMU YA 32...
Kila mmoja aliyekuwa akimwangalia Tatiana, alikiri kwamba msichana huyo alikuwa mzuri kwa umbo na sura japokuwa alikuwa kipofu.
Tatiana alizoeana na Maria sana, yeye ndiye alikuwa rafiki wake wa dhati, kila alipokuwa, msichana huyo alikuwa pembeni yake na huku akichukua jukumu la kumuongoza kila alipotaka kwenda.
Baada ya wiki mbili kutimia, bwana Warren akafika jijini Dar es Salaam, kitu cha kwanza kilikuwa ni kuwaita na kisha kuwaweka katika chumba cha mkutano na kuanza kuzungumza nao.

Alitumia muda mwingi kuwatoa wasiwasi na wajisikie huru na kwamba wangeweza kushindana mpaka kushinda, hata yeye aliamini kwamba mshindi wa shindano lile kwa mwaka ule angetokea barani Afrika japokuwa hakujua ni nchi gani.
“Jua kwamba wewe ni mshindi, sijajua kwa nini, moyo wangu unaniambia kwamba mshindi wa shindano hili anatokea Afrika japokuwa sijajua ni nchi gani. Ila ninachoamini, mshindi anatokea katika kundi hili la watu,” alisema bwana Warren huku uso wake ukiwa na tabasamu tele.

Baada ya wiki moja nyingine, washiriki hao wakapanda ndege binafsi ya bwana Warren na familia ya mzee huyo na kuanza safari ya kuelekea nchini Marekani kwa ajili ya kushindana katika Shindano la kumtafuta kumtafuta mwanamuziki bora lililoitwa American Pop Idol, ila kwa kipindi hiki liliitwa America & Africa Pop Idol.

*****
Matangazo yalibandikwa kila kona nchini Marekani, mengine yakatangazwa sana kwamba lile shindano lililokuwa likisubiriwa kwa hamu, American & Africa Pop Idol lilikuwa limebakiza mwezi mmoja kabla ya kuanza.
Watu waliokuwa na uwezo wa kuimba waliendelea kujiandikisha, kila mmoja alitaka kuonyesha uwezo wake na mwisho wa siku kuchukua kitita cha dola milioni tano kilichokuwa kimewekwa.

Fedha zilikuwa nyingi mno na kila mmoja alizitolea macho. Maandalizi yaliendelea kufanyika zaidi huku Wamarekani wengi waliokuwa wamejiandikisha katika shindano hilo, waliwaita walimu wao waliokuwa na kazi ya kuwafundisha namna ya kuimba vizuri ili mwisho wa siku mmojawapo aweze kushinda kitita hicho cha fedha.
 
SEHEMU YA 33...
Hakukuwa na Mmarekani ambaye alitaka kuona fedha hizo zikichukuliwa na mtu mwingine kutoka nje ya Marekani, kwa sababu shindano lilikuwa lao, liliandaliwa nchini mwao na kufanyika humo, hivyo walifanya kila juhudi kuhakikisha kwamba hata fedha hizo zinakwenda katika akaunti ya mtu yeyote ila awe Mmarekani.

Wakati ndege kutoka nchini Tanzania inawasili uwanjani, watu zaidi ya elfu tano walikuwa wamekusanyika mahali hapo kwa ajili ya kuwaona watu hao waliotoka barani Afrika tena katika nchi kama Tanzania ambayo haikuwa ikijulikana sana.
Washiriki hao walipokuwa wakiteremka, kila mmoja alibaki akiwaangalia, kwa muonekano wao wa nje, walionekana kutokuwa na uwezo wowote ule jambo lililowapelekea Wamarekani wengi kuwadharau kwamba hawakuwa na uwezo wowote ule.

Mbali na Watanzania hao waliokuwa wakiingia uwanjani muda huo, Waafrika wengine walikuwa wamekwishaingia na tayari walikwishaanza mazoezi katika Ukumbi wa Abraham Lincoln Theatre uliokuwa katika Jiji la California.
Watanzania hao wakachukuliwa na kisha kupelekwa katika Hoteli ya Cassavana Hill iliyokuwa pembezoni mwa Ufukwe wa Julien. Huko, wakakutana na Waafrika wenzao ambapo moja kwa moja urafiki wao ukaanzia hapo huku wakijipa moyo kwamba iwe isiwe ilikuwa ni lazima kuchukua ushindi katika shindano hilo.
“Where do you come from?” (Umetoka wapi?) aliuliza Maria.

