Niliuwa kwa kukusudia-1

Niliuwa kwa kukusudia-1

Leo Shigongo kahamia huku! Kashafungua branch humu jf. Shigongo endelea uko kazini...
 
Niliua kwa Kukusudia -7-

Baada ya ukimya huo Mwarabu alifungua kijaluba cha bati kilichokuwa juu ya meza yake. Ndani ya kijaluba hicho kulipangwa sigara. Niliziangalia kwa pembeni mwa macho nikagundua zilikuwa aina ya Embassy.
Alichomoa sigara moja akaipachika midomoni mwake kisha akaokota kibiriti cha gesi.


"Samahani," akaniambia kabla ya kuiwasha sigara iliyokuwa midomoni mwake.
Sikujua alinipa samahani ya nini, samahani ya kutaka kuvuta sigara katika ofisi yake mwenyewe au alinipa samahani kwa kujua kuwa angenitia moshi?

Vyovyote ambavyo alifikiria niliona samahani yake haikuwa na maana yoyote kwangu. Ukimya wake wa takriban dakika tano ulikuwa umenipotezea muda wangu mwingi.
Alikuwa ameniacha njia panda nikiwa sijui nitaelekea wapi, kwenye kupata kazi au kuambiwa nije siku nyingine.

Simu yake ya mkononi iliyoonekana kuwa na thamani kubwa ambayo ilikuwa pale juu ya meza, ikaita. Akaitupia jicho kisha akanyoosha mkono na kuichukua.
Alipotazama namba iliyokuwa inaita alitabasamu. Akapuliza moshi wa sigara yake bila kujali kuwa moshi huo ungenifikia mimi na kuniumiza.

Akaipokea ile simu huku akiondoka kwenye kiti.
"Hallo Gulam!" alisema wakati akielekea kando ya dirisha.
Nilimtupia macho nikamtazama kwa nyuma. Makalio yake yalikuwa yamepigwa papi na suruali yake ilikuwa imeshuka chini ya kiuno. Mara kwa mara alikuwa akiipandisha.

Alisimama kando ya dirisha na kujinyoosha.
"Ndiyo, nilishazipeleka benki," akasema kwenye simu na kuongeza;
"Zilikuwa milioni mia moja."
Alisita kidogo, akavuta sigara na kupuliza moshi kabla ya kuendelea.
"Zilikuwa pesa taslim si hundi."

Nilishukuru alivyoondoka pale kwenye kiti kwani moshi wote ungekuwa unaniingia mimi.
"Bado namdai milioni hamsini," akasema kwa mkazo huku akionesha ishara kwa mkono wake. Akaongeza;
"Nazihitaji pesa hizo. Nataka nifanye ukarabati wa hoteli yangu. Umenielewa?"
Mwarabu huyo akasikiliza simu kisha akasema; "Sawa." Aliushusha mkono uliokuwa na simu, akarudi kwenye meza.
Kitu cha kwanza aliizima sigara kwenye kizimio kilichokuwa juu ya meza ikiwa imebaki nusu. Alikuwa akivuta kitajiri sana. Hata hivyo hali ya hewa iliyokuwa kwenye ile ofisi ilikuwa imeshaharibika.

"Sasa sikiliza," akaniambia huku akiketi. "Unaitwa nani?"
"Naitwa Tunu Rajab."
Alichomoa kalamu kutoka mfuko wa koti lake akaandika jina hilo kwenye karatasi iliyokuwa juu ya meza.
"Una umri gani?"
"Umri wangu!" Nikasema huku nikifikiria.

"Umri wako ndiyo."
"Nina kama miaka 24 hivi."
"Ulisoma hadi darasa la ngapi?"
"Niliachia kidato cha tatu wazazi wangu walipofariki."
"Hukuwa na kaka zako wa kukuendeleza?"

