SEHEMU YA 113...
“Kama mnataka kwenda sawa ila si kwa kesho. Tayari tushafanya maandalizi, tiketi zishapatikana, kama mnataka kwenda nafikiri inatakiwa kufanyika keshokutwa,” alisema Dk. Kimario.
Huo ndiyo uamuzi uliofikiwa, japokuwa hawakutakiwa kuondoka kesho yake lakini wakaomba ruhusa ya kutaka kumuona binti yao, hilo wala halikuwa tatizo, wakachukuliwa na kupelekwa katika chumba alicholazwa Tatiana.
Walipofika hapo, macho yao yalipotua kwa msichana huyo, mzee Sangiwa ambaye macho yake yalikuwa makavu, akashangaa kuona yakianza kulengwalengwa na machozi na ndani ya sekunde kumi tu, machozi yakaanza kumbubujika mashavuni mwake.
Alihisi maumivu makali ya moyo, kwa jinsi binti yake alivyokuwa kimya kitandani pale, alijikuta akikata tanmaa ya kuona akinyanyuka tena kitandani pale. Wakamsogelea, bi Frida alikuwa hoi, tayari machozi yaliyokuwa yamekauka kwa muda yakaanza kububujika tena mashavuni mwake.
Picha ile iliyokuwa ikionekana mbele yake ilimuumiza mno, hakuamini kama binti yake aliyempenda kwa moyo wote, msichana aliyetokea kuwasaidia wao kama wazazi wao na kijiji kizima alikuwa kimya kitandani.
“Tatiana amka mwanangu,” alisema bi Frida huku akiendelea kububujikwa na machozi ya uchungu.
Bandeji kubwa ilifungwa tumboni mwake huku bandeji nyingine kubwa ikifungwa kwa wingi ubavuni mwake ambapo hapo ndipo kulipokuwa na jeraha lile la kuchomwa kwa kisu. Mbali na hiyo, hata mkono wake wa kushoto kulikuwa na bandeji nyingine ambayo kwa mbali ilionekana kuchafuliwa kwa damu zilizokuwa zikiendelea kumtoka japo kwa taratibu sana.
“Dokta, mwananagu ataamka lini?” aliuliza mzee Sangiwa huku akionekana kuchanganyikiwa.
“Ataamka tu.”
“Lini?”
“Hatujajua, ila India ndioyo watatuambia kila kitu. Tumejitahidi sana kuokoa maisha yake, tunatumaini ataamka tu,” alisema Dk. Kimario.
Japokuwa walikuwa na huzuni sana, kulia sana lakini hiyo haikutosha kumuinua Tatiana kitandani pale. Watu walijazana mno hospitalini, kila mtu aliyefika mahali hapo alitaka kuingia ndani ya chumba kile kwa ajili ya kumuona mwanamuziki huyu aliyekuwa hoi kitandani.