SEHEMU YA 29...
“Tunakwenda Marekani sasa, wewe unaitwa nani?” aliuliza msichana mmoja aliyekuwa amekaa na Tatiana.
“Naitwa Tatiana, wewe?”
“Mimi naitwa Maria. Nimefurahi kukufahamu,” alisema Maria.
“Na mimi pia nimefurahi kukufahamu.”
“Nikwambie kitu Tatiana?”
“Niambie, kitu gani?”
“U msichana mrembo sana, sijawahi kuona. Una sura nzuri mpaka nakuonea wivu,” alisema Maria.
“Kweli?”
“Hakika.”
“Utukufu kwa Mungu,” alisema Tatiana, muda huo walikuwa kwenye ndege wakielekea jijini Dar es Salaam.
*****
Kwa jinsi uso wa Peter ulivyokuwa tu, tayari alionyesha kwamba mudawowote ule machozi yangeanza kumbubujika. Bi Frida akaanza kumuelezea kile kilichokuwa kimetokea mpaka binti yake kuchukuliwa na kuelekea nchini Marekani.
Moyo wa Peter ulikuwa kwenye maumivu makali, hakuamini kile alichokisikia lakini kutokana na hali ilivyoendelea, hakuwa na jinsi kuamini kila kilichokuwa kikielezwa mbele ya masikio yake.
Moyo wake ulinyong’onyea huku kipindi kingine akihisi kwamba huo ndiyo ungekuwa mwisho wa kuwa na msichana huyo mrembo, hata nguvu ya kuendelea kukaa kijijini hapo hakuwa nayo tena.
Angewezaje kukaa kijijini na wakati yule aliyemfanya kuwa mahali hapo hakuwepo? Kila alipofikiria kwamba ni kwa jinsi gani angeendelea kukaa kijijini hapo, akakosa jibu.
“Kwa hiyo atarudi lini?”
“Bado hatujajua, nahisi mpaka atakapotoka kwenye mashindano,” alijibu bi Frida.
Kwa kuwa muda ulikuwa umekwishakwenda sana, Peter hakuwa na jinsi, siku hiyo akalala hapohapo kijijini japokuwa muda mwingi kitandani alikuwa na mawazo tele juu ya mpenzi wake huyo.
Hakupata usingizi kwa haraka kama ilivyokuwa siku nyingine, alibaki akibimbirika kitandani tu, kila alipogeuka, taswira ya uso wa Tatiana ilikuwa ikionekana kichwani mwake jambo lililomfanya kukosa usingizi mpaka ilipofika saa kumi alfajiri.
“Ninataka kuondoka,” alisema Peter, alikuwa ameamka asubuhi huku mwili wake ukiwa umechoka mno.
“Mbona mapema?”
“Sina amani kukaa hapa, Tatiana hayupo, unafikiri nitaendeleaje kuishi hapa mama?” aliuliza Peter.
“Sawa, hakuna tatizo. Ila siku ya mwisho alivyoondoka alisema nikwambie kwamba anakupenda, anakupenda na kukupenda sana anataka umuoe na muishi pamoja,” alisema bi Frida.