OPERATION GOTHIC SERPENT: Nguvu ya Itikadi, Imani na Ushujaa uliotukuka

OPERATION GOTHIC SERPENT: NGUVU YA ITIKADI, IMANI NA USHUJAA ULIOTUKUKA





Katika sehemu iliyopita tulitazama namna ambavyo vikosi vya marekani vilishambulia 'safe house' katikati ya mji wa mogadishu wakihisi labda Aidid yuko ndani yake. Lakini matokeo yake yalikuwa ni kuuwawa kwa idadi kubwa ya akina mama na watoto ambao hawakuwa na hatia.

Hali hii iliamsha hasira za wananchi wote wa somalia na kufanya hata vikundi vya wapiganaji ambavyo vilikuwa vinapigana miezi mingi kugombea umiliki wa maeneo vyote kugeuka na kuwafanya vikosi vya UNOSOM kuwa ndiye adui yao.


Tuendelee…


Siku ya tarehe 08 August 1993, wapiganaji wa Aidid walifanya shambulio la bomu la kutegesha kwenye msafara wa vikosi vya wanajeshi wa Marekani na kuu wanajeshi wanne papo hapo.
Wiki mbili baadae lilifanyika shambulio lingine dhidi ya vikosi vya marekani na kuwajeruhi vibaya wanajeshi wengine saba.

Huko mwanzoni nilieleza kwamba vikosi vya umoja wa mataifa mwanzoni vilikuwa na lengo la kulinda misafara ya misaada ya kiutu ya umoja wa mataifa ambayo awali ilikuwa inavamiwa na kuibiwa na wapiganaji wa kisomali wenye silaha za moto. Baadae vikosi hivyo vikaongezewa jukumu la kuwa walinzi wa amani ndani ya somalia. Pamoja na jukumu hilo pia waliagizwa kuhakikisha wanaunganisha vikundi vyote vya wapiganaji na kuunda serikali moja ya kitaifa kama ambavyo nilieleza kwenye sehemu iliyopita.

Lakini baada ya mfululizo wa mashambulio haya, Rais wa Marekani kipindi hicho, Bill Clinton aliamua kukubaliana na kutia saini ombi la jeshi la Marekani kupeleka vikosi vya weledi (Special Forces) nchini Somalia ili kukabiliana na tishio la mashambulizi mfululizo ambayo yalikuwa yanalenga vikosi vya Marekani.

Kwa hiyo tarehe 22 mwezi August mwaka 1993 jumla ya Makomando wa weledi wa juu kabisa 400 waliwasili nchini Somalia chini uongozi Meja Jenerali William F. Garrison ambaye kwa kipindi hicho alikuwa ni kamanda wa kamandi maalumu ya pamoja ya vikosi vya weledi (Joint Special Operations Command - JSOC).

Makomando hawa 400 ambao waliowasili nchini Somalia walikuwa wanajumuisha vikosi vifuatavyo;

- Army Rangers (75th Ranger Regiment)
- Delta Force Operators (1st Special Forces Operarional Detachment)
- Navy SEALs
- Waokozi wa kijeshi katika Oparesheni maalumu za weledi kutoka kikosi cha Air Force Pararescuemen (24th Special Tactics Squadron)
- Helikopta za kivita 16 na marubani kutoka kitengo cha Oparesheni Maalumu za Anga (160th Special Operations Aviations Regiment). Helikopta hizi zilikuwa zinajumuisha helikopta adhimu kama vile "Black Hawks" (MH-60) pamoja na "Little Birds" (AH/MH-6)

Makomando hawa 400 walitua nchini Somalia siku ya tarehe 22 August kama ambavyo nimeeleza. Siku moja tu baadae, yaani siku ya tarehe 23 August walifanya oparesheni ndogo ambayo walifanikiwa kumtia nguvuni moja ya wafadhili wa Aidid aliyeitwa Osman Ali Atto.

Huu ulikuwa usbindi muhimu kwa vikosi vya Marekani na vikosi Umoja wa Mataifa kwa ujumla, lakini ushindi huu ulizidisha hasira zaidi kwa Aidid na Wasomali kwa ujumla.
Hasira hizi zilidhihirishwa na kitendo cha wapiganaji wa Aidid ambao walikuwa karibu na Bandari ya Mogadishu kudungua helikopta aina ya "Black Hawk" ya jeshi la Marekani kwa kutumia bomu la kurusha kwa roketi, RPG. Tukio hili lilisababisha vifo vya wanajeshi wote watatu wa Marekani ambao walikuwa ndani ya helikopta.

