Chizi awasilisha barua kwa Waziri Mkuu kupinga 'tuhuma' za Dkt. Mwakyembe dhidi yake - wavuti
Aliyekuwa Kaimu Mkurugenzi wa Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL), Paul Chizi ambaye hivi karibuni alitenguliwa katika cheo hicho na Waziri wa Uchukuzi, Dkt. Harrison Mwakyembe wiki jana, amefikisha ramsi malalamiko yake kwa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda.
Uchunguzi wa gazeti la
Habari Leo umebaini kuwa Chizi amewasilisha malalamiko yake kwa Waziri Mkuu akipinga tuhuma zilizoelekezwa kwake na Waziri, Mwakyembe akidai si za kweli na kwamba zimelenga kumshushia hadhi kwa jamii.
Pamoja na barua hiyo, Chizi amewasilisha lundo la vielelezo vikifafanua tuhuma mbalimbali zilizotolewa na Dkt. Mwakyembe dhidi yake, ili kuthibitisha kutokubaliana na tuhuma hizo kwake. Kaimu Mkurugenzi huyo wa zamani wa ATCL alipotafutwa jana ili kuzungumzia suala hilo alikiri suala hilo kuwasilishwa ofisi ya Waziri Mkuu, ingawa hakuwa tayari kulizungumzia zaidi kwa madai kuwa liko kwenye mamlaka za juu sasa.
Tuhuma ya sare za milioni 80/-
Maelezo ya Chizi kwa Pinda, yanafafanua kwamba ATCL ilinunua loti 30 za vifaa mbalimbali vya wafanyakazi zikiwamo sare zilizotajwa na Dk Mwakyembe kwa thamani ya dola za Marekani 18, 920 na si dola za Marekani 50,000 kama alivyodai Waziri Mwakyembe, hatua ambayo ilifanya ATCL kuokoa zaidi ya Sh milioni 44 kama ingenunua sare hizo nchini kulingana na bei ya ununuzi iliyowasilishwa ATCL.
Tuhuma ya ukodishaji wa ndege
Anapinga pia kuhusishwa na ukodishaji wa ndege aina ya Airbus ambayo Waziri Mwakyembe alisema haikuwa na sababu ya kukodishwa, akisema ndege hiyo ilikodishwa mwaka 2007 na kufanya kazi hadi mwaka 2008, wakati yeye aliteuliwa kuwa Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa ATCL Agosti 2011. Dk Mwakyembe akizungumzia mkataba huo tata wa Airbus, alisema umeifanya nchi kudaiwa Sh bilioni 69 na kusisitiza kuwa kutokana na hali hiyo, Serikali haikuwa tayari kufumbia macho mambo mengine ya ovyo yanayoendelea katika shirika hilo.
"Kuhusu ukodishaji wa ndege aina ya Boeing 737 – 500 kutoka Kampuni ya Aerovisto, utaratibu wa kawaida wa ukodishaji wa ndege kwa njia ya wetlease ulifanyika, taratibu zote kama zinavyotakiwa kisheria zilifuatwa.
"Ilikuwa ni suala la kushitua sana kwangu pale nilipopata maelekezo kutoka kwa Katibu Mkuu (Wizara ya Uchukuzi, Omar Chambo) kwamba taratibu hazikufuatwa, na hivyo ndege tuliyoikodi haikutakiwa kuruka kinyume na barua ya Waziri Mwakyembe mwenyewe ya Mei 12, akieleza kuridhishwa na hatua tulizochukua katika ukodishaji ndege na kuturuhusu kuendelea na mchakato," ilisema barua hiyo.
"Suala la kupeleka mkataba wa ACMI kwa AG (Mwanasheria Mkuu wa Serikali) ambao si utaratibu wa kawaida, lilikuja wakati mchakato wa kuleta ndege uko katika hatua za juu kabisa. Hata hivyo, maagizo yalizingatiwa; mkataba ulikwenda kwa AG hata baada ya Waziri kutoa maoni yake kuwa ni mzuri. Waziri alitoa kauli kama hiyo pia kwenye kikao cha Kamati ya Bunge ya Miundombinu kilipokaa Ofisi Ndogo za Bunge hivi karibuni," ilisema barua hiyo.
Tuhuma za fedha na akaunti
Barua hiyo kwa Waziri Mkuu ikifafanua kuhusu suala la sare za ATCL ilisema lilishafanyiwa uchunguzi baada ya Chambo kuunda Tume kuchunguza ubadhirifu huo ikiongozwa na DAP wa Sekretarieti ya Utumishi wa Umma Shekiondo Magesa na Tume kubaini hakukuwa na ubadhirifu wowote na kumpongeza Chizi kwa kuokoa fedha za Kampuni.
"Madai ya Waziri Mwakyembe kuhusu fedha za bima ni kwamba kampuni ya Alexander Forbes ilitoa taarifa, kuwa fedha za bima zingetumwa kwenye akaunti yetu wiki ya nne ya Mei 2012.
Menejimenti ya ATCL ilikaa na kutafakari agizo la Wizara kutaka fedha hizo zipelekwe CHC (Kampuni Hodhi ya Mashirika ya Umma).
"Tulisubiri kupata akaunti ya CHC ili tutoe maagizo hayo. Hata hivyo, akaunti hiyo tulichelewa kuipata, ndipo tulipokwenda benki kutaka kupata njia mbadala ya kuhakikisha usalama wa fedha zetu. Mei 28 dola za Marekani milioni 3 zililipwa kwenye akaunti yetu ya Stanbic na Menejimenti ya ATCL ikaagiza benki ihamishe fedha hizo ili zishikiliwe kama dhamana ya ATCL kupata mtaji wa kujiendesha.
"Maagizo ya kuhamishwa pesa hiyo ili zihifadhiwe na benki yalitolewa kwa benki siku hiyo hiyo Mei 28. Asubuhi ya Mei 29 wakati mchakato wa kuzihifadhi haujakamilika, tulitaarifiwa kuwa dola milioni moja zimezuiwa na amri ya mahakama kutoka Kampuni ya Ultimate Security yenye thamani ya dola 993,000.
"Hapo hapo tulielekeza wanasheria wetu wazuie utekelezaji wa amri hiyo na jambo hilo lilifanyika na pesa hiyo ipo kwenye akaunti salama hadi leo, hakuna aliyelipwa kama alivyosema Waziri Mwakyembe. Shauri hilo litatolewa uamuzi Juni 18," ilisema barua hiyo.
Kulingana na vielelezo vilivyowasilishwa Ofisi ya Waziri Mkuu, gazeti la
Habari Leo limebaini kuwa wakati Wizara ya Uchukuzi ikiwasilisha barua ya maagizo ya fedha hizo za bima kuwekwa kwenye akaunti ya CHC, malipo hayo ya bima yalikuwa yamelipwa kupitia akaunti ya Stanbic na kampuni ya Alexander Forbes asubuhi siku hiyo.
Gazeti la
Habari Leo lilipowasiliana na Katibu Mkuu wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Peniel Lyimo jana, alithibitisha kupokewa kwa malalamiko hayo kutoka kwa Kaimu Mkurugenzi Mkuu huyo wa ATCL na kusema ofisi yake ilikuwa bado inayafanyia kazi ili kufahamu mwenendo mzima wa suala hilo kabla ya kulizungumzia.
Soma habari nzima katika tovuti ya
gazeti la HabariLeo
Source:
Previous Posts - wavuti