SEHEMU YA 12...
Hali hiyo ilimshangaza, haikuwa kawaida kwani alikuwa na watoto, tangu walipokuwa na muda huo, kila alipokuwa akiuchezesha mkono wake, zile mboni nyeusi zilikuwa zikihama kwenda huku na kule kuufuata mkono ule.
“Huyu mtoto ana nini?” aliuliza Frida.
“Kwa nini?”
“Mboni zake hazichezi kabisa.”
“Unasemaje?”
“Ndiyo hivyo! Hebu jaribu kuchezesha vidole vyako mbele yake,” alisema Frida, alikuwa akimwambia mumewe, Sangiwa ambaye akafanya hivyo, kweli mboni hazikuwa zikicheza.
Hilo likaonekana tatizo kubwa, wazazi hao wakachanganyikiwa, wakajua kwamba kulikuwa na kitu hakikuwa sawa kabisa, walichokifanya ni kusafiri mpaka Shinyanga mjini ambapo huko wakampeleka katika Hospitali ya mkoa ambapo madaktari wakaanza kumpima na kugundua tatizo.
“Poleni sana,” alisema daktari kwa sauti ya taratibu.
“Kuna nini? Mbona pole tena?”
“Mtoto wenu ni mzuri ila ni kipofu.”
“Unasemaje?”
“Tatiana ni kipovu, ana upofu wa kuzaliwa,” alijibu daktari yule.
Frida akashindwa kujizuia, majibu ya daktari yule yalimfanya kuhuzunika na baada ya sekunde chache tu, akaanza kulia kama mtoto huku akimlaumu Mungu kwa kile kilichotokea.
Mume wake, Sangiwa akashindwa kumfariji kwani hata na yeye alikuwa akibubujikwa na machozi tu, moyo wake ulimuuma pia mpaka kufikia kipindi akahisi hasira zake zikipanda dhidi ya Mungu.
Moyo wake ulikuwa kwenye maumivu makali, hakuamini kama mtoto wake wa mwisho ambapo baada ya hapo angejizuia kuzaa tena alikuwa kipofu, kila alipokuwa akimwangalia, moyo wake uliendelea kumuuma mno.
Hawakuwa na jinsi, wakarudi kijijini huku wakiwa na huzuni tele. Hawakutaka kuficha chochote kile, wakawaambia wanakijiji wengine ambao walizipokea taarifa hizo wakiwa na majonzi tele.
“Poleni sana.”
“Asanteni, haina jinsi, kila kitu ni mipango ya Mungu,” alisema Frida huku akiendelea kububujikwa na machozi.
Huo ndiyo uliuwa mwanzo wa kila kitu. Mtoto Tatiana akaanza kukua, alipofikisha mwaka mmoja, akaanza kujifunza kutembea. Hapo ndipo Frida alipoumia zaidi, kila alipomwangalia mtoto wake, alikuwa akipapasa kila alipokwenda, hakuona, aliishi kwa hisia, kuna wakati alikuwa akijikwaa na kudondoka, alisimama na kuendelea tena.