"Mimi ndiyo mtoto wa kwanza."
Naweza kukutafutia nafasi nzuri baadaye lakini kwa sasa nitakuweka katika sehemu ya mazingira ya hoteli. Yaani kuangalia usafi. Nadhani nikisema usafi unanielewa?"
"Hebu nifafanulie."

"Kuna siku utakuwa unalimalima kwenye bustani. Kuna siku utakuwa unafua na kuna siku utapiga deki. Utakuwa pamoja na wenzako."
"Sawa."
"Mshahara wako utakuwa shilingi laki moja na nusu."


Nini kitaendelea?Usikose kufuatilia usiku wa leo.....
 
Niliua kwa Kukusudia -8-

ILIPOISHIA :
Naweza kukutafutia nafasi nzuri baadaye lakini kwa sasa nitakuweka katika sehemu ya mazingira ya hoteli. Yaani kuangalia usafi. Nadhani nikisema usafi unanielewa?"
"Hebu nifafanulie."

"Kuna siku utakuwa unalimalima kwenye bustani.
Kuna siku utakuwa unafua na kuna siku utapiga deki. Utakuwa pamoja na wenzako."
"Sawa."
"Mshahara wako utakuwa shilingi laki moja na nusu."
ENDELEA SASA…


Hakuna shida," nilijibu kwa haraka sana.
"Sasa ngoja nimuite meneja nimpe maelekezo sahihi," akasema kisha akanyanyua simu ya mezani.
"Haloo Robert!" Akaanza kuzungumza kupitia simu hiyo ya mezani huku nikiwa namtumbulia macho na kuendelea kushangaa uzuri wa ofisi ile.
"Haya, basi njoo mara moja hapa ofisini kwangu," alisema na kisha kukata simu.

Japokuwa sikujua walichokizungumza kwa kina, lakini nikajua ni lazima atakuwa amemwagiza huyo meneja aje kwa ajili ya kunitambulisha kwake.
Baada ya dakika tatu au nne, akaja kijana mmoja mweupe kidogo akiwa amevalia suti nyeusi.
"Naam bosi."

"Unamuona huyu binti," alisema huyo Mwarabu huku akininyooshea kalamu aliyokuwa nayo mkononi.
"Nimemuona bosi," akaitikia huyo meneja na kuniangalia tena.
"Kuanzia leo atakuwa pamoja nasi hapa, nimempangia sehemu ya mazingira kwa maana ya usafi," alisema na kisha kutulia kidogo.

"Sasa nataka umchukue kwa ajili ya kumtambulisha na kumwelekeza baadhi ya taratibu nyingine za kazi."
"Sawa," akajibu meneja na kunionesha ishara ya kumfuata.
Tukatoka nje, nikiwa nyuma yake lakini mkimya sana.
"Twende huku," akaniambia lakini sikujibu chochote zaidi ya kumfuata kwa nyuma.

Tukazunguka upande mwingine wa pili wa hoteli hiyo. Kulikuwa na bustani nzuri ya kupendeza sana. Kulikuwa na watu wengine wakiendelea na kazi mbalimbali za usafi. Kulikuwa na waliokuwa wakikata maua kwa kutumia mikasi mikubwa.
Wengine walikuwa wakimwagilia maji na kuchimbua udongo kabla ya kuusawazisha kwenye mashina ya baadhi ya maua.

"Hawa ni wenzako, utakuwa nao kwenye kazi mbalimbali za usafi ila kwa leo ni heri uungane nao ili kesho tukupangie sehemu zingine za usafi," alisema meneja.
"Sawa, niko tayari."
"Sasa ngoja nikupe sare za usafi."
"Sawa."

Meneja alitoka na kuniacha nikiwa naendelea kuwaangalia wenzangu waliokuwa bize na kazi. Kila kitu kilikuwa kigeni kwangu.
Muda mfupi baadaye, meneja alirejea akiwa na sare mkononi.
Akanipa na kunionesha sehemu ya kubadilishia nguo. Nikaingia chumba hicho na kuvaa zile sare.
Nilifanana kabisa na wenzangu. Nikapangiwa sehemu moja na mvulana mmoja aliyeonekana kuwa mpole na mkimya sana.
Tukasalimiana. Kazi zikaendelea kama kawaida.

