Niliua kwa Kukusudia-17-
ILIPOISHIA:
Bosi na yule mgeni walinisisitizia kwa hamasa kubwa. Nikajikuta nimekubali na kunawa. Yule mhudumu akatumiminia kahawa na kutuwekea sawa vitafunwa. Akatukaribisha. Alipoondoka tu, bosi Elhakimu alinigeukia.
"Tunu."
"Abee, bosi."
"Huyu mdogo wangu ana shida ambayo naamini utaweza kumsaidia, najua huwezi kuniangusha."
SASA ENDELEA...
SIKUWA na haraka ya kuitikia. Nikabaki kimya huku nikiwatazama kwa zamu mmoja baada ya mwingine. Mapigo ya moyo yakawa yananienda mbio kwa kuwa sikujua kabisa jambo ambalo walitaka niwasaidie.
"Unasikia Tunu," Bosi alinishitua kutoka kwenye lindi la mawazo ambalo lilikuwa limenivamia ghafla kwa wakati ule.
"Nakusikia bosi."
"Shida yenyewe ni ndogo sana," bosi akazidi kusisitiza na kunifanya nimuangalie usoni hasa baada ya kusema kuwa shida yenyewe ilikuwa ni ndogo sana.
Alipofika hapo akatulia kidogo, akakohoa kisha kuendelea;
"Shida yenyewe ni kwamba anahitaji mtumishi wa ndani," alisema na kumtazama usoni yule mgeni ambaye alitingisha kichwa kuashiria kukubaliana na alichokisema bosi.
"Sasa, nakumbuka uliwahi kuniambia kuwa una mdogo wako kule kijijini, naona anaweza kufaa."
"Naomba utusaidie kumshawishi aje kufanya kazi kwa huyu mdogo wangu, naamini ni msichana aliyetulia kama wewe hivyo hawezi kuleta usumbufu," alisema Bosi Elhakimu na kunifanya nitabasamu kwa furaha.
Hakika alikuwa amegusa kwenye furaha yangu. Kwa siku nyingi sana nilikuwa nikiwaza ni kwa jinsi gani nitaweza kumtoa mdogo wangu huko kijijini ili aje kuishi nami Dar es Salaam.
"Umenisikia Tunu?" bosi aliuliza baada ya kuona niko kimya kwa muda.
"Nimekusikia bosi, nitafanya hivyo," nilimjibu huku nikionesha furaha ya hali ya juu kabisa.
"Nimefurahi kusikia hivyo, basi inapaswa uondoke sasa hivi kuelekea Chalinze ili kesho uje naye hapa maana huyu bwana anahitaji mtumishi haraka sana," alisema bosi na kumuangalia tena Ashraf ambaye alitingisha kichwa kama ishara ya kuunga mkono alichokizungumza bosi Elhakimu.
"Sawa, niko tayari."
Baada ya kauli yangu, bosi alimgeukia Ashraf.
"Umesikia bwana, yuko tayari kutusaidia."
"Nashukuru sana Tunu kwa hilo, sasa chukua hii kama nauli ya kwenda na kurudi pamoja na huyo mdogo wako," alisema Ashraf huku akinipa noti nyekundu ambazo kwa wakati huo sikujua ni kiasi gani.
"Ahsante."
"Sasa utapitia hukuhuku au utaenda hadi Buguruni ukaage nyumbani?"
"Itabidi niende Buguruni nikaage, lakini nitaondoka leo hii," nilimjibu kwa haraka.
Tuliagana, nikatoka nje ambako nilipitiliza hadi kwenye kituo cha mabasi nikarudi Buguruni. Nilipofika nyumbani nilimkuta shangazi akiendelea na shughuli zake. Akashituka na kuacha kila alichokuwa akifanya.
"Kulikoni tena, mbona umerudi asubuhi yote hii?" aliniuliza kwa hamaki kubwa huku akinitazama usoni.
"Nina safari ya kwenda Chalinze tena."
"Chalinze?"
"Ndiyo."
"Kuna kitu ulisahau?"
"Hapana, namfuata Inana."
"Inana! Wa nini?"
"Nimempatia kazi."
"Wapi na kazi gani?" shangazi aliuliza mfululizo.
Ilibidi nikae chini na shangazi ambapo nilianza kumuelewesha kwa kina zaidi. Nashukuru Mungu shangazi alinielewa.
"Kwa hiyo tutakuwa tukiishi naye hapa, siyo?"
"Hapana."
"Sasa atakuwa akiishi wapi?"
"Hukohuko nyumbani kwa bosi wake?"
"Wewe unawaamini hao watu?"
"Hawana shida shangazi."
"Sawa, lakini ni vizuri kuwa makini sana maana kwa sasa ulimwengu umeharibika."
"Sawa shangazi, mimi nawaamini."
"Mimi sina neno, kwa hiyo unasafiri kesho?"
"Hapana, inabidi niende sasa hivi, kesho nitakuwa hapa."
"Sawa."
Niliingia ndani na kuanza kujiandaa. Nikatoka na kushika njia.
"Haya shangazi, naondoka."
"Safari njema mwanangu."
"Ahsante."
Nikaanza safari ya kurudi Chalinze tena. Nikatembea hadi kituoni ambapo nilipanda mabasi ya kwenda Ubungo.
Nilikuta gari la Chalinze likiwa na abiria wachache. Nikakata tiketi na kuingia ndani ambapo nilichagua siti. Nikatulia na kuanza kuyafikiria maisha. Furaha niliyokuwa nayo haikuwa na maelezo, kwani kitendo cha Inana kupata kazi kilinifurahisha mno.
Muda mfupi baadaye, safari ikaanza, tuliwasili Chalinze majira ya saa tisa na nusu. Nikakodi baiskeli hadi nyumbani na kumkuta Inana akipepeta mchele.
Kabla sijamfikia, nilishangaa baada ya kumuona akijiinamia na kuanza kulia.
Je, nini kiliendelea? Usikose kufuatilia usiku wa leo......