*NYUMA YAKO (MSIMU WA PILI) -- 12*
*Simulizi za series*
ILIPOISHIA
Basi baadada ya majadiliano hayo, Marshall akamweleza Jack juu ya haja yake, kwa mkono wake anataka kuwasaka watu wanaohusika, mmoja baada ya mwingine, na kuwatia adabu.
Hatajali itachukua muda gani, ila atawakamata asibaki hata mmoja.
“Kesho tutaenda kuonana na Miss Danielle,” akasema akiwa anakotoa vidole vyake. Alikuwa amejawa na fikira lakini pia hasira.
ENDELEA
Basi usiku huu ukaenda kwa mang’amung’amu sana. Kila alipokuwa akijilaza kuutafuta usingizi, haukuja, mwishowe akaamua kutoka kitandani na kujongea dirisha, akakamata nondo na kutazama nje akiwaza.
Alikuwa amebebelea uchungu usiomithilika ndani yake. Alikuwa anahisi kifua chake kizito, kizito kwa kinyongo, alikuwa anahisi kichwa chake kizito, kizito kwa mawazo. Kwa mara hiyo alitamani angepata kidongea ama dawa yoyote ya kumfanya alale.
Mwili ulikuwa mchovu lakini kila akifumba macho usingizi hauji! Ni kama alikuwa amepewa laana.
Akiwa hapo dirishani anaendelea kuwaza na kuwazua, akasikia sauti ya kike. Hakujua sauti hiyo imetokea wapi lakini alikuwa ana uhakika inatoka nje.
Alikuwa anaota ama? Ni maruweruwe ya kukosa usingizi ama? Alijikuta akijiuliza, lakini alipotega sikio zaidi, akabaini si kwamba alikuwa amekosea, ni kweli kuna sauti ilikuwa inasikika kwa nje.
Basi akarusha macho yake kuangaza huku na kule, ni nani huyo alikuwa akiongea muda huo? Saa ya ukutani ilikuwa inasema saa nane na robo!
Alipoangaza zaidi, kwa mbali, kama macho yake hayakuwa yanamdanganya, akamwona mtu. Alikuwa amewekelea simu yake sikioni akiongea, alikuwa kwenye giza hivyo ngumu kutambulika.
Punde mtu huyo akamaliza kuongea na simu yake na kisha akapiga hatua kurudi ndani, hapo ndipo Marshall akapata uhakika kuwa kulikuwa na mtu, na mtu huyo alikuwa ni Vio, mpenzi wake Jack!
Mwanamke huyo alikuwa amevalia gauni jeupe la kulalia, na akiwa anajirejesha ndani alikuwa akiminya simu yake kubwa. Marshall akamtazama mpaka alipoishilia.
Akabakiwa na maswali, kwanini mwanamke yule alikuwa ameenda kuongelea simu yake kando? Anamficha nini Jack?
Badala ya kupunuguza mawazo, akajikuta akiyaongea maradufu. Sasa hakuwa na uhakika atalala muda gani.
**
Alipoufikia mlango, Vio akapunguza ukali wa vishindo vyake vya miguu, akanyata taratibu na kutengua kitasa cha mlango.
Kabla hajazama akarrusha macho yake kutazama hali ya Jack, alah mwanaume huyo alikuwa anakoroma, basi akazama ndani na kuurejeshea mlango taratibu. Sasa akajihisi yu salama, akashusha pumzi ndefu na kwenda zake bafuni.
Punde akatoka huko na kujirejesha kitandani, akajilaza kandokando ya Jack, lakini asichukuliwe na usingizi upesi, akatazama dari kwa mawazo.
Muda si mrefu simu yake ikamulika, haraka akaitazama na kuikwapua, na kabla hajafanya kitu, akamtazama kwanza Jack, bado mwanaume huyo alikuwa amelowea usingizini.
Basi akafungua simu yake kwa kutumia alama ya kidole, akatazama na kukuta ujumbe, mtu aliyemtumia ujumbe huo hakuwa ametunzwa kwa jina bali namba tu.
Ujumbe ulisomeka, ‘Usiku mwema, kipenzi. Natazamia mengi.’
Vio akaufuta ujumbe huo upesi alafu akazima simu na kufumba macho yake.
**
EDGAR HOOVER, Makao makuu ya FBI.
“Umeshafanya ile kazi?” mwanamke mrefu mwembamba aliinama kidogo apate kuongea na Miss Danielle. Mwaname huyo alikuwa ameseti vyema nywele zake na mwili wake ukiwa umekaa vema ndani ya suti yake nyeusi.
Macho yake makali yalimkodolea Danielle, punde Danielle akanyoosha mkono wake kwenye meza yake na kumpatia mwanamke huyo faili fulani.
“Calm down, miss Danielle,” akasema mwanamke yule mwembamba, acha tumwite Beatha. Kwa sas alipoozesha macho yake akiwa anamtazama Danielle kwa namna ya kuguswa.
“Beatha, nilishakwambia nipo sawa,” akasema Danielle, “Waweza kunielewa hata mara moja?”
“Lakini hauonekani kama upo sawa!” Beatha akasisitiza akiwa amekunja ndita.
“Nipo sawa,” Danielle akasema akimtazama Beatha usoni. “Nipo sawa sawia.”
Basi Beatha akamtazama Danielle kwa muda kidogo kisha akasema, “Najua hili swala ni kubwa sana kwako. Pengine mabega yako yameelemewa, lakini litapita tu. Usijali.” aliposema hivyo akaweka mkono wake begani mwa Danielle na kumpatipati,
“Si kila mara aliye mwema hushinda, na si kila mara nyota hung’aa angani,” Beatha akasema na kisha kwenda zake. Danielle akabaki akiwa mpweke ametingwa na kazi.
Mwanamke huyu mrembo alikuwa ameketi nyuma ya meza iliyokaliwa na tarakilishi lakini pia faili kadhaa. Pembeni yake kulikuwa na kuta zenye kubebelea vipande vingi vya magazeti na ramani. Nyuma yake kulikuwa na picha kubwa ya Raisi wa nchi.
Ofisi yake ilikuwa imetulia lakini kichwani mwake kukiwa na fujo. Tangu kesi ya kupotea kwa Raisi imalizike hakuwa na furaha kabisa. Alijiona amefeli, alijiona amepwaya.
Ingawa kesi ilikua imefutwa, bado kichwani mwake ilikuwa inaendelea na kumtafuna vilevile.
Alivuta kikombe chake cha kahawa akakiweka kinywani, akanywa mafundo mawili alafu akakirejesha kikombe hicho mezani na kutazama tarakilishi yake. Kidogo simu yake ikaita, alipotazama akaona jina ‘Adv. Marble’.
Akapokea simu na kuiweka sikioni.
“Tunaifuta kesi, sio?” aliuliza mtu kwenye simu, yaani Adv. Marble.
“Ndio, futa na ikiwezekana uache kun’tafuta kabisa, sawa?” alisema Miss Danielle kisha akakata simu, kidogo tena, simu ikaita. Miss Danielle alipotazama akaliona jina lilelile lililotoka kumpigia hapo punde, akasonya, akapokea na kuweka sikioni, “unasemaje?
“Vipi kuhusu malipo yangu?” aliuliza Marble.
“Malipo gani?” Danielle akauliza akikunja uso. “Si nimeshakupa pesa yako yote, ama?”
“Hapana,” Marble akajibu na kuongezea, “Bado ya usiri. Unakumbuka tulivyokubaliana?”
Basi Miss Danielle kuondoa zogo, maana hakuwa kwenye ‘mood’ hiyo, akamwambia bwana Marble kwamba atamtumia pesa yake hiyo jioni. Baada ya maongezi hayo, akakata simu na kuizima kabisa.
Bwana Marble ni nani? - ndugu huyu, mwanaume mrefu mwenye nywele ‘blonde’ na macho yanayofunikwa na vioo, ni wakili ambaye alikuwa akiisimamia kesi ya Marshall ingali yu gerezani baada ya kuhukumiwa kifo.
Bwana huyu alikutana na Miss Danielle siku ambayo mwanamke huyo alienda kukutana na Marshall gerezani, na kwa makubaliano, bwana huyu alipeleka kesi mahakamani kupinga hukumu ya Marshall kwa lengo moja tu, la kusogeza muda wa Marshall kuwapo gerezani.
Kwasababu basi kesi ilikuwa inanguruma mahakamani, ndiyo maana siku ya kunyongwa kwa Marshall ikawa inasogezwa mbele na mbele kuitikia rufaa.
Lakini kwenye zoezi hilo, bwana Marble alikubaliana na Miss Danielle kwamba mlolongo wote huo wa kesi utakuwa wa siri, Miss Danielle hakuwa anataka kujulikana kama ni yeye ndiye anamlipa wakili huyo kwasababu za kiusalama. Endapo ingebainika basi ingemletea matatizo.
Basi kwasababu hiyo, Marshall akapata kutekeleza haja yake ya kutoroka, na sasa, Marble akiwa anatumia fursa, anataka pesa zaidi.
Miss Danielle akashusha pumzi ndefu akikuna kichwa chake kilichojaa nywele. Hakuwa na cha kufanya isipokuwa kuitikia hitaji la bwana Marble. Na hivi ambavyo Marshall ametoroka gerezani, akibainika itakuwa shida sana.
**
Saa mbili usiku …
Chumba kilikuwa kina giza nene, lakini kiza hakikudumu, mlango ukafunguliwa na mara taa ikawashwa tap! Mwanga ukatamalaki, alikuwa ni Miss Danielle. Mkononi alikuwa amebebelea koti lake la suti akiburuza miguu.
Akarusha macho yake vitini, akamwona Marshall na Jack. Walikuwa wameketi hapo isijulikane ni muda gani waliingia.
“Marshall!” Danielle akatokwa na maneno.
**