Huu ulikuwa ni ushindi mkubwa wa kisaikolojia kwa wapiganaji wa Kisomali kwa sababu hii ilikuwa ni mara ya kwanza kwa helikopta ya kijeshi kuwahi kudunguliwa ndani ya Somalia.

Lakini tukio hili pia lilitoa ishara kwa vikosi vya Marekani kwamba wanatakiwa kumsambaratisha Aidid na washirika wake haraka mno kama wanataka vikosi vyao kuwa salama na amani kurejea nchini Somalia.

Vikosi vya Marekani walihaha kweli kweli kwa wiki kadhaa kukusanya intelijensia kuhusu nyendo za Mohamed Farrah Aidid pamoja na viongozi wenzake wa ngazi za juu ndani ya kikundi chake cha Somali National Alliance (SNA).

Naomba tukumbuke kwamba katika kipindi hiki, Aidid alikuwa amejitangaza kuwa yeye ndiye Rais wa Somalia na aliwachagua viongozi wenzake wa juu wa SNA kuwa mawaziri katika 'serikali' yake.

Baada ya kuvuja jasho usiku na mchana kukusanya intelijensia, hatimaye vikosi vya Marekani vilipata taarifa juu ya kikao kitakachofanyika kwenye moja ya jengo katikati ya Mogadishu kati ya Viongozi wawili wa juu kabisa wa SNA ambao ni watu watu wa karibu sana wa Mohamed Farrah Aidid… viongozi hawa walikuwa ni Omar Salad Elmi ambaye alikuwa ni Waziri wa Mambo ya Nje wa serikali ya Aidid ambaye alikuwa anakutana na Mohamed Hassan Awale ambaye alikuwa ni mshauri mkuu wa masuala ya siasa wa SNA.

Baada ya kupata taarifa hii na kuthibitisha uhalali wake, vikosi vya Marekani wakaa chini kwa haraka na kuweka mkakati wa weledi juu ya oparesheni ya kuwakamata washirika hao wajuu wa Aidid.

Mkakati wenyewe ulikuwa ni kwamba; Makomando wa Delta Force watafika mpaka kwenye nyumba ambayo kikao hicho kilikuwa kinafanyika kwa kutumia helikopta aina ya MH-6 "little bird" na kuwakamata washirika hao wa Aidid.
Wakati makomando wa Delta Force wakiwa ndani ya jengo wakiwakamata washirika hao wa Aidid zitawasili helikopta aina ya Black Hawks zikibeba 'chalk' nne Rangers. Hili neno 'chalk' ni sawa sawa kabisa na 'platoon' katika misamiati ya kijeshi. Tofauti yake ni kwamba 'chalk' kinakuwa ni kikundi cha wanajeshi ambao 'wanadeploy' kutoka kwenye chombo cha anga.
Kama wapo ambao hawajui maana ya msamiati wa 'platoon' kwa kifupi ni kwamba, ukubwa wa platoon unategemea na Jeshi la nchi husika na tawi (kikosi) cha jeshi. Kwa mfano kwenye nchi nyingi kwa kadiri ninavyofahamu, platoon inakuwa na wanajeshi 39 kama ni wanajeshi wa miguu au wanajeshi 43 kama ni wanajeshi wa Majini. Lakini pia platoon inaweza kuwa na wanajeshi 18 kama ni platoon ya Snipers au inaweza mpaka kufikia wanajeshi 69 kwa mortor platoon.

Kwa hiyo nikisema 'Ranger Chalk' nadhani unapata picha ni nini hasa naongelea.

Hivyo basi kama nilivyoeleza, mpango ulikuwa kwamba makomando wa Delta force wakishakamata 'targets' basi black hawks zitaleta 'ranger chalk' nne ambao wata-fast rope mpaka chini na kutengeneza mzingo (perimeter) wa pande nne kuzunguka jengo husika ili kuhakikisha kwamba hakukuwa na adui anayeweza kuingia au kutoka ndani ya jengo hilo.

Kisha msafara wa magari tisa aina ya HMMWV pamoja na magari matatu makubwa ya kijeshi aina ya M939 yalitakiwa kuwasili mahala husika kwenye jengo hilo kuchukua makomando wote hao pamoja na wafungwa wao waliowakamata. Msafara huu wa magari ulikuwa unatakiwa kuwasili eneo la tukio dakika kadhaa mbele baada ya oparesheni kuanza.

Oparesheni hii ilipangwa ifanyike ndani ya muda usiozidi dakika thelathini tu ili kuepuka wapiganaji wenye silaha wa kisomali na raia wanaowaunga mkono kujaa eneo la tukio na kuwashambulia na kusababisha ugumu wa oparesheni kufikia lengo na pengine kufanya oparesheni ifeli kabisa.
Hii ilikuwa ni oparesheni ambayo ilikuwa inatakiwa kufanyika kwa kasi mno, ufanisi na weledi wa hali ya juu kabisa.


Michoro ikachorwa. Mikakati ikawekwa. Maandalizi yakafanyika. Kila komando, kila helikopta… black hawks na little birds… wote walikaa 'standby' wakisubiri amri ya oparesheni kuanza.

Nimeeleza kwamba intelijensia waliyoipata ilikuwa inaeleza kwamba kikao cha washirika wa Aidid kitafanyika siku hiyo. Kwa hiyo Kamanda, Meja Jenerali William Garrison alikuwa anasubiri confirmation kwamba targets (Omar Salad Elmi na Mohamed Hassan Awale) tayari wakiwa wamefika kwenye jengo la kikao chao ndipo 'afungulie nyuki'.

Hatimaye… mida ya saa nane na dakika hamsini mchana wa jua kali kabisa… katika vyombo vya mawasiliano (radio channels) vya makomando na chopa za kijeshi lilisikika neno moja likirudiwa mara nyingi tena na tena…

"Irene… Irene… Irene... Irene.!!"

Hii ilikiwa ni code word kumaanisha kwamba 'target' wameingia ndani ya jengo na hivyo mission inatakiwa kuanza.

Chopa mbili za kwanza zikaenda hewani… MH-6 Assault Little Birds zikibeba makomando wa Delta Force. Zilienda kwa kasi na kwa ufanisi.

Saa tisa na dakika arobaini na mbili 'little birds' zilikuwa zimewasili kwenye jengo lengwa. Ubaya ni kwamba kipindi hicho Mogadishu haikuwa kama ilivyo sasa. Katikati ya mji kulikuwa na vumbi jingi japo mji ulikuwa umejengeka kwa kuridhisha kabisa.
Hivyo chopa zilipokuwa zinaruka chini chini juu ya jengo husika ili kuwezesha makomando wa delta force ku-fast rope kwenda kwenye jengo… upepo ulikuwa unasababisha vumbi jingi kutimka hewani kiasi kwamba mpaka rubani alikuwa haoni.

Chopa ya kwanza ikashusha makomando… chopa ya pili ilibidi izunguke kidogo kurudi nyuma kuruhusu vumbi lipungue na kisha kurejea tena kushusha makomando.

Makomando wa Delta Force wote walishuka kwa mafanikio na kwa kasi kubwa kuingia ndani ya jengo lenye washirika wa Aidid.

Kizaa zaa kilianza ulipofika muda wa kushusha makomando wa 'ranger chalk'.

Baada ya Chopa zile mbili za mwanzo, Little Birds kushusha makomando wa Delta Force… sasa ulikuwa ni muda wa Black Hawks kuleta 'ranger chalk' nne ili waweze kuweka perimeter kuzunguka pande zote za jengo hilo. Hizi chalk za ranger zililetwa na chopa za Black Hawks.
Black Hawks za kwanza zilishusha makomando kwa ufanisi kabisa. Bundi alikuwa kwa makomando wa 'Chalk Four' ambao walibebwa na chopa ya Black Hawk Callsign Super 67.

Kutokana na vumbi jingi kutanda angani, uharaka na presha… rubani alijikuta anakosea na kwenda kuwashusha makomando jengo moja mbele kaskazini mwa jengo husika.