"Karibu sana dada," alinikaribisha huyo kijana nami nikamjibu kwa sauti ya chini kabisa.
Jua lilikuwa kali sana siku hiyo. Ilipowadia saa nane, tukapumzika kidogo ambapo wenzangu walianza kuzungumza na kusimuliana habari mbalimbali.

Nilikuwa kimya sana. Sikuwa na mtu wa kuzungumza naye kutokana na hali ya ugeni. Lakini pia hata ukimya wa yule mvulana niliyepangwa naye sehemu moja, ulichangia kunifanya mpole na mkimya mno.
Wakati tumepumzika, nikapata wasaa wa kumuwazia mdogo wangu Inana. Nikawaza jinsi nilivyomuacha huko kijijini na kujikuta nikitamani sana kujua anaendeleaje na maisha ya Chalinze. Kichwa changu kikajawa na kughubikwa na mawazo.
Nikaona wenzangu wakifuata chakula upande wa pili kulikokuwa na jiko la hoteli hiyo.

Kila mmoja akawa anatoka na sahani ya wali na kabeji. Sikuwa na hamu ya kula kabisa, sijui ni kwa sababu gani!
Tukaendelea kupumzika, lakini mawazo yaliendelea kunisumbua sana kichwani hasa nikimfikiria mdogo wangu.
"Mungu yupo," nikajikuta nikitamka maneno hayo kwa sauti na kumfanya yule mvulana niliyekuwa nimekaa naye karibu ageuke na kuniangalia kwa umakini kidogo.

Akanikazia sana macho na kuonesha dalili zote za kutaka kunisemesha jambo japo hakuthubutu kufunua kinywa.
Tukiwa tumejipumzisha, ghafla yule meneja akatokea na kutufanya sote tuendelee na kazi.
Ilipohitimu saa kumi jioni, meneja alikuja na kutuambia kuwa tukabadilishe nguo ili tuwapishe wenzetu waliotakiwa kuingia jioni na kuendelea na kazi.

"Wewe njoo huku," alisema meneja kwa ishara ya kunitaka nimfuate.
"Vipi, najua hutakuwa na nauli ya kurejea nyumbani Buguruni kama nilivyoelekezwa na bosi, chukua hii itakusaidia, lakini kesho ukifika unione kabla ya kufanya chochote," akaniambia yule meneja huku akinikabidhi shilingi elfu kumi.
"Sawa, ahsante," nikaitika na kumshukuru.
"Haya, basi tutaonana kesho."

"Haya," nikamjibu na kuelekea kwenye chumba cha kubadilishia nguo.
Baada ya kubadili nguo, nilitoka pamoja na baadhi ya wafanyakazi wengine.
"Dada," nilisikia sauti kutoka nyuma yangu ikiniita.
Nikageuka bila kuitikia.
Kumbe alikuwa ni yule kijana niliyekuwa nimepangwa naye sehemu moja ya kazi.

"Unasemaje kaka?"
"Samahani."
"Nakusikia."
"Naomba kuzungumza na wewe kidogo."
"Endelea."

"Unaitwa nani vile?"
"Tunu, kwani vipi?"
"Nilitaka tufahamiane, mimi naitwa Hemed."

"Nashukuru kukufahamu," nilimjibu huku nikianza kupiga hatua kuendelea na safari yangu.
"Kuna jambo moja nataka nikuulize."
"Jambo gani tena?" Nikamuuliza kwa sauti ya juu na ukali kidogo kutokana na uchovu pamoja na mawazo niliyokuwa nayo.

Nini kitafuata? Usikose kufuatilia jumatano usiku....
 
Maskini Tunu naiona harufu ya mitihani ya paka shume inaanza kumyemelea.
 
Back
Top Bottom