“ Monrovia, Liberia. My name is Nathan, my pleasure to meet you Maria) alisema mwanaume mmoja mwenye sura nzuri aliyekuwa akizungumza na Maria, rafiki yake Tatiana.
Kwa kumwangalia, ungeweza kusema Nathan alikuwa Mtusi. Alikuwa mwanaume mrefu aliyekuwa na mwili mwembamba, sura yake, iliwavutia wanawake wengi waliokuwa wakimwangalia. Hakuwa mzungumzaji sana, alikuwa mkimya na mpaka alipokuwa akizungumza na Maria, msichana huyo ndiye aliyeanza kuzungumza naye.

Moyo wa Maria ulikwishatekwa na kijana huyo, alipomwangalia kwa mara ya kwanza tu, alihisi moyo wake ukifurukuta, hakujiweza, alitokea kumpenda Nathan kupita kawaida na ndiyo maana alishindwa kujizuia kabisa.
 
SEHEMU YA 34...
Mazoezi yalianza rasmi. Mbali na uzuri wa Nathan uliokuwa ukiwapagawisha wasichana wengi katika ukumbi huo lakini uzuri wa msichana Tatiana ndiyo uliokuwa gumzo zaidi. Alikuwa kipofu lakini uzuri wa sura yake ulimfanya kila mwanaume kuvutiwa naye.

Tatiana hakuwa na habari, kitu pekee alichokuwa akikifahamu ni kwamba alifika nchini Marekani kwa kuwa tu kulikuwa na shindano la kumtafuta muimbaji bora, suala la kuwadatisha wanaume wengi wala hakulifahamu.
“I can’t tolerate, I must see her,” (Siwezi kuvumilia, lazima nikutane naye) alisema Nathan.
“Whom do yo want to see?” (Unataka kumuona nani?)
“Sorry man! I miss my home buddy,” (Samahani bwana! Nimepakumbuka nyumbani mshikaji) alisema Nathan.

Alikuwa na mawazo juu ya Tatiana tu kiasi kwamba alijikuta akiropoka pasipo kujua kwamba kijana aliyekuwa naye karibu alikuwa amemsikia na hivyo alitaka kufahamu mtu aliyetaka kumuona. Uvumilivu ukamshinda Nathan, akajikuta siku hiyohiyo akimfuata msichana Tatiana kwa ajili ya kuzungumza naye tu, alitaka kumwambia ukweli wa moyo wake kwamba alikuwa akimpenda sana.
“Tatiana....” aliita Nathan.
“Nathan...” aliita Tatiana, Nathan akashtuka.
“Umenijuaje?”

“Nimeweza kukujua tu, nawajua wote humu ndani.”
“Umenishangaza sana. Umejiandaaje na ushindani?”
“Kawaida tu, nataka dunia iamini kwamba nina kipaji cha kuimba. Siangalii fedha zao, ningependa nionyeshe uwezo wangu tu,” alijibu Tatiana.
“Kwa hiyo hutaki fedha?”

“Unapokuwa na kipaji, fedha zitajileta tu, ngoja niionyeshe dunia kwamba kulekule nchini Tanzania, tena kijijini kabisa kulikuwa na mtu aliyekuwa na kipaji cha kuimba,” alisema Tatiana.
Kila alipokuwa akizungumza, Nathan alikuwa akimwangalia Tatiana usoni tu, bado kichwa chake kilikuwa kikijiuliza kama kweli msichana aliyekuwa na uzuri ule alipatikana kweli duniani au alikuwa ameshushwa kutoka Mbinguni.
“Nathan...” aliita Tatiana.
“Naam.”
“Naomba usiniangalie sana, nasikia aibu,” alisema Tatiana.
“Nisikuangalie sana?”
“Ndiyo!”
“Kwani nilikuwa nakuangalia sana?” aliuliza Nathan huku akishangaa msichana huyo alijuaje.
“Ndiyo!”
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom