Nov 05, 2023 06:50 UTC
Kwa mujibu wa shirika la habari la Mehra ambalo limenukuu taarifa hiyo kutoka kwenye tovuti ya al Mash'had al Yamani, Barack Obama amesema kuwa, utawala wa Kizayuni ndio unaobeba dhima ya hali ya hivi sasa na maafa ya kibinadamu ya miaka hiyo miaka iliyopita huko Palestina.
Amesema hayo katika mahojiano aliyofanyiwa na gazeti la Politico la nchini Marekani na kuonya kwamba, kuendelea kwa vita huko Ghaza kunatubebesha majukumu sisi sote; sote tunalaumika kutokana na hali hiyo na ni wajibu wetu tuwajibike.
Taarifa hiyo imeongeza kuwa, katika mahojiano yake hayo Obama ametahadharisha kuhusu madhara ya kupuuzwa vita kati ya Israel na Hamas na kutoa mwito wa kuchukuliwa hatua za haraka za kukomesha vita hivyo.
Amesema, haungi mkono shambulio la Hamas la tarehe 7 Oktoba, lakini mauaji makubwa yanayoendelea kufanywa na utawala wa Kizayuni wa Israel hivi sasa na maafa wanayopata Wapalestina hasa wa Ukanda wa Ghaza, hayavumiliki.
Aidha amekiri kwamba maafisa wote wa Marekani wanahusika katika kujitokeza hali ya hivi sasa ya Ghaza, na kusisitiza kwa kusema: "Hakuna mikono ya mtu iliyo safi. Ikiwa unataka kutatua tatizo, unapaswa kuzingatia ukweli wote."
Rais huyo wa zamani wa Marekani pia amesema: Lazima tukubali kwamba, sote tuna jukumu na tunapaswa kulaumiwa kwa kiasi fulani. Bado ninawaza, ningefanya nini wakati wa urais wangu ili kudumisha amani? Ingawa nilijaribu, lakini juhudi hizi hazikufaulu.