Nilieleza kwamba mtindo wa ushukaji kwenye chopa ulikuwa ni fast roping. Stadi hii ya fast roping niliieleza kwa uzuri sana nilipoandika makala kuhusu Operation Barras iliyotekelezwa na SAS ya Uingereza kuokoa wanajeshi wao nchini Sierra Leon.
Ni kwamba… katika stadi hii, chopa ya kijeshi inaruka chini chini kabisa karibu na ardhi au paa la jengo (mara nyingi umbali wa futi 70 (mita 21) kwenda juu) na kisha kamba zinaning'inizwa kutoka kwenye chopa na kisha makomando wanatumia kama hizi kushuka kwenye chopa na kutua ardhini au juu ya paa. Lakini ushukaji wake ni wa kasi kubwa, kana kwamba wanateleza kwenye ile kamba. Hiyo ndio fast roping.

Sasa chopa hii ambayo rubani alikosea na kwenda kwenye jengo lingine kaskazini mwa jengo husika… wakati chopa ya Black Hawk iko futi 70 kutoka ardhini na makomando wakiwa wana-fast rope… kwa bahati mbaya, komando mmoja, Todd Blackburn hakushika kamba sawa sawa wakati anashuka na akajikuta amedondoka chini ardhini umbali wa futi 70 kutoka angani. Ajali hii ilisababisha Todd kuumia vibaya kichwani na kuvunja shingo.

Wakati makomando wakijaribu kumpa huduma ya kwanza mwenzao, rubani aligundua kwamba amewashusha kwenye jengo ambalo si sahihi… ikabidi awaambie hili makomando kwa kutumia vinasa sauti masikioni mwao… kwamba ashushe chopa chini ili awapakie na kuwapeleka kwenye jengo husika na kumrudisha Todd kambini kwa ajili ya kupatiwa huduma ya kidaktari.

Lakini makomando wakakataa pendekezo hili la rubani kushusha chopa kwa kuhisi kwamba huo mlolongo wa chopa kutua chini, wapande, wampakie Todd na kisha chopa iruke tena itachukua dakika nyingi na watakuwa exposed kwa muda mwingi kuliko kawaida na wanaweza kushambuliwa. Kwa hiyo wakamruhusu rubani wa Black Hawk aondoke wakisema kwamba watambeba mwenzao na kurudi nyuma kwa weledi mpaka kwenye jengo husika na ule msafara wa magari ukiwasili watampakia mwenzao.

Rubani akaondoa chopa yake hewani akiwaacha 'Chalk Four' pale chini kwenye jengo ambalo si sahihi. Makomando wa Chalk Four wakanza kujiandaa kuanza kurudi nyuma kwa tahadhali na weledi kuelekea jengo husika wanakotakiwa kuwa.

Lakini ghafla walisikia mfululizo wa mvua za risasi kuja upande wao… risasi mfululizo kana kwamba kuna watu wanajaribu 'kuwa-pin' wasielekee kule wanakotaka kwenda.
Walibakia wameduwaa wasijue nini kilikuwa kinatokea. Hawakutegemea hili… hawakuelewa nini kinatokea… mvua za risasi zilirindima mfululizo bila kukoma. Walijaribu kujibu mapigo… lakini kadiri walivyokuwa wanajibu mapigo ndivyo ambavyo walikuwa wanazidi kuchelewa kuwepo kwenye eneo wanalotakiwa kuwa, kutengeneza perimeter kwenye jengo walilomo washirika wa Aidid.

Bundi alikuwa ametua kwenye oparesheni… walikuwa wanatakiwa kufikiri haraka na kutumia weledi wao wote kujinasua hapa na pia kuwahi kwenye jengo wanalotakiwa kuwemo kwa sababu kuchelewa kwao kulikuwa kuna hatarisha maisha ya wenzao makomando wa Delta Force walioko kule ndani ya jengo ambako wanawakamata washirika wa Aidid.


Nitarejea… stay here!



Habibu B. Anga 'The Bold' - 0718 096 811
To Infinity and Beyond

WhatsApp, Follow and Subscribe
IMG-20180514-WA0014.jpg
IMG-20180514-WA0012.jpg
IMG-20180514-WA0013.jpg
IMG-20180514-WA0011.jpg
 
Back
Top